Buriani Ta Mwalimu Elias



BURIANI TA MWALIMU ELIAS BILAULI LWAKATARE
Tunamlilia na kumsindikiza kwa pambio Baba yetu, Babu yetu, Mwalimu wetu, Ndugu yetu, Rafiki yetu, Jirani yetu, muumini mwenzetu  na Mtanzania mwenzetu. Wimbo wa “Engozi za Omukama..” (Upendo wa Mungu) umsindikize kwenye nyumba yake ya milele. Kwa umri wa miaka 95 na miezi 9, tuna haki ya kuimba “Engozi za Omukama”. Tulipenda kuendelea kuishi naye na kufurahia “Ubaba” na “Ualimu wake”, lakini yametimia, na jina la aliye juu lihimidiwe!
Ta Mwalimu Elias Bilauli Lwakatare, aliaga dunia tarehe 8.11.2013 jijini Dar-es-Salaam, na kusafirishwa hadi kijijini kwake Ibwera Bukoba na kuzikwa kwa heshima kubwa. Umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuaga mwili wake kwenye Ibada katika kanisa la Lutheran Msasani, na umati mkubwa uliojitokeza kwenye mazishi yake kule Bukoba ni ishara kwamba mzee huyu alikuwa miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa wa  kulijenga Taifa letu la Tanzania.
Pamoja na ukweli kwamba Mwalimu Elias, alikuwa na watoto wenye majina makubwa kama vile Bwana Samwel  Lwakatare, mtoto wake wa kwanza, ambaye kumbukumbu zinavyoonyesha ndiye Mwafrika wa kwanza kuwa General Manager wa mgodi wa Almasi wa Mwadui na badaye alishika nyadhifa  kubwa serikalini, Dkt Johnson Lwakatare, bingwa wa magonjwa ya moyo, Bwana Muganyizi Lwakatare, mwanasiasa machachari na wengine waliobaki; Mwalimu Elias Lwakatare alilijenga jina lake yeye mwenyewe na hakuruhusu umaarufu wa watoto wake uyumbishe msimamo wake ndani ya jamii. Aliishi maisha ya kawaida ya kijijini, akishirikiana na kila mwana kijiji. Kabla magari hayajawa mengi na usafiri ukiwa wa shida, Mwalimu Elias, alilitumia gari lake kuwasafirisha watu kutoka Ibwera hadi Bukoba mjini. Alikuwa dreva mzuri sana, na aliendesha gari hadi kwenye uzee wake wa miaka  themanini.
Wale wote aliowafundisha na wale waliozaliwa wamkuta amestaafu ualimu waliendelea kumtambua na kumheshimu kama Ta Mwalimu Elias. Ualimu, ulikuwa ndani ya damu yake, aliendelea kufundisha hata baada ya kustaafu na alitamani watoto wote, wa ndugu, jamaa na majirani zake wasome na kufanikiwa kama watoto wake mwenyewe. Hivyo kijijini Ibwera, alikuwa ni mtu wa kutafuta shule na kuwaelekeza wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye shule mbali mbali. Wakati ambapo shule za sekondari zilikuwa chache, Ta Mwalimu Elias, alikuwa kama mitandao ya kisasa ambayo ukibofya unapata habari yoyote unayoitafuta. Watu wengi walikimbilia kwake kupata habari za shule na elimu kwa ujumla. Aliwapenda vijana na alifurahia mafanikio ya vijana wote wa Ibwera na eneo lote la Ikimba.
Ta Mwalimu Elias, aliupenda sana mchezo wa mpira wa miguu, aliucheza na kuufundisha kwa vijana. Alipenda kuimba na alishiriki kwenye kwaya na kuiongoza, pia alikuwa kiongozi msaidizi wa kikundi cha tarumbeta. Pia alikuwa skauti na kuwaongoza vijana kwenye uskauti.

Mbali na mambo ya Elimu, Ta Mwalimu Elias, alikuwa mtu mcha Mungu. Alikuwa muumini mwaminifu wa kanisa lake la KKT usharika wa Katwe. Alilihudumia kanisa lake na kulipenda, lakini pia aliheshimu imani za watu wengine. Alikuwa karibu sana na Wakatoliki waagilikana na Waislamu. Hakuwa na ubaguzi wa kidini, na jambo hili limejionyesha wazi wakati wa mazishi yake; watu wa dini mbali mbali walishirikiana kumsindikiza kwenda kwenye nyumba yake ya milele.
Ta Mwalimu Elias, alizaliwa katika kijiji cha Kibeta jirani kabisa na mji wa Bukoba, tarehe 12/01/1918, akiwa mtoto wa kwanza wa Mama Mkalinda na Baba Ntangeki. Alikuwa na wadogo zake Paulo Kyebereka, Ephraim Mutagurwa, Josephata Katente, Geraldina na Evelina.

Msingi wa Imani na Elimu aliupata kutoka kwa Mzee Isaya Mukoyogo, ambaye alikuwa karibu na familia yao. Mafunzo ya Imani aliyoyapata kutoka kwa Mzee Isaya, yalipelekea Ta Mwalimu Elias, kuingizwa kwenye Imani ya Kikristu na kubaziwa na Mchungaji W. Hopser wa kanisa la Kashura, mchungani huyo ndiye alimchagulia jina la Elias, na kuzaliwa upya katika imani ya Kikristu, wazazi wake wa ubatizo walikuwa Mzee Isaya Mukoyogo na mke wake.

Ta Mwalimu Elias, alisoma shule ya msingi Kibeta hadi darasa lanne na kuhamia Ditrict school ya Kigarama. Enzi hizo hapo hapo Kigarama kulikuwa na Chuo cha Ualimu, hivyo alijiunga na chuo cha Ualimu na kuhitimu vizuri. Baada ya kuhitimu alifanya mazoezi ya kufundisha kwa vitendo hapo hapo Kigarama. Alipoonyesha kufuzu, aliajiriwa kama Mwalimu wa Kanisa la Kilutheri shule ya Kibeta, akilipwa mshahara  wa shilingi 18, wakati huo zikiwa ni fedha nyingi. Baada ya kufundisha kwa muda hapo Kibeta, alipandishwa cheo na kuwa mkuu wa shule hiyo. Kwa vile Ta Mwalimu Elias, alikuwa mwalimu mzuri na alifanya kazi yake kwa moyo wake wote, alipandishwa cheo tena kuwa Mkaguzi wa shule, kazi aliyoifanya kwa miaka mingi hadi kustaafu.

Ta Mwalimu Elias, mbali na kazi za Ualimu na ukaguzi wa mashule, alifanya kazi nyingine nyingi za kanisa. Alishiriki katika kutafsiri Biblia katika Lugha ya Kihaya ambayo inatumika hadi leo hii. Kazi za kanisa zilimpatia nafasi ya kusafiri sana ndani na nje ya nchi. Alitembelea nchi za Denmark, Sweden, Norway na Uingereza.
Ta Mwalimu Elias, alifunga ndoa takatifu na Mama ma Ephrazia Mitanda, katika Kanisa la KKT Kashura mnamo mwaka wa 1939. Katika ndoa yao hiyo wamejaliwa kuwapata watoto 12, wajukuu 46 na vitukuu 40. Watoto wao ni: Samuel Lweyemamu, Elisa Kaijage,Lena Hulda,Kokushubila;Emiliana Kokubelwa;Johnson,Muhumuliza;Dina Kokuganyilla; Godwin Mushobozi,Gracewell Mwesiga, Lilian Murungi;Stella Abela;Wilfred,Muganyizi na Victor Bainomugisha. Kati yao, wawili Godwin Mushobozi na Gracewell Mwesiga, wametangulia mbele ya haki, Mungu awalaze mahali pema peponi.

Ta Mwalimu Elias na mke wake Ma Ephrazia Mitanda, waliendelea kuishi Kibeta-Buguruka hadi mnamo mwaka 1952, walipohamia Ibwera, Bukoba vijijini. Na wote sasa wamezikwa huko huko Ibwera, ingawa bado wana shamba lao la Kibeta ndani ya Manispaa ya  Bukoba.

Pamoja na kumlilia Ta Mwalimu Elias, awe kwetu mfano wa kuigwa. Mzee wetu alifanya kazi za serikali, kazi za dini na kazi za kijamii bila kuwa na mgongano wa maslahi. Amekuwa muumini wa Kanisa la KKT, lakini aliwafundisha watoto wa dini zote na kuwapenda, ameshirikiana na watu wote kwenye jamii bila kuangalia imani za dini zao, hakutumia umaarufu wa watoto wake kama kinga ya aina yoyote ile au ukuta wa kumtenganisha na jamii iliyomzunguka, alikuwa mzalendo na mwaminifu wa Taifa lake na alilolitumikia kwa nguvu zote hadi siku yake ya mwisho. Apumzike kwa amani Ta Mwalimu Elias Bilauli Lwakatare. Amina.

Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22.






0 comments:

Post a Comment