WANYARWANDA WANAMKUBUKA MWALIMU.


Mwalimu Nyerere alikuwa Baba wa taifa la Tanzania, Baba wa Afrika na Baba wa watetea haki za binadamu duniani kote. Jambo hili inajidhihirisha wazi kila mwaka watu wanapokusanyika kumkumbuka na kumwombea. Sala kubwa ni ile ya kumtaka Mwenyezi Mungu, kumweka kwenye kundi la watakatifu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hapa Tanzania, kila mwaka tarehe 14.10.2011 ni Nyerere Day na ni siku ya mapumziko. Afrika kusini nao siku hii ni ya   kumkumbuka Mwalimu kwa majadiliano na tafakuri juu ya mawazo yake na mawazo mengi yanayofanana na ya Mwalimu ya Haki za binadamu na maswala ya uchumi wa dunia hii ya Utandawazi. Kule Amerika, wapenda amani na watetezi wa haki za binadamu wanakusanyika kusali na kuomba siku ya kukumbuka kifo cha mwalimu Nyerere. Serikali ya Rwanda, imetangaza rasmi tarehe 14. 10. 2011 kuwa ni Nyerere Day. Wanyarwanda wanasema kwamba kumbukumbu ya mwalimu ni Sherehe, maana Mwalimu aliacha mambo mengi mazuri nyuma yake.

Sherehe hizi za kumkumbuka Mwalimu nchini Rwanda zinaratibiwa na Jumuiya ya Urafiki baina ya Wanyarwanda na Watanzania – RWATAFA (Rwanda Tanzania Friendship Association). Kwa faida ya msomaji wa makala hii ni bora kutambua kwamba RWATAFA ina ndugu yake Tanzania,  Jumuiya ya Urafiki baina ya Watanzania na Wanyarwanda –TARAFA (Tanzania Rwanda Friendship Association). Kwa pande zote mbili Jumuiya hizi za urafiki zimesajiliwa na kutambuliwa kisheria.

Mwaka huu sherehe za kumbuka Mwalimu Nyerere zimefanyika kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Kigali-KIST kwa ibada nzuri ya misa iliyoongozwa na mapadri watatu walioishi Tanzania na baadaye ngoma, nyimbo, mashairi na hotuba za kumbukuka Mwalimu Nyerere.

RWATAFA, chini ya mwenyekiti wake Mzee Isidore Gahamanyi katika jitihada zake za kutaka kudumisha undugu na urafiki na TARAFA, iliamua mwaka huu kuwaalika Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Kagera, Wabunge wa mkoa wa  Kagera, Madiwani wa Mkoa wa Kagera, Walimu wakuu wa shule ambazo wakimbizi wa Rwanda walisomea nchini Tanzania, na wawakilishi wa TARAFA, ili kushiriki nao kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere. Ujumbe wa TARAFA kutoka Dar-es-Salaam uliongozwa na Mwakilishi wa mwenyekiti na Mama Eva Chiwele aliyemwakilisha katibu wa Tarafa. Kwa bahati mbaya wabunge wote hawakuweza kufika Kigali kwenye sherehe hizi, kwa sababu wako kwenye vikao vya kamati za Bunge, lakini Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Kanali mstaafu Fabian Massawe, akiongozana na Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali mstaafu Salum Nyakonji, Mkuu wa wilaya ya Missenyi/Karagwe Kanali mstaafu Issa Njiku, mkuu wa wilaya ya Muleba Bibi Angelina Mabula, Mkuuwa Wilaya ya Biharamulo Bwana Kahindi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Karagwe Bwana S.R.Kashunju, Mwenyekiti wa  Halimashauri ya wilaya ya Ngara Bwana John Shimimana, Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Karagwe bwana Alex Bantu, Kaimu Mkurugenzi wa wilaya ya  Karagwe bwana Ernest Kahabi, madiwani wa Ngara, Biharamulo na Karagwe, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Muyenzi, Ngara Mama Consolata Ndayagowe na wajumbe wa TARAFA, Mama Eva Chiwele na mwakilishi wa Mwenyekiti wa TARAFA walifika Kigali kwenye sherehe hizi za Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere.

Makala hii ina malengo makuu matano: Kwanza ni kuwa habarisha watanzania kwamba Wanyarwanda wanamkumbuka na kumuenzi Mwalimu kwa heshima kubwa. Mwandishi wa makala hii ameshuhudia mwenyewe jambo hili. Wanyarwanda wanasema wana sababu nyingi za kumkumbuka mwalimu: Wanasema,  baada ya vita ya 1959, Umoja wa Mataifa uliamua wakimbizi wa Rwanda wapelekwe Canada, lakini mwalimu alikataa na kuwapatia hifadhi Tanzania, na kwamba wakimbizi wa Rwanda waliokwenda Burundi, DRC na Uganda, hawakupata uraia wa nchi hizo, lakini wale waliokimbilia Tanzania walipatiwa uraia, walisoma kwenye shule za serikali, walitibiwa kwenye hospitali za serikali na walipata huduma zote kama watanzania wengine, na kwamba mauaji ya kimbali yalipotokea, Mwaimu Nyerere, alikuwa kiongozi wa kwanza duniani kukemea na kuyalaani mauaji hayo.

Lengo la pili la makala hii ni kuwashukuru wanajumuiya ya RWATAFA, kuwakaribisha watanzania na kuwatunza nchini Rwanda, kuanzia tarehe 14.10.2011 hadi tarehe 18.10.2011. Ukarimu wao ulikuwa mkubwa mno, Mungu peke yake ndo anaweza kuulipa wema huo.

Tatu ni kuishukuru Nyerere Foundation, kwa kukubali kulipa tiketi za ndege za Kwenda Kigali na Kurudi Dar-es-Salaam za Mwakilishi wa Mwenyekiti wa TARAFA na mama Eva Chiwele, aliyemwakilisha katibu wa TARAFA kwenye sherehe hizo. Ni jambo la kujivunia kuona Nyerere Foundation, inazilea na kuziwezesha jumuiya zinazojitokeza kumuenzi Mwalimu Nyerere. Ni imani yetu kwamba Nyerere Foundation, itaendelea na kazi hii nzuri ya kuilea TARAFA,  ili Jumuiya hizi mbili TARAFA na RWATAFA ziwe daraja imara la kuunganisha Tanzania na Rwanda.

Nnne ni kuwajulisha watanzania kwamba Rwanda kuna utulivu na amani. Nchi hii ya jirani ni fursa nzuri kwa watanzania kwenda na kuwekeza. Kuna watanzania ambao wameanza kuwekeza Rwanda na wataalamu wengi wanaofundisha kwenye vyuo vya Rwanda wanatoka Tanzania. Hata hivyo bado kuna nafasi kubwa ya kuwekeza nchini Rwanda. Nchi hii sasa hivi inapiga hatua kubwa ya maendeleo. Mji wa Kigali ni msafi kuzidi miji mingi hata na ya Ulaya ambao nimewahi kuitembelea. Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe, alisema ni lazima ajifunze siri ya usafi huo ili naye afanye hivyo mkoani Kagera. Mkuu wa Wilaya ya Muleba Bi Angelina Mabula, alituchekesha aliposema “ Usafi wa Kigali unatisha, kiasi hata miti inaogopa kupukutisha majani”. Ukweli si kwamba miti inaogopa kupukutisha majani, bali kuna watu wanafanya usafi kila wakati. Mkuu wa wilaya ya Biharamulo, Bwana Kahindi, alilalamika kwamba watu wake wa Biharamulo wanahama hama, hivyo ni vigumu kufikia hatua ya usafi wa Rwanda, lakini alisema kwa vyovyote vile ni lazima afanye jitihadi kuuweka mji wa Biharamulo katika hali  ya usafi kama alivyoona kule Rwanda.

Tano, ni kuishukuru serikali ya Rwanda, Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania na Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda. Mwaliko wetu ulikuwana ni wa wananchi, maana TARAFA na RWATAFA wanalenga kujenga mahusiano ya wananchi kwa wananchi. Hata hivyo serikali ya Rwanda ilikuwa tayari kukutana na sisi na kutuelezea maendeleo, matumaini na changamoto nchini Rwanda. Tuliweza kukutana na Mawaziri, Maseneta, Wabunge, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Jambo la kufurahisha na kujifunza ni kwamba viongozi hawa wote umri wao ni kati ya miaka 30 hadi 45. Vijana ndo wanaiongoza nchi, wazee wamebaki kama washauri. Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania, ulitusaidia ushauri wakati wa kuandaa safari yetu ni mlezi wa karibu wa TARAFA. Balozi wa Tanzania nchi Rwanda, Dk. Marwa Mwita Matiko alishiriki na sisi sherehe za kumbukumbu ya Mwalimu na kutukaribisha Ubalozini.

Kusema kweli Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, hapa Kigali, lilikuwa ni tukio la kujenga undugu kati ya Tanzania na Rwanda. Na jambo la kufurahisha ni kwamba undugu huu unajengwa katika ngazi ya wananchi kwa wananchi. Ni imani ya RWATAFA na TARAFA kwamba undugu ukijengeka baina ya wananchi wa nchi hizi mbili, serikali zitatekeleza zinataka zisitake.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment