MWANA MAMA.




LUCY SELINA LAMECK SOMI.

Ingawa jina hili la Mwana Mama Lucy Lameck halisikiki sana siku hizi, lakini mama huyu ni kati ya wanawake wachache walioingizwa serikalini baada ya uhuru. Mchango wake ni mkubwa kama ulivyokuwa kwa wanaume wengine waliolitumikia taifa letu kwa uaminifu uliotukuka! Alianzia kwenye chama, akiwa Mwanamke wa TANU, kama walivyokuwa akina Bibi Titi na wenzake. Lakini huyu kwa vile alikuwa amesoma, hakusukumwa jikoni na kulea watoto kama walivyotendendewa wanawake wengine wa TANU bali aliendelea kupambana serikalini na kutoa mchango wake kwenye baraza la mawaziri na kwingineko.

Ingawa kasi ya kuwapatia wanawake nafasi za juu serikalini haikuwa kubwa, lakini wale wachache waliozipata nafasi hizo walionyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuonyesha kwamba msemo ule wa “Wanawake wanaweza” ni kichekesho kama si tusi kwa wanawake. Tungekuwa makini wa kutunza kumbukumbu, tusingekubali kuimba wimbo huu ambao sasa unaanza kuwa kama fasheni na silaha ya wanaume kukwamishana na kuwekeana vizingiti kama ilivyotokea kwa spika wa Bunge. Wanawake, walipigania uhuru wa taifa letu, watashindwa vipi kushiriki uongozi? Kama wanawake waliweza huko nyuma, watashindwa kuweza leo hadi tukumbushane kwamba wanaweza? Ni uamuzi tu wa kukubali kuwatoa jikoni na kulea watoto kwa kutengeneza mifumo ya kuwawezesha kutembea na wakati, kuliko kuendelea kuimba wimbo ule ule kila kukicha.

Lucy Selina Lameck Somi, alizaliwa Kilimanjrao katikati ya miaka ya 1930. Baba yake alikuwa mkulima na wakati mwingine alifanya kazi ya usafirishaji. Mama yake, petronilla Lameck Somi, alijihusisha sana na siasa, wakati Lucy na dada zake watatu walipokuwa wadogo. Katika kitabu cha Wanawake wa TANU, Lucy anasema:

“Kila mara Nyerere alipokuja Moshi, alimtembelea mama yangu nyumbani, akanifahamu mimi na kutammbua kazi niliyokuwa nikifanya.Tulikuwa tunakula pamoja kila jioni, kwa hiyo akawa rafiki wa familia. Nyerere alimfahamu mama yangu kwa vile mama alikuwa anajihusisha sana na siasa kwa miaka mingi.TANU ilipoanzishwa, sote tulifanya kazi ya kuandikisha wanachama” (Wanawake wa TANU uk 78)

Lucy, kwa ujana wake na kiwango chake cha elimu, alikuwa wa kipekee, miongoni mwa wanawake wanaharakati wa TANU. Alitambuliwa kitaifa kama sauti yenye shauku kubwa ya kupigania hali za maisha ya wanawake baada ya uhuru.

Lucy alisoma shule ya msingi kijijini kwake, Moshi Njoro. Alisoma shule ya kati huko Kilema na sekondari huko Tanga, ambako alisomea vilevile miaka mitatu ya unesi na ukunga. Baada ya kumaliza masomo ya unesi, Lucy alichagua kurudi Moshi mwaka 1955. Huko Moshi alihudhuria masomo ya jioni ya kupiga chapa na hatimkato, akaanza kufanya kazi KNCU.

Alijiunga na chama cha TANU kama mwanachama wa kawaida na kufanya kazi ya kuandikisha wanachama hadi mwaka 1957. Alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya Wilaya ya Moshi ya TANU hadi 1957, alipoondoka kwenda masomoni Chuo cha Ruskin ,Oxford. Huko alisoma diploma ya Utawala,Sayansi ya Jamii, Saikolojia na Uchumi.

Alipoongea na mwandishi wa Kitabu cha Wanawake wa TANU, alisema:

“Ni vigumu kuelezea ni kwa nini nilijiunga na Tanu nikiwa mdogo hivyo. Nakumbuka vizuri kwamba sikupenda kabisa kufanya kazi chini ya mfumo wa ukoloni kwa sababu kulikuwa na ubaguzi wa wazi wa rangi. Kwa mfano manesi wa Kiafrika walitendewa vitu tofatui na Wazungu.Chakula kilikuwa tofauti, nyumba, saa za kazi, saa za kula, mtizamo wao mzima kuhusu sisi ulikuwa tofauti… ni mkusanyiko wa vitu vingi. TANU ilipokuja, ilikuta watu waliokuwa tayari kukiunga mkono. Halafu, unafika mahali unajikuta kuwa ni wa daraja la chini katika nchi yako…Kulikuwa na shule za Kizungu kwa watoto wachache wa Kizungu, shule za Wahindi kwa Wahindi walioshika uchumi wa nchi, halafu tulikuwa na shule masikini,silizokwisha, hizo zilikuwa za Waafrika…” (Wanawake wa TANU uk 80-81)

Mwaka 1960 Lucy Lameck, alikwenda Amerika chuo Kikuu cha Michigan, na huko alisoma mahusiano ya kimataifa. Aliporudi alifanya kazi ndani ya chama na baadaye alichaguliwa na rais kuingia Bungeni.

Mwaka 1962,Mwalimu Nyerere, alitambua mchango wa wanawake katika chama, na alifahamu fika kwamba kushiriki kwao kikamilifu kunahitajika katika kuendeleza nchi. Enzi hizo wimbo uliozoeleka siku hizi wa “Wanawake wanaweza” ulikuwa haujavumbuliwa! Hakuna aliyekuwa na mashaka juu ya uwezo wa wanawake; hivyo Mwalimu, alimteua Lucy Lameck, kuwa waziri mdogo wa Ustawi wa Jamii na Ushirika. Na mwaka 1966, alihamishiwa Wizara ya Afya na Nyumba hadi 1972. Hivyo alifanya kazi ya unaibu waziri kwa muda wa miaka 10, alipoondoka na kuweka nguvu zake katika shughuli za wanawake na jimbo lake la uchaguzi. Aliendelea kuchapa kazi na kuisaidia jamii iliyomzunguka hadi 1980, aliaga dunia Machi 21,1992.

Njozi ya Lucy Lameck kwa wanawake ilikuwa kuanzishwa kwa asasi za mafunzo mbalimbali katika kila wilaya, zitakazotoa elimu ya kilimo na ustawi wa mama na mtoto, pamoja na teknolojia inayofaa kwa kupunguza ugumu wa kazi za wanawake. Njozi hii ingetekelezwa, ingefuta kabisa ule wimbo wa “Wanawake wanaweza”. Jitihada pekee ya mkomboa mtoto wa kike ni kuhakikisha anakwenda shule; wasichana wana uwezo sawa na wavulana na hakuna ulazima wa kuwaisha watoto wetu kasumba ya “Mtoto wa kike anaweza”. Uwezo wa mtoto wa kike upo na wala hakuna haja ya kuutungia wimbo na kuwafanya watoto wa kike wawe wanyonge na kufikiri kwamba ni lazima kila wakati waonewe huruma.

Lucy Lameck alipiga vita mila na desturi zinazozuia wanawake kutofikia usawa na wanaume. Aliamini kwamba ni lazima ziwepo harakati za kupigania haki sawa kwa wanawake katika ngazi zote za kijamii ,kuanzia ngazi ya chini ya umma, kwenye chama na bungeni. Na kwamba tafiti kuhusu matatizo ya wanawake zinazofanywa na Chuo Kikuu ca Dar-es-salaam na asasi nyingine ziongeze kasi, maana wanaume watashawishika juu ya umuhimu wa mabadiliko kwa kutumia taarifa za kisayansi pekee. Hili ni muhimu zaidi ya ule wimbo. Taarifa za kisayansi zitaonyesha jinsi mtoto wa kike anaweza kuelewa mambo sambamba na mtoto wa kiume.

Kuwataja watu waliojitolea kulijenga taifa letu kwa uzalendo na uaminifu mkubwa, bila jina la Lucy Lameck, ni kuisaliti historia ya taifa letu. Tumekuwa na utamaduni wa mfumo dume wakati wa kuandika na kusimulia kumbukubu za kulijenga taifa letu. Mara nyingi yanatajwa majina ya wanaume peke yao, kwakati nchi yetu imejengwa na akina mama wengi waliojitoa muhanga kulitumia taifa letu kama Lucy Lameck.

Kwa maneno yake mwenyewe Lucy Lameck, anasema : “… Na hatukuanza kwa kuvaa nguo ghali na dhahabu, tulikuwa wanyenyekevu, wanawake wa kawaida tu, wawakilishi wa watu maskini wa vijijini na nchi hii.. Ukiniuliza kama kulikuwa na mwanamke aliyefikiria suala la mshahara bora, nina wasiwasi sana. Ni kweli, wanawake walikuwa na matatizo, na wanawake wa TANU walikuwa na matatizo… lakini tulijifunga kibwewbe kuitumikia nchi yetu” (Wanawake wa TANU uk 114).

Hivyo Lucy Lameck, kama walivyo wanawake wengine walishiriki kiasi kizima kulijenga taifa letu. Ni muhimu kuwakumbuka na kuwaenzi kama inavyofanyika kwa wanaume.

Na,

Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment