UKATILI WA KIJINSIA TANZANIA



UKATILI  WA KJINSIA BADO NI KITENDAWILI TANZANIA
Tarehe 25.11.2013, tunaanza siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ni kampeni ya kimataifa iliyoanzia kwenye mkutano wa kwanza wa Taasisi ya Uongozi wa Wanawake Duniani (Women’s Global Leadership Institute)  uliofadhiliwa na Kituo Cha Uongozi wa Wanawake Duniani (Center for Women’s Global Leadership ) mwaka 1991. (. Washiriki walichagua tarehe 25 mwezi Novemba, Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake, na Desemba 10, Siku ya Haki za Binadamu Duniani, ili kuhusianisha ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu na kuhamasisha kuwa ukatili kama huu ni ukiukaji wa haki za binadamu. Kipindi hiki cha siku 16 pia kinaangalia siku nyingine muhimu, ikiwemo tarehe 29 Novemba, ambayo ni Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Desemba 1 Siku ya Ukimwi Duniani na Desemba 6, Kumbukumbu ya Mauaji ya Montreal. 

Ukatili Dhidi ya Wanawake ni ukiukwaji  ulionea wa haki za binadamu , ni janga la kibinadamu katika jamii, na kikwazo cha kufikia usawa, maendeleo, usalama na amani. Maneno “ukatili dhidi ya wanawake” na “ukatili wa kijinsia” yanatumika kumaanisha mlolongo wa unyanyasaji unaofanyika dhidi ya wanawake  unaotokana na kutokuwepo na usawa wa kijinsia na hadhi ya chini wa wanawake katika jamii ukilinganisha na wanaume. Mwaka 1993, Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake uliutafsiri ukatili dhidi ya wanawake kama:
 “kitendo chochote cha ukatili wa kijinsia kinachosababisha au kinachoweza kusababisha maumivu au mateso ya kimwili, kingono au kiakili kwa wanawake, ikiwamo vitisho, kulazimishwa au kunyimwa uhuru, vinavyotokea katika jamii au kwenye maisha binafsi .”  Inakadiriwa kuwa mmoja kati ya wanawake watatu duniani atakumbana na ina Fulani za ukatili wa kijinsia katika maisha yake. Hivyo ni wazi kabisa kwamba wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia ni wanawake, ingawa si lazima kwamba ukatili huu unafanywa na wanaume peke yao.
Lengo la siku hizi 16 ni kupinga ukatili wa kijinsia, lakini kwa wengi siku hizi zimechukuliwa kama kupinga ukatili dhidi ya wanawake. Na kwa mtizamo finyu ni ukatili unaofanywa na wanaume kwa wanawake. Lakini hali halisi na matukio ya siku kwa siku na hasa hapa Tanzania yanaonyesha tofauti kabisa, kiasi cha kulifanya suala zima la ukatili wa kijinsia kuwa ni kitendawili.
Hata ukiiangalia mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu na maazimio yaliyofikiwa ndani ya Umoja wa Mataifa kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na inayohitaji Serikali kuchukua hatua yote imelenga ukatili dhidi ya wanawake, ikiwemo Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ukatili Dhidi ya Wanawake  (CEDAW, 1979), Mkataba wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake (DEVAW, 1993),Azimio la  Beijing na Ulingo wa Hatua(1995), Mkataba wa Mahakama ya Uhalifu Kimataifa  (Mkataba wa Rome , 1998), Azimio la Milenia  (2000) na Azimio la  Baraza la Usalama 1325 juu ya  Wanawake, Amani na Usalama (2000), na mengineyo.
Wimbi kubwa la kuwanyanyasa wafanyakazi wa majumbani ambao asilimia kubwa ni wasichana linabadilisha kwa kiasi fulana dhana nzima ya ukatili wa kijinsia. Manyanyaso haya kwa kiasi kikubwa yanatekelezwa na wanawake. Ingawa kwa kiasi Fulani wafanyakazi hawa wa majumbani wananyanyaswa na kudhalilishwa na wanaume, kama kuwabaka au kuwageuza nyumba ndogo, lakini mateso makubwa dhidi ya utu wao na uhuru wao yanatendwa na wanawake.
Biashara ya ngono, kwa kiasi Fulani inaendeshwa na wanawake. Wanawakusanya wasichana wadogo sehemu mmoja, na hasa kwenye miji mikubwa na kuwatumikisha kingono,  ni aina Fulani ya utamaduni wa kule mkoa wa Mara, ambako wanawake wanao kwa lengo la kuwa na wasichana wa kuwatumikisha kingono na kujipatia watoto. Utamaduni huu unajulikana kama “Nyumbantobu”. Katika utamaduni huu, msichana anayeolewa na mwanamke, anakuwa hana uhuru wa aina yoyote na mwili wake au na watoto anaowazaa. Hii ni aina ya ukatili wa kijinsia, ambao ingawa wanatendewa wanawake, lakini si ukatili wa wanaume.
“Idadi ya wanaume wanaofika kwenye kituo cha polisi kulalamika kupigwa na wake zao imeanza kuongezeka kwa kasi katika Jiji la Dar-es-Salaam” Hayo yalisemwa na  Kaimu Kamishana wa Polisi, Adolphina Chialo, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ulioratibiwa na Shirika la wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF).

Utafiti uliofanywa tarehe 22.11.2013 kwenye Bar ya Kisuma- Mwembeyanga-Temeke- Dar-es-alaam, umeongeza giza nene kwenye suala zima la ukatili wa kijinsia. Wanawake sita ambao ni miongoni mwa wanawake wengi wanaohudumia kwenye Bar hiyo walikuwa na maoni tofauti na yanayopingana juu ya ukatili wa kijinsia. Wakati wanawake watatu  walikataa kushuhudia aina yoyote ile ya  ukatili na udhalilishaji wa wahudumu kwenye baa hiyo, wanawake wengine watatu walilalamikia manyanyaso na udhalilishaji wa hali ya juu kwenye baa hiyo ya Kisuma.
Utafiti ulifanywa Kisuma, baada ya kuwepo na taarifa za unyanyasaji wa kijinsia kwenye baa nyingi za Dar-es-Salaam. Wahudumu kulazimishwa kuvaa nguo fupi, kuonyesha sehemu kubwa ya matiti yao, kulazimishwa kushikwa shikwa na wateja, kufanyishwa kazi masaa mengi kwa malipo kidogo na matendo mengi  ambayo ni kinyume na haki za Binadamu.
Adela Joseph (jina la kubuni), mhudumu wa Baa ya Kisuma, alilalamika “ Tunafanya kazi masaa mengi, mshahara kidogo. Tunashikwa shikwa na wanaume, ukilalamika unafukuzwa au unaambiwa hii si hoteli ya chai, hivyo ni lazima kuvumilia… ukibeba mimba, unakuwa umejifuta kazi, maana ukienda kujifungua, ndo mwisho wa kazi yako… hakuna haki hapa, tunanyanyaswa na kudhalilishwa”
Meneja wa Bar ya Kisuma, bwana Peter Jackob (jina la kubuni), aliungana na wale wanawake watatu waliosema Kisuma hakuna udhalilishaji. “ Mtu akimshika shika mhudumu bila ridhaa yake, sheria inachukua mkondo wake. Tunatenda haki na kuhakikisha kila mhudumu anapata haki yake, mishahara yetu ni mizuri na wana marupurupu mengi.
Bwana Kafana Mbyango (Jina la kubuni) mteja wa Kisuma, aliyefuatilia maongezi yetu kwa karibu alisaidia kufumbua kitendawili cha Kisuma; wanawake watatu na meneja wanasema mambo safi, wakati wanawake wengine wanasema Kisuma kuna unyanyasaji wa kijinsia. “ Unajua wale wanaotetea, ni wale wenye mishahara mikubwa, ni wale wenye mahusiano ya karibu sana na Meneja au mwenye Bar, ni wale wakivunja gilasi, mishahara yao haikatwi. Kusema kweli hapa Kisuma kuna unyanyasaji wa hali ya juu, nimeshuhudia mara nyingi wahudumu wakidhalilishwa..”.
“Kisuma, kuna udhalilishaji wa hali ya juu. Kwanza, kwa maoni yangu mimi wanawake wote wa Kisuma, ni Malaya tu! Ukifanya kazi kwenye Baa, wewe ni Malaya..” Alichangia kijana mmoja aliyeonekana kuwa ni mteja wa kila siku pale Kisuma.
Ina maana pale Kisuma, wahudumu wanawake wenye hali nzuri kimaslahi, wanabariki unyanyaswaji na udhalilishwaji wa wanawake wenzao? Kwa maneno mengine, huu ni unyanyasaji wa wanawake unaoendeshwa na wanawake wenyewe! Hiki ndicho tunachokiita kitendawili. Kazi kubwa iliyo mbele ya wanaharakati na wale wote wenye mapenzi mema ya kutaka kuona ukatili wa kijinsia unakomeshwa, wajitahidi kutegua kitendawili hiki. Tusipumbazwe na utamaduni wa wanaume kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake, tuliangalie na kulishughulikia suala zima la unyanyasaji wa kijinsia: Wanaume wanawanyanyasa wanawake, lakini pia kuna wanawake wanaonyanyasa na kuwadhalilisha wanawake wenzao na wakati mwingine kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wanaume.
Ukatili wa kijinsia, uzingatie suala zima la haki za watoto: Wasichana kwa wavulana, haki za wanawake na haki za wanaume.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

0 comments:

Post a Comment