MFUMO WA UBEPARI UNA MAADILI MACHAFU

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

MFUMO WA UBEPARI UNA MAADILI MACHAFU.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema Ubepari ni unyama. Wengine walielewa na wengine hawakuelewa kabisa. Lakini hata na wale walioelewa wakati ule, sasa hivi wanajifanya kutoelewa tena. Hakuna anayehoji wala kujadili tena juu ya msamiati huu. Wale ambao ndio wangehoji, sasa hivi wamezama kwenye udaku na kutafuta, maana walichelewa! Hata hivyo ukweli unabaki palepale kwamba ubepari ni unyama, ni mfumo unaojali pesa na si pesa inavyopatikana. Ukiwa na kilabu cha usiku ambacho watu wanatembea uchi kufurahisha wateja hakuna shida maana biashara hiyo inazalisha kodi ya serikali.!

Kwenye mji Fulani wa nchi zilizoendelea na zinazoukumbatia mfumo wa ubepari nilikuta tangazo la ajabu katika mashine ya kuuza sigara. Hii ni mashine ambayo unatakiwa uweke pesa na ikupe pakiti ya sigara. Tangazo linasema hivi: “Sheria zetu zinatukataza kumuuzia sigara mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 16”(tafsiri ni yangu). Mimi kilichoniogopesha si tangazo wala si sigara. Nilishtuka jinsi teknolojia ilivyopanuka. Yaani mashine kuweza kupima umri wa mnunuaji. Nilishangaa na nikaanza kuuliza kwa watu mbalimbali kama teknolojia imefikia kiwango hicho. Wapi? Jamaa wote niliowauliza wameniambia haipimi umri wanachotaka ni pesa. Hata kama una miaka miwili ukiweka pesa unapata pakiti ya sigara. Sijuhi tangazo ni la nini! Zipo mashine nyingi za kuuza vileo vya kila aina na kila kona. Hazipimi umri unatakiwa uweke pesa yako upate kilevi. Lakini tangazo lipo sheria zinakataza umri mdogo kuuziwa kilevi!

Mfumo unaojali pesa bila kujali zitakavyopatikana ni hatari. Hata kama ni kwa kuhatarisha afya za binadamu hakuna ubaya wowote. Leo hii vyakula tunavyokula ni vya ajabu kabisa. Mbegu zinawekwa kemikali za ajabu zinakuzwa kwa siku chache, lengo kuu ni faida kwa mabepari. Kuku ambao nasikia wamejaa Shoprite usidhani ni kuku wale, na ukienda kununua usijisifu kwamba umekula kuku. Kuku wanakuzwa kwa wiki mbili halafu anakuwa mkubwa kuliko kuku wale tuliowazoea wanaoishi maisha ya kujitegemea kwa miaka lukuki. Hao kuku na vyakula vingine vya kijenetiki ndivyo vinawafanya watoto siku hizi kukua kwa kasi ya ajabu na kuzeeka vivyo hivyo. Ingekuwa inaishia kukua tuu tusingejali sana. Ukuaji unaambatana na magonjwa ya kutisha ambayo yanawezesha tena mabepari kupata faida isiyo na kipimo. Faida ya kuuza dawa.

Dawa za magonjwa ya binadamu zina faida ya kubwa sana. Nyingi ya dawa hizo hazitengenezwi kukutibu au angalau kukuwekea kinga ya muda mrefu, zinakujengea utegemezi mbaya sana. Zinakufanya uwe mtumwa wa dawa, zinapunguza kinga ya asili ya mwili taratibu. Unatengenezwa kuwa soko milele. Historia ya utabibu inatuambia kwamba kabla ya chanjo kugunduliwa miaka ya 1700, mwili wa binadamu ulikuwa unaweza kabisa kupambana na magonjwa mbalimbali. Tangu kugunduliwa kwa chanjo, matatizo yamezidi kuwa mengi mno. Miili ya binadamu inafanyiwa majaribio ya dawa hatari za sumu. Lakini nieleweke kwamba hata mabadiliko ya dunia na shughuli za binadamu ambazo pia hazijali athari za mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa duniani zimefanya magonjwa kuongezeka. Sasa hivi magonjwa ya kansa yameongezeka kwa kasi duniani sababu mojawapo ikiwa ni mtindo wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula na unywaji wa vinywaji ambavyo ni hatari kwa miili ya binadamu. Siku za nyuma tatizo la kansa lilikuwa si kubwa sana katika nchi za dunia ya tatu. Sasa hivi limeongezeka kwa kasi sana na tunaambiwa kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 60 ya wagonjwa wa kansa watatoka Afrika. Hali hii inatisha ukiongeza Malaria, Kipindupindu, UKIMWI na magonjwa mengine ya umasikini. Kuna hatari Afrika itakwisha.

Unatakiwa uelewe wazi kwamba kuna dawa zinazotengenezwa kukuza biashara ya kampuni za dawa za nchi za magharibi. Leo hii madaktari, wafamasia na watafiti wengi wa magonjwa wanasomeshwa na kampuni za dawa za nchi za magharibi si kwa lengo la kutafuta suluhisho la matatizo ya binadamu, ni kuja kusaidia kutangaza soko lao la dawa. Hawataki kabisa kusikia utafiti wa dawa mbadala za jadi kwa mfano. Wakisikia watazipinga mpaka mwisho. Watatumia kila mbinu. Watatumia wanasiasa, wataalamu wa fani zote na yeyote anayeweza kutumika kwa masilahi yao na kwa vile nchi za dunia ya tatu zimefungwa kabisa kufikiri basi wataimba na kutukuza dawa za magharibi na kuacha hata kusikiliza chochote kuhusu dawa za asili ambazo nazo zina umuhimu wa kipekee kabisa katika miili yetu.

Leo UKIMWI umekuwa sekta nyeti kweli na dili la nguvu kwa kampuni za dawa za magharibi ndio maana makuhani wa ubepari wanakataa nchi changa zisijiingize katika kutengeneza hizo dawa. Wanajua nchi kama India, Brazili na Uchina ambapo gharama za uzalishaji ni chini wakianza kuzalisha basi bei zitashuka na faida zao zitapungua. Wanalinda kweli zisizalishwe katika nchi hizo. Wanatumia hilo dubwasha lao waliloanzisha linaloitwa Shirika la Biashara Duniani (WTO). Wanatunga sheria kali zenye lengo la kuzizuia nchi nyingine kuzalisha dawa. Kisa? Tunaambiwa ukishaanza kutumia hizo sumu zinazoitwa ARVs utazitumia mpaka mwisho wa safari yako. Sasa watakubali kweli kupoteza soko hilo? Wataalam wengine wanatuambia hizo ni sumu za ajabu zinakausha mwili kabisa.

Rais wa Marekani George Bush siku hizi anajiita mlokole hataki tena watu watumie kondomu. Nchi iliyokuwa ikitoa misaada ya kondomu kwa mamilioni miaka michache iliyopita, sasa Rais wake kageuka kabisa. Katika mkutano wa UKIMWI uliofanyika Thailand mwaka jana (2004) alisema sasa ni wakati wa kuacha zinaa kabisa. Wanaofuatilia siasa na habari za Marekani wanasema hii ilikuwa ni kampeni ya kusaidia kampuni za dawa zilizokuwa zinamsaidia katika kampeni mwaka huo. Anajua kabisa kwamba dini zimekuwa zikihubiri kuacha zinaa tangu zianzishwe lakini wapi, watu bado wanafanya zinaa kama kawaida. Sisemi kwamba watu hawawezi kuacha lakini ukweli ni kwamba si hivyo. Hakuna mahali ambapo hiyo nadharia imefanikiwa hapa duniani. Anajua kabisa watu watafanya ngono bila kondomu wataambukizwa kwa mamilioni, kampuni za dawa zitatengeneza dawa na kuziuza kwetu kwa miaka mingi ijayo. Tutadanganywa na kiini macho cha misaada, viongozi wetu watamshangilia na kumwimbia mapambio. Tutaacha kufanya jitihada zozote zenye lengo la kutafiti dawa zetu za asili tukingoja msaada wa dawa toka nje. Hayo ndiyo maadili ya mfumo wa wataka fedha.

Ile migahawa ambayo sasa inashamiri kwa kasi Jijini Dar-es-Salaam kama vile McDonalds, Nandos, Steers, KFC na mingineyo ambayo tunaaminishwa ni maendeleo ni ya hatari. Vyakula vinavyopikwa humo hasa kuku ndio hao waliokuzwa kwa wiki mbili kwa kutumia vimiminika vya kikemikali ambavyo si salama kwa mwili wa binadamu. Yote haya ni katika kukuza biashara ya mabepari. Haijalishi afya ya mlaji. Pesa kwanza halafu wanajua magonjwa yatakufuata baadaye na utanunua dawa kwao tena. Chakula kinazalisha ugonjwa na ugonjwa utazalisha pesa kwa kuuza dawa,

Biashara ya silaha nayo usiseme. Inaendelea kwa kasi ya ajabu. Mbaya zaidi silaha hizo zinapelekwa nchi zenye matatizo ya kivita ili watu waendelee kuchinjana. Wanakuwa kwanza na ajenda ya kutoa msaada wa kijeshi kwa nchi changa. Watakuambia wanakusaidia kufundisha jeshi lako, na kwa vile tumeshaapa kutofikiri tunakubali haraka bila kuuliza kwa nini tunapewa msaada? Takwimu zinaonyesha kwamba misaada na mauzo ya silaha za kijeshi toka Marekani kuja Afrika kusini mwa jangwa la Sahara imeongezeka kwa kasi sana. Kwa mfano fedha kwa ajili ya msaada wa kijeshi zitaongezeka toka $ milioni 12 mwaka 2000 hadi kufikia $ milioni 24 inayopendekezwa mwaka 2006. Hii ni mara mbili ya kiwango cha mwaka 2000. Misaada hii ni ya kupumbaza Waafrika ili kesho ukiwa na mahitaji ya silaha ukimbilie kwao uzidi kuwaongezea fedha na huku tukizidi kuuana. Wakati tunanichinjana kwa hizo silaha, watakuwa wanakunywa mvinyo na kusherehekea huku wakiiba rasilimali zetu.

Kuna watu wanafikiri kwamba vita nyingi katika nchi za Kiafrika zinashindwa kwisha. Si kweli ni kwamba hawa mabepari wakishagundua kwamba kukiwa na vita kuna faida kuliko amani basi watataka hiyo vita iendelee. Vita itaendelea mpaka pale ambapo itaonekana kwamba hailipi kuendelea kupigana au pale wanapoona kwamba wameshapata kibaraka atakayeshirikiana nao kupora wanachotaka. Haya ndiyo yaliyotokea Angola wakati wa marehemu Jonas Savimbi. Baada ya kuiba almasi za Uhambo akishirikiana na Marekani kwa miaka zaidi ya 20 na kuua Waangola kwa maelfu, wakaamua sasa kumuua kwa vile wizi wa almasi na mafuta ungeweza kuendelea hata Savimbi asipokuwepo. Hawa jamaa ndicho wanachofanya na kwa vile wamegundua nasi tunawaamini sana watakuja na vizawadi kama wanavyotupa sasa hivi ili kuendelea kutumaliza, wakishindwa kutushawishi wanaanzisha vita wakishirikiana na baadhi ya Waafrika wanaokubali kuhadaiwa na vifedha na kuchinja ndugu zao kibao. Wakati mnaendelea kumalizana wanaendelea kupora walichofuata.

Zamani wakati tunasoma historia shule za msingi na sekondari tulifika mahali tukaanza kuwalaumu kina Mangungo wa Msovero na Lobengula wa Mashonaland kwa kukubali kulaghaiwa na Wazungu. Kuna tofauti yoyote na sasa wanavyolaghaiwa viongozi wetu wanaoitwa wasomi kwa lugha za misaada, uwekezaji na misamiati mingine? Ni njia za ulaghai na misamiati tuu imebadilishwa. Misamiati ya kibepari imekuwa tofauti na inaficha ulaghai wa moja kwa moja siku hizi lakini ukiwa na akili zako utagundua hakuna tofauti. Ni kama watu wengine wanavyofikiri kwamba kuna tofauti ya mifumo ya mwanzo ya ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo na kinachoitwa utandawazi sasa. Mambo ni yale yale mbinu ndizo zimebadilika tuu kutokana na maendeleo na hasa teknolojia ya habari na mawasiliano. Ukikumbuka jinsi Kwame Nkrumah alivyouelezea ubeberu basi haitakiwi uyatofautishe hayo mambo. Nkrumah alisema Ubeberu ni kama kinyonga, hubadilika rangi kutokana na mazingira. Suala ni kwamba anaendelea kuwa kinyonga yule yule.

Ni lazima tuwe macho na kujali maadili yetu, tamaduni na taratibu zetu. Tamaduni na mitindo yetu ya maisha ni mizuri tuu, vyakula ndio usiseme, McDonalds unatafuta matatizo ya bure kabisa. Dawa za asili ni kiboko ni kwa vile tumeamua kuziacha na hazitafitiwi lakini angalia Wazungu wanawatuma wanafunzi wao kuja kuzitafiti wanajua watazipora zote na kuzimaliza. Tulinde chetu kidogo kilichobaki, tusiachie kila kitu angalau tubaki na cha kusema hiki ni chetu. Likini tukikalia udaku na kupuuzia kupanua fikira zetu, tutamezwa na kupoteza kila kila kitu.
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment