MAKAMANDOO WA CHADEMA, ADEN RAGE NA BASTOLA

Wakati Katibu Mkuu wa CCM, Wilson  Mukama, akikituhumu chama cha CHADEMA, kuingiza makomandoo zaidi ya 30 wilayani Igunga, Gazeti la Mwananchi, Ijumaa Septemba 23 2011, limetoa picha ya Mheshimiwa  Ismail Aden Rage,mbunge wa Tabora Mjini akiwa na bastola kiunoni akihutubia mkutano wa kampeni kule Igunga.

Mukama, anasema CCM, haijaingiza makomandoo Igunga, kwamba wao wanafanya kampeni za kistaarabu. Kampeni ambazo mheshimiwa Mbunge, anapanda jukwaani akiwa na bastola kiunoni? Huo ndio ustaarabu? Kama mheshimiwa Mbunge, amebeba Bastola kiunoni, vijana wa CCM watakuwa wamebeba nini? Mizinga au mabomu ya mkononi?

Mukama anawafananisha CHADEMA na utawala wa Gaddafi; lakini ukweli ni kwamba CCM ndo ilikuwa kipenzi cha Gaddafi, kiasi kwamba Waziri Membe, alisimama kidete kuutetea utawala wa Gaddafi kiasi cha kumlazimisha Balozi wa Libya, kuishusha bendera ya waasi. Na tujuavyo Gaddafi, alikuwa akitembea na Bastola kiunoni kama alivyofanya Mheshimiwa Aden Rage. Kwa maneno mengine wa kufananishwa na Gaddafi si CHADEMA bali ni CCM.

Kwa mtu mwenye akili timamu hakuna haja ya kuwasubiri CHADEMA kulalamika kwamba makada wa CCM wamejiandaa kupambana kufa na kupona kulikomboa jimbo la Igunga. CCM, wakilalamikia Makomandoo wa CHADEMA, inaeleweka, maana hadi ninapoandika makala hii hakuna kamera yoyote ile, hata za CCM iliyowanasa makomandoo hawa, kiasi cha kumshawishi kila Mtanzania kwamba CHADEMA wamewaandaa Makomandoo.

Nitashangaa sana kama watanzania hawatasimama na kuhoji Mheshimiwa Mbunge kubeba bastola kiunoni. Ismail Aden Rage si mwanajeshi, si polisi; kwa nafasi yake kama ni ulinzi wa usalama wa maisha yake, basi bastola hiyo ingekuwa imebebwa na mlinzi wake, na wala si yeye binafsi. Sote tunajua hatari ya waheshimiwa kubeba silaha za kujilinda wenyewe. Tukio la Mheshimiwa Ditopile, lingekuwa fundisho kubwa. Kama silaha ya mheshimiwa Ditopile ingekuwa imebebwa na mlizi kwake, kilichotokea pale kisingetokea. Mlinzi angeliitumia silaha ile pale ambapo uhai wa Mheshimiwa ungekuwa hatarini. Tujuavyo Ditopile hakuwa kwenye hatari yoyote; kwa vile alikuwa na silaha, maamuzi yalikuwa ni hasira na haraka hadi kuyakatisha maisha ya kijana mdogo. Mheshimiwa kufikia hatua ya kubeba silaha ya kujilinda yeye mwenyewe, maana yake ni kwamba hali ni mbaya na ni hali ya hatari.
Kama mtu unajua wananchi wanakipenda chama chako na unajua ukisema watakusikiliza, ina maana gani kupanda Jukwaani na silaha? Kujilinda na adui gani? CHADEMA? Watapita wapi kama wananchi wanakupenda? Kama si vitisho kwa wananchi ambao hawakuzoea kuona silaha kama hizo? Tumeshuhudia picha za polisi waliojiandaa kivita wakiwa kwenye mji wa Igunga, sasa tunaanza kushuhudia na waheshimiwa wakiwa wamebeba silaha majukwaani. Wananchi wataweza kupiga kura kwa amani na utulivu? Huku si kuwatisha na kuwalazimisha kuchagua wasiyemtaka?

Kama kamera ya waandishi wa habari ingemnasa Mbunge wa vyama vya upinzani akiwa na silaha kwenye jukwaa, ni wazi hata Tume ya uchaguzi ingelikemea kwa nguvu zote kitendo hicho na hatua za haraka za kumwajibisha mbunge husika zingechukuliwa haraka iwezekanavyo.

Sasa Ismail Aden Rage, ni mbunge wa CCM chama tawala, chama kikongwe, chama chenye sera safi, hakuna wa kumgusa. Anabeba silaha kiunoni na kupanda jukwaani kuwahutubia wananchi; anawaomba kura kwa maneno matamu ya Utulivu na Amani. Kuna utulivu na amani kwa mtu anayebeba bastola kiunoni?

Tanzania ni nchi ya kijeshi? Kiasi kwamba Mbunge abebe bastola kiunoni? Kumbukumbu nilizonazo za Kiongozi wa Tanzania kubeba silaha ni za aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bwana Kafanabo. Alikuwa akibeba bastola kiunoni wakati wa vita vya Iddi Amin. Ni huyo ni mkumbukaye na sasa mwingine ni Mheshimiwa Ismail Aden Rage, Mbunge wa Tabora Mjini. Wakati wa Kafanabo, nchi ilikuwa vitani; leo hii kuna sababu gani ya Mbunge, mwakilishi wa wananchi kubeba bastola kiunoni?

Je kama makomandoo wa CHADEMA wamepata mafunzo Afghanistan, Libya na Palestina kama alivyotueleza Katibu wa CCM, na Aden Rage amepata mafunzo ya ukomandoo nchi gani? Kubeba bastola kwa aina ya Rage,  ni ukomandoo; angeweza kuifunika bastola hiyo na shati lake, lakini kwa vile alitaka kuwaonyesha watu kwamba yuko tayari kwa lolote ndo akahakikisha bastola inakuwa wazi kwa kila mtu kuiona.

Tulishasema na tutaendelea kusema kwamba ikitokea amani ya nchi hii kupotea CCM ndo watakuwa chanzo: Matukio yanatokea Igunga, ya uvunjifu wa amani ukijumlisha na hili la Mheshimiwa Mbunge kupanda jukwaani na bastola; chanzo chake ni CCM. Tulisikia tukio la Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, ambalo sasa linageuzwa kuwa swala la kidini; ni vurugu za CCM, maana kwa nini mkuu wa wilaya ambaye ni kada wa CCM apange mikutano ya siri maeneo ambayo CHADEMA walikuwa wakifanya mkutano wao? Tumesikia la shahada kuuzwa na viongozi wa CCM kukamatwa na orodha ya majina ya watu; tumesikia mheshimiwa Lusinde, akisema kwamba CCM, ikishindwa atakunywa sumu; maana yake ni nini? Kwamba CCM haiwezi kushindwa au ni lazima CCM ishinde. Hapa kuna demokrasia ya kweli? Hivi si ni vitendo vya kuanzisha vurugu?

Bunge letu si la kijeshi. Kama Mheshimiwa Aden Rage, amechoka kuwa mbunge wa kiraia, basi ajiunge na jeshi na kuachia nafasi hiyo kwa watu ambao wako tayari kuwawakilisha wananchi wa Tabora, bila kubeba bastola kiunoni. Tunawachagua wabunge wa kuingia Bungeni kupambana kwa hoja na si kupambana na bastola. Kama ameweza kuibeba jukwaani anaweza kuibeba Bungeni. Ni wazi kwenye ukumbi wa bunge kuna mitambo ya kumzuia kuingia na silaha, lakini hotelini kwake ataibeba; anaweza kuwa mtu wa hatari kwa wabunge wenzake na hasa wa wabunge wa upinzani.

Makala hii ni wito wangu kwa wananchi wa Igunga, kukataa vitisho hivyo vya mheshimiwa Aden Rage, na kuonyesha kwamba wao wana uhuru wa kumchagua wanayemtaka bila vitisho hivyo. Pia ni wito wangu kwa watanzania wote kushikamana na kulaani kitendo cha Mheshimiwa Mbunge kupanda jukwaa la kisiasa akiwa amebeba silaha kiunoni. Tumshinikize aachie ngazi kwa kitendo chake cha kupanda jukwaa la kisiasa akiwa na bastola kiunoni, maana Tanzania si nchi ya kijeshi!

Pia nawaomba viongozi wa dini ambao wamekuwa mstari wa mbele kuombea amani na utulivu katika nchi yetu, walaani kitendo cha Mheshimiwa Aden Rage, kupanda jukwaa la kisiasa na bastola kiunoni. Wakione kitendo hicho kama ishara ya wazi ya CCM, kuelekea kuleta vurugu katika taifa letu. Wakikataa kulaani kitendo hicho basi nao  tuwapuuze na kuacha kuwasikiliza!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment