TUNAWAHITAJI VIONGOZI AINA YA MAGUFULI.


Siungi mkono kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Magufuli, kwamba watu wa Kigamboni watakaoshindwa kupata nauli ya shilingi mia mbili wapige mbizi. Na baadaye kwenye vyombo vya habari tukamshuhudia “kichaa” mmoja akipiga mbizi kutoka Kigamboni hadi Magogoni. Haikujulikana vizuri kama mtu huyo alifanya hivyo kupinga ongezeko la nauli. Najua na yeye Mheshimiwa Magufuli  alilisema hilo la kupiga mbizi kwa utani, tukichukulia utani wa miaka mingi wa Wazalamo na Wasukuma. Kwamba aombe msamaha, nafiki yeye binafsi atapima na kuona uzito wake. Lakini kwa hoja yake ya msingi ya kupandisha nauli ya kivuko kutoka mia moja hadi mia mbili, niko naye kabisa. Tunawahitaji viongozi aina yake, viongozi wanaofuata sheria na kufanya kazi bila kutanguliza matakwa ya  vyama vyao vya siasa na bila kujitafutia sifa.

Tumeambiwa nauli ya kivuko cha Kigamboni imekuwa shilingi mia moja miaka kumi na minne. Tujiulize sote, leo hii unaweza kununua nini na shilingi mia moja? Hata chapati yenyewe ni shilingi mia mbili. Kilo ya sukari imefikia elfu mbili na mia tano. Mafuta ya taa, petroli na dizeli ndio bei inaendelea kupaa. Kivuko kinakunywa mafuta hayo ambayo bei yake inapaa kila siku, kivuko kinahitaji vipuli na wafanyakazi wanahitaji mishahara, tena mishahara ya kwenda na wakati huu tuliomo. Mapato ya kivuko ni nauli, hivyo bila nauli hiyo kwenda na wakati, haiwezekani kivuko hicho kikafanya kazi kwa ufanisi. Ni wakati wa watanzania kuacha kulalamika na kuangalia hali halisi. Tusipende kuishi kwa kutegemea miujiza.

Magufuli, hapendi porojo wala kuchanganya siasa na utendaji. Akifanya uamuzi, anakutajia kifungu cha sheria na mwaka ambapo sheria hiyo ilitungwa. Yeye ni tofauti na watendaji wengine ambao tumezoea kuwasikia wakisema: “Nimeagizwa na Mheshimiwa Waziri mkuu” au  “ Nimeagizwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa” au “  Hata mheshimiwa Rais anaunga mkono wazo hili”. Watu wa aina hii hawawezi kukutajia kifungu cha sheria, wanasubiri kuagizwa kana kwamba hata wakiagizwa kujiweka kitanzi watatimiza! Sheria zipo ili mambo yaende kwa utaratibu na wala si kwenda kwa kufuata mapenzi ya mtu fulani hata kama mtu huyo ni  Kiongozi mkubwa wa nchi.

Nimeziangalia bei za kivuko. Kama ni mtu kulalamika, labda kwa upande wa magari na guta. Kwa mfano inashangaza Guta, kulipishwa shilingi 1,800 wakati gari dogo linalipa shilingi 1,500. Kwa maana zote, kwa kuzingatia uzito na bei ya kifaa, Guta inakuwa bado chini. Hata kwa hali ya maisha yule wa Guta, huwezi kumlinganisha na mtu mwenye uwezo wa kununua gari. Na mara nyingi unakuta hawa wenye Guta, wanakuwa wamekodisha kusombea mizingo. Hivyo shilingi 1,800 ni nyingi! Waheshimiwa wabunge wetu wa mkoa wa Dar-es-Salaam, wangefanya uchambuzi huo nafikiri wangeeleweka kwa wengi. Lakini kushikia bango la ongezeko la shilingi mia moja, ni kuwazomea tu!

Ninaandika makala hii nikijua kwamba Tanzania leo hii maisha yanaendelea kuwa magumu na mimi nimekuwa kati ya watu wanaopinga  mfumuko wa  bei. Lakini kuna vitu ambavyo ni lazima kukubaliana navyo kufuatana na hali halisi. Tunapima thamani ya fedha zetu kwa kulinganisha na dola; siungi mkono mfumo huu, lakini ndio ukweli uliopo sasa. Shilingi yetu inaendelea kudidimia, kiasi kwamba shilingi mia moja hazina thamani tena. Ndio maana ninakubaliana na Magufuli na wataalamu wake kuhusu nauli ya Kigamboni. Walichokifanya pamoja na kuzingatia mambo mengine mengi wakiongozwa na sheria ni kuangalia hali halisi.

Tatizo la Tanzania tunapenda sana siasa, na tunafanya kosa la kuchanganya siasa na utendaji na hapo ndipo tunakwama. Magufuli alipotangaza  bei ya shilingi mia mbili, wananchi wa Kigamboni, walilalamika. Inaeleweka maana mazoea ni vigumu kuyaacha hivi hivi. Walizoea kulipa mia moja, sasa kuwaambia mia mbili inakuwa nongwa. Walioshangaza zaidi ni wabunge wa CCM wa mkoa wa Dar-es-Salaam, kushikamana kupinga nauli hiyo ya mia mbili. Mambo makubwa ya nchi hii yamekuwa yakijadiliwa kule bungeni, hatuzisikii sauti hizi za Wabunge wa CCM wa Dar-es-Salaam, tunazisikia leo hii nauli inapopanda kutoka mia moja kwenda mia mbili. Wanaogopa wasiosikika wakisema kitu juu ya nauli, wakati wananchi wamekuwa wa kwanza kulalamika, watatoswa 2015.

Muswada wa sheria ya kubadilisha katiba, ulipitishwa kishabiki na wabunge hao hao wa CCM. Hatukusia sauti ya za wabunge wa CCM wa Dar-es-Salaam, wakisimama kidete kutoa maoni yao juu ya sheria hii ambayo wataalamu kama Profesa Shivji, wanasema ni sheria mbaya. Kwa maoni ya wengi, mchakato wa kuipata katiba mpya ni muhimu zaidi ya hiyo shilingi mia wanayoipigia kelele.

Hatujazisikia sauti za waheshimiwa wabunge wa CCM mkoa wa Dar- es-Salaam wakiishinikiza serikali yao kuwashughulikia mafisadi wanaohujumu uchumi wa nchi na kuziweka rasilimali za nchi hii mifukoni mwao. Kwa maoni ya wengi kupambana na ufisadi ni muhimu zaidi ya hiyo shilingi mia wanayoipigia kelele.

Magufuli, amesimama imara na kusema kule jimboni kwake, nauli ya kivuko ni shilingi elfu tatu. Wapiga kura wake, wamchague , wasimchague nauli ndio hiyo. Anasema hivyo bila kuogopa, maana yeye hafanyi kazi kisiasa, anafanya kazi kwa mujibu wa sheria. Anayasimamia yale yatakayoleta manufaa kwa taifa leo na kesho na hata baada ya yeye kuondoka madarakani.

Tunawahitaji viongozi aina ya Magufuli, viongozi wanaoiangalia Tanzania ya leo na kesho. Tunawahitaji wabunge ambao wanaingia bungeni kushiriki kuiweka misingi ya  Tanzania iliyo imara leo na kesho na siku za mbeleni. Wabunge wanaoingia bungeni kujiandalia makazi ya kudumu bungeni hawatufai! Wabunge wanaoshindwa kutetea ukweli na kusimamia sheria kwa woga wa kutoswa kwenye uchaguzi mkuu, hawatufai kabisa!

CCM mkoa wa Dar-es-Salaam imemkalia kooni Magufuli, na jinsi kansa ya kufukuzana ilivyoingia kwenye vyama vyetu vya siasa, haitashangaza kusikia CCM Mkoa wa Dar-es-Salaam, ikipendekeza Magufuli kufukuzwa kutoka kwenye chama cha CCM kwa sababu ya kupandisha nauli ya kivuko cha Kigamboni. Inawezekana, nani alifikiri Hamad Rashid, Mtu ambaye alipanda kufikia kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni angefukuzwa kutoka CUF? Au Kafulila kufukuzwa kutoa NCCR?

Wakati wabunge wa CCM wa Dar-es-Salaam, wanashikia bango nauli ya shilingi mia mbili, mkoa wa Dar-es-Salaam una matatizo kibao ambayo hatujasikia wabunge hao wakiyajadili na kutafuta ufumbuzi. Kuna suala zima la foleni. Kwa maoni ya wengi, foleni ni tatizo kubwa zaidi ya hiyo shilingi mia mbili wanayoipigia kelele. Kuna tatizo la maji, watu wa mkoa wa Dar-es-Salaam, wanatumia fedha nyingi kununua maji. Kwa maoni ya wengi tatizo la maji ni kubwa zaidi ya hiyo shilingi mia mbili wanaoipigia kelele. Kuna tatizo la ardhi na utapeli wa viwanja. Baadhi ya viongozi wamejilimbikizia viwanja na wanaviuza kwa bei ya mabilioni. Kwa maoni ya wengi tatizo la ardhi mkoa wa Dar-es-Salaam ni kubwa zaidi ya  hiyo shilingi mia moja wanayoipigia kelele.

Inashangaza hata Mbunge wa Segerea, anaungana na wabunge wengine wa  CCM Dar-es-Salaam kupigia kelele ongezeko la nauli ya kivuko cha Kigamboni wakati jimboni kwake kuna matatizo kibao. Mbali na tatizo la maji ambalo ni sugu, mafuriko yameharibu miundombinu. Barabara ya Segerea Bonyokwa, imeharibika kiasi wananchi ndio wanachangishana kuitengeneza. Njia ya dala dala ya Tabata-Chang’ombe imefutwa kinyemela. Dala dala  zimeandikwa Chang’ombe lakini zinakwenda Kimanga na Segerea. Watu wa Tabata –Chang’ombe wanapata shida. Kutoka Barakuda hadi Chang’ombe mwisho mtu analipa mia tano hadi elfu moja kwa bajaji na mia tano kwa piki piki. Hatujamsikia mbunge huyu wa Segerea, akiwahurumia wapiga kura wake, kulipa nauli ya elfu moja hadi mia tano, badala yake tumemsikia akiibukia Kigamboni akiwahurumia walioongezewa shilingi mia moja kwenye nauli na kuifanya nauli hiyo kuwa shilingi mia mbili. Ni maajabu ya Musa!

Wabunge wa Dar-es-Salaam, wasitafute umaarufu na kubembeleza kura. Wafanye kazi yao na kujitoa muhanga kama alivyofanya Magufuli, ndipo mambo yataenda. Mfano, wakati wabunge wetu wakipinga kupanda kwa nauli ya Kigamboni, mbona hatujawasikia wakipinga kupanda kwa kodi ya pango ndani ya Jiji la Dar-es-Salaam. Wenye nyumba wanapandisha kodi kila siku ya Mungu, na kuyafanya maisha ya Dar-es-Salaam kuwa machungu. Chumba ambacho zamani mtu aliweza kupanga kwa shilingi kumi na tano hadi ishirini, leo hii ni hamsini hadi sitini. Nyumba ya vyumba vitatu ambayo mtu alikuwa akipanga shilingi laki moja hadi laki na nusu leo hii ni laki tatu hadi laki nne. Mbona wabunge wetu wasipigie kelele juu ya suala hili la pango?

Sikukuu  za Christmas na mwaka mpya bei ya nyama ilipanda kutoka elfu nne kilo moja hadi shilingi elfu saba. Sikusikia wabunge wa CCM wa mkoa wa Dar-es-Salaam, wakipiga kelele kupanda kwa bei ya nyama na kulalamika kwamba wapiga kura wao watashindwa kufurahia sherehe hizi, badala yake wanapigia kelele ongezeko la shilingi mia moja kwenye nauli ya Kigamboni.

Bei ya umeme inaongezeka, ni watanzania wangapi watamudu ongezeko hili? Haya ndiyo tunayotaka kuwasikia wabunge wetu wa CCM Dar-es-Salaam wakiyatetea na  wala si ongezeko la shilingi mia moja kwenye nauli ya Kigamboni.

Kuna tatizo hili la wahanga wa mafuriko. Wanahamishwa kupelekwa Mabwepande. Watoto wao watasomea wapi? Je wao watapata wapi fedha za kujikimu? Wengi wao waliweza kuyaendesha maisha yao kwa kuwa karibu sana na Jiji la Dar-es-Salaam, Jiji lenye mishe mishe na uwezekano wa kupata kazi, biashara na mambo mengine mengi ya kutengeneza fehda. Sasa wanapelekwa mbali na Jiji na sehemu ambayo haijaendelezwa  bado. Hili ni tatizo ambalo tulitegemea waheshimiwa wabunge wetu wa CCM mkoa wa Dar-es-Salaam walisemee kwa nguvu zote. Kwa vile ni serikali imetamka, wanafyata mkia. Hawa hawatufai kama wawakilishi wa watu!

Vyuo vikuu kuna migomo ya kila siku. Wanafunzi wanahitaji mikopo ili waendelee na masomo yao. Tunahitaji kizazi kipya kuliendesha taifa letu. Bila kuwapatia elimu bora tutakuwa tunajimaliza sisi wenyewe. Hivyo tunawategemea waheshimiwa wabunge wetu wa CCM mkoa wa Dar-es-Salaam, kupambana na serikali ili itoe mikopo kwa wanafunzi badala ya wao kushikia bango ongezeko la shilingi mia moja kwenye nauli ya kivuko cha Kigamboni.

Taifa letu liko nyuma kimaendeleo, tunalazimika kukimbia wakati wengine wanatembea. Tunawahitaji watu wa kujitolea kufanya kazi kwa nguvu zao zote; watu wenye uwezo na karama ya kusukuma mambo yakaenda. Mfano kivuko ni lazima kifanye kazi na kuweza kujiendesha na kutengeneza ziada, ili ruzuku ambayo Serikali ingetoa kuendesha kivuko hicho ielekezwe kwenye miradi  mingine ya maendeleo. Hivyo akijitokeza mtu aina ya Magufuli, tumpatie nafasi, tuache utamaduni wa kuingiza siasa kwenye utendaji. Tunawahitaji viongozi aina ya Magufuli, ili taifa letu lipige hatua na kusonga mbele kuelekea maendeleo endelevu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment