AGPAHI 3

TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA: USHUHUDA KUTOKA GEITA NA SHINYANGA.
 
Tarehe 26 Septemba,2013 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mheshimiwa Magalula S. Magalula, alifungua jengo la kliniki ya huduma na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU), katika kituo cha Afya Masumbwe wilaya mpya ya Mbogwe – Mkoa wa Geita. Na tarehe 27 Septemba 2013 Mheshimiwa AnnaRose Nyamubi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, akafungua jengo jingine la Kliniki ya tiba na matunzo kwa watu wenye VVU, katika kituo cha Afya Kambarage – Shinyanga mjini.
Majengo haya mawili, la Masumbwe na la Shinyanga, yamejengwa na Shirika la Kitanzania AGPAHI(Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative) kwa msaada wa watu wa Amerika, kupitia shirika la CDC (Centre for Disease Control).
Shirika la AGPAHI lilianza kazi nchini Tanzania, mwaka wa 2011, (Kwa kuzaliwa na Shirika la Kimataifa la EGPAF ‘Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation’ na kuendeshwa na watanzania) linafanya kazi zake katika Mikoa ya Geita, Shinyanga na Simiyu katika jitihada za kupambana na Virusi vya Ukimwi katika Mikoa hii mitatu kwa msaada wa watu wa Marekani na kwa kusaidiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia  Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa yaani TAMISEMI ili kuwezesha upatikanaji wa tiba na matunzo kwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi lakini pia upatikanaji wa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
 
Kwa kipekee shirika hili la AGPAHI, linakazania huduma hii ya kuzuia virusi kutoka kwa mama mwenda kwa mtoto. Kwa maoni ya shirika hili jambo hili linawezekana kabisa, kila mtu akitimiza wajibu wake; wananchi wakapima afya zao kwa hiari, serikali na wadau wengine wakatoa huduma za uhakika, tunaweza kwa asilimia 100 kuzuia virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na hatimaye kutokomeza virusi kwa watoto.
Majengo haya mawili yaliyofunguliwa Masumbwe na Shinyanga, ni mazuri na yamejengwa kisasa. Yana idadi ya vyumba 5 ambavyo ni chumba cha usajili wa wagonjwa, chumba cha ushauri nasaha, vyumba viwili vya waganga na chumba cha kutunzia dawa. Pia majengo  haya yana vyoo vizuri na vya kisasa. Ni majengo yanayolenga kupunguza unyanyapaa na watu wenye virusi kujiona wametelekezwa. Huko nyuma kwenye vituo vya afya huduma hii ilitolewa kwenye chumba kimoja na msongamano ulikuwa mkubwa kiasi cha kuwakatisha tama wagonjwa na wengine kuamua kuikimbia huduma hii.
Pamoja na majengo mawili yaliyofunguliwa, AGPAHI, inafanya kazi pamoja na watendaji wa Mkoa na Halmashauri katika kuboresha huduma kwenye vituo 68 vinayotoa huduma za matunzo na matibabu kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI na vituo 284 vinavyotoa huduma za kukinga maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto(PMTCT) katika mikoa hiyo mitatu.
Kliniki ya Masumbwe ilianza kutoa huduma ya matunzo na matibabu mwaka 2006 kwa kupata msaada kutoka shirika la CDC chini ya uratibu wa Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation na baadaye AGPAHI (Tunaweza kusema kwamba AGPAHI ni mtoto wa Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation). Hadi kufikia Juni 2013, kliniki ya Masumbwe imeweza kuhudumia jumla ya wateja 1,437, wanaume wakiwa 538 na wanawake 899.  Kati yao  ni watoto 106 walio chini ya miaka 15. Katika kliniki hii, wateja 1,030 wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU na UKIMWI na kati yao ni watoto 79 walio chini ya umri wa miaka 15. Kufikia Juni 2003 jumla ya wateja 714 walikuwa hai na kati yao watoto 50.
Kliniki ya Kambarage- Shinyanga nayo ilianza kutoa huduma mwaka 2006. Nayo kufikia Juni 2013, imeweza kuhudumia jumla ya wateja 1,713 wanaume wakiwa 488 na wanawake 1,225.Kati yao ni watoto 113 walio chini ya umri wa miaka 15. Katika kliniki hii wateja 854 wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU na UKIMWI. Kati yao ni watoto 66 walio chini ya umri wa miaka 15. Hadi Juni mwaka huu jumla ya wateja 553 walikuwa hai na wanaendelea kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU na UKIMWI, na kati yao watoto 9 chini ya miaka 15 wako hai.
Takwimu hizi zinaonyesha umuhimu wa kliniki za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI, maana idadi ya vifo inapungua sana na hasa uwezekano wa Mama wenye virusi kuzaa watoto wasiokuwa na virusi. Ushuhuda uliotolewa na wanawake 16 wa Kliniki ya Masumbwe, ni kwamba jambo hili linawezekana. Wanawake hawa wanaishi na virusi, lakini kwa vile wanatumia dawa za kufubaza virusi, wamezaa watoto wasiokuwa na virusi. Tatizo linalojitokeza ni mwitikio mdogo wa wanawake wajawazito kupima ili kujua hali zao. Mkurugenzi mtendaji wa shirika la AGPAHI Bwana Laurean Rugambwa, kwenye risala yake kwa Mgeni Rasmi, wakati wa kufungua jengo la kutoa huduma ya tiba na matunzo kituo cha Masumbwe, wilaya na Mbogwe, alieleza  tatizo hili: “ Ndugu mgeni rasmi, hatua ya kwanza kabisa katika jitihada za kuzuia maambukizi ya virusi toka kwa mama kwenda kwa mtoto ni kupima kwa hiari wajawazito wote. Taarifa zinaonyesha kuwa kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu, kinamama 2,649 tu kati ya 6,796 (39%) waliopimwa hali zao katika wilaya ya Bukombe na Mbogwe ikiwamo. Kiwango hiki ni kidogo sana hivyo ndoto ya kutokomeza maambukizi kwa watoto haitaweza kutimia. Hivyo ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana kuwafikia akinamama wengi zaidi”
Na kwa upande wa Shinyanga, Bwana Laurean Rugambwa, alieleza: “.. Taarifa zinaonyesha kuwa kwa kipindi cha Mwezi Aprili hadi Juni ni kinamama 1857 tu kati ya 2968(63%) ndio waliopimwa hali zao katika manispaa ya Shinyanga. Vile vile, katika halmashauri ya wilaya Shinyanga vijijini, kipindi cha Aprili hadi Juni, akinamama 2,434 tu ndio waliopima hali zao kati ya 4,150 (59%) ya akinamama ambao waliotakiwa kupima hali zao.  Kiwango hiki bado kiko chini hivyo ndoto ya kutokomeza maambukiki kwa watoto haitaweza kutimia.”
Ushuhuda huu wa Bwana Laurean Rugambwa, mkurugenzi mtendaji wa AGPAHI, unaonyesha kwamba “TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA” kila mwananchi akitimiza wajibu wake. Jambo hili haliwezi kutimia kwa hotuba tu za majukwaani bila kuhimizana, kushauriana, kuelekezana na kuwa na mifumo ya utekelezaji. Panahitajika jitihada za pekee kuhakikisha wanawake wajawazito wote wanapima hali zao ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Ni lazima sote kushiriki  kama alivyobainisha Bwana Laurean Rugambwa kwenye risala yake:
“ ...Zaidi ya hayo, wanaume lazima tubadili tabia, na pia tuwe tayari kupimwa afya zetu tukiwa pamoja na wenzi wetu. Tukifikia hatua hii, tutaweza kuzuia maambukizi ya VVU kwa watoto wanaozaliwa kwani baba na mama watakuwa wanajua afya zao kabla ya kuamua kupata mtoto, na mama akipata ujauzito afahamu kwamba anaweza kupata dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwake kwenda kwa mtoto. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumezuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”
Mbali na changamoto hii ya idadi ndogo ya wajawazito kupima hali zao, Bwana Laurean Rugambwa, alielezea changamoto nyingine: “ Ndugu mgeni rasmi, changamoto kubwa tunazozipata katika manispaa hii ya Shinyanga ni kupotea kwa wateja walioanza kupata huduma katika kliniki zetu, unyanyapaa wa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi katika jamii na ushiriki mdogo wa wanaume katika huduma za uzuiaji wa maambukimi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto”.
Changamoto hii ya kupotea kwa wateja, pamoja na jitihada zinazofanywa na AGPAHI na wadau wengine kuwarudisha, ziko kwenye maeneo yote ambayo AGPHAI, inatoa huduma hizi; Mkoa wa Shinyanga, Geita na Simiyu. Chanzo cha kupotea kwa wateja hawa, ni waganga wa jadi na imani za kidini. Kuna waganga wa jadi wanaowaaminisha watu kwamba wana uwezo wa kutibu UKIMWI, lakini ni ujanja wa kujipatia fedha. Pia kuna viongozi wa kiroho wanaoamini kwamba UKIMWI utapona kwa miujiza ya Mungu, matokeo yake ni watu wanaotumia dawa za kufubaza virusi, kupoteza maisha wanapoacha kutumia dawa na kukimbilia kwa waganga wa jadi na imani za kidini.
Changamoto nyingine iliyotajwa na Bwana Laurean Rugambwa, katika jitihada za shirika lake kuhudumia watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ni “ Mheshimiwa mgeni rasmi, pamoja na juhudi zetu za kutoa huduma, tunakwamishwa na uhaba wa watoa huduma katika vituo vilivyo vingi, na wengine kuacha kazi. Hapa inabidi tuangalie kwa jinsi gani tunaweza kuboresha huduma hizi kwa kutumia rasilimali watu zilizopo”
Akijibu risala ya Mkurugenzi mtendaji wa AGPAHI, Mkuu wa Mkoa wa Geita, alisema: “ Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo AGPHAI katika kuendelea kutatua changamoto hizi. Naomba nitumie nafasi hii kuwataka viongozi wote hasa timu za uendeshaji wa afya na Halmashauri zote kuhakikisha kuwa wanatengeneza mpango wakuwezesha vituo vingi vya afya kuwa na uwezo wa kutoa huduma za tiba na matunzo na hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hizo kwa urahisi.  Halikadhalika, halmashauri kupitia idara zake mbalimbali zitengeneze utaratibu unaozihusisha idara mbalimbali nje ya idara ya afya kuhakikisha kuwa wale wote waliokwisha andikishwa kwenye huduma za tiba na matunzo wanaendelea kubaki kwenye huduma. Na ni muhimu zaidi kutengeneza utaratibu utakaowezesha kuwafuatilia na kuwarudisha kwenye huduma wale wote walioacha kuhudhuria kwenye kliniki zao”.
Msimamo huu wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, ndio uliokuwa Msimamo wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, hivyo msimamo wa Serikali. Tuna imani kwamba Serikali ikitekeleza msimamo huu na kuhakikisha kuna mifumo ya kuwadhibiti waganga wa jadi wenye ujanja wa kutaka kujipatia fedha kwa ulaghai, imani za kidini ambazo zinawapumbaza watu wenye virusi kuamini kupona kwa miujiza, kuzuia watu kutoroka huduma na tiba kwenye kliniki hizi za watu wanaoishi na Virusi, mifumo ya kuhakikisha wajawazito wote wanapima hali zao, wanaume nao wanashiriki kwenye zoezi la upimaji, wahudumu wa afya wanapatikana, unyanyapaa unapungua na kila mwananchi anatimiza wajibu wake katika zoezi zima la kutokomeza UKIMWI, hapana shaka kwamba Tanzania bila UKIMWI inawezekena.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22

0 comments:

Post a Comment