TIDO MUHANDO, MAMA LUHENA NA PROFESA CHACHAGE

MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

TIDO MUHANDO,MAMA LUHENA NA PROFESA CHACHAGE.

Jumamosi ya tarehe 9.4.2005, Tido Muhando, katika amka na BBC, kipindi cha wiki hili, aliendesha majadiliano juu ya Maisha ya Marehemu Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili, kati ya Profesa Chachage wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na Mama Luhena Mkatoliki wa hadhi ya juu katika Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam. Majadiliano hayo yalijikita juu ya mafanikio chanya na hasi wakati wa uhai wa Papa Yohana Paulo wa Pili.

Mama Luhena, alisimamia mafanikio chanya. Alijitahidi jinsi alivyoweza kukwepa dhambi ya mauti kwa kutoangalia upande mwingine wa Papa Yohana Paulo wa Pili. Aliyataja mema yote aliyoyafanya Marehemu Baba Mtakatifu. Kwamba alikuwa mtetezi wa wanyonge, alikuwa mchungaji mwema, alitembelea dunia nzima na Tanzania ikiwemo, alitetea uhai kwa kupinga utoaji mimba, matumizi ya kondomu na uzazi wa mpango, alipinga vita na sifa nyingine nyingi. Kwa maoni ya Mama Luhena, hakuna upande mwingine wa Baba Matakatifu. Alikuwa mtu mwema, atangazwe Mtakatifu haraka iwezekanavyo!

Profesa Chachage, aliangalia pande zote mbili; chanya na hasi. Aliungana na watu wote wanaomsifia Marehemu Baba Mtakatifu. Alikubali kwamba hakuwa mtu wa kawaida. Kwamba alijitoa na kuwatumikia watu kwa moyo wake wote. Aliziunga mkono sifa zote za Mama Luhena. Lakini aliyataja mambo matatu ambayo kama Papa Yohana Paulo wa Pili, angeyafanya basi angevunja rekodi ya watakatifu wote:
1. Mauaji ya Rwanda, 2.UKIMWI na 3. Theolojia ya Ukombozi.

Profesa Chachage, alielezea kwamba Baba Mtakatifu, aliitembelea nchi ya Rwanda mwaka 1990. Mwaka 1994, yakatokea mauaji ya kuangamiza. Kanisa Katoliki likashutumiwa kushiriki kikamilifu katika mauaji hayo. Kwa maoni ya Profesa Chachage, Baba Mtakatifu angefanya matembezi mengine Rwanda, baada ya vita ili kuwatuliza Wanyarwanda na kulisafisha jina la Kanisa. Hakufanya hivyo! Hakuwakemea na kuwawajibisha wale waliotajwa kushiriki kikamilifu katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda . Baadhi ya walioyashirikia mauaji ya Rwanda, wanaendelea kulindwa na Kanisa katoliki katika nchi za Ulaya.

Mama Luhena, aliitetea hoja hii kwa nguvu zake zote. Kwa maoni yake kanisa halifanyi makosa! Hata kule Rwanda, kanisa halikufanya makosa! Waliofanya makosa ni watu binafsi! Hivyo lisishutumiwe kanisa wala Baba Mtakatifu, bali watu binafsi.
Hapa kuna haja ya kumkumbusha Mama Luhena, kwamba Kanisa Katoliki, lina historia ya kuwashughulikia watu binafsi waliokuwa wakifanya makosa na kuichafua sura ya kanisa. Miaka ya nyuma watu walichomwa moto, walifungwa na kuteswa na wakati mwingine kutengwa na kanisa kwa makosa yao binafsi dhidi ya Kanisa. Hata leo hii bado tunashuhudia adhabu mbali mbali katika kanisa. Mkristu akioa bila kufunga ndoa kanisani anaadabishwa, Mkristu akizaa nje ya ndoa anaadabishwa, Mkristu anayekwenda kinyume na maelekezo ya Askofu, kama kukahidi amri ya kutofanya sherehe za usiku hapa Tanzania, anaadabishwa nk. Mama Luhena, mwenyewe ameshuhudia pale Dar-es-Salaam, jinsi wanawaombi wa Padre Nkwera, waliyoadabishwa, kufukuzwa makanisani na kutengwa. Ndio maana Profesa Chachage, alihoji tukio la Rwanda. Kama Kanisa Katoliki lina utamaduni wa kuwawajibisha watu binafsi wanaoichafua sura ya kanisa, mbona wale walioshirikia mauaji wa Rwanda, hawakushughulikiwa? Mbona Baba Mtakatifu alikaa kimya? Hakukemea, hakuomba msamaha au kuitembelea Rwanda? Ameacha makovu, ameacha chuki na visasi! Siku ya mazishi ya Papa Yohana Paulo wa Pili, Burundi, nchi iliyo jirani na Rwanda, ilitangaza siku ya mapumziko, lakini Rwanda, kazi ziliendelea kama kawaida! Hii inaleta picha gani katika nchi ambayo karibu robo tatu ya wananchi wake wote ni Wakatoliki?. Tido Muhando, ndiye aliuliza swali hili ambalo lilionekana kama la uchokozi kwa upande wa Mama Luhena. Halikupata jibu. Labda watetezi wengine watatupatia jibu siku moja!

Kuhusiana na UKIMWI, Profesa Chachage, alisema kwamba Baba Mtakatifu, alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kupambana na ugonjwa huu lakini misimamo yake ya kupinga matumizi ya kondomu na kuhimiza mambo( Uaminifu katika ndoa, kujinyima na kuacha kabisa) ambayo kwa hali ya kawaida hayawezekani imekwamisha kwa kiasi kikubwa mapambano haya.

Mama Luhena, aliendelea kumtetea Baba Mtakatifu, kwa kutaja kwamba kwa upande wa matumizi ya kondomu Baba Mtakatifu hakuwa peke yake. Dini zote zinapinga matumizi ya kondomu. Maana kuruhusu matumizi ya kondomu ni kuhalalisha uzinzi! Kwa maoni ya Mama Luhena, msimamo wa Baba Mtakatifu wa kupinga kondomu, uzazi wa mpango na kutoa mimba ni wa kuigwa na kuzingatiwa maana unatetea uhai.

Kwenye hoja hii ya utoaji wa mimba, Tido Muhando aliuliza swali la uchokozi tena: “ Msichana akibakwa, akapata mimba, afanye nini? Na kama hampendi aliyembaka au ana uhakika kwamba huyo aliyembaka hataweza kumtuza mtoto. Kama kuna njia salama kwa nini binti kama huyu asiruhusiwe kuitoa mimba?”
Mama Luhena, alibaki kwenye msimamo wa Kanisa: “ Kanisa Katoliki, haliruhusu kutoa mimba, matumizi ya kondomu na uzazi wa mpango. Linatetea uhai”.

Mtu anaweza kuhoji: Pamoja na misimamo hiyo, kanisa katoliki lina mpango gani wa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao wengi wao wanatokana na mimba zisizotarajiwa? Mbona kanisa la Mtakatifu Joseph la Dar-es-Salaam, limezungukwa na watoto wa mitaani wanaoishi bila uangalizi wowote ule, wanalala nje, hawana nguo wala chakula? Wale mabinti wanaobakwa, au kulazimishwa kuzaa kabla ya wakati, wanapokoswa soko la wachumba na kuamua kujitupa mitaani, mbona tunawanyoshea kidole na kuwaita “Changudoa”? Wangezitoa mimba si wangebaki kwenye “Chati”? Kanisa Katoliki lina mpango gani wa kuzisaidia familia zinazoamua kutekeleza amri ya Mungu “Zaeni na kuujaza ulimwengu”. Kuzisaidia familia kuwalea watoto katika maadili mema, afya njema, maisha mazuri, elimu bora nk. Haina maana kuutetea uhai, bila kuhakikisha huyu mwenye uhai anaishi maisha ya heshima, furaha na matumaini.

Lakini jambo linalochekesha? Hapana! Linalosikitisha? Hapana! Haitoshi kusikitika kwa mtu aliyemakini. Ebu, niseme linalochanganya, ni kwamba tunapoongelea kuhusu kupinga uzazi wa mpango, kuhusu kutoa mimba, kupinga matumizi ya kondomu, kuhusu kutetea uhai na kutimiza amri ya Mwenyezi ya “ Zaeni na kuujaza Ulimwengu”, hatuwezi kuwa upande mmoja na Mapadre, Maaskofu na Baba Matakatifu. Useja ni aina fulani ya uzazi wa mpango! Useja ni sawa na kutumia kondomu au kutumia vidonge vya majira! Useja ni mfumo wa kuishi bila kuoa, bila kuzaa na bila kujenga familia. Mseja hawezi kutimiza amri ya Mwenyezi Mungu ya “Zaeni na kuujaza Ulimwengu”.

Mapadre, Maaskofu na Baba Mtakatifu ni waseja. Hawaoi, hawazai wala hawashiriki Utukufu wa mwenyezi Mungu wa kuumba na kujenga familia. Kundi hili ni vinara wa uzazi wa mpango! Ndio maana ninasema inachanganya watu hawa wanaposimama na kupinga uzazi wa mpango. Wanapinga vidonge vya majira, wanapinga kondomu, wakati wao wanaishi uzazi wa mpango asilimia miamoja! Mtu asiyependa kuzaa kwa makusudi, hawezi kupinga uzazi wa mpango, hawezi kutetea uhai….atatetea uhai wakati yeye hashiriki kuutengeneza uhai huo? Labda kama anatetea uhai wake mwenyewe! Mbele ya jamii huo ni ubinafsi mkubwa!

Profesa Chachage, alihitimisha hoja yake kwa kugusia Theolojia ya Ukombozi. Kwa maoni yake kuinyamazisha Theolojia ya Ukombozi ni sawa na kuunga mkono sera za akina Bush za Utandawazi na Soko huria. Sera ambazo haziwezi kuwasaidia wanyonge na masikini.

Theolojia ya Ukombozi, chimbuko lake ni katika nchi za “Latin Amerika”. Nchi hizi zinaongoza kwa kuwa na idai kubwa ya Wakatoliki dunia nzima. Katika nchi hizi umasikini ulikithiri na unaendelea kukithiri kupita kiasi. Kasi ya ufukara iliongezwa na sera za serikali za kubinafsisha na kuuza ardhi kwa wageni. Wananchi waliswagwa na kutupwa kwenye ardhi zisizo kuwa na rutuba. Watawala wa nchi hizi waliongoza kwa kuwanyenyekea na kuwaogopa matajiri na wafanyabiashara kutoka Marekani. Maisha ya wananchi wa kawaida yalikuwa magumu kiasi kwamba kuishi na kufa ilikuwa sawa. Kanisa lilishikamana na viongozi wa serikali na matajiri na kuwatelekeza wananchi wa kawaida. Mafundisho ya kanisa hayakuleta usalama wala amani mioyoni mwa waumini na wanyonge. Hata ujenzi wa hospitali, mashule na miradi mbali mbali ya kanisa havikuwa na faida kwa sababu walionufaika navyo walikuwa ni wale wenye hali nzuri na kufahamiana ama na viongozi wa kanisa au dola. Kanisa Katoliki la Latin Amerika, likawa na sura ya unyanyasaji, ubaguzi na la matajiri.
Katika hali hiyo wamisionari wa Kijesuiti wakazindua Theolojia ya ukombozi, ambayo machoni mwa dola na utawala wa kanisa ilionekana kuwa “Ugaidi” uliovaa sura ya “Ukomunisti”. Theolojia ya Ukombozi ililenga kutumika kama chombo cha kujenga imani ya jamii na kulitengeneza kanisa linalofanana na ujumbe linaouhubiri na lifanane na watu linaowatunza.

Marehemu Askofu Mkuu Oscar Romero wa El-Salvador, ni mhanga wa Theolojia ya Ukombozi. Yeye aliona hakuna njia nyingine ya utume wa kanisa isipokuwa kusisitiza umuhimu wa Theolojia ya ukombozi. Alipingwa na maaskofu wenzake na uongozi wa kanisa katoliki kule Roma. Alionekana mzushi na mwasi kwa kanisa na dola. Serikali ya El-Salvador ilianzisha operesheni maalumu ya kuwasaka na kuwaua makasisi wote wa Kijesuti, walioendesha Theolojia ya Ukombozi. Mauaji haya yaliendelea wakati uongozi wa kanisa ukiwa kimya. Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili, hakuwa na la kusema zaidi ya “ Mapadri wa Latin Amerika wanachanganya dini na siasa”. Theolojia hii ilinyamazishwa kwa nguvu zote kwa vile ilionyesha dalili za kuchanganya dini na siasa.

Askofu Mkuu Romero, hakukubali kuiachia Theolojia ya Ukombozi. Hatimaye aliuawa na Serikali ya El-Salvador kutokana na msimamo wake wa kupinga unyonyaji na kuwatetea maskini. Serikali ilijisifu kuyamaliza maisha ya “gaidi”! Kanisa lilikaa kimya hadi Baba Mtakatifu Yohana Paulo, alipoitembelea El-Salavador na kusali kwenye kaburi la Askofu Mkuu Romero.

Pamoja na changamoto za Profesa Chachage, Mama Luhena, alisimama imara hadi mwisho wa majadiliano akimtetea Baba Mtakatifu kwamba alikuwa mtetezi wa wanyonge na masikini. Sidhani kuna wa kupingana na mama Luhena kwa jambo hili, aliyoyasema juu ya Baba Mtakatifu ni ukweli unaoungwa mkono na dunia yote. Jambo linaloshangaza ni Baba Mtakatifu kutetea wanyonge na masikini, wakati akiipiga vita mifumo ya kuwasaidia wanyonge na masikini kujikomboa. Msimamo huu si mchango chanya katika dunia ya leo inayoendelea kwa kasi ya kutisha. Bila mifumo kama Theolojia ya Ukombozi, yenye lengo la kulifanya kanisa lisimame upande wa wanyonge, masikini na wanaonewa, bila mifumo kama Utandawazi wenye sura ya ubinadamu, soko huria lenye sura ya ubinadamu, wanyonge wataendelea kuwa wanyonge na masikini wataendelea kuwa masikini. Mfano mzuri ni wa nchi za Latin Amerika.

Na mfano mwingine ni wa hapa kwetu Tanzania. Tulipoamua kutupilia mbali mifumo ya kutetea wanyonge na masikini kama vile Siasa ya ujamaa na Kujitegemea, siasa ambayo Kanisa Katoliki, halikuiunga mkono hata siku moja, tunaanza kushuhudia ufa mkubwa kati ya walionacho na wasiokuwa nacho. Tunashuhudia wanyonge wanadidimia katika unyonge wao na masikini wanaendelea kuwa masikini.

Siku za mwisho wa maisha yake Baba Mtakatifu, alianza kuukemea ubepari. Huu ni mchango chanya, lakini haileti maana kuukemea ubepari wakati kanisa katoliki ninaendelea kuikumbatia mifumo ya kibepari, linafanya kazi, biashara na kuwekeza kwenye miradi ya kibepari.

Si lengo la makala hii kumlaumu Baba Mtakatifu, amefanya mengi, na ikiwezekana atangazwe Mtakatifu mapema iwezekanavyo. Wala si lengo kumlaumu mama Luhena, Profesa Chachage na Tido Muhando. Hoja ni kuchochea fikra ya kujifunza kuagalia pande zote mbili, chanya na hasi. Hakuna mtu anayeweza kutenda mema tu au mabaya tu. Nyongeza ya hapo ni kujifunza kutokana na matendo ya watu mashuhuri kama Baba Mtakatifu. Mema yake yanatusaidia vipi sisi kutenda mema, na mabaya yake yanatusaidia vipi kujizuia kutenda mabaya.

Sote tunafahamu jinsi ubaguzi wa rangi ulivyo mbaya. Mfumo wa ubaguzi wa rangi uliendeshwa Afrika ya kusini hadi ukakoma bila Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili, kusema neno lolote, kuandika barua ya kiuchungaji au kuukemea kwa aina yoyote ile. Je, hakuguswa na ubaya wa mfumo huo? Au ni hali ile ile ya myonge kumwacha aendelee na unyonge wake?

Imejionyesha wazi wakati wa mazishi ya Papa Yohana Paulo wa Pili, kwamba:
- Kati ya makadinali 60 weupe kuna Kadinali mmoja mweusi!
- Kati ya watu laki tano weupe kulikuwa na mweusi mmoja!
- Kanisa katoliki ni la weupe, ni la matajiri ni la wenye uwezo wa kufika ROMA. Hivyo kanisa hili litatawaliwa daima na wenye uwezo. Wanyonge, masikini na weusi hawawezi kulitawala kanisa hili.
- Kumpata Papa Mweusi, na hasa kutoka Afrika, ni ndoto!
Hivyo wakati tunaendelea kujadiliana juu ya maisha na kazi za Marehemu Papa Yohana Paulo wa Pili, ni muhimu tukaanza kutafakari kwa kina uhusiano wa kanisa hili na wanyonge, uhusiano wa kanisa hili na weusi wa Afrika. Mungu amlaze mahali pema peponi Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili. Amina.
Na,
Padri Parivatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment