Makala hii ilitoka kwenye gazeti la Rai 2004

WAKO WAPI WANATEOLOJIA WETU

Ninakumbuka kuandika makala juu ya Wako Wapi Wanateolojia Wetu (1),makala ambayo yaliibua mjadala wa wazi na wa nyuma ya mapazia, baadhi ya wasomaji wa RAI, walijitokeza na kutoa maoni yao wazi gazetini, wengine ambao ndo walio wengi walinitumia ujumbe wa barua pepe wakitoa maoni yao na wakitaka kujua maana ya neno “Teolojia”. “Teolojia” ni elimu ya dini na mabo yote yahusuyo imani na Mungu. Mwanateolojia, ni mtaalamu aliyesomea teolojia na kuibuka na uwezo wa kuchambua kwa ufasaha nadharia ya madhehebu ya dini na kuielezea ili iendane na kueleweka katika sehemu fulani na kwa wakati uliopo.

Wanateolojia wanaandika vitabu vya kuiongoza jamii katika mambo ya imani ndani ya maisha ya siku siku kwa kuzisoma alama za nyakati. Wanafundisha mashulei na vyuoni ili kujenga imani pevu miongoni mwa vijana. Wanateolojia wengine ni waanzilishi wa shule za mawazo “School of thoughts”. Katika nchi zilizoendelea wanateolojia ni watu mashuhuri na wanaheshimika maana dini umekuwa msingi mkubwa wa maendeleo katika nchi hizo.

Pia ikumbukwe kwamba wanateolojia ndo kundi linalounda jumuiya ya viongozi wa kidini. Hawa ndo mapadre, mashehe,maaskofu, makadinali na mapapa.

Kwasababu ya historia na “unyonge”, wanateolojia wa Tanzania, hawasikiki, wamejawa woga na wala si mashuhuri. Tunao mapadre,wachungaji,mashehe, maaskofu na kadinali. Tunao wanaofundisha mashuleni na vyuoni na wengine wanaandika vitabu, lakini ukiwabana kwa hoja nzito wako tayari kuyakana hata maandishi yao wenyewe. Kama anavyosema Frieder Ludwig, kwenye kitabu chake cha “Church and State in Tanzania: Aspects of Changing Relations,1961-1994. London,2001”,Kanisa barani Afrika linatuhumiwa kwa kutotumia “madaraka ya kuseama” na hii ni kasoro ya matumizi ya madaraka.Anadhani sababu kadhaa zinazuia kanisa kusema kama:,Viongozi wa kanisa wanaishi mbali na watu wanaopaswa kuwasemea,Dhambi za kanisa zisizotubiwa zinalizuia kusema; ustaarabu na uungwana wa kutunza urafiki; na kanisa kutoguswa na yale linayopaswa kuyasemea.

Mkutano wa kumi na mbili wa hali ya Siasa Tanzania. Ulioandaliwa na REDET, tarehe 10-11,August 2004, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee,Dar-es-salaam, ulishuhudia mabadiliko katika mwenendo wa wanateolojia wa Tanzania. Mada kuu ya mkutano huu ilikuwa: Kujenga Imani ya Jamii na Amani. Mada ndogo ya: Uzoefu wa Viongozi wa Dini katika Kujenga Imani ya Jamii na Amani, ilisukumwa kwa wanateolojia wetu, baadhi yao akiwemo Askofu Kilaini na Askofu Bagonza, waliingia ulingoni kwa kupanda jukwaa la majadiliao na maoni! Askofu Kilaini, ambaye ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-es-salaam, ana shahada ya udaktari katika historia ya kanisa kutoka katika vyuo vya Roma-Italia. Askofu Bagonza, ambaye ni Askofu, wa KKT-Dayosisi ya Karagwe, ana shahada ya udaktari katika Theolojia ya Maendeleo kutoka katika vyuo vya nchini Marekani. Makala haya yatajadili maoni ya Askofu Bagonza, aliyoyatoa kwenye mada ndogo ya : Uzoefu wa Viongozi wa Dini Katika Kujenga Imani ya Jamii na Amani. Makala yatakayofuata baada ya haya yatajadili maoni ya Askofu Kilaini, kwenye mada ile ile.

Askofu Bagonza, amevunjilia mbali ukimya, ububu, kigugumizi, woga na kutojiamini kwa wanateolojia wa Tanzania. Amefungua ukurasa mpya katika historia ya kanisa nchini Tanzania. Maneno yake yanayochomoza kwenye hitimisho la mada yake, yanampandisha kwenye ngazi ya mwanateolojia shupavu mwenye nia na lengo la kujenga Imani, Amani, Haki na kuchangia maendeleo ya Taifa letu,Kanisa si kama chama cha siasa kwa sababu halina wanachama,linapaswa kuwa na wafuasi/wanafunzi (disciples).Kwa ajili ya kurahisisha kazi zake, historia sasa inaonyesha limekukwa na wanachama zaidi kuliko wafuasi/wanafunzi.Kwa sehemu, hii inatokana na muumdo wake unaowatenga viongozi na wafuasi wao. Kanisa limepoteza mawasilinao na wasomi ambao waliliacha na hao hao ndio wanaofanya maamuzi makubwa ya sera na mifumo katika nyanja za siasa, uchumi na jamii,kwa kuwa si wanafunzi tena bali ni wanachma wa kanisa, waanaibadilii jamii bila nguvu ya ushawishi wowote katika kanisa hata kama kuna wanaodhani wanakanisa walio serikalini wanafanya hivyo kwa maagizo ya kanisa. Kanisa limepoteza mawasiliano ya kweli na masikini wavijijini ambao ndio wengi. Linawahudumia kimwili kwa kuwapa huduma, lakini kiroho wanahudumiwa na vikundi vipya vinavyoibuka, na amabvyo ujuzi wake katika kuijenga jamii endelevu haujapimwa,

Kwa kutambua hali hii, taasisi za dini zinahitaji kuwa na mkakati wa kudai na hatimaye kurejea katika mshikamano wake na masikini wa vijijini, na pia kuunda daraja la maongezi na wasomi walio mijini. Hatua hii yaweza kupeleka mabadilliko makubwa katika muundo na mazoea ya kanisa. Hii inahitaji moyo jasiri, kwa sababu ni ama kanisa libadilike au libakie ni nafasi ya waoga wasiopenda kuukubali ukweli unaowahusu. Kisiasa na kijamii, kanisa naamini, lina ruhusa ya kuunda maoni yake lenyewe na kuwa tayari kuyatetea.Tatizo ni kupinga bila kupendekeza jipya, au kupinga kwa msimu kama ilivyo sasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu. Ni hatari kuwa na kanisa au taasisi ya kidini isiyo na mshikamano na masikini au wasomi.......
Ukiachia mbali kizazi cha Marehemu Askofu Mwoleka,Askofu Sangu na Marehemu Askofu Kibira, maoni haya ya Askofu Bagonza, ni mapya katika kizazi hiki tulichomo. Askofu Bagonza, anaamini kwamba ujenzi wa imani ya jamii na amani ni mradi wa pamoja tena wa muda mrefu. Tanzania tuna kipindi cha miaka 43, katika mradi huu wa pamoja,Pamoja na kutenganisha dini na serikali, historia imeonyesha kwa wema na ubaya, kuwa mashirika ya dini ni washirika pamoja na serikali katika kujenga imani ya jamii na amani. Mathalani makanisa tangu hata kabla ya uhuru, yamejihusisha na utoaji wa huduma za jamii: mashule,ustawi wa jamii, afya ya msingi, na afya ya jamii, Maendeleo:Kilimo, maji, miundo mbinu, ufundi,jinsia na nyinginezo, Utetezi: Elimu ya haki za msingi, maafa, kampeni dhidi ya deni la nchi, sera bora, masingira na uraia.

Katika uchambuzi wake Askofu Bagonza, anataja wazi kwamba,Kutokana na mnyumbuliko wa historia hiyo hiyo safari ya miaka 43 ya uhuru imetuonyesha wazi kuwa mshikamano wa kujenga imani hii si kitu cha kudumu. Hutokea katika safari, baadhi ya wajenzi wakageuka wabomoaji wa imani ya jamii, wengine kuwa watazamaji na hata wengine kuwa waathirika wa makundi haya mawaili. Likitokea hilo, ujenzi wa imani ya jamii huchukua sura ya mgogoro wa kijamii na hatimaye kuua kabisa imani ya jamii na amani katika jamii.

Kwa maoni ya Askofu Bagonza, ili kujenga imani ya jamii na amani, ni lazima kiongozi; awe kiongozi wa dini ama serikali, awe na maadili ya madaraka na matumizi yake,Madaraka yasiyokuwa na maadili ni chanzo cha kukosekana kwa imani na amani. Pia anapendekeza kiongozi awe mtu wa Kujitoa au Kujitolea,Viongozi wengi katika jamii hapa Tanzania bila kujali taasisi gani wanatoka, hivi sasa wanafanana kwa jambo moja kubwa: kwamba, wanaamini kuwa nguvu yao ya ushawishi katika jamii inatokana na wingi wa mali walizonazo, visomo walivyopata na pengine wanatoka vyama gani. Wapo wengine lakini wachache wanaodhani dini zao, makabila yao, na jinsia zao vina nafasi katika kauwafanya waaminike katika jamii......,Njia ya uhakika ni kuwa makini katika kuchagua viongozi walio tayari kujitoa mhanga na kushi hivyo (Sacrificial versus privileged ledership).

Anaendelea kushambulia tamaa na uchu wa mali kama kigezo cha uongozi,Tamaa na uchu wa mali kwa viongozi wa jamii imeharibu kizazi cha viongozi wazuri hasa vijana na kuzalisha kasumba kuwa si rahisi kuwa kiongozi bila kuwa na mali. Vipawa vingi vizuri vya viongozi vijana vimeharibiwa na dhana hii na uwezekano wa kuharibika zaid ni mkubwa kuliko kinyume chake. Uwezekano wa kubaki kiongozi mwadilifu ukiwa na mali nyingi ni dhana isiyotekelezeka kwa sababu mali nyingi huondoa unyenyekevu na kubadilisha hali ya kiongozi katika kufikiri, kuamua, kutenda, kuvumilia, kukosoa au kukosolewa.

Askofu Bagonza, anatoa changamoto kwa taasisi za kidini,Maeneo yaliyoathirika sana ndani ya taasisi za dini na kupunguza imani ya jamii kwa taasisi hizo ni pamoja na kukosekana kwa uwazi katika utawala wa fedha, kashfa za maadili binafis, maisha ya anasa, kugombanbia madaraka, ukabila, n.k. Kwa maoni yake, Imani ya jamii kwa taasisi hizo itaimarika kutokana na uwezo wa taasisi za dini na viongozi wake kushughulikia hayo kwanza, na hilo litadhibitisha kuwa wana uwezo wa kushughulikia matatizo ya jamii huria. Kwamba,Hata hivyo, kwa kuwa waumini wa taasisi hizo ndiyo hao hao wako katika jamii, kazi zote mbili inabidi zifanyike kwa wakati mmoja(kusafisha na kujisafisha).
Changamoto nyingine anayoitoa kwa taaasisi za kidini,Taasisi za dini hazina rekodi nzuri ya kutafiti na kuchambua sera na maamuzi ya kisiasa na athari zake kwa jamii. Matokeo yake ni ama kuyapinga bila uhakika, au kuyaunga mkono kijumla jumla na kutelekeza ushuhuda wake.Kwa hili, imani ya jamii hujengwa au kubomolewa. Mpaka sasa taasisi zimechangia kidogo sana katika kuchambua bajeti ya taifa na ufuatiliaji wake; andiko la mikakati ya kuondoa umasikini(PRSP),misamaha ya madeni;sera ya ubinafsishaji nk. Katika hili la kutofanya utafiti, Askofu Bagonza, anatoa mfano wa Ujamaa, Kanisa kama taasisi ya dini halikuwa na falsafa yake yenyewe katika uwanja huu zaidi ya huruma, maendeleo ya kweli ni zaidi ya huruma. Kwahiyo, dola ilipokoma kuelezea ujamaa kama dira ya taifa kijamii na kiuchumi, na kanisa lilikoma maana kwa kweli ujamaa haukuwa wake hata kama mafundisho yake kadhaa yana mfanano na ujamaa. Pili, tofauti na dola, kanisa haliwezi kukana matamko yake ya nyuma yaliyounga mkono itakadi ya ujamaa kisha likawa salama;ama haliwezi kurukia msimamo mpya wa uchumi unaofuatwa na dola na kisha likawa na uhakika wa kujenga imani ya jamii na amani.......,Kwa hiyo taasisi za dini ni ama ziamue kuwa sehemu ya maamuzi hayo na kuishia kuganga wahanga wa maamuzi hao, au zijitenge na maamuzi hayo na kuwa sehemu ya wahanga au chachu ya kubadili maamuzi hayo!

Kiini, upekee na umahiri wa Askofu Bagonza, katika kuchangia mada ya Ujenzi wa Imani ya Jamii na amani, umejikita katika mambo matatu ambayo anayaelezea kwa ufasaha na uwazi mkubwa:
“Teolojia ya kuingilia”, “Teolojia ya ukombozi” na “ Teololojia ya maendeleo”. Kila aina ya teolojia alizozitaja, alitoa mfano:

“Teolojia ya kuingilia”. Hii ni teolojia iliyoanzishwa na Mchungaji kijana Dietriech Bonhoeffer, Ujerumani, wakati wa utawala wa Hitler. Kitu cha kujifunza katika teolojia hii ni misemo miwili ya kijana Bonhoeffer, aliyenyongwa kwa kupinga utawala wa Hitler:

“ Ikiwa gurudumu limechomoka na linaendelea kugonga na kujeruhi watu, kazi ya kanisa isiwe kuendelea kuganga vidonda vya majeruhi kwa kufunga bandeji, bali kuchukua kigingi na kusimamisha gurudumu hilo
Msemo wa pili ni:
“ Kanisa likishiriki kusafisha chombo kichafu ni lazima lijiandae kuchafuka mikono yake”.

Hitler,aliwaua mamilioni ya watu aliodhani ni chanzo cha matatizo ya uchumi wa Ujerumani. Viongozi wa dini walilazimishwa kula kiapo cha kumtii na yeye akijiita Mungu wa duniani.Ilipita miaka ya ukimya, ububu, kigugumizi na woga,Hitler akakubalika.Taassisi za dini zilikwepa mateso na kifo na kuamua kukaa kimya! Dietriech Bonhoeffer, alikatisha kimya hicho kwa kuanzisha kanisa mafichoni. Ingawa alinyongwa, lakini ushawishi na cheche alizozianzisha kupitia kwenye “teolojia ya kingilia” zilienea duniani kote. Lengo la "Teolojia ya kuingilia” ni: Ni heri kuzuia kuliko kuponya. Tanzania, inaweza kuiga teolojia hii!

“Teolojia ya ukombozi”, hii ni teolojia iliyozinduliwa na wamisionari wa Kijesulit, kule Amerika ya kusini baada ya kuona uchumi wa nchi unaangukia mikononi mwa watu wachache. Watu waliowengi waliishi kwenye umasikini. Kanisa na viongozi wake walishiriki neema hii ya wachache kumiliki uchumi wote. Teolojia ya ukombozi, iliyolenga kuwakomboa masikini wa nchi za Amerika kusini, machoni mwa dola na utawala wa kanisa ilionekana ni “ugaidi” uliovaa sura ya “ukomunisti”. Askofu Mkuu Oscar Romero, wa El-Salvador, aliona hakuna njia nyingine ya utume wa kanisa isipokuwa kusisitiza umuhimu wa Teolojia ya ukombozi. Alipingwa na maaskofu wenzake na kuonekana mzushi na mwasi kwa kanisa na dola. Dola nayo ilianzisha operesheni maalum ya kuwashika na kuwaua makasisi wote wa Kijesuit. Hatimaye na Askofu Mkuu Romero, aliuawa kutokana na msimamo wake wa kupinga unyonyaji na kuwatetea maskini. Teolojia ya ukombozi, inatufundisha kwamba ili kujenga imani ya jamii na amani, viongozi wa dini wasimame upande wa masikini na kuwaletea ukombozi!

“Teolojia ya maendeleo”, hili ndilo eneo la Askofu Bagonza, anasema,Wana maendeleo wa siku hizi wanatuasa kuwa inawezekana sana “kutofanya maendeleo, ikawa ni hatua ya maendeleo endelevu” wakimaanisha, ikiwa hujui mkazo wa maendeleo ni bora kutofanya!, Ili kuleta maendeleo ni lazima kupigana na umasikini, Uzoefu wa taasisi za dini na viongozi wake uaainisha sura kuu nne za umasini katika Tanzania, yaani umaskini wa madaraka (power), umasikini wa kukosa mshikamano(kutelekezwa),umasikini wa jinsia na umaskini wa eneo aliko mtu. Imani ya jamii kwa taasisi za dini ni budi ijengwe kwa kuangalia ni jinsi gani vyombo hivyo na viongozi wake wanafanya kuondoa sura hizi sa umaskini, badala ya kukazana kuondoa uhaba wa vitu na kufanya mambo ya kisasa (modernization) na kudhani hayo ndiyo maendeleo......,Ni vema maendeleo ya taifa changa kama la Tanzania yakaze vitu vinne yaani, utambulisho(identity), uhuru(freedom), ushirikishwahi(participation) na kujitegemea (self-reliance). Kwa kuwa dhana nyingi maarufu za maendeleo ( hasa za ki-magharibi) zimejengwa katika harakati za kuondoa uhaba na kuhodhi mali, ni bora kabisa taasisi za dini zikajenga katika uwanja wa kuichambua nadharia ya maendeleo ili kuionya na kuiangaliza jamii dhidi ya athari za maendeleo yasiyotokana na upevu wa fikra za watu wenyewe. Taasisi za dini zikizama katika harakati za maendeleo zinazofanywa kwa kuegemea dhana za kigeni, jamii ikiharibikiwa itazilaani taasisi hizo kwa sababu ni wajibu wa taasisi kubainisha kasoro zilizomo katika dhana ngeni za maendeleo.

Askofu Bagonza, anachomoza kama nyota njema, nyota ya matumaini miongoni mwa wanateolojia wetu wa Tanzania, anaposema hivi,Mifano iko mingi inayoonyesha kuwa imani ya jamii kwa taasisi za dini hailetwi na mali za taasisi hizo (vituo,miradi, na program) tu, bali inajengwa na misimamo ya taasisi hizo na viongozi wake katika kutetea haki iliyo katika umbo lolote inayomhusu mwanadamu na mazingira yake.Inaleta heshima kama taasisi ya dini na kiongozi wake wanafahamika wanasimama wapi katia masuala ya msingi katika jamii ili imani ya jamii iweze kujengwa, na misimamo ya namna hiyo si lazima iwe ni ile inayopendwa na watu wengi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment