https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjVSV1caXKW6EdPOn47eLUoj-1ng9yUB3SeRerLVlpgYQuj_MydJbrffH_FLd_82YCFTF4j8VEpUZnbkC7ope94mBFPglk0V9sDPNdaMPwHf-8eq_hyphenhyphenNdM8niFuTxKa9SHtsHdtOpfFupdH/s1600/1597.jpg


MWANA MAMA CHRISTOWAJA GERSON MTINDA
Leo katika safu yetu ya Mwana mama tunawaletea Mheshimiwa Christowaja Mtinda, msomi ambaye ameamua kuingia kwenye siasa. Kuna kelele nyingi kwamba wasomi wanatelekeza taaluma zao na kutimkia kwenye siasa; na mara nyingi wamelaumiwa wanaume! Kumbe kuna na wanawake wasomi waliotimkia kwenye siasa. Mama huyu ambaye alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, sasa ni mbunge wa viti maalum kupitia chama cha CHADEMA.
Pia kumekuwa na tuhuma kwamba CHADEMA, wanachagua wabunge wa viti maalum kwa upendeleo na wakati mwingine bila kuangalia uwezo na elimu ya mhusika. Mama huyu ni mfano mzuri wa Mbunge wa viti maalum, ambaye ana uwezo mkubwa hata wa kupigania Jimbo lake akalipata. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010, alikuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za chama chake ili kuhakikisha kinapata wabunge wengi wa kuchaguliwa na Mgombea  urais kupitia chama chake anafanikiwa kuingia Ikulu. Ingawa hilo halikuwezekana, lakini kura nyingi alizozipata Dr.Slaa kwenye uchaguzi mkuu huo na mchango wa Mheshimiwa Christowaja, ulikuwepo.
Si lengo la safu hii kugeuka uwanja wa wanasiasa! Tukifanya hivyo tutajiingiza kwenye matatizo makubwa ya kufuatwa na waheshimiwa ili tuandike habari zao. Tunaandika bila kuombwa; tunaandika kwa kumfuatilia Mwana mama kwa muda na kubaini mchango wake katika taifa letu. Na tunafanya hivyo baada ya kutafiti kwenye magazeti na mitandao ya kijamii na kuona kwamba Mwana Mama huyu hajaandikwa sana, hasa juu ya mchango wake. Na kusema kweli mama wengi wanafanya mambo mengi mazuri, lakini hawaandikwi wala kutajwa popote! Tunalenga kutoa nafasi ya wanawake wanaotoa mchango mkubwa katika jamii, lakini hawajulikani na habari zao haziandikwi, wajulikane na kusikika. Ni imani yangu kwamba kwa nafasi ya Ubunge, Christowaja, anaandikwa sana, maana ni miongoni mwa wabunge wanawake wanaochangia hoja Bungeni. Hata hivyo mwana mama huyu hakuanzia Bungeni na wala hakuwa kwenye siasa muda mrefu.  Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mwanafunzi wa digrii ya uzamivu chuo kikuu cha Sussex Uingereza. Hivyo mama huyu ni msomi. Yangejulikana haya, uzushi kwamba Chadema, wanachaguana tu bila vigezo yasingesikika.
Sina lengo langu kuandika maisha binafsi ya Mheshimiwa Christowaja, ninamlenga mwana mama Mwalimu, ambaye amechangia kufundisha watoto wetu, watoto wa taifa hili la Tanzania. Ninaandika juu ya Christowaja, mama mwenye bidii na kiu ya elimu. Mama huyu amepanda hatua kwa hatua. Alianza na diploma, akapanda hadi kupata digrii ya kwanza, digrii ya uzamili hadi kuelekea uzamifu. Ni mfano mzuri kwa wanawake wengine ambao kwa namna moja ama nyingine wamepumbazwa kiasi cha kuambiwa “ Mwanamke anaweza akiwezeshwa”; wakati ukweli wenyewe ni kwamba Mwanamke anaweza siku zote.
Sababu nyingine kubwa ya kuamua kuandika juu ya Mheshimiwa Christowaja, ni msimamo wake wa kuunga mkono hoja zote za kizalendo bila kutanguliza chama chake. Pamoja na mapenzi makubwa anayoyaonyesha kwa chama chake cha Chadema, lakini mama huyu amekuwa miongoni mwa wabunge wachache sana wanaoangalia matatizo ya taifa letu bila ushabiki wa vyama vya siasa. Pamoja na ukali wa kawaida wa vyama vya upinzani, maana wao wanafanya kazi ya kuisahihisha na kuisimamia serikali, mama huyu amekuwa akiwasilisha hoja zake kwa busara na hekima. Ni mpole kwa kuongea, lakini mkali kwa kupenyeza hoja bila kuipindisha. Huyu ni mpambanaji kama walivyo wabunge wengine wa vyama vya upinzani, na kwa sababu anazungumza na kuchangia; hatuna budi kuhakikisha anajulikana na habari zake kuandikwa.
Mama huyu ni miongoni mwa wabunge walio upande wa wanyonge; watetezi wa watoto, anatetea elimu bora kwa watoto wetu, wanawake na watu walio pembezoni. Ni mwana mama anayelilia uongozi bora katika taifa letu, anapiga vita rushwa na ufisadi. Ni mwanaharakati ambaye anapigania rasilimali za Tanzania kuwanufaisha watanzania wote. Pia ni miongoni mwa wabunge waaminifu wa kukalia viti vyao. Bunge letu lina sifu ya kuwa na viti wazi. Wakati wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, tulimsikia Mbunge, akilalamika Bunge kujadili wizara nyeti kama ya kilimo wakati Bungeni kulikuwa na Mawaziri watano na manaibu mawaziri watano. Pia kwa kuangalia kupitia luninga mtu aliweza kuona viti vingi vikiwa vitupu. Na wakati mwingine hata vile ambavyo vina watu, wabunge wanakuwa kwenye michapo wakati Bunge likiendelea. Kinara wa zoezi hili ni Waziri Mkuu, ambaye mara nyingi anaonekana akijadiliana na watu kwenye kiti chake wakati Bunge likiendelea. Pamoja na utetezi kwamba anakuwa kazini, ukweli una baki kwamba anakuwa hafuatilii yanayojadiliwa Bungeni. Kama ni kazi, si ni bora abaki kwenye ofisi yake, kuliko kuwadanganya watu yuko Bungeni wakati anaendesha mikutano ndani ya mkutano!
Hata yeye Mheshimiwa Christowaja, atashangaa, kusoma habari hizi, maana tunaandika bila kuhojiana naye. Tunaandika yale tunayoyaona juu yake. Tunaandika ili wengine wakamtafute na kufanya naye mahojiano. Hivyo katika makala zitakazofuata, tutasikia juu ya familia yake na mengine mengi juu yake. Tunaandika ili wengine wajiulize huyu ni nani? Ni mbinu mpya ya kuwachokoza waandishi kuanza kuwafuatilia watu mbali mbali na kuwahoji na hasa wanawake ambao kwa miaka mingi wamewekwa pembeni.
Christowaja Mtinda, alizaliwa tarehe 13.5. 1968. Alisoma shule ya msingi Kititimo kati ya mwaka 1976 hadi 1982. Alijiunga na shule ya sekondari ya Msalato mnamo mwaka 1983- 1986 na kidato cha tano na sita shule ya sekondari ya Kilakala Morogoro mwaka wa 1987-1989. Alipomaliza masomo ya sekondari alijiunga na chuo cha DSA kusomea Diploma ya Material Management. Baada ya kupata Diploma hiyo, mwana mama huyu hakutulia, aliendelea kuisaka elimu na mwaka 1996 hadi 1998, alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Morogoro kusomea diploma ya Ualimu. Alipomaliza Diploma yake ya Ualimu, alifundisha shule ya Sekondari ya St Mary’s 1998- 1999 na shule ya sekondari ya Airwing ya Dar-es-Salaam, mwaka 1999-2000. Kiu yake ya elimu haikukoma na mwaka  2000 hadi 2004 alijiunga na Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam kuchukua shahada yake ya kwanza ya Ualimu. Bidii aliyokuwa nayo kwenye masomo, aliendelea na shahada ya uzamili hapo hapo chuo kikuu cha Dar-es-Salaam mwaka wa 2004-2006.
Mbali na kuwa mwalimu kwenye shule za sekondari na Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Mkwawa, mama huyu alifanya pia kazi kwenye Baraza la mitihani Tanzania. Ni mama mwenye uzoefu katika Nyanja mbali mbali. Hata na michango yake kwenye Bunge, inaonyesha kwamba si mtu aliyeingia kwenye siasa kutafuta kazi, bali ni mtu alikuwa na kazi yake; msomi, mtaalamu wa elimu na mambo mengine mbali mbali kama kufanya kazi kwenye duka la dawa la Twiga.
Huyo ndiye Mheshimiwa Christowaja Gerson Mtinda, msomi aliyetimkia kwenye siasa!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

0 comments:

Post a Comment