UCHAGUZI WA IGUNGA, MKAPA ANATUKUMBUSHA YA NYUMA.



Waswahili wanasema yaliyopita si ndwele, lakini kwa vile Rais Mstaafu William Benjamin Mkapa, ameamua kupanda tena jukwaani na kuendeleza siasa “Uchwara” alizoziacha nyuma yake hatuna budi kuyafufua ya nyuma. Tulishauriwa kutomgusa ili apumzike kwa amani; yeye hataki kupumzika! Yuko Igunga akipigana kufa na kupona ili kiti hicho cha ubunge kisiende upinzani. Pamoja na idadi kubwa ya wabunge wa CCM , bado Mkapa ameona ni muhimu sana kupigana kufa na kupona kutetea kiti hicho. Je huo ni U- Tanzania?

Tumkumbushe hotuba yake ya kufunga mwaka 2004: Hotuba hiyo
 ilikuwa nzuri na ya kumgusa kila “Mtanzania”. Ambaye hakuguswa na hotuba hiyo basi huyo si “Mtanzania”. Nimeweka neno Mtanzania kwenye mabano, maana si kila Mtanzania ni Mtanzania! Hili linahitaji mjadala unaojitegemea!  Kama mtu hakuguswa na maelezo ya Mkapa juu ya hali ya kisiasa, basi atakuwa aliguswa na maelezo yake juu ya hali ya uchumi, hali ya kijamii, mambo ya nje au basi atakuwa aliguswa na hitimisho. Kila mtu atakuwa aliguswa kwa namna yake. Kama alivyosema yeye mwenyewe kwenye hotuba hiyo. 
“ Penye wengi, pana mengi. Nasi tuko wengi, zaidi ya milioni 35. Hivyo haishangazi wakitokea wachache wenye sababu zao za kuziba macho na masikio wasiyaone wala kuyasikia yale ambayo Serikali yenu ikishirikiana nami tumeweza kufanya au kuyaanzisha. Watu hao ni wa kuonewa huruma, wanapigana na ukuta”.

Ni kweli watanzania ni wengi na namna ya kuangalia na kuamua vitu inatofautiana. Ndiyo maana ninasema hotuba yake  itakuwa ilimgusa kila mtu kwa namna yake. Bahati mbaya hotuba hiyo haikutoa takwimu ili kuonyesha wachache kati ya milioni 35 ni ngapi?  Hivyo ni vigumu kujua watu wa kuhurumiwa ni wangapi – inawezekana pia kwamba wale anaodhani ni wengi ndio wanaopigana na ukuta. Wakati ukuta, Waswahili wanasema.

Kwenye hotuba hiyo Rais Mstaafu William Benjamin Mkapa alisema:
“ Utaona pia watu wanabishana juu ya mambo mengine madogo, au hata ya kipuuzi kabisa. Lakini ubishi huo ndiyo unaitwa ushindani wa kisiasa, unachangamkiwa pia na vyombo vya habari”,

 Bahati mbaya katika hotuba hiyo  hakuweka bayana maana ya mambo madogo  na mambo ya kipuuzi. Hakutoa mifano! Malalamiko ya walio wengi ni rushwa, kuiba kura, kujilimbikizia mali, kupora nchi, kujiingiza kwenye utandawazi bila mbinu na maandalizi, kuuza mashirika ya umma kwa wawekezaji wa nje bila ya uangalifu wa kutosha. Siku chache kabla ya hotuba hii tulisikia kwenye vyombo vya habari wawekezaji waliokamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, wakitoroka bila kulipa ushuru. Hao walikamatwa, ni wangapi wametoroka bila kukamatwa?  Inawezekana haya ni mambo madogo na ya kipuuzi? Kwa vile Mheshimiwa Mkapa, hakutoa mifano – labda wasaidizi wake walipitiwa. Kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mifano yake. Na kujiuliza ni yapi mambo madogo na yapi ni ya kipuuzi! Kwa Mtanzania wa kawaida, wale tunaozoea kuwaita walalahoi ununuzi ndege ya Rais ya bilioni 40, ya aina yake Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na yenye uwezo wa kuruka kwa masaa mengi bila ya kutua kujaza mafuta na yenye uwezo wa kutua kwenye viwanja vichache nchini Tanzania, ni upuuzi wa hali ya juu. Watu wanakufa kwa njaa, malaria inawaua watoto, barabara mbovu, watu hawana maji, hawana umeme, hawana kipato cha kutosha nk – inawezekana kuyajadili haya ni upuuzi? Lakini kwa yule aliyeshiriki kuiagiza ndege ya Rais na kupokea michuzi ya asilimia kumi, atauita mjadala wa kununua au kutonunua ndege ya Rais kuwa ni kujadili mambo madogo!

Hoja  nyingine kwenye hotuba hiyo ilikuwa:
 “ Na sera haiwezi KUINGIA IKULU. Sera ya kuingia IKULU ni sera ya ubinafsi; tena ubinafsi wa hali ya juu. Maana hoja si kwenda IKULU: hata tausi wanaishi IKULU. Hoja ni unakwenda  IKULU kuwafanyia nini Watanzania”, 
 Ni mtu gani asiyejua kwamba IKULU, kuna Neema? Bila Neema, hata tausi wataikimbia Ikulu!

Hotuba hiyo iligusia mambo mengi;
 “ Kwanza, kuhakikisha kuwa asilimia 93 ya Watanzania ambao hawajaambukizwa virusi vya UKIMWI hawaambukizwi. Kila mbinu na kila silaha itumike. Wakati wa kuchagua silaha kwenye vita hivi umepita. Wakati wa unafiki nao umepita. Tukifanya ajizi taifa litaangamia.”,

 Kwa kipindi chote cha utawala wake Rais Mkapa, hakuonyesha mzimamo wake waziwazi juu ya kudhibiti ugonjwa huu. Kwenye hotuba yake alishindwa kutuelezea ni mbinu gani zitatumika kuhakikisha asilimia 93 haiambukizwi. Ni mbinu gani? Miujiza? Hakuunga mkono matumizi ya kondomu, waziwazi bila ya kuzunguka na bila ya mafumbo. Yeye kama Rais wa nchi alikuwa na nafasi ya pekee ya kuhakikisha kila mbinu inayofaa inatumika bila kuangalia au kulenga kuyafurahisha baadhi ya makundi fulani katika jamii yetu. Vita ni vita na vita haina macho! Aliendelea na mbinu potovu ya kutotaka kupoteza uhusiano mzuri na viongozi wa kidini. Kwa mshangao wa wengi amehitimisha hotuba yake kwa kupiga marufuku tangazo la “Usione Soo”. Tunajua sote jinsi wanawake walivyo kwenye hatari kubwa ya kushambuliwa na UKIMWI, utamaduni wetu umekuwa ukimkandamiza mwanamke na kumfanya “Aone Soo”, akubaliane na kila kitu asemacho mwanaume. Utamaduni huu umewaingiza wanawake wengi kwenye matatizo yasiyokuwa yao. Utafiti unatuonyesha kwamba sehemu ambazo wanaume wanawaacha wanawake vijijini na kwenda kufanya kazi na kuishi mijini, imeshambuliwa sana na UKIMWI. Wanaume wanapokuja likizo nyakati za Christmas na mwaka mpya wanabeba virusi. Wanawake vijijini wanaona Soo, kuwauliza waume zao juu ya hali zao. Pamoja na zawadi za Christmas wanazozipata kutoka mijini ni UKIMWI. Utamaduni huu wa mfumo dume umekuwa hatari kubwa katika dunia ya leo. Mtu yeyote anayetaka kuuendeleza, hatufai kabisa. Huyu ni adui wa UMMA! Adui wa UMMA, ni lazima kumkataa na kusema, hapana huo si U-Tanzania!

Katika hotuba hiyo mimi binafsi niliguswa na nukuu ya Mwalimu:

 “ Hoja lazima ijengwe kwamba hatimaye kinga madhubuti ya haki za raia, uhuru wa raia, na mambo yote wanayoyathamini, hatimaye yatahifadhiwa na maadili ya kitaifa. Taifa linapokuwa halina maadili yanayowezesha Serikali kusema: ‘ Hatuwezi kufanya hivi, huu si U-Tanganyika.’ Iwapo watu hawana maadili ya aina hiyo, haisaidii sana hata kama wangekuwa na  Katiba iliyoandikwa vizuri sana. Bado raia wanaweza kukandamizwa…. Tunachopaswa kukifanya ni kujenga maadili ya taifa hili, kila mara kuimarisha maadili ya taifa hili, maadili yatakayomfanya Rais yeyote yule kusema, ‘Ninayo madaraka ya kufanya  jambo hili chini ya Katiba, lakini sitalifanya, maana huu si U-Tanganyika. Au kwa watu wa Tanganyika, iwapo wamekosea na kumchagua mwenda wazimu kuwa Rais, mwenye madaraka ndani ya katiba ya kufanya XYZ, akijaribu kufanya hivyo, watu wa Tanganyika waseme, ‘Hatukubali hili lifanyike, hata alitake Rais au Rais maradufu, hatulikubali, maana huu si U-Tanganyika’."

 Haya maneno ya Mwalimu, yaliyotamkwa tarehe 28 Juni 1962, wakati mwalimu akiwasilisha Bungeni mswada wa kuifanya iliyokuwa Tanganyika kuwa jamhuri, ni kipimo cha  Vyama, Viongozi na watanzania wanaojigamba kwamba wao ni “Watanzania”.

Bahati nzuri au mbaya viongozi wetu wote wa kitaifa tulionao hadi leo hii ni wa CCM. Chama kinachotawala ni cha CCM. Je, Chama hiki na viongozi wake wametufikisha mahali pa kusema kwamba huu ni U-Tanzania? Ni kiongozi gani mnyenyekevu, tumtaje kwa jina, nani? Unyenyekevu unaonekana wakati wa uchaguzi, baada ya hapo viongozi wetu wanakuwa miungu watu! Ni kiongozi gani asiyetafuta kutumikiwa bali kutumikia? Tumtaje kwa jina!

Waasisi wa taifa letu walituachia utamaduni wa kutolimbikiza mali. Ni kiongozi gani leo hii halimbikizi  mali? Tumtaje kwa jina!

Waasisi wa taifa letu walituachia utamaduni wa kung’atuka. Ni kiongozi gani wa Tanzania, ameonyesha dalili  za kung’atuka kwa hiari? Je CCM, yenyewe imezingatia utamaduni huu wa kung’atuka. Ikafika mahali ikaviachia vyama vingine. Maana huu ndio utamaduni wetu na huu ndio U-Tanzania?

Je ni U-Tanzania, kiongozi wa nchi kutamka:
“ Maana wanaojaribu kupanda mbegu za chuki, mbegu za udini, mbegu za ukabila, ni wachache. Kwa pamoja tutang’oa mbegu zao, na ikibidi tutawang’oa wao”.

“ikibidi utawang’oa wao” ina maana gani? Hapa kuna utetezi wa  uhai? Tujuavyo sisi uking’oa kitu kinakufa. Je, ni U-Tanzania, kuwatishia wananchi? Huku si kutangaza vita au kutaka kuwanyamazisha wenye maoni tofauti?

“ Ninarudia. Tutanya kila liliko ndani ya uwezo wa Serikali, kwa mujibu wa sheria, kuhakikisha wanaotaka kuleta fujo, vurugu na uvunjifu wa amani hawafanikiwi kamwe, na hasa mwaka ujao wa Uchaguzi Mkuu.”

Kama hakuna maelezo ya fujo na vurugu ni nini ni lazima wananchi wawe na mawazo tofauti, wanaofikiri CCM, haikufanya vizuri wawe na wasiwasi wa maisha yao. Ni lazima watafute mbinu za kuyalinda maisha yao. Historia imetufundisha kwamba wapambanaji wote daima wanawekwa kwenye kundi la watu wa fujo, vurugu na ugaidi. Makaburu, walikuwa wakitumia nguvu za serikali na mujibu wa sheria kumdhibiti Mandela na juhudi za ANC, za kutaka kuleta mabadiliko Afrika ya kusini. Wapigania huru wote waliwekwa kwenye orodha ya watu wenye fujo, vurugu na wanavunja amani.

CCM, imeshindwa kupambana na rushwa. Nchi nzima inanuka rushwa ndogo na rushwa kubwa kubwa. Tumeshuhudia miradi hewa. IPTL, inaleta hasara kwa Taifa. Viongozi wenye mishahara ya kawaida wanajenga mahekalu, wana magari ya bei mbaya, watoto wao wanasoma nchi ze nje nk. Haya yote yanatendeka chini ya uongozi wa CCM. Hakuna hatua inayochukuliwa. Hakuna anayewajibishwa. Inaendelea kuwa kero kwa wananchi wa kawaida na wale wote wanaojali maendeleo ya taifa zima la Tanzania. Je, ni vurugu au ni fujo, watu wakianza kuhoji uwezo wa CCM, kuendelea kuliongoza taifa letu? Je, hawa ndio watakaong’olewa na Serikali ya CCM? Hawa ndio watakao poteza maisha yao? Ni nchi gani duniani iliyoendelea kwa kuongozwa na viongozi wala rushwa?

Tujiulize, U-Tanzania, unanyesha kama mvua? Inatosha kuzaliwa Tanzania, mtu akatenda na kuishi ya U-Tanzania? Mtanzania, hawezi kuisaliti nchi yake, hawezi kuipora nchi yake. Mtanzania wa kweli ni mzalendo. Mtanzania wa kweli analitanguliza taifa bila kuangalia kwanza maslahi yake binafsi, analitanguliza taifa bila kutanguliza tumbo lake. Huyu yuko tayari kuyapoteza maisha yake kwa kutetea uhai wa taifa lake. Ili kuujenga U-Tanzania, mwalimu  Nyerere na waasisi wengine, walibuni mbinu na mifumo mbali: Lugha moja, siasa ya ujamaa na kujitegemea, vijiji vya ujamaa, kuwasambaza watoto kwenye shule za mikoa mbalimbali, jeshi la kujenga taifa, mwenge wa  uhuru nk.

Leo hii Lugha yetu tunaipiga vita. Tunataka kutumia lugha za kigeni! Ujamaa tumeuweka kaburini. Vijiji vya ujamaa havisikiki tena. Jeshi la kujenga taifa liliokuwa linawakutanisha vijana waliomaliza kidato cha sita, limekufa kifo kitakatifu! Mwenge wa huru umetaifishwa na CCM, badala ya kujenga umoja wa kitaifa unatumika kukipigia debe  chama cha Mapinduzi. Tuna mbinu gani za kujenga U-Tanzania?Ni nani mwenye sera ya wazi ya kuujenga U-Tanzania? Tusijidanganye  na kuamini kwamba jambo hili linaweza kunyesha kama mvua. Ni jambo la kufanyia kazi. Na mwenye nafasi ya kufanya jambo hili, hawezi kupata nafasi ya kujilimbikizia mali, nafasi ya kuwa na viwanja na kujenga nyumba kila mkoa, Mwalimu Nyerere, alikuwa na nyumba ngapi? Je, nyuma yake ameacha vitabu vingapi vyenye sera, vision, falsafa na mambo mengine mengi ya kuujenga U-Tanzania na Ubinadamu? Alitumia muda wake, kufikiri, kusoma, kupanga na kuandika. Kujenga U-Tanzania, kunahitaji umakini. Huwezi kushinda na kulala kwenye pombe, kufukuzia dogodogo, kujenga nyumba ndogo, kugombania viwanja, kufukuzia asilimia kumi kwa kila mradi upitao, ukapata muda na uwezo wa kujenga vision.

Majumba yamejengwa, viongozi wetu wanavaa suti za Ulaya, wanaendesha magari ya bei mbaya, ofisi zinapendeza – lakini uko wapi urithi wa vitabu? Ni nani anaandika, ni kiongozi gani anakaa chini kusoma, kufikiri na kutunga sera. Viko wapi vitabu hivi tuvisome. Viongozi wetu wa sasa wanaongozwa na falsafa ipi? Ni nani mwenye kuitetea falsafa hii na kuifundisha?

Tulitegemea baada ya kustaafu Mheshimiwa Mkapa, angekaa chini na kuangalia ya nyuma. Kuona alikosea wapi na alifanikiwa wapi. Angetumia muda wake uliobaki kuandika vitabu vya kuwashauri na kuwaongoza watanzania na si kujiingiza kwenye upuuzi huu wa “Siasa Uchwara” kutumia fedha nyingi kuhakikisha jimbo la Igunga linabaki CCM. Wapinzani nao ni Watanzania, kama Mkapa halioni hili, basi kumbe naye hakufaa kuiongoza Tanzania!
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment