KWA NINI TUPOTEZE MUDA MWINGI NA FEDHA NYINGI KUJADILI “NDIYO”?

“Ukisema, ‘Ndiyo’, basi, iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi hayo  hutoka kwa yule Mwovu” (Matayo 5:37). Haya ni maneno ya Yesu Kristu wa Nazareti wakati akiwafundisha wafuasi wake. Somo lenyewe lilikuwa juu ya mtu kuwa na msimamo, uadilifu na uaminifu; kuwa na msimamo wa mtu binafsi, msimamo wa familia na hatimaye msimamo wa taifa zima la Israeli; Kwamba mtu ukiamua kuisimamia “Ndiyo” basi aisimamie bila kuteteleka na akiamua kuisimamia “Siyo” vile vile aisimamie bila kuyumba. Na kwamba mtu akiisimamia “Ndiyo” ukijua kwamba ni “Siyo” ni unafiki na uovu. Vile vile akiisimamia “Siyo” ukijua kwamba ni “Ndiyo” ni unafiki na uovu!

Kwa maneno mengine mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu hawezi kujiwekea kikao cha kujadili “Ndiyo” anayoijua ni “Ndiyo” na “Siyo” anayoijua ni “Siyo”. Mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu daima anakuwa mbali na unafiki na uovu. Hii ni falsafa ya Yesu wa Nazareti, aliyowafundisha wafuasi wake; bila kuingilia maswala ya imani, mtu yeyote anaweza kuitumia falsafa hii katika maisha yake maana ina msingi chanya wa kuendesha maisha katika jamii yoyote ile.

Wakati Yesu wa Nazareti akifundisha falsafa hii ya msimamo, uadilifu na uaminifu katika jamii ya Wayahudi; jamii yenyewe ya Wayahudi ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha mabadiliko; watawala waliabudu madaraka na mali; walipinduana katika utawala, walisalitiana na wakati mwingine waliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe; unafiki na uovu viliongoza maisha yao ya siku kwa siku; kuna wanaojenga hoja kwamba Yesu wa Nazareti, alikuwa mwanasiasa aliyeguswa na hali ya maisha ya watu katika jamii yake ya Wayahudi. Kwa wale wanaoipokea imani ya Kikristu bila kuchimba kwa kina historia, theolojia na elimu ya Biblia, watasema mimi ni mzushi; lakini ukweli utabaki pale pale kwamba Yesu wa Nazareti alizaliwa katika jamii Fulani na kuishi akizungukwa na historia, utamaduni na desturi za watu wake; ingawa sisi hapa Tanzania hatujafikia hatua ya kupigana vita vya wenyewe kwa wenyewe; hatujabaguana na kushindana kama walivyokuwa wana wa Israeli; unaweza ukafananisha hali ya Uyahudi ya wakati ule na hali ambayo taifa letu la Tanzania linapitia hivi leo. Unafiki na uovu vinawaongoza watawala wetu; hivyo tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Tunahitaji viongozi watakaosema “Ndiyo” wakimaanisha “Ndiyo” na watakaosema “siyo” wakimaanisha “Siyo”. Hali ilivyo sasa hivi ni kwamba viongozi wetu wanasema “Ndiyo” wakimaanisha “Siyo” na wanasema “Siyo” wakimaanisha “Ndiyo”. Tuna viongozi ambao wanacheka kumbe wanalia, na ambao wanalia kumbe wanacheka! Tuna wabunge wanaosinzia Bungeni wakisingizia kutafakari; wakibanwa zaidi wanasema huo ni uchochezi wa waandishi wa habari. Wabunge wetu walipambana kufa na kupona waitwe “Waheshimiwa” na kusahau kabisa kwamba waheshimiwa ni wananchi waliowatuma Bungeni.

Katika familia zetu, katika jamii zetu na katika taifa letu, tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Hatuwezi kujenga familia, jamii na taifa imara bila kuwa mbali na unafiki na uovu. Bila kujenga utamaduni wa “Ndiyo” kuwa ni “Ndiyo na “Siyo”  kuwa ni “Siyo”, hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo bila kuizingatia falsafa hii.

Lengo la makala hii si kujadili “Ndiyo” ni nini katika maisha Mtanzania na “Siyo” ni nini? Kama inavyofafanuliwa katika falsafa ya Yesu wa Nazareti, maana jinsi mambo yanavyokwenda ni kwamba sisi kama taifa hatujakubaliana “Ndiyo” ni nini na “Siyo” ni nini. Na kama makubaliano haya yapo, kitu ambacho sina imani kubwa nacho, basi ni lazima tukubaliane kwamba msimamo, uadilifu na uaminifu vimezikwa kaburi moja na Azimio la Arusha! Huu ni mjadala mrefu ambao ninafikiri unahitaji makala inayojitegemea. Ni mjadala ambao ni lazima kuendeshwa kwa uangalifu mkubwa ili kukwepa ushawishi wa kuichukulia falsafa yenyewe kama  kichocheo cha udini. Watanzania wakitaka kupindisha ukweli wanauweka udini mbele. Wakati mwingine udini ni silaha ya kuifumba midomo ya watu na kulenga kuwatenga watanzania kwenye makundi ili wasishirikiane kudai haki zao kutoka kwa watawala. Hivyo falsafa hii ya “Ndiyo” na “siyo” nitaijadili wakati muafaka ukifika.

Hoja ninayoijenga leo  kwenye makala hii ni kule kupoteza muda mwingi na fedha nyingi kuijadili “Ndiyo” ambayo hata kama watu wengi wanajua na kuamini kwamba ni “Siyo” lakini watawala na mfumo uliopo unaamua kwamba ni “Ndiyo”. Tunahitaji muda kuyashughulikia mambo mengine mengi maana taifa letu  bado ni masikini; tunahitaji fedha kutekeleza mipango mingi ya maendeleo; kwa nini basi muda huu unaohitajika hivyo na fedha hizi za maendeleo vitumike kujadili “Ndiyo”.

Tunalalamikia ufinyo wa bajeti. Kila wizara inalalamika kupata mgawo kidogo kutoka kwenye mfuko wa taifa letu. Watanzania walio wengi wanashauri wizara zote bajeti zao zipanuliwe na kuongezewa fedha nyingi na hasa fedha inayowalenga watanzania wanaoishi pembezoni.; badala yake tunawaweka wabunge pale Dodoma kwa kipindi cha miezi miwili, wakitumia fedha za Watanzania. Siku za kuishi Dodoma zikipunguzwa, ni wazi fedha nyingi zitapatikana ili ziongezewe kwenye bajeti za wizara mbali mbali. Ingawa sina takwimu za fedha wanazolipwa wabunge wetu, ni wazi siku zaidi ya 30  zikipunguzwa kwenye siku ambazo wabunge wanalazimika kuishi Dodoma, tutapata fedha ya kutosha kufanya miradi mingine ya maendeleo.

Bajeti yetu ya taifa inayojadiliwa kila baada ya mwaka mmoja kwa utawala na mfumo uliopo sasa ni “Ndiyo”. Ijadiliwe isijadiliwe ni lazima ipitishwe. Hata pale inapoonekana wazi wazi kwamba kuna ulazima wa kubadilisha kama inavyojionyesha kwenye bajeti ya mwaka huu ya Nishati na Madini, bado bajeti inapitishwa hivyo hivyo maana wabunge wa chama tawala ni wengi kuliko wa upinzani. Wakati mwingine inasikitisha zaidi bajeti inapopitishwa hata bila kujadili vifungu vyote kwa kisingizio cha kukimbizana na muda. Hoja ni kwamba kwa nini wabunge wakae Dodoma miezi miwili wakijadili “Ndiyo”. Ni busara gani inayotumika? Ni msimamo gani? Ni uadilifu gani na ni uaminifu gani wa wabunge wetu kutumia muda wote huo na fedha nyingi hivyo wakijadili “Ndiyo”? Kama lengo ni wabunge kuibariki bajeti, kwa nini bajeti isisomwe kwa siku mbili au  tatu na kupitishwa ili kuokoa muda na fedha?

Bunge letu lina utamaduni wa kupitisha mambo kwa swali: Wanaokubali waseme “Ndiyo” na wasiokubali waseme “Siyo”. Kufuatana na utawala na mfumo tulio nao kwa sasa hivi jibu ni “Ndiyo”. Hata pale ambapo na watoto wadogo wanaweza kutambua kwamba “Ndiyo” ni “Siyo”, na wakati mwingine sauti za wabunge wanaosema “Siyo” ni nyingi zaidi ya wale wanaosema “Ndiyo”, Spika na wasaidizi wake watasema wa “Ndiyo” wameshinda maana vichwani mwao hakuna kitu kingine zaidi ya “Ndiyo”.

Sina magomvi na Spika na wasaidizi wake kujaza “Ndiyo” vichwani mwao; maana huu pia ni mjadala mkubwa. Mfumo wetu wa utawala unamlazimisha Spika kuyatanguliza maslahi ya chama chake kabla ya kitu kingine kile. Spika wetu anatoka chama cha CCM ambacho ndicho chama tawala, hawezi kwenda kinyume na matakwa ya chama  chake; chama kinataka bajeti ipite jinsi ilivyo; hata kama busara ya Spika inamwelekeza kuunga mkono hoja za wapinzani zenye kujenga, ni lazima yeye aangukie upande wa chama chake: Kwa maneno mengine, Spika anakuwa mlinzi na msimamizi wa masilahi ya chama chake ndani ya Serikali. Hili linaeleweka, hata kama halikubaliki! Magomvi yangu si kwa spika tu bali kwa Bunge zima: Kwa nini tupoteze muda mwingi na fedha nyingi kujadili “Ndiyo”?

Mfumo wetu wa utawala, ni kwamba Mawaziri na manaibu wao ni lazima wawe wabunge. Hivyo Bunge linapokaa Dodoma miezi miwili kujadili “Ndiyo” mawaziri na manaibu wao wanakuwa Dodoma; ndivyo inavyopaswa kuwa ingawa wakati mwingine tunashuhudia viti vikiwa wazi. Wakiwa Dodoma, majukumu yao mengine yanakwamba au yanakwenda kwa kasi ndogo. Na mbaya zaidi kukaa kwao Dodoma ni matumizi mengi ya fedha, mbali na posho zao wa kibunge kuna matumizi mengine ya ziada ya kuzitunza ofisi mbili za mawaziri Dar-es-Salaam na Dodoma kwa wakati mmoja.

Kwa kupendekeza muda wa bunge la bajeti kupunguzwa kutoka miezi miwili ya sasa hadi siku  tatu, sina lengo la kubeza na kutoutambua mchango wa wale wanaotoa hoja nzito za kuonyesha kwamba “Ndiyo” inaweza kugeuka na kuwa “Siyo”. Ninaheshimu sana mchango wa wabunge wa upinzani. Wanafanya kazi nzuri; wanaonyesha msimamo, uadilifu na uaminifu kwa wapiga kura wao. Nguvu zao hazipotei bure, ingawa wakati mwingine wanatia huruma; maana mtu kuwaonyesha wenzako mwanga, wakaukataa na kukumbatia giza ni jambo linaloumiza na kukatisha tamaa, lakini hata hivyo hakuna hitaji la kukata tamaa maana historia inaandikwa, vizazi vijavyo vitasoma na kutoa hukumu. Na kusema ukweli wapinzani wanavikalia viti vyao Bungeni kwa uaminifu, ukilinganisha na wabunge wa chama tawala ambao mara nyingi viti vyao vinakuwa wazi. Pamoja na kuheshimu na kuukubali mchango wa wapinzani Bungeni, nafikiri ingekuwa bora kwao kutoa mchango wao kwa maandishi ili kuepusha kurefusha muda wa Bunge la bajeti. Kufuatana na uzoefu na kwa mfumo wa utawala uliopo sasa hivi “Ndiyo” itabaki kuwa “Ndiyo”, si busara kujadili “Ndiyo” hata kama wapinzani wanao mchango mzuri. Ni kiasi cha waziri kusimama na kusoma bajeti yake; bila majadiliano ikapitishwa. Majadiliano hayana amaana yoyote wakati kitu kimeamuliwa tayari.

Tumeshuhudia jinsi wabunge wa upinzani walivyoshikilia bango la kupinga posho za wabunge.  Hoja yao imeeleweka na imeungwa mkono na watanzania wengi. Nafikiri wakati umefika wabunge hawa wa upinzani  kushika bango jingine la kupinga Bunge la bajeti kukaa miezi miwili likijadili “Ndiyo”. Ni imani yangu kwamba na hoja hii itaeleweka na kuungwa mkono na watanzania wengi na kuchochea kilio cha kutaka katiba mpya. Wengine wanafikiri katiba si suluhisho la matatizo yetu kama taifa, ukweli ni kwamba ikiandikwa kwenye katiba kwamba ili “Ndiyo” ifikiwe ni lazima wabunge wajadili kwa kina na kupiga kura za siri bila shinikizo lolote kutoka kwenye chama chake.

Ni lazima kushirikiana sote; vyama vya upinzani, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, mashirika ya dini  na watu wengine wenye nia njema tuungame kwa pamoja kupinga Bunge letu kupoteza muda mwingi  kujadili ”Ndiyo”

Na
Padri Privatus Karugendo,

0 comments:

Post a Comment