WAAFRIKA TUSIPIGANE

WAAFRIKA TUNA MATATIZO MENGI, TUSIPIGANE!

Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ndiye amiri jeshi mkuu wa taifa letu la Tanzania, ametoa tamko kali kwamba atakayeichokoza Tanzania, tutamchapa. Inafurahisha kujua kwamba jeshi letu liko imara. Hapana shaka kwamba tuna jeshi zuri la kizalendo na Jeshi letu ni Jeshi la Wananchi. Pamoja na pongezi hizi kwa Rais wetu na jeshi letu, ni lazima tuwe wazi kabisa kwamba vita si kitu kizuri. Vita ni kumwaga damu, vita ni kupoteza maisha, vita ni kuzalisha wakimbizi na mahangaiko ya watu na hasa watoto na wanawake, vita ni kuvuruga uchumi. Na vita si mpango wa Mungu! Kama kuna njia nyingine ya kumaliza tatizo, bila kuingia kwenye vita, ni busara kuifuata njia hiyo.
La pili, ni je hawa wanaotuchokoza, na tunataka kuwachapa ni watu gani? Ni Wachina, Wajapani, Wamarekani au Waafrika wenzetu? Kama ni Waafrika, tuseme hapana: Waafrika tuna matatizo mengi, tusipigane! Tunahitaji kuungana zaidi ya kupigana; hatuna chakula cha kutosha, hatuna maji, hatuna makazi bora kwa kila mwananchi, tunakufa kwa magonjwa yanayotibika kama malaria na mengine, watoto wengi bado wanakufa wakiwa chini ya umri wa miaka mitano, hatuna elimu ya kutosha na matatizo mengine mengi yanayotufanya kujuliana kama “Masikini” wa dunia hii au watu wa dunia ya tatu. Tuna maadui wengi, na maadui wetu wanafanana, hivyo ni lazima kuungana ili kupambana nao. Wale wanaotuchukia wanatukejeli kwamba Afrika hatuna la kutufanya kuungana:  tunaunganisha umasikini wetu? Tunaunganisha ufisadi wetu? Tunaunganisha nini? Kama tumeshindwa kujenga utaifa,  tutaweza kujenga Afrika moja iliyoungana? Kama makabila bado yanatengana na kubaguana ndani ya nchi mmoja, itawezekana kuunganisha bara zima la Afrika?  Ingawa utaifa ni kitu kilichopandikizwa vichwani mwetu na wakoloni, lakini sasa hivi ndiyo ukweli uliopo kwamba tuna nchi za Afrika, zina mipaka na uhuru wake. Hata tukifanikiwa kuondoa mipaka hii siku moja, swali ni je watu wa nchi hizi ni wamoja? Watu wa nchi hizi wana mshikamano?  Maana huwezi kuwa na mshikamano na wengine kama wewe huna mshikamano nyumbani kwako. mbona hadi leo hii hakuna sauti moja ya Afrika? Mbona Afrika inashindwa kutatua matatizo yake yenyewe?
Afrika inahitaji mshikamano kupambana na utandawazi na matatizo mengine mengi. Tukumbuke utandawazi hauna rangi. Afrika inahitaji mshikamano kupambana na Ubeberu unaosambaa kwa kasi na kutishia uhai na ustawi wa Waafrika. Vita nyingi kwenye bara la Afrika inakuwa na msukumo wa nje; inakuwa na msukumo wa wale wanaotaka tupigane ili watutawale tena kwa njia za kisasa zenye kubeba maneno ya kinafiki “ dunia ni kijiji kimoja”. Ubeberu hauna rangi. Tulizoea ubeberu wa Wazungu, lakini sasa hivi kuna tishio la ubeberu wa Kichina na hata ubeberu wa Kiafrika; maana kuna nchi za Afrika ambazo zinaanza kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi na nyingine zinatumiwa na nchi za magharibi kuzinyanyasa nchi changa za Afrika. Je sababu zilizowasukuma wazee wetu kusimama na kupinga ukoloni bado zipo? Ni kiasi gani Mwafrika amejikomboa kifikira baada ya Uhuru? Ni kiasi gani Mwafrika ametambua kwamba mipaka ya nchi za Afrika iliwekwa na wakoloni?
Mshikamano wa Waafrika, ni tofauti na muungano wa nchi za Afrika. Wakati muungano wa nchi za Afrika unatengenezwa na viongozi, mshikamano unachipuka kwa njia nyingine tofauti; Maana mshikamano unatengenezwa na watu wenyewe; vuguvugu hili linajenga mazingira ya kwamba Mwafrika popote alipo akishikwa sote tumeshikwa. Mshikamano unaweza kuzaa muungano imara kuliko muungano unaoshinikizwa na viongozi wa Afrika.
 Mfano, mshikamano wa Watanganyika na Wazanzibari; unaweza kuunda muungano wa nchi hizi mbili ulio imara. Watu wakihusiana kwenye mambo ya kijamii ya kuoana, kufanya  biashara kwa pamoja, kutembeleana, kuabudu pamoja na kuibua uzalendo imara wa nchi hizi mbili, swala la muungano linakuja lenyewe. Leo hii watu wameanza kuhoji Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, maana kuna ushahidi kwamba muungano huu ulizaliwa au ulitengenezwa na urafiki wa watu wawili; inawezekana pia kwamba watu hawa walisukumwa na hekima, busara na mapenzi ya nchi zao, lakini ukweli unabaki pale pale, kwamba Marehemu Mwalimu Nyerere na Marehemu Abed Karume, hawakuwashirikisha wananchi juu ya swala la muungano.
Na kuziunganisha nchi za Afrika ni wazo ambalo mpaka sasa limekuwa likishughulikiwa na viongozi wa Afrika bila ya kuwashirikisha wananchi wa Afrika. Kwa kifupi ni kwamba umoja wa nchi uhuru za Afrika ni umoja wa viongozi wa nchi za Afrika. Viongozi wanafanya mikutano na kutafuta namna ya kuunganisha nchi zao. Lakini hatujasikia viongozi hawa wakitafuta maoni ya wananchi juu ya kuziunganisha nchi hizi za Afrika. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni mfano mzuri wa umoja wa nchi za Afrika. Vingozi wa nchi hizi mbili walikutana na kukubaliana juu ya muungano wa nchi zao mbili bila kuuliza maoni ya watu. Historia imetufundisha kwamba muungano huu umeendelea kuwa na matatizo hadi leo hii. Ni wazi waanzilishi wa muungano walikuwa na nia njema kwa watu wao. Lakini leo hii mambo yamegeuka; huwezi kumwakilisha mtu bila kusikia matakwa yake.
La kujifunza hapa ni kwamba tunahitaji sauti moja ya Afrika. Na sauti moja hii haiwezi kujengwa na viongozi wa nchi hizi za Afrika. Sauti moja ya Afrika italetwa na wananchi wa Afrika. Mshikamano wa Waafrika, ndio chombo pekee  cha kuleta sauti moja na kusukuma kasi ya maendeleo ya nchi za Afrika. Marais wetu wakitupiana maneno, haina maana kwamba wananchi wa nchi hizo wana magomvi miongoni mwao. Marais wetu wakichukiana, haina maana kwamba nyuma yao kuna wananchi wanaochukiana pia.
Kuna watu wana utata juu ya Umajumui (Pan Africanism) na Umoja wa Afrika,  ingawa maneno haya yanafanana, yana maana mbili tofauti. Umajumui unamaanisha zaidi Mshikamano wa Waafrika; au Mshikamano wa watu weusi popote walipo duniani. Na  Umoja wa Afrika unamaanisha zaidi kuunganisha nchi zote za Afrika. Na kuna ndoto kwamba siku moja Afrika itakuwa na rais mmoja na kuwa na fedha moja ya Afrika.
La msingi, na lenye maana kubwa kwetu ni mshikamano wa Waafrika. Hili likifanikiwa, hatuwezi kuwa  na vita katika Bara letu la Afrika. Mara nyingi wanaoleta vita, si wananchi bali ni viongozi. Ni wakati wa kusimama kidete na kuwaambia viongozi wetu kwamba hatutaki vita. Kama kuna matatizo, ni muhimu kukaa kwenye meza ya majadiliano. La muhimu ni ushirikishwaji. Viongozi wasijadili peke yao na kugombana hadi kufikia hatua ya “Kutishiana” kwa kupigana, bali viongozi wetu watushirikishe mabishano ili na sisi tuchangie na mjadala wetu uanze na hitimisho kwamba tutajadiliana, tutatofautiana, tutachukiana hata kwa sura, lakini hatutoani uhai!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122.
 
 
 
 

2 comments:

Travis Smith said...


I do not know whether it's just me or if everyone else experiencing issues with your blog. It appears as though some of the text on your content are running off the screen. Can someone else please comment and let me know if this is happening to them too? This may be a issue with my web browser because I've had this happen previously. Many thanks itunes login

Theodor said...

The TD Mortgage Payment Calculator may help you better understand what your repayments may look like once you borrow to get a home. mortgage payment calculator You accept to use Third Party Content only at your own risk. canadian mortgage calculator

Post a Comment