TWAWEZA KULIJENGA TAIFA BILA UAMINIFU?

Hali ilivyo sasa hivi katika taifa letu la Tanzania, mtu anaweza kujiuliza uaminifu maana yake nini? Na je, ni kwa nini mtu awe mwaminifu? Anaogopa nini? Anawajibika kwa nani? Kipimo cha uaminifu wake nini? Je uaminifu ni wa watanzania wote au kuna baadhi ya watu ambao ndio lazima wawe waaminifu. Uaminifu ni wa maskini tu au na matajiri nao ni lazima wawe  waaminifu? Je umasikini unachangia kiasi gani watu kukoswa uaminifu? Je ukosefu wa huduma muhimu katika jamii yetu unachangia kiasi gani watu kutokuwa waaminifu?

Bila kuyaangalia yote haya na kuyafanyia kazi ni ndoto kuongelea uaminifu. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo! Pia tunakumbushwa kwamba: "Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini kutoka miti ya michongoma, wala hawachumi matunda ya mizabibu kutoka mbigili. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake, na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka  katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake" (Luka 6:43-45).

Tunataka tusitake, hatuwezi kulijenga taifa bila ya kuwa na uaminifu. Tumeanza kunyosheana vidole ju ya madawa ya kulevya; hata viongozi wa dini ambao katika mazingira ya kawaida ndio wangekuwa mstari wa mbele kufundisha, kulinda na kuutetea uaminifu, wameshukiwa kufanya biashara hii haramu. Tunapiga kelele juu ya mikataba mibovu, tunapiga kelele juu ya mafisadi na wizi mkubwa wa rasilimali za taifa letu. Tunapiga kelele juu ya uporaji wa ardhi na uwekezaji unaoelekea kutuingiza katika dimbwi la ukoloni mambo leo. Yote haya yanasababishwa na uaminifu mdogo miongoni mwetu. Mataifa yote yaliyoendelea duniani, yamefikia hatua hiyo kwa kujenga uaminifu  imara miongoni mwa wananchi wake.

Watanzania walio wengi wamekulia katika mazingira ya udanganyifu, rushwa na uzembe. Tunaelekea kusherehekea miaka 50 ya uhuru wetu tukiwa tumetanguliza udanganyifu na uzembe. Matatizo mengi tuliyo nayo yanatokana na udanganyifu na uzembe. Tuna tatizo la umeme kwa sababu ya udanganyifu na uzembe, tuna umasikini wa kutisha kwa sababu ya udanganyifu na uzembe. Katika serikali ya awamu ya pili, ya tatu na sasa hii ya nne  tabia hizi zimejionyesha wazi na kufumbiwa macho. Watu wachache wamefanya kazi kwa uaminifu na kwa bidii kubwa, lakini asilimia kubwa ni udanganyifu, rushwa na uzembe. Mitihani inanunuliwa, vyeti vinanunuliwa na watu  wanapata mafanikio ya haraka maishani ( wanajenga majumba, wanakuwa na magari, wanakuwa viongozi wa juu serikalini, wana kuwa na viwanda, pesa nyingi hadi mabilioni) bila kusoma, walau kuwa na digrii moja au cheti na wakati mwingine bila hata kumaliza  sekondari. Hadi kuna msemo kwamba mafanikio maishani si kusoma!

Hata hivyo uaminifu ni neno pana na linazua maswali kuliko majibu. Mtu mwenye uchokozi anaweza kutoa maoni kwamba hata na majambazi wana uaminifu mkubwa miongoni mwao. Ikiwa na maana kwamba mtu akiongelea uaminifu ni bora kutoa maelezo ya kina. Jambazi akikamatwa, anakubali kuteswa na wakati mwingine kuyapoteza maisha yake bila kuwataja majambazi wengine. Huu ni uaminifu wa kiwango cha juu!  Mtu anayechota pesa za serikali ili kukiendeleza chama chake cha siasa, anakuwa anakoswa uaminifu katika serikali, lakini ni mwaminifu katika chama chake.  Mtu anayechota pesa za serikali ili kuwasomesha watoto wake, jamaa zake na kuleta maendeleo katika wilaya yake, anakuwa anakoswa uaminifu serikalini, lakini ni mwaminifu kwa familia yake na kabila lake.

Uaminifu unahitaji malengo, kipimo na uwajibikaji. Ni lazima mtu ajiulize ni kwa nini anatakiwa kuwa mwaminifu, na kwa nani? Kwa familia yake, kwa kabila lake, kwa dini yake au kwa taifa lake, na je ni kipimo gani kitatumika kuupima uaminifu wake. Na ni lazima uwepo mfumo wa kumsaidia mtu kutekeleza malengo, kukumbushwa malengo na kupimwa mara kwa mara. Mtu akiachwa peke yake ni lazima atangulize uaminifu unaolenga katika kumletea  manufaa yake binafsi. Kwa vile watanzania wameachiwa bila kuwa na chombo cha kuwakumbusha, kila mtu anajijenga binafsi badala ya kulijenga taifa letu.

Majambazi, wana mifumo yao ya kulinda na kukuza uaminifu miongoni  mwao. Wana viongozi, wana viapo, wana nafasi za kukutania kufanya mikutano na majadiliano na wana waganga wao wa kuwafanyia zindiko na matambiko. Majambazi wana kipimo cha kupima uaminifu wa kila mshirika. Anayeshindwa kipimo hicho  anakwenda maji! Hivyo na sisi kama tunataka kuendelea kama taifa ni muhimu kuwa na mfumo wa kupima uaminifu wetu.

Wakati nikitafakari swala zima la uaminifu katika taifa letu la Tanzania,  nimekumbuka yale tunayoelezwa katika Biblia  kuhusu Anania na Safira. Hawa ni mme na mke walioishi kwenye jumuiya za kwanza za Kikristu zilizokuwa zimejiwekea malengo, kipimo na uwajibikaji:

" Jumuiya yote yote ya waamini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo........ Hakuna mtu ye yote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmmoja kadiri  ya mahitaji yake".(Matendo ya Mitume 4:32-35).

" Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vile vile. Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizozipata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume. Basi, Petro akamwuliza, "Anania, mbona Shetani ameungia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba? Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo, kwa nini ,basi, uliamua moyoni kwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu, umemdanganya Mungu". Anania aliposikia hayo, akaaguka chini, akafa. Watu wote waliosikia habari ya tukio hilo waliogopa sana.....Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani( neno mle ndani, ni kutaka kumaanisha, mahali pa kukutania, mkutano wa jumuiya, nafasi ya majadiliano, kukumbushana malengo na wajibu) Petro akamwambia," Niambie Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?"  Yeye akamjibu, "Naam, ni kisi hicho". Naye Petro akamwambia, "Mbona umekula njama kumjaribu Roho wa Bwana?........ Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa...... Kanisa lote pamoja na wote waliosikia habari ya tukio hilo, waliogopa sana" (  Matendo ya Mitume 5:1-11).

Wataalamu wa Biblia wanatuelezea kwamba kifo cha Anania na Safira, hakikuwa kifo kama tunavyojua sisi mtu kufa akazikwa kaburini. Ni kwamba walitengwa na jumuia ya waamini. Ukosefu wa uaminifu katika Jumuiya za Kikristu za mwanzo kulimaanisha kifo. Kutengwa na jumuiya kulilinganishwa na kifo. Woga wa kutengwa na jumuiya kuliwafanya watu kuwa waaminifu wakati wote. Kila mtu aliujua wajibu wake wa kutanguliza jumuiya kabla ya kuyatanguliza maisha yake binafsi. Walisali pamoja, walionyana, walikumbushana, walitiana nguvu.

Kabla ya uaminifu kwa jumuiya nzima, kila mtu alichunguza uaminifu katika moyo wake. Kila mtu alijipima kwa kipimo cha Anania na Safira. Ni kiasi gani mtu alijiamini yeye mwenyewe. Anania na Safira, walitaka watoe nusu ya mali yao, kwa kisingizio cha kutoa kila kitu walichokuwa nacho. Na kwa vile jumuiya nzima iliamua kwamba hawa hawakuwa waaminifu kwa jumuiya hayo, walitengwa! Kwa msemo wao wa kiimani, walikufa!

Mfano huu wa Anania na Safira, unaweza kutusaidia sisi watanzania. Je, sisi tuna malengo gani? Kipimo chetu cha uaminifu ni kipi? Anayekoswa uaminifu anafanywa nini? Tunakutania wapi ili kuonyana, kukumbushana  malengo na kutiana nguvu? Ni nani anaogopa kutengwa na jamii akifanya mambo ya udanganyifu? Tunaogopa nini? Ni yapi yaliyojaa mioyoni mwetu?

Ni muhimu kukumbushana kwamba hatuwezi kujenga uaminifu miongoni mwetu  kwenye majukwaa, kwenye luninga au kwenye magazeti, kwamba huwezi kujenga uaminifu bila ya kuwa na malengo, mfumo na kipimo. Huko nyuma  lengo letu lilikuwa ni kujenga Ujamaa na Kujitegemea. Kila aliyekwenda kinyume na sera ya ujamaa, alionekana kuwa mtu asiyekuwa mwaminifu. Sasa hivi hatujengi ujamaa, na hakuna mwenye uhakika tunachokijenga ni kitu gani. Wengine wanasema Utandawazi, wengine wanasema kazi yao au malengo yao ni kujenga barabara, wengine wanasema soko hulia,  wengine wanaingia ubia na wawekezaji , wengine eti ni mlengo wa kulia, wengine eti ni mlengo wa kushoto na wengine mlengo wa kati, wengine wanasema ubinafsishaji. Sasa hivi ni vurugu! Hatuna kipimo!

Mtu, akipora pesa za serikali, akajenga hekalu, watu wanamshangilia. Huyu anaonekana kama shujaa. Kila Mtanzania, anataka awe kama yeye. Mazingira kama haya hayawezi kujenga uaminifu. Tume ya Warioba, ilifichua watu na mazingira yanayosababisha ukosefu wa uaminifu (rushwa), hakuna kilichofanyika! Kwanini basi " Bongo land" isimaanishe ubazazi? Watu wana macho na akili. Wakiona kiongozi anaanzisha ubazazi, nao wanafuatisha! Na tunatembea kifua mbele tukijitangaza kwamba sisi ni “Bong land”: ukitaka bidhaa bandia karibu “Bongo land”, ukitaka kutajirika haraka, kuchota na kujiondokea, karibu “Bongo land”, ukitaka kushuhudia viongozi wa watu masikini wanaoogelea kwenye utajiri mkubwa karibu “Bongo land”.

Watu wengi , wametajwa mara nyingi kuogelea kwenye dimbwi la udanganyifu. Hakuna kinachofanyika! Na la kushangaza zaidi wale wote wanaotajwa kuwa wadanganyifu ndo wanajiweka mstari wa mbele kutaka kuliongoza taifa letu la Tanzania na kuonyesha wazi wazi kwamba hii ni  "Bongo land",  Kama huu si ubazazi ni kitu gani? Kuna haja ya kuweka wazi malengo ya kitaifa na kutengeneza mifumo ya kutekeleza malengo hayo. Wengine wanafikiri kwamba tunahitaji pia katiba ya nchi itakayokuwa inaelezea wazi hatua za kumchukulia mtu anayevunja uaminifu wa kitaifa. Katiba inayowapatia wananchi uwezo wa kuwakataa viongozi wala rushwa. Katiba inayoruhusu wagombea binafsi, jambo ambalo linaweza kuleta ufanisi wa kisiasa katika Taifa letu maana kuna watu wanapenda kulitumikia taifa letu lakini hawapendi ukiritimba wa vyama vya siasa.  Katiba itakayo toa mwanya wa kuunda  tume huru ya uchaguzi, ili wananchi wawe na uhuru wa kuichagua serikali yenye sera ya kujenga uaminifu wa  kitaifa. Tunahitaji kuwa chombo katika ngazi zote kuanzia vijijini hadi taifani cha kuweza kukumbusha, kujadiliana, kutiana nguvu na kupima uaminifu wa kila Mtanzania.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment