TUNAWAAMINI MAMA ZETU KUTULEA KWANINI LEO TUSIWAAMINI KUTUONGOZA?

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

TUNAWAAMINI MAMA ZETU KUTULEA KWANINI LEO TUSIWAAMINI KUTUONGOZA?

Mambo mawili yamenisukuma kuandika makala hii. Jambo la kwanza ni maneno ya mwandishi mmoja katika mojawapo ya magazeti ya hapa nchini. Maneno hayo au maoni hayo yalikuwa yanasema hivi: “ Nakumbuka Sheikh Yahya Hussein alitabiri kwamba mteule wa CCM kugombea urais wa Muungano angekuwa mwanamke .Sasa ameteuliwa Jakaya Kikwete (mwanamume); yeye amegeuza na kusema kwamba utabiri wake upo pale pale kwa kuwa Kikwete ana sura ya nyota ya kike, Haya si matusi kwa Kikwete?” (Tanzania Daima Jumapili 12.6.2005).

Kilichonigusa kwenye maoni haya si ule utabiri wa Sheikh Yahya Hussein, bali nilikerwa na maoni ya mwandishi anayesema kwamba kuifananisha sura ya Kikwete na kusema kwamba Kikwete ana nyota ya kike ni matusi. Hili ndilo ninapenda tujadili, tuelimishane na ikiwezekana jambo hili tulikemee.

Jambo la pili ni kwamba jana wakati nikiwa bado ninatafakari kwa kina juu ya udhalilishaji na unyanyasaji huu wa kijinsia nilitembelea ofisi za shirika la KIVULINI. Shirika hili linatetea haki za wanawake na hasa limelenga kuzuia ukatili majumbani. Lina makao yake Jiji Mwanza. Si kuwa na lengo la kuamsha majadiliano juu ya mwandishi anayefikiri kumfananisha mwanaume na mwanamke ni tusi, nilikwenda kwenye ofisi hiyo kwa mambo mengine, hasa juu ya ukatili majumbani, lakini ofisi hiyo ikazua jambo jingine ambalo linahusiana kwa karibu na lile la mwandishi niliyemzungumzia kwenye jambo la kwanza lililonisukuma kuandika makala hii. Kwenye ofisi hiyo nilikaribishwa na Bango, lenye maneno: “Tunawaamini mama zetu kutulea kwa nini leo tusiwaamini kutuongoza?”.

Hili la pili lilinikumbusha lile la kwanza na kuniingiza kwenye tafakuri ya nguvu. Hili Bango la KIVULINI, lililotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na mashirika mengine ya kutetea haki za wanawake kama TAMWA, linaweza kuzaa mabango mengine kama kwa mfano: “ Tunawapenda wanawake, kwa nini basi tusiwathamini na kuuheshimu utu wao?” au “ Mungu ,kaumba jinsia mbili, mwanamke na mwanaume, kwa nini basi jinsia moja iwe bora kuliko nyingine?”.

Bango hili la KIVULINI bila shaka lilikuwa likilenga kwenye uchaguzi mkuu unaokuja. Ni bango la kuwakumbusha wapiga kura kwamba uongozi si wa wanaume peke yao. Pia ni bango la kuwakumbusha wanawake kwamba kama wanaaminika katika malezi ni lazima waaminike katika kuongoza. Hili ni bango la kuchochea fikira juu ya usawa wa kijinsia katika maisha yote ndani ya jamii yetu. Kwamba mtu kuwa mwanamke si bahati mbaya, si dhambi na wala si tusi! Kwamba mwanamke anaweza mambo muhimu katika jamii kama vile malezi.

Lakini hata tukirudi nyuma na kuangalia maisha ya kila siku. Ukitaka kuiona hasira ya mwanaume yeyote yule katika jamii yetu mwambie yeye ni mwanamke au ana mawazo ya kike. Ni lazima yatokee magomvi makubwa. Hakuna mwanaume anayependa kufananishwa na mwanamke! Upande mwingine ukimwambia mwanamke ni shupavu kama mwanaume, au ana hekima, busara na kipaji kama mwanaume anafurahi sana, ingawa kuna ukweli kwamba kuna wanawake shupavu, wenye hekima, busara na vipaji vingi hata kuwazidi wanaume. Wanaume hawapendi kufananishwa na wanawake! Inashangaza sana, maana wanawake wanatuzaa, wanatulea, wanalinda usalama wetu tukiwa watoto hadi tunapokuwa na akili ya kujitegemea, wanatupenda, wana huruma ya hali ya juu – lakini hakuna mwanaumme anayependa kufananishwa na huruma hii na upendo huu!

Wanaume, wanawapenda wanawake na kuwatamani tu. Mtu anaweza kupoteza pesa zote na mali yote akimtafuta mwanamke aliyemvutia na kuingia moyoni mwake. Watu wanatelekeza familia na kupoteza kazi wakiwatafuta wanawake waliowavutia, wengine wanajiingiza kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa na wakati mwingine wanapoteza maisha yao wakipigana kuwapata wanawake waliowavutia – lakini hakuna anayependa kufananishwa na kile anachokitafuta kwa gharama yoyote ile. Hakuna mwanaume anayependa kufananishwa na kiumbe anayependwa na kupinganiwa na kila mwanaume. Hivi kweli ni tusi kufananishwa na mwanamke au kuna kasoro Fulani katika mfumo wa jamii yetu, kasoro inayohitaji tiba ya haraka?

Malaya ni mwanamke, changudoa ni mwanamke, wazinzi ni wanawake. Ndoa ikivunjika anayelaumiwa kwa kutokuwa na uaminifu ni mwanamke. Lakini Malaya anatembea na mwanaume, changudoa anatembea na mwanaume, yeyote anayezini katika hali ya kawaida ni lazima azini na mwanamke. Anayelaumiwa kwa matendo yote hayo machafu ni mwanamke! Hivi ni kweli mwanamke ndiye anayefanya yote haya au kuna kasoro Fulani katika mfumo wa jamii yetu, kasoro inayohitaji tiba ya haraka?

Kusema kwamba Jakaya Kikwete ana sura na nyota ya kike ni tusi gani? Ukweli ni kwamba Kikwete, ana baba na mama. Kama sura yake haifanani na ya baba yake, itafanana na ya mama yake – au itachangia pande zote mbili. Hata tukiingia katika mambo ya kisayansi, ni lazima Kikwete, ana chembe chembe za uhai kutoka kwa baba na mama yake. Kumfananisha na mwanamke, haina maana atageuka na kuwa mwanamke. Lakini hata hivyo mwanamke ni mtu, ni binadamu. Hakuna dhambi mwanamke kumfanana mwanaume na mwanaume kumfanana mwanamke.

Mwenye mawazo kama haya kwamba kufanana na mwanamke ni matusi asingependa kabisa mwanamke achaguliwe kushika nafasi ya uongozi. Kama kumfanana mwanamke ni tusi, itakuwaje mwanamke akishika madaraka ya kuongoza au kufanya kazi ambazo wenye mawazo potofu wanaamini ni kazi za wanaume peke yao? Maana kama kumfanana mwanamke ni tusi, basi huyu ni kiumbe asiyekuwa na nafasi na wala hafai kuwepo!

Kwa bahati nzuri TLP na NCCR-Mageuzi, wameleta mapinduzi makubwa katika mtazamo huu potofu. Wamesimamisha wanawake kuwa wagombea wenza. Hili ni jambo la kupongezwa na kuigwa. Hii ni changamoto kubwa katika jamii inayotawaliwa na mfumo dume, jamii yenye watu wanaofikiri kwamba kumfanana mwanamke ni matusi. Jamii inayoamini kwamba wanawake hawawezi kitu zaidi ya kukaa jikoni kupika na kuipendezesha nyumba. Hata hivyo na hawa wa TLP na NCC-Mageuzi bado wananuka harufu ya mfumo dume, maana kama wangetaka kufanya mapinduzi ya kweli, basi wangewasimamisha wanawake kuwa wagombea urais! Kwanini mwanamke awe mgombea mwenza, asiwe mgombea Urais? Na mwanaume akawa mgombea mwenza? Wanawake wameonyesha uwezo huu katika nchi mbalimbali, inawezekana pia na hapa Tanzania, tukikubali kubadilika.

CCM , chama “dume”, chama chenye uzoefu wa kutawala kwa miaka mingi, bado kinatawaliwa na mfumo dume! Wagombea wa urais wa Muungano na Visiwani ni wanaume. Mgombea mwenza wa Muungano ni mwanaume, na katika historia yake ya kutawala CCM hakijawahi kuwa na mwenyekiti mwanamke, rais mwanamke, makamu wa rais mwanamke, waziri kiongozi mwanamke au waziri mkuu mwanamke. Ngazi za juu katika uongozi wa chama na serikali vinashikiliwa na wanaume! Si kweli kwamba CCM, haina wanachama wanawake wenye uwezo wa kuwa mwenyekiti au rais. Wapo akina mama wengi wenye uwezo wa kuongoza. Lakini tatizo ni kama bango la KIVULINI, Linavyosema: “ Tunawaamini mama zetu kutulea kwa nini leo tusiwaamini kutuongoza?”.

Ni nani asiyeamini katika malezi ya mama yake? Ni nani asiyemwaini mama yake? Mama ni kimbilio, mama ni ufunguo wa kufunga siri zote, mama ndiye anayejua udhaifu wa kila mja na kuutunza. Kama ni mwizi, atasema mtoto wake anasingiziwa. Mama huyo awe wangu au wako, hana tofauti na mama wengine, hana tofauti na wanawake wengine. Karama za mama ni zile zile. Karama hizi zilizojaa utu na wema, upendo na uvumilivu, unyenyekevu na kusamehe kama ni matusi, basi ni heri tusi hilo!

Waswahili wana msemo usemao: “Nani kama mama?” Maana yake ni kwamba mama ana ubora uliotukuka! Huwezi kuulinganisha ubora huu na kitu chochote kile. Mama huyo ni mwanamke! Mara nyingi ninajiuliza ni kwa nini wasiseme: “Nani kama baba?”. Walioutunga msemo huu walikuwa na maana kubwa: Hakuna anayemjali mtoto wake kama Mama, hakuna anayempenda mtoto wake kama mama na hakuna anayemlea mtoto na kumlinda kama Mama. Msingi wa familia ni mama. Mama akiyumba kimaadili, familia nzima inayumba! Hivyo mama ni kiongozi wa familia. Uzoefu huu wa kuziongoza familia, unaweza kuwa mchango mkubwa wa akina mama katika kuiongoza jamii yetu. Hata hivyo jamii inajengwa juu ya msingi wa familia. Wema wa akina mama, upendo wa akina mama, uvumilivu wa akina mama, unyenyekevu wa akinamama unaweza kuchangia kujenga jamii yenye upendo, wema unyenyekevu na uvumilivu – jamii isiyokuwa na vita wala mashindano. Ni ukweli usiopingika kwamba mfumo dume, unavuruga amani popote duniani. Wanaume hawana uvumilivu na unyenyekevu, wanaume wanapenda mashindano na wamejaa uchu wa madaraka!

Bahati mbaya akina mama hawapewi nafasi ya kuongoza. Wanawake hawajitokezi kugombea ubunge na udiwani, wengi wao wanasubiri nafasi za viti maalumu. CCM, kati ya wagombea 11 walijitokeza kuwania kiti cha urais hakuna mwanamke hata mmoja aliyejitokeza! Uongozi unabaki mikononi mwa wanaume na mbaya zaidi ni kwamba jamii imewapumbaza wanawake kuamini kwamba hawawezi. Kama mtu angeandika bango jingine lingesema hivi; “ Mama zetu mna uwezo wa kulea na kuongoza, mbona mnakubali kupumbazwa kwamba hamna uwezo wa kuongoza?”

Wapiga kura wengi ni wanawake. Wangekuwa wamejikomboa na kukombolewa, ingekuwa patashika kumpitisha mgombea mwanaume. Lakini sasa hivi Ukimpanga mwanaume na mwanamke, wanawake watamchagua mwanaume na kumuacha mwanamke mwenzao. Inasikitisha, ila ndiyo hali halisi!

Kwa vile wanawake wamepumbazwa, mtu anaweza kusema chochote juu yao, na wanakaa kimya bila kujitetea. Mfano kusema kwamba kumfananisha Mheshimiwa Kikwete na mwanamke ni tusi, tulitegemea akina mama walipigie kelele. Wasimame na kupinga kwa nguvu zote. Kumfananisha Kikwete, na mwanamke ni kumfananisha na binadamu wa jinsia nyingine, si kumfananisha mheshimiwa huyu na mnyama wa aina nyingine au kitu kingine chochote kisichokuwa na uhai.

Tunahitaji mabadiliko katika jamii yetu. Tunahitaji mfumo wa kutuelekeza katika kutegemeana, kushirikiana, kukamilishana na kuthaminiana. Tunahitaji mfumo wa kuleta uwiano katika jinsia. Mfumo ambao hautukuzi jinsia moja na kuinyanyasa nyingine.

Mfumo huu ungekuwa wa kiroho zaidi ya kisiasa. Dini zingetusaidia kuwaandaa watu kiroho, ili wajenge moyo wa kupendana na kuthaminiana miongoni mwa jinsia zote. Bahati mbaya dini zote tulizonazo zinaongozwa na mfumo dume! Haziwezi kuwa za msaada mkubwa. Mfumo wowote unaotukuza jinsia moja na kunyanyasa nyingine, hauwezi kujenga amani ya kweli, hauwezi kuleta uhuru wa kweli na hauwezi kujenga umoja wa kitaifa. Kama alivyosema Mwalimu Nyerere, kwamba ukishafanya ubaguzi wa aina yoyote ile, ni lazima mzimu wa ubaguzi ukuandame kila sehemu.

Tunapofikiria na kupanga mikakati ya kuboresha uchaguzi mkuu wa mwaka huu, na hili la kujenga mifumo ya kuleta usawa wa kijinsia tuliweka kwenye agenda.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment