CHRISTMAS NA UJUMBE WA YESU KRISTU

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2004.

CHRISTMAS NA UJUMBE WA YESU KRISTU

Christmas imefika. Ni wakati wa kufurahi, kusherehekea na kukutana na ndugu, jamaa na marafiki. Christmas sasa hivi ni utamaduni usiopingika katika jamii yetu ya Tanzania. Huu ni wakati wa kutumiana salaam, zawadi na kutakaiana mema. Watu wanaofanya kazi mbali na nyumbani, huu ni wakati wao wa likizo na kusafiri hadi vijijini kwao kusherehekea Christmas. Kila mtu anajitahidi kununua nguo mpya, kuandaa chakula kizuri na kinywaji cha kutosha. Kwa Wakristu ni wakati wa kwenda kanisani, hasa kwa wale wasiokuwa na utamaduni wa kusali kila Jumapili, Christmas unakuwa wakati wao mzuri wa kuingia kanisani. Huu ni wakati wa makanisa kujaa hadi watu wengine kusalia nje. Kwa upande wa mapadri na wachungaji huu ni wakati mzuri wa kukusanya mapato.

Hivyo Christmas, ni furaha, kusherehekea, kusali, kula na kunywa. Inajulikana karibu kwa kila mtu Mkristu na asiyekuwa Mkristu kwamba sikukuu hii ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu kristu wa Nazareti.

Kama sikutokea msiba, ajali, ugomvi au tukio jingine baya, imezoeleka kuchukuliwa kijumla kwamba Christmas ni siku ya furaha kwa kila mtu. Hata mapadre na wachungaji wanapoendesha ibada za Christmas wanachukulia kijumla tu kwamba waumini wote wanakuwa wamejawa na furaha ya kusherehekea siku ya kuzaliwa mwokozi wao, kristu, mwanga wa mataifa. Ukweli wenyewe ni kwamba ibada ya Christmas inakusanya wote, wenye furaha na wenye huzuni, wenye moyo safi na wenye chuki, wenye upweke wa rohoni, wagonjwa wa mwili na roho, maskini na matajiri. Wakati ibada ikiendelea, kuna waumini wanaokuwa kwenye mawazo ya ndoa zao zenye matatizo, wanawake wengine wanakuwa wakiwalaani wale wanaowaibia waume zao na “wezi” hao wanakuwa kwenye ibada wamevalia nguo za bei mbaya – wanakuwa na mawazo kwamba hizo zitakuwa ni pesa za waume zao. Wanawake hawa wenye hasira wanasali nusu nusu na furaha ya Christmas inakuwa chungu tupu. Pia kuna wale wanaokwenda kwenye ibada bila kuwa na uhakika wa kupata mlo wa sikukuu na wakati mwingine bila kuwa na uhakika wa sehemu ya kulala! Wengine ni wagonjwa, wanaingia kwenye ibada ya Christmas, ili wapone kwa miujiza maana hawana pesa za kwenda hospitali ingawa wakati mwingine watu hawa wanakuwa na pesa za kutoa sadaka ya Christmas!! Kwa vile muundo wa ibada tulizoziozea hautoi nafasi ya kujuliana hali, umejengeka utamaduni potovu wa kuamini kwamba kila anayekuwa kwenye ibada ya christmas au ibada nyinginezo anakuwa na furaha, amani na utulivu wa rohoni!

Utamaduni mwingiane uliojengeka kuizunguka sherehe ya Christmas ni watu kusherehekea bila kutafakari kwa kina ujumbe wa Yesu Kristo. Ukweli uliojificha ni kwamba la msingi si kusherehekea, bali ni kuupokea ujumbe wa Yesu Kristo, kuutafakari na kuuingiza katika maisha yetu ya kila siku. Jambo hili limekuwa gumu si leo tu bali hata kwenye karne nyingi za nyuma.

Ipo mifano mingi ya kuonyesha kwamba sherehe za Christmas, za kuzaliwa mkombozi wa ulimwengu, mwana wa Mungu, zimepindishwa na kupopotoshwa. Watu wanasherehekea na kuendelea kuishi kinyume na mafundisho yake. Ujumbe wa Yesu unawekwa pembeni na badala yake vinaundwa vitu vingine tofauti kabisa. Vitu kama sadaka, ibada za kupendeza na kuvutia, nyimbo nzuri na zenye mvuto, wingi wa watu, mahubiri yenye vitisho vya kuashiria mwisho wa dunia, sheria, utukufu wa viongozi, uchu wa madaraka nk.

Ebu nitoe mifano michache ya mafundisho ya Yesu Kristo, yanayotupwa pembeni:

“ Yohana Mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Yesu. Basi, akawatuma wanafunzi wake wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohana mambo mnayoyasikia na kuyaona: vipofu wanaona tena, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia tena; wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari njema.” ( Matayo 11:2-5).

Je, tunaposherehekea Christmas ya mwaka huu wa 2004, vipofu wanaona? Viwete wanatembea na viziwi wanasikia? Je, wafu wanafufuliwa? Wakoma wanatakaswa? Bila ya kujiingiza kwenye mabishano ya kitekinolojia, kiimani na kitaalam ya kuchambua na kujiuliza kipofu ni nani? Na kiwete ni yupi! Ni bora kujiuliza swali la kawaida: Ni nani anajishughulisha na maisha ya jirani yake? Na swali la pili linataka kufanana na la kwanza, je jirani yako ni nani? Swali la pili linaweza kujibiwa na mfano wa Yesu mwemewe wa Msamaria mwema. Jirani yako anaweza kuwa ni mpita njia na mtu wa mataifa! Yesu, alitoa mfano huu kuunyoshea upana wa ujumbe wake. Alitoa mfano huu kupinga ubaguzi uliokuwepo kati ya Wasamaria na Wayahudi. Ni kiasi gani hivi leo wale wanaojiita Wakristu wanapinga ukabila na kupinga ubaguzi wa aina yoyote ile ni swali gumu! Hili linahitaji mjadala unaojitegemea. Tuendelee na la kwanza: Yesu, anatufundisha kumpenda jirani kama nafsi yetu. Asiyempenda jirani ni kipofu! Maana yake ni kwamba anaiona tu nafsi yake na kushindwa kuziona nafasi za watu wengine. Kama mwili wote ungekuwa sikio na mkono ungekuwa wapi? Anauliza Mtakatifu Paulo. Akiwa na maana kwamba hakuna mtu anayesimama peke yake, na kwamba utu wa mtu unakamilishwa na utu wa watu wengine. Asiyeuona utu wa watu wengine na kuuthamini, atanyosha upanga na kumchinja ndugu yake, atachukia pua ya jirani yake, atachukia rangi ya jirani yake, atamnyanyasa jirani yake, atapenda amtawale jirani yake au amwibie jirani yake. Matendo kama haya yanatokea kila siku miongoni mwa watu wanaojiita Wakristu. Rwanda ni mfano mzuri, Wakristu walichinjana wao kwa wao wakishirikiana na mapadre na maaskofu wao. Upofu uliwatawala! Asiyempenda jirani ni sawa na kiwete. Mtu anakamilika katika jumuiya ya watu wengine, mtu akibaki peke yake anakuwa hakukamilika. Asiyempenda jirani ni sawa na ugonjwa wa Ukoma. Tabia ya ugonjwa huu ni kukata sehemu ya viungo vya mwili. Hivyo kutompenda jirani ni sawa na kukata viungo vya mwili, viungo vya Jumuiya wa waumini. Pia asiyempenda jirani ni kiziwi, maana masikio yake yanaisikia tu nafsi yake bila kusikia sauti za nafsi nyingine zinazomzunguka. Mtu asiyesikia sauti za nafsi nyingine, hawezi kujizuia kutenda mabaya katika jumuiya wa waumini!

Bila ya kuingilia mabishano ya kitekinolojia, kiimani na kitaalam ya kuhoji maana ya mtu mfu na mtu hai, tujiulize swali la kawaida: Yesu aliwafufua wafu. Na aliuhakikishia ulimwengu kwamba yeyote anayemfuata na kuwa mfuasi wa kweli atafufua wafu na kufanya miujiza mingi. Je, ni nani anawafufua watu katika enzi zetu hizi tulizomo? Kwa maneno mengine ni nani anawapatia watu Imani hai? Imani ya Kikristu! Imani ya ushirikiano, kuheshimiana, kuchukuliana, imani isiyokuwa na ubaguzi wa rangi, tabaka, ubaguzi wa kijinsia, ukabila na udini? Imani isiyojenga chuki, isiyoleta vita. Imani yenye uhai, ndio tendo pekee lenye nguvu ya kuwafufua wafu. Ni nani anafanya miujiza hii siku hizi?

Bila ya kujiingiza kwenye mabishano ya kiteknolojia, kiimani na kitaalam ya kujiuliza na kuchambua maana ya umaskini, kwa vile kuna umaskini wa roho, umaskini wa akili na umaskini wa kutokuwa na mali, tujiulize ni nani anaupenda umaskini? Uwe umaskini wa roho, wa akili na wa kutokuwa na mali ni nani anaupenda? Mtakatifu Matayo anatwambia kwamba:
“ Heri wanaojiona kuwa maskini mbele ya Mungu, maana Utawala wa mbinguni ni wao.” ( Matayo 5:3).
Ni umaskini gani huu anauongelea Matayo? Ni watu wangapi wangependa kuwa maskini, kuishi na maskini au kuwakaribia maskini? Ni wangapi Christmas hii wamekula chakula meza moja na maskini? Ni wangapi wametoa huduma kwa maskini na ni wangapi wanashiriki katika harakati za kuupunguza umaskini katika taifa letu. Ni nani anahubiri habari njema ya haki, wema na huruma kwa maskini? Ni nani anafanya kazi na miujiza aliyoifanya Yesu wa Nazareti, ambaye kila mwaka tunasherehekea sikukuu yake ya kuzaliwa?
Mfano mwingine wa kuonyesha jinsi ujumbe wa Kristo unavyowekwa pembeni:

“ Tena mmesikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: ‘ Usivuje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.’ Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu maana ni kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa dunia maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu maana ni mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Ukisema, ‘Ndiyo’, basi , iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi, iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu.” (Matayo 5: 33-37).

La kushaangaza ni kwamba makanisa yote sasa hivi yamejaa viapo vya kila aina, kuanzia viapo vya ndoa, utawa, useja, kutokunywa pombe na viapo vya kuacha hili ama lile! Viapo vinaendekezwa na kutukuzwa licha ya kuonywa na Yesu Kristo, kwamba chochote kitakachoongezeka juu ya “Ndiyo” na “Hapana” kitakuwa kinatokana na yule Mwovu! Watu wanapoteza muda mwingi kukazana kutunza viapo, kuliko kukazana kumpenda na kumkaribishana jirani. Anayebahatika kutunza kiapo chake, anaonekana kuwa mtu wa maana katika jamii, ingawa mara nyingi mkazo mtu anaouweka katika harakati za kutunza kiapo unamsukuma mbali na jamii – anakuwa hana msaada wowote katika jamii anamoishi. Anatukuzwa si na wale watu anaoishi nao bali vizazi vijavyo. Ndiyo maana si kawaida karne kumtangaza mtakatifu wake, inatokea kwa nadra sana!

Mfano mwingine wa kuonyesha jinsi ujumbe wa Kristo wa Nazareti, unavyowekwa pembeni:
“ Wala msimwite mtu ye yote, “Baba” hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu aliye mbinguni. Wala msiitwe ‘Viongozi’, maana kiongozi wenu ni mmoja tu ndiye Kristo. Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu. Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa.” ( Matayo 23:9-12).

Kanisa katoliki linaongozwa na Baba mtakatifu, Baba Askofu na Baba paroko! Na hawa ndio viongozi wa kanisa. Ubaba wao umejaa utukufu mkubwa na wala si utumishi. Wana utukufu wa kujikweza na wala si wa kukwezwa. Mtu unaweza kujiuliza mababa hawa wanaposoma mistari niliyoitaja hapo juu wanailewa vipi? Wanaitafakari? Licha ya kwamba Yesu, alionya mtu yeyote asiitwe baba, ubaba huu unalifanya kanisa lionekane ni la wanaume peke yao. Linaongozwa na wanaume na wanawake hawana nafasi yoyote katika kufanya maamuzi. Mpaka leo haijatokea tukasikia: Mama Mtakatifu, Mama Askofu na Mama paroko. Na labda hii isingepingana na mafundisho ya Yesu. Alizuia mtu kuitwa Baba, lakini hakuzuia mtu kuitwa Mama. Mtume aliyempenda sana alimwacha mikononi mwa Mama yake!:

“Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake na dada ya mama yake,Maria wa Kleopa, na Maria Magdalene. Yesu alipomwona mama yake, na, karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.” ( Yohane 19:25-27).

Hivyo Mama, ana nafasi ya peke katika kanisa. Mama Mtakatifu, Mama Askofu na Mama paroko si tusi. Lakini kwa vile tunatawaliwa na upofu, linaweza kuonekana kama tusi. Na kama ni tusi, basi ni tusi takatifu!

Tuache tabia ya kusherehekea Christmas na sherehe nyingine za kidini bila ya tafakari ya kina na hasa kuzingatia ujumbe wa waanzilishi wa dini hizi za kigeni! Pamoja na yote hayo, tutakiane Christmas njema na mwaka mpya wenye mafanikio.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment