MWALIMU NYERERE MIAKA KUMI NA MIWILI SASA

Tarehe 14/11 kwa mara nyingine itakuwa ni siku ya mapumziko kwa watanzania wote ikiwa ni siku aliyofariki Mwasisi wa taifa letu Mwalimu Julius K. Nyerere. Kwa wengi pengine walimjua mwalimu kama rais mstaafu tuu. Mwalimu alikuwa zaidi ya hapo. Mwalimu alikuwa  Mwanazuoni mashuhuri, Mwandishi wa vitabu na maandiko ambayo leo yananukuliwa dunia nzima. Mwalimu alikuwa mpigania haki za wanyonge si kwa Tanzania tu bali kwa Afrika na dunia nzima. Zaidi ya hapo alikuwa mwanafalsafa mwenye mawazo yanayojitegemea na aliyeweza kujenga shule yake ya mawazo. Japo Mwalimu hayupo nasi tena, mawazo yake, busara zake na hekima zake bado zinakumbukwa na wengi. Maandiko yake yapo katika maktaba duniani kote yanasomwa, yananukuliwa na yataendelea kusomwa
Kuna mambo mengi ambayo mwalimu aliyasema miaka mingi iliyopita, lakini hadi leo hii viongozi wetu wameshindwa kuyatekeleza. Mfano mwaka 1995, Mwalimu aliongea kwa wazi kabisa juu ya jukumu la Serikali kukusanya kodi. La kushangaza ni kwamba hadi leo hii serikali yetu haijafanikiwa kukusanya kodi kiasi cha kutosha.

Mwalimu aliongea kwa uwazi kabisa kwamba chama kinachoshinda uchaguzi kitafakari kwa makini kuvishirikisha vyama vingine vinavyokuwa vimepata kura nyingi na wabunge wengi. Kwa kujenga umoja wa taifa changa, na kwa kuepusha migawanyiko isiyokuwa ya lazima; kama vile ukabila, udini na mambo mengine ya kuelekea kuvunja muungano. Mwalimu, aliona mbali kwamba kuiga mifumo ya mataifa ya nje, bila kutilia maanani hali yetu na uchanga wetu hatuwezi kufika mbali.
Lakini pia Mwalimu, aliongea juu ya  mgombea binafsi. Kwa ukali alisema kwamba kila raia ana haki ya kupiga kura na kupigiwa kura, hivyo kutokuwa kwenye vyama vya siasa kusiondoe haki ya raia kupigiwa kura. Pamoja na Mwalimu kulisisitiza hili la Mgombea binafsi, hadi leo hii bado halijaruhusiwa.
Ingawa Mwalimu alikuwa mwanachama wa CCM, na alikuwa Mwenyekiti wake, lakini hakusita kukisema chama chake na kukikosoa pale alipohisi chama hicho kinafanya madudu.
Sote tunakumbuka jinsi Mwalimu, alivyowakumbusha wanasiasa kwamba hata kama chama kina nguvu namna gani, kikipuuza maoni ya wananchi, chama hicho hakiwezi kusimama. Na kwamba vyama vinaposimamisha wagombea, na hasa kiti cha urais, ni lazima kuwa na umakini mkubwa, maana rais si wa chama bali ni wa nchi nzima.

Umaarufu wa mwalimu mpaka leo unadhihirika ndani na nje ya mipaka yetu. Chuo Kikuu cha Western Cape kila mwaka kina mhadhara wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambao lengo lake ni kuenzi juhudi za mwalimu katika kufuta ujinga Tanzania na mchango wake katika falsafa ya elimu kwa wote.  Hii ni heshima kubwa kwa Mwalimu na nchi yetu kwa ujumla. Mchango wa mwalimu ambaye kwake elimu ni njia ya kumkomboa mwanadamu na usawa katika jamii unatambulika ma kuheshimika. Zaidi ya hayo mchango wake wa elimu ya watu wazima na maendeleo umekuwa chachu kwa watu na taasisi duniani kote; nchi tajiri na nchi masikini

Amerika, Jumuiya ya watanzania wanaoishi kule pamoja na wenyeji wanaikumbuka siku ya kifo cha Mwalimu. Wanakutana na kujadiliana juu ya mawazo ya mwalimu na mchango wake katika dunia nzima.

Rwanda, nao wanaisherehekea siku ya Mwalimu kwa uzito mkubwa. Wao wanasema Mwalimu ni rafiki wa Wanyarwanda. Sote tunaijua historia ya Rwanda miaka ya nyuma. Wakimbizi wa Rwanda waliokimbilia DRC, Burundi, Uganda na Kenya, hawakupata uraia, lakini wale waliokimbilia Tanzania, walipata uraia. Mwalimu Nyerere, hakuona sababu ya Waafrika, jirani zetu kukaa kwenye makambi ya ukimbizi. Aliamua kuwapatia uraia na kuwaruhusu kuishi popote Tanzania. Walichanganyika na watanzania; mpaka leo hii uhusiano huu mkubwa hauwezi kufutika.

Upendo wa mwalimu kwa taifa lake na kwa watu wake, kutopenda kwake matabaka na kuhubiri usawa miongoni mwa watu wote wakati mwingine kulifanya falsafa zake kupindishwa kwa makusudi, ama kwa watu kutosoma aliyokuwa akiandika kwa kina ama kusoma na kutoelewa ama wakati mwingine kusoma na kuelewa na kupindisha kwa makusudi. Kuna watu mpaka leo wanamlaani sana mwalimu kwa ajili ya ule msemo wa “ Fedha si msingi wa Maendeleo”. Wanasema mwalimu aliwakataza watu wasiwe matajiri. Wanasema aliendekeza umasikini. Lakini ukisoma kwa undani maana ya ule msemo na ukauelewa ndio utaona ni kwa nini fedha si ndio maendeleo kweli. Suala kamili la msemo ule ni jinsi ambavyo kila mtu angetamani apate fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo. Kila mbunge akienda bungeni anataka waziri wa fedha ampe fedha kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lake. Kila waziri angetaka fedha kwa ajili ya Wizara yake ziongezeke. Lakini hizo fedha zitatoka wapi? Kiuchumi fedha ni lazima zizalishwe. Sio zizalishwe kwa kuchapwa kiwandani. Zizalishwe kwa kuongeza uzalishaji viwandani, mashambani, mauzo ya bidhaa nje nakadhalika. Kwa hiyo chanzo cha fedha ni uzalishaji. Kama hujazalisha hakuna fedha. Unaweza ukawa mpumbavu ukazichapisha kiwandani. Matokeo yake ni cha moto. Mfumuko wa bei  utakuwa wa ajabu kabisa. Utakuwa na makaratasi yasiyo na thamani. Kama huwezi kuongeza uzalishaji inabidi upate hizo fedha mahali pengine. Chanzo kikuu cha fedha isiyozalishwa ni misaada ya nje. Misaada ipo ya aina mbili. Mikopo na zawadi. Ukichukua mkopo ni lazima ulipwe baadaye. Utalipwaje? Ni kwa kuongeza uzalishaji. Kwa hivyo pesa ni lazima izalishwe. Ukikopa leo lazima kesho ulipe. Kama si mkopo utapata zawadi ambayo ni kama Sadaka. Hii inakupotezea uhuru wako. Unakuwa huna maamuzi, huna mamlaka na fedha unazopewa ndio maana zinakuja na masharti mengi sana. Unakuwa mtumwa katika nchi yako mwenyewe. Isitoshe, anayekupa msaada leo, kesho na keshokutwa unatarajia iwe bure tuu? Ni lazima kutakuwa na sababu ya msingi kabisa ya kukupa fedha. Kila mfadhili  ana malengo yake ama ya mazuri au mabaya. Lakini kwa vyovyote wafadhili wengi wana malengo ya muda mrefu yatakayowanufaisha wao.

Tunapopumzika kumkumbuka Mwalimu ni lazima tujikumbushe yale mambo ya msingi ambayo ni muhimu kwetu, aliyoyapigania hadi kifo chake, mambo ambayo hayajapitwa na wakati kabisa na yatachukua muda kupitwa na wakati. Kupumzika bila kujadili hoja zake hakutasaidia kitu. Tumuenzi kwa kukumbuka busara na mchango wake katika nchi ya Tanzania, bara la Afrika na duniani kwa ujumla.
Changamoto iliyo mbele yetu  wakati tunakumbuka miaka 12 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ni je ni Kweli tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele? Sifa ya Tanzania ya kuwa kimbilio la mataifa, sifa ya Tanzania ya kuwa kisiwa cha amani, sifa ya Tanzania ya kutokuwa na ubaguzi bado ipo?
Na,
Padri Privatus Karugendo


0 comments:

Post a Comment