AFRICARE NA MCHANGO WAKE TANZANIA 5

AFRICARE NA MCHANGO WAKE KATIKA JAMII: TANZANIA.( 5)

Baada ya kuzunguka katika mikoa yote sita, jibu nililolipata, si la ni nani alichagua mikoa, wilaya na vijiji kwa vigezo gani; bali kwa mtizamo binafsi, ni kwamba vijiji vyote vitakavyonufaika na mpango huu wa kusogeza huduma ya umeme vimesheheni madini na rasilimali nyingi. Ardhi ya vijiji hivi ina rutuba na nzuri kwa uwekezaji wa kilimo, uwindaji, utalii na viwanda. Kwa maana hiyo inawezekana Wamarekani wenyewe walipendekeza ni mikoa ipi inufaike na huduma hiyo kwa malengo yao binafsi? Kwa kujua na kutambua faida watakayoipata kutoka kwenye mikoa hiyo pindi ikiwa na huduma ya umeme? Wakapendekeza na serikali yetu ikakubali? Au serikali yetu ilikubali kwa vigezo? Ni vipi hivyo? Nasubiri jibu!

Mfano, wilaya ya Morogoro vijijini, Kata ya Matombo, itanufaika na huduma hii ya umeme. Kata ya Matombo, inajulikana kwa uzalishaji wa matunda na mazao mengine mengi. Inaaminika kwamba msitu wa asili ya Kimboza umesheheni madini ya kila aina. Njia ya kwenda Matombo ni njia ya utalii na kuna uwezekano wa kuipanua njia hii kwa siku za usoni. Je, inawezekana mfuko wa changamoto za milenia unatumika kutengeneza miundombinu ya wawekezaji kutoka Amerika? Wakija kuwekeza wakute umeme? Kwao iwe ni rahisi kuvuta na kuutumia jinsi watakavyo? Ni msaada au ni upole wa njiwa na ujanja wa nyoka?

Dodoma, itanufaika na mradi huu! Sote tunajua kwamba Mkoa huu umesheheni madini muhimu sana. Wilaya ya Mpwapwa tayari ina machimbo yanayoendelea. Inawezekana zoezi zima la kusogeza umeme vijijini ni kuandaa miundombinu ya wawekezaji? Katika vijiji vya Tubugwe na Hogoro, wilaya ya Kongwa, asilimia tisini (90) ya wanavijiji walisema hawana uwezo wa kuuvuta umeme kuingiza kwenye nyumba zao. Mradi wa kuziboresha nyumba zao ungekuwa muhimu zaidi ya umeme. Na wale waliosema wanaweza kuuvuta, hawakuwa na uhakika wa kulipa bili kila mwezi.
Wilaya ya Geita, vijiji vingi vyenye machimbo ya dhahabu vitanufaika na mradi huu. Nyumba nyingi za wananchi hazina ubora wa kuunganisha umeme. Ni wazi huduma hii imewalenga wawekezaji zaidi ya wananchi. Geita, wana shida ya maji- wangepata mradi wa maji watu wengi wangepata huduma hii; Geita wana shida ya barabara; wanawake wajawazito wanapoteza maisha wakiwa njiani kwenda hospitali, usafiri ni shida; wanapanda pikipiki za Mchina ambazo si salama kwa maisha yao. Hoja hapa ni kwamba umeme itakuwa huduma ya wachache ambavyo maji na Ifakara, nao wako katika mpango huu.

Ni wazi nilipofika Ifakara, nilifikiri watu hawa wanaihitaji daraja la Mto Kilombero, zaidi ya umeme! Nina imani wangeshirikishwa, wangechagua daraja badala ya umeme! Mbali na ajali za kivuko zinazotokea mara kwa mara na kupoteza maisha ya watu, inashangaza kuona miaka hamsini baada ya uhuru, Tanzania imeshindwa kujenga daraja la kuiunganisha Ifakara na Mahenge. Upana wa mto pale kivuko kilipo ni mita hamsini au sabini! Kwa nini tushindwe kujenga daraja? Shughuli zinazofanyika kwenye kivuko hicho, mazao yanayovushwa na rasilimali nyingine zinazovuka kutoka Mahenge kwenda Ifakara na kwingineko ni nyingi kiasi cha kuhitaji daraja. Pato la Mahenge na Ifakara katika mfuko wa Taifa, linatosheleza kujenga daraja.

Kilombero, kijiji cha Kidogobasi, watanufaika na mradi huu. Inajulikana jinsi bonde la mto Kilombero lilivyo muhimu kwa kilimo cha miwa, mpunga na mahindi. Kiwanda cha sukari cha Kilombero, kinahitaji uwekezaji zaidi. Inawezekana kwamba Wamarekani wanaandaa miundombinu ya kuwekeza Kilombero siku za usoni? Kama wao ndo walipendekeza mikoa ya kuihudumia, basi watakuwa na lao jambo, kama ni serikali ilipendekeza; tuelelezwe vigezo maana kuma mikoa mingine ya Tanzania imeachwa nyuma kwenye huduma ya umeme na iko nje ya mpango huu wa mfuko wa milenia.

Lushoto na Makete, nao watanufaika na mradi huu. Mtu yeyote anayezifahamu vizuri wilaya hizi, atakubaliana na mimi kwamba hizi ni wilaya zenye maeneo mengi ya uwekezaji; kilimo, madini, makazi na utalii. Uwezekano wa Wamarekani kuwaandalia miundombinu watu wao kuja kuwekeza Tanzania ni mkubwa kuliko msaada wao kwa watu wa Lushoto na Makete.

Ni wazi umeme ni muhimu katika maendeleo, na Tanzania tunahitaji huduma hii; hoja hapa ni kwamba kuna mambo mengine ambayo ni muhimu zaidi, kama daraja, barabara, nyumba bora, kilimo cha uhakika kama vile umwagiliaji. Vijijini uchumi wao unategemea kilimo, bila maji ya uhakika hawawezi kuzalisha kiasi cha kumudu maisha kama kulipa bili za umeme. Kama mfuko wa changamoto za milenia, unakuja kama msaada, basi ungeangalia kwanza njia za kuinua uchumi wa watu wa vijijini ili wawe katika hali na uwezo wa kutumia umeme.

Tulipowahoji wenye uwezo wa kutumia umeme kule vijijini, mbali na mwanga walitaja kufanya biashara ya kucharge simu, kuonyesha video, kusaga nafaka na saloni za nywele. Hawafikirii zaidi ya hapo, hawana mawazo ya viwanda, kutumia umeme kusukuma maji ya kumwagilia katika mashamba yao na mambo mengine ya uzalishaji.


Haiwezekani Wamarekani wakatusaidia sisi bila wao kuwa na malengo yao; ni wapole kama njiwa, lakini wajanja kama nyoka. Wito wangu ni kwamba na sisi tusipokee msaada bila kuwa na malengo yetu; wao wanasogeza umeme kwenye maeneo yenye madini na yenye uwezekano wa kuwekeza kwenye mambo mbali mbali; hawana mpango wa kuanzisha vyanzo vipya vya kuzalisha umeme; basi sisi tuanze mkakati wa kusambaza umeme vijijini na kutoa elimu juu ya matumizi ya umeme sambamba na kuanzisha vyanzo vipya ya kuzalisha umeme. Kwa njia hii Wamarekani watanufaika na sisi tutavuna vya kutosha!

Nimalizie makala hii ndefu kwa kuwashukuru tena AFRICARE kwa mchango wao na kuwahimiza waendelee kutusaidia na hasa kuwawezesha watafiti, waandishi na watu wenye nia njema kuitembelea mikoa mbali mbali na kujifunza mengi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment