TUJIFUNZE KUTOKA KWA MZEE MANDELA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.

TUJIFUNZE KUTOKA KWA MZEE MANDELA

Mzee Nelson Mandela, ni kati ya watu wachache waliofanikiwa kuyaishi na kuyashika mafundisho magumu. Mafundisho ambayo walio wengi tunayaita ndoto, lakini tunayafundisha na kuwahimiza watu wengine wayashike na kuyafuata. Alipohukumiwa kifungo cha maisha, Mzee Mandela, alipokea hukumu hiyo bila ya woga, ni kitu alichokifahamu hata kabla ya kuanza mapambano na serikali ya makaburu. Alifahamu nguvu na uwezo wa serikali ya makaburu. Alijua walivyokuwa wameshikilia vyombo vya dola na silaha nzito nzito, alijua angekamatwa na kufungwa au kuuawa. Pamoja na kuyajua yote hayo aliamua kuendelea kupambana na makaburu kwa vile alitanguliza uhai wa taifa lake na wala si uhai wa maisha yake binafsi. Lakini pia alijua jinsi nguvu na uwezo wa makaburu vilivyokuwa vinaishia kwenye kuutesa mwili wake bila ya kuwa na uwezo wa kuigusa roho yake hata hivyo mafundisho magumu ambayo roho yake haikuwa na uwezo wa kuyakwepa yalikuwa mbele ya macho yake:
“ Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho..” (Matayo 5:28).
Makaburu waliutesa mwili wa mzee Mandela, alifanyishwa kazi za suluba, alidhalilishwa alipokonywa uhuru wake, alinyimwa uhuru wa kuwa na familia yake, alinyimwa uhuru wa mawasiliano, alipofiwa na mtoto wake wa kiume, alinyimwa ruhusa ya kuhudhuria mazishi yake. Unyama wote aliofanyiwa akiwa gerezani uliugusa na kuutesa kwa kiasi kikubwa mwili wake tu, lakini roho yake ilibaki madhubuti. Alipochaguliwa kuwa Rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika ya kusini huru, Mandela, alimshangaza kila mtu pale alipowakumbatia adui zake na kukaa nao meza moja ya chakula. Hakulipiza kisasi! Tulivyozoea, angelilipiza kisasi kama ilivyofanyika kule Rwanda, baada ya RPF kuingia madarakani au magomvi na kutoelewana miongoni mwa vyama vya kisiasa kwenye baadhi ya nchi za Afrika na Tanzania, ikiwemo! Unyama aliotendewa gerezani, haukuigusa roho yake! Mzee Mandela, amekuwa mwalimu wa kuwafundisha watu kuishi na kuyashika mafundisho magumu, mambo ambayo tumezoea kuyaita ndoto. Watanzania tuna utamaduni wa kuogopa mwenye nguvu na uwezo wa kuua mwili Pia tuna utamaduni wa kulipa kisasi, wawe ni viongozi wa dini au viongozi wa serikali, tabia hii ipo. Tujifunze kwa Mzee Mandela: Mwili unateswa, unanyanyaswa na kudhalilishwa na mwanadamu, lakini roho ya ukweli, amani na wema viko juu ya uwezo wa mwanadamu! Hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kuiua roho ya wema, hata kama mtu huyo angekuwa na nguvu za kidunia kama za Amerika! Pia tujifunze kwamba ukipambana na mtu, ukimshinda, mnashikana mikono na kukumbatiana – si kujenga chuki wala uhasama!

Watu wanaouona mwanga huu wameanza kugundua kwamba yale tunayoita mafundisho magumu na ndoto yanawezekana, Mzee Mandela, ametuonyesha mfano:
“ Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino’. Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la pili..” (Matayo 5:38-39).
Haya ni mafundisho magumu ambayo yamewashinda watu wengi hata na wale walioyafundisha na kuyaeneza. Hadi leo hii hata viongozi wa dini bado mafundisho haya yanawapatia shida. Bado wanashikilia ‘Jicho kwa jicho, na jino kwa jino’. Migogoro inayowakumba viongozi wa dini inasababishwa na kutokubali kupigwa shavu la kulia, na kugeuza la kushoto. Wakipigwa kofi, wanarudisha. Hii inavuruga amani na kuleta magomvi yasiyoisha. Mandela, hakurudisha kofi! Alisamehe! Mafundisho magumu yalikuwa mbele ya macho yake na roho yake iliyoandaliwa kwa umakini na kwa miaka mingi haikuwa na uwezo wa kuyakwepa:
“Mmesikia kwama ilisemwa: ‘Utampenda jirani yako, lakini utamchukukia adui yako.’ Lakini mimi nawaambieni ,wapendeni maadui wenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi…” ( Matayo 5:43-44).

Tunakumbuka jinsi Mzee Mandela, alivyowashauri Wamarekani: “Tumejifunza jinsi ya kuishi na maadui zetu, na nyinyi mjifunze kuishi na maadui zenu..”

Tume ya maridhiano ya Afrika ya Kusini, ilifanya kazi kwa uhuru na kumsikiliza kila mtu. Haikuwa na upendeleo wala kukikumbatia chama tawala. Haki ilitendeka kwa kila mwananchi na watu wote walifurahia kazi yake. Hizo zilikuwa mbinu za Mzee Mandela, za kukumbatia mafundisho magumu ya kumpenda adui.

Juma lililopita Mzee Mandela, alimpoteza mtoto wake wa kiume kwa ugonjwa wa UKIMWI. Kwa masikitiko makubwa(maana huyu ndio mtoto pekee wa kiume aliyekuwa amebakia) alitangaza wazi mbele ya vyombo vya habari bila aibu kwamba mtoto wake alikufa kutokana na ugonjwa wa UKIMWI. Hapa pia mafundisho magumu ambayo roho yake haikuwa na uwezo wa kuyakwepa yalikuwa mbele ya macho yake:
“ Jihadharini na chachu ya Wafarisayo, yaani unafiki. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila siri itajulikana. Kwa hiyo, kila mlichosema gizani, watu watakisikia katika mwanga, na kila mlichonong’ona, faraghani ,milango imefungwa ,kitatangazwa juu ya nyumba.” (Luka 12:1-3).
Hili limekuwa fundisho jingine kutoka kwa Mzee Mandela, la mafundisho magumu ambayo wengi wetu na hasa Barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara, tumekuwa tukidhani ni ndoto. Tumezoea kusikia watu mashuhuri wakifa kutokana na shinikizo la damu, kisukari, ugonjwa wa muda mrefu na ugonjwa wa ghafla nk. Ni nadra kusikia mtu mashuhuri amekufa kwa UKIMWI. Ugonjwa huu, umezungukwa na unafiki mkubwa. Ndio maana ugonjwa huu umekuwa wa hatari katika nchi zetu hizi masikini. Ugonjwa unafichwa na unafiki unaendelea kutawala. Hawa watu mashuhuri wanaokufa kwa shinikizo la damu wanatoa mwanya wa wenzi wao kuendelea kusambaza virusi vya UKIMWI, hakuna anayeshughulika kuchukua tahadhari maana shinikizo la damu si ugonjwa wa kutisha kama UKIMWI!! Matokeo yake ni janga kama tunavyoendelea kushuhudia. Ni lazima tumpongeze Mzee Mandela, kwa ujasiri wake na tuendee kujifunza kutoka kwake.
Hadharani, karibu kila mtu anapiga vita tendo la ngono na matumizi ya kondomu. Tendo la ngono linachukuliwa na wengi kuwa ni kitu cha aibu na labda kitu kisichofaa kwa mwanadamu! Sirini, karibu kila mtu (aliyemzima) anachangamkia tendo la ngono! Baadhi ya wanaopiga vita matumizi ya kondomu hadharani, wanazitumia kondomu mafichoni, wanawapotosha watu wengine na kuwaacha waangamie huku wao wanayalinda maisha yao. Unafiki mkubwa!

Mzee Mandela, alipougua ugonjwa wa saratani ya kibofu cha mkojo, alitangaza wazi. Hakuficha ugonjwa wake. Alipatiwa matibabu, na sasa anaendelea kuishi! Hapa Tanzania, tumewapoteza watu wengi kwa ugonjwa huu kwa sababu ya aibu na unafiki! Pia watu wanakufa kwa kuficha magonjwa ya zinaa yanayotibika kwa sababu ya aibu na unafiki. Magonjwa yakigusa sehemu za siri, watu wanakuwa na aibu. Aibu hii inatokana na mawazo ya kulichukulia tendo la ngono kama la aibu. Ingawa kuna ukweli kwamba si magonjwa yote yanayozishambulia sehemu za siri yanasababishwa na tendo la ngono. Baadhi ya watu wakiugua sehemu za siri, wanataja kichwa, tumbo na mgongo. Madaktari wanatibu kichwa, tumbo na mgongo, kumbe mgonjwa ana saratani ya kibofu cha mkojo au magonjwa mengine ya zinaa. Inapotokea bahati ya kuugundua ugonjwa, mgonjwa anakuwa amezidiwa na kufa! Aibu na unafiki vinasababisha vifo visivyokuwa vya lazima katika taifa letu na katika nchi nyingine za Kiafrika.

Kama tunataka kupambana na UKIMWI tuachane na unafiki. Kila Mtanzania aachane na unafiki na kuwa wazi. Mtu akifa kwa UKIMWI, tuseme wazi kama alivyofanya Mzee Mandela, ili watu wote wanaomzunguka marehemu na kuwa kwenye mtiririko wa mkufu wa mahusiano yake waanze kuchukua tahadhari. Mpaka sasa hivi silaha pekee dhidi ya UKIMWI ni Kinga. Kuna kinga za aina tatu: Uaminifu, kuacha kabisa tendo la ngono na kutumia kondomu. Tukiacha unafiki kinga hizi zinaweza kusaidia kupunguza maambukizo ya UKIMWI. Bahati mbaya kwa upande wa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, kinga hizi tatu zimegubikwa na unafiki mkubwa.

Ripoti za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulika kutetea haki za wanawake, yanaonyesha ongezeko kubwa la ukosefu wa uaminifu katika ndoa. Kesi za kufumaniwa zinaongezeka, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wadogo unaota mizizi, tabia za ushoga na usagaji zinaanza kujipenyeza, nyumba ndogo zinashika kasi ya kutisha na kuna ongezeko kubwa la watoto wa nje ya ndoa. Imegundulika pia kwamba hata wale wanaoendesha “porojo” za uaminifu kama kinga dhidi ya UKIMWI, wanaogelea katika dimbwi la nyumba ndogo na unyanyasaji wa kijinsia! Unafiki mkubwa!

Kuacha kabisa tendo la ngono, hii ni siri ya mtu na Mungu wake. Hakuna mwenye uwezo wa kuhakikisha jambo hili – labda kwa vile maendeleo yanashika kasi, kutagunduliwa mtambo wa kuwapima wale wasiofanya tendo hili hadi kufa kwao! Takwimu zinaonyesha kwamba hata watu wanaoaminika kuacha kabisa tendo la ngono wanakufa kwa ugonjwa wa UKIMWI. Kwa vile ugonjwa huu una njia nyingi za kuambukiza, tunabaki kujituliza (unafiki) kwamba “watakatifu wa Mungu” waliambukizwa ugonjwa huu kwa njia nyingine na wala si ngono. Kwa mantiki hii wenzi wao hawachukui tahadhari yoyote na wanaendelea kusambaza virusi.

Unafiki unaoyazunguka matumizi ya kondomu, unajulikana. Kuna wale wanaojitangaza kwamba wanatumia kondomu, lakini hawazitumii – ni unafiki wa kutafuta pesa na kuwafurahisha wahisani. Watu hawa ni hatari, wanatoa matumaini yasiyokuwepo! Kuna wale wanaotumia kondomu, siku za mwanzo za kukutana na wapenzi wao, wakizoeana kidogo, hata bila ya kupimwa, wanazitupilia kondomu mbali na kuendelea na tendo la ngono bila ya kinga kwa kisingizio cha kujenga uaminifu katika kuzoeana! Hawa pia ni hatari, maana wanaongozwa na unafiki. Kumzoea mtu, haina maana hawezi kuwa na virusi na ikizingatiwa kwamba mtu mmoja anaweza kuwa na watu zaidi ya kumi wa kuzoeana naye! Kuna wale wanaopiga vita matumizi ya kondomu, likini wao wanazitumia, hawa si hatari tu bali ni mashetani, maana wanajikinga na kuulinda uhai wao wakati jamii nzima inateketea. Kuna wale wanaoeneza uvumi kwamba virusi vya UKIMWI, vinawekwa kwenye kondomu, kwamba ni mbinu za Wazungu kuwamaliza Waafrika! Kama ni kutumaliza mbona Wazungu wana nafasi nyingi? Madawa tunayotumia yanatengenezwa na Wazungu, cocacola, inatengenezwa na Wazungu, vyakula mbali mbali vinatengenezwa na Wazungu hata na computer ninayoitumia kuandika makala hii inatengenezwa na Wazungu, wakitaka wanaweza kuweka vitu vya kumaliza uhai – kwa nini watumie kondomu, kumaliza maisha ya Waafrika? Wengine wanasema kondomu ni miradi ya watu, wanatengeneza pesa. Wataalam wengine wanasema virusi vinapenya kwenye kondomu. Ni mengi, mengine ya kweli na mengine ni unafiki mtupu!

Lengo la makala hii ni kuonyesha jinsi tulivyo na mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mzee Mandela. Taifa letu la Tanzania halijawa na mwelekeo mzuri wa kupambana na ugonjwa huu wa UKIMWI. Bahati mbaya viongozi wetu wa dini na serikali ni woga. Hatujapata viongozi wa kuyashika na kuyaishi mafundisho magumu kama alivyofanya Mzee Mandela. Hatujapata viongozi wasioogopa macho na masikio ya watu, viongozi wasiojali kudhalilishwa na ikibidi kuupoteza uhai wao katika harakati za kutetea ukweli na kupingana na unafiki.

Tunapojifunza kutoka kwa Mzee Mandela, ni lazima tumwangalie yeye na historia yake. Si kwamba misimamo yake hii ya kuishi na kuyashika mafundisho magumu, ilimnyeshea kama mvua. Ni mtu aliyefanya maandalizi, ni mtu aliyeitafuta elimu akiwa na malengo katika maisha yake – hakusoma tu kwa vile kusoma ni lazima – hakusoma kuishinda mitihani, bali alisoma kwa vile alikuwa na lengo la kuikomboa nchi yake. Lengo hili lilijaa kwenye roho
yake. Hata ungeupiga na kuumiza mwili wake, usingeliligusa lengo lililokuwa kwenye roho yake. Alijiandaa kwa maamuzi magumu –alijua jinsi njia ya kulifikia lengo lake ni kupitia kwenye maamuzi magumu. Alijifunza na kujiandaa kulitanguliza taifa lake kwa kila kitu. Hakuangalia tumbo lake, cheo chake au biashara yake (mambo ya mwili) aliangalia uhai wa taifa zima(mambo ya kiroho) Ndiyo maana hata leo katika uzee wake bado anafanya maamuzi magumu ya kutangaza ugonjwa wa mtoto wake ili achangie kuliokoa taifa zima!

Tunapojiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka huu, tujiulize ni nani hapa Tanzania, ataweza kuyaweka mafundisho magumu mbele ya macho yake na kuamua kuyafuata. Ni nani atalitanguliza taifa kabla ya kulitanguliza tumbo lake, familia yake, kabila lake na dini yake? Ni nani atashinda uchaguzi akakaa meza moja na wapinzani wake bila kulipiza kisasi? Ni nani ataangalia uhai wa taifa na kuteua watendaji wa serikali bila kuangalia vyama vyao vya siasa, bila kuangalia mchango wao katika kampeni, bila kuangalia sura zao na dini zao akaongozwa kwa kuangalia uwezo na uaminifu wa mtu kwa taifa letu? Ni nani atapambana na ugonjwa wa UKIMWI, bila woga na bila kuogopa kupoteza “mapenzi” kwa viongozi wa dini? Ni nani atapambana na rushwa, umasikini na kuangalia maendeleo ya watanizaania wote. Ni nani mwenye maandalizi kama haya?

Na,
Padri, Privatus Karugendo.

1 comments:

Mija Shija Sayi said...

Padri Karugendo asante kwa mada nzuri. Kwa kweli waafrika tumezidi lawama unafiki na chuki za bila sababu na ni kitu hiki ndo kinachoturudisha nyuma. Sasa unadhani tufanyeje ili kubadilisha mwelekeo wa taifa letu?

Mungu ambariki Mzee Mandela.

Post a Comment