MTU KUVUTIWA NA JINSIA YAKE

MAKALA HII LICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

MTU KUVUTIWA NA JINSIA YAKE

Tunataka tusitake, ni lazima sasa tuanze kujadili juu ya tukio la Padri Kulawiti. Hili si tatizo la Kanisa katoliki peke yake. Ni tatizo la dunia nzima iliyokubali kujiingiza kwenye kijiji kimoja cha utandawazi. Misamiati kama ushoga na usagaji limekuwa jambo la kawaida. Tumeanza kushuhudia ndoa za mashoga na wasagaji. Huu si wakati wa kukaa kimya na kuendelea kufunika mambo, kuendeleza “usiri” na kukaribisha giza badala ya mwanga. Huu ni wakati wa majadiliano, utafiti, kuelimishana na kusaidiana.

Tarehe 1Oktoba 1986 Kadinali Ratzinger (sasa ni Papa Benedict wa 16), alitoa mwongozo wa Kanisa Katoliki juu ya watu wanaovutiwa na jinsia zao (homosexuality). Mwongozo huu ilikuwa ni barua aliyowaandikia Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki:
“ON THE PASTORAL CARE OF HOMOSEXUALS”. Katika barua hii Kadinali Ratzinger, aliwakumbusha maaskofu juu ya mwongozo mwingine kuhusu swala hili hili uliotolewa Desemba 1975: “ Declaration of Certain Questions Concerning Sexual Ethics” uliosisitiza kwamba hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake ifanyiwe utafiti na ichukuliwe kwa uangalifu na busara.

Katika barua hiyo Kadinali Ratzinger, aliwashauri maaskofu kwamba hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake inahitaji wachungaji (mapadri) wenye kufanya utafiti kwa uangalifu mkubwa, wenye kujali, wa kweli na wenye theolojia isiyokuwa ya msimamo mkali.

Ingawa Kadinali Ratzinger, anapinga hali hii na kuiona kama hali Fulani ya ugonjwa na kufanya mambo kinyume na maumbile, anashauri watu wenye matatizo ya kuvutiwa na jinsia zao wasitengwe. Wapatiwe huduma za kiroho, washauriwe na kuvumiliwa hadi pale watakapobadilika.

Tatizo linalojitokeza kwenye barua hii ni kwamba Kadinali Ratzinger, anapinga hali hii kwa kutumia biblia. Msingi mkubwa wa hoja yake ni Biblia. Mfano anatumia kitabu cha mwanzo ambacho kinaelezea kwamba Mungu, aliwaumba Mwanamke na Mwanaume. Pia katika agano jipya anatoa mifano ya Mtakatifu Paulo anapolaani vitendo vya kulawiti na kufira.

Kama nilivyosema mwanzoni mwa makala hii kwamba matendo ya ushogo na usagaji si matatizo ya Wakristu peke yao. Haya ni matatizo ya dunia nzima. Hivyo kuyapinga ni lazima tuwe na misingi inayokubalika kwa watu wote. Ikibidi na sayansi itumike. Si watu wote wanaoamini kuumbwa kwa mwanamke na mwanaume kama kunavyoelezwa kwenye Biblia. Hata hivyo si watu wote wanaoiamini Biblia.

Lakini hata ukitumia biblia utakutana na changamoto. Ebu tuangalie mistari hii kutoka kwenye barua ya kwanza ya Paulo kwa wakorinto:
“ Au, je, hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi Utawala wa Mungu? Msijidanganye! Watu wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wafiraji au walawiti, wanyang’anyi, wachoyo, walevi, wenye kusengenya, walaghai, hao wote hawatashiriki Utawala wa Mungu” (1Wakorinto 1:9).

Wakati sisi tunaishikia bango kubwa hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake, wakati tunalaani matendo ya kulawiti, kufira, usenge, ushoga na usagaji, Paulo, anazichanganya dhambi hizi na dhambi nyinginezo kama vile uchoyo, ulevi, kusengenya na kulaghai. Na bahati mbaya hakutofautisha ili kuonyesha ni dhambi ipi ni ndogo na ipi ni kubwa. Kama ushoga na usagaji zingelikuwa ni dhambi kubwa kuliko nyingine, basi Paulo, angezitaja peke yake ili kuuonyesha mkazo. Lakini yeye anaziweka kwenye ngazi moja na dhambi nyingine. Tuna watu wangapi katika jamii zetu wanaosema uongo, walevi, walaghai na wanaosengenya? Na je hawa tumewashikia bango mara ngapi kama tunavyowashikia mashoga? Je, wachoyo ni wangapi? Dunia yetu imegawanyika katika makundi ya maskini na matajiri kwa sababu uchoyo wa mali ni mkubwa sana. Hili tumelishikia bango? Hili tunalilaani kama tunayolaani ushoga na usagaji? Katika hali ya kawaida uchoyo wa mali ni dhambi kubwa, maana uchoyo wa mali unasababisha vita, mashindano na kuvuruga amani katika dunia yetu. Ushoga umeleta vita? Umeleta matabaka katika jamii? Hili ni jambo la kujadiliana kwa kina na wala si kulipinga kwa kufuata mkumbo.

Pia tukiangalia Barua ya Paulo kwa Waroma tutakutana na kitu kilele:
“ Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile ya miili yao kwa yale yasiyopatana na maumbile. Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu…Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya, na kusingiziana……” (Waroma 1:18-32).

Hivyo kufuatana na maoni ya Paulo, ugomvi, uuaji, wivu, udanganyifu, dhuluma, ulafi na ufisadi, ni tamaa mbaya kama ilivyo kuacha kufuata matumizi ya maumbile ya mme na mke na watu kuwakiana tamaa wao kwa wao (wanawake kwa wanawake na wanaume kwa wanaume). Kwa maoni ya Paulo, hizi ni dhambi ambazo ni lazima zishughulikiwe kwa pamoja.

Barua ya kwanza ya Paulo kwa Timoteo, inafafanua vizuri kile ninachotaka kusema:
“ Twajua kwamba Sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo. Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia. Watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale; sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wanaowaiba watu, waongo, na wanaoapa uwongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho ya kweli.” (1 Timoteo 1:8-10).

Kama tunasema kwamba ushoga na usagaji ni kinyume na maumbile, kama tunasema mashoga na wasagaji wana kasoro, ni wagonjwa na wana kilema kikubwa, basi tukubali kwamba na wasema uongo, walafi, mafisadi, wasengenyaji wana kasoro, ni wagonjwa wana kilema kikubwa na wanaishi kinyume na maumbile!

Hata tukiachana na Biblia. Tukiangalia Mwongozo wa kanisa Katoliki kuhusu swala hili uliotolewa Desemba 1975 na ule wa Kadinali Ratzinger, yote inakazia Utafiti juu ya hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake. Je jambo hili limefanyika? Tuangalie hapa Tanzania. Utafiti huu umefanyika? Kanisa katoliki la Tanzania limejenga mazingara ambamo watu wenye kilema hiki wanaweza kujitokeza wazi na wakakubalika na kusaidiwa bila kungoja matukio kama lile la padri kulawiti. Kadinali Ratizinger, alishauri kwamba watu wenye matatizo haya wasitengwe, wapatiwe huduma zote za kiroho, wasikilizwe na kusaidiwa kwa kutumia hekima na busara kubwa. Tumesikia kwamba huyu Padri aliyelawiti, amesimamishwa kutoa huduma za kiroho. Je, huku si kumtenga? Kama kuna mapadri wengine wenye matatizo kama haya watakubali kujitokeza ili wasaidiwe? Je, kama kuna waumini wengine wenye matatizo kama haya watajitokeza? Kama padri amesimamishwa kutoa huduma za kiroho si waumini wakijitokeza watafungiwa huduma za sakramenti na kutengwa na kanisa?

Tusikae kimya. Tujadiliane, tufanye utafiti, tuelimishane na kusaidiana ili tuweze kuendelea kuishi hapa duniani kwa furaha, heshima na matumaini.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment