MWANA MAMA MAREHEMU DAKTARI YVONA SWAI

Leo katika safu yetu ya Mwana mama, nawaletea Marehemu  Daktari Yvona TwagilaYesu Swai, Mtanzania mwenye asili ya Rwanda ambaye alilitumikia taifa la Tanzania kwa uaminifu na uzalendo uliotukuka. Labda mambo haya ya kufanya kazi kwa uamini na uzalendo yanazaliwa kwenye damu? Baba wa Daktari Yvona, ambaye naye ni Daktari, ndiye daktari wa kwanza kugundua mgonjwa mwenye virusi vya Ukimwi mwaka 1983 katika hospitali ya Ndolage. Ni daktari ambaye pamoja na uzee wake wa miaka 82, bado anaendelea kuwahudumia watanzania. Jina la Daktari TwagilaYesu, linasikika mkoa mzima wa Kagera, Tanzania na hata kwenye mataifa mbali mbali maana mzee huyu amezunguka dunia nzima akielezea na kufundisha juu ya ugonjwa hatari wa Ukimwi. Amefanya kazi kwa uzalendo na anaendelea kuchapa kazi kwa uaminifu mkubwa.
 Katika mpangilio wangu wa kuwaletea wasifu wa mwana mama mmoja kila siku ya Jumamosi, nilikuwa na mpango wa kuwaletea Mwana mama Daktari Yvona Swai, lakini kwa vile alikuwa anaumwa kwa muda mrefu, sikutaka kuandika juu yake bila kumjulia ali . Nilifunga safari hadi Bukoba na kwenda kijijini kwao Kamachumu-Bukoba, huko nilikutana na Baba yake Mzazi ambaye naye ni Daktari TwagilaYesu. Bahati mbaya siku hiyo niliyofika nyumbani kwao, ndiyo siku Mungu alimuita kwake mpendwa wetu Daktari Yvona Swai. Hivyo sikuweza kuongea naye! Atazikwa Moshi siku ya Jumamosi tarehe 30.3.2013. Mungu amlaze mahali pema peponi!
Daktari Yvona Swai, alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mgongo. Alifanyiwa upasuaji na kupona, lakini baadaye ulijitokeza ugonjwa wa kansa ambao umemsumbua zaidi ya miaka miwili hivi. Alijitahidi kupambana na ugonjwa huo bila ya kukata tamaa. Mama huyu alikuwa mchapakazi na wakati mwingine hakujihurumia. Nakumbuka kumgombeza, nilipoikutana naye akiendesha gari kubwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo. Jibu lake, wakati ule nikilikumbuka leo hii tunapouaga mwili wake, machozi yanatoka. Alinijibu hivi: “ Kaka, sipendi kuendesha gari, lakini nikilala nani atawatunza watoto wangu?...”. Muda wote walihangaikia watoto wake. Sasa amelala milele, je nani atawatunza watoto wake? Je Mungu anakisikia kilio hiki? Na kama anasikia, amekubali kumtenga Yvona na watoto wake? Amekubali watoto hawa wabaki yatima? Mipango yake ni mkubwa, tubaki kusema tu Jina lake lihimidiwe!
Watu wa Karagwe, Bukoba na Tanzania nzima wamepata pigo la kuondokewa na Daktari huyu ambaye kama walivyo madaktari wanaofanya kazi vijijini alikuwa mchapakazi. Kwa miaka yote aliyoifanya ameokoa maisha ya watu wengi hasa wanawake na watoto. Alifanya kazi bila kujihurumia na bila kusubiri mshahara; madaktari wanaofanya kazi vijijini, pamoja na kuunga mkono mgomo wa madaktari wenzao, pamoja nao kutaka kufanya kazi katika mazingira mazuri hawakuacha kuwahudumia watu. Kama serikali ingekuwa sikivu na yenye shukrani madaktari wanaofanya kazi vijijini na hasa Madaktari wasaidizi popote walipo wangeshukuriwa kwa namna ya pekee. Daktari Yvona, aliendelea kuchapa kazi kwa moyo wote. Siku za mwisho wa maisha yake alikuwa  Katibu mtendaji wa Shirika la Msalaba mwekundu mkoa wa Kagera. Alikuwa mstari wa mbele kushughulikia majanga ya kila aina yaliyokuwa yakijitokeza mkoa wa Kagera na kwingineko. Aliendesha kwa ufanisi mradi wa kukusanya damu salama na kuiweka kwenye benki ya damu kwa matumizi ya  baadaye.
Daktari Yvona, alizaliwa tarehe 23.8.1960, alisoma shule ya msingi Kashasha na sekondari ya Kilosa. Alipomaliza kidato cha sita alisomea Diploma ya uganga katika Chuo cha Bugando na baadaye alijiendeleza hadi kuwa Daktari Msaidizi. Pia alijiendeleza kwa kozi mbali mbali katika nyanja ya Afya.
Daktari Yvona, aliolewa na Daktari Swai, ambaye walikutana Karagwe, wote wakiwa watumishi wa serikali. Mungu aliwajalia watoto wanne, Lilian, Sylivia, Rogers na Frank. Kwa mapenzi ya Mungu, kama  tunavyosema na kuamini siku zote, Daktari Swai, alipoteza maisha yake kwenye ajali ya MV Bukoba mnamo mwaka wa 1996. Bahati mbaya mwili wa Dakta Swai hakupatikana, hivyo kuongeza majonzi kwa Daktari Yvona,  ndugu  na jamaa wote.
Wakati ule watoto wote walikuwa bado wadogo. Daktari Yvona, alijifunga kibwebwe kuwalea watoto wake na kuendelea kuchapa kazi za kulijenga taifa letu. Huyu ni mama wa mfano ambaye ameweza kwa kiasi kikubwa kuwatunza watoto akiwa amesimama peke yake bila mme wake. Leo hii Lilian ni mwalimu, Sylivia amemaliza shahada ya kwanza ya Ufamasia,  Rogers na Frank wameanza mwaka wa kwanza shahada ya udaktari. Ili kukamilisha usemi wa Daktari TwagilaYesu, baba wa Daktari Yvona, kwamba udaktari uko kwenye damu!
Tuna utamaduni wa kumsifia mtu akiwa amekufa. Ndo maana nilitaka kuandika wasifu huu wa Daktari Yvona akiwa hai, ila imeshindikana. Binafsi nimepata bahati ya kufanya kazi na mama huyu ambaye leo hii tunamlilia. Huyu alikuwa ni mama wa aina yake! Aliwapenda watu wote, hakuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile, alishirikiana na wasomi, walishirikiana na watu wa kawaida kabisa hadi wale wa vijiweni! Hakujiona wala kujikweza. Bila kuambiwa au kumkuta kazini kwake, ilikuwa vigumu kutambua kwamba huyu alikuwa ni daktari. Ni mama ambaye huruma ilikuwa kubwa kuliko uwezo wake! Pamoja na kwamba baada ya kuondokewa na mume wake, alikuwa akifanya kila kitu kuwasomesha na kuwatunza watoto wake, hakuacha kutoa misaada kwa wengine.
Kuna mambo mengi niliyojifunza kwa mama huyu na la kwanza ni hili la “kaka” na “dada”. Watu wote walikuwa “Kaka” na “Dada”. Kusema kweli alijitahidi kiasi chake kuishi maisha ya hayo. Binadamu ni binadamu, inaezekana aliteleza hapa na pale, lakini kwa asilimia kubwa “Udada” na “Ukaka” alikutimiza. Hili limejionesha wazi wakati wa msiba wake jinsi watu wa kila aina, watu wa kutoka sehemu mbali mbali walivyofika kumlilia na kumuaga.
Jambo jingine jingine nililojifunza kwa mama huyu ni Kumtegemea Mwenyezi Mungu, na siku zote kuomba na kushukuru. Magumu mengi aliyoyapata katika maisha yake, kama lile la kuondokewa na mme wake, silaha yake kubwa ilikuwa ni kuomba na kushukuru. Niseme tu kwamba mama huyu alikuwa mcha Mungu!
Na jambo jingine ni kusamehe na kusahau. mama huyu hakutunza kinyongo. Alijaliwa kusahau haraka wale waliomtenda vibaya. Kwa kuiga tabia tunaweza kujenga jamii isiyokuwa na visasi.
Mama huyu alinifundisha kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa uzalendo na hasa kuwatumikia watu maana hiyo ndiyo faraja ya kuendelea kuishi hapa duniani. Daima alisema “ Kaka sisi si bora zaidi ya wale waliotutangulia, kama Mungu ametupendelea kuendelea kuishi, basi tutumie nguvu zetu na uwezo wetu kuwatumikia watu. Ipo siku nasi tutaitwa na kuiacha dunia hii…”. Siku yake ya kuitwa imefika, ametuacha nyuma ingawa hatuko bora kuliko yeye aliyetutangulia. Na sisi siku yetu yaja, hivyo faraja yetu iwe kuwatumika watu!
Tumesikitika kumpoteza dada yetu mcheshi, mwenye utundu, mbunifu na shupavu wa kupambana na changamoto za maisha. Mungu amlaze mahali pema peponi Daktari YvonaSwai.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment