E, KILA KERO WANANCHI WAKIAMUA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI MWAO NANI ATAKUWA SALAMA?

Tumezoea kushuhudia vibaka wakichomwa moto; hili ni jambo linaloendelea na tunaelekea kulikubali katika utamaduni wetu! Ni utamaduni wa kutisha maana tutafika mahali kila kero wananchi wanajichukulia sheria mkononi kama ilivyosikika juzi Jijini Dar-es-Salaam vijana wakitishia kuviweka moto vituo vya mafuta kwa kitendo cha vituo hivyo kusitisha huduma hiyo ili kuishinikiza serikali kubadilisha bei ya mafuta. Vituo vya mafuta vilijichukulia sheria mkononi (Mgomo), na vijana walitaka kujichukulia sheria mkononi (Kuvichoma vituo vya mafuta), ni hatari!

Zamani, wengine watahoji zamani ya lini? Sina maana zamani ya mwaka 2000, kwa wengine ni zamani!, Sina maana zamani ya miaka ya tisini au thamanini katikati, ninamaanisha zamani ya miaka ya 50,60,70 na 80 mwanzoni, kulikuwepo na wahalifu wa aina mbali mbali: majambazi, wezi, vibaka, wahaini nk. Walikamatwa, walifikishwa polisi, polisi  walifanya kazi yao kwa uaminifu na uzalendo na wahalifu walifikishwa mahakamani na sheria ilichukua mkondo wake kwa msingi wa haki. Wahalifu walipatiwa haki yao ya kikatiba ya kusikilizwa na kujitetea. Mwamwindi, alinyongwa baada ya kesi yake kusikilizwa kwa muda wa kutosha na baada ya jitihada za serikali za kuhakikisha  kama Mwamwindi, alikuwa na akili timamu wakati wa kitendo cha mauaji aliyoyafanya ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa  Iringa. Baada ya mauaji hayo ya kwanza na ya aina yake hapa Tanzania, ya kiongozi wa ngazi  ya juu katika serikali, Mwamwindi, alijisalimisha mwenyewe na kuubeba kwenye gari mwili wa marehemu hadi kwenye kituo cha polisi. Polisi, hawakujichukulia sheria mkononi, kwa kumpiga risasi Mwamwindi, hapohapo. Alikuwa amefanya kosa kubwa la mauaji ya kiongozi wa serikali. Aliwekwa ndani na kesi yake iliendelea na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Hakukuwepo na siri hadi kila mtu aliamini kwamba haki ilitendeka!

Wale waliotaka kuipindua serikali ya  Kambarage, na njama zao kugundulika dakika za mwisho, kesi yao iliendelea kwa miaka mingi na kutaganzwa kwenye vyombo vya habari. Karibu wahaini wote waliachiwa huru.

 Zamani hizo wahalifu waliopatikana na makosa, walipatiwa adhabu ya vifungo. Baadhi yao kifungo ilikuwa ni nafasi ya ukarabati, elimu na toba. Wengi walijifunza mambo mbali mbali kama ufundi, kilimo, ufugaji na lugha mbali mbali. Baada ya kifungo majambazi, wezi na vibaka waligeuka na kuwa raia wema na kuendelea kutoka mchango wao katika kulijenga taifa letu la Tanzania.

Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba zamani kila raia alikuwa na haki sawa mbele ya sheria kama inavyosema katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania:
Ibara 13(1) “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
         13(3) “ Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamriwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa  sheria.”
         13(6) “Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria, mamlaka ya nchi itaweka taratibu zinazofaa  au zinazozingatia misingi kwamba :-
             (6) a) “ Wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo kinginecho kinachohusika;
              (6) d) “ Kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli nyinginezo ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu;
                (6) e) “ Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.”

Leo hii majambazi, wezi na vibaka wanahukumiwa kifo bila kufikishwa polisi au mahakamani. Wananchi wenye hasira wanajichukulia sheria mkononi. Mtu asiyekupenda, mwenye chuki binafsi nawe, akikunyoshea kidole na kusema wewe ni mwizi, katikati ya jiji la Dar-es-Salaam, Mwanza au miji mingineyo ya hapa nchini, atakuwa anakutakia kifo; utavikwa tairi shingoni, utamwagiwa petroli na kuchomwa moto! Matukio kama haya ni mengi kiasi cha mtu kuwa na maswali mengi juu ya umuhimu wa kuwa na katiba. Watu, ambao wengi wao ni vijana wa kulijenga taifa hili wanapoteza maisha yao kwa kukwapua saa, mikufu ya dhahabu, pesa, simu nk.

Hakuna mtu anayeunga mkono matendo ya ujambazi, vibaka na wezi. Haya ni matendo yanayovunja amani na utulivu katika jamii. Jambo  muhimu la kujiuliza ni je, jambazi, kibaka au mwizi hana haki ya kujieleza mbele ya sheria kama inavyotajwa kwenye katiba ya nchi yetu? Je, jamii yetu haina la kujifunza kutokana na matendo haya? Je, jamii haina la kuwafundisha na kuwakarabati majambazi, vibaka na wezi? Je, jambo la msingi ni kuwaua watu hawa au ni kutafuta chanzo cha matendo yao kiovu na kutafuta mbinu za kuyaponya? Vibaka na majambazi wana mangapi ya kuilaumu na kuishutumu jamii yetu? Wana kero ngapi ndani ya roho zao? Ni mangapi yamewazunguka na kuwalazimisha kutenda yale ambayo wasingependa kuyatenda? Je, wanaiba ili kuwapeleka watoto shule? Wanaiba ili kupata pesa za kulipia matibabu? Wanaiba ili kupata pesa za kununua viwanja na kujenga nyumba za kuishi? wanaiba ili wanunue nguo, chakula na kuishi maisha bora? Je, wanaiba ili watoe sadaka na zaka kwenye dini zao - maana pesa zafanana, ziwe za wizi au zile zilizopatikana kwa njia za halali – viongozi wa dini wanapokea tu bila kuhoji – kwao la msingi ni pesa! Wanaiba kwa vile hawana kazi? Au wanaiba kwa vile karibu watanzania wote ni wezi – kama si majambazi wa kuvamia, basi wanaiba na kupora mali ya taifa! Je, bila ya kuwapatia majambazi, vibaka na wezi nafasi ya kuwasikiliza tunawezaje kugundua chanzo? Mbona kadri majambazi, vibaka na wezi wanavyouawa na wananchi wenye hasira ndivyo ujambazi na matendo mengine ya uovu yanavyoongezeka kwa kasi ya kutisha? Je, si kweli kwamba majambazi, vibaka na wezi wanakuwa na watu wengi nyuma yao? Je, si ukweli kwamba matendo haya ya uovu yanaongozwa na vigogo? Vigogo hawa, si wanaendelea kuishi na kuyafurahia maisha wakati watu wanyonge wanakamatwa na kuchomwa moto?

Je, kama uchumi wa nchi unakuwa mikononi mwa watu wachache, tunawezaje kuthibiti ujambazi? Wananchi wanasema majambazi, vibaka na wezi ni kero kubwa katika jamii ya leo. Tofauti na zamani ambapo vibaka na majambazi walikuwa wanashughulikiwa na sheria, siku hizi  wakikamatwa baada ya siku mbili au tatu wanakuwa tena mitaani wakienelea na vitendo vyao viovu. Rushwa na hongo inatumika kuwaachia. Hivyo wananchi wanaona njia pekee ya kumaliza kero hii ni kifo. Serikali yetu inayaona haya yakitendeka, badala ya kuyakemea na kuielimisha jamii juu ya kuifuata katiba, utawala wa kisheria, elimu ya uraia na kuheshimu haki za binadamu, inashikwa na kigugumizi. Viongozi wetu kama vile waheshimiwa wabunge wanaogopa kuwakemea wananchi wanaojichukulia sheria mkononi ili wasinyimwe kura. Wanatanguliza maslahi binafsi, bila kutanguliza maslahi na heshima ya taifa letu.

Jambo tunalolisahau wote ni kwamba Tanzania, kuna kero nyingi. Je, kila kero wananchi wakiamua kujichukulia sheria mkononi mwao, ni nani atakuwa salama? Waheshimiwa Wabunge hawatakuwa salama, viongozi wa serikali hawatakuwa salama, viongozi wa kidini hawatakuwa salama, matajiri hawatakuwa salama na sisi sote hatutakuwa salama! Mifano ni mingi. Rwanda, Maaskofu walichinjwa, mapadre, masista, viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa serikali, matajiri na kila mnyarwanda hawakupona. Ni hatari wananchi wakiamua kujichukulia sheria mkononi. Ni bora kuthibiti mapema hali hii inapojitokeza katika jamii.

Msemo wa Waswahili wa: “ Usipoziba ufa utajenga ukuta” utufikirishe. Ilianza kero ya vibaka. Wananchi walichoka na kuamua kujichulia sheria mkononi. Sasa hivi imekuwa ni desturi ambayo ni kazi ngumu kuizuia! Akikamatwa kibaka anavikwa tairi shingoni, anamwagiwa petroli na kuchomwa moto! Ikafuata kero ya majambazi. Wananchi walichoka na kuamua kujichukulia sheria mkononi. Ukisikiliza taarifa ya habari, utasikia jinsi wananchi wanavyowazingira majambazi na kuwaua. Baada ya hapo utasikia pongezi za polisi! Ni muhimu kufuata sheria, kuongozwa na katiba na kuheshimu haki za binadamu, vinginevyo ni hatari kubwa!
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment