POSTA NA SIMU AFRIKA 1942-1993

UHAKIKI WA KITABU: MIAKA 53 YA UTUMISHI KATIKA POSTA NA SIMU AFRIKA 1941- 1993.


1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Miaka 53 ya utumishi katika Posta na Simu Afrika 1941 – 1993 na kimetungwa na Mzee Rajabu M. Yusuf. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Tanzania Publishing House Limited na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9976 1 0212 3 kimechapishwa mwaka 2008 kikiwa na kurasa 132. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI.

Kitabu hiki ambacho bado hakijazinduliwa, kimeandikwa na Mzee Rajabu M.Yusuf. Kinaelezea kwa kifupi historia ya Posta na Simu katika Afrika kwa kadiri ya mtazamo wa mwandishi kwa kuhusisha uzoefu na mang’amuzi katika utumishi wa mwandishi. Kwa kifupi kitabu hiki kina ujumbe wa aina mbili: Maisha ya Mzee Rajabu M. Yusuf na Maisha Posta na Simu Afrika (1941- 1993).

Ni watu wa chache katika taifa letu waliofanikiwa kuifanya kazi kama alivyoifanya Mzee Rajabu M.Yusuf. Kama anavyosema Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, katika dibaji ya kitabu hiki “ Kihifadhiwacho kifuani hupotea, kiandikwacho karatasini hubakia...” Kitabu hiki kitatuelimisha wengi, maana kilichoandikwa kimeandikwa! Bahati mbaya watanzania walio wengi hatujakubaliana na msemo huu na kukubali kuandika chini yale tunayofahamu, yale tunayoyaishi na yale tunayoyashuhudia siku hadi siku. Mengi yanapotea na kusahaulika!

Kitabu kinazo sura 19, Kiambatisho na marejeo, ramani ya Afrika, ramani ya Afrika mashariki na picha zinazoonyesha matukio mbalimbali ya Historia ya Posta na Simu Afrika, paia na picha za mwandishi akiwa kwenye matukio mbali mbali na kwenye mikutano mbali mbali ya kimataifa. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Baada ya awamu nne za Uongozi wa taifa letu, kizazi kilichoshuhudia awamu zote hizi kinaanza kutoweka. Bila kuandika ushuhuda wa kizazi hiki, tutabaki bila historia. Bahati nzuri kuna maandishi ya historia ya Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere, pia kuna maandishi ya historia ya Marehemu Abed Amani Karume na wengine wachache kama vile Wanawake wa Tanu wakiongozwa na Bibi Titi. Wengine wanaondoka bila kuandika na hakuna kinachoandikwa juu yao.

Mzee Rajabu M. Yusuf, ameamua kutufanyia kazi hii. Ametuandika historia ya maisha yake na hasa historia ya kazi aliyoifanya kwa kipindi cha miaka 53! Kwa kusoma kitabu chake tunapata historia ya Posta na Simu. Kwa mfano tunatambua kwamba:

Kwa upande wa Tanganyika, koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki lililojumuisha nchi za Tanganyika, Rwanda na Burundi, huduma ya Posta pamoja na ile ya telegrafu zilianzishwa mnamo mwaka wa 1893. Baada ya Vita vya kwanza vya dunia, huduma za Posta na Simu zilitolewa chini ya Idara ya Posta na Simu ya serikali ya kikoloni ya Kiingereza nchini Tanganyika. Wakati huo, nchi za Rwanda na Burundi ziliwekwa chini ya Serikali ya ukoloni wa Ubelgiji. Pia kwamba Benki ya Posta iliuundwa 1927 na kuwekwa chini ya uendeshaji wa Mkurugenzi wa Posta na Simu kwa niaba ya Hazina ya Serikali Kuu.

Kwamba kwa upande wa Kenya, huduma za Posta na simu zilianzishwa mnamo mwaka 1890 na Uganda huduma hii ilianzishwa mnamo mwaka wa 1895.

Ilipofika 1933 Idara za Posta na Simu za nchi tatu (Kenya, Uganda na Tanganyika) ziliungana na kuwa idara moja chini ya mamlaka ya Postamasta Mkuu. Makao Makuu yalikuwa Nairobi, Kenya. Wakati huohuo, kila nchi ilikuwa na Mkurugenzi wake aliyewajibika kwa Postamasta Mkuu, kupitia kwa Katibu Mkuu (Chief Secretary) wa nchi husika.

Kwamba mnamo mwaka wa 1948 iliundwa East African Posts & Telecommunications Administration. Tanganyika, ilipopata uhuru kulikuwa na mabadiliko na huduma hii ya Posta na simu ilijulikana kama East African Common Services Organisation (EACSO). Nchi tatu za Tanganyika, Uganda na Kenya zilipopata uhuru na kuunda Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, huduma ya Posta na Simu, ilibadilika na kuwa East African Posts & Telecommunication Corporation. Makao yake yakahamia Kampala Uganda.

Mwaka 1977 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilisambaratika, wakati huo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Posta na Simu wa Jumuiya hiyo, alikuwa ni mwandishi wa kitabu hiki, Mzee Rajabu Mabula Yusuf, mkataba wake ulimalizika Aprili 1978.

Tarehe 27.10.1977 Shirika la Posta na Simu Tanzania (TPTC) liliundwa ili kuchukua nafasi ya East African posts&Telecommunications Corporation. Na kuanzia 1Jaunari 1994 TPTC iligawanyika na kuunda Shirika la Posta Tanzania (TPC), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hii ndiyo historia nzuri ya Posta na Simu, anayotuletea mwandishi katika kitabu chake. Labda bila historia hii mwandishi asingesukumwa na lolote kutuletea historia yake! Karibia maisha yake yote yamekuwa ni ya Posta na Simu:

Rajabu Mabula Yusuf, alizaliwa tarehe 8 Agosti 1924. Alipata elimu ya msingi Handeni Chanika mwaka 1931-1934, na shule ya kati mjini Tanga 1935 – 1938 na hatimaye elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Tanga mwaka 1939-1940. Kati ya 1941 na 1942 alipata mafunzo ya mawasiliano ya posta na simu, Dar-es-Salaam. Kadhalika, alipata mafunzo nchi za nje, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Marekani na Japani.

Amefanya kazi katika asasi za posta na simu kwa takriban miaka hamsini na mitatu, huku akishika nyadhifa mbalimbali. Mathalani, alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mkurugenzi Mkuu wa Posta na simu Afrika Mashariki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Simu Barani Afrika. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. MUHTASARI WA KITABU.

Sura ya kwanza inaelezea Historia ya Mawasiliano Duniani na mchango wa Posta katika Maendeleo. Hapa tunaelezwa mengi juu ya aliyeanzisha huduma ya mawasiliano na hatua za huduma hii kuanzia mfumo wa mawasiliano ulioendeshwa kwa njia ya maneno ya kinywa au kwa maandishi kwa kutumia matarishi wapanda farasi au waenda kwa miguu, mashirika ya dini yalianzisha kusafirisha barua hadi teknolojia mpya za “Analogue” na “digital”. Mawasiliano yameharakisha maendeleo na kuwasogeza watu karibu.

Sura ya Pili, mwandishi anaelezea historia ya Mawasiliano katika Afrika ya Mashariki. Hapa tunaelezwa jinsi hali ya mawasiliano ilivyokuwa katika Koloni la Wajerumani Afrika Mashariki, yaani Tanganyika, Rwanda na Burundi. Baadaye jinsi mawasiliano yalivyokuwa Tanganyika ilipokuwa chini ya utawala wa Waingereza. Pia tunaelezwa huduma ya Posta na Simu ilivyokuwa kule Uganda na Kenya na baadaye nchi hizi tatu zilivyounda umoja wa huduma hii baada ya Uhuru.

Katika sura hii ya pili, ndipo Mwandishi anaelezea maisha yake ya utoto, shule na wazazi wake. Yeye mtu wa Tabora, lakini wazazi waliishi Tanga na baadaye walirudi kwao Tabora.

Katika Sura ya Tatu, mwandishi anatuelezea jinsi alivyopata ajira katika idara ya Posta na Simu. Na jambo muhimu katika sura hii ni kujifunza kutoka kwake pale anaposema hivi:

“Maskini, baadaye nilikuja kugundua kwamba kumbe ningefanya makosa kutokana na uelewa wangu mdogo kuipuuza sekta hii. Kwa yamkini, mawasiliano ya Posta na Simu yana mchango mkubwa sana katika kuchochea maendeleo ya watu katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na sekta ya afya kitaifa na kimataifa. Maendeleo ya maana hayawezi kupatikana bila mawasiliano safi na ya kutosha. Niligundua pia kwamba Posta na Simu ndio ushirikiano mkongwe zaidi duniani ulio na manufaa kwa wanadamu wote. Kama nilivyoeleza chini ya Historia ya Mawasiliano Duniani kwa upande wa simu, ushirikiano huo ulianzishwa mwaka 1865 wakati ulipoundwa Umoja wa Simu Duniani (ITU) na kwa upande wa Posta wakati ulipoundwa Umoja wa Posta Duniani (UPU) mwaka 1874. Ni utaratibu wa ushirikiano wa kimataifa mkogwe zaidi kuliko hata Umoja wa Mataifa....” (Uk wa 15).

Hapa kuna funzo na kutusaidia kutambua kwamba ushirikiano wa Posta na Simu ni mkongwe. Hivyo mawasiliano ni chombo cha umoja kuliko mengine yote!

Sura ya nne, mwandishi anasimulia juu ya kipindi chake cha Mafunzo ya posta. Hapa la kujifunza ni huduma ya posta iliyokuwa ikitolewa kwenye vituo vya treni. Huduma hii iliyokuwa nzuri ilisitishwa miaka 1950 kwa sababu ya kukosa tija.

Sura ya tano na sita mwandishi anaelezea maisha katika vituo vyake vya kazi: Mbeya, Tukuyu, Dodoma, Tanga, Arusha, Bukene, Urambo, Tabora. La kujifunza ni uzalendo wa kukubali kufanya kazi sehemu yoyote ya Tanganyika na jinsi utendaji ulivyokuwa wakati wa mkoloni. Uwajibikaji ulikuwa mkubwa kuliko leo hii!

Sura ya saba, mwandishi anaelezea maisha yake katika nchi ya Kenya, alikokwenda kufundisha kwenye chuo cha Posta na Simu. Huko anatuelezea ubaguzi wa rangi kati ya Wazungu na Waafrika na kati ya Wahindi na Waafrika. Pia tunaelezwa vita vya Mau Mau na habari za ndoa ya kwanza ya mwandishi. Ndoa hii iliyofungwa 1951, ilidumu miaka 20 na kuvunjika 1971.

Sura ya nane, ni maelezo mengine juu ya vituo vya kazi alikoishi na kufanya kazi mwandishi: Tabora, Mpanda, Mwanza, Geita na Kigoma. Hapa tunasikia vuguvugu la Waafrika kutaka usawa katika kazi: “ Pale Mwanza chama chetu hakikuchoka kuwakumbusha viongozi wa Posta, Wazungu na Wahindi kwamba tulichokuwa tukidai kama wazalendo haukuwa upendeleo maalumu bali fursa sawa kwa wote. Utaratibu wa enzi hizo ulimweka Mzungu juu, Mwasia kati na mzalendo chini na kwa hiyo hata mishahara nayo ilichukua sura hiyohiyo hata kama Mwafrika alikuwa na elimu sawa au ya juu na uzoefu mkubwa kazini.” (Uk wa 43).

Sura ya tisa tunasimuliwa “Naizesheni” (Africanisation”. Kipindi cha Uhuru. Mwandishi anatumwa Uingereza kusoma zaidi juu ya Posta na simu na anafunga ndoa yake ya Pili mwaka 1962 na kwa bahati mbaya nayo inavunjika mwaka 1971.

Sura ya kumi na ya kumi na moja mwandishi anasimulia mkutano Mkuu wa 15 wa Umoja wa Posta Duniani, uliofanyikia Vienna na safari za mafunzo Amerika na Japani.

Sura ya kumi na mbili na simulizi juu ya kuundwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki na ndoa ya tatu ya mwandishi. Alifunga ndoa tena mnamo mwaka wa 1972.

Sura ya kumi na tatu ni simulizi juu ya Mikutano ya Kimataifa ambayo mwandishi alihudhuria: Mkutano wa 16 wa Umoja wa Posta Duniani, uliofanyikia Tokyo Japan 1969 na Mikutano mingine ya Kimataifa iliyofanyika 1971 na 1977.

Sura ya kumi na nne, ni simulizi juu ya Mwandishi kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Posta na Simu Afrika Mashariki. Utumishi wake hadi Jumuiya inakufa na Shirika la Posta na Simu Tanzania linazaliwa.

Sura ya kumi na tano, ni kuundwa kwa Umoja wa Simu Afrika, na Mwandishi akahamia Kinshasa kufanya kazi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Simu Barani Afrika.

Sura ya kumi n asita inaelezea Miradi mikubwa miwili ya kuunganisha nchi za Afrika kimawasiliano. Miradi hii ni PANAFTEL NA RASCOM. Sura ya kumi na saba na kumi na nane zinaelezea utumishi wa mwandishi ndani ya Shirika na Posta na Simu Tanzania. Yeye kama mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, matatizo na mafanikio ya Shirika hili.

Sura ya Kumi na tisa inaelezea matukio muhimu katika Historia ya Huduma za Posta na Simu Afrika mashariki.

V. TATHMINI YA KITABU.

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Mzee Rajabu M. Yusuf, mzee wa Posta na Simu!

Awali ya yote lazima niseme kwamba kwa kuangalia hadhira anayoikusudia mwandishi, kitabu hiki kinasisimua sana, ukikianza hutaki kukiacha. Masimulizi hayachoshi na kwa vile yanaelezea matukio ya kihistoria yanayovutia sana kuyasoma.

Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kuandika historia ya maisha yake na historia ya Posta na Simu. Au kwa maneno mengine Rajabu Yusuf ni Posta na Simu, na Posta na Simu ni Rajabu Yusuf. Kwa simulizi lake, yeye na Posta na Simu ni kitu kimoja.

Tatu. Mwandishi amefanya kazi nzuri ya kutufundisha juu ya historia ya mawasiliano. Ametufumbua macho pale anapoelezea kwamba Umoja wa Posta na Simu, ni mkongwe hata kuliko Umoja wa Mataifa. Hii ni elimu nzuri na kumbukumbu nzuri katika historia ya Taifa letu.

Nnne, Pamoja na umoja wa Posta wa dunia, tunapata somo hapa kwamba hata Umoja wa Afrika Mashariki, ulianza zamani hata kabla nchi hizi kuwa huru. Mwaka 1933, nchi hizi ziliendesha huduma ya mawasiliano kwa pamoja. Hivyo tunapoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, hatufanyi kitu kipya. Ikumbukwe pia kwamba Rwanda na Burundi zilikuwa zikishiriki huduma ya mawasiliano na Tanganyika kabla ya kuwa chini ya utawala Wabelgiji.

Tano, mwandishi amefanikiwa kutushawishi kutambua kwamba utumishi katika sekta ya mawasiliano ni utumishi unaogusa jamii zote za binadamu kwa ujumla kwa vile mawasiliano ni kiungo muhimu kati ya watu takriban katika nyanja zote za maisha yao kitaifa na kimataifa katika mahusiano yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kisiasa, kiutawala, kiutamaduni, kibiashara na kiuchumi.

Sita, mwandishi ameonyesha jinsi alivyofanya kazi kwa uzalendo na uadilifu mkubwa. Pia anawashauri watanzania kuiga mfano wake. Lakini pia anahimiza serikali kuwalipa vizuri wataalamu wetu ili wasikimbie nchi yao kutafuta kazi nje ya nchi.

Saba, mwandishi anaonyesha wazi undugu wa watanzania, kwamba mtu anaweza kuishi na kupokelewa sehemu yoyote ile bila kujali kabila lake. Amekulia nakusomea Tanga, lakini nyumbani kwao ni Tabora – familia yao ilipokelewa vizuri Tanga, kama inavyopokelewa na kukubalika nyumbani kwao Tabora.

IV. HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania wakitafute kitabu hiki na kukisoma. Kitabu hiki kinapatikana kwenye duka la vitabu la TPH Bookshop, mtaa wa Samora, ili wapate elimu juu ya historia ya mawasiliano Tanzania na historia ya mambo mengine mengi ya taifa letu, Afrika Mashariki, Afrika na dunia nzima ambayo mwandishi anayataja katika kitabu chake.

Lakini kwa upande mwingine, napendekeza Shiriki la Posta Tanzania, Kampuni ya Simu Tanzania na Tume ya Mawasiliano Tanzania, wampatie Mzee Rajabu M.Yusuf, tuzo ya pekee kwa kazi aliyoifanya ya kuandika historia ya taasisi zao;

Na pia kwa vile Mzee huyu anaonekana kufanya kazi kwa muda mrefu katika Mawasiliano, ni bora akipata kumbukumbu ya aina yoyote ile katika mashirika haya: Mfano mojawapo ya majengo au vyuo vyao kupewa jina la Rajabu Yusuf, kama njia mojawapo ya kumkumbuka na kutambua mchango wake. Huyu ni miongoni mwa watanzania wachache waliofanya kazi za umma ndani na nje ya nchi kwa uaminifu mkubwa, kuna haja ya kumtuza. Tumejenga utamaduni wa kuwakumbuka wanasiasa na kuwasahau kabisa wale wanaofanya kazi za Utumishi wa Umma.

Pendekezo jingine ni kitabu hiki kutumika kwenye shule na vyuo katika somo la historia. Lakini pia vyuo vya mawasiliano vinaweza kukitumia kitabu hiki kwa kumbukumbu za huduma ya mawasiliano katika Taifa letu na bara letu la Afrika kwa ujumla.

SAA YA UKOMBOZI

UHAKIKI WA KITABU: SAA YA UKOMBOZI

1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Saa ya Ukombozi na kimetungwa na Nkwazi Nkuzi Mhango. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Tanzania Educational Publishers LTD na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9987 07 039 8. Kimechapishwa mwaka jana 2009 kikiwa na kurasa 179. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

11. UTANGULIZI

Kitabu hiki ambacho ni Riwaya, kinachambua dhana nzima ya Uhuru. Na hasa uhuru wa nchi za Afrika. Riwaya, inauweka uwazi kwamba baada ya uhuru viongozi walijinufaisha na kuwasahau kabisa wananchi.

Riwaya inawahimiza wananchi kuamka na kudai haki zao. Kwa lugha nyingine Saa ya Ukombozi , ni mapinduzi! Kinyume na mapinduzi tuliyoyazoea ya kumwaga damu, Saa ya Ukombozi inasisitiza mapinduzi ya kutumia haki ya kupiga kura.

Tunakumbushwa wananchi, yaani watawaliwa kuhakikisha wanawawajibisha viongozi wao. Mfumo unaopendekezwa ni ule wa watawala kuwatumikia watawaliwa. Nchi zote zilizoendelea zinatumia mfumo huu; ndio maana tunasikia kwamba demokrasia ya kweli ndio inajenga Uhuru wa kweli. Bila Demokrasia, watawala wanageuka na kuwa Miungu watu.

Riwaya hii inapinga ufisi, ukuku, umbwa, ukondoo, usindano, ukijiko na tabia nyingine kama hizo; inashajihisha usimba, umizani na utambuzi, utendaji na ulinzi wa haki.

Hapo ndipo utamwona mhusika mkuu, Mzee Njema, akipambana na uongozi mbovu kuanzia kijijini mwake hadi wilaya na hatimaye, taifa. Cheche ya shujaa inawasha moto unaouamsha na kuukengeua umma kiasi cha kuangusha serikali dhalimu ya Mizengwe kupitia sanduku la kura.

Riwaya, inazo sura 27. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Riwaya hii ni ya kubuni. Hata nchi inayoongelewa ni ya kubuni. Lakini kama anavyoandika Ngugi wa Thiong’o, hata kama nchi ni ya kubuni, jina lake linakuwa na maana ya kufikirisha. Ukisoma vitabu vya Ngugi, bila kufahamu lugha yake ya Kikikuyu, ni wazi unapoteza utamu na ujumbe wa riwaya zake. Kwa Mswahili anayesoma Saa ya ukombozi, anapata utamu na ujumbe wa riwaya, maana hata majina yamebeba ujumbe mzito.

Jina la nchi ni Mizengwe. Jina hili linampatia msomaji hamu ya kutaka kujua nchi hii ya mizengwe. Penye mizengwe mambo hayawezi kwenda vizuri. Kufuatana na mila za Kiafrika, majina yanatokana na matukio fulani katika jamii. Kama nchi ni Mizengwe, ni kuna mizengwe au huko nyuma kulikuwa na mizengwe iliyoendeshwa katika nchi hii ya kufikirika. Jina la kijiji kilichozaa Saa ya Ukombozi ni Githakwa, sina habari kamili ya mwandishi anatoka kabila gani, lakini kufuatana na uandishi wake ni lazima jina la kijiji linamaanisha kitu fulani kuhusiana na uhuru wa wanakijiji hicho, maana vuguvugu la mapinduzi linazaliwa hapa. Jina la Mkoa ni Chelewa! Inaonyesha jinsi mkoa ulivyokuwa umechelewa kufikia ukombozi wa kweli.

Lakini pia ukiangalia majina ya wahusika, unaona kwamba yanatoa ujumbe: Matatizo, Mafanikio, Huzuni, Njema, Kupata, Furaha nk., yanaongeza si utamu tu wa hadithi bali yanafikisha ujumbe kwa haraka na kumfanya msomaji kutafakari wakati akisoma.

Ujumbe unazama zaidi pale kikosi cha kuzuia vurugu kinapopatiwa jina la PPK ( Pinga Pata Kipigo). Msomaji atatambua haraka Mizengwe ni nchi ya namna gani na inaongozwa vipi. Inaonyesha vyombo vya usalama vipo kuhakikisha hakuna mtu mwenye kutoa mawazo huru, kutoa mawazo huru ni kupinga na ukipinga ni lazima upate kipigo.

Wataalamu wanasema kwamba fasihi ni kioo cha jamii. Mbali na majina yaliyotumika katika Riwaya hii, matatizo yanayotajwa yanafanana kabisa ya yale hapa Tanzania. Kijiji cha Githakwa, kinakataa ardhi yake kumegwa na kugawiwa kwa mwekezaji wa madini. Haya ni matatizo yanayozikumbuka sehemu nyingi za Tanzania. Loliondo, tumeshuhudia Wamasai wakifukuzwa kwenye makazi yao ili ardhi apewe mwekezaji. Lakini maeneo mengi ya madini, watu wamekuwa wakihamishwa ili kupisha miradi ya madini. Tumeshuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira; kule Musoma maji yenye kemikali kali yameingia kwenye mkondo wa maji wanayotumia wananchi na watu wameathirika.

Wataalamu na wachambuzi wa maswala ya kidunia wanasema vita kuu ya tatu ya dunia italetwa na kugombea maji. Lakini nafikiri kabla ya hapo kutazuka vita kali ya kugombea ardhi. Serikali za nchi huru za Afrika, zimefanya uzembe au viongozi wamefumba macho na kuendeleza ufisadi wa Ardhi na kutengeneza bomu litakalowalipukia vizazi vijavyo. Kuwamilikisha wawekezaji wa nje ardhi kwa kipindi cha miaka 99, ni uwendawazimu usiokuwa na mipaka!

Ingawa mwandishi anaandika kwa kuficha sana na kutufanya tuamini kwamba anazungumzia nchi ya kufikirika ukweli unabaki kwamba Mizengwe ni Tanzania. Mwandishi huyu ni miongoni mwa watanzania wengi ambao wamekuwa wakifikiri kwamba tunahitaji mapinduzi makubwa katika nchi yetu. Na maoni ni kwamba mapinduzi haya yatalewa na watu wa chini kabisa kule vijijini au watoto wa mitaani waliojazana kwenye miji yetu. Kwa vyovyote vile Saa ya ukombozi haikwepeki!

Pamoja na kwamba mwandishi anapenda ukombozi uje kwa njia ya kura, anasahau kwamba umezuka mtindo wa kuiba kura. Yaliyotokea Kenya, si kwamba watu walitaka kuchinjana – bali wizi wa kura ulileta tatizo hilo! Mazingira yanayoizunguka riwaya hii; pamoja na nia njema ya mwandishi ya kutaka kutuaminisha kuleta mapinduzi bila kumwaga damu, utabiri wake unaweza ukawekwa pembeni na hali halisi inayotokea kwenye nchi mbali mbali za Afrika. Uganda mfano haiwezi kuleta mabadiliko au mapinduzi au ukombozi kwa sanduku la kura; sote tunafahamu jinsi Mseveni anavyotumia nguvu zote kubaki madarakani. Tanzania, pia tumeshuhudia mara nyingi ujanja na wizi wa kura. Kuna saa itafika, na bila shaka itakuwa saa ya ukombozi watu watakaposema hapana na kuamua kushika silaha za kumwaga damu. Utabiri wa Saa ya Ukombozi unakuja katika mazingira magumu!

Mwalimu Nkwazi N. Mhango, ni pacha wa Mwandishi maarufu Mpayukaji na Msemahovyo katika gazeti la Tanzania Daima. Mwalimu Nkwazi anasoma nchini Kanada. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. MUHTASARI WA KITABU.

Riwaya inaudurusu na kuzulu uhuru na dhima nzima ya kuwa huru. Inaona shaka na uhuru wa baadhi ya nchi barani Afrika unaowanufaisha watawala waliojigeuza miungu pamwe na walamba viatu wao. Watu wa kawaida hawaruhusiwi kutia mkono kwenye deste nao wale halua!

Riwaya hii inaualika umma kushika hatamu. Inashadidisha utathimini na kuuhoji upya uhuru wanaoambiwa ni wake si wake. Katika kufanikisha hilo, tofauti waathirika waishio kwa matumaini kuupigania na kuupata uhuru wa kweli kupitia kwenye sanduku la kura.

Riwaya inahimiza watawaliwa kuhakikisha wanawajibisha watawala kama sehemu ya uwajibikaji wao. Kila mmoja awajibike kwa mwenzake. Inawataka watawala wawatumikie watawaliwa badala ya kuwatumia kama punda wa kuwabeba wao na mizigo yao.

Riwaya inapinga ufisi, ukuku, umbwa, ukondoo, usindano, ukijiko na tabia nyingine kama hizo; inashajiisha usimba, umizani na utambuzi, utendaji na ulinzi wa haki. Riwaya inaielezea nchi ya Mizengwe ambayo ina tabia kuu tatu zinazoweza kufananishwa na nchi yoyote, nazi ni matatizo, mafanikio yake na hamu ya kujikomboa kutoka mikononi mwa adha zote zinazoikabili nchi hii.

Tofauti na nchi nyingine iwayo, wananchi wa Mizengwe hasa wanakijiji, wanafanikiwa kuudekua mfumo wa kiunyonyaji na wa ukandamizaji uliokuwa ukiwadhalilisha na kuwadhulumu. Hapo ndipo utamwona mhusika mkuu Mzee Njema akipambana na uongozi mbovu kuanzia kijijini mwake hadi wilaya na, hatimaye, taifa. Cheche ya shujaa inawasha moto unaouamsha na kuukengeua umma kiasi cha kuangusha serikali dhalimu ya Mizengwe kupitia sanduku la kura.

Ukiachia mapinduzi ya wafanyakazi nchini Ufaransa, kwa Afrika wanakijiji wa Githakwa wakiongozwa na mzee Njema na wenzake, wanafungua ukurasa mpya kwa kuanzisha na kufanikisha mapambano ya ukombozi kutokea kijijini kwenda mijini na kutoka kwenye mapambano ya bunduki kwenda kwenye sanduku la kura. Pamoja na kwamba wanakijiji walikuwa na uwezo wa kutumia silaha zao kama mapanga, mikuki hata mawe, hawakufanya hivyo. Kwani siyo jibu wala njia ya kistaarabu ya kujikomboa.

Riwaya, licha ya kuwatia shime wanyonge watawaliwa, inawapa changamoto. Inalenga kuamsha ari na mori wa kujiletea ukombozi wa kweli. Wakijitambua na kuamua kwa dhati, kila kitu kinawezekana.

Wanakijiji wa Githakwa wamejikusuru ili kujinusuru na kushinda hila na njama za wezi wachache wenye madaraka kutaka kubinafsisha kijiji chao kwa tajiri wa Kizungu, Bwana Sucker.

Hata baada ya mzee Njema kuleta ukombozi kwa kuondoa serikali ya kidhalimu, hajiungi na serikali mpya; wala hataki kulipwa fadhila wala kusaliti ukombozi. Kwa sababu ukombozi ni jukumu la kila mwanajamii. Anakaa nje ili awapime na kuwapa changamoto viongozi wapya kama nao watalewa madaraka.

Hakika riwaya hii inafungua ukurasa mpya ambapo kwa mara ya kwanza, wanakijiji wanatoa somo adimu na adhimu kwa nchi ya Mizengwe.

V. TATHMINI YA KITABU

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Mwalimu Nkwazi N. Mhango.

Awali ya yote lazima niseme kwamba kwa kuangalia hadhira anayoikusudia mwandishi ya Saa ya ukombozi, kitabu chake kinasisimua sana kutokana na mtindo alioutumia mwandishi.

Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kubainisha na kisha kutoa majibu kamilifu ya Saa ya Ukombozi.

Tatu, kama nilivyosema mwanzo ni kwamba matumizi ya majina kama vile nchi ya Mizengwe, na wahusika wengine kama vile Matatizo, Mafanikio, Huzuni, Njema, Kupata, Furaha yanafanya kitabu chake kusomeka kwa mvuto na kumsaidia msomaji kusafiri na mwandishi hadi mwisho.

Nne, Mwandishi anatabiri Saa ya Ukombozi kwa kupitia sanduku la kura. Amejitahidi sana kukwepa umwagaji damu kama ule anaoutabiri Mwalimu Mkuu wa watu, katika kitabu chake. Ukiangalia kwa makini na kusoma kwa uangalifu, utagundua kwamba riwaya ya Saa ya ukombozi na Mwalimu Mkuu wa Watu, ni mtu na pacha. Nani kamwangalizia mwingine? Nani kaiba kazi ya mwingine? Au hawa ni mapacha wenye mawazo yanayofanana? Hadithi zote mbili zinahusu wawekezaji wa nje, uroho wa viongozi kuwakubali wawekezaji kwa vile wanawajaza matumbo yao bila kuangalia masilahi ya taifa zima, msimamo ya wa wananchi kukataa kuuzwa na kusimama kutetea haki zao. Tofauti ni kwamba Mwalimu Mkuu wa Watu, anamwaga damu wakati Saa ya Ukombozi, ni ukombozi bila kumwaga damu.

Ingawa mimi ninayehakiki kitabu hiki nachukia kwa nguvu zote umwagaji wa damu, ninakuwa na mashaka makubwa sana kwa pendekezo la Mwandishi wa Saa ya Ukombozi. Tungekuwa na Demokrasia ya kweli, tungekuwa na sera nzuri ya siasa ya vyama vingi, pendekezo lake lingewezekana. Lakini leo hii hakuna uchaguzi unaofanyika bila kupindishwa. Fedha zinatumika kuwanunua wapiga kura, kununua shahada zao ili wasipige kura na wakati mwingine Tume ya Uchaguzi, inatangaza mshindi si kwa wingi wa kura bali kwa maelekezo ya serikali inayokuwa madarakani.

Uchaguzi wa Kenya, ni mfano mzuri. Dunia nzima ilishuhudia jinsi Kibaki, alivyolazimisha ushindi na matokeo yake yalikuwa ni kumwaga damu. Uganda, Mseveni, hakubali kuona chama kingine au mtu mwingine anaitawala Uganda. Huko nako ni lazima mwisho wake uwe kumwaga damu. Tanzania, tumeshuhudia yale ya Mbeya, Busanda, Biharamulo na kwingineko, ushindi unatangazwa jinsi Chama tawala kinavyotaka. Katika hali kama hii ni vigumu Saa ya Ukombozi ikaja kwa amani, ni lazima ije kwa kumwaga damu.

Tano, mwandishi ameshindwa kwa kiasi kikubwa kuacha matukio kujisemea. Ameshindwa kuwaacha wahusika kujisemea na kujielezea. Kama ni unyanyasaji kama ni umaskini, ni vizuri kutovielezea, bali vijielezee vyenyewe. Riwaya ni nzuri, lakini mwandishi anamwelezea msomaji yanayokuja, badala ya msomaji kugundua mwenyewe kutokana na mwenendo wa wahusika.

Mfano Faslu ya Saa ya Ukombozi na Utangulizi vinavyotokea mwanzoni mwa riwaya, havikupaswa kuwepo. Kwa kusoma sehemu hizi msomaji anapata muhutasari wa kitabu kiasi kwamba utamu unapungua. Ni kazi ya msomaji kusoma na kugundua kwamba riwaya inalenga Saa ya Ukombozi. Ni kazi ya msomaji kusoma na kugundua kwamba watu wa Mizengwe walikuwa wakipinga ufisi, ukuku, umbwa, ukondoo, usindano,ukijiko na tabia nyingine kama hizo. Ni kazi ya mwandishi kuandika katika mtindo wa kumfanya msomaji kuyaona haya mwenyewe na kuamua mwenyewe kwamba hapa ni ufisi au ukuku.

Sita, lugha iliyotumika ni sanifu, mwanzoni mwa kitabu kuna cheti kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa, cha ithibati, kuhakikisha kwamba lugha iliyotumika ni sanifu. Hata hivyo, kwa vile mwandishi alishindwa kuficha kwamba yeye ni mwanaharakati na mpambanaji wa Haki za binadamu na utetezi wa wanyonge, anatumia lugha nzito kuwatukana viongozi wanaopora rasilimali za taifa. Na kama nilivyodokeza, lugha hii inakuwa yake mwenye badala ya kuwa ya wahusika anaowachora yeye mwenyewe.

IV. HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania na wote wanaotumia lugha ya Kiswahili kukinunua kitabu hiki na kukisoma. Lakini kwa upande mwingine napenda kumshauri mwandishi, kwa maandishi yake yanayokuja, kama ni riwaya, ajaribu awezavyo kuwaacha wahusika kujisemea na yeye kama anataka kutoa ujumbe aupitishe kwenye midomo ya hao wahusika.

Riwaya inapendeza pale ambapo inajisimamia na kutoa sauti, kuliko mwandishi kutumia riwaya kama jukwaa la kuhubiri. Ni vyema msomaji akisoma aone Njema, aone Matatizo, Mafanikio na wananchi wa Mizengwe. Kusoma riwaya na kuona sura ya mwandishi badala ya wahusika inatoa utamu wa riwaya.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

MV BUKOBA

UHAKIKI WA KITABU: SITASAHAU MV BUKOBA

1. Rekodi za Kibibliografia.

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni SITASAHAU MV BUKOBA na kimeandikwa na Nyaisa Simango. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E & D Vision Publishing na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978- 9987- 521- 43- 2. Kimechapishwa mwaka 2009 kikiwa na kurasa 167. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi.

Kitabu hiki ni kumbukumbu ya kupinduka na kuzama kwa meli ya MV Bukoba katika ziwa Victoria mnamo mwaka wa 1996. Hadi leo hii kuna maswali mengi juu ya tukio hili lililochukua roho za watu zaidi ya 800. Je, ni nini hasa kilichosababisha meli ya MV Boboka kuzama? Je, ajali hiyo ingeweza kuzuilika? Watu wamekuwa na mawazo tofauti kuhusu ajali hii. Kuna watu walioamini kuwa kuzama kwa meli hii kulihusiana na uchawi. Hili lilikuwa ni tukio la kwanza katika taifa letu, meli kupinduka na kuzama. Watanzania waliamini sana usafiri wa meli; ulikuwa salama na wa bei nafuu. Lakini baada ya ajali ya MV Bukoba, imani ya watanzania kwa usafiri wa meli iliyumba sana. Kuna baadhi ambao hadi leo hii hawapendi kabisa kusafiri kwa usafiri huu wa meli.

Mwandishi wa kitabu ni mmoja wa abiria wachache walionusurika. Tukio lenyewe la kunusurika lilikuwa la ajabu. Hivyo mwandishi anajaribu kuandika yale aliyoyashuhudia na yale yaliyotangulia kabla ya ajali yenyewe. Inawezekana mwandishi asingeyakumbuka matukio haya yaliyotokea katika meli kama ajali isingetokea. Uwezekano wa kifo ulifanya akili yake kuwa makini kupita kiasi wakati akitafuta njia ya kujiokoa. Anajaribu kuelezea tangu mwanzo wa safari yake toka Dar-es-Salaam kwa treni hadi Mwanza, na kutoka Mwanza kwenda Bukoba, na safari yake ya kurudi kutoka Bukoba na meli hiyohiyo hadi ilipoishia kwa kupinduka na kuzama, kiasi cha maili kumi hivi kabla ya kufika bandarini Mwanza. Amejaribu kuelezea matatizo mbalimbali ya MV Bukoba tangu mwanzo wa safari hadi kuzama kwake, na athari za ajali hii kijamii, kiuchumi na kisiasa. Mwisho anahitimisha kwa kutoa uchambuzi wa majanga kama haya, mapendekezo na ushauri kwa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa jamii.

Kitabu hiki kinazo sura 15, Mtiririko wa matukio ya Ajali ya Mv Bukoba kama yalivyoripotiwa na vyombo vya habari na picha za kumbukumbu ya ajali hii. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. Mazingira yanayokizunguka kitabu

Ajali ya MV Bukoba, lilikuwa ni janga la kitaifa. Ajali hii ilikuwa ni kati ya changamoto alizozipata Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa; na ni kati ya mambo ambayo hayakupatiwa ufumbuzi wa haraka katika utawala wake.

Ingawa ajali hii lilikuwa ni janga la kitaifa, waliopata pigo kubwa ni kanda ya ziwa na hasa mkoa wa Kagera. Kuna familia iliyopoteza zaidi ya watu 28 katika ajali hii. Lilikuwa pigo kubwa. Watu wa Kagera, wanajulikana kama “Nshomile” (wasomi), la kushangaza ni kwamba “Nshomile” hawa hakuna aliyechukua jukumu la kuandika kumbukumbu ya ajali hii hadi mjukuu wao Nyaisa Simango, alipoamua kufanya kazi hiyo.

Sehemu zilizoiunda MV Bukoba zilitengenezwa Ubelgiji na kuja kuunganishwa mjini Mwanza, mnamo mwaka 1978, na meli hiyo kuanza kazi mnamo mwaka 1979. Kiwango cha abiria ambacho kilitarajiwa kuchukuliwa na meli hiyo kilikuwa ni 400 tu na wafanyakazi 3 na tani 200 za mizigo. Hati ya usalama ya kusafiri baharini (Certificate of Seaworthiness) ambayo meli hiyo ilikuwa nayo iliruhusu abiria 400, wafanyakazi 22 na tani 85 za mizigo. Lakini meli hiyo ilikuwa na abiria mara mbili zaidi ya hao, mbali ya shehena ya mizigo iliyokuwemo ambayo nayo ilikuwa ni zaidi ya mara mbili ya uzito ulioruhusiwa.

Hakuna Kiongozi wa ngazi ya juu aliyewajibishwa kwa ajali hii ambayo kiasi kikubwa ilionyesha uzembe wa hali ya juu. La kushangaza ni kwamba baada ya ajali hii bado kuna ajali nyingine za meli zilifuata kwa uzembe ule ule unaofanana na wa MV Bukoba. Ajali za basi zinaendelea kuyamaliza maisha ya watanzania. Juzi tu ajali tatu zilitokea Nzega, na watu wengi wamepoteza maisha. Hakuna anayewajibishwa. Jitihada za kupunguza ajali zinakwenda kwa mwendo wa kinyonga.

Prof. Haroub Othman, aliyeandika neno la utangulizi katika kitabu cha Sitasahau MV Bukoba, anasema kwamba “Kila kifo kina siku yake”, na kweli Kila kifo kina siku yake! Pamoja na maneno mazuri ya kukitambulisha kwetu kitabu hiki, amekufa kabla kitabu hakijazinduliwa. Mungu, ailaze roho yake mahali pema peponi.

Prof. Haroub Othman, anasema: “ Cha kujiuliza ni; je,
ingekuwa MV Bukoba imefanyiwa matengenezo kwa zile
kasoro zilizojitokeza tangu wakati inaanza kazi…;
Ingekuwa uongozi wa TRC umetekeleza jukumu lake la
uangalizi na usimamizi wa shughuli zote za shirika kwa
uangalifu sana….; Ingekuwa wahusika bandarini Bukoba
na Kemondo Bay walihakikisha kuwa waliopanda melini ni
abiria wanaotakiwa tu na si zaidi, na uzito wa mizigo ni ule
unaoruhusiwa…; Ingekuwa….. Ingekuwa… Lakini
haikuwa hivyo, na ajali ikatokea kwa sababu ya uzembe wa
jinai uliofanywa na binadamu mwenyewe. Sasa cha
kujiuliza tena ni: je, ufanye nini? Cha kufanya sasa ni
kutorejea makosa kama haya, sio tu katika usafiri wa
baharini, angani barabarani na kwenye treni, lakini pia
katika kujenga majumba yetu, shule, hospitali na hata
magereza yetu" (Uk 8).

Nyaisanga G.Simango alizaliwa Wilaya ya Kinondoni,
Dar-es-Salaam. Alisoma Elimu ya Msingi na Sekondari, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kuanzia mwaka 1981 hadi 1991. Alipata Stashahada ya juu ya Ubaharia katika chuo cha Uongozi wa Maendeleo, Mzumbe. Aidha, mwaka 2004 alihitimu shahada ya Uzamili katika Uongozi wa Biashara, mchepuo wa Fedha na Benki Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro. Kwa sasa, Nyaisa Simango ameajiriwa kama Afisa Ugavi, Benki Kuu ya Tanzania. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. Muhtasari wa Kitabu

Sura ya kwanza, mwandishi anaelezea Meli ya MV Bukoba; wasifu wa meli hiyo na idadi ya watu na mizigo ambayo iliruhusiwa kubeba, ila siku ya ajali ilibeba mara mbili ya uzito uliokuwa ukiruhusiwa.

Sura ya pili ni maandalizi ya Safari ya Mwandishi, kutoka Dar, kuelekea Mwanza. Sura ya tatu ni safari yake kuelekea Mwanza. Sura ya nne ni maelezo juu ya mji wa Mwanza na maandalizi ya safari ya kuelekea Bukoba kwa usafiri wa Mv. Bukoba.

Sura ya tano ni safari ya Mwandishi kuelekea Bukoba, akimsindikiza mfungwa wake aliyetokanaye Dar. Sura ya sita ni maelezo juu ya Bukoba. Sura ya saba ni maelezo juu ya safari ya kurudi kutoka Bukoba kuelekea Mwanza na Mv Bukoba, safari iliyoishia majini! Anaelezea watu walivyokuwa wamejaa, starehe za melini na mengine mengi.

Sura ya nane inaelezea dalili za hali ya hatari kuanza kujitokeza melini. Sura ya tisa ni kupinduka kwa MV Bukoba na yote yaliyofuatia; maji kujaa melini, watu kufa watu kutapatapa huku na kule kutafuta msaada.

Sura ya kumi na kumi na moja zinaelezea jinsi wale waliookoka walivyo panda juu ya mgongo wa MV Bukoba na jinsi walivyoanza kuwa na matumaini ya kuokolewa.

Sura ya kumi na mbili ni maelezo ya kuokolewa na kupelekwa hospitali ya rufaa Bugando. Sura ya kumi na tatu ni maelezo kuhusu kutoka hospitali ya Bugando. Sura ya kumi na nne na kumi na tano na maelezo ya mwandishi kwenda nyumbani kwao Musoma.

Baada ya sura ya kumi na tano inafuata mtiririko wa matukio ya ajali ya MV. Bukoba kama yalivyoripotiwa na vyombo vya habari na mwishoni kabisa ni hitimisho.

V. TATHMINI YA KITABU

Baada ya kuona muhtasari wa kitabu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Nyaisa Simango.

Ingawa kitabu hiki kimeandikwa zaidi ya miaka kumi baada ya ajali ya MV Bukoba, ni ukweli usiopingika kwamba kazi iliyofanyika ni nzuri sana. Ni lazima tumpongeze mwandishi kwa kazi yake hii ambayo itakuwa na manufaa hata kwa vizazi vijavyo. Mwandishi ametuonyesha umuhimu wa kuandika kumbukumbu ya matukio mbali mbali katika taifa letu. Kama alivyosema Marehemu Prof. Haroub Othman, katika neno la Utangulizi: “ Nyaisa anafaa kushukuriwa kwa kazi hii nzuri na adhimu. Kunusurika kwake kutokana na kifo ndiko kumetuwezesha leo kujua nini kilitokea. Ikiwa wengine waliokuwemo katika meli ile ya MV Bukoba na kubahatika kuwa hai leo hawataelezea kimaandishi au kwa kuhadithia wengine ili yaandikwe, basi polepole janga hili la kitaifa litapotea katika kumbukumbu zetu” (Uk 9).

Hiki ni kitabu cha kwanza kuandikwa juu ya ajali ya MV Bukoba. Hivyo ni vigumu kufanya tathimini juu ya matukio yote yanayoelezwa na Nyaisa. Tunaweza kuwa na mashaka kwamba mwandishi aliwezaje kukumbuka yote hayo katika hali ya kupigania maisha yake. Wakitokea watu wengine baada ya kusoma aliyoyaandika Nyaisa, wakaongezea, wakakosoa na kuboresha zaidi, tunaweza kuwa na kumbukumbu nzuri ya ajali hii ambayo ilichukua roho za watu wengi.

Au labda kama Nyaisa, angefanya juhudi za kutafuta watu waliopona, na kujadiliana nao na kumbushana matukio mbalimbali ndani na nje ya meli, kitabu kingekuwa na sura tofauti. Bukoba, kuna watu wengi waliopona kwenye ajali hii; tungeweza kupata ushuhuda wao pia lingekuwa ni jambo jema na la kudumisha kumbukumbu na historia ya taifa letu.

Katika utangulizi Nyaisa, anasema hivi: “ Nimeelezea kwa ufupi tu baadhi ya matukio niliyoyaona na kushiriki ndani na nje ya MV Bukoba wakati wa safari. Inawezekana nisingeyakumbuka matukio haya yaliyotokea katika meli kama ajali isingetokea, kwani uwezekano wa kifo ulifanya akili yangu kuwa makini kupita kiasi wakati nikitafuta njia za kujiokoa”

Pia Marehemu Prof. Haroub Othman, alisisitiza jambo hili kwenye neno lake la utangulizi: “ Nyaisa hakuwahi kuwa mwandishi, na sidhani kwamba kabla ya ajali hii hata aliwaza kuwa angekuwa mwandishi siku moja. Changamoto, au tishio lolote la nafsi (mtu, jamii, taifa) ni mama wa ubunifu na ujasiri pia. Katika maelezo haya, Nyaisa ametuelezea kwa ufasaha mambo aliyoyaona na kuyapitia katika ajali ile”.

VI. HITIMISHO

Kwa kuhitimisha, ningependa kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki cha Nyaisa. Pia ni muhimu kwa wale waliopona kwenye ajali hii kukisoma kitabu hiki na kutoa maoni yao.

Mipango ikienda kama ilivyopangwa, kitabu hiki kitazinduliwa hivi karibuni Jijini Dar-es-Salaam na kule Mwanza. Mpango ni kukizindua kitabu hiki tarehe 21.5.2010, kule Mwanza, siku ambayo ni kumbukumbu ya kuzama kwa MV Bukoba. Litakuwa ni jambo zuri kama watu watakusanyika kwa wingi kushuhudia uzinduzi wa kitabu hiki ambacho kinatuletea kumbukumbu ya ajali ya MV. Bukoba.

Shukrani za pekee ziwaendee E&D Vision Publishing, kwa kuona umuhimu wa kukichapa kitabu hiki na kwa kufanya jitihada za pekee kutafuta nyongeza za ziada ambazo ni muhimu sana katika kutunza kumbukumbu ya ajali hii mbaya.

Kila Kifo Kina Siku yake. Prof. Haroub Othman, aliandika neno la utangulizi la kitabu hiki lakini kwa vile kila kifo kina siku yake, ametangulia mbele ya hukumu kabla ya uzinduzi wa kitabu hiki. Baadhi ya wale waliopona kifo kwenye Ajali ya MV Bukoba, ni marehemu, maana Kila kifo kina siku yake!

WACHUNGAJI WANAWAKE-BUKOBA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2006.

HATIMAYE NA BUKOBA WAMEBARIKI WANAWAKE WACHUNGAJI.

Mwaka 1992, Kanisa La Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) liliamua kuwabariki wanawake wachungaji. Uamuzi huu ulipokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya waumini wa kanisa hili. Utekelezaji wake ulikuwa mgumu kwa baadhi ya diosisi za kanisa hili. Baadhi ya diosisi zilitekeleza uamuzi huu kwa haraka na nyingine zilisita. Msimamo mkali wa kukataa kuwabariki wanawake ulikuwa Kanda ya ziwa, na hasa mkoa wa Kagera. Diosisi za Karagwe na Kagera zilikataa kabisa kukubaliana na uamuzi wa kuwabariki wanawake.

Sababu kubwa zikiwa ni zile zile tulizozizoea kwamba Yesu Kristu hakuwachagua mitume wanawake. Lakini zilikuwepo na sababu nyingine kwa mfano kwamba mwanamke akiwa mja mzito atawezaje kusimama mbele za waumini! Au kwamba mwanamke akiwa kwenye siku zake atawezaje kuendesha ibada. Au kwamba mwanamke akiwa mchungaji ataolewa na nani? Sababu nyingine ni kwamba mchungaji ni kama baba wa familia ya waumini, hivyo mwanamke akiwa mchungaji, ataitwa Baba? Watu wamezoea kusikia Baba Paroko, baba mchungaji – sasa mchungaji mwanamke ataitwa Mama Paroko au mama Mchungaji. Wengine ukisema mama mchungaji, wanaelewa ni mke wa mchungaji. Kuna ambao waliuangalia uchungaji kama kazi ya wanaume.

Mwaka juzi, Askofu Dk. Benson Bagonza, wa diosisi ya Karagwe, aliamua kuuvunja mwiko na kukubali kuwabariki wachungaji wanawake. Hata hivyo haukuwa uamuzi wake, jambo hili liliamuliwa na Diosisi ya Karagwe, kwa kuitikia uamuzi wa KKKT uliofanyika mwaka 1992 kule Morogoro, hata hivyo uamuzi huo ulibaki bila kutekelezwa kwa zaidi ya miaka kumi. Maaskofu wawili waliomtangulia Askofu Bagonza, waliogopa kutekeleza uamuzi huo. Kila mmoja wao hakukubali kuhukumiwa na historia kwa kuwabariki wachungaji wanawake. Askofu Dk.Bagonza, hakuogopa kuhukumiwa na historia.

Askofu Bagonza, alipoamua kutekeleza uamuzi huo, alifanya hivyo kwa kulipatia tukio hilo umuhimu na uzito wa pekee. Aliwabariki wachungaji wawili wanawake bila kuchanganya wachungaji wengine wanaume. Hivyo siku hiyo ilionekana kuwa ya pekee na kubeba ujumbe mzito kwa watu wote wa Karagwe, Kagera, Tanzania, Afrika na dunia nzima. Watu wote waliotoka pande zote za dunia, walikuja wakijua kwamba siku hiyo ilikuwa ni kuwabariki wachungaji wanawake. Walijua ni tukio jipya na la aina yake katika diosisi ya Karagwe. Madhehebu na dini mbalimbali zilialikwa kushuhudia tukio hila la kihistoria.

Tarehe 8.1.2006, Diosisi ya Bukoba, wamefuata nyayo za Askofu Bagonza, na kukubali kuwabariki wachungaji wawili wanawake; Alice Kabigumila na Faith Lugazia Kataraiya. Mbali na kufuata uamuzi wa KKKT uliofanyika 1992, Diosisi ya Bukoba (Kaskazini Magharibi) walifanya uamuzi kwa sauti moja miaka miwili iliyopita kuwabariki wanawake, lakini ikachukua muda kutekeleza. Miaka miwili si haba. Wanawake waliobarikiwa tarehe 8.1.2006,walimaliza masomo yao ya theolojia miaka mingi wakasubiri wanaume kukubali kuwabariki. Mchungaji Alice Kabigumila, ni mwanamke wa kwanza mteolojia Afrika nzima. Alisoma theolojia na kupata phd, lakini alikaa miaka mingi akisubiri kubarikiwa. Tofauti na Karagwe, Bukoba, walijitahidi kupunguza makali ya siku yenyewe. Walibarikiwa wachungaji sita, wanne wanaume na wawili wanawake. Kwa kufanya hivyo walitaka kuonyesha kwamba hili lilikuwa tendo la kawaida la kuwabariki wachungaji. Ingawa ukweli wenyewe ni kwamba hilo halikuwa tendo la kawaida. Na kama wangependa kuwa wa kweli, basi wangefanya kama walivyofanya Karagwe, kwa kuwabariki wanawake peke yao. Na wala hii isingekuwa ubaguzi wa kijinsia, lakini ingeonyesha uzito na ukweli wa mambo kwamba hatua ya kuwabariki wanawake ilifikiwa kwa njia ndefu, kwa kusita, kutafakari na kwa manung’uniko ya moyoni.

Ingawa wakati wa mahubiri Askofu Elisa Bubelwa, Askofu wa Diosisi ya Bukoba , alielezea njia hiyo ndefu, kwamba kufikia uamuzi huo walitembea safari ndefu na mara kwa mara walikaa chini ya kivuli na kupumzika na kutafakari, wakati mwingine walisimama kwenye mto na kunywa maji, waliowashauri vibaya, waliwakatalia maana Bukoba, wana uzoefu wa imani ya Kikristu zaidi ya miaka miamoja! Walitembea pole pole lakini kwa uhakika na hatimaye tarehe 8.1.2006, walihitimisha safari yao na kuwabariki wachungaji wanawake.

Safari hiyo haikuonyeshwa kimatendo wakati wa siku yenyewe. Siku ilifunikwa kwa namna Fulani. Ingawa wanawake walijitahidi kufurukuta wakati wa kusoma risala na kutoa zawadi. Walionyesha jambo hili kwa kuwapatia zawadi wachungaji wanawake na kuwaacha solemba wachungaji wanaume. Mchungaji Alice Kabigumila alipata zawadi ya pikipiki aina ya Yamaha, kutokana na michango ya akina mama wa Diosisi ya Bukoba. Mchungaji Faith Lugazia Kataraiya, kwa vile bado anasomea shahada ya uzamifu kule Marekani, alipata zawadi ya computer ya mkononi (Portable Computer). Tendo hili la akina mama ndio lilionyesha kidogo kwamba kulikuwa na kitu kisichokuwa cha kawaida katika Ibada ya kuwabariki wachungaji tarehe 8.1.2006 kwenye kanisa kuu(Kengele tatu) mjini Bukoba.

Bahati nzuri Mchungaji Alice Kabigumila na Faith Lugazia Kataraiya, wameolewa. Wanaume wao Bwana Kabigumila na Bwana Joeivan Kataraiya, walikuwa wamewasindikiza kwenye Ibada ya kuwabariki. Hivyo swali la nani atawaoa wachungaji wanawake halikujitokeza Bukoba, kama lilivyojitokeza kule Karagwe. Hadi leo hii bado ni swali kubwa kule Karagwe, kuhusu ni nani atawaoa wachungaji wanawake. Ni kweli kwamba wanachapakazi bila kuwa na tofauti na wachungaji wanaume, lakini bado kuna tatizo la wachungaji hawa kupata wanaume. Tatizo jingine ni lile la kuwapanga kwenye sharika wachungaji wanawake na wanaume. Mfano wanapojikuta mchungaji mwanamke na mchungaji mwanaume wamepangwa kwenye usharika mmoja. Kama mchungaji mwanamke ameolewa na mchungani mwanaume ameoa na anaisha na familia yake, tatizo linakuwa si kubwa, ni sawa na yale yaliyo katika jamii ya uhusiano wa familia na familia. Lakini kama mchungaji mwanamke hakuolewa kama hawa wa Karagwe, akajikuta kwenye usharika na mchungaji aliyeoa ,lakini hakai na familia yake kwenye usharika. Wakajikuta mchungaji mwanamke na mchungaji huyo aliyeiacha familia nyumbani na kuishi kwenye usharika, tatizo linakuwa kubwa kidogo. Wachungaji wanaume wa Karagwe, wameanza kulitafakari hili kwa kina. Linahitaji ufumbuzi wa hekima na busara.

Kwakukataa kuwabariki wachungaji wanawake, KKKT, Bukoba, ilikuwa karibu sana na Jimbo Katoliki la Bukoba. Msimamo wao ulijenga uhusiano wa karibu sana na Kanisa Katoliki, maana kanisa hili linapinga kitendo hicho. Sasa kwa vile KKKT, Bukoba, imekubali kuwabariki wanawake, itakuwa imeweka ukuta mkubwa kati ya uhusiano wao. Na hili lilionyeshwa na kutokuwepo mjumbe yeyote kutoka kwenye kanisa hili kwenye sherehe za kuwabariki wachungaji wanawake. Makanisa haya mawili yana utamaduni wa kukaribishana kwenye sherehe mbali mbali. Wakatoliki, walioamua kuwepo kwenye sherehe hizo za kuwabariki wanawake walifanya hivyo kwa uamuzi wao, wakijulikana ni lazima wawe matatani.

Ingawa kulijitokeza tofauti ndogo kati ya kuwabariki wachungaji wanawake wa Karagwe na Bukoba. Kitendo cha kuwabariki ni kile kile, ni ukweli kwamba sasa mkoa wa Kagera una wachungaji wanawake. Ni ukweli kwamba sehemu nyingi za Tanzania, zina wachungaji wanawake. Ni ukweli kwamba wanawake wanaweza. Ni ukweli kwamba wanawake wanaweza kuwa wachungaji, basi wanaweza kuwa mapadri! Na hatimaye maaskofu! Ni fundisho kwa kanisa katoliki. Ni bora viongozi wa Kanisa Katoliki, kuharakisha hatua ya kuwaparisha wanawake, vinginevyo waumini wenyewe wataanza kudai jambo hili. Sasa hivi waumini wana mifano ya kutoa, wameanza kuona jinsi wanawake wanavyoweza kuwa wachungaji. Sasa hivi waumini wa kanisa katoliki wameanza kuona jinsi sababu zilizokuwa zikitolewa si za msingi. Kwamba Yesu, hakuwachagua mitume wanawake si kigezo cha kuwafanya wanawake wasiwe wachungaji. Hata hivyo ukweli kwamba Yesu Kristu, alizaliwa na mwanamke Mama Maria, ukweli kwamba Yesu Kristu, aliambatana na baadhi ya wanawake wakati wa mahubiri yake, ukweli kwamba mtu aliyekuwa karibu na Yesu Kristu ni Mwanamke Maria Magdalena, inatosha kuonyesha kwamba Yesu, hakuwatupa kando wanawake. Hivyo kuwabariki kuwa wachungaji au kuwaparisha si jambo la kumkana au kumsaliti Kristu.

Makala hii imeandikwa kwa lengo la kuwapongeza waumini na viongozi wa kanisa la kiinjili la Kilutheri la Bukoba, kukubali kuwabariki wanawake wachungaji. Na kubwa zaidi kuwapongeza wachungaji wanawake Alice Kabigumila na Faith Lugazia Kataraiya, kwa uvumilivu waliouonyesha katika harakati za kuomba kubarikiwa. Moyo wao wa kutokukata tama, ni ishara na ukomavu mkubwa wa imani. Ukomavu huu waliouonyesha ni chachu kubwa katika utumishi wao. Mungu awalinde na kuwapatia nguvu ili wawe nuru ya kuonyesha kwamba wanawake wanaweza.

Na
Padri Privatus Karugendo.

2005 KUELEKEA 2006

MAKALA HII ILICHAPWA NA GAZETI LA RAI 2005

2005 KUELEKEA 2006.

Tunaelekea kuumaliza mwaka wa 2005, na kuuanza mwaka wa 2006. Wale wote watakaofanikiwa kuingia mwaka wa 2006 wanawajibika kumshukuru Mwenyezi Mungu. Si kwa ubora wao wameendelea kuishi, si kwa wema wao wameendelea kuishi na wala si kwa umuhimu wao wameendelea kuishi. Tulikuwa na watu bora wenye wema wa kupindukia na muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu, lakini hatunao tena! Hawakubarikiwa kuiona 2006! Kuendelea kuwepo, kuendelea kuishi ni neema na huruma ya Mwenyezi Mungu. Hivyo kwa wale waliobahatiwa kuendelea kuishi ni lazima kumshukuru Mwenyezi Mungu. Uhai ni zawadi. Tunazawadiwa bila ya kustahili! Zawadi hii inaweza kuondoka saa yoyote bila taarifa na bila ya majadiliano. Anayeitoa ndiye anayeitwaa. Kwanini anatwaa ya huyu na kuacha ya yule, hiyo ni kazi yake! Anayebahatiwa kuendelea kuishi, kazi yake kubwa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, wale wote waliopata bahati ya kuendelea kuishi wana changamoto mbele yao. Je, ni kwa nini Mungu, amewaruhusu kuendelea kuishi? Wanaishi ili wafanye nini? Wanaishi ili wale na kunywa? Wanaishi ili wayashughulikie maisha yao tu au wayashughulikie maisha ya watu wengine? Wanaishi ili wacheze ngoma, muziki na kuimba nyimbo? Wanaishi ili walete amani na utulivu au walete vurugu na kuuweka uhai hatarini? Kwanini waendelee kuwepo? Je, Mungu, anataka nini kutoka kwao? Uhai tunazawadiwa, hakuna anayeuomba ! Lakini baada ya kuzawadiwa kila mwenye uhai ana wajibu wa kuulinda . Uhai ukishapotea haurudi tena! Hivyo ni wajibu wa kila mwenye uhai, kila aliyebahatika kuumaliza mwaka 2005 na kuingia mwaka wa 2006 kuulinda uhai wake, uhai wa wengine na uhai wa viumbe vingine vyote vinavyomzunguka. Ni wajibu wa kila mwenye uhai kuulinda uhai wa mazingira yetu ili na mazingira yetu yachangie kuulinda uhai wetu!

Mwanateolojia wa theolojia ya ukombozi Boff, ameanza kuhubiri theolojia mpya kabisa. Theolojia ya mazingira. Ana wito kwa viongozi wa dini kuanza kuyaangalia mazingira yetu kwa jicho la kiimani. Mazingira yanalinda uhai wa binadamu, hivyo binadamu huyu ambaye ni mcha Mungu, ambaye anaamini kwamba maisha yake yanaongozwa na Mwenyezi Mungu, ni lazima ayatunze mazingira kwa misingi ya kiimani. Kwa maneno mengine ni kamba kutunza mazingira ni wajibu wa kiimani na hakuna mtu wa kukwepa wajibu huu. Anasisitiza kwamba huu sasa ndio msingi wa mahubiri yanayoendana na wakati.

Kwa bahati mbaya Tanzania, bado ina mambo mengi yanayotishia uhai wa wananchi. Nchi nyingine na hasa nchi za mataifa yaliyoendelea, zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyapunguza mambo yanayotishia uhai. Na hii imefanikiwa kwa sababu nchi hizi zimekazania utawala bora, demokrasia na kuziheshimu haki za binadamu. Hapa Tanzania, akinamama wajawazito bado wanapoteza uhai wakati wa kujifungua. Hili ni jambo la kusikitisha maana uhai huu wa akinamama unapotea pasipokuwa na sababu yoyote ile. Katika ulimwengu wa leo, ulimwengu wa utandawazi, wakati mwanadamu ameendelea kiasi cha kwenda mwezini na kutalii kwenye anga za mbali, mjamzito kupoteza maisha ni dhambi ya Ulimwengu mzima. Pamoja na maendeleo yaliyofikiwa na dunia ya kwanza, kuendelea kutuacha nyuma kiasi hicho ni dosari kubwa na ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu, maana yote waliyonayo wanapewa bure na Mwenyezi Mungu, bila yao kuwa bora kuliko wanadamu wengine na bila ya kustahili! Hata hivyo hii haiondoi lawama kwa serikali isiyowajibika na kuuthamini uhai wa watu wake. Serikali ikiboresha huduma za afya, ikaboresha huduma kwenye hospitali za serikali na zahanati za vijijini, ikaboresha barabara za vijijini na kuhakikisha zahanati zina usafiri wa kuaminika vifo hivi vya wajawazito vitakoma! Hivyo katika jitihada za kila Mtanzania kuulinda uhai ni pamoja na umakini wa kila Mtanzania kuishi kwa kutafakari juu ya mambo mbali mbali yanayojitokeza katika jamii yetu.

Magonjwa kama Malaria na UKIMWI yanatishia uhai wa watanzania. Wale waliopata bahati ya kuuanza mwaka wa 2006, wana mashaka makubwa ya kuuona mwaka wa 2007, maana Malaria na UKIMWI, ni tishio kubwa. Pamoja na jitihada za serikali inayowajibika, magonjwa haya yanamtaka kila mtu kuwajibika. Ni lazima watu kujenga tabia ya kutumia chandarua na kuwapeleka haraka watoto hospitali wanapoonyesha dalili za malaria. Watoto wengi wa Tanzania wamepoteza uhai kutokana na uzembe wa wazazi wao. Ni wazi kuna familia ambazo haziwezi kumudu kununua chandarua na kulipia matibabu ya watoto. Kwa vile kuulinda uhai ni mradi wa pamoja, basi viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa dini wasaidie kuwatambua watu hawa ili wasaidiwe. Kama kauli mbiu ya kampeni dhidi ya malaria inavyosema kwenye vyombo vya habari: Malaria haikubaliki! Iwe mwiko kwa Mtanzania yeyote kupoteza uhai wake kwa ugonjwa huu wa malaria!

UKIMWI ni hatari zaidi. Hadi leo hii ni ugonjwa usiokuwa na tiba. Mbaya zaidi ni ugonjwa ambao ni vigumu kwa kutazama tu kujua ni wangapi wameambukizwa. Maisha yanaendelea kama kawaida! Ni nani anaweza kusema ana mke mmoja? Ni nani anaweza kusema hatembei nje ya ndoa yake? Ni nani anaweza kusema ana mpenzi mmoja? Hili linabaki kwa mtu binafsi, hii ni siri inayobebwa kwenye moyo wa kila mwanadamu. Mwanadamu si kisiwa, daima anaishi miongoni mwa watu, na kila kukicha ni lazima kujitokeze mahusiano mapya – swali ni je ni upi mpaka wa mahusiano? Ni rahisi kujibu na daima tunajibu haraka bila ya kuwa wa kweli. Mtu asipokamatwa anajifanya kuishi kana kwamba ukweli wa siri iliyo moyoni mwake haupo! Tunajidanganya hivyo hadi pale tunapoumbuliwa na ugonjwa. Aliye salama leo ni mashaka makubwa kama kesho atakuwa salama! Watu walio wengi hawajakubaliana na ushauri wa kupima. Kwa vile kulinda uhai ni mradi wa pamoja, hatuna budi kushirikiana kwa pamoja kupambana na ugonjwa huu wa hatari. Kwa vile wale ambao bado tunaishi tunalindwa na Mwenyezi Mungu, pasipokustahili, hakuna haja ya kushutumiana wala kulaumiana. Hakuna haja ya kunyosheana kidole cha uzinzi. Maana neno hili ni pana kidogo na hakuna shujaa. Mtu aliye timamu, lolote linaweza kutokea kama mwizi wa usiku!:
“ Mmesikia ya kuwa watu waliambiwa: ‘Usizini!’ Lakini mimi na wambiieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.” (Matayo 5:27-28).

Kwa mantiki hii ni nani wa kuukwepa Uzinzi! Labda yule anayeishi juu mbinguni. Lakini anayeishi kwenye dunia hii, jambo hili ni gumu sana. Wanafiki wanaweza kujigamba mbele ya binadamu lakini si mbele ya Mwenyezi Mungu. Mungu, anaona yote na kupenyeza kwenye unafiki wetu! Jambo la msingi ni kushirikiana kupambana na adui. Kwa pamoja tuhimizane kupima afya zetu, tuhimizane kuwa waaminifu na tuhimizane kujikinga. Tuzingatie ukweli kwamba sote ni wadhaifu mbele ya uhusiano kati ya mtu na mtu; iwe ni chuki, kusengenya, kupendelea, mapenzi, kulaumiana kusingizia, kuvutia upande mmoja nk., hakuna mwenye kipimo cha kujivuna na kujigamba. Sote tunalindwa na huruma ya Mwenyezi Mungu. Mungu yule yule anayeturuhusu kuendelea kuishi ndiye anayetupatia akili za kutengeneza kinga. Ni wajibu wetu kushirikiana na muumba wetu.

UKIMWI, unatishia uhai wa familia zetu. Ndoa nyingi zimesambaratika, watoto yatima wamezagaa kila sehemu kuanzia mitaani hadi machimboni. Wakati tunatafuta tufanye nini ni bora kuwasikiliza waathirika wa ugonjwa huu. Tuwasikilize pia na watu wanaoyaishi maisha ya ndoa, wanaoguswa na tatizo zima la ukosefu wa uaminifu, tatizo la kumpoteza mwenza wa maisha, tatizo la kutengwa na jamii. Mtu hata akisoma kufika mwezini, kama hana uzoefu wa kitu ni vigumu kukisemea. Mtu asiyecheza mchezo ni vigumu kutunga sheria za mchezo! Mtu anaweza kusoma juu ya ndoa na maisha ya ndoa, akawa mtaalam wa kuzishauri ndoa, bila yeye kuishi maisha ya ndoa ushauri wake utakuwa na walakini. Ndio maana wataalam wa aina hii wanauona UKIMWI, kama kilema na kwamba wale wenye ugonjwa huu waachane na ngono!

UKIMWI ni tishio la uhai kiasi kwamba tusipokubali kushirikiana na kuacha unafiki, huruma ya mwenyezi Mungu, itatutupa mkono na kufikia 2110, uhai wa watanzania wengi utakuwa mashakani. Kizazi kitafutika! Utakuwa ni uzembe wa kizazi chetu hiki na historia itatuhukumu! Uzembe wa kizazi hiki unaionyesha pia katika mambo mengi mengine. Kizazi chetu kimeshindwa kufanya maandalizi mazuri ya vizazi vijavyo. Tunapenda kuangalia ya leo tu. Tunaangalia amani na utulivu wa leo, lakini tunashindwa kuandaa amani na utulivu kwa vizazi vinavyokuja. Ufa mkubwa unaojitokeza kati ya masikini na matajiri hapa Tanzania, si ishara nzuri ya amani na utulivu kwa vizazi vijavyo. Kwa njia hii hatuwezi kukwepa hukumu ya historia. Na kweli tunakuwa tunafisha uhalali wetu wa kuishi leo hii!

Njaa nayo ni tishio la uhai. Mvua isiponyesha ya kutosha. Baadhi ya maeneo ya Tanzania, yanakumbwa na uhaba wa chakula na miaka mingine inakuwa mbaya kiasi cha watu kufa. Ni aibu jambo hili kutokea kwenye nchi yenye maziwa na mito na ardhi ya kutosha. Wakati mwingine ni uzembe na kutowajibika. Kuna mikoa inakuwa na chakula kingi wakati mikoa mingine watu wanakufa kwa njaa. Tatizo kubwa likiwa usafiri wa kusafirisha chakula hicho kutoka mkoa hadi mwingine. Barabara zilikuwa mbaya! Sasa hivi barabara zinatengenezwa.

Umaskini na ujinga vinatishia pia uhai wa watanzania walio wengi. Pamoja na jitihada za serikali inayowajibika, kuondoa umaskini na ujinga ni mradi wa pamoja pia! Ni lazima kila Mtanzania kushiriki katika jitihada za kuutokomeza umaskini na ujinga. Hatuwezi kuutokomeza umaskini bila kufanya kazi kwa bidii. Watanzania tuna utamaduni wa uzembe. Kazi iliyofanyika wakati wa Mjerumani, aliyewalazimisha Watanganyika kufanya kazi kwa viboko, haikufanyika wakati wa utawala wa Mwingereza, wakati wa uhuru hadi leo hii. Mjerumani aliondoka na viboko vyake na juhudi ya kazi ikayoyoma. Kiboko cha Mjerumani kitarudi kwa namna nyingine katika ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki, tutakapomezwa na kunyimwa ajira kwa sababu ya uzembe wetu ndipo tutakapozindukana na kuanza kufanya kazi kwa bidii zote!

Je, Mungu, ametuacha hai ili tushuhudie awamu ya nne ya uongozi wa taifa letu? Tuushuhudie uchaguzi mkuu wa 2005? Tushiriki kuiandika historia hai ya taifa letu na kushuhudia demokrasia ikikua na kukomaa?

Hata hivyo ukweli unabaki pale pale kwamba mwanadamu ni yule yule, mwenye tamaa, uchu wa madaraka, kujipenda, chuki, kulipiza kisasi nk. Na ukweli mwingine ni kwamba pamoja na ukorofi wa mwanadamu, Mungu, hachoki kumvumilia. Huruma ya Mungu, ndiyo inatufanya tuendee kuishi. Kwa vile bado Mungu bado ametusimamia, tushirikiane naye kuulinda uhai wetu na uhai wa taifa letu. Heri ya mwaka mpya!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

MTWARA, KOROSHO NA OMBA OMBA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.

MTWARA, KOROSHO NA OMBA OMBA

Ninaandika makala hii nikiwa Mtwara. Mji wa Mtwara ni wa kihistoria, ni kati ya miji ya zamani iliyoshuhudia historia ya biashara ya watumwa na maendeleo ya kujenga nyumba imara ambazo nyingine sasa hivi ni magofu. Ukiondoa barabara ya lami inayoingia mji huu kutokea Dar, na ile inayokatisha Bima, Sokoni na kurudi tena kwenye makutano ya Uwanja wa mashujaa, hakuna barabara nyingine ya lami katika mji huu. Barabara nyingine kama za kwenda Shangani, Ligula na maeneo mengine ya mji zimetengenezwa na magari yanayopita mara kwa mara. Leo jioni nilitembelea Bandari ya Mtwara yenye kina kirefu kuliko cha Dar na Tanga. Ni bandari kubwa yenye shughuli kidogo kulinganisha na ukubwa wake. Inakuwa na shughuli nyingi kidogo wakati wa msimu wa korosho. Vinginevyo ni bandari iliyolala usingizi! Si lazima nikumbushe kwamba bandari zimechangia sana katika maendeleo ya nchi nyingi duniani.

Meli kubwa ambazo haziwezi kutia nanga kwenye Bandari za Dar na Tanga zinatia nanga kwenye Bandari ya Mtwara. Zilizo nyingi zinakuja kusomba korosho. Zinasomba utajiri mkubwa wa Mkoa wa Mtwara na kuacha nyuma umaskini na ufukara unaonuka. Hata kama mtu hakusoma uchumi, vipo vipimo vya kupima maendeleo ya neema ya watu: Nyumba imara na bora, mavazi wanayovaa watu, afya, barabara nzuri na imara, huduma ya maji nk.

Sikuwa na nia ya kuzungumzia bandari ya Mtwara, hapana, nimeigusia tu kwa vile nimeitembelea leo. Nimeambiwa kwamba na uwanja wa ndege wa Mtwara, miaka ya nyuma ndio ulikuwa uwanja wa pili kwa ukubwa hapa Tanzania. Uwanja uliochangia kiasi kikubwa mapambano ya kusini mwa Afrika. Leo hii uwanja huu uko vipi? Hili nalo si nia yangu kuliongelea kwa leo, labda kesho ama keshokutwa!

Mjini Mtwara, kuna sehemu ijulikanayo kama Bima. Sikuuliza ni kwa nini panaitwa Bima. Lakini ukweli ni kwamba ukifika Bima, umefika Mtwara! Hiki ni kijiwe cha kila kitu, kuanzia siasa, ushabiki wa mpira, dadalada zote na mabasi ni lazima yapite Bima, kuna nyama choma na vinywaji vya kila aina. Unataka usitake baada ya kazi na joto la Mtwara, ni lazima utapumzika kidogo Bima kula au kunywa chochote. Sehemu hii na watu wa kila aina, matapeli, waandishi wa habari, wanasiasa, wahubiri, wafanyabiashara. Ni sehemu ambayo utasikia majina ya kila aina kuanzia Osama hadi Tarimo. Na ukisikia mtu anaitwa Tarimo, Mosha, Marandu au Macha, usifikirie ni Mchaga wa kutoka Moshi. Usishangae ukimkuta Mmakonde, anaitwa Marandu! Unaweza usiwaelewe watu hawa, lakini nilijitahidi kuwaelewa. Kama mimi ninaitwa Privatus, jina la Kiuulaya, kwa nini Mmakonde asiitwe Marandu, jina la kichaga?

Siku moja nilikaa pale Bima. Niliagiza kinywaji na kwa vile nilikuwa Mtwara, nilitamani kula Korosho. Mawazo yangu, nilifikri kwa vile Korosho, inalimwa Mtwara, basi bei yake itakuwa ya chini. Kumbe bei yake ya juu kuliko hata ile ya Dar-es-Salaam! Niliagiza Korosho za Elfu mbili. Kilo moja ni shilingi Elfu tano! Nilipoanza kula, watu wawili walikuja na kukaa karibu na mimi. Niliwakaribisha na kuwaagizia soda mbili. Hapo ndio maajabu ya Mtwara, yakaanza. Ile shukrani yao haikuwa ya kawaida. Walinishukuru hadi nikaguswa. Ni kawa na maswali mengi, kwa nini mtu ashukuru hivyo kwa kununuliwa soda na kukaribishwa korosho? Mtu wa Mtwara, anayelima korosho, atoe shukrani nzito kwa kukaribishwa Korosho? Au mtu ashukuru hivyo kwa kununuliwa soda, ingawa tunashauriwa kushukuru kwa jambo.

Nilikuwa na hamu ya kuongea na marafiki hawa wa Mtwara, ili niweze kujua kiini cha shukrani zao. Kabla sijaanzisha maongezi, mhudumu alileta bili ya soda tatu, shilingi elfu moja miatano. Maana yake kila soda shilingi miatano. Baadaye niliambiwa wengine wanauza mianne. Ninakumbuka nikiwa Mwanza, nililalamika kunywa soda ya shilingi miambili hamsini, nilikuwa nimezoea za miambili kule Bukoba. Wakati wa mongezi, na hao marafiki zangu nikagundua kwamba kwa kipato cha kawaida hapa Mtwara, inamchukua mtu zaidi ya miezi miwili bila kupata shilingi miatano. Hivyo wanaokunywa soda ni watu wenye kipato cha juu! Kilo moja ya korosho, inanunuliwa shilingi mia sita kwa mkulima! Hivyo kwa soda tatu ni lazima kuuza zaidi ya kilo tatu! Ndio nikaelewa ni kwa nini marafiki zangu walishukuru kwa soda.

Na korosho je? Wao si wakulima wa korosho? Kumbe walikuwa na hamu ya korosho? Na kweli hawakuweza kuificha hamu waliyokuwa nayo. Mmoja wao alisema alikuwa na zaidi ya mwaka bila kuonja korosho. Si kwamba hapendi kula korosho, bali bei yake ni ya juu. Mtu anayeshindwa kupata shilingi miatano kwa kipindi cha miezi miwili, atapata wapi za kununua korosho ambazo kilo moja ni shilingi elfu tano, tena hizo ni zile za Grade ya chini, ukitaka za Grade ya juu inayosafirishwa kwenda nchi za nje, kilo tano ni shilingi elfu kumi! Haya ndio maajabu ya Mtwara. Mtu analima korosho, lakini hawezi kula korosho.

Niliongea mambo mbali mbali na hao marafiki zangu, ingawa maongezi yetu yalikuwa yakikatishwa mara kwa mara na watu wanaopitapita wakiomba. Ukiwa mgeni huwezi kuwafumbia macho. Wakiomba unashawishika kuingiza mkono mfukoni na kutoa chochote kuwapatia. Tatizo ni je, utawasaidia wangapi, maana ni wengi. Siku hiyo tu nilifanya mahesabu kwa kumpatia kila aliyeomba shilingi 200 tu, ningetoa shilingi elfu ishirini! Wenyeji wamezoea, wakipita wanaomba, wanawaambia warudi kesho. Ndio hivyo na mimi nikajifunza, nikawa ninawaambia warudi kesho. Tatizo la omba omba si la Bima tu, hili ni taitzo sugu la mji wa Mtwara. Nimetembelea miji mbali mbali hapa Tanzania, lakini tatizo hili nilikuwa sijakumbana nalo. Ndiyo wapo omba omba katika miji yetu, lakini ninaona hapa ni utamaduni uliojengeka na kukubalika! Huwezi kukaa sehemu yoyote ile ya starehe, ya ibada au shughuli nyingine, bila kuwaona watu wakipita na kuomba omba. Si mmoja wala wawili ni zaidi ya kumi. Wanaomba kila siku ya Mungu. Sehemu nyingine tumezoea watu kuomba siku ya Ijumaa, lakini Mtwara, kila siku ya Mungu, ni ya kuomba!

Wengine ni walemavu, lakini linaloshangaza namba kubwa ni watu ambao hawana tatizo lolote kimwili la kuwazuia kujishughulisha na kupata chochote. Ni watu ambao wakipata wa kuwaelekeza na kuwasaidia kidogo wanaweza kujitegemea. Bahati mbaya tatizo hili haliingii kwenye sera za watanzania wanaojali!

Marafiki zangu niliokaa nao pale Bima, waliwatetea hawa omba omba, kwamba hawana la kufanya. Korosho ndio hivyo bei yake ya chini, ajira haipatikani na ikipatikana, mtu anafanyishwa kazi kama punda na kulipwa mshahara kidogo. Walitoa mfano wa kiwanda cha Korosho. Kiwanda hiki kinatoa ajira nyingi na hasa kwa akina mama, kazi ya kubangua korosho ni kubwa na inatesa. Lakini wanacholipwa akina mama hawa ni kidogo hivyo kiasi wengine wanalazimika kufanya kazi ya omba omba ili waongezee kipato chao. Kila anayeomba anasema “saidia masikini”. Na kweli ukimwangalia anayeomba, unaona amepambwa kwa ufukara na afya mbaya, anakuwa ni maskini katika nchi inayojigamba kupiga hatua kubwa katika kukuza uchumi. Watu wa nje wanayaona maendeleo, lakini hawa omba omba wa Mtwara, wakiyaona, basi watakuwa ni vipofu wanaojifanya kuwa vipofu!

Hayo ndio maajabu ya Mtwara, mkoa wenye utajiri mwingi. Mtwara, ni kati ya Mikoa inayochangia kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa. Mkoa unaolima korosho zao ambalo lina bei kubwa nchi za nje. Hata kule kwa wenyewe si kila mtu ana uwezo wa kununua korosho – bado mkoa huu unaongoza kwa omba omba na umaskini unaoonekana kwa vigezo vingi bila hata kuingia kwenye utaalam wa kimazingaombwe wa kuhesabu, takwimu na uchumi.

Mtwara, ni mkoa wenye maeneo mengi ya kuwekeza. Mfano mji mdogo wa Mikindani, ni sehemu nzuri iliyo chini ya usawa wa Bahari. Ni eneo zuri la kujenga mahoteli ya kisasa na ya kitalii – panavutia. Ingawa nyumba nyingi bado ni za makuti na zimejengwa kienyeji, bado panavutia. Bahati mbaya ni kwamba wenyeji wanaishi pale bila hati miliki, kesho na kesho kutwa wanaweza kutolewa mikindani na kuhamishiwa kwingine bila fidia yoyote ile.

Nimekaa Mtwara, zaidi ya miezi miwili. Sikusikia mtu akiongelea hili la mkulima wa korosho kuwa na hamu ya kula korosho, au mkulima korosho kufaidika na korosho. Kiasi kwamba Mtu, mgeni akiingia Mtwara, anuse maendeleo yaliyozalishwa na korosho. Kuna mataifa mengi ambayo hayajui kwamba korosho inatoka Tanzania. Wanajua inatoka India! Maana kuna korosho inayonunuliwa bila kubanguliwa, inabanguliwa kule India na kuuzwa Ulaya na Amerika. Wakiona ina nembo za India, wanafikiri inatoka India, kumbe ni ya Mtwara.

Nimekaa Mtwara, miezi miwili sikusikia mtu anayeongelea tatizo hili la Omba omba. Kusikia mtu anapanga mpango wa kuliondoa tatizo hili.

Nimekaa Mtwara, miezi miwili sikusikia mtu akinung’unika juu ya bei ya vitu. Tanzania yetu ni moja, kwa nini soda inunue shilingi miambili sehemu moja na miatano sehemu nyingine? Eti tatizo ni usafiri! Mji wenye Bandari, utakuwa na tatizo la usafiri? Ninasikia kuna mwekezaji aliyeleta meli nzuri na ya kisasa, kufanya safari za Dar- Mtwara, lakini akaihamisha kwa kutokuwa na wateja!

Kila kitu ni bei ya juu Mtwara. Wakorofi, wasioheshimu usawa wa kijinsia, wanasema kitu kisichokuwa na bei Mtwara ni chumvi na wanawake! Eti Mtwara, mwanamke, hajui neno hapana! Ni ukweli si ukweli, kwangu si hoja, ila wasiwasi wangu, ni kwamba sikuona wala kusikia aina yoyote ile ya kampeni juu ya ugonjwa wa UKIMWI, labda nimeweka chumvi, ila ukweli ni kwamba UKIMWI si agenda ya wanasiasa wa Mtwara. Nimetaja wanasiasa, maana nimekuwa Mtwara, wakati wa kampeni za uchaguzi, nilitegemea, kama unavyotegemea wewe msomaji wa makala hii kwamba korosho, omba omba, umasikini na UKIMWI, ni mambo ambayo yangekuwa kwenye agenda za wanasiasa wa Mtwara, lakini ni kinyume. Nilifikiri wanasiasa wana majibu ya maswali mengi yanayowasumbua watanzania wa Mtwara, kumbe si kweli. Lakini la kushangaza zaidi ni kwamba hata maswali ya wananchi si yale ambayo mtu angetegemea. Wale wakorofi walionielezea kwamba kitu chenye bei nafuu Mtwara ni chumvi na wanawake, waliongezea kwamba kisomo si hoja kwa wananchi wa Mtwara. Swali kubwa, kama unataka kufanya siasa au kama unataka kuwa kiongozi wa kisiasa, utaulizwa kama una uwezo wa kupika pilau, kama unashiriki mazishi, kama unawasalimia wafiwa, kama unasali na kama una uwezo wa kutoa misaada mbali mbali katika jamii. Hayo ndio ninayataja kama maajabu ya Mtwara, mkoa wenye utajiri mwingi lakini bado kuna kigugumizi cha maendeleo. Mfano uvuvi tu, ungeweza kubadilisha maisha ya omba omba wengi. Hata hiyo chumvi ambayo ina bei nafuu kuliko kila kitu, ingefanyiwa mpango mzuri na kutengeneza viwanda vya kisasa tofauti na inavyovunwa sasa hivi kwa njia za kienyeji, ungekuwa ni mradi wa kupunguza au kukomesha omba omba wa Mtwara. Kazi za mikono, Wamakonde, ni mafundi wa kuchonga vinyago, wangepata mpango mzuri wa kusafirisha vinyago hivi hadi nchi za nje. Meli zinazosomba korosho zingeweza kusomba na vinyago. Bandari tu ya Mtwara ni utajiri ambao vizazi vijavyo vitauliza mengi juu ya matumizi yake. Nimeondoka Mtwara, nikiwa na maswali mengi kichwani. Ni nani mwenye majibu ya maswali kama haya? Nina hakika si wanasiasa wa leo wa Tanzania!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

MADAKTARI WASIGOME LAKINI.....

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

MADAKTARI WASIGOME LAKINI PIA WASIPUUZWE!

Mgomo wa Madaktari umekuwa gumzo, kero, aibu na kwa upande mwingine ushindi wa aina Fulani! Inawezekana Serikali ikajiona mshindi kwa kufanikiwa kupambana na madaktari na kuwashinda kwa kuwafukuza kazi. Na inawezekana madaktari wakaonekana washindi pale serikali itakapolazimika kuajili madaktari kutoka nje ya nchi na kuwalipa pesa nyingi mara tatu ya zile walizokuwa wakidai madaktari. Ipo mifano mingi ambapo mtaalam kutoka nje analipwa zaidi kuliko mtaalam wa ndani, hata kama ujuzi wao na kisomo vinalingana.

Wamejitokeza watu mbali mbali kuandika juu ya mgomo huu. Mfano Tanzania Daima Jumapili, iliyopita ilikuwa na makala mbili zinazopingana juu ya mgomo huu. Makala moja ilikuwa inasema kwamba madaktari sheria inawazuia kugoma. Imeandikwa vizuri na hoja ni nzito. Mwandishi wa makala hii alienda mbali zaidi kwa kuwaweka madaktari waliogoma kapu moja na wauaji, maana vifo vilitokea wakati madaktari wakigoma. Makala ya pili ilikuwa ikiwasifia madaktari kwa kugoma kwao, na kwamba hawa ni wazalendo, maana badala ya kuikimbia nchi na kwenda kufanya kazi nchi za nje ambako wangepata mishahara mikubwa, wameamua kubaki hapa nchini. Na ili kuonyesha uzalendo wao, wameamua kutumia njia ya amani kudai kile wanachokiita haki yao. Mgomo unachukuliwa kama njia ya amani ya kushinikiza mambo katika serikali inayoelekea kukwepa wajibu wake.

Mbali na makala hizi mbili, majadiliano yanaendelea kila sehemu, vijiweni, kwenye daladala, kwenye vikao vya pombe na wakati mwingine kwenye mijadala ya kisomi inayoendeshwa sehemu mbali mbali kama kwenye redio na kwenye luninga. Kama nilivyosema hapo juu, watu wamegawanyika, wengine wanawatetea madaktari na wengine wanawalaani.

Binafsi nisingependa kuwatetea wala kuwalaani. Lengo la makala hii ni kuwakumbusha watanzania kwamba mgomo wa madaktari usichukuliwe kama mgomo wa madaktari. Mgomo huu ni kielelezo cha mambo mengi ambayo hayajapata ufumbuzi. Yapo mambo mengi ambayo yanahitaji majadiliano na hasa tukigusa keki ya taifa na ustawi wa jamii.

Mfano, siku hizi umekuwa utamaduni kwamba bila mgomo mambo hayafanyiki. Mheshimiwa Mkono, alisema kwamba Bodi ya Mkopo, ina pesa nyingi. Pesa hizi hazikutoka hadi wanafunzi wa Chuo Kikuu, alipogoma kwenda madarasani. Juzi tena wanafunzi wa uandisi walilazimika kugoma ili wapate haki zao. Ni imani yangu kwamba baada ya mgomo wa madaktari utafuata mgomo mwingine, sitaki kuwa mtabiri, lakini unaweza kufuata mgomo wa walimu.

Kabla ya kuwalaani au kuwatetea madaktari, ni lazima tujiulize ni kwa nini madaktari hawa waliamua kugoma siku hizi za kampeni? Kwanini waliamua kugoma siku ambazo kila Mtanzania anaona wazi jinsi serikali inavyotumia pesa nyingi kwenye zoezi zima la uchaguzi na kampeni zinazoendelea? Ukimwambia mtu kwamba Taifa letu ni masikini atakuita mwendawazimu. Mabango yote ya kampeni yametengenezwa kwa pesa, kofia na t-shirts ni pesa, magari yanatumia mafuta kuzunguka nchi nzima. Nchi masikini haiwezi kumudu kufanya yote hayo.

Inawezekana kabisa kwamba madaktari wetu waliamini kwamba nchi yetu ni masikini, hivyo ilikuwa ni wajibu wao kama watanzania kushikamana na kufanya kazi kwa kujitolea zaidi ya kuangalia mishahara mikubwa. Ninasema walifikiri hivyo maana karibu kila Mtanzania anafikiri na kuamini kwamba nchi yetu ni masikini. Lakini baada ya kuona yale tunayoyaona, pesa zinavyotumiwa kwa mambo ambayo si muhimu, madaktari nao kama binadamu ni lazima waanze kuhoji. Ndio maana ninasema ni jambo la msingi kujiuliza ni kwa nini mgomo huu uje wakati ambapo taifa letu linaonyesha dalili za kuwa na pesa nyingi. Kwanini mtu aendelee kufanya kazi kwa kujitolea wakati taifa lina pesa nyingi na za kumwaga? Kwanini mtu aendelee kujitolea wakati yeye anafanya kazi nyingi hadi kukesha na kutembelea daladala, wakati wale wasiofanya kazi yoyote wanatembelea mashangingi? Wanasomesha watoto wao nje ya nchi na kuishi maisha kifahari? Wana majumba makubwa na wala hawana kitu chochote kinachosumbua akili yao.

Jambo la pili ambalo ningependa watanzania wazingatie juu ya mgomo huu wa madaktari ni neno uzalendo. Mtu mzalendo analipenda taifa lake na kulitumikia na taifa linampenda na kumtumikia. Mzalendo anawajibika kulitumikia taifa lake, na taifa linawajibika kumtunza na kumjali raia wake. Taifa linalojali linajua kwamba madaktari wanashughulikia maisha ya watu, daktari akifanya kosa, maisha yanapotea. Hivyo ni lazima daktari awe kwenye mazingira mazuri ya kumwezesha kutulia kiakili. Kama daktari ana wasiwasi na karo ya mtoto, kama daktari ana wasiwasi na kodi ya nyumba, pesa za chakula, hawezi kutulia kiakili na kufanya kazi zake ipasavyo. Jinsi daktari anavyowajibika kuyatunza maisha ya raia kwa gharama yoyote ile, ndiyo taifa linavyopaswa kuwajibika kuhakikisha daktari anaishi kwenye mazingira yanayomwezesha kufanya kazi vizuri. Na daktari anayejali akishindwa kufanya kazi kwa matatizo yanayosababishwa na taifa, ni lazima atasema. Kwa maana nyingine, kile kinachoonekana kuwa mgomo, hadi wengine wanataja sheria inayozuia mgomo wa madaktari, si mgomo, ni njia ya kufikisha ujumbe kwa wanaohusika kwamba madaktari hawawezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa na utulivu, vinginevyo watasababisha vifo badala ya kuokoa maisha.

Hii ni kinyume, kwa mfano madaktari wangeamua kufanya mgomo baridi. Wanakwenda kazini, lakini hawafanyi kazi. Mwisho wa mwezi wanapata mshahara. Tuna mifano mingi ya watanzania ambao, hawajagoma, lakini hawafanyi kazi ipasavyo. Wanashinda kazini, lakini hakuna wanachokifanya. Mtu mwenye akili nyingi, anaweza kusema ni bora hao, maana hawakugoma, kitu kibaya ni mgono na sheria inazuia mgomo. La msingi ni kuitii sheria! Madaktari wetu wangefanya hivyo, hakuna ambaye angepiga kelele. Jinsi ilivyo tunatawaliwa na giza la unafiki uliofungamana na ujinga mkubwa!

Mwandishi aliyewaweka madaktari kwenye kapu moja na wauaji, amewakosea kabisa. Maana kamani kuangalia kwa mtazamo huo, basi watu wengi hapa Tanzania wanashiriki mauaji. Mfano, ni watu wangapi hapa Tanzania, wanakufa kwa kupotoshwa kutotumia kondomu? Ni watu wangapi wanakufa kwa kutoweza kununua dawa ya malaria? Ni watu wangapi na hasa akina mama wanakufa kwa kushindwa kusafiri hadi kwenye zahanati au hospitali wakati wa kujifungua? Wanakufa bila sababu yoyote. Mbona hatupigi kelele na kusema kwamba Serikali kushindwa kusambaza huduma za jamii inashiriki katika mauaji?

Pia ninashindwa kukubaliana na mwandishi huyu anaposema kwamba Madaktari walicheza ndombolo mbele ya wagonjwa. Huku ni kuweka chumvi. Madaktari hawakuwa na magomvi na wagonjwa, itakuwaje wawachezee ndombolo. Kama walicheza, waliilenga Serikali, na wala si wagonjwa. Ni bora kueleza ukweli kuliko kupotosha. Si busara kuongeza chumvi kwenye swala nyeti kama hili.

Madaktari ni watu wanaofanya kazi kubwa na kwa kujitolea na kuyaweka maisha yao hatarini. Madaktari walio wengi wanakesha kwa kufanya kazi masaa mengi zaidi ya watanzania wengine. Ni vigumu kuwalipa kwa kile wanachokifanya. Kama wanadai nyongeza ya mshahara, maana yake ni kwamba wanataka wafanye kazi akili yao ikiwa imetulia. Wanataka wafanye kazi wakijua kwamba nyumbani watoto wanakwenda shule, wana chakula cha kutosha na wana nyumba ya kulala. Si vibaya pia wakiwa wanajua kwamba wana usafiri wa kuaminika na wana pesa ya akiba kwa tatizo lolote linaloweza kujitokeza kama mwizi wa usiku!

Madaktari wetu wanaishi ndani ya jamii. Wanaona jinsi watu wengine wanavyotesa tena bila ya kuwa na kazi wala biashara inayoonekana. Wanaona jinsi viongozi wa serikali wanayoyafurahia maisha, na wakati mwingine wale wanaofurahia maisha na kuishi maisha ya starehe ni watu ambao hawakusoma sana kama madaktari. Binadamu yeyote ni lazima aguswe na hali kama hii.

Tusiwalaumu madaktari na wala tusiwatetee. Jambo la msingi ni kuchunguza chazo cha mgomo wao. La muhimu ni serikali kukaa chini na kuzungumza nao na kuyachunguza madai yao. Pesa wanayoidai si nyingi ukilinganisha kazi nzito wanayoifanya. Pesa wanayoidai si nyingi ukilinganisha na pesa zinazotumika sasa hivi kutengeneza kofia, t-shirts na shughuli nyingine za uchaguzi. Kama hizo pesa zinapatika, kwa nini zisipatikane pesa za kuwahudumia madaktari wetu ili waweze kufanya kazi kwa utulivu?

Kule tunakoelekea panahitaji majadiliano zaidi ya kutumia nguvu na mabavu katika maamuzi mbali mbali katika jamii yetu. Panahitaji hekima na busara badala ya kutumia madaraka na majigambo. Ni kweli kwamba si halali madaktari kugoma, lakini pia si halali serikali inayowajali raia wake kuwafukuza madaktari.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

BARUA YA WAZI KWA MAREHEMU KAINAMULA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2006

BARUA YA WAZI KWA MAREHEMU GOSBERT RUTABANZIBWA KAINAMULA.

Mpendwa marehemu Kainamula. Nilitamani kukuandikia barua hii mwezi wa tano mwaka jana baada ya kura za maoni za CCM. Bahati mbaya nilishambuliwa na kigugumizi cha mikononi na sababu kama tatu hivi zilifunga akili yangu. Si kwamba niliacha kufikiri, lakini nilishindwa kabisa kuyaweka chini kwa maandishi yale niliyoyafikiri.

Sababu ya kwanza iliyoifunga akili yangu ni kwamba nilikuwa na mashaka kama kweli huko ulipo kuna uwezekano wa kusoma barua. Ingawa hadithi ya Aliyeonja pepo inatupatia matumaini kwamba huko maisha yanaendelea kwa njia nyingine ambayo ni bora zaidi, mfano kwamba huko hakuna kuoa na kuolewa, hakuna tajiri na masikini, hakuna mwenye taabu, kila kitu ni raha tupu, lakini wengi wetu ni kama Thomas, bila kuona kuamini ni vigumu. Nimekuwa nikisoma barua ambazo watu mbali mbali wamekuwa wakimwandikia marehemu Mwalimu Julius Nyerere. Labda hii ingekuwa sababu tosha ya kunishawishi kukuandikia. Lakini pia sikuwa na uhakika kama wewe na Mwalimu Nyerere, mko sehemu mmoja. Kwa vile yeye atatangazwa mwenye heri, basi yeye yuko mbinguni. Nilifikri ikitokea wewe uko motoni, usalama wa barua yangu kukufikia bila kuungua ni mdogo.

Sipendi kuamini kwamba uko motoni, lakini ninajua fika kwamba ulikuwa na dosari ndogo ndogo za kukufungia milango ya mbinguni. Kitulizo changu ni kwamba kazi za kujitolea ulizozifanya kwenye shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross), kwenye ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa, zinatosha kukufungulia milango ya mbinguni. Ulijitolea kiasi kikubwa na kuliongoza shirika la Msalaba Mwekundu katika Wilaya ya Karagwe. Pia ulichangia kiasi kikubwa katika uongozi wa Mkoa wa Kagera na Taifani. Mbali na kazi za Red Cross, ulionyesha upendo mkubwa kwa watu. Kama Mwenyezi Mungu, hakuona mema yako na kuamua kuangalia dosari ndogo ndogo ulizokuwa nazo, basi wa kuiona Mbingu ni wachache sana. Kasoro ulizokuwa nazo ni zile zinazowakumba binadamu wote ambao wameumbwa kwa ukamilifu. Dosari hizo mtu wa kuzikwepa ni yule mwenye sifa ya marehemu! Wapo wachache wenye kufanikiwa kuzificha kasoro hizi macho pa watu, wanafiki ambao kwa kufanikiwa kufanya hivyo wanajiona ni bora kuliko wengine na wanakuwa mahakimu wa wengine, lakini hawawezi kufanikiwa kuficha lolote mbele za Mwenyezi Mungu. Ninabaki kujituliza kwamba Mungu, alizifumbia macho kasoro ndogo na kuangalia mema yako mengi.

Sababu ya pili iliyonifanya nichelewe kuandika barua hii ni kwamba mara baada ya kura za maoni za CCM, zilizompitisha rafiki yako wa Karibu Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Freeman Mbowe, wa CHADEMA, alitangaza kugombea kiti cha urais kupitia chama chake. Unaukumbuka urafiki na undugu wangu na Mbowe. Siwezi kukana uhusiano huo. Pia siwezi kukana kutofahamu uwezo, uzalendo na ukomavu wa kisiasa wa rafiki yangu Mbowe. Wengine wanasema ni mchanga katika siasa, wengine wanasema ni mhuni kwa vile anaendesha biashara ya “Nights Clubs”. Wengine wanasema yeye ni pandikizi la CCM, kwa vile baada ya Tume ya uchaguzi kumtanga JK, kama mshindi, Mbowe, alimkumbatia. Yalisemwa mengi, lakini kwa watu kama mimi ambao tuko karibu naye, bado tuliamini kwamba kijana huyu ni hazina kubwa katika taifa letu. Hivyo Kikwete upande mmoja na Mbowe, upande mwingine kilikuwa ni kigugumizi tosha.

Sababu ya tatu iliyochelewesha barua hii ni kwamba wakati wa uchaguzi mkuu TEMCO, ilinipatia kibarua cha kuwa mwangalizi wa ndani. Nilipangwa Mkoa wa Mtwara. Kazi yangu ilikuwa kuangalia na kutoa ripoti TEMCO, hivyo TEMCO, ndio wasemaji wakuu. Nisingeweza kukuandikia wakati huo ingawa nilikuwa na mengi ya kukushirikisha. Mfano umasikini wa mkoa wa Mtwara, ni kitu kilichoisimbua roho yangu hadi leo hii. Mbaya zaidi ni kwamba wakati wa kampeni, pesa nyingi zilitumika. Wagombea walionyesha kuwa na pesa nyingi za kutisha. Kwamba walikuwa na pesa si swali, lakini ni wapi pesa hizi zilipatikana miongoni mwa watu maskini hivyo ni swali gumu hata kwa Mheshimiwa Jakaya Mlisho Kikwete. Lakini kwa vile Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi- Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, atakuwa na jibu. Tumpatie muda. Ni imani yangu kwamba watu wa Nanyamba, waliomkataa mama huyu mbele yake watafurahi kusikia jibu hilo.

Pamoja na sababu hizo tatu ni kwamba nilianza kusahau kukuandikia kama nisingetembelea Karagwe wakati wa mwaka mpya. Nikiwa Karagwe, kumbukumbu zilikuja, na hasa baada kukutana na ndugu na jamaa zako. Nilipokutana na Sabi Rwazo, mtu anayeipenda CCM kuliko maisha yake, mtu anayeitumikia CCM bila kusubiri shukrani. Mtu ambaye kwa miaka mingi amekuwa msingi wa uhai wa CCM katika Wilaya ya Karagwe na mkoa mzima wa Kagera. Sabi Rwazo, ambaye pamoja na mapenzi ya CCM, hana chuki yoyote ile na wapinzani, mtu wa watu, nilishindwa kujizuia kujadili juu yako wewe Marehemu Gosbert Rutabanzibwa Kainamula.

Lakini hasa nimesukumwa na habari nilizozisikia Karagwe, kwamba Mheshimiwa Jakaya Kikwete, alimkumbatia baba yako Mzee Kainamula “Mfalme wa Nyuki”, kwa furaha kubwa wakati wa kampeni zake mjini Kayanga. Nimesikia, alimwambia baba yako kwamba wewe ulikuwa rafiki yake mkubwa. Ni ishara kwamba mtu huyu ana kumbukumbu. Hii ni ishara nzuri kwa kiongozi.

Nimeandika kukujulisha kwamba Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ni Rais wa Tanzania. Binafsi simfahamu kwa karibu Mheshimiwa Kikwete. Kumfahamu kama vile ninavyomfahamu kwa karibu Mheshimiwa Freeman Mbowe. Wewe mwenyewe unafahamu jinsi nilivyomfahamu Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kupitia watu mbali mbali. Nilimfahamu kupitia kwako, kupitia wanamtandao na ndugu zangu waliobahatika kufanya kazi naye kwa karibu.

Nilipoandika makala ya Fisadi na Mwenye Virusi ni nani zaidi, niliandika kwa kupinga dhana nzima ya kuwanyanyapaa watu wenye UKIMWI. Kwangu niliona bora kuongozwa na mtu mwenye virusi kuliko fisadi. Ingawa huu ulikuwa ni uvumi ulioenezwa kwa nia ya kumdidimiza Jakaya Kikwete, nilisimama upande wake si kwa vile ni mtu niliyemfahamu kwa karibu au kuwa rafiki yangu kama alivyokuwa rafiki yako. Nilisimama kutetea haki!

Ninakumbuka miaka mitatu iliyopita tukiwa tumekaa “Farida CafĂ©” Kanyanga- Karagwe, ulinielezea juu ya ndoto za Jakaya Kikwete, kuwa rais wa Tanzania. Ingawa nilikuwa na habari za Jakaya Kugombea Urais wa Tanzania mwaka 1995, sikufahamu kwamba mtu huyu alikuwa na ndoto hii kwa muda mrefu. Hili jambo la pekee kidogo na ni la Afya kwa Taifa letu. Mtu mwenye ndoto hama hii ni lazima awe makini, mzalendo na mwenye upeo mkubwa. Uliniambia kwamba miaka ya nyuma mkiwa Tabora, Jakaya alikudokezea juu ya nia yake ya kutaka kuwa kiongozi wa Taifa la Tanzania. Na ukaongezea kwamba siku hiyo ikifika basi a wewe utakuwa mkuu wa Wilaya! Siku hiyo sasa imefika. Jakaya ni Rais! Bahati mbaya wewe ni marehemu! Wilaya yako, ni nani ataiongoza? Ni kweli ungekuwa Mkuu wa Wilaya, maana inavyoelekea Jakaya, hana tabia ya kuwasahau rafiki zake, na hasa rafiki wachapakazi kama ulivyokuwa wewe Kainamula. Amemteua rafiki yenu Lowasa, kuwa Waziri Mkuu na kusimama kidete kutetea uchaguzi wake kwamba si urafiki bali ni kwa vile Lowasa, ni mchapa kazi. Watu wengi waliotegemea jambo hili walijitahidi kumkatisha tama kwa kuandika juu ya uhusiano wao kwenye magazeti na kwenye mikutano isiyokuwa na mwenyekiti wala katibu, lakini Jakaya, hakuyumba!

Mpendwa Marehemu Kainamula, wewe ulikuwa mtu wa kwanza kunifunulia uwezo wa Jakaya. Uliniambia kwamba Jakaya ni mzalendo wa kweli, ni mchapa kazi, si mtu wa kupendelea rushwa, mtu wa watu, mtu wazi na kwa kutaka kuwa mwaminifu kwa maneno yako, ulisema kwamba yeye ni Nyerere wa pili! Hotuba yake ya kulifungua Bunge, ilionyesha jinsi ulivyomfahamu vizuri Jakaya. Sasa hivi hotuba hiyo ni gumzo. Mbali na ujumbe mzito uliokuwa kwenye hotuba hiyo, ni ule uwezo aliouonyesha wa kutoa hotuba ndefu bila kusoma, kuzivuta na kuzigusa hisia za watu, kucheka yeye mwenyewe na kuwachekesha wale wanamomsikiliza kama alivyokuwa akifanya baba wa taifa. Pia ameonyesha hali ya kujisimamia kama alivyokuwa Mwalimu. Ile namba yake ya kusema mara kwa mara “ Tusilaumiane mbele ya safari” imeonyesha kwamba hana ndugu wala rafiki kwenye kazi.

Ninakumbuka uliniambia kwamba tatizo pekee ulilolifahamu kwa Jakaya, ni kutofuata muda. Kwamba alikuwa na tabia ya kuchelewa kwenye mikutano na sehemu mbali mbali. Lakini pia ulimtetea kwamba tatizo kubwa ni hali yake ya kutaka kumlizisha kila mtu. Kwamba anapenda kumaliza tatizo moja kabla ya kuanza jingine, anapenda kumsikiliza mtu hadi mwisho bila kumkatisha tama kwa kumwambia kwamba ana ahadi na watu wengine. Kwa njia hii alishindwa kufuata muda. Lakini kwa vile sasa ni Rais, muda wake utapangwa na hatakuwa na uhuru wa kumlizisha kila mtu kama alivyokuwa amezoea.

Mbali na yale uliyonielezea kuhusu Jakaya, nilipata pia bahati ya kukutana na wanamtandao wakati wa mchakato wa kura za maoni. Swali langu kubwa kwao lilikuwa ni je kama Jakaya, asipotitishwa na CCM, atajiunga na vyama vya upinzani. Waliniambia kwamba ukitaka kukosana na Jakaya, uliza swali hilo. Hakutaka kulisikia, maana aliamini asilimia miamoja kupitishwa na chama chake. Wanamtandao hawa walinisaidia kumfahamu zaidi Mheshimiwa Jakaya Kikwete.

Ninapokuandikia barua hii tayari amemaliza kuwateua mawaziri. Majina mengi ni mapya, lakini wengi wao ni wanamtandao, hivyo utakuwa unawafahamu. Namba ya wanawake imeongezeka kuliko wakati wa utawala wa hamu zilizopita. Na wengine wachache ni wazee wetu wa siku nyingi kama Mungai, Muramba na Mzee Kingunge. Baraza lenyewe ni kubwa. Mawaziri na manaibu mawaziri jumla inakuja watu 60! Kwa mtindo wa zamani, hayo ni mashangingi mapya 60, bila kutaja mengine. Serikali iliyomakini, idadi hiyo si kubwa, lakini kwa mtindo wa kuonyesha ufahari na ukubwa wa uwaziri, ni hatari ambayo kila mtu anasubiri kwa hamu miujiza ya Jakaya. Tumpe muda!

Kuna mambo mengi mapya katika serikali ya Jakaya. Mfano Ofisi ya Waziri Mkuu ina naibu Waziri anayeshughulikia Maafa na Kampeni Dhidi ya Ukimwi. Hili limeonyesha umakini wa Jakaya. Maana kama kweli tunataka kupamba na ugonjwa huu wa hatari ni lazima kuonyesha kwa matendo. UKIMWI, ni adui mkubwa wa taifa letu. Unawachukua watu ambao wangelisaidia kulijenga taifa letu.

Jakaya, ameitisha mjadala wa kitaifa. Ameonyesha wazi nia ya kutaka kujenga Jukwaa la majadiliano. Mtu kama mimi ni lazima nifurahi sana, maana nimekuwa nikipigia kelele Jukwaa la majadiliano. Ni vigumu nchi yoyote ile kupata maendeleo ya kweli bila kuwa na jukwaa la majadiliano. Na nitakuwa mtu wa kwanza kuingia uwanjani:

Nimeiangalia kwa makini serikali ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Sikuona vizuri anapotaja maadili ya vijana wetu. Nilitegemea jinsi Maafa na kampeni dhidi ya Ukimwi, ilivyopatiwa Naibu waziri, basi na kwa upande wa Elimu, maadili ya vijana wetu yangempata Naibu waziri. Hali ilivyo sasa hivi ni kwamba tunawatelekeza vijana wetu. Tunawaachia vijana wetu kutafuta msimamo wao juu ya maadili, na hasa juu ya uhusiano wa msichana na mvulana. Hakuna mwongozo unaoeleweka wa kuwaongoza vijana wetu katika bahari ya mahusiano. Zamani tulikuwa na vitabu kama Mvulana Je, na Msichana je,- Mheshimiwa Willbrod Slaa, Mbunge wa Karatu, ni kati ya watu waliokuwa wameshirikia kuviandaa vitabu hivi. Siku hizi vitabu hivi havisikiki tena. Mbaya zaidi ni kwamba kile kizazi ambacho ndicho kingepanga mfumo mzuri wa kuwaongoza vijana, ndicho kinachochea maadili mabaya kwa vijana wetu. Badala ya kuwasaidia vijana wetu kuongelea na kulivuka salama dimbwi la mapenzi wanawasaidia kuzama na kuangamia! Inakuwa vigumu kupambana na UKIWMI, inakuwa vigumu kutengeneza familia bora ambazo zinaweza kuwa msingi wa taifa imara. Tunawaachia vijana wetu kuliona tendo la ndoa kama kitu cha kawaida, kitu cha starehe, burudani, biashara, silaha ya kushinda mitihani kwa wasichana nk., tunashindwa kuwafundisha utakatifu wa tendo hili, umuhimu wa tendo hili na hasa jinsi tendo hili linavyoweza kukomaza na kuendeleza uhusiano wa mtu na mtu, jinsi tendo hili linavyoweza kusaidia kujenga familia bora ambazo zinaweza kuwa msingi wa taifa lililo imara. Ingawa ni mapema sana kusema, lakini kwa muundo wa serikali inaonyesha kwamba hata na kwa mtu makini kama Jakaya, swala hili la malezi ya vijana bao limetupwa kando!

Nimekuandikia mengi, bila kuwa na uhakika kama utapata nafasi ya kuyasoma na kunijibu. Lengo langu kubwa lilikuwa kukujulisha kwamba, kama ulivyoniambia, miaka mitatu iliyopita, sasa hivi Jakaya Mrisho Kikwete, ni Rais wa Tanzania. Sina shaka kwamba yeye sasa hivi ni tumaini la taifa letu. Akifanya vizuri nitakujulisha, akifanya vibaya nitakulalamikia! Ni bahati mbaya kwamba wewe uliikimbia nafasi yako ya Ukuu wa Wilaya. Unafikiri angekupatia Wilaya gani? Tabora mjini? Mungu, ailaze roho yako mahali pema peponi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

TUSOME ALAMA ZA NYAKATI

MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA RAI 2006.

TUSOME ALAMA ZA NYAKATI.

Sipendi makala hii kuiita Barua ya wazi kwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania, nafikiri si busara na ni kutokuwa na heshima kuwaandikia waheshimiwa viongozi wa Kanisa barua ya wazi. Hivyo basi makala hii ninaiandika kwa unyenyekevu mkubwa na kwa kupima kila neno nitakalolitumia. Ninajua vizuri umuhimu na ushawishi wa maaskofu katika Jamii yetu. Nimesita sana kuandika makala hii, lakini nimesukumwa na ukweli kwamba ni lazima tusome alama za nyakati. Tukishindwa, Tukumbushane si dhambi na wala si kushambuliana, si chuki wala kinyongo – kukumbushana ni jambo muhimu sana katika jamii yoyote ile. Wengine wakikumbushwa jambo wanakuwa mbogo, maana kuna utamaduni kwamba kuna watu wasiokosea. Lakini kwa jambo linalohusu uhai wa mwanadamu, ni lazima kukumbushana hata kama inaelekea kutoa picha ya tabia mbaya, tabia ya kutokuwa na heshima kwa viongozi. Ningependa kukumbusha kwamba:

Ni lazima tuipongeze serikali yetu kwa kusimamia maamuzi yenye utata kwa faida ya watanzania walio wengi. Na kweli hii ni kazi ya serikali. Serikali ni lazima iangalie faida ya wengi na hasa jambo linalogusa uhai wa watu wake. Serikali yoyote ile inayojali uhai wa raia ni Serikali ya kupongezwa na inakuwa inatekeleza wajibu wake mkubwa. Msimamo wa serikali wa kupinga tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ni la kupongezwa. Bila kuwa na nia ya kuonyesha aliyeshinda au aliyeshindwa maana nia ni kujali uhai wa watanzania. Kwa kutosoma alama za nyakati, maaskofu walitoa tamko la kupinga mpango wa serikali wa kufundisha matumizi ya kondomu kwenye shule za msingi. Serikali imekataa kukubaliana na maaskofu na itaendelea na mpango wa kuwafundisha watoto wa shule za msingi juu ya matumizi ya kondomu.

Ni wajibu wa serikali kutoa elimu kwa watu wake. Matumizi ya kondomu ni elimu muhimu sana maana inagusa uhai wa wananchi wote bila ya ubaguzi. Hakuna aliye huru mbele ya ugonjwa wa UKIMWI, labda yule anayeishi mwezini, na kufuatana na tamko la Maaskofu wetu, labda watoto wafundishiwe Mwezini, lakini kwa yoyote aliye kwenye jamii ya watu wa hapa duniani, hawezi kukwepa kushambuliwa, kwa kutaka yeye au kwa kutotaka. La msingi ni kujikinga kwa maana ya kujikinga, bila porojo, mchezo na unafiki. Hili linahitaji maelezo ya kina, lakini mwenye nia ya kuelewa anaweza kusoma katikati ya mistari.

Sote kwa pamoja ni lazima tusome alama za nyakati. Ukweli ni kwamba watoto wa darasa la tatu wanakuwa wanafahamu kila kitu juu ya tendo la ndoa. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba siku hizi watoto wanapata mimba wakiwa na umri wa kuanzia miaka kumi. Hivyo maaskofu wanaposema shule za msingi watoto wana umri mdogo wa kufundishwa matumizi ya kondomu, wanajidanganya na kujifanya vipofu.

Mapadre wa Kanisa katoliki kupitia sakramenti ya kitubio ni ushahidi wa kutosha wa jambo hili. Bila kuingilia siri za kitubio. Ni imani yangu kwamba Padre wote wanafahamu vizuri kwamba tendo la ndoa linaanza katika umri mdogo. Mwanzo mtu akiwa anasikiliza maungamo kwa mara yake kwanza, anaweza kufikiri labda watoto wanatania au hawajui wanachokisema. Lakini huo ndio ukweli kwamba tendo hili linafanyika katika umri mdogo. Kuna vichocheo vingi. Video zimetapakaa sasa hivi kila mahali, kuna magazeti yenye hadithi na picha zinazoonyesha mambo ya ngono. Mtandao nao umesheheni mambo mengi kweli. Mtoto anaanza kujua na kutambua umuhimu wa tendo la ndoa akiwa na umri mdogo!
Hivyo maaskofu wasiongelee kondomu tu, waongelee na video, tv, redio, miziki, magazeti na mambo mengine katika jamii yetu. Waongelee kutengeneza mfumo wa kurudisha maadili bora.

Na tujuavyo ugonjwa wa UKIMWI umejikita sana sana akika tendo la ndoa. Kwa kuona hivyo na kwa vile serikali inajali uhai wa watu wake, ndio maana imepitisha uamuzi wa kufundisha matumizi ya KONDOMU kwenye shule zi msingi. Kinyume na hapo ni kutaka watu waendelee kufa na kuteketeza kizazi chote. Ni heri Serikali imeona hivyo, maana kwa hili sote ni wadau!

Malengo ya Maaskofu wetu ni mazuri. Hakuna anayepinga jambo hili. Sote tunajua kwamba Maaskofu ni lazima wafundishe maadili mazuri na ni lazima wahakikishe tendo la ndoa linabaki kwenye ndoa na ndoa zilizobarikiwa. Hakuna anayeweza kuwapinga wakati wanafanya kazi yao.

Utata unaojitokeza ni kwamba maadili yameanguka. Ni nani wa kubisha? Na dawa yake ni nini? Hatoshi mtu kusema kwamba wasichana wasivae nguo fupi, haitoshi kusema vijana waache vitendo vya ngono, haitoshi kukemea tu panahitajika kazi ya ziada. Kazi ya kuunda mfumo wa kurudisha maadili. Ugonjwa wa UKIMWI unapita kwenye tendo la ndoa ambalo sasa hivi linaonekana kuwa kitu cha kawaida. Tukitaka kuwa wa kweli tendo hili linaonekana kuwa la kawaida kwa watu walio wengi, viongozi wa serikali, viongozi wa dini, vijana hata na watoto wadogo. Je, tufanye nini? Tuache watu waendelee kufa kwa kusisitiza uaminifu, kujinyima na kuacha wakati ni ukweli kwamba haya ni mambo yasiyowezekana. Hapa ni lazima serikali iingilie, tena bila woga. Siku za nyuma serikali ilikuwa na woga wa kufanya maamuzi kama haya. Serikali iliwaogopa sana viongozi wa dini. Lakini woga huu umefikia mwisho maana hata na viongozi wa dini ni kelele tupu. Hawana njia nyingine. Wanabaki kuimba wimbo ule ule wa kwamba wao wanapinga matumizi ya kondomu na kwamba kuruhusu kondomu ni kuruhusu uzinzi, wanabaki pale pale kutaja amri za Mungu, na kutaja vifungu vya Neno la Mungu lakini hawaji na mfumo mzuri wa kurudisha maadili.

Si kweli kwamba mtu akifundishwa kondomu ni lazima aende kufanya tendo la ndoa. Kuna ushahidi wa watu wengi wanaofahamu matumizi ya KONDOMU, lakini hawazigusi, ila wanafahamu kwamba wakati ukifika zinaweza kuwasaidia. Siku za nyuma vijana wote waliomaliza kidato cha sita na vyuo walikuwa wanapitia mafunzo ya Jeshi, walikuwa wanakwenda Jeshi la Kujenga Taifa. Huko walifundishwa matumizi ya silaha. Walifundishwa kushika bunduki na kutumia bunduki. Silaha si kitu kizuri, silaha inatoa uhai wa mtu na kuvuruga amani. Lakini mbona hatukusikia vijana waliotoka Jeshi la Kujenga Taifa, wakitumia bunduki kutoa uhai wa raia, mbona hatukusikia amani inavurugika kwa vile vijana wamefundishwa silaha na mbinu za kupigana. Ujambazi tunaoushuhudia siku hizi haukuwepo wakati vijana walipokuwa wakienda Jeshi la kujenga taifa.

Siri yake ni kwamba. Kulikuwa na mfumo wa kuwafundisha vijana. Serikali iliandaa mfumo wa kuwafundisha vijana silaha na kuwaelekeza ni lini mtu anaweza kutumia silaha. Mafunzo ya Jeshi la kujenga taifa yalikuwa yamepangwa vizuri kwa mbinu nyingi za kumwezesha kijana kuwa raia mwema na kulinda taifa lake. Walifundishwa nyimbo za kimapinduzi na za kujenga uzalendo, walishindiliwa kasumba za kila aina ili walipende taifa lao. Ni mfumo mzuri ulioweza kuwakutanisha vijana wa Musoma, Mwanza, Mtwara, Arusha , Dodoma nk. Ni mfumo ambao ulifundisha kwa matendo.

Tunahitaji mfumo kama huo kuwafundisha vijana matumizi ya kondomu. Ili wasifundishwe uzinzi, bali kujua maana ya kondomu na ni wakati gani mzuri wa kutumia kondomu.

Vinginevyo Maaskofu, wabuni mfumo wa kurudisha maadili kwenye mstari. Wabuni mfumo wa kaufundisha uhusiano wa mtu na mtu, uhusiano wa mtu na jinsia tofauti. Sasa hivi jambo hili halifundishwi na Kanisa limeshindwa kuwaandaa viongozi wa kiroho kwenye mashule na vyuo. Mafunzo ya kiroho yangeanzia kwenye shule za msingi na kuendelea hadi vyuo vikuu. Sasa hivi vijana wanaachiwa kuogelea tu katika mahusiano bila kiongozi wa kiroho. Ni nani anaongoza maisha ya kiroho ya vijana wanaoishi kwenye hosteli kama ile ya Mabibo? Maaskofu wetu wanasema nini juu ya hili?

Kwa maoni yangu, badala ya Maaskofu Kupinga mpango wa Serikali, wangeomba kushirikiana na Serikali. Au kwa namna nyingine wangeitisha Jukwaa la Majadiliano, ili watu wote washiriki na kutoa maoni. Wazazi watoe maoni juu ya kuwalea watoto, serikali ichangie na viongozi wa dini wachangie. Serikali ifundishe matumizi ya kondomu, lakini kanisa iingize mafundisho ya kiroho. Ili hivi vitu viwili viende kwa pamoja. Mtoto afundishwe matumizi ya kondomu, lakini hapo hapo ajue mwongozo na maelekezo kuhusu maisha safi ya kiroho. Endapo ataanguka, maana hakuna shujaa wa hili, basi ajue kwamba ni lazima kujilinda yeye na wale wote wanaomzunguka.

Maaskofu wakazane kutengeneza mifumo ya kufundisha kwa matendo au kufundisha kwa kuonyesha mfano. Yawepo makundi ya watu katika jamii yetu wanaoishi maadili ya kweli. Ushuhuda wa Yesu, ulikuwa vipofu kuona, vilema kutembea na wafu kufufuka. Ushuhuda wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki ni upi? Ni kikundi gani katika jamii yetu kinaishi maadili safi, ili watu wajifunze kwa kuona na kwa vitendo. Ni familia gani inawalea watoto katika maadili safi ili na familia zingine zione mfano. Ni ndoa gani inaishi maadili bora ya ndoa ili na ndoa nyingine zione mfano? Maaskofu wangekuwa na wasiwasi na haya zaidi ya kuwa na wasiwasi na vijana kufundishwa matumizi ya KONDOMU. Maana kama kuna mfano, hakuna wa kupotosha!

Mikutano na kutoa matamko si mfumo mzuri wa kuisaidia jamii. Yesu, aliishi na watu, alifundisha kwa matendo, alisafisha miguu ya watu, alijenga jumuiya za mfano. Maaskofu pia ni lazima wafanye hivyo. Wajenge jumuiya za watu, wawe karibu na watu na kufahamu matatizo yao, washiriki kabisa maisha ya watu, wawasafishe watu miguu, kwa njia hii wanaweza kuyagusa matatizo ya watu. Kwa njia hii wanaweza kutengeneza mifumo mizuri ya kubadilisha maadili na kuyapatia sura nzuri. Kwa njia hii wanaweza kufundisha vizuri maisha ya kiroho na hasa uhusiano kati ya mtu na mtu. Kwa kukaa kwenye mikutano na kutoa matamko bila kuyagusa maisha ya watu na kutoa matamko yanayopingana na maisha ya kila siku ya wananchi ni ishara kwamba hawasomi alama za nyakati. Na mtu asiyesoma alama za nyakati daima anabaki nyuma. Mfano ni huu wa kutoa tamko, Serikali ikafumba macho na kusonga mbele. Kwa njia hii mambo mengi yatajitokeza na maamuzi yatapitishwa na tutasonga mbele na kuwaacha Maaskofu wetu umbali mkubwa.

Kwa vile bado tunawahitaji maaskofu wetu, bado tunahitaji uongozi wao, basi ni lazima wasome alama za nyakati na kujitahidi kutembea na jamii. Kama wanavyosema, ni kweli kwamba KONDOMU zipo siku nyingi. Lakini nyakati zinabadilika na mambo mapya yanakuja. Huko nyuma UKIMWI, haukuwepo. KONDOMU, zilitumika kuzuia magonjwa ya zinaa na hasa kusaidia uzazi wa mpango. Leo hii ingawa wengine bado wanazitumia KONDOMU kwa uzazi wa mpango, lakini matumizi ambayo ni muhimu na ya kulinda uhai ni yale ya kuzuia maambukizo ya UKIMWI. Hivyo kuna tofauti, na maaskofu wetu ni lazima walione hili.

Na,
Padri Privatus Karugendo.