TEOLOJIA YA UKOMBOZI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005

TEOLOJIA YA UKOMBOZI

“Roho wa Bwana yu pamoja nami, kwani ameniteua rasmi niwaletee maskini habari Njema. Amenituma niwatangazie wafungwa kwamba watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na niutangaze mwaka ambao Mungu atawakomboa watu wake” ( Luka 4:18-19).

Gazeti hili na karibu kila gazeti hapa nchini limekuwa likiandika juu ya ugonjwa, kifo na historia ya Papa Yohana Paulo wa Pili. Teknolojia ya mawasiliano imesaidia kusambaza habari za msiba huu mkubwa duniani kote. Kupitia kwenye luninga, dunia nzima ilishuhudia jinsi mazishi ya Papa yanavyoendeshwa. Kwa wengi na hasa kwa watu wa dunia ya tatu ambao hawana uwezo wa kufika kule Roma, kila kitu kilikuwa kigeni.

Baada ya mazishi ya Papa, sasa hivi vyombo vyote vinatafakari na kuanza kufanya utabiri juu ya ni nani atavaa viatu vya Papa Yohana Paulo wa Pili, kuvaa pete ya mvuvi na kukalia kiti cha Mtakatifu Petro. Yanatajwa majina mbali mbali hata na baadhi ya Makadinali wa Afrika.

Ingawa si lengo la makala hii kuwakatisha tamaa wale wanaofikiria Kadinali Mwafrika kuwa Papa, ningependa kudokeza tu kwamba sasa hivi hali ya Kanisa Katoliki ilivyo, ni ndoto mtu mweusi kuwa Papa. Kuna mambo mengi ya kufanyika kabla ya kumfikiria Papa mweusi. Mfano idadi ya makadinali weusi ni ndogo, ushawishi wa dunia ya tatu katika maamuzi ya Kanisa katoliki ni mdogo, Vatikani imezungukwa na weupe watupu: Hii imejionyesha wazi wakati wa mazishi ya Papa Yohana Paulo wa Pili. Mamilioni yale yaliyofika pale Roma, uliwaona Waafrika au weusi wangapi? Tutasema Roma ni mbali! Lakini weupe wanatoka Amerika na Japan, ambako nako ni mbali na Roma.

Nimenukuu Injili ya Mtakatifu Luka, ili itusaidie kutafakari ni Papa wa aina gani anafaa kuliongoza kanisa kwa wakati huu. Tuachane na ndoto za kumfikiria Mwafrika. Ingekuwa vyema awe Mwafrika, lakini kanisa bado si letu! Au kwa maneno mengine, dunia ya tatu, dunia si yetu! Huu ni mjadala unaojitegemea.

Alipochaguliwa Papa Yohana Paulo wa Pili, Kanisa Katoliki na dunia ya kwanza, dunia ya matajiri, mabepari, wenye viwanda, wenye mashirika ya kiunyonyaji, wenye nguvu na uamuzi wa kila kitu, walikuwa wakimtaka Kiongozi wa Kanisa Katoliki atakayeweza kupambana na Ukomunisti. Na kosa halikufanyika maana Papa Yohana Paulo wa Pili, amepambana na Ukomunisti na kuusambaratisha kuanzia kwao Poland, Urusi na nchi nyingine zilizokuwa zikifuata mfumo wa Ukomunisti. Leo hii dunia haina tatizo la Ukomunisti. Lakini pia si kweli kwamba dunia ni salama, inafuata haki na imeneemeka zaidi kwa kuuondoa Ukomunisti.

Marehemu Papa Yohana Paulo wa Pili, baada ya kuuangusha Ukomunisti, alianza kuushambuliwa Ubepari. Alianza kuuona uovu ulio kwenye ubepari. Amerika, ilipopanga kuishambulia Iraq, alitaka kwenda kule kuwa kinga ya watu wa Iraq! Hata hivyo vita iliendelea na hadi sasa hivi watu wanaendelea kufa bila kuwa na hatia yoyote ile.

Tatizo la dunia ya leo si Ukomunisti. Ingawa Ukomunisti haukuwa tatizo la dunia nzima bali lilikuwa tatizo la mabepari na wanyonyaji. Leo hii dunia yetu haina amani: Vita imezagaa kila pembe ya dunia. Dunia yetu ya leo ina kiu ya haki: haki katika jamii, haki za kijinsia, haki za uchumi, haki za kuishi nk. Papa wa kuliongoza kanisa katika hali ya sasa hivi ni yule anayetetea amani, haki na usawa. Ni yule anayetetea maisha ya masikini na wanyonge. Ni yule anayeweza kusema, kuishi nakutekeleza maneno ya mwanzilishi wa Kanisa:
“Roho wa Bwana yu pamoja nami, kwani ameniteua rasmi niwaletee maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie wafungwa kwamba watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa na niutangaze mwaka ambao Mungu atawaokoa watu wake.”

Papa anayeweza kutetea na kuisimika Theolojia ya Ukombozi. Papa Yohana Paulo wa Pili, aliipiga vita Theolojia ya Ukombozi, kwa sababu ilifanana fanana na ukomunisti. Kule ilikotekelezwa, Latin Amerika, wanyonge walipinga mifumo ya kibepari na kuikumbatia mifuko iliyokuwa ikihubiri haki, usawa na heshima ya binadamu wote. Watu wengine wanafikiri Theolojia ya Ukombozi, ilianzishwa na mapadri wa Kijesuiti waliokuwa wakifanya kazi kule Latin Amerika. Si kweli! Theolojia ya Ukombozi ilianzishwa na Yesu mwenyewe. Maneno niliyoyanukuu mwanzoni mwa makala hii ndicho chanzo cha theolojia ya ukombozi.

Hali aliyoiongelea Yesu Kristu: Kuwaletea maskini habari njema, wafungwa kupata uhuru, kuwakomboa wanaoonewa, kuwaponya vipofu na kuutangaza uhuru, ndiyo hali waliyokumbana nayo mapadri wa Kijesuiti waliokuwa wakifanya kazi Latin Amerika: Umaskini ulikithiri, asilimia tano ya watu wote kule waliishi maisha ya kifahari wakati asilimia tisini na tano iliishi katika umaskini wa kutupwa. Mapadre na maaskofu waliangukia kwenye asilimia ile tano iliyokuwa ikiishi maisha bora. Ardhi nzuri iliuzwa kwa mabepari na watu wa kawaida walilazimishwa kuishi kwenye ardhi isiyokuwa na rutuba. Mahospitali, mashule na miradi mingine ya kanisa iliwahudumia watu matajiri. Hali hii iliwalazimisha mapadri wa Kijesuiti kuamua kutekeleza Theolojia ya Ukombozi kwa lengo la kujenga imani ya jamii na kulifanya kanisa lifanane na ujumbe linalohubiri na watu linaowatunza.

Kwa vile Theolojia hii iliwatetea wanyonge na kupinga unyonyaji na ugandamizaji, machoni mwa dola na utawala wa kanisa ilionekana ni “ugaidi” uliovaa sura ya “ukomunisti”. Ilipingwa na kanisa na Serikali za Latin Amerika. Mapadri walioiendeleza walifukuzwa upadri na wengine waliuawa na Serikali kwa kisingizio kwamba ni magaidi, maana walilazimishwa kujiunga na makundi ya waasi yaliyokuwa yakipinga sera za unyonyaji na unyanyasaji.

Mtu huyu wa kuliongoza Kanisa Katoliki ambaye si lazima awe Kadinali, Bishop wala padri – sheria ya kanisa inaruhusu achaguliwe Mkristu yeyote yule mwenye sifa, hawezi kutoka dunia ya kwanza. Papa wa kuitetea Theolojia ya Ukombozi, hawezi kutoka katika jamii ya mabepari na wanyonyaji. Ni lazima atoke miongoni mwa maskini, miongoni mwa wanyonge na miongoni mwa wanaoteswa. Hata Yesu, hakuzaliwa kwenye majumba ya kifahari. Alizaliwa katika umaskini!

Wakati tunatafakari na kutaja taja majina ya wale wanaofaa kuliongoza Kanisa Katoliki katika milenia hii yenye mabadiliko mengi, ni lazima kutanguliza ujumbe wa Yesu, ni lazima kutanguliza wazo kwamba kanisa kama linataka kuisafisha sura yake na kuwa na sura mpya ni lazima achaguliwe kiongozi atakayetetea maskini, wanyonge, wanaoonewa na kutangaza Uhuru wa watoto wa Mungu. Ni lazima achaguliwe kiongozi anayejua maana ya umaskini na unamgusa, anayejua maana ya unyonge na unamgusa, anayejua maana ya kuonewa na inamguza, anayejua maana ya kufungwa na inamgusa. Tajiri hawezi kutetea haki za maskini na wanyonge. Mtu anayekumbatia mifumo ya kibepari hawezi kuitetea na kuiendeleza Theolojia ya Ukombozi. Hawezi kueneza ujumbe wa Yesu Kristu! Ingawa tunaamini kwamba roho mtakatifu anafanya kazi kwa uhuru na bila ya upendeleo! Kwa hili tunaomba ampendelee yule atakayelipatia kanisa katoliki sura yake!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment