BURIANI PADRI DESIDERY KASHANGAKI 1911 – 2011.

Tarehe 26.10.2011, padri Desidery Kashangaki, aliaga dunia na kuzikwa Rubya-Bukoba tarehe 28.10.2011 akiwa na umri wa miaka miamoja na miezi mitano! Mungu amlaze mahali pema peponi.

Kuna mambo mengi ya kuandika juu ya padri huyu mzalendo, maana miaka 100 si haba. Ni watu wachache wanaobahatika kufikisha umri huu. Jambo la kwanza juu ya padri huyu ni kwamba yeye ndiye padri wa kwanza wa Bukoba kufikisha umri wa miaka miamoja. Pili ni kwamba padri huyu alilitumikia kanisa na taifa la Tanzania kwa kipindi  cha miaka sitini (60). Mbali na kazi zake za kiroho, yeye alikuwa mwalimu wa chuo cha walimu cha Butimba Mwanza. Alifundisha pale muda mrefu na kwa njia hiyo amewafundisha walimu wengi hapa Tanzania. Kwa Tanzia hii basi wanafunzi wake popote walipo wapate habari kwamba mwalimu wao hatunaye tena duniani.

Tatu, ni padri aliyependa elimu. Mbali na masomo yake ya theolojia, alisoma digrii ya Elimu ya watu wazima Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, akiwa na umri wa miaka 60. Kupenda kwake kusoma kulimfanya abaki kijana muda wote. Ingawa alikuwa mtu mzima wa miaka 100, maongezi yake na uelewa wa mambo ulikuwa ni kama wa kijana mdogo. Nilipomtembelea mwezi wa tano mwaka huu wakati alipofikisha miaka 100, nilishangaa sana kuona anavyofahamu dunia inavyokwenda. Alikuwa na redio yake ndogo, akisikiliza habari za dunia.
Nne, alikuwa mshauri wa kiroho wa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hata masomo yake ya chuo kikuu cha Dar-es-Salaam, alilipiwa na Mwalimu.

Tano , ni mtu aliyekuwa amejaliwa afya ya pekee. Hakuwai kuugua katika maisha yake yote. Anakumbuka kudungwa sindano mwaka wa 1935 kule Katigondo Uganda. Hakukumbuka ulikuwa ni ugonjwa gani. Lakini baada ya hapo yeye hakujua malaria au magonjwa mengine kama shinikizo la damu, kisukari na mengine. Daima aliuliza dalili za malaria. Hata kifo chake hakikutokana na ugonjwa, tarehe yake ilifika tu akaitika kwa Muumba wake.

Sita, alikuwa mtanashati, mtu wa majivuno, mwenye kiburi cha elimu, lakini mwenye kuipenda na kuiheshimu kazi yake ya upadri. Majivuno yake na kiburi havikuigusa roho yake ya wema, ucheshi na kuwapenda watu. Alipenda sana lugha ya mafumbo, na maisha kwake lilikuwa ni fumbo la imani. Aliwachukia watu waliotumia lugha ya wazi na kuyachukulia maisha kuwa ni kitu cha wazi. Alisisitiza umuhimu wa kuyafumba mambo na kuyafumba maisha! Alitaka kuishi kwa staha, alikula kwa staha na kunywa kwa staha, asingeweza kunywa bia zaidi ya mbili na chakula kama hakuna uma na kisu, basi hawezi kula!

Saba, na labda hii ndiyo sehemu mbaya na ngumu sana katika maisha yake; aliadhibiwa na Askofu wake, akiwa na umri wa miaka  80. Inashangaza na kusikitisha, lakini ndio ukweli wenyewe. Askofu wake hakuweza kumsamehe kwa zaidi ya miaka 20, hadi juzi siku mbili kabla ya kifo chake. Maana yake ni kwamba Askofu, kiongozi wa kiroho, alitunza hasira moyoni mwake zaidi ya miaka 20. Swali la kujiuliza ni je, kama Askofu hawezi kusamehe, Wakristu wengine watafanya namna gani? Je hii ndiyo imani ya Yesu wa Nazareti, aliyetwambia tusamehe saba mara sabini; na kwamba mtu akikupiga shafu la kushoto umgeuzie na la kulia? Ni imani ya Mungu wetu wa upendo na huruma?

Chanzo za adhabu yake ni nini? Padri Desidery Kashangaki, alipostaafu kazi ya kufundisha Chuo cha Ualimu na kurudi nyumbani kwao Bukoba, akiwa na umri mkubwa, maisha ya Parokiani yalikuwa magumu. Posho aliyokuwa akiipata akiwa mwalimu hakuipata kule parokiani. Alianza kufuatilia na kuuliza juu ya maisha ya mapadri wanaoishi parokiani na hasa mapadri wazee kama yeye. Baadaye aligundua kwamba Roma kila mwaka inatuma pensheni ya mapadri waliofikisha miaka 60. Yeye alikuwa na miaka 80, bila kupata pensheni. Ina maana pensheni yake ya miaka 20 ilikuwa inaingia mfuko gani? Alianza mchakato wa kudai pensheni yake kwa Askofu wake. Hiki ndicho chanzo cha magomvi yake na Askofu wake, Askofu Nestory Timanywa, wa Jimbo Katoliki la Bukoba.

Magomvi ya Padri Desidery Kashangaki na Askofu Timanywa, yalikuwa makubwa kiasi cha Askofu kuomba msaada wa polisi ili kumwondoa Padri Kashangaki kwenye nyumba za kanisa. Adhabu yake ilikuwa kwenda kuishi nyumbani kwao alikozaliwa. Mtu mwenye miaka 80, na amelitumikia kanisa miaka 60, tukio hilo la kumfukuza kwenye nyumba za kanisa halikuwa la kawaida. Iliwashangaza watu wengi, hata kama Padri Desidery Kashangaki, alitumia kiburi na majivuno kudai pensheni yake, umri wake na miaka aliyolitumikia kanisa ilitosha kumchukulia alivyo, kuliko kumfukuza na kumtupa mitaani.

Watu wengi walijitokeza kumwombea msamaha Padri Desidery Kashangaki kwa Askofu wake, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba. Askofu hakutaka kusikia wala kupatanishwa na padri wake. Alikuwa na hasira kubwa ambayo iliibua hata makosa ambayo Padri Desidery Kashangaki, aliyatenda akiwa kijana wa miaka 40.

Bahati nzuri, Askofu wa jimbo la jirani la Rulenge, wakati huo, siku hizi linaitwa Rulenge-Ngara, Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, alimwonea huruma Padri Kashangaki na kumkaribisha jimboni kwake. Hivyo Padri Kashangaki, aliishi kama “Mkimbizi” kwenye jimbo la Rulenge. Waswahili wanasema Ng’ombe wa masikini hazai…. Mwaka 1996, Askofu Mwoleka, alistaafu. Roma ilimteua Askofu mwingine, Mheshimiwa sana Askofu Severine NiweMugizi, ambaye kwake maisha ni sheria. Hakuna hekima, busara wala utu – sheria ni msumeno. Ni lazima kufuata sheria. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba hata yeye mwenyewe anashindwa kuzifuata baadhi ya sheria, lakini anataka wengine wazifuate sheria. Aliposhika utawala wa Jimbo Katoliki la Rulenge, alimfukuzia mbali Padri Desidery Kashangaki, maana hakuwa Jimboni Rulenge Kisheria. Askofu Mwoleka alimpokea Padri Kashangaki, kiubinadamu maana alikuwa mkimbizi. Kumtakisha mkimbizi hati ya kusafiria, ni uwendawazimu. Ingawa Padri Kashangaki, alifukuzwa na Askofu wake, mtu aliyefanya dhambi kubwa ni yule aliyemfukuza mara ya pili; aliyemfukuza mkimbizi. Hata sheria za Kimataifa, ukiachia mbali hekima na busara, zinazuia kumfukuza mkimbizi. Hivyo Padri Desidery Kashangaki, alihama kutoka nyumba za kanisa la Jimbo Katoliki la Rulenge na kuishi mitaani. Aliishi maisha magumu. Watu wengi Wakristu kwa Waislamu walijitokeza kumsaidia na hasa wanafunzi wake. Hata hivyo kipindi kilikuwa ni kirefu kiasi cha wale waliokuwa wakimsaidia kuanza kuchoka.

Miaka ya mwisho ya maisha yake, kwa kushirikiana na mapadri waliokuwa na roho ya utu, walimsaidia “kuitekea nyara” parokia ya Bugene Karagwe na kuishi pale. Lengo lake na matumaini yake ilikuwa ni kurudi kwao Bukoba kudai pensheni yake. Nilipomtembelea mwezi wa tano mwaka huu, aliniambia kwamba atakwenda Bukoba kudai pensheni yake. Bahati mbaya mauti yamemkuta kabla ya kulipwa pensheni yake. La kumshukuru Mungu, ni kwamba amezikwa nyumbani kwao Bukoba, kama alivyokuwa akitamani. Mungu, amlaze mahali pema peponi rafiki yetu, ndugu yetu na Mtanzania mwenzetu padri Desidery Kashangaki.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment