TUNA TATIZO KUBWA KAMA TAIFA



Nimekuwa nikiandika juu ya swala hili kwa miaka mingi kwamba tuna tatizo kubwa kama taifa; tunashindwa kulinda mali zetu, madini yetu yanaibwa, ardhi yetu inaporwa, tunauza shahada zetu za kupiga kura na kukubali kuwachagua watu wanaotupatia sukari na kanga wakati wa uchaguzi, tunamchagua mkulima kuwawakilisha wafugaji, tunamchagua mvuvi kuwawakilisha machinga, tunamchagua mzee kuwawakilisha vijana, tunawachagua wanaume kuwawakilisha wanawake, tunashindwa kuipenda lugha yetu, tunaukataa utamaduni wetu, tunakataa ngozi yetu nyeusi  na kukazana kujichubua, tunazikataa nywele zetu na kukazana kuvaa za bandia, tunashindwa kufanya kazi masaa yanayotakiwa na kutaka tulipwe mshahara kwa kazi ambazo hatufanyi; waandishi na wachambuzi wengine wa maswala ya -kijamii wameandika pia juu ya swala hili na kuonyesha kwamba watanzania tuna matatizo makubwa kama taifa; kwa maneno mengine namna yetu ya kufikiri ina matatizo. Maendeleo ya taifa letu yanakwama kwa kushindwa kuwa na fikra pevu; tunadaganywa, tunapumbazwa na kubakia kuwaabudu na kuwasujudia watu badala ya kuliabudu na kulisujudia taifa letu la Tanzania.

Inawezekana nimekuwa nikiandika uzushi na labda mimi ndo nina matatizo ya kufikiri; inawezekana pia kwamba na waandishi wengine waliokuwa wakiandika juu ya swala hili na bado wanaandika juu ya swala hili wana matatizo  vichwani mwao. Vyovyote vile ukweli unabaki pale pale kwamba Watanzania tuna tatizo kubwa; tunahitaji dawa ya kututibu vinginevyo tunaelekea kubaya kama taifa:

Tunaweza kuacha mengine yote ya nyuma, na kuchukua mfano wa hivi karibuni wa Mheshimiwa Rostam Aziz, kujiuzulu nafasi za uongozi katika chama chake cha CCM na kuachia kiti chake cha Ubunge wa Igunga. Tumeshuhudia kwenye vyombo vya habari baadhi ya watu wa Igunga wakilia na kuzirai; hili nalo ni tatizo kubwa, maana kwa nini watu walie na kuzirai mtu kuacha kiti cha Ubunge, na kuacha kulia  na kuzirai kwa matatizo makubwa waliyonayo watanzania? Tuna matatizo makubwa ambayo kama si kulia na kuzirai basi mtu atasimama na kupambana kiume; atapigana kufa na kupona akitetea uhai wa  taifa lake kuliko kumlilia mtu mmoja ambaye wala si kitu si lolote kwenye uhai wa taifa letu; Sina haja ya kuyataja matatizo ya watanzania, maana sote tunaishi ndani ya taifa hili na matatizo yetu ya umasikini, njaa, magonjwa na ugumu wa maisha kwa ujumla tunayafahamu sote. Hata hivyo kulia na kuzirai kwa watu wa Igunga si msingi wa hoja yangu ninayotaka kuijenga kwenye makala hii. Walio mlilia Rostam Aziz, wanajua wenyewe watakayoyakosa: Kupanda kisiasa kwa kutumia nguvu za fedha, kutupiwa kanga na sukari na vijisenti ambavyo havimsaidii mtu kujitegemea.

Hoja yangu ya kuonyesha kwamba tuna tatizo kubwa kama taifa ni je, Huyu Rostam Aziz ni nani? Amelifanyia nini taifa hili kiasi ajiuzulu, magazeti yote yamwandike Rostam Aziz, na vyombo vyote vya habari viimbe habari za Rostlam Aziz, kuachia ngazi. Yangeanika magazeti yake ya Habari Coporation, ingeeleweka, lakini magazeti yote ya Tanzania kuandika juu ya Rostam Aziz, inaacha alama ya kuuliza. Alivinunua vyombo vyote vya habari viandike habari zake? Alilipia habari yake kama matangazo kwenye vyombo vyote vya habari? Habari yake ina uzito  gani katika maisha ya Mtanzania wa kawaida anayeshuhudia bei ya sukari na mafuta ya taa ikipanda kila kukicha? Ina maana kwamba tukio la Rostam Aziz, ndizo habari ambazo watanzania wanataka kusikia? Tuna watu wengi waliolifanyia taifa letu mambo mengi, tuna watanzania waliokuwa mawaziri, waliokuwa mabalozi, wanakufa, na hakuna gazeti lolote au chombo chochote cha habari kinachoandika au kutangaza historia ya maisha yao.

Rostam Aziz ni nani asimame na kusema; kwa kejeli na kiburi kwamba CCM, chama kinachotawala, kinaendesha siasa “Uchwara” na siasa za “Ovyo” tusisikie karipio la aina yoyote kutoka kwa viongozi wa serikali? Ina maana viongozi wetu wanakubali kwamba wanaendesha siasa “Uchwara”? Wanakubali kwamba wanaendesha siasa za “Ovyo”. Ni nani huyu mwenye uwezo mkubwa wa kuitukana serikali – na viongozi wakafyata mkia? Ni wazi  tuna tatizo kubwa kama taifa!

Rostam Aziz, alikuwa kwenye mtandao; anajua vizuri maana ya kugombania madaraka; anajua jinsi alivyoendesha mapambano ya kuingia madarakani kwenye uchaguzi wa 2005, ndivyo na watu wengine wanavyoendesha mapambano ya kuingia madarakani 2015; anashangaa nini? Yeye na wenzake walianzisha utamaduni wa kuingia madarakani kwa nguvu za fedha; kura zinanunuliwa, watu wananunuliwa na uongozi unanunuliwa. Katika mfumo wa kuuuza na kununua kuna kupata faida na kupata hasara; kuna kutajirika sana na kuna kufilisika; amefilisika ni lazima akubali ukweli huo. Yeye anajua vizuri kwamba mtandao uliwachafua watu wengi, uliwaumiza watu wengi, ulizima ndoto za watu wengi. Leo hii anasema vyama vya upinzani na vyombo vya habari vina ajenga ya kuchafuana na kuunga mkono siasa “Uchwara”. Leo hii anatumia vyombo vya habari na watu wa Igunga kutuonyesha kwamba ameonewa, kutuonyesha kwamba watu wa Igunga walimpenda sana? Kama tunayakubali hayo, ndio hivyo tuna matatizo katika vichwa vyetu; kufikiri kwetu na kuyaona mambo  kuna dosari kubwa.

Rostam Aziz, anatwambia kwamba yeye ni Mfanyabiashara wa kimataifa. Je anafanya biashara gani? Hizo biashara zake zinalinufaisha taifa letu? Analipa kodi? Tukienda TRA, tutapata takwimu zake za kulipa kodi? Amewaajili watu wangapi? Mbona hatujamuona kwenye umoja wa wafanya biashara wa Tanzania? Mbona hatujaona matangazo ya makampuni yake kama tunavyoona IPP, Precision Air na makampuni mengine mengi yanayotangaza biashara zake kwenye maonyesho ya biashara kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere kama yaliyofungwa hivi majuzi?

Tunachokijua ni kwamba amekuwa akitajwa kwenye kashifa zote za ufisadi ndani ya taifa letu.  Ametajwa kwenye EPA na kampuni yake ya Kagoda, ametajwa kwenye Richmond na Dowans. Kwa nini atajwe yeye? Ni kuonewa? Ni kuonewa wivu? Yeye ni nani kiasi aonewe na kuhusishwa na kila aina ya ufisadi? Hawezi kukana uhusiano wake wa karibu na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, hawezi kukana uhusiano wake wa karibu na Rais Dkt Jakaya Kikwete, hawezi kukana uhusiano wake na Mheshimiwa Edward Lowassa. Hawezi kukana uhusiano wake wa karibu na chama chake cha CCM; na kama hiyo ni kweli, hawezi pia kukana yale yote anayohusishwa nayo.

Rostam Azizi, anasema siasa “Uchwara” zimevuruga biashara zake na kuigusa familia yake. Lakini kwenye vyombo  vya habari tunamshuhudia akisimama peke yake na wanachama wa CCM wa Igunga bila familia yake kuwa upande wake wa kulia. Hiyo familia yake iko wapi kama hatuioni Igunga kwenye Jimbo lake la uchaguzi, itakuwa wapi? Na sisi tunaendelea kumlilia mzalendo huyu ambaye familia yake hatuioni na hatuna uhakika kama familia hii inashiriki na kuguswa na hali yetu ya maisha? Ndo maana kwa maoni yangu ninaona tuna tatizo kubwa kama taifa! Tunapumbazwa na kukubali kupumbazwa!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment