NI KUGOMEA SENSA AMA NI KUIGOMEA SERIKALI?
Wakati nasubiri zoezi la sensa kwa hamu kubwa kuna habari kwamba kuna baadhi ya watanzania hawataki kushiriki zoezi hili la sensa. Kuna ambao wanatoa visingizio vya dini, wengine wanatoa masharti ya kushiriki zoezi hili;kwamba wachinjiwe ngamia, na wengine kwamba mijusi ya Tanzania iliyopelekwa ulaya irudishwe ndo wataweza kushiriki zoezi la sensa. Kusema kweli vyote hivi ni visingizio tu na wala havina uhusiano na soezei zima la sensa. Swali la kutaka kujua wakristu, waislamu na wale wa dini za jandi, halina maana yoyote. Huduma zote Tanzania hazitolewi kwa kuangalia imani ya mtu. Hivyo kinachotakiwa ni takwimu ya watu na vitu vingine muhimu katika taifa letu. Na tumeshuhudia nguvu za ziada zikitumiwa na viongozi kufafanua kwa kirefu maana ya sensa na umuhimu wa zoezi hili; na kwa nyakati tofauti tumesikia kwamba hata ikibidi nguvu kubwa itatumika “kuwalazimisha” wanaotaka kugoma, kushiriki zoezi hili.
Swali la kwanza na muhimu linalokuja kichwani ni je huku ni kutaka kugomea sensa au ni yale yale tuliyoyazoea ya kuigomea serikali? Na kama jibu ni ndiyo, ni kwa nini ugonjwa huu wa kugoma unaendelea kusambaa kwa kasi ya kutisha? Awamu ya nne ya utawala wa taifa letu, tumeshuhudia migomo mingi: Migomo ya wanafunzi, mgomo wa madaktari, mgomo wa walimu, mgomo wa daladala kwenye baadhi ya miji, migomo kazini hadi migomo majumbani na sasa mgomo huu wa sensa.
Asilimia kubwa migomo yote iliyotanguliwa imekuwa ikihusishwa na ushawishi wa vyama vya upinzani na hasa hasa chama cha CHADEMA. Si ntoshangaa kama hata na mgomo huu wa kukataa kushiriki kwa zoezi la sensa watabebeshwa CHADEMA. Yawezekana Chadema ina ushawishi mkubwa hivyo?Sitaki kujiweka mbele kukanusha ushawishi mkubwa wa CHADEMA, ila kwa hili la sense haiwezekani likatoka kwa chama hiki ambacho kina viongozi makini; viongozi wanaofahamu umuhimu wa zoezi zima la sensa. Najua kabisa Chadema wangependa kujua Tanzania ina watu wazima wangapi ambao wamefikisha umri wa kupiga kura ili waanze maandalizi ya uchaguzi wa 2015. Chadema wamekuwa kipigia kelele mfumo wa majimbo, ni lazima wanataka kujua idadi ya watu kwa kila jimbo, ila kuona namna ya kuyatenga majimbo haya kufuatana na wingi wa watu. Chadema wana sera ya kutoa elimu bure, nafikiri ni muhimu kwao kufahamu idadi ya watoto wa kwenda shule. Hivyo kuwashawishi watu wasishiriki mchakato wa sense ni kitu kisichowezekana.
Katika hali ya kawaida inashangaza sana watu kukataa kushiriki zoezi hili muhimu. Zoezi hili linafanyika duniani kote, ni muhimu kupanga mipango ya maendeleo ambayo haifungamani na itikadi wala dini. Kufahamu kuna watoto wangapi, ili ifanyike mipango mizuri ya kuwasomesha na kuwahudumia watoto hao, kufahamu tuna wazee wangapi wanaokaribia kustaafu na kuona jinsi ya kuziba mapengo hayo. Kwa kifupi zoezi la sensa linasaidia kufahamu takwimu za kuaminika za taifa. Hivyo mtu yeyote mwenye akili zake timamu hawezi kugomea sensa.
Zoezi hili limefanyika hata huko zama za kale. Tunasikia hata kwenye Biblia: “ Siku zile tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandishe. Kujiandikisha huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kurenio alipokuwa mkuuu wa mkoa wa Siria. Basi wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu kwenye mji wake. Yosefu pia alifanya safari kutoka mji wa Nazareti katika Galilaya. Kwa kuwa likuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethelemu katika mkoa wa Yuda, alikozaliwa Mfalme Daudi. Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito…” (Luka 2:1-5).
Maana yake ni kwamba Yosefu na Maria, wazazi wa Yesu Kristu wa Nazareti, walisafiri kwenda kuhesabiwa. Pamoja na kwamba walikuwa kwenye mikono ya utawala wa kigeni, lakini bado walilazimika kwenda kwenye mji wao,ili wahesabiwe. Katika safari hiyo, ndo akazaliwa Yesu Kirstu. Hata ukiangalia upande wa waislamu, utakuta na wo walikuwa na zoezi hili kuhesabu watu na hadi leo hii duniani kote zoezi linaendelea. Kwa njia hii tunajua idadi ya watu wanaoshi kwenye miji na wale wanaoishi vijijini. Na si hilo tu, zoezi la sensa linafichua mambo mengi yanayokuwa yamejificha kwa kipindi cha miaka 10.
Hivyo hili si zoezi geni na hapa Tanzania zoezi hili limeendeshwa zaidi ya mara mbili na hatukusikia aina yoyote ile ya kugomea zoezi hili. Ndo maana wengi wetu tunashangaa na kujiuliza kama kugoma huku kunalenga sensa yenyewe ama ni ujumbe kwa serikali kwamba kuna mambo hayaendi vizuri? Ni njia( kwa kufikiri na ni mawazo yangu) au uwanja wa wale ambao si walimu, si madaktari, si wafanyakazi wa umma na wala si wanafunzi, kupaaza sauti zao? Maana ukweli ndo huo kwamba hadi leo hii Tanzania haina jukwaa la majadiliano; magazeti yenye msimamo mkali kama vile Mwanahalisi yamefungiwa. Hivyo inawezekana kabisa hawa ndugu zetu wanaoigomea sensa wanataka nao kupata nafasi ya kuigomea serikali?
Nyongeza ya hapo ni swali la pili: Je wanagomea sensa kama wanavyogomea uchaguzi mkuu? Wanaojiandikisha kupiga kura ni wengi. Mfano uchaguzi wa 2010, walijiandikisha milioni 20? Waliojitokeza kupiga kura ni chini ya milioni 10? Wengi wao wakisema “Upige kura usipige kura, matokeo ni yale yale”. Wamesikika wanaosema “ Sensa ina faida gani? Watoto wanaendelea kukaa chini, wanawake wanakufa wakijifungua kwa kushindwa kufika kwenye huduma bora, hakuna nyumba za walimu na mengine mengi…”. Inawezekana kabisa kwamba baadhi hawaoni faida ya sensa kama wasivyoona faida ya kupiga kura.
Ingawa migomo mingi inahusishwa na CHADEMA, kuna dalili zak utosha kuonyesha kwamba kuna kitu kisichokuwa sawa sawa katika utawala wa awamu ya nne katika taifa letu. Mbali na migomo ya mara kwa mara, tunashuhudia imani ya wananchi kwa Jeshi la polisi inapungua, imani ya wananchi kwa Mahakama inapungua na imani ya wananchi kwa Bunge lao inaendelea kupungua kila kukicha. Jeshi la polisi kimekuwa chombo cha kuthibiti wapinzani; kuzuia maandamano ya wapinzani na wakati mwingine kuzuia mikutano ya hadhara ya wapinzani. Baadhi ya viongozi wa polisi wanapostaafu, wanakimbilia chama tawala kugombea nafasi mbali mbali za uongozi kiasi mtu unahoji msimamo wao wakati wakilitumikia Jeshi la Polisi. Mahakama kwa upande mwingine kimekuwa ni chombo serikali kugandamiza haki za wananchi. Tumeshuhudia jinsi mahakama ilivyotumika kuzima mgomo wa madaktari, mgomo wa walimu na labda tutasikia mahakama ikitumika kuzima mgomo wa sensa.
Serikali imeamua kutumia nguvu za ziada, vyombo vya usalama na ulinzi na wakati mwingine kutumia vitisho ili isikilizwe na kuendelea kutawala. Uzoefu unaonyesha kwamba nguvu na mabavu bila ushirikishwaji, majadiliano na kukubaliana, ni jambo ambalo halijawahi kufanikiwa popote duniani na Tanzania hauwezi kuwa tofauti.
Inawezekana kabisa kutumia vitisho kuwarudisha madaktari kazini, lakini hii haina maana kwamba madatari hao watafanya kazi kwa kujituma na kwa moyo wa kizalendo. Inawezekana kuwarudisha walimu wote kazini na kukomesha mgomo, lakini haina maana kwamba walimu hao watafundisha kwa moyo na kuwalea watoto wetu kwa misingi iliyo sahihi. Inawezekana kabisa kuwalazimisha watu shiriki sense, lakini hii aina maana kwamba watanzania hawa watatoa majibu sahihi kwa makarani wa sensa.
Ingekuwa ni busara kabla ya kuwalazimisha madaktari kurudi kazini, kabla ya kuwalazimisha walimu kurudi kazini na kablaya kutumia nguvu nyingi kuwalazimisha watu kushiriki zoezi la sensa ni muhimu kuchunguza tatizo lilipo. Bila kutambua chanzo cha tatizo, hata malaika wa Bwana juu mbinguni hawawezi kutusaidia kupiga hatua ya maendeleo.
Na hili si la CCM, peke kwa vile ndicho chama tawala leo, huu ni ujumbe kwa vyama vyote vinavyojiandaa kuingia madarakani. Bila ushirikishwaji, bila majadiliano na bila kuzingatia maamuzi ya wananchi ambao ndio msingi wa utawala; migomo, maandamano na kususia kupiga kura na sensa ni wimbo usiokuwa na kikomo. Watanzania ni wale wale, haina maana kwamba CCM ikitoka madarakani watazaliwa watanzania wapya, ni wale wale. Bila msingi imara, itakuwa ni kubalisha uongozi, lakini matatizo yetu yatabaki ni yale yale.
0 comments:
Post a Comment