Wanateolojia

Makala hii ilitoka kwenye gazeti la Rai 2004.

WANATEOLOJIA WETU

Wakati nikichambua maoni ya Askofu Benson Bagonza, aliyoyatoa kwenye mkutano wa kumi na mbili wa hali ya siasa Tanzania, nilikuwa na kishawishi cha kuunganisha uchambuzi huo na wa maoni ya Askofu Kilaini, maana wote ni Maaskofu, wasomi, Wakristu na wote waliongelea kitu kile kile: Uzoefu wa Viongozi wa Dini katika kujenga imani ya jamii na amani. Nilisita kufanya hivyo. Baada ya kusoma maoni yao kulijitokeza tofauti ndogo, lakini yenye maana kubwa: Askofu Benson Bagonza, hajitofautishi na maoni yake, ukisoma maoni yake unapata harufu na picha yake; kama, Askofu Bagonza, angeandika maoni yake na kumpatia mtu mwingine kuyasoma, yasingekuwa na mvuto, uzito, ujumbe na ushawishi uleule. Hii ni tofauti na Askofu Kilaini, ambaye maoni yake yangewasilishwa na mtu yeyote ambaye si mlei, na kubaki na “mlio” ule ule, bila ya kutoa harufu na picha ya Askofu Kilaini. Hii ni sababu tosha iliyonisukuma kuandika makala mbili tofauti.

Askofu Kilaini, aliipamba mada yake kwa misemo inayochoma na kugusa, misemo inayomvua nguo mtu na kumwacha uchi, misemo ya kujisuta na imejaa changamoto kwa kila anayejiita kiongozi wa dini na hasa mfuasi wa Kristu:,
- “Kuwa na imani katika mtu ni kumwamini, kujiweka mikononi mwake ukijua kwamba atakutendea haki na kwamba anavyoonekana nje ndo alivyo kweli na si unafiki,
- Imani katika mtu ni kujua kwamba huyu ni mkweli na muwazi,
- Imani katika jamii ni kutoa na kupata heshima kutoka kwa watu, kuvumiliana,
- Kujua kwamba wengine wanastahili hiyo heshima kwa sababu ni watu wa kutegemewa hasa kama wako katika sehemu ya madaraka,
- Kujenga imani katika jamii huwa kama dawa katika kutibu madonda ya mafarakano na kuleta amani,
- Viongozi wa dini ni waalimu na wahamasishaji wa ujenzi wa Imani ya Jamii na Amani,
- Viongozi wa dini wawe kila mara wahubiri wakubwa wa kupinga mambo yote yanayoharibu Imani katika jamii na amani kama uvunjaji wa haki za binadamu,
- Muda mrefu wa kutoaminiana umeacha makovu ambayo yanapaswa kutibiwa na dawa ni kufanya alichoasa kanisa Papa Yohana XIII “ Watoto wangu tafuteni kila kinachowaunganisha na si kile kinachowatenganisha”.”
Funga yote ni msingi mkubwa wa maoni yake:

“ Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la pili. Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwachie achukue pia koti lako. Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili. Akuombaye mpe, na mtu akitaka kukukopa kitu usimnyime. Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Mpende jirani yako na kumchukia adui yako.’ Lakini mimi nawaambieni, wapendeni adui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangaza jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu.” (Mt.5:1-39).

Mimi ningeongezea maneno ya mtakatifu Paulo, kwa Wagalatia:
“Kwa njia ya imani, ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika kuungana na Kristo. Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanaume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja katika kuungana na Kirsto Yesu...” (Wagalatia 3:26-28).

Jamii yenye tabaka, ubaguzi wa kijinsia na ukabila, haiwezi kujenga imani ya kweli na amani. Migogoro iliyo kwenye kanisa katoliki la Tanzania, inasababishwa na tabaka, ubaguzi wa kijinsia na ukabila, ingawa Askofu Kilaini, alilikwepa jambo hili kwa ujanja kwa nia ya kuyalinda maslahi yake na ya kanisa, ukweli unabaki palepale. Tuna mifano mingi inayoonyesha jinsi Taifa letu linavyoshambuliwa na tabaka na ukabila. Tabaka hizi zinashika kasi na kutengeneza makundi mawili ya hatari sana ya walionacho na wasiokuwanacho.Huu ni uwanja wa kuvuruga amani katika jamii.

Mtu mwingine, anaweza kuongezea kwa kutoa ushuhuda wa mitume. Tunaambiwa kwamba waliishi kwa nguvu za “ mikutano ya jumuiya”. Walijadiliana, waliheshimu maoni ya kila mwanajumuiya. Kwa maneno mengine, walikuwa na jukwaa la majadiliano. Jamii isiyokukwa na jukwaa la majadiliano haiwezi kujenga imani ya kweli na amani. Kanisa katoliki, halina jukwaa la majadiliano, ndoa maana mchango wake katika kujenga imani ya jamii na amani ni mdogo na msemo wa Baba Mtakatifu Yohana XIII “ Watoto wangu tafuteni kila kinachowaunganisha na si kile kinachowatenganisha” umebaki kuwa upepo unaovuma. Hakuna aliyeyazingatia! Tunachoshuhudia miongoni mwa viongozi wa kanisa katoliki ni chokochoko za yale yanayotenganisha. Mfano mzuri aliutoa Askofu Kilaini, katika mada yake:

“ Hadi sasa kanisa Katoliki limeshindwa kusuluhisha mgogoro wa kikundi cha wanawaombi. Kikundi hiki kimejisajili serikalini na kina ibada zake tofauti na kanisa Katoliki lakini bado wanataka watambuliwe na kanisa Katoliki bila kanisa hili kuingilia mambo yao. Mazungumzo na uelewano vimeshindikana kwa sababu kikundi hiki hudai kwamba maamuzi yao hutoka juu peponi na si kwa watu. Kufikia makubaliano ingebidi kufanya kikao na waamuzi hao wa peponi...”

Ukichunguza kwa makini utaona yanayotajwa ni yale yanayotenganisha:
- Kikundi kujisajili Serikalini
- Maamuzi kutoka juu peponi.

Papa Yohana wa XIII, alishauri kutafuta yale yanayounganisha. Mfano, ni kitu gani kinawaunganisha wanawaombi na Kanisa Katoliki. Hili ndio lingekuwa jambo la kuongelea na kujadiliana.

Kwa upande mwingine kikundi cha wanawaombi kinafuata mfumo mzima wa kanisa Katoliki. Kwa muumini wa kawaida Mtanzania, au niseme asilimia 99 ya waumini Wakatoliki wa Tanzania, Roma, ni sawa na juu peponi! Ni wangapi wanapata bahati ya kufika huko? Na hata wakifanikiwa kufika huko, ni wangapi wanaweza kushiriki katika kutoa maamuzi ya msingi katika kanisa lao? Maamuzi yote ya Kanisa Katoliki, hufanyika Roma na hufanywa na watu wachache ambao hawafikii asilimia moja ya waumini wote duniani, ni watu wa jinsia moja, maamuzi yao hayakosei wala kukosolewa. Je, hawa si ni sawa ni miungu wa peponi? Wana tofauti gani na wanawaombi wanaosema kwamba maamuzi yao hutoka juu peponi? Mfumo huu wa kusubiri maamuzi kutoka juu peponi(Roma au kwa Askofu) unakwamisha shughuli nyingi katika utendaji wa siku kwa siku, na hii husababisha migogoro inayojitokeza kukua na kufikia hali mbaya, na mara nyingi maamuzi yanapotolewa hayaangalii mahitaji ya jamii husika, yanaangalia matakwa ya juu peponi! Mgogoro wa kikundi cha wanamaombi na uongozi wa Kanisa Katoliki umevunja imani na amani katika jamii yetu. Ni nani amepigwa shavu la kulia akageuza na la kushoto. Tunachoshuhudia ni jino kwa jino! Kuko wapi kuvumiliana? Iko wapi dawa ya kutibu vidonda makovu ya mafarakano? Wako wapi viongozi ambao tunaambiwa ni walimu wa kujenga imani ya jamii na amani? Ni nani anakubali kujiweka mikononi mwa mwingine?

Katika kuonyesha jitihada za kanisa katoliki la Tanzania kuchangia katika kujenga imani ya jamii na amani, Askofu Kilaini, kwa namna ya kustaajabisha, anamtaja marehemu Askofu Mwoleka:

“ Mwanaharakati mkubwa wa mfumo huu katika Tanzania na Afrika nzima alikuwa Christopher Mwoleka, askofu wa jimbo la Rulenge, ili kujenga imani ya jamii katika mfumo huu yeye mwenyewe alihama nyumba yake na kwenda kuishi katika kijiji cha ujamaa: Akianzia katika kijiji cha ujamaa alijenga jumuiya ndogo ndogo katika jimbo zima. Hii ilisaidia sana kwa sababu katika vikundi vidogo vya familia zisizozidi 20 aliweza kujenga miundombinu ya uongozi pakiwemo ushauri juu ya uchumi, usuluhishi, afya na mengine. Mfumo wa Mwoleka ulikuwa umefika mbali sana kwani leo jumuiya tulizonazo sasa zinaishia katika kujuana, kuzungumza pamoja na kuongelea juu ya matatizo walionayo na kusaidiana katika shida. Jumuiya hizi zikiweza kwa namna fulani kuwashirikisha hata wale wasio wa imani yao zinasaidia sana kujenga ujirani mwema na amani.”

Askofu Kilani, ni kati ya watu walioshuhudia Jumuiya za Mwoleka, zikianza, zikiishi na kufanya kazi, zikifa na kuzisindikiza hadi kaburini. Kama jumuiya hizi zilikuwa kitu kizuri, kwa nini ziliachiwa kufa? Mgogoro uliojitokeza baada ya kifo na matanga ya jumuiya hizi ulisambaratisha haki, imani na amani ya watu wengi ambao wanayachukulia maoni ya Askofu Kilaini, juu ya uzuri wa jumuiya hizo kama maneno ya kutoka juu peponi, na wala si ya mtu wa kawaida tunayeishi naye hapa duniani!

Jitihada nyingine ya Kanisa Katoliki, katika kujenga imani ya jamii na amani, inayotajwa na Askofu Kilaini, ni Tume ya Haki na Amani. Tume hii imefanya mambo mengi mazuri, kama semina na makongamano ya kuwaelimisha watu juu ya haki na amani. Imechapa vitabu mbali mbali: Kijitabu cha Kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Haki za wafungwa na Hali ya Magereza, Haki za Raia na Jeshi la Polisi. Kuna vijitabu vingine vimeandikwa kama sheria ya ardhi Tanzania, Uchaguzi kwa nini tunajali na Maskini unganeni kuondokana na umaskini.

Hii ni kazi nzuri ya Tume ya Haki na Amani. Tatizo linalojitokeza katika tume hii ni uundwaji wake. Tume ya Haki na Amani, ni vyema ikifuata haki na kuwa Tume huru. Sasa hivi si tume huru. Inateuliwa kutoka juu peponi. Waumini hawana uhuru wa kujichagulia wajumbe wanaowapima kwa vigezo na kuona wanafaa kuingia kwenye Tume ya Haki na amani. Haitoshi kuwa padre, ukafuzu kuwa mtu wa haki na amani!

Ni imani yangu kwamba kila mtu atakubaliana na Askofu Kilaini, pale anaposema:
“ Elimu ya mtu inasaidia au inaathiri mtazamo wake katika jamii. Elimu hii huanzia ngazi za chini za chekechea (madrasa) hadi chuo kikuu. Elimu siyo tu elimu dunia bali vile vile elimu ya maadili na mtazamo wa dunia. Kuwapo kwa elimu bora kunajenga imani ya jamii na amani na kukosa elimu au kuwa na elimu potovu kunaathiri imani na amani katika ya watu...... Viongozi wa kanisa wamefikia kuona kwamba mafundisho yao hayatakuwa na nguvu kama wataacha wataalamu wa kesho bila maadili mazuri....Mwaka 1996, kanisa Katoliki lilifungua Chuo Kikuu hapo Nyegezi, Mwanza kufundisha upashanaji habari, uongozi na uhasibu..”

Huu ni ukweli. Lakini watu wanahoji, mbona mpaka sasa hakuna chuo kinachofundisha theolojia kwa walei? Migogoro mingi ya kidini, au magomvi kati ya dini na dini au dhehebu na dhehebu inasababishwa na elimu ndogo ya waumini juu ya imani yao. Ukizingatia kwamba dini zote tulizonazo ni za kigeni, zimepita kwenye historia ndefu yenye tamaduni tofauti, lugha mbalimbali na mazingira tofauti kabisa na ya Tanzania. Mapadre, Maaskofu, Wachungaji na mashehe wanaweza kucheza mpira pamoja na kukaa pamoja katika majadiliano, kwa vile wao wana elimu ya kutosha juu ya dini hizi za kigeni. Waumini wa kawaida wameachwa kwenye giza nene! Na hii si ishara nzuri ya kujenga imani ya jamii na amani.

Ni ukweli usiopingika kwamba: “Mwelimishaji wa kwanza wa binadamu ni mama. Viongozi wa kanisa katika mikakati ya kujenga jamii yenye amani, wamesisitiza juu ya ulazima wa elimu ya wasichana. Katika miaka 20 iliyopita kanisa Katoliki limetoa kipaumbele chake kwa elimu nzuri ya wasichana kwa kujenga shule nzuri kwa ajili yao. Mafanikio ya mkakati huo yalionekana wazi mwaka 2002 ambapo shule za wasichana za kanisa zilichukua nafasi 4 kati ya kumi bora ikiwemo shule ya kwanza na ya pili. Hii ilionyesha kwamba wasichana wakiwekwa katika mazingira mazuri wanaweza kushinda hata wavulana.”

Nina imani hakuna anayepingana na Askofu Kilaini, kwa jambo hili. Swali ni je, hawa wasichana wanaonyesha ushindani mkubwa katika nyanja za elimu, wanapewa nafasi gani katika kanisa ili waweze kutoa mchango wao katika kuchangia harakati za kujenga imani ya jamii na amani? Kama wameweza masomo mengine yote, watashindwa theolojia? Kama wameweza kazi nyingine zote, tunavyoshuhudia nyakati hizi, watashindwa kazi na wito wa upadre? Ili mtu atoe mchango katika maamuzi ya msingi katika kanisa katoliki ni lazima awe padre, Askofu, Kadinali na Papa. Vyeo hivi ni vya wanaume. Hivyo na maamuzi yanayogusa moja kwa moja mambo yanayohusiana na maisha ya wanawake huamuliwa na wanaume! Huku ni kukiuka haki za binadamu. Jamii inayokiuka haki za msingi za binadamu kama uhuru wa maoni, ubaguzi wa kijinsia nk itakuwa ya mwisho katika harakati za kujenga imani ya jamii na amani.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment