AFRICARE NA MCHANGO WAKE TANZANIA 2

AFRICARE NA MCHANGO WAKE KATIKA JAMII: TANZANIA.( 2)

Pamoja na mafanikio niliyoyataja, bado huduma hii ya Huduma Majumbani ina changamoto kubwa. Tulipoongea na walengwa katika utafiti wetu kuna mambo matatu ambayo yalitajwa kila kata tuliyoitembelea. Walengwa, na hasa wale wanaoishi na virusi vya ukimwi wanaishukuru sana serikali kwa kuwapatia dawa za kurefusha maisha. Pamoja na shukrani hizi wanaiomba serikali iwasaidie chakula na hasa kwa kipindi hiki ambacho hawajaweza kujitegemea. Hoja yao ni kwamba madawa haya yana nguvu sana. Mtu akiyatumia ni lazima ale vizuri. Bahati mbaya wengi wao hawawezi kumudu zaidi ya mlo mmoja kwa siku. Na kuna wagonjwa wengine waliolazimika kuacha dawa kwa vile hawakuwa na chakula. Mbali na chakula, walengwa hawa wanaoiomba serikali kuwapatia mtaji, ili waanzishe miradi ya kujitegemea. Kwa vile baada ya kutumia dawa za kurefusha maisha wana afya na nguvu za kufanya kazi wasingependa kulishwa kama watoto wadogo. Wanapenda kujitegemea! Tatizo ni mtaji maana walio wengi ugonjwa umerudisha nyuma maendeleo yao. Baadhi walipendekeza wapate mitaji ya mtu mmoja mmoja, lakini walio wengi waliomba serikali iwapatie mitaji ya kuendeleza vikundi vyao vya kusaidiana.

Ombi la tatu la walengwa wa Huduma majumbani ni usafiri. Wanapendekeza vituo vyote vya afya viwe na usafiri wa kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa ya kusendeka. Kiasi kwamba mgonjwa akizidiwa akimbizwe kwenye kituo cha afya au Hospitali ya Wilaya. Wanasema, kama Serikali haiwezi kumudu kununua magari, hata Bajaji inaweza kusaidia katika maeneo fulani yasiyokuwa na milima mikali. Pamoja na usafiri wa kituo cha afya, walengwa hawa wanapendekeza wahudumu wao wa kata ni bora wakipatiwa usafiri wa baiskeli au pikipiki maana wahudumu wengine wanatembea mwendo mrefu kuwafikia walengwa.

Changamoto nyingine ambayo inaleta utata mkubwa katika kuwahudumia wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI, ni pale wao wanaofikiri wanatumiwa kama mtaji. Kuna baadhi waliokataa kuhojiwa. Wanasema wanahojiwa mara nyingi na mashirika mbali mbali. Mashirika hayo yakipata fedha haziwafikii walengwa. Hoja hii ilijitokeza mara nyingi katika utafiti wetu na hasa pale ilipobainika kwamba baadhi ya wahudumu si waaminifu. Misaada inayotolewa na mashirika mbali mbali kwenda kwa lengwa haiwafikii. Misaada mingine inapotelea wilayani, lakini hata ile inayofanikiwa kufika kwenye kata haifiki kwa walengwa na ikifika inakuwa ni nusu na wakati mwingine walengwa wanapigiwa simu kwenda kwa muhudumu kuchukua mizigo yao na kuondoa dhana nzima ya huduma majumbani. Katika kata zingine tulizotembelea, walengwa walipendekeza kwamba wahudumu wa kata wawe ni walengwa wenyewe. Wanashindwa kuelewa mtu asiyekuwa mlengwa anaguswa na huruma gani?

Walitoa mfano wa wahudumu wanaogombania walengwa. Yakijitokeza mashirika ya kutoa misaada, wahudumu wananyang’anyana wagonjwa. Tulishuhudia jambo hili wakati wa utafiti. Unakuta mhudumu hajawahi kumtembelea mlengwa, akisikia kuna watu wanafanya utafiti au kuna shirika la kuleta misaada anatengeneza orodha ndefu na wakati mwingine kuingilia wagonjwa wanaohudumiwa na muhudumu mwingine.

Lakini pia kuna hili tatizo la mashirika kuleta misaada bila kuongea na kujadiliana na walengwa. Wanawaletea chakula wakati wao wanahitaji majembe na mbegu ili walime na kujitegemea kwa chakula. Wanawaletea sabuni na sukari wakati wao wanahitaji mitaji ili waanzishe miradi ya kujitegemea. Kuna haja ya kuwasikiliza walengwa kabla ya kuwaletea misaada. Na tatizo jingine linalojitokeza ni pale mashirika yanapowahudumia walengwa kwa ubaguzi. Ukiliondoa Shirika la World Vision, tuliambiwa mashirika mengine na hasa yale ya kidini yana ubaguzi. Walio wengi wanawahudumia waumini wao.

Wahudumu tuliowahoji walilalamikia ushirikiano hafifu kati yao na viongozi wa serikali za mitaa. Hii nayo ni changamoto kwa huduma majumbani. Wakati wahudumu wanajitahidi kutunza maadili yao ya kutotoa siri za wagonjwa, viongozi wa serikali za mitaa wanatoa shinikizo la kutaka majina ya walengwa wote kuorodheshwa na kutundikwa kwenye ubao wa matangazo. Kisingizio kikiwa usambazaji wa huduma. Wahudumu wanapokataa kufanya hivyo kunatokea kutoelewana na kunyimwa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa serikali za mitaa. Pia serikali za mitaa hazina mpango wa kuwashughulikia walengwa wa magonjwa ya kusendeka.

Pia kuna changamoto ya imani za dini na utamaduni. Viongozi wa dini hawapendi kusikia wahudumu wa huduma majumbani wakipita kwenye kaya wakifundisha matumizi ya kondomu. Viongozi wa dini wanasisitiza uaminifu na kuacha kabisa. Ukweli wenyewe ni kwamba uaminifu na kuacha kabisa ni vitu visivyowezekana. Utamaduni nao unaingilia kati, mfano mfumo dume na Nyumba ntobu.

Changamoto nyingine, ni kwamba wahudumu wa msingi wengi ni wanawake. Kama mgonjwa ana hali mbaya, kiasi cha kutofanya kazi. Wanawake wanakuwa na mzigo mkubwa wa kumtunza mgonjwa na wakati huo huo kutafuta muda wa kuihudumia familia nzima, kama vile kutafuta chakula, kutafuta kuni, kuchota maji na kupika. Ni matukio machache tulipokuta wanaume na watoto ni wahudumu wa msingi. Ingekuwa vizuri kwa mashirika yanayotoa mafunzo kwa wahudumu wa msingi, kuyatoa mafunzo hayo kwa wanafamilia wote bila kujali jinsia, ili akijitokeza mgonjwa kwenye familia wote watoe huduma, mzigo asiachiwe mwanamke peke yake.

Wakati walengwa, wanaishukuru serikali kuwapatia dawa za kurefusha maisha, wale wanaofikiri hawajaambukizwa ( wengi wao hawajapima afya zao) wanailaumu serikali kuwafufua watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Wanafikiri kuwapatia dawa za kurefusha maisha ni njia ya kuueneza ugonjwa huu. Ingawa kusema kweli unyanyapaa umepungua kwa kiasi kikubwa na hasa Mkoa wa Manyara, bado kuna mawazo kwamba ni bora wagonjwa wenye virusi vya ukimwi wafe, ikiwa ni mkakati wa kupunguza maabukizi mapya. Tuliohojiana nao kwa sharti la kutotaja majina yao, walisema serikali ni adui wa umma. Walitoa mfano wa wagonjwa wanaowafahamu ambao walikuwa kwenye dakika zao za mwisho hapa duniani, lakini walipotumia dawa za kurefusha maisha wamepona na wanaendelea na tabia yao ya kufanya mapenzi kwa vurugu na bila kinga. Wanasema maambukizi mapya yanasababishwa na serikali kwa uamuzi wake wa kusambaza dawa za kurefusha maisha. Siku za nyuma watu waliuogopa UKIMWI, maana walijua ugonjwa huu ni kifo. Leo hii hakuna mwenye kuogopa maana kupata virusi vya UKIMWI si kifo tena. Dawa zipo na serikali inazitoa bure.

Haya ni mawazo ambayo baadhi ya wahojiwa wetu waliyatoa, haina maana tunakubaliana nayo. Tunapingana nayo vikali, maana tunaamini kila mtu ana haki ya kuishi. Tumeyatoa kwenye ripoti hii ili kuelezea yale tuliyoyapata katika utafiti wetu. Ni vizuri serikali na wale wote wanaoendesha vita ya kupambana na UKIMWI na kutoa huduma kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI, kuelewa mawazo ya upande mwingine.

ARVs zimeonyesha uwezo mkubwa wa kurefusha maisha. Kuna malalamiko kwamba baadhi ya wagonjwa wanapata madhara, na tumeambiwa wakati wa utafiti kwamba Tanzania, imeamua kubadilisha aina ya ARVs zilizokuwa zikitumika na kuingiza mpya. Jambo la kushangaza ambalo bado tunafuatilia kwa ukaribu ili kupata ukweli wake ni kwamba walengwa wamebadilishiwa dawa bila kupimwa upya. Kuna ambao ARVs za zamani zilikuwa zimewakubali na ingekuwa ni busara kuendelea na hizo. Uamuzi wa kuwabadilishia wagonjwa wote dawa na kuwaanzishia mpya ni wa kutilia shaka. Ndio maana nikasema tunafuatilia kwa karibu ili kubaini ukweli wake. Mkoa wa Mara, tulisikia malalamiko kutoka kwa walengwa kwamba dawa hizi mpya zina madhara makubwa kuliko zile za zamani na baadhi ya walengwa wameamua kuachana na hizi mpya na ni bahati mbaya kabisa kwamba hawawezi kuzipata zile za zamani. Hii ni changamoto kubwa kwa mpango mzima wa huduma majumbani maana watakutana na maswali ambayo hawatakuwa na majibu yake.... itaendelea.

Na,
Padri Privatus Karugendo.
0754 633122
pkarugendo@yahoo.com
www.karugendo.com

0 comments:

Post a Comment