RUBYA SEMINARI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2004

MIAKA 100 YA SEMINARI YA RUBYA: MATUNDA NI MENGI ZAIDI YA MAPADRI NA MAASKOFU!

Seminari ya Rubya iliyo kwenye uwanda wa juu katika wilaya ya Muleba ambayo ni mojawapo ya wilaya tano za mkoa wa Kagera, kaskazini mashariki ya Tanzania, ilianzishwa na Askofu John Joseph Hirith, miaka miamoja iliyopita.

Askofu Hirth, alizaliwa Alsace, Ufaransa. Alipadirishwa tarehe 15 Septemba 1878. Tarehe 4 Desemba 1889, alichaguliwa kukwa Askofu wa Nyanza. Wakati huo Vikariati ya Nyanza ilichukua eneo lote la Uganda, Rwanda, Kaskazini mwa Tanzania na Kenya mpaka mlima Kenya. Askofu Hirth, alikufa na kuzikwa Kabgayi Rwanda, tarehe 6 Januari 1931.

Maoni ya wachambuzi wa historia ni kwamba tendo la kwanza la sherehe za jubilee ya Rubya zilizofanyika Novemba mwaka huu, lingekuwa hija kwenye kaburi la marehemu Askofu Hirth, kule Kabgayi Rwanda. Maana huyu ndiye alikuwa mwanzilishi na mtetezi wa seminari ya Rubya. Bila yeye seminari hii isingesimama au ingeanza miaka ya baadaye kabisa. Mbali na kuianzisha seminari ya Rubya,Askofu Hirth, ndiye aliyepanda mbegu ya imani ya Kanisa katoliki katika Jimbo Katoliki la Bukoba na Rulenge na maeneo mengine yanayoyazunguka majimbo haya.

Baada ya hija ya Kabgayi, ndio lingefuata tendo la pili la kuyasherehekea matunda ya seminari ya Rubya. Kama sikosei tendo la kwanza bado halijafanyika! La pili ndio limefanyika Novemba mwaka huu!

Miongoni mwa matunda ya Rubya ni sifa za seminari hii kwa ufundishaji bora na matokeo mazuri ya mtihani wa kidato cha nne na sita. Ni kati shule kumi bora zinazofanya vizuri kila mwaka. Kati ya 1974-1976, ilishika nafasi ya kwanza kitaifa katika mitihani ya kidato cha nne. Mwaka wa 1993,1998 na 2000 ilishika nafasi ya pili na nafasi ya tatu kitaifa mwaka wa 1990 na 1999.

Matunda ya kujivunia ya Seminari ya Rubya ni:- -Hayati Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, ambaye alikuwa Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Dar-es-saam. Pia alikuwa Kardinali Mwafrika wa kwanza wa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.
- Mhashamu Askofu Gervasius Nkaranga, alikuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, sasa yuko katika monasteri ya Peramiho-Songea.
- Hayati Askofu Christopher Mwoleka, ambaye alikuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge.
- Mhashamu Askofu Nestory Timanywa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba.
- Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi,Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga.
- Mhashamu Askofu Desderius Rwoma,Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida.
- Mhashamu Askofu Method Kilaini,Askofu msaidizi wa Jimbo kuu katoliki la Dar-es-Salaam na bila ya kuwasahu wahashamu Maaskofu watakaoteuliwa siku za usoni!

Hadi kufikia jubilee, Seminari ya Rubya ilikuwa imezalisha mapadre 267 wa jimbo katoliki la Bukoba na majimbo mengine.

Seminari ya Rubya, imefanikiwa kutoa makatibu wakuu watatu wa baraza la maaskofu Tanzania katika vipindi tofauti, nao ni: Hayati Monsinyori Robert Rweyemamu, aliyekuwa miongoni mwa makatibu wakuu wa kwanza wa Baraza la maaskofu katoliki Tanzania 1967-1971, Baadaye Monsinyori Robert Rweyemamu, alifanya kazi kwa muda mrefu katika shirika la Kipapa la kueneza imani huko Roma kutoka 1972-1992. Katibu wa pili ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam Method Kilaini, alikuwa katibu wa Baraza la maaskofu kuanzia 1991-2000. Wa tatu ni katibu wa sasa wa Baraza la Maaskofu Tanzania Padri Pius Rutechura.

Seminari ya Rubya imebarikiwa kwa kutoa magombea (Rectors) wengi wa Seminari kuu za Tanzania nao ni:
- Askofu Damian Kyaruzi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, alikuwa Gombera wa Ntungamo Seminari tangia 1973-1978.
- Padri Deogratias Rweyongeza (Sasa hivi ni Monsinyori) alikuwa Gombera wa Seminari kuu ya Ntungamo tangia 1979-1984 na Kibosho 1986-1996. Na ndiye aliyekuwawa vice-chancellor wa kwanza wa chuo kikuu cha mt Augustine cha Tanzania. Hata na vice-chancellor wa sasa hivi Dk.Pd. Charles Khitima, wa Jimbo katoliki la Singinda ni matunda ya Seminari ya Rubya.
- Padre Emmanuel Mutabazi ( Jimbo katoliki la Rulenge) alikuwa Gombera wa Kibosho 1981-1984 na Ntungamo Seminari 1985.
- Padre Gaudiosus Rutakyamirwa, alikuwa Gombera wa Kibosho 1984-1986.
- Padre Vedasto Rugaijamu, alikuwa Gombera wa Seminari kuu ya Segerea 1986-1991.
- Padre Joseph Kamugisha, alikuwa Gombera wa Kipalapala Seminari 1988-1991.
- Gombera wa sasa hivi wa Segerea Seminari Padri Daudi Mubirigi na Gombera wa Sasa hivi wa Seminari Kuu ya Kipapala Padri Philibert Rwehumbiza ni matunda ya Rubya!

Aidha Rubya Seminari inajivunia kumtoa mjumbe wa kwanza Mtanzania kufanya kazi kwenye ubalozi wa Baba Mtakatifu kule Roma naye ni Monsinyori Novatus Rugambwa. Mwingine ni Padri Gosbert Byamungu, ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha kipapa cha umoja wa makanisa kule uswizi wakati huohuo yuko kwenye kamati yawale wanaomshauri Baba Mtakatifu katika masuala ya umoja wa makanisa ya Kikirstu(Ekumene).

Si nia ya makala hii kuchafua furaha ya Jubilii ya Seminari ya Rubya. Lengo ni lilelile la kuendelea kushangilia na kuipongeza Seminari ya Rubya kwa kufikisha miaka 100. Nia hasa ni kutaka kukumbusha kwamba matunda ya Rubya seminari ni mengi zaidi ya Kardinali, Maaskofu, Mapadre, Makatibu wakuu, Magombera na wajumbe wa Baba Mtakatifu. Jinsi linavyosahaulika kaburi la mwanzilishi wa Seminari marehemu Askofu Hirth, ndivyo yanavyosahaulika na matunda mengine ya Seminari ya Rubya.

Seminari ya Rubya ina matunda mengine mengi ambayo hata kama si mapadre, matunda haya ni matamu sana na wala si machungu! Rubya, imezaa waziri, mabalozi, maprofesa, wanauchumi, madaktari, wanasheria, mawakili na familia za mfano. Yeyote atakayeiandika historia ya Seminari ya Rubya ni lazima ayataje majina ya watu hawa sambamba na yale ya mapadri!

Kwa mfano kati ya mwaka 1904-1956 walikuwa wamepita wanafunzi 1004 kwenye seminari ya Rubya. Kati yao 58 tu ndo walipata daraja la upadri na 5 waliingia utawa wa wanaume. Namba kubwa ya wanafunzi waliopita Rubya kwa miaka hiyo walienda kuzijenga familia na kufanya kazi nyingine za kuchangia maendeleo ya taifa letu la Tanzania. . Miongoni mwao walifanya kazi kwa uaminifu mkubwa serikalini, kwenye mashirika mbalimbali ya serikali, dini na mashirika ya kimataifa.
Kufuatana na malezi bora ya seminari watu hawa walifanikiwa kujenga familia bora na za mfano. Hawa walikuwa chachu ya kueneza Injili. Baadhi ya mapadri na watawa wa kike tulionao sasa hivi wametokana na familia za waseminari wa zamani wa Rubya. Waliwasomesha watoto wao hadi kwenye ngazi ya juu – hawa watoto ndio madaktari, wanasheria na wataalam mbalimbali tunaowaona siku hizi! Kutoziunganisha familia hizi katika historia ya Seminari ya Rubya, ni kuisaliti historia na kuendeleza ufinyo wa mawazo.

Wakati wa kuazimisha Jubilee ya miaka 100 ya Seminari ya Rubya jimbo Katoliki la Bukoba limetoa kitabu chenye kurasa 144 kuelezea historia ya seminari. Jina la kitabu hiki ni: Seminari ya Mt. Maria ya Rubya Miaka 100 Iliyopita.

Licha ya kasoro nyingi za uhariri kitabu hiki kinalalia upande mmoja wa kuonyesha kwamba matunda ya Seminari ya Rubya ni mapadri na maaskofu peke yao! Huku ni kuipotosha historia, kuikosea haki historia ya Seminari ya Rubya na kuwakosea haki wale wote waliopitia Seminari ya Rubya. Mbali na picha ya Bwana Andrea Tham, mwalimu aliyejitolea kutoka Austaralia katika shirika la Kimisionari la Palm tangu Januari 2001 hadi Novemba 2002, hakuna picha nyingine ya mlei anayetajwa jina na kazi anayoifanya na maisha yake ya sasa hivi katika kitabu hiki!

“Miongoni mwa wakufunzi alikuwemo pia mlei bwana Laurent Ishungisa. Huyu alikuwa wa tabia njema na mstahimilivu. Aliacha alama nzuri ya kuajili walei.” (Seminari yaMt.Maria ya Rubya Miaka 100 Iliyopita Uk.30).

Mzee Laurent Ishungisa, ambaye bado anaishi hadi leo hii katika kijiji cha Nyakaiga-Bushangaro-Karagwe na ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Karagwe, ni Mkristu safi mwenye familia ya mfano. Bado ana tabia yake ileile njema na ni mstahimilivu. Picha ya familia yake ingelikipamba vizuri sana kitabu cha historia ya rubya. Huyu ni kati ya waumini wachache wa Tanzania, waliopata bahati ya kumtembelea Baba Mtakatifu na kuongea naye katika makao yake Makuu Vatican Roma. Ana picha nzuri ya kumbukumbu akiwa na Baba Mtakatifu Yohana wa 23, Kardinali Rugambwa, Askofu Nkaranga na Padri Justin Bamanyisa. Hata mahojiano tu na mzee Laurent Ishungisha, yangeipamba vizuri historia ya Rubya. Huyu angetupatia sehemu nyingine ya sarafu. Alikuwa mwalimu mlei kati ya waalimu padri tena Wazungu wa wakati ule. Huyu ana mengi ya kusema juu ya Seminari ya Rubya.

Ukrasa wa 140 wa kitabu cha historia ya Rubya kuna picha mbili za Wana-rubya Alumni waliokutana huko Dar-es-Salaam Segerea Seminari, na Wana-rubya Alumni wakikutana na Mh. Askofu Nistory Timanywa, kurasini 2004. Hakuna jina hata moja linalotajwa kwenye picha hizo za Wana-rubya Alumni! Labda mtu anayewafahamu atasema huyu ni Salva Rweyemamu, wa Habari Corporation, huyu ni Dr.Boniventure Rutinwa wa kitivo cha sheria cha Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam, au huyu ni Rweyemamu, mkurugenzi mtendaji wa shirika la SATF nk. Wana-rubya Alumni wa Dar-es-Salaam walichanga pesa nyingi za kufanikisha sherehe za Jubilei ya miaka 100 ya Rubya. Watu hawa wanajivuna kwa bahati waliyoipata ya kusomea katika seminari ya Rubya. Hawa ni sehemu ya historia ya Rubya. Seminari ya Rubya imechangia kuwajenga na kuwawezesha kuchangia kiasi kikubwa maendeleo ya taifa letu. Maelezo ya maisha yao, wako wapi, wanafanya nini yangeipamba vizuri historia ya miaka 100 ya Seminari ya Rubya.

Jambo jingine la kusikitisha linaloonyesha kwamba kitabu cha historia ya Rubya kinalalia upande mmoja ni picha za madarasa kuanzia mwaka wa 1930. Kwenye picha hizo yanatajwa majina ya wale tu waliofikia daraja la upadri. Mfano darasa la Prima Desemba 26,1964 lilikuwa na wanafunzi 8, wawili tu ndio walifikia daraja la upadre na hao tu ndio majina yao yanatajwa katika picha ya darasa. Mwaka 1966 walikuwa wanafunzi 29, wawili tu ndio walifikia daraja la upadre na hao tu ndio majina yao natajwa katika picha ya darasa! Ni hivyo hivyo kwa kila mwaka. Hii inaendeleza dhana potovu inayoelezewa kwenye kitabu chenyewe kwenye ukurasa wa 77:

“Katika muda huu ambapo mama yetu Rubya anasherehekea Jubilii ya miaka 100 tunayofuraha ya kuchambua, kutangaza na kuweka wazi mchango wake kwa kanisa la Tanzania na kanisa katoliki Duniani. Mpaka sasa hivi tunaposherehekea jubilee mama Rubya amelea wanafunzi 2930. Hata hivyo hatujataja wote, ila wale mashuhuri na wale ambao wametoa mchango mkubwa katika kanisa katoliki.”

Kwa maneno mengine watu mashuhuri na waliotoa mchango mkubwa katika kanisa katoliki ni mapadri na maaskofu, maana hawa ndio wamepewa nafasi ya pekee ya kuipamba historia ya Seminari ya Rubya. Hatuwezi kuwa na kanisa bila familia! Hivyo na Wana-rubya Alumni walioamua kujenga familia ni mashuhuri na wametoa mchango mkubwa katika kanisa katoliki. Hivyo wanayo haki ya kuipamba historia ya Seminari ya Rubya.

Mbali na mambo yote yaliyofanyika kama kumbukumbu ya miaka 100 ya Seminari ya Rubya, Jimbo Katoliki la Bukoba, lingefanya jambo moja la ziada ingawa ni la msingi. Mwanafunzi wa Rubya, mzee kuliko wote angepata zawadi! Kama sikosei, na kama historia inasema ukweli, mtu huyu si mwingine isipokuwa ni Padri Desderius Kashangaki. Aliingia Seminari ya Rubya mnamo mwaka wa 1923! Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alikuwa na umri wa mwaka mmoja! Alipata daraja la upadri 14.12.1941. Padri huyu mzee wa miaka 93, anaishi maisha mabaya kabisa. Hatunzwi na kanisa! Karibu miaka kumi sasa anatumikia adhabu aliyopewa na Askofu wake akiwa na umri wa zaidi ya miaka 80! Kama furaha ya Jubilee ya 100 ya Seminari ya Rubya haikuyeyusha hasira ya Mhashamu Askofu Nestory Timanywa, iliyodumu zaidi ya miaka kumi juu ya Padri Desiderius Kashangaki, basi matunda ya Seminari ya Rubya, si matamu! Ni matunda machungu na ni UBATILI MTUPU!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment