MAREHEMU ASKOFU CHRISTOPHER MWOLEKA- KUMBUKUMBU YA MIAKA TISA

Wanyakyusa,  wana utamaduni mzuri wa kumaliza matanga. Niliushuhudia utamaduni huu mnamo mwaka wa 1986,nilipoishi Mbeya. Baada ya mwaka mmoja  wa kifo cha marehemu, na hasa kama mtu huyo alikuwa ni mzee, huandaliwa kikundi cha ngoma kikiandamana na ndugu, jamaa na marafiki, ambacho huzunguka sehemu zote kijijini ,vijiji vya jirani na mjini alipokuwa akipendelea kutembea marehemu. Kazi inayofanyika kwenye sehemu hizo ni kuimba, kucheza, kunywa na kufurahi kwa lengo la kufuta kabisa kumbukumbu za marehemu. Ni njia ya kujihakikishia kwamba sasa marehemu hayupo kati yao tena.

Leo tarehe 16.10.2011, ni kumbukumbu ya miaka tisa ya kifo cha marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge(Sasa jimbo hili limetengwa na kutengeneza majimbo mawili; Jimbo la Kayanga na Jimbo la Rulenge-Ngara) Labda zamu hii, tofauti na miaka mingine, utamaduni wa Kinyakyusa ungetusaidia. Tuandae kikundi cha ngoma: Saida Karoli, Mau,Kakau Band au kikundi cha Taarabu- (Marehemu Askofu Mwoleka, alipenda kusikia nyimbo na kuangalia mikanda ya taarabu, siku za mwisho wa maisha yake) tuzunguke sehemu zote alizopenda kutembelea Askofu Mwoleka, tucheze, tuimbe, tule na kunywa na kufurahi kama njia mojawapo ya kujihakikishia kwamba sasa Mwoleka hayupo kati yetu tena. 

Wasiwasi wangu ni kwamba utamaduni wa Kinyakyusa, ungeshindwa kufuta kabisa kumbukumbu ya Mwoleka, kwenye nyoyo za watu walioishi na kufanya kazi naye kwa karibu. Alikuwa ni mtu mwenye matendo yasiyosahaulika haraka:

Mfano: Mwoleka, alikuwa mtu mwenye ukarimu mkubwa. Hakujua amsaidie mtu hadi kiasi gani, wakati mwingine kiasi cha yeye kubaki mifuko mitupu! Hakujua kupima kiwango cha zawadi. Angeweza kumnunulia mtu kilo 25 za nyama, kusalimia msiba au kumpongeza mtu aliyepata mtoto, badala ya kilo mbili au tatu. Angeweza kumzawadia mtu sukari kilo 50, badala ya kilo nne au tano. Kwa rambirambi za msiba, ambazo kijijini tunatoa elfu moja hadi tano, yeye alitoa laki yote! Tulimpachika jina la “Old Man of the Big quantity”.Mtu aliyekuwa mbali naye angeshawishika kusema, Anafuja mali! Hakuambatana na mali wala pesa. Aliambatana na wanadamu na Mungu wao!
 Yeye alikuwa hanywi pombe, na si kwamba alikuwa anakunywa na kuamua kuacha baada ya kushukiwa na Roho wa Bwana! Hakunywa kabisa, lakini nyumba yake ilikuwa na pombe za aina mbali mbali kwa kuwakaribisha na kuwafurahisha wageni wake. Yeye alikuwa tofauti  na watu wengine ambao huanzia kwenye ulevi, tena ulevi wa kupindukia wa kuvua nguo nakutembea uchi, wakishukiwa na Roho Mtakatifu na kuacha ulevi na kuacha kuonja pombe kabisa, wanakuwa na misimamo mikali ya kuchukia pombe na kuwachukia marafiki zao walevi waliokuwa wakipigana na kubebana enzi zile za ulevi, Wanafiki wakubwa. Askofu Mwoleka, hakuwa mnafiki!

Askofu Mwoleka, asingeweza kula chakula bila kuhakikisha anawahudumia (yeye mwenyewe) wale wote aliokaa nao kwenye meza ya chakula. Wakati mwingine alihitaji msaada wa kumkumbusha alipokula chakula au kuwakaribisha watu hotelini, aliendeleza huduma yake huko! Alikuwa ni mtu wa kuwahudumia wengine. Alikuwa mtumishi, si utumishi wa ishara na maneno, bali matendo. Aliwafulia watu nguo zao, aliosha vyombo baada ya chakula, aliwalimia watu mashamba yao, alishiriki kuvuna mazao, kujenga nyumba nk.

Mbali na ukarimu wake, kitu kingine ambacho hakisahauliki  kwa urahisi katika maisha ya Askofu Mwoleka, ni nia yake ya kutaka kuwajengea nyumba bora na za kisasa wananchi masikini wa Karagwe,Biharamulo na Ngara.Hakupenda kuishi kwenye nyumba bora zaidi ya nyumba za wenyeji waliokuwa wakimzunguka. Kama kuna dhambi kubwa aliyoiacha nyuma yake ni kushindwa kujenga nyumba ya kifahari ya Askofu na wala hakuwa na mpango. Kilichomsumbua sana ni kuwajengea watu masikini nyumba bora, imara na za kisasa. Wazo hili lilimchukulia muda wake mwingi. Yeye alikuwa ni mtaalamu wa kutumia mashini ya kuchapa na kompyuta. Hivyo alichora kwa kutumia mashini ya kuchapa na kompyuta michoro ya nyumba hizi alizotaka kuwajengea watu masikini. Kilichomsumbua zaidi ni kujenga nyumba bora na za kisasa kwa gharama nafuu. Sementi ilikuwa inapatikana kwa shida na kwa bei ya juu. Padre Jacob Mwenge(marehemu), alimshauri kwamba kulikuwa na uwezekano wa kujitengenezea sementi, na yeye alimhakikishia kuufahamu mmea fulani unaoashiria kuwepo sementi kwenye ardhi. Baada ya kuutambua mmea huo, ambao na mimi nilionyeshwa, Askofu Mwoleka, alianza kuyazungukia mapori yote ya Biharamulo,Ngara na Karagwe, akitafuta uwezekano wa kupata sementi kwa kuangalia mmea alioonyeshwa na Padre Jacob Mwenge!

Baadaye walijitokeza wataalamu kutoka Kigoma, sisi tuliwapachika jina la “Self made geologist”, wataalamu hawa walidai kwamba miamba ya mlima ulio karibu na Keza, kwenye barabara ya Nyakahura-Rulenge,ingeweza kutengeneza chokaa. Utaalamu wenyewe ilikuwa ni kuipasua miamba na kuyachoma mawe kwa moto mkali sana, yakiisha chemka sana unayamwagia maji na kuyeyuka, vumbivumbi anayotokana na myeyuko huo inatengeneza  chokaa. Mawe alichomwa kwelikweli. Yalipomwagiwa maji hakuna kilichotokea! Yalibaki vilevile! Mradi huu ulichukua pesa nyingi bila ya mafanikio yoyote. “Wapelelezi wa Roma” waliomshitaki Askofu Mwoleka, kwa kosa la ubadhirifu wa pesa, itakuwa waliutaja na mradi huu na mingine mingi ambayo haikufanikiwa. Ingawa mara nyingi Askofu Mwoleka, alikuwa hafanikiwi katika miradi yake, lakini daima alikuwa na lengo la kuwasaidia watu masikini. Hakutumia pesa kwa matumizi binafsi!
Kwa kutaka kukwepa gharama za mabati, alitaka nyumba za watu wa masikini ziezekwe kwa Vigae. Aliamini watu wangeweza kujitengenezea vigae. Hii inanikumbusha mwaka 1983, nilipokutana naye Ujerumani na kunielezea nia yake ya kutaka kujenga nyumba za vigae. Aliwaomba Wajerumani wampatie vigae viwili vya mfano. Alinificha nia yake ya kutaka kubeba vigae hivyo hadi Tanzania. Vigae vyenyewe vilikuwa vizito. Siri yake ilifichuka kwenye uwanja wa ndege wa Munich. Mzigo wake ulizidi uzito. Alipoambiwa kulipia au kupunguza uzito wa mzigo, alifungua mzigo wake na kutoa vigae viwili na kusema: Ninaomba mnisaidie, vigae hivi ni vya kufundishia watu wangu masikini, wajue kuvitengeneza na kujenga nyumba bora, imara na za kisasa. Maneno yake yaliulainisha moyo wa binti mdogo aliyekuwa anapima mizigo, alicheka tu na kumruhusu Askofu Mwoleka, kupita na vigae vyake bila kuvilipia. Zoezi la kujenga nyumba za vigae lilifanikiwa kiasi fulani. Hadi leo zipo nyumba ambazo chini zimejengwa kwa udongo, lakini paa ni za vigae. Askofu Mwoleka, alinunua mashini ndogo za kutengeneza vigae na kuzisambaza kwenye vituo mbalimbali. Bahati mbaya wajanja wachache waliiba hizi mashini na kuzitumia kufanya biashara kwa kuezeka nyumba za matajiri. Hivyo nia kamili ya Mwoleka ya kuwajengea maskini nyumba bora ikawa haikufanikiwa kiasi kizima. “Wapelelezi wa Roma” wakapeleka habari kwamba anafuja pesa!

Askofu Mwoleka, alikuwa mjenzi. Alikuwa na upeo, karama na roho ya kutaka kuwajengea watu wake nyumba bora, imara na za kisasa. Aliamini Mungu, anatutaka tuishi vizuri, tule vizuri, tuwe na afya bora na tushirikiane katika kujenga Ufalme wake. Sambamba na hili, Askofu Mwoleka, alitaka kujenga jamii bora, imara na ya kisasa. Theolojia yake ilikuwa Theolojia ya ujenzi. Maoni yake yalikuwa kwamba wamissionari walifyatua matofali na kuacha marundo. Walileta imani, walibatiza na kugawa sakramenti, lakini hawakujenga jumuiya za Kikristo. Watu walisali pamoja kanisani, lakini baada ya hapo kila mmoja alirudi nyumbani kwake na kuendelea kuishi maisha yake peke yake. Kanisa, halikuunganisha jirani na jirani, familia na familia, kitongoji na kitongoji na kijiji na kijiji. Waumini walibaki kama rundo la matofali! Wamissionari Walishughulikia imani ya mtu mmoja mmoja, kwa maneno mengine waliacha rundo la Wakristu, rundo la matofali, bila kujenga nyumba bora, imara na ya kisasa. Kazi ya wanateolojia wazawa, ni kuyatumia matofali hayo, mabaya na mazuri, kujengea nyumba bora, imara na ya kisasa. Kujenga kanisa la kisasa, lenye sura mpya. Maisha yake yote, Askofu Mwoleka, alijishughulisha na ujenzi huu wa nyumba bora, imara na ya kisasa. Ni wazi katika ujenzi kuna makosa ya hapa na pale, kuna kukwama na kuishiwa vifaa! La msingi ni lengo, na nia.

Tutakukumbuka daima Christopher Mwoleka, uliyekuwa Askofu wa jimbo Katoliki la Rulenge.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment