WABUNGE WETU WATENGENEZE MAJUKWAA YA MAJADILIANO MAJIMBONI KWAO.


Ukisikiliza jinsi mjadala unavyokwenda kwenye Bunge la Bajeti linaloendelea Dodoma, utagundua kwamba wabunge wetu hawana mawasiliano na wananchi waliowatuma bungeni. Wabunge wanawasilisha maoni yao binafsi badala ya kuwasilisha maoni ya wananchi; wanaunga mkono hoja zote, kana kwamba hoja hizo zimetengenezwa na malaika; kama huo ndio ukweli, ya nini basi hoja hizo kuletwa Bungeni? Kwanini wabunge wapoteze miezi miwili wakijadili kitu ambacho wanafahamu fika kwamba mwisho wake ni ndiyo asilimia mia moja? Kama mchango wa maoni ya wabunge hauwezi kusaidia kubadilisha chochote ndani ya bajeti inayowasilishwa na serikali, ina maana gani basi bajeti hiyo kupelekwa Bungeni? Huku si kufuja fedha za walipakodi wa Tanzania? Kama wabunge hawana mchango wowote kwa bajeti, kwa nini kuijadili? Ni busara na ni kubana matumizi kama serikali ingeandaa Bajeti na kutusomea na maisha yakaendelea kama kawaida kuliko kupoteza muda na fedha nyingi tukijadili kitu ambacho kimefanyiwa maamuzi tayari! Wabunge wanaviogopa vyama vyao vya siasa kuliko wanavyowaogopa wananchi waliowatuma Bungeni; Mbunge anapotangazwa na Tume ya uchaguzi, anakuwa si mbunge wa chama bali ni mbunge wa wananchi wa jimbo zima; hivyo kukiogopa chama chake wakati wa kujadili maswala ha kitaifa ni kuwasaliti na kuyazika maendeleo ya wananchi waliomtuma Bungeni. Jinsi Bunge letu lilivyo hivi sasa lenye wabunge wengi wa chama kimoja chenye kujali maslahi yake na kuziba masikio kwa kilio cha wananchi walio weni, hata mswada wa kutunga sheria ya kuruhusu madawa ya kulevya ukiwasilishwa Bungeni utapitishwa, maana ni utamaduni wa “ndiyo” na “kuunga mkono asilimia mia moja” bila kutafakari na kuzingatia maoni ya wananchi.

Mfano mzuri ni Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa juzi Bungeni. Uliletwa Bungeni ujadiliwe; lakini jinsi  mjadala ulivyokwenda ilijionyesha wazi kwamba mpango huo ulishapitishwa tayari na yeyote aliyekuwa na maoni tofauti alionekana kama msaliti. Swali la kujiuliza ni kama  Mpango huo ulishapitishwa tayari, kwa nini ulipelekwa Bungeni? Ili wa wabunge wetu wapate posho? Ili tutambue kwamba CCM ndicho chama tawala? Hoja hapa si kuupinga mpango huo, na ni imani yangu kwamba hata wabunge waliokuwa na maoni tofauti si kwamba walilenga kuupinga mpango wenyewe. Ukweli ni kwamba hata wale waliouandaa mpango huo si malaika; na si kweli kwamba kabla ya kuuandaa walizunguka nchi nzima kuomba maoni ya wananchi juu ya mpango huo. Kuna wananchi wanaoishi pembezoni na hasa wanawake; waliulizwa juu ya mpango huu? Mbona hatuoni vizuri mikakati ya kuwanufaisha walio pembezoni ndani ya mpango wenyewe? Mheshimiwa Mnyika, Mbunge wa Ubungo alihoji juu ya Barabara ya Morogoro ambayo hivi karibuni itapanuliwa; mradi wa Mabasi yaendeayo kasi. Lakini ndani ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano haionyeshi kwamba zitatengenezwa barabara mbadala za kuingia katikati mwa jiji wakati barabara ya Morogoro ikijengwa upya: Msongamano wa magari utakaojitokeza wakati huo, haukutiliwa maanani na waandaaji wa Mpango huo? Pia Mnyika alihoji juu ya huduma ya maji, wakati mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaongelea mpango mpya wa huduma ya maji, bado mpango uliokamilika “ wa Wachina” bado maji hayajatoka! Hizi ni hoja za msingi kuzipuuza ni kujitangazia hali ya hatari, kama si leo ni kesho. Maana kama ni mpango wa maendeleo ya watanzania ni lazima watanzania wote washirikishwe; yasiwe ni mawazo ya mtu mmoja, kwamba siku akiondoka basi na mpango mzima unakufa; usiwe mpango wa chama kimoja kwamba siku kikiondoka madarakani mpango mzima unakufa.

Mpango huu wa miaka mitano kwa bahati mbaya au nzuri unakuja wakati Tanzania inasherehekea miaka hamsini ya uhuru wake; lakini pia unakuja wakati tumeshuhudia mipango mingi ya maendeleo na kukuza uchumi ambayo mafanikio yake yakama yanaonekana basi ni kwa watu wanaoishi dunia nyingine na wala si hapa Tanzania. Ndio maana watu wanakuwa na maswali mengi juu ya tumefanya nini ndani ya miaka hamsini. Kwamba yaliyoshindikana ndani ya miaka hamsini yatawezekana ndani ya miaka mitano? Kuuliza hivyo haina maana kwamba hatujafanya chochote ndani ya miaka hamsini; kuishikia bango hoja hii kwamba kuna watu wanasema Serikali haijafanya chochote ndani ya miaka hamsini ni kutaka kuipotosha hoja yenyewe:

Tanzania, imefanya mengi ndani ya miaka hamsini: ukiachia mbali wimbo wetu wa taifa wa “Amani na Utulivu”; kwenye michezo tunakuwa wa mwisho, tunaimba “Amani na Utulivu”, uchumi wetu unadidimia, tunaimba “Amani na Utulivu”, kiwango cha elimu kinashuka tunaimba “Amani na Utulivu”, kipindupindu, malaria na magonjwa ya kusendeka  yanatuteketeza hadi tunakimbilia Loliondo tukiimba, “Amani na Utulivu”, rasilimali zetu zinachotwa na wajanja wachache, tunaimba “Amani na Utulivu; Tulijenga Siasa ya Ujamaa na kujitegemea; ikafa na tukaizika. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii? Tulianzisha mashirika ya umma yakafa na kuzikwa. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii? Tulianzisha maduka ya vijiji yakafa yote. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii? Tulianzisha viwanda vikafa vyote na kuzikwa. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii? Tulikuwa na sekondari nzuri zikijulikana ndani na nje ya nchi, kama  vile Ihungo, Tabora Boys, Milambo na nyingine nyingi, ubora wa shule hizi umekwenda wapi? Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani? Chuo Kikuukuu cha Dar-es-Salaam kilikuwa tishio Afrika nzima na duniani kote. Ubora wa chuo hiki umekwenda wapi? Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii?

Ndani ya miaka hamsini hatuwezi kutengeneza wembe! Hatujavumbua kitu chochote zaidi ya panya wa kutegua mabomu! Tunanunua hata njiti za kuchokonoa meno kutoka nchi za nje. Viongozi wetu wakiugua wanakimbilia nchi za nje na kule wanatibiwa na madaktari wetu walioikimbia nchi. Ndani ya miaka hamsini tumezalisha  madaktari wengi na namba kubwa imekimbilia nchi za nje kutafuta maslahi zaidi. Ndani ya miaka hamsini tumenunua ndege ya raisi wakati tunaomba msaada wa kujenga vyoo kwenye mashule yetu. Ndani ya miaka hamsini tumenunua magari ya kifahari kwa viongozi wetu wakati tunaomba msaada wa fedha za kuiendesha serikali yetu.

Ndani ya miaka hamsini Tanzania bado tuna matatizo mengi. Wale maadui tuliowatangaza wakati wa Uhuru: Ujinga, maradhi   na umaskini,  bado yametuzunguka. Ndio maana ninapendekeza kwamba kuna haja wabunge wetu kutengeneza Jukwaa la majadiliano ndani ya majimbo yao; wapate nafasi ya kuwasikiliza watu na kupokea maoni yao. Hii itawasaidia kuondokana na utamaduni huu uliojengeka wa mbunge kuwasilisha maoni yake binafsi na kuegemea zaidi kwenye chama chake badala ya kuegemea kwa wananchi waliomtuma bungeni.

Wabunge wetu waige mfano wa TGNP; huu ni mtandao a Jinsia Tanzania; ni shirika la kiraia na kiuanaharakati, linalotetea mabadiliko ya -kijamii kwa mtazamo wa kifeministi, ambayo yanalenga kwenye usawa wa jinsia, ukombozi wa wanawake, haki za -kijamii, kufikia na kumiliki rasilimali kwa wanawake, vijana na makundi mengine yaliyoko pembezoni. Dhana ya TGNP ni kujenga tapo la mabadiliko katika jamii, ambalo litachangia kuwepo kwa jamii yenye mabadiliko, ambayo inatambua na kuthamini masuala ya jinsia, demokrasi, haki za binadamu na haki za -kijamii.

TGNP ilianzisha jukwaa la majadiliano. Kila Jumatano jioni pale Mabibo – Dar-es-salaam kuna mijadala inaendelea.  Ni mijadala ya wazi inayomkaribisha kila mtu. Wanajadilia maswala mbali mbali ya -kijamii na siku hizi wanaendesha mijadala juu ya katiba mpya. Wabunge wetu wangekuwa wanatembelea jukwaa hili ( Wabunge wengi wa Tanzania wanaishi Dar-es-Salaam) wangeweza kupata mengi na kutambua mahitaji ya wananchi; pia wangeweza kujifunza mbinu za kuanzisha majukwaa kama haya kwenye majimbo yao. Ni kupitia kwenye majukwaa ya majadiliano tunaweza kuwa na uwakilishi wa kweli na wenye tija kwa taifa letu.

Mbali na jukwaa la majadiliano la kila Jumatano, TGNP, inaandaa pia matamasha ya jinsia. Kila baada ya miaka miwili kuna tamasha la Jinsia pale Mabibo. Tamasha la jinsia ni nafasi ya wazi kwa ajili ya watu binafsi, mashirika na mitandao, walio katika mapambano yanayofanana, kubadilishana uzoefu,  taarifa, kujengana uwezo, kusherehekea mafanikio na kutathmini changamoto zilizo mbele yao, kujenga na kuimarisha mitandao; na kupanga kwa pamoja mikakati kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya -kijamii kwa mtazamo wa kifeministi, kujengeana uwezo ili kuchangia katika mijadala ya wazi kuhusu maendeleo ya jamii na binafsi.

Mwaka huu mwezi wa tisa kuanzia tarehe 13 hadi 16, TGNP itaendesha tamasha la jinsia la kumi na mada kuu ya tamasha hili itakuwa ni Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Ajira na Maisha Endelevu. Ni Tamasha linalokuja wakati kumejitokeza wimbi kubwa la uporaji wa ardhi. Serikali bado ina kigugumizi juu ya wimbi hili na baadhi ya viongozi wa serikali wanashiriki wimbi hili la kupora ardhi. Hivyo ni wakati mzuri wa kukutana na kujadiliana juu ya swala hili na mengine mengi. Haina maana kukaa na kupanga mpango wa maendeleo wa miaka mitano wakati ardhi inaporwa. Tunajua kwamba uchumi  wetu unategemea kiasi kikubwa sekta ya Kilimo; kama wananchi wetu hawana uhakika wa ardhi yao; kama ardhi inaporwa na matajiri wakishirikiana na wageni; wananchi watapata wapi ardhi ya kulima na kuzalisha? Hata hivyo ni muhimu kutambua kwamba ardhi ndio uhai wa kila binadamu. Bila ardhi hakuna uhuru!

Ni bahati mbaya kwamba viongozi na wabunge wetu wanalikwepa tamasha hili. Tamasha la jinsia la tisa, sikubahatika kukutana na kiongozi yoyote kwenye tamasha hilo, hata viongozi wanaojulikana kuwa wapambanaji na watetezi wa haki za binadamu na wapenda maendeleo ya Tanzania, sikuwaona kwenye tamasha hili. Natumai mwaka huu viongozi wetu na wabunge watafika kwenye tamasha hili la jinsia, maana kila mwenye akiri nzuri na kujali uhai wa taifa letu anaona wazi kwamba sasa tunayumba,  bila kuwa na majukwaa kama hili la TGNP na mengine mengi, tunazama! Napenda kuwashauri viongozi wetu na wabunge  kwamba matamasha kama hili la TGNP na mengine yanayoruhusu mijadala ya wazi ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu. Ni muhimu kuwasikiliza watu kabla ya kukaa na kuwapangia mipango ya miaka mitano. Unaweza kufikiri wananchi wanahitaji maji, kumbe wao wanahitaji moto!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment