TEITI

MPANGO WA UHAMASISHAJI UWAZI KATIKA MAPATO YA MADINI,GESI ASILIA NA MAFUTA UENDE MBALI  ZAIDI!

Makala iliyopita katika safu hii, tuliwaelezea mpango wa TEITI hapa Tanzania na faida zake. Maswali  yanayokuja kutoka kwa baadhi ya wasomaji wa gazeti hili, yanaonyesha wazi kwamba mpango huu bado haujafahamika vizuri na wengi wanaonyesha hawakufahamu kabisa kwamba kuna mpango kama huu napa kwetu Tanzania. Ni wazi TEITI wana kazi ya ziada ya kuhakikisha taarifa zao zinasambazwa na kufafanuliwa kwa wananchi.  Ni jambo la kujipongeza kwamba sasa kupitia mpango huu, kwa yeyote anayejali na kufuatilia masuala ya mapato katika  taifa letu, anaweza kupata takwimu za uhakika juu ya mapato yanayotokana na madini, mafuta na gesi asilia.
Ni wazi si kazi ya TEITI  kufuatilia fedha hizi zinazolipwa na makampuni ya uziduaji wa madini, mafuta na gesi asilia zinatumika vipi? Zinanunua mashangingi na kulipia safari za viongozi nje ya nchi? Zinatumika kulipia matibabu ya viongozi na vigogo wengine nje ya nchi? Zinatumika kulipa posho za wabunge na viongozi wengine serikalini au zinatumika kwa lengo la “Maisha bora kwa kila Mtanzania” na “Big results now”? Hii ni kazi ya wabunge wetu, kufuatilia na kupiga kelele juu ya matumizi ya fedha hizi. Hata na wananchi wenyewe baada ya kusoma na kuelewa taarifa hizi za  TEITI wanaweza kuhoji na kuwashinikiza wawakilishi wao, madiwani na wabunge kufuatilia kwa karibu matumizi ya mapato haya yanayotokana na madini, mafuta na gesi asilia.  Fedha hizi zitakuwa ninaingizwa kwenye mfuko wa maendeleo kwa malengo ya kujenga barabara, kununua dawa, kulipia elimu ya juu ya vijana wetu na kazi nyingine nyingi za kijamii. Je fedha hizi zinafika kweli na kufanya kazi hizi? Pamoja na ukweli kwamba makampuni haya ya uziduaji yanatuibia bado kuna ulazima wa kuhakikisha ukweli huu  na kuuelezea bila kuacha utata wa aina yoyote nyuma yake.
Ingawa bado kuna utata kwenye takwimu hizi ambazo TEITI wanatoa;  makampuni yakionyesha kulipa zaidi, na serikali ikionyesha kupokea pungufu, ni  masuala ambayo kwa ufuatiliaji wa karibu yanaweza kupata maelezo. Pia utata mwingine, kwamba asilimia 99 ya mapato yote yatokanayo na madini, mafuta na gesi asilia yanalipwa na makampuni 23, ni jambo ambalo bado linahitaji maelezo ya kina. Ni kitu gani kinatokea kwa makampuni mengine zaidi ya 400 yaliyosajiliwa  na yanafanya kazi ? Ni kwamba hayapati faidia kabisa kiasi cha kushindwa kulipa kodi, au hayazalishi chochote? Na kama hayazalishi chochote ni kwa nini yaendelee kuwepo?
Pamoja na mwanga unaotolewa na mpango huu wa TEITI ,bado kuna hoja kwamba mpango huu ungeweza kwenda mbali zaidi. Hoja yenyewe ni kwamba, kwa nini usifanywe ulinganifu wa  faida wanayoipata makampuni na kodi  wanazozilipa? Madini, mafuta na gesi asilia vinauzwa kwenye soko la dunia. Hivyo si kazi ngumu kufahamu makampuni haya yanapata faida kiasi gani. Mfano ukiangalia bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, na ukaangalia kiasi cha dhahabu ambacho makampuni haya yanaripoti kuchimba na kuuza nje ya nchi utapata takwimu kubwa ambayo bila maelezo ya kina ni kana kwamba taifa letu linayapatia makampuni haya zawadi! Ukifanya ulinganifu wa faida wanayoipata, baada ya kuondoa fedha za uendeshaji, ni kweli inawiana na kile wanachokilipa?
Mfano sasa hivi ulinganifu uliofanyika kwenye taarifa tatu za TEITI, unaonyesha wazi kabisa kiasi ambacho makampuni yanalipa. Na hii imewezekana kwa makampuni na serikali kuonyesha risiti za malipo na vielelezo vingine. Hivyo mawazo yaliyokuwepo kwamba makampuni haya hayalipi kabisa sasa haipo. Kinachotakiwa sasa ni makampuni kuonyesha risiti za mauzo, risiti za uendeshaji ili kubaini faida wanayoipata mwishoni ili kufanya ulinganifu wa kodi zinazotolewa na faida inayopatikana. Ulinganifu huu ndio wenye tija kwa taifa letu. Yawezekana pamoja na makampuni haya kulipa kodi, wanapata faida kubwa na kutuachia mashimo na uharibifu wa mazingira.
Mpango huu wa kuhamasisha uwazi una uwajibikaji, unaweza kwenda mbali kiasi cha kuwezesha mikataba ya  uchimbaji madini na uzinduaji wa mafuta na gesi asilia kuwekwa wazi? Maana swali la kujiuliza ni lini makampuni haya yanapoanza kulipa kodi hizi serikalini? Kuna taarifa kwamba kuna Resolute kule Nzega, ambao umekuwa ukichimba dhahabu kwa kipindi cha miaka 16,  ulianza kulipa kodi miaka miwili ya mwisho. Pia kuna taarifa za kuaminika kwamba kuna migodi ya kuchimba dhahabu ambayo itafikia mwisho wa kuchimba dhahabu bila kulipa kodi, kwa kisingizio kwamba kwa miaka yote hiyo wamekuwa wakifanya hasara? Inashangaza kuona kampuni inapata hasara na inaendelea kuwepo na kuchimba madini zaidi ya miaka 16?
Kama hili ni kweli, kwa nini basi mango huu wa TEITI, usifanye utafiti ili kubaini ukweli huu? Maana kama mtu anapata hasara kila mwaka, kwa nini aendelee kuchimba au kutafuta  mafuta na gesi asilia kwa kipindi  cha miaka  kumi? Haya ni maswali ambayo watu wanajiuliza kama ambavyo huko nyuma walikuwa wakilalamika kwamba tunaachiwa mashimo, wakati makampuni yanalipa kodi. Ukweli huu umewekwa wazi na mpango wa TEITI. Hata kama taarifa hii ya TEITI haijasambazwa kiasi cha kutosha, ukweli umejulikana na hasa kwa wale walio kwenye ngazi ya kutoa maamuzi.  Ndio maana ni muhimu pia kwa TEITI kutuweka wazi juu ya hoja hii ya watu kuendelea kuchimba na kuendeleza shughuli za uziduaji wakati wanafanyia hasara. Tunaposema TEITI waende mbele zaidi ya hapa walipo tuna maana ya kufanya ulinganifu wa faida ya makampuni na kodi wanazozilipa. Na pia kuhakikisha taarifa zao zinasambazwa kwa njia mbali mbali; kwa radio, luninga, magazeti, semina na hata mashuleni.
Uelewa mpana, uwazi na uwajibikaji katika miradi ya madini, mafuta na gesi  asilia utaliepushia taifa letu na balaa itokanayo na miradi hii kama tunavyosikia kwenye nchi nyingine za Afrika. Vurugu za gesi kule Mtwara ni dalili za balaa kubwa linaloweza kulikumba taifa letu. Dawa pekee ni uwazi na uwajibikaji; hivyo mpango huu wa TEITI uwezeshwe ili uweze kwenda mbali zaidi.
Na
Padri Privatus  Karugendo
255 754 633122

0 comments:

Post a Comment