WAHAMIAJI HARAMU, TUNA
MPANGO WA KUDUMU?
Tanzania inapakana na
nchi nyingi, hivyo suala la kuwa na wahamiaji haramu si la kushangaza. Na hapa
ni lazima tutofautishe “Uhamiaji haramu” wa kihistoria na ule ulioibuka siku za
hivi karibuni wa watu kutoka nchi za Somalia na Ethiopia wanaopitia Tanzania
wakielekea Afrika ya Kusini kutafuta kazi. Hili ni wimbi jipya, mipango yao
ikikwama wanajikuta wakiishi Tanzania kinyume na sheria. Binafsi nimeandika
sana juu ya suala hili la wahamiaji haramu wa kihistoria na wachambuzi wengine wamelielezea mara kwa
mara, lakini kwa vile kuna dalili za suala hili kutoeleweka vizuri miongoni mwa
watanzania na hasa viongozi wetu kama
vile wabunge ni vyema kulijadili tena na kutafuta njia ya kuwa na mpango wa
kudumu kuhusu suala hili.
Ni muhimu sana kwa
wabunge wetu ambao ndio wawakilishi wa wananchi, ambao ndio wanaotunga sheria
za nchi kuifahamu vizuri historia ya taifa letu, kufahamu vizuri mazingira ya
majimbo yao ya uwakilishi na kuyafahamu vizuri mahitaji ya siku kwa siku ya
wapiga kura wao. Inapotokea mbunge akaonyesha dalili za kutofahamu mahitaji
muhimu ya watu wake, inatia simanzi na
ni hatari kubwa. Kwa mbunge aliye makini, kinachotangulia si chama chake
cha siasa na wala si serikali iliyo madarakani, bali ni wananchi wake
waliomchagua na kumtuma awawakilishe Bungeni.
Ukiachia mbali historia
ya bara letu la Afrika ya mipaka ya nchi zetu kuibuka 1884? Mwalimu Nyerere,
alifungua mipaka ya nchi yetu kwa Waafrika wote. Tanzania, iliwapokea wakimbizi
na wapigania uhuru. Kwa miaka mingi Tanzania, ilikuwa ni kimbilio la wengi na
msamiati huu wa “Wahamiaji haramu” haukujulikana. Kwa njia hii watu wengi wa
nchi jirani walipata uraia wa Tanzania na wengine waliendelea kuishi hivyo
hivyo bila hata kujishughulisha kuomba uraia. Kwa maana nyingine, huko nyuma
hakukuwa na mpango wa kudumu wa kulishughulikia suala la wahamiaji haramu.. au
hakukuwa na umuhimu wa kutengeneza mpango wa kulishughulikia suala hili.
Leo hii tunahitaji mpango
huu wa kudumu. Tunahitaji kuwatambua wahamiaji haramu na kuwatungia sheria na
mpangilio wa kuendelea kuishi hapa Tanzania. Busara si kuwafukuza, maana kuna
wahamiaji haramu wanaoweza kuishi hapa Tanzania kama wawekezaji; wanaweza kutoa
kodi na kuchangia pato la taifa.
Inawezekana kabisa kukaa kwao ndani ya nchi bila kibali, ni makosa yetu kama
taifa kutokuwa na mpango wa kudumu kuhusu suala zima la wahamiaji haramu. Hivyo
badala ya kelele za wabunge juu ya wahamiaji haramu, tunataka kusikia
wakijadili mchakato wa kuanzisha mpango wa kudumu juu ya wahamiaji haramu na
sheria ya kusimamia mpango huu. Hayo ndiyo mambo ya kujadiliwa na wabunge
makini, si kulalamika bali ni kutafuta majibu na kupanga mipango ya kusonga
mbele.
Tanzania, tunaelekea
kusherehekea miaka 50 ya uhuru wetu bila kuwa na vitambulisho vya uraia.
Mchakato wa vitambulisho hivi uko mbioni, lakini hatuwezi kuwa navyo kabla ya
sherehe za miaka 50 ya uhuru wetu. Zoezi hili likianza tunaweza kushuhudia
idadi kubwa ya watu ambao ni wahamiaji haramu. Hata ikitokea hivyo, zoezi zima
liendeshwe kwa misingi ya utu na roho ili aliyoipandikiza Mwalimu Nyerere ya
Umajumui wa Afrika. Watu wasiwekwe ndani, wasinyang’anywe mali zao na
kurudishwa kwa nguvu kwenye nchi zao za asili.
Kama nilivyosema mwanzoni
mwa makala hii, ni kwamba Tanzania inapakana na nchi nyingi, hivyo mikoa mingi
ina tatizo hili la wahamiaji haramu, lakini tatizo hili ni kubwa zaidi katika
Mkoa wa Kagera. Ni vigumu kuelewa ni kwa nini tatizo hili linasikika sana
Kagera, kuliko kwingine. Mfano Mtwara, watu wa Msumbiji wanaingia na kutoka na
wengine wanaishi Tanzania bila kelele za “Uhamiaji haramu”. Arusha ndugu zangu
Wamasai wanaingia Kenya na kurudi Tanzania na kuishi bila kuitambua mipaka ya
nchi hizi mbili, lakini hakuna kelele za “Uhamiaji haramu”. Juzi bungeni suala
la wahamiaji haramu katika mkoa wa Kagera, liliibuka tena. Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Benedict Ole
Nangolo, alionyesha kulifahamu vizuri suala hili na kutoa jibu kwamba suala
hili linahitaji “ Ushirikishwaji mkubwa”.
Jibu la Benedict Ole
Nangolo, linaonyesha umakini mkubwa, ni aina ya wabunge tunaowahitaji
kuliendeleza taifa letu ni aina ya wabunge wanaoguswa na maisha ya wananchi ni
kinyume na mawazo ya viongozi wengine wanaofikiri jibu la tatizo la wahamiaji
haramu ni kuwafukuza na kuwarudisha makwao. Kama nilimwelewa vizuri Mheshimiwa
Benedict Ole Nangolo, ni kwamba suala hili la wahamiaji haramu linahitaji
mpango wa kudumu. Mpango ambao chombo pekee cha kuutengeneza ni Bunge letu
tukufu.
Kwa faida ya msomaji wa
makala hii ni kwamba Mkoa wa Kagera unapakana na nchi tatu. Uganda, Rwanda na
Burundi. Na kuna historia ya miaka mingi ya watu wa nchi hizi kuingiliana, kuwa
na utamaduni unaofanana na lugha zinazofanana. Mipaka ya nchi hizi
haikufanikiwa kuondoa udugu ulioanzishwa na mababu zetu. Nakumbuka kuandika
makala Fulani nikisema kwamba mwenyeji wa Mkoa wa Kagera ambaye hana chimbuko
Rwanda, Burundi au Uganda si mzaliwa wa mkoa huo! Kwa hiyo mbali na wakimbizi
kuna wahamiaji wa aina nyingi mkoani Kagera, kuna wale wanaovuka mpaka kuja
kusalimia ndugu na jamaa na wakinogewa wanahamia, kuna wakimbizi wa kisiasa na
wakimbizi wa njaa wanaovuka mpaka kutafuta ardhi yenye rutuba lakini wanao
lalamikiwa sana ni wale wahamiaji wafugaji. Hata juzi bungeni Mbunge wa
Karagwe, alikuwa akiwalalamikia wahamiaji haramu wafugaji.
Hawa wahamiaji haramu
wafugaji wanajulikana kama Wahima. Ni wafugaji kama vile Wamasai na wasukuma.
Wanahama kutoka sehemu moja hadi nyingine kutafuta malisho ya mifugo. Wahima,
kama walivyo Wamasai hawatambui mipaka ya nchi, kwao mifugo ni muhimu zaidi ya
kila kitu. Mifugo ni muhimu kuliko mipaka ya nchi na kuliko vitambulisho vya
uraia. Na kawaida hawana utamaduni wa kumiliki ardhi, wao wanatafuta malisho ya
mifugo. Daima wanahama kutafuta maeneo mazuri ya kulisha mifugo yao. Magonjwa
yakishambulia mifugo yao ikafa, ni lazima wahame kwenye maeneo hayo. Hawajengi
nyumba za kudumu, na kwa maana hiyo hawana makazi ya kudumu!
Wahima, ni kabila ambalo
limeishi miaka mingi katika maeneo ya maziwa makuu. Wamekuwa wakihama kutoka
eneo moja hadi jingine wakitafuta malisho ya mifugo yao. Mipaka ya wakoloni ndo
iliwatenganisha Wahima wa Burundi, Wahima wa Rwanda, Wahima wa Uganda na Wahima
wa Tanzania. Hata hivyo Wahima hawa wamekuwa wakivuka mipaka ya nchi hizi bila
kujali vitambulisho wakiwa katika harakati zao za kutafuta malisho.
Kwa maana hii basi,
Wahima wamekuwa wakitoka Uganda, Rwanda na Burundi na kuja Tanzania kutafuta
malisho ya mifugo yao. Lakini kuna wahima ambao wamekuwa wakiishi Tanzania
miaka yote. Wanazunguka wilaya za Mkoa wa Kagera, bila kuvuka mipaka ya nchi.
Mkoa wa Kagera unazalisha maziwa mengi na nyama kutokana na wafugaji hawa
wahima.
Tanzania ilipoingiliwa
na kirusi cha “wahamiaji haramu”, wahima wote bila kujali wale ambao ni
watanzania, wamekuwa wakisumbuliwa. Wanakamatwa na kuwekwa ndani,
wananyang’anywa mifugo yao na wakati mwingine wanasombwa na kupelekwa Rwanda.
Kwa vile hadi leo hii hatuna vitambulisho vya uraia, mkoani Kagera, sura za
watu zimekuwa zikitumika kama vitambulisho!
Kwa sura wahima
wanafanana na Watutsi. Bila vitambulisho na mpango wa kudumu juu ya wahamiaji
haramu, wahima wote watachukuliwa kuwa ni wahamiaji haramu. Wilaya ya Karagwe,
ambayo ina wahima wengi, imekuwa ikitajwa kuongoza kwa kuwa na “Wahamiaji
haramu”. Ukweli ni kwamba baadhi ya “Wahamiaji haramu” hawa ni wahima na
kufuatana na mipaka ya kikoloni ya 1884? Hawa ni watanzania!
Hawa wahima wa Karagwe,
wamesumbuliwa sana. Baadhi yao wamefungwa mara nyingi na kutozwa “hongo” ya
ng’ombe. Kwa kutotaka usumbufu, wahima hawa wamekuwa wakitoa ng’ombe na fedha
kwa viongozi wa serikali na wafanyakazi wa Uhamiaji ili wasikamatwe na
kupelekwa Rwanda. Hata hivyo kuna baadhi waliokumbwa na zoezi hili la kupelekwa
Rwanda. Walinyang’anywa mifugo yao, kwa maneno mengine walinyang’anywa maisha
yao na kupelekwa ugenini Rwanda.
Serikali ya Rwanda,
inalitambua tatizo hili la Wahima, na inaamini suluhu si kuwasomba wahima na
kuwapeleka Rwanda, bali ni kutunga sera na sheria juu ya watu hawa wafugaji.
Wanavyohama hama wakiwa Tanzania, ndivyo watakavyo hama hama wakiwa Rwanda,
Burundi au Uganda. Jibu si kuwasomba na kuwapeleka Rwanda nchi inayodhaniwa
kuwa ni asili yao, bali ni kuwajengea watu hawa mazingira ya kuishi na
kuendesha ufugaji wa kisasa. Kwa vile maisha yao ni mifugo kuna hitaji la
kuhakikisha wanaendeleza maisha yao hayo kwa njia za kisasa bila kuvunja sheria
za nchi husika. Rwanda, imeanza kuwafundisha wafugaji kwamba kufuga si lazima
kuwa na mifugo wengi kiasi cha kulazimika kuhama hama kutafuta malisho, bali ni
kuwa na mifugo kiasi na kuitunza vizuri. Mapato yanayotokana na mifugo michache
iliyotunzwa vizuri ni makubwa kulinganisha na mifugo mingi isiyotunzwa vizuri.
Hili linaweza kuwashawishi wafugaji kuachana na utamaduni wa kuhama hama
kutafuta malisho.
Kuna haja kubwa ya kuwa
na mpango wa kudumu juu ya jamii hii ya Wahima. Kama ilivyo muhimu pia kuwa na
mpango wa kudumu juu ya Wamasai wa Kenya na Tanzania na wasukuma wanaohama
kutoka mkoa moja hadi mwingine wakitafuta malisho ya mifugo yao kiasi cha kuvuka
hata mipaka ya nchi. Kule Sumbawanga, kuna habari kwamba wasukuma wameanza
kuvuka na kuingia nchi jirani.
Nchi za Rwanda, Burundi,
Uganda na Tanzania, zikae pamoja na kutunga sheria ya Wahima. Watu hawa
waruhusiwe kuzunguka popote kwenye nchi hizi, mradi wasivunje sheria za nchi
husika. Watu hawa wajulikane, wapatiwe vitambulisho maalum na kuruhusiwa
kuendelea na maisha yao ya ufugaji. Tunapoelekea kwenye ushirikiano wa Jumuiya
ya nchi za Afrika ya Mashariki, jambo hili la kuwatambua wahima kama jamii ya
watu wanaohama hama kutafuta malisho ya mifugo yao ni muhimu sana. Kuendelea
kuwachukulia wahima kuwa ni wahamiaji haramu ni kuwakosea haki yao ya msingi.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment