NANI ADUI WA UMOJA WETU WA KITAIFA?

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

NANI ADUI WA UMOJA WETU WA KITAIFA?

Hakuna taifa linaloweza kusimama bila ya kuwa na umoja wa kitaifa. Tanzania imesimama imara hadi leo hii kwa sababu ya umoja wa kitaifa uliojengwa na waasisi wa taifa letu. Tunasifiwa kwa utulivu na amani. Sifa hizi ni za kweli na kilichotukifisha hapa tulipo ni umoja. Na hili halikunyesha tu kama mvua ni jambo liliofanyiwa kazi usiku na mchana. Waasisi wa taifa yetu walijitahidi kuujenga umoja katika taifa letu. Kuna mambo mengi yaliyowasaidia kuujenga umoja huu: Tulikuwa na chama kimoja cha siasa. Chama kilitunga sera na kutoa vision. Hivyo chama kilikuwa ni chombo kimojawapo cha kuujenga umoja wa taifa letu. Ingawa kulikuwa na watu wachache walioupinga mfumo wa chama kimoja, hawakuwa tishio la kuuvunja umoja wetu. Walikuwa wapinzani wenye kulenga kujenga umoja wa kitaifa.

Waasisi wa taifa letu hawakuzitanguliza dini zao, jambo la kuabudu lilibakia kuwa la mtu binafsi. Watanzania walikuwa na dini, lakini Tanzania, haikuwa na dini – haikutawaliwa kidini. Jambo hili lilionekana wazi katika katiba ya nchi yetu. Mwalimu Nyerere, alikuwa mcha Mungu na Mkatoliki hodari, lakini hakuthubutu kujenga nyumba ya ibada ndani ya Ikulu.

Ukabila ulipigwa vita na utawala wa machifu ulifutiliwa mbali. Lugha ya Kiswahili ilipewa kipaumbele na kuwa chombo cha kuwaunganisha watanzania wote. Nchi ambazo zinatumia lugha za kigeni kama lugha zao za kitaifa, hadi leo zinapata shida ya kujenga umoja wa kitaifa. Ni watu wachache wanaozimudu lugha hizi za kigeni, walio wengi wanaendelea na lugha zao za kikabila jambo ambalo linafanya mawasiliano kuwa magumu. Mfano nchini Uganda, taarifa ya habari ili iwafikie wananchi wote inatangazwa kwenye lugha zaidi ya sita!

Jeshi la kujenga taifa lilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha vijana waliomaliza kidato cha sita na vyuo wa Tanzania nzima. Kipindi chote cha mafunzo ya vijana hawa uzalendo na umoja wa kitaifa ni mambo yaliyosisitizwa. Mfumo huu ulipunguza kasi ya ukabila, kasi ya ukanda, majivuno na kiburi. Jeshi liliwatendea vijana wote sawa, bila ya kujali mtoto wa tajiri, kiongozi na mtoto wa masikini, wasichana wala wavulana.

Mfumo wa elimu wa kuwasambaza vijana kwenye shule mbali mbali za mikoa ya Tanzania, ulisaidia kuwakutanisha vijana na kujenga umoja wa kitaifa. Vijana kutoka Kagera, walipelekwa kusoma Mtwara, Moshi au Dar-es-Salaam. Wa Kigoma, walipelekwa Arusha, Kagera, Musoma au Dodoma nk.

Mwenge wa huru ulibuniwa kwa malengo ya kujenga umoja wa kitaifa. Mbio za kuuzungusha Tanzania nzima, zilichochea cheche za umoja wa kitaifa.

Mwaka 1995, Tanzania, ilijiingiza katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Tunayoyashuhudia sasa hivi hakuna chama kinachoonyesha sera ya kujenga umoja wa kitaifa. Wapinzani wa leo ni tofauti kabisa na wapinzani wa zamani wakati wa utawala wa chama kimoja. Wapinzani wa leo pamoja na chama tawala cha CCM, wanaangalia zaidi umoja wa vyama vyao kuliko umoja wa kitaifa, wanatanguliza kuingia Ikulu, ruzuku, mbwembwe za madaraka na ushindani wa chuki na utengano. Wakati wanasiasa wa zamani walikuwa na sera ya uhuru na umoja, wanasiasa wetu wa leo wana sera ya ukoloni mambo leo (Utandawazi, ubinafsishaji, soko huria) na utengano.

Katika awamu ya pili ya utawala wa taifa letu tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini kuanzisha mtindo wa kujenga nyumba za ibada katika ofisi za serikali. Uteuzi wa viongozi kufuatana na dini zao. Dini ilianza kutangulizwa. Waheshimiwa wengine walianza kubadilisha dini zao kwa siri. Malumbano kati ya Waislamu na Wakristu yalishika kasi. Magomvi yalizuika kati ya Waislamu na Wakristu.

Mfumo wa elimu umevurugika, shule nyingi za binafsi zimeanzishwa na kuchochea watoto wengi waziweze kuivuka mikoa yao. Watoto wa matajiri hawasomi tena na watoto wa masikini. Kiwango cha elimu kimeanza kutofautiana na kuleta hatari ya kuanza kuunda tabaka katika taifa letu. Tabaka ni adui mkubwa wa umoja na amani. Baadhi ya watoto wameanza kuvuka mipaka ya nchi na kusomea Uganda, Kenya na nchi nyingine jirani kama Zambia na Malawi. Hii haiwezi kusaidia kujenga umoja wa kitaifa. Maana watoto hawa itakuwa vigumu kulelewa katika misingi ya utamaduni wa Mtanzania.
Jeshi la kujenga taifa limefutwa na Mwenge wa uhuru kimekuwa chombo cha kampeni! Badala ya kueneza amani katika taifa letu, Mwenge, wa huru umegeuka na kuwa chombo cha kusambaza virusi vya UKIMWI. Mwaka jana Mwenge, huu ulipowashwa mjini, Bukoba, uliacha kumbukumbu ya watu kubakwa ndoa kuvunjika, watu kufa na vitendo vingine vya kusambaza virusi vya UKIMWI.

Mfumo uliokuwa umejengwa na waasisi wetu wa kuunda umoja wa kitaifa umeanza kupotea! Ni wajibu wa kila Mtanzania kujiuliza: Ni nani adui wa umoja wetu? Kama nilivyosema hapo juu, ni vigumu taifa lolote kusimama bila ya umoja. Kama tunataka taifa letu liendelee kusimama ni lazima tukazane kujenga umoja.

Tukigundua adui wa umoja wetu ni lazima tumpige vita kwa nguvu zetu zote. Kati ya mambo ambayo yanaonyesha dalili za kutishia uhai wa umoja wetu ni dini! Na hasa hizi dini mbili kubwa katika Taifa letu, Uisilamu na Ukristu. Kabla ya kuendelea na makala hii ngoja nitoe nukuu ya mteolojia mmoja wa Brazil,Leonard Boff. Mteolojia huyu aliyekuwa padri mtawa wa Kanisa katoliki, alipambana na mifumo ya kanisa iliyokuwa inafumbia macho unyanyasaji, ukiukwaji wa haki za binadamu, uvunjaji wa umoja wa kitaifa, hadi akalazimishwa na utawala wa kanisa katoliki kuacha huduma ya upadri. Mteolojia huyu aliishia kufundisha kwenye vyuo vikuu nchini Brazil na kuunda jumuiya ndogo ndogo za Kikristu.

“Kueneza Injili hakuna maana ya kueneza mifumo ya Ukristu.
Kueneza Injili maana yake ni kuishi pamoja kama dada na kaka, kushirikiana katika kazi, kuwajibika kwa upendo katika maisha ya watu wengine, kuheshimu utamaduni, mila na desturi za watu wengine, maana kila utamaduni umejaa ukweli wa milele.

Kueneza Injili maana yake ni: kuishi, kulia, kucheka, kufanya kazi na kujiingiza kikamilifu katika maisha ya watu wengine ili sote kwa pamoja tupate wokovu” (Kutoka kwenye Sinema ya “On the Way Together.” Tafsiri ni yangu.”

Pale niliposema “Kueneza Injili”, unaweza kuweka neno “Kueneza imani mpya kwa watu wengine”. Nikiangalia hali ya sasa hivi ya nchi yetu ninashawishika kukubaliana na maneno ya Leonard Boff.

Wakati tunajianda kwa uchaguzi mkuu mwaka huu. Majadiliano makali yanaendelea. Waislamu wanamtaka rais Mwislamu na Wakristu wanamtaka rais Mkristu. Maoni haya yanafunika hekima na busara yote. Si uwezo wa mtu na wala si mapenzi ya mtu katika taifa lake. Jambo muhimu ni dini! Haya si maoni ya kujenga umoja na wala haya si mawazo ya waasisi wa taifa letu.

Bahati nzuri tuliyo nayo ni kwamba hata mfumo wa vyama vingi umeanza chini ya uongozi wa waasisi wa taifa letu ndio maana hakuna vyama vya kisiasa vya kidini. Lakini tunakoelekea jambo hili litakuja tu! Kama tumeanza kujiuliza rais anatoka dini gani, utafika wakati waka kujiuliza rais anatoka kwenye chama cha dini gani. Kuna nchi ambazo zina vyama vya kidini. Ili uwe mwanachama ni lazima uwe mfuasi wa dini au dhehebu Fulani. Nchi hizi hazisifiki kwa umoja wa kitaifa. Mfano nchini Uganda, kuna chama ambacho ili uwe mwanachama ni lazima uwe Aglicana na kingine ni lazima uwe Mkatoliki na kingine Mwislamu au dini ya kujitegemea kama ya Joseph Konny.

Chimbuko la tatizo ni wale walioeneza imani hizi za kigeni katika nchi za Afrika. Badala ya kueneza imani walieneza mifumo ya dini zao. Na kila dini ilishikilia kuwa ndiyo yenye wokovu Na malengo hayakuwa ya kuishi kama dada na kaka, bali bwana na mtwana! Hakukuwa na ushirikiano katika kazi za kila siku wakati wa kueneza dini hizi za kigeni wala uwajibikaji wa wageni katika maisha ya watu wenyeji Historia inatueleza jinsi Ukristu na Uislamu zilivyoenea duniani kote kwa upanga, chuki na ubaguzi. Dini hizi zilifuta utamaduni, mila na desturi za watu wengine. Dini hizi hazikucheka na wanaocheka na wala hazikulia na wanaolia. Dini hizi hazikujiingiza kikamilifu katika maisha ya watu wengine ili watu wote wapate wokovu. Aliyezikumbatia dini hizi alipokelewa kwa mikono miwili, aliyezikataa alilaaniwa na wakati mwingine kuuawa!

Watanzania walio wengi wamejiingiza kwenye dini hizi mbili. Ni vigumu kuwaambia wazikimbie maana zinahatarisha umoja wa taifa letu. Ushauri wa pekee ni kuzilazimisha dini hizi zikakubali utamaduni wetu. Waasisi wa taifa letu walitujengea utamaduni wa umoja, utulivu na amani, hivyo ni lazima dini zetu ziheshimu utamaduni huu. Mtanzania Mwislamu ni Mtanzania, na ni lazima apate haki zote za Mtanzania. Aheshimiwe na watanzania wote kufuatana na karama zake alizonazo na mchango wake kwa taifa letu. Mtanzania Mkristu ni mtatanzania na ni lazima apate haki zote za Mtanzania, aheshimiwe na watanzania wote kufuatana na karama zake na mchango wake kwa taifa letu. Mtanzania anayefuata dini za jadi ni Mtanzania na ni lazima apate haki zote za Mtanzania, aheshimiwe na watanzania wote kufuatana na karama zake na mchango wake katika taifa letu.

Wale wanaoiona hatari iliyo mbele yetu ya kuuvuja umoja wetu, na hasa hatari ya dini za kigeni, ni lazima wafikirie kwa haraka jinsi ya kuunda chombo cha kujenga umoja wa kitaifa. Nilivyodokeza hapo juu vyama vya kisiasa tulivyonavyo kwa sasa haviwezi kujenga umoja wa kitaifa. Dini za kigeni ni adui mkubwa wa umoja wetu. Mifumo mingine imeharibiwa makusudi! Ni lazima sasa kuundwe chombo cha kujenga umoja wa kitaifa. Chombo ambacho hakitatawaliwa na vyama vya kisiasa, chombo ambacho hakitatawaliwa na dini, chombo ambacho hakitatawaliwa na matajiri, wawekezaji kutoka nje, ushawishi na nguvu kutoka nje ya nchi, ukabila wala ukanda .Chombo cha kujengwa na watanzania wenyewe na wala si chombo cha kujengwa na umoja wa mataifa au umoja wa nchi huru za Afrika. Chombo ambacho kitamfanya kila Mtanzania kumthamini Mtanzania mwenzake si kwa vile ni wa chama fulani, dini fulani au kabila fulani, bali kwa vile ni Mtanzania.

Kuna tetesi kwamba sasa hivi Wakristu wanaomba na kusali kwa nguvu zote ili Tanzania, isitawaliwe na rais Mwislamu. Na Waislamu wanasali kwa juhudi ili Tanzania, isitawaliwe tena na rais Mkristu! Kwa vile tumezoea kutawaliwa na unafiki, mambo haya hayasemwi na kuonyeshwa wazi – ni agenda za siri ambazo kila kikundi kinazitunza kwa uaminifu mkubwa. Mwelekeo huu si wa umoja na wala si wa kujenga amani.
Kazi kubwa ya rais ajaye mwaka huu ni kuunda chombo cha kujenga umoja wa kitaifa. Bila ya hivyo Tanzania, inaelekea kubaya.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment