TUKIBADILIKA YAWEZEKANA, VINGINEVYO....

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.

TUKIBADILIKA YAWEZEKANA,VINGINEVYO….

Nimeguswa kwa namna ya pekee na makala ya “Mwandishi wetu” RAI 587 “Tukibadilika Yawezekana, vinginevyo….”. Bahati mbaya au ni makusudi mazima mwandishi hakutaja jina lake. Ingekuwa ni vyema kufikia mahali majadiliano kama haya yakazaa kitu kinachoonekana cha kuchangia maendeleo ya taifa letu. Ili jambo kama hilo litokee, ni lazima watu kufahamiana na kujadiliana na karibu, wakati mwingine kufahamiana kunaweza kusaidia kuondoa “Ndoto”!

Sikuguswa na makala hii kwa vile mwandishi anaunga mkono maoni yangu nimekuwa nikiguswa na makala zote zinazochangia juu ya maoni yangu, hata zile za kunitukana na wakati mwingine kunidhalilisha zimekuwa zikinisaidia kufikiri na kutafakari maana hayo ndiyo majadiliano na uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake. Mchango wa “Mwandishi wetu” umenichonyota kwa vile anagusia kitu kinachoisumbua akili yangu na roho yangu. Ni imani yangu kwamba kitu hiki kinawasumbua pia na baadhi ya watanzania wengine: Kuijenga jamii inayoishi kwa kutenda Haki, Wema na Huruma. Mwandishi wa makala hii aliguswa na makala yangu ya “Mkia wa Shetani”. Niliandika makala hii baada ya kupata fundisho; niliwatetea vibaka, wakanifundisha kwa kunikwapulia wallet yangu Niliumia kuibiwa, lakini hadi leo hii siamini kwamba ni haki kuwachoma moto vibaka. Badala yake ninajiuliza: Ni kwa nini tuna vibaka katika jamii yetu, kwa nini tuna majambazi, wezi na walarushwa, kwa nini tumeshindwa kuijenga jamii inayoishi kwa kutenda haki, wema na huruma? Sina haja ya kuandika kwamba hadi leo vibaka wanachomwa moto, kupigwa hadi kufa na wananchi wanaendelea kujichukulia sheria mkononi. Si kwamba ninajifanya nabii, bila mabadiliko, hali ikiendelea jinsi ilivyo, kasi ya kuwachoma vibaka itaendelea. Jambo la kuogopesha ni kwamba dalili za kuacha kuwachoma vibaka wa kukwapua simu, vijisenti, saa na mikufu na kuanza kuwachoma vibaka wa uchumi wa taifa letu, vibaka wanaoiba mabilioni, zinaanza kujitokeza. Hii ni hatari maana vibaka wa uchumi wana uwezo wa kujilinda. Historia inatuonyesha kwamba wanyonge wanaoonewa wakishirikiana wanaweza kupambana vilivyo na vibaka wa uchumi Tukio kama hilo linajulikana kama vita ya wenyewe kwa wenyewe Si lazima kutoa mifano. Tuendelee kufanya mchezo, matukio mabaya(ya uzembe) ni mwalimu mzuri. Lengo la makala hii ni kutaka kushirikiana na “Mwandishi wetu” na wengine wanaojali kutafakari; “Tufanye nini ili tubadilike?”. Ni chombo gani au ni mfumo gani wa kutusaidia kuleta mabadiliko? Huwezi kuleta mabadiliko katika jamii bila ya kuwa na chombo au mfumo.

Je ni watu gani wa kutusaidia kuleta mabadiliko? Ni kweli kwamba watanzania wote ni lazima tubadilike! Ili mabadiliko ya kweli yatokee ni lazima kila mtu ajibadilishe yeye mwenyewe. Kosa kubwa linalojitokeza ni kwamba daima tunataka wengine wabadilike. Tunataka watu waache uzinzi, ujambazi, rushwa. Je ni kiasi gani kila mtu anahoji nafsi yake juu ya uzinzi anaoufanya yeye mwenyewe? Kama hili lingekuwa linatokea, basi uzinzi ungepungua. Je ni nani anaihoji nafsi yake kuhusu kutowatendea watu wengine haki, wema na huruma? Hili lingetokea basi ujambazi na rushwa vingepungua. Udhaifu wetu ni kwamba tunataka tutendewe haki, wema na huruma, hatuangalii ni kiasi gani sisi tunawajibika kwa wengine! Mtu wa kufikia hatua ya kuanza kuihoji nafsi yake ni lazima awe ameandaliwa, nia lazima awe ameelekezwa, ni lazima awe amepitia katika mfumo wa aina fulani, ni lazima awe anaishi kwa malengo, ni lazima awe anaguswa na maisha ya jamii nzima. Kwa vile mwanadamu ana tabia ya kusahau, mifumo inasaidia kumkumbusha!

Mtu ambaye ameonja adha ya kuomba chumvi kwa jirani, akipatana nafasi ya kuingia madarakani atahakikisha anashiriki kikamilifu kurekebisha mifumo ya uchumi ili watu wasipate adha ya kuomba chumvi kwa jirani. Mtu ambaye ameonja adha ya kugombana na mwenye nyumba kwa kushindwa kulipa pango, akifanikiwa kuingia madarakani atapigia debe mpango wa kujenga nyumba nafuu kwa wananchi. Mtu anayejua adha ya kushindwa kulipia matibabu, akifanikiwa kuingia madarakani atajitahidi kupiga kelele juu ya huduma bora za afya. Mtu anayejua adha ya taabu ya usafiri, akiingia madarakani atajitahidi kuboresha huduma ya usafiri nk. Lakini kwa vile mwanadamu anabaki ni mwanadamu, aliyeonja adha anaweza akajisahau akiingia kwenye neema, kama kuna mfumo mzuri, ni rahisi kumsuta na kumrekebisha mtu aliyeonja adha mbali mbali katika jamii kuliko yule anayeshuka kutoka mbingu nyingine!

Nimetoa mifano hii ili kuonyesha kwamba wakati tunalilia mabadiliko katika taifa letu, ni bora kujiuliza ni nani wa kutuletea mabadiliko, pamoja na kwamba tunahitaji mifumo na vyombo, na pamoja kwamba ni lazima kila Mtanzania abadilike, lakini kuna watu muhimu wa kuhimiza mabadiliko. Mtu asiyejua adha ya kuomba chumvi kwa jirani, asiyejua adha ya kufukuzwa kwenye nyumba ya kupanga, asiyejua adha ya usafiri, anayeugua mafua akakimbizwa kwenye hospitali za London na Afrika ya Kusini, asiyejua adha ya usafiri, anayesomesha watoto wake nje ya nchi, anaweza kuchangia mabadiliko gani katika nchi masikini kama ya Tanzania? Kuna msemo kwamba, Ndege wenye bawa moja huruka pamoja! Mabadiliko ya kweli ni ya ndege wanaoruka pamoja!

Viongozi wetu wa serikali, viongozi wetu wa dini, hawaguswi na adha zote nilizozitaja na ambazo sikuzitaja, wana mabawa tofauti na jamii! Wanaruka kivyao na jamii inaruka kivyake. Hali kama hii haiwezi kuleta mabadiliko!

Mwandishi wetu anasema: Utawala bora hauwezi kuwapo kama hakuna mtawala/kiongozi bora. Utawala bora ni ule tu unaojali haki za raia, maslahi ya raia au taifa na unaongoza watu kufikia matarajio yao, utawala bora ni kujikana na kujitoa kwa dhati utumike kwa wengine. Kwa kuyazingatia mawazo kama haya waasisi wa taifa letu waliamua kuanzisha chama cha siasa cha CCM. Kirefu chake: Chama Cha Mapinduzi. Kamusi ya Kiswahili sanifu inaelezea neno Mapinduzi: Mabadiliko ya haraka katika mfumo wa maisha ya jamii ambayo huwanufaisha watu walio wengi. Kwa mtu anayeona mbali anaweza kusema CCM, ni chama kilichokuwa kimelenga mabadiliko. Kililenga kujenga jamii yenye kutenda haki, wema na huruma. Ni chama kilichokuwa kimelenga kufuta mifumo ya kikoloni ya unyanyasaji ubaguzi, matabaka, kupunguza ufa kati ya walionacho na wasiokuwa nacho. Ni chama kilichokuwa kimelenga kuleta mapinduzi katika maendeleo ya taifa letu; mapinduzi katika huduma za kijamii, watu wapate maji, umeme, shule, hospitali, makazi bora, chakula cha kutosha na kuumiliki uchumi wa nchi yao. Sera ya ujamaa na kujitegemea ilikuwa inalenga kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa letu. Hivyo tunapotafakari juu ya ni chombo gani cha kutusaidia kuleta mabadiliko katika nchi yetu kila mtu angekuwa anajibu kwa haraka hata bila ya kufikiria kwa, ni CCM. Kwa vile bado tunajiuliza ni chombo gani kitusaidie, ni wazi kwamba CCM, imeshindwa kutekeleza malengo yake. Badala ya kusema Chama Cha Mapinduzi, tunasikia Chukua Chako Mapema! Hali hii ya kutokielewa chama, imezaa matatizo mengi katika jamii yetu. Rushwa, imeongezeka na kuwa na mizizi kwa sababu ya Chukua Chako Mapema. Ni wanaCCM wachache, labda silimia mbili wanaofahamu maana ya neno “Mapinduzi”. Asilimia kubwa ni Chukua Chako Mapema. Malengo ya waasisi wa chama yametupiliwa mbali. Sera ya Ujamaa na kujitegemea, imefutwa! Walioifuta hawakuwa na uwezo wa kubuni mfumo mwingine. Wameliacha taifa kwenye “utupu” unaoendelea kuzaa matatizo juu ya matatizo. Ninalotaka kusema ni kwamba CCM,(Sina maana ya Chama Cha Mapinduzi, cha Mwalimu, ninaongelea kivuli tulichonacho leo hii) haiwezi kutusaidia kuleta mabadiliko.

Vyama vya upinzani ni vyama vya kuipinga CCM na wala si vyama vya kuleta mabadiliko. Vyama hivi vinatumia nguvu nyingi kupambana na CCM, badala ya kuutumia muda uliopo kuunda sera na mifumo ya kusaidia kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa letu. Ni mapambano yaleyale ya Chukua Chako Mapema. Ingawa si haki kuvipima vyama vyote kwenye mizani ile ile, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba hakuna chama chenye mfumo wa kuleta mapinduzi ya kweli. Mfumo wa kupunguza adha ya kuomba chumvi na wananchi kuumiliki uchumi wa taifa. Mfumo wa kujenga utaifa na uzalendo. Mfumo wa kufuatilia kila Mtanzania na kumbadilisha awe raia mwema wa kutenda haki, wema na huruma kwa ndugu zake.

Wale wote wanaotaka kuingia Ikulu. Hakuna hata mmoja mwenye mfumo wa kuleta mabadiliko ya kweli. Ni nani na mfumo wake unapatikana wapi ili tuujadili na kutoa maoni?. Mimi binafsi nisingemlaumu Mheshimiwa Frederick Sumaye, kwa kutumia pesa za serikali kuendesha kampeni ili chama chake kimpendekeze kugombea urais. Kama ana mfumo mzuri wa kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa letu, ni ruhusa kutumia pesa zote hata kama zikiisha. Tatizo langu si kwa Sumaye, ni kwa wote hata wale wanaotumia pesa zao walizoziiba kutoka serikalini, wanataka kuupata urais ili kufanya nini? Wana mfumo gani wa kule mabadiliko ya kweli katika taifa letu? Si lazima kuwasikiliza, tunajua kusoma! Tusome wapi aina ya mfumo wao, mawazo yao na sera zao? Wana nini cha kutuelezea zaidi ya matumbo yao, mali walizonazo, wake zao na dogodogo, utukufu wao na mbwembwe zao? Ni nani kati yao anaijua adha ya kuomba chumvi kwa jirani au kulala njaa?

Dini zetu zimeshindwa kutuletea mabadiliko. Au labda niseme kwamba si lengo la dini hizi kuleta mabadiliko katika taifa letu. Tuchuke mfano wa kibaka. Huyu kibaka akifanikiwa kukwapua pesa bila ya kuonekana, atakwenda kanisani Jumapili au msikitini Ijumaa, kusali, atatoa sadaka, itakubaliwa na kubarikiwa na kiongozi wa Ibada. Kibaka, huyu ataungama na kuondolewa dhambi zake. Kwa vile hakuna mfumo wa kumfuatilia kibaya huyu, kujua matatizo yake, maisha yake, kipato chake nk., ataendelea kufanya kazi yake ya kuiba. Siku atakapokamatwa na kupigwa hadi kufa, ni wengi watakaoikosa huduma yake, kuanzia kwa kiongozi wa ibada hadi familia yake. Viongozi wetu wa dini wanaijua mishahara ya viongozi wetu wa serikali, mbona hawatusaidii kuhoji ufa uliopo kati ya viongozi wa serikali na wananchi, mbona hawahoji michango mizito inayotolewa na viongozi wa serikali kusaidia taasisi za kidini? Wanakaa kimya na kwa unafiki wanalaani rushwa!

Viongozi wa dini wameshindwa kubuni mfumo wa kufundisha elimu ya dini na maadili katika shule na vyuo. Huwezi kuleta mabadiliko ya kweli bila kuwafundisha na kuwaelekeza vijana. Haitoshi kuendesha mahojiano kwenye luninga, ni watanzania wangapi wenye uwezo wa kununua luninga? Haitoshi kuhubiri Jumapili na Ijumaa, ni waumini wangapi wanakwenda kwenye Ibada? Walio wengi wanautumia muda wa kenda kwenye Ibada kupamba na ugumu wa maisha. Viongozi wa dini hawaijui adha ya kuomba chumvi na kushinda njaa. Waumini wanaofanikiwa kuujua ukweli huu, wameanza kupuuzia kwenda kwenye Ibada, labda uwe msiba, ndoa au sherehe kubwa kama Iddi ,Christmas na Pasaka! Mfumo wa kufundisha elimu ya dini mashuleni na vyuoni ungesaidia.

Kuna NGO mbali mbali katika jamii yetu. Nyingine zinahudumia watoto yatima, nyingine watoto wa mitaani, nyingine zinatetea haki za akina mama, nyingine za kulinda mazingira nk, hakuna NGO, ya kuhimiza mabadiliko katika taifa letu. Sijasikia NGO, yenye malengo ya kuwaandaa watanzania kulipenda taifa lao, kutoa maisha yao katika kulijenga taifa lao, kutenda haki wema na huruma na kufundisha maadili mema. NGO, inayoweza kumfuatilia kibaka na si kumsaidia kujirekebisha tu bali kumsaidia kujitegemea. NGO, inayoweza kumsaidia changudoa kubadilisha maisha yake.

PCB, inasaidia kuwafichua wale wanaokula rushwa. Ingawa sina uhakika inasaidia kiasi gani na wale wanaofichuliwa wanachukuliwa hatua gani. La msingi si kuwafichua wala rushwa, ni kuwa na mfumo wa kuidhibiti rushwa. Mfumo wa kujenga jamii ya watu wanaowajibika. Bila hivyo, hata PCB, kinaweza kugeuka chombo cha wala rushwa.

Tunamuhitaji kiongozi anayeyaona haya. Kiongozi mwenye uwezo wa kubuni mfumo na kutengeneza chombo cha kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa letu. Kiongozi ambaye hawezi kufungwa mikono na miguu na chama chake cha siasa, ambaye hawezi kunyamazishwa na nguvu za pesa, ambaye hawezi kutekwa na nguvu za viongozi wa dini, ambaye si mlevi wa madaraka na ambaye anajua kuutawala vizuri mwili wake, ambaye anasoma, kuandika na kufanya utafiti wa mara kwa mara, kiongozi mwanamapinduzi na mwenye kuchochea mabadiliko katika mawazo ya kila Mtanzania.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment