TUTAFAKARI UTENZI WA SALIMU ALLY

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2004

TUTAFAKARI UTENZI WA SALIMU ALLY

Utenzi uliotungwa na kusomwa na Salimu Ally wa Morogoro, siku ya mwanzo ya ufunguzi wa semina ya viongozi na watendaji wa umoja wa vijana wa CCM mjini Dodoma, si wa kupuuza. Lisemwalo lipo, na kama halipo litakuwa njiani. Utenzi huu unailenga CCM na wanaCCM. Lakini kufuatana na maelezo ya mzee wa CCM niliyekutana naye juzi mjini Mwanza, CCM inazaa marais, CCM inazaa mawaziri, CCM inazaa wabunge wengi, CCM inaongoza serikali….., maana yake ni kwamba CCM inashikilia hatima ya Taifa letu mikononi mwake. Kwa maneno mengine utenzi wa Salimu Ally, unalenga hatima ya Taifa letu la Tanzania.

Gazeti hili toleo la 577,lilinukuu beti kama nne za utenzi wa Salimu Ally. Sina uhakika kama utenzi mzima ulikuwa na beti nne tu au hizi ndio zilikuwa zimeubeba ujumbe mzito wa utenzi huo. Mambo muhimu yanayochomoza kwenye utenzi huu ni: Bila kufuata katiba, CCM itaelekea kugumu. Matokeo ya kutofuata katiba ni vurugu, makundi, madhalimu na matapeli.

“Kiendako ni kigumu, chama chetu CCM, machungu sio matani taweza kutufikia, machungu tutayapata, huzuni mwisho kujuta, ikiwa hatutafuata katiba nawaambia”

Ubeti huu una ujumbe wote. Ingetosha Salimu Ally, kuachia hapa. Beti nyingine tatu ni ufafanuzi wa ubeti wa kwanza. Salimu Ally, hakupenda liwe fumbo. Waswahili wanasema, “Fumbo mfumbie mjinga……”. Ingawa wale wote wanaowania madaraka na uongozi katika Taifa letu kupitia chama cha CCM ni welevu watupu, ukweli unabaki palepale kwamba uchu wa madaraka unaweza kumgeuza mwelevu kuwa mjinga na mpumbavu wa mwisho. Salimu Ally, anashuhudia jambo hili katika utenzi wake pale anaposema: “Huko kuna madhalimu, waliopungua fahamu….”. Uchu wa madaraka unaweza kuibadilisha roho ya mtu mwema kuwa mbaya na kumfanya mtu kutenda kama mnyama. Uchu wa madaraka unasababisha vita, umwagaji damu wa watu wasiokuwa na hatia. Uchu wa madaraka ni hatari kubwa katika jamii yoyote ile. Hapa kwetu Tanzania, hatari hii imekuwa ikielekezwa upande wa vyama vya upinzani; kwamba wapinzani wana uchu wa madaraka, kwamba tukivichagua vyama vya upinzani, amani itapotea, vurugu itatawala, tutaingia vitani na damu nyingi itamwagika. Tunapoelekea uchaguzi wa 2005, tunapata picha tofauti. Uchu wa madaraka umejikita ndani ya CCM. Ni lazima tutafakari kwa makini beti hizi katika utenzi wa Salimu Ally, na tutafute la kufanya haraka iwezekanavyo:

“Tuendako ni kuzito, kuna kimbunga na moto, kuna misitu mito, yenye mamba nakwambia. Huko kuna madhalimu, waliopungua fahamu, wanaiweka sumu, CCM nawaambia.

“Huko kuna matapeli, waliokuwa tayari, kupewa shilingi mbili, waiuze Tanzania. Tupo nao watu hao, chama wanasema chao, na wengine wana vyeo, vikubwa nawaambia.

“Tusizifuate vurugu, za watu wenye majungu, watatugawa mafungu, tushindwe kuendelea. Mheshimiwa Wiliamu(Mkapa) wakemee madhalimu, wanaotaka hujumu, chama chetu nakwambia. Usiwaonee aibu, ambao wanajaribu chama kutuchafulia.”

Penye majungu, madhalimu, makundi, hujuma, matapeli, wauza nchi, hakuna uzalendo. Uzalendo ukitoweka, amani inapotea na hatari kubwa kuikumba jamii. Mifano ni mingi katika nchi mbali mbali zinazotuzunguka.

Nionavyo mimi, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake maana swala hili linatuhusu wote tunaoamini kwamba sisi ni watanzania, ni ukosefu wa uzalendo katika chama cha CCM. Ni kutanguliza chama na maslahi binafsi, bila ya kulitanguliza taifa letu la Tanzania. Makundi yote yanayojitokeza ndani ya chama cha mapinduzi si ya kizalendo. Ni makundi ya maslahi binafsi majungu, utapeli, vurugu na hatimaye vita!

Kundi la Wazanzibari ndani ya chama cha Mapinduzi limegawanyika pia katika makundi mawili ya “vijana” wa CCM na “wazee” wa CCM. Katika hali ya unafiki na kudanganyana “vijana” wa CCM wa visiwani na “vijana” wa CCM wa bara wanakuwa na sauti moja. Vilevile “wazee” wa CCM wa visiwani na “wazee” wa CCM wa bara wanakuwa na sauti moja. Inapogusa maslahi binafsi ya Zanzibar “vijana’ wa CCM wa visiwani wanakuwa kitu kimoja na “wazee” wa CCM wa visiwani! Wazanzibari, wana utamaduni wa kuficha makucha yao na kusubiri kura yao ya turufu kwenye halmashauri kuu na mkutano mkuu.

Utaratibu wa nchi yetu, ambao si wa kikatiba. Ni utamaduni na sasa umezoeleka hivyo, ni kwamba rais akitoka bara, uchaguzi unaofuata ( baada ya miaka kumi) rais anatoka visiwani. Mwaka kesho anapomaliza rais Mkapa, ni wazi Wazanzibari wanasubiri zamu yao! Jambo hili halisikiki wala kupigiwa kelele na Wazanzibari. Kawaida yao ni wapole na wanyenyekevu lakini ni wajanja. Wanaisubiri kura yao ya turufu. Ukiuangalia muundo wa muungano. Bara tumetoa rais mara mbili, Unguja mara moja na Pemba, bado. Dk. Ali Mohammed Shein, ni mpemba. Ingawa yeye haonyeshi wazi kutaka kuwania urais wa muungano, lakini kura ya turufu kwa kulinda maslahi binafsi ya Zanzibar, inaweza kumwangukia wakati wowote ule. Ingawa jambo kama hili halitegemewi kutokea maana “vijana’ wa CCM wa bara walimsaidia sana kijana mwenzao Amani Karume, kwenye uchaguzi wa 2000, wakitegemea naye alipe fadhila wakati wa uchaguzi wa 2005, kwa kutumia kura ya turufu ya Wazanzibari, kumpitisha mgombea urais kijana. Kati kura za maoni kule Zanzibar, Amani Karume, alitupwa mbali. Dodoma (mwiba mkubwa wa Wazanzibari) Karume, aliibuka mshindi kwa kusaidiwa na vijana wa bara. Ndio hivyo tena, Wazanzibari hawatabiriki. Inawezekana na Amani, mwenyewe akaibuka na kura ya turufu ya Wazanzibari kuwania urais wa muungano.

Tukiachana na kundi la Wazanzibari, kuna makundi makubwa mawili katika CCM, na hasa CCM bara. Kundi la wazee na kundi la vijana. Kundi la vijana linaongozwa na Mheshimiwa Kikwete. Kundi hili linaelekea kuwa na ushawishi mkubwa na wafuasi wengi. Tatizo la kundi hili ni kutokuwa na mshikamano, uzalendo, sera na “vision” Inashangaza na kusikitisha kuona jinsi vijana wenyewe akina Kikwete, Magufuri, Mwandosya, Sumaye n.k., wanavyopigana vikumbo na vijembe.

Kundi la wazee linaongozwa na Mzee Malecela, mtu anayeaminika kwa “kukishika” vizuri chama na
“kuwashika” vizuri viongozi wa chama na wanachama. Wachunguzi wa mambo ya siasa katika chama cha mapinduzi wanasema kambi ya mzee Malecela, imekwisha teka asilimia 75 ya wajumbe wa mkutano mkuu utakao pitisha jina la mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM. Maana yake ni kwamba yule atakayeungwa mkono na Mzee Malecela, ndiye atakayepita! Mzee Malecela, akiamua kusimama mwenyewe, hatakuwa na mpinzani! Mwakibaki wa Kenya, ni mzee zaidi ya Malecela, Abdullahi Yusuf Mohamed, aliyechaguliwa kuiongoza Somalia, ni mzee wa miaka 70. Nelson Mandela, aliiongoza Afrika ya Kusini, akiwa mzee. Kwanini Malecela, asiweze? Pamoja na jitihada za makusudi za marehemu Mwalimu Nyerere, za kuonyesha udhaifu wa Malecela, katika uongozi, wanaCCM, hawakuchelea kumchagua kama makamu mwenyekiti wa CCM upande wa bara! Hii inaonyesha anavyopendwa ndani ya chama. Kwa maelezo ya Mwalimu, katika kitabu chake cha “Uongozi wetu na hatima ya Tanzania”, sifa za Mzee Malecela, zinaonyeshwa vizuri. Kama sikutaka kuleta vurugu, moto na kimbunga katika taifa letu, Mzee Malecela, angekaa pembeni na kutoa ushauri. Kama wanaCCM, hawaogopi kumsaliti Mwalimu, Baba wa taifa, kuna wazalendo ambao wako tayari kutoona hilo likitokea!

Sasa hivi kuna tetesi na minong’ono kwamba wazee wa CCM wanamlaumu rais Mkapa, ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM, kwa kukitelekeza chama na wanachama. Chama kinachozaa marais, mawaziri, wabunge wengi na kuiongoza serikali, kimetelekezwa. Ofisi za chama katika ngazi zote hazina hadhi ya kuridhisha. Wenyeviti wa wilaya na mikoa hawana magari mazuri aina ya shangingi. Magari yao ni ya kizamani na yamechoka. Posho za watendaji ndani ya chama zinapatikana kwa shida. Wenyeviti wa wilaya na mikoa, hawapati upendeleo wa kutibiwa nchi za nje au kulipiwa matibabu. Rais Mkapa, analaumiwa kwa kuweka nguvu zake zote kulitumikia taifa na kukitelekeza chama. Hakuhakikisha chama kinashika utamu. Wakubadilisha hali hii, mtu anayekijua chama – maana CCM ina wenyewe – mtu anayewathamini wanachama na viongozi wa chama si mwingine bali Mzee Malecela. Wazee wanaogopa kukiweka chama mikononi mwa vijana. Wanaogopa kumchagua mgombea urais kijana. Wanaogopa kijana asije kuwatelekeza kama alivyofanya rais Mkapa. Wazee wana pesa za kuweza “kuwashika” vizuri wajumbe wa mkutano mkuu, hivyo kumpitisha mzee mwenzao si kazi kubwa. Hapa ndio kuna vuta ni kuvute katika chama cha mapinduzi. Swali la kujiuliza ni je, Tanzania, tunamuhitaji rais “anayekishika” vizuri chama na wanachama wa chama chake au tunamuhitaji rais “anayelishika” vizuri taifa lote na wananchi wake? Mandela, alitawala akiwa mzee, lakini alikuwa na “vision” ya kuikomboa Afrika ya Kusini. Alikuwa na “mission” ambayo tunaweza kuisoma kwenye vitabu alivyoviandika yeye mwenyewe au walivyoviandika watu wengine juu yake. Uzee si tatizo! La msingi ni “vision” na “mission” anayokuwa nayo kiongozi kwa Taifa lake Ni wapi tunaweza kusoma “vision” na “mission” za wale wote wanaotaka kuliongoza taifa letu? Wameandika wapi au wameandikwa wapi? Majigambo yao ni yapi Historia haiandikwi mtu anapoingia Ikulu. Historia ya nyuma ni kigezo kikubwa kumwingiza mtu Ikulu, vinginevyo mtu anaweza kuingia Ikulu na kutoka bila historia yoyote nyuma yake. Je, nchi inayoendelea ina haja gani na rais asiyekuwa na uwezo wa kuandika historia? Hata mtu mpumbavu kama Iddi Amin, aliandika historia. Uchumi wa Uganda, sasa hivi uko mikononi mwa wazawa. Sisi tumelala, wale wanaojiita “wazawa” wameteka uchumi wote na tunaendelea kuwatetemekea na kuwaabudu. Ni nani ameandikwa awe kijana au mzee? Mzee Malecela, ameandikwa na mwalimu, alivyoandikwa, inashangaza kuona bado ana nafasi ya uongozi katika chama kinachotawala. Nchi za wenzetu wanaothamini historia ya mtu, Mzee Malecela, angewekwa pembeni, si kutupwa kapuni, maana kuna mema mengi aliyoyatendea taifa letu, angebaki kama mshauri tu! Sasa anaongoza chama na “kukishika” vizuri!

Makundi mengine mawili ya udini na ukanda yaliyo ndani ya CCM hayana nguvu sana. Lakini bila busara ya kutosha makundi haya yanaweza kuwa ya hatari. Kuna mawazo potovu kwamba kwa vile Nyerere, alikuwa Mkristu, akarithiwa na Mwislamu Mzee Mwinyi na kufuata Mkristu ambaye ni rais Mkapa, hivyo 2005 ni zamu ya Waislamu. Hili ni shinikizo la kipumbavu linaweza kupelekea kumchagua mtu si kwa sifa na uwezo wake bali kwa kufuata dini yake.

Mwalimu Nyerere, alikuwa mzaliwa wa kanda ya ziwa, Mwinyi, visiwani na Mkapa, kusini. Hivyo 2005 ni zamu ya maeneo mengine ya nchi yetu kumtoa rais! Hili limeanza kuleta chuki miongoni mwa wale wanaotamani kuliongoza taifa letu.

Vilevile ndani ya CCM, kuna wale wenye mawazo ya uzawa na wale wanaoyapinga mawazo ya uzawa. Kuna wanaounga mkono sera ya utandawazi, ubinafsishaji na uwekezaji, na wale wanaopinga sera hii kwa nguvu zote.

Ni kawaida kuwa na makundi na maoni mbali mbali katika jamii au katika chama. Maoni yote yakiwa yanalenga katika kujenga, hakuna hatari yoyote. Mfano, kama makundi yote niliyotaja kama yangekuwa yanalitanguliza taifa letu la Tanzania, hakuna ambaye angekuwa anapiga kelele. Tatizo linalojitokeza sasa hivi ni kutanguliza maslahi binafsi. Kama anavyosema Salimu Ally: “Huko kuna matapeli waliokuwa tayari, kupewa shilingi mbili, waiuze Tanzania..”

Jinsi CCM, ilivyo na wenyewe, Tanzania, pia ina wenyewe. Siku ambayo wenye nchi watasema “hapana”, wakadai kwa nguvu zote kuwa na kiongozi “anayeishika” vizuri nchi na “kuwashika” vizuri wananchi – bila busara ya chama kinachotawala na kinachotaka kuendelea kutawala milele itatokea hatari kubwa. Hatari hii imeingizwa vizuri katika utenzi wa Salimu Ally: Machungu,kimbunga, moto, huzuni, mamba na mwisho ni kujuta.

Nina imani kuna watanzania wengi wenye mawazo kama ya Salimu Ally. Hali ndio ilivyo ndani ya CCM na katika vyama vingine vya siasa. Bado tuna muda wa kukaa chini na kujadiliana na kutafakari na kuweza kuliponyesha taifa letu na janga kubwa lililo mbele yetu. Mashirika yasiyokuwa ya serikali, makundi mbali mbali katika jamii, viongozi wa dini, wasaidie kuendeleza majadiliano na tafakuri, wasaidie kuwaelimisha wananchi juu ya demokrasia, uongozi na uzalendo. Tusiangalie rais anayekuja anatoka chama gani, anatoka kabila gani, anatoka dini gani. Tuangalie uwezo wa mtu, uzalendo, sera, “vision” na “mission” yake. Kwa njia hii kila mtu anaweza kushiriki kuliponyesha taifa letu na janga kubwa. Mungu ibariki Tanzania.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment