UHAKIKI WA KITABU: MZIZI WA CHUKI 1. Rekodi za Kibibliografia. Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni Mzizi wa Chuki, Kimeandikwa na Novati Rutenge Mchapishaji wa kitabu hiki ni Mwandishi mwenyewe na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987- 467- 01 –6. Kitabu kina kurasa 81 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. Utangulizi Mwezi wa kwanza mwaka huu, Wanyambo wa Karagwe walikuwa na siku ya kuonyesha utamaduni wao pale Nyumba ya Makumbusho. Mimi pia nilishiriki maonyesho hayo, na rafiki yangu alinunulia kitabu cha Mzizi wa Chuki. Sina uhakika kama vitabu hivi vilikuwa vinauzwa pale Nyumba ya Makumbusho au kitabu hiki alikinunua sehemu nyingine na kuniletea. Kwa vile nimejenga utamaduni wa kusoma kila kitabu kinachopita machoni mwangu, nilianza kukisoma kitabu hiki na kukimaliza ndani ya siku moja! Inawezekana kwamba hata mwandisi wa kitabu hiki alikuwa kwenye maonyesho ya Wanyambo, maana naye ni mnyambo wa Karagwe. Bahati mbaya sifahamiani naye, hivyo sikuweza kukutana naye. Nimefanya uchambuzi wa kitabu chake kuendeleza utamaduni niliouanzisha wa uhakiki wa vitabu, kwa lengo la kujaribu kuwashawishi watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu. Lakini pia nimefanya uchambuzi wa kitabu hiki kuendeleza mchango wangu wa maonyesho ya siku ya wanyambo; Kitabu chenyewe kimeandikwa na Mnyambo na kinazungumzia mazingira ya Karagwe. Siku ya utamaduni wa Mnyambo, ilisaidia kutoa utata uliokuwa unaendelea siku nyingi juu ya Kabila hili. Watu walio wengi walifikiri kwamba Wanyambo ni wahaya. Kumbe ukweli ni kwama haya ni makabila mawili tofauti. Kila Kabila lina mila na desturi zake na Kila kabila inajitegemea. Hata mwandishi wa kitabu hiki anajaribu kuonyesha ukweli huu katika hadithi yake. Kuna ukweli kwamba Karagwe, haijazalisha waandishi wengi wa vitabu. Ukiachia mbali vitabu vya kitaaluma kama kile cha Profesa Katoke, cha Karagwe Kingdom, na vile vya Profesa Josephat Rugemalila vya Kamusi ya Kinyambo na sarufi ya kinyambo hakuna vitabu vingi vya hadithi vilivyoandikwa na Wanyambo. Hivyo uhakiki wa kitabu hiki umelenga pia kuwachochea wanyambo kuandika vitabu juu ya utamaduni wao, mila na desturi; na haya yanaweza kuelezewa vizuri katika vitabu vya hadithi. Kabla ya kufanya uhakiki wa kitabu hiki ningependa kuelezea mazingira yanayokizunguka. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Riwaya hii ya Mzizi wa Chuki, iliandikwa miaka mingi ya nyumba wakati mwandishi akiwa kijana. Kwa bahati mbaya hakuweza kuichapisha kwa sababu wakati ule uchapajji wa vitabu ulikuwa mgumu sana. Riwaya imeandikwa enzi za Azimio la Arusha. Hivyo inafunua wazi migongano ya kijamii na kisiasa katika enzi ambazo taifa hili lilikuwa limeamua kujenga ujamaa. Ndwano ambaye ndiye mhusika mkuu, anawakilisha tabaka la watawala ambalo baada ya kuaminiwa na kukabidhiwa madaraka, lilitumbukia katika ufisadi wa kufuja fedha za umma na kuwaharibu watoto wa kike. Wale wenye umri wa kutosha, watakumbuka tabia iliyokuwa imejengeka ya kuandaa blanketi la viongozi wakati wakitembelea mikoani. Msichana mzuri aliandaliwa kumliwaza kiongozi. Mtu aliyepingana na tabia hii ni Marehemu Sokoine, aliyewakemea wale waliokuwa wakimwandalia blanketi. Tena bado tuna viongozi ambao waliaminiwa na Mwalimu, ili waendeleze mapambano ya kujenga Ujamaa katika taifa letu, lakini walikumbwa na kirusi cha tamaa ya mali na kuubadilisha Ujamaa kuwa Ubepari uliopitiliza. Mwandishi anadokeza kwamba ingawa mazingira ya riwaya yake ni ya kipindi kilichopita, lakini yawezekana kuwa ufisadi unaopigiwa kelele sasa hivi ni matunda ya mbegu iliyopandwa na kupaliliwa wakati huo. Tumeshuhudia wenyewe jinsi wale waliokuwa wafuasi wa mwalimu, wakivaa kama mwalimu, wakiongea kama mwalimu; sasa hivi wanavaa suti za Kizungu na kuongea lugha tofauti na ya mwalimu. Lakini pia hivi saa kuna vuguvugu la kutaka kurudisha Azimioa la Arusha. Wale wanaolitamani, ni bora wakafahamu upande mwingine wa shilingi; kwamba hata katika mfumo wa Ujamaa, ufisadi ulipenyeza hadi ukawa Mzizi wa chuki. Mwandishi wa riwaya hii ni wakili wa kujitegemea, aliyezaliwa zaidi kidogo ya nusu karne iliyopita huko Mabira, wilayani Karagwe katika mkoa wa Kagera. Aliwahi kufundisha katika shule za sekondari za Karagwe (KARASECO) NA Kishoju (Balimi), Muleba. Pia amewahi kufanya kazi kama wakili wa serikali na katibu wa Shirika la Madini la Taifa. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. Muhtasari wa Kitabu Riwaya, inaonyesha jinsi Ndwano ambaye ndiye mhusika mkuu, anavyoyatumia vibaya madaraka yake. Fedha za umma, zinamchochea kuoa wanawake wengi na kuwachezea watoto wa kike. Ndwano anakwenda mbali hadi kufanya mapenzi na msichana aliyekuwa mchumba wa kijana wake. “Ndwano aingiapo katika penzi jipya, watu wote hujua. Alipofika nyumbani siku hiyo hakuna aliloona zuri. Wake zake wote walikuwa na makosa. Wanawake wote hawakuwa na adabu…… Ngesho, mke wake alishajiweka tayari kupambana na mume wake ili asimwoe Koku – mtoto wa kike aliyekuwa kipenzi cha mwanawe Magezi” Uk. 3 Itaendelea. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment