MWANA MAMA KAROLA KINASHAKatika safu yetu ya Mwana Mama, leo tunawaletea mwanamuziki mkongwe wa nchini Tanzania, Karola Kinasha. Mwana mama huyu ni mmoja kati ya wanamuziki wa kwanza kabisa wa kike kuvunja mwiko wa kusimama stejini na kuburudisha wapenzi wa muziki. Alianza muziki kipindi kile tasnia hii ikiwa bado imetawaliwa na wanamuziki wa jinsia ya kiume.

Huyu ni mwanamuziki/msanii anayedumisha utamaduni wa Mwafrika. Anajivunia utamaduni wa kabila lake la Wamasai. Usanii wake unabeba ujumbe kwetu sote kupenda na kudumisha utamaduni wetu. Mavazi yake na mwonekano wake, daima unatangaza utamaduni wetu wa Kitanzania na Afrika kwa ujumla. Hivyo huyu si msanii wa kuigiza au kutoka kimaisha, bali ni msanii mwenye malengo ya mbali kwake yeye na kwa taifa zima.

Huyu ni Mwana Mama aliyesomea sheria chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, lakini akaamua kuimba! Ina maana alifanya uamuzi na kuchagua kitu kilichoyagusa maisha yake na wala si kwenda kwenye usanii kwa mkumbo au kutafuta maisha. Alitafuta namna ya kutoa mchango wake kwa taifa kwa kupitia usanii. Ndo maana nyimbo zake zote zimesheheni tafakuri na wala si zile nyimbo za mapenzi tulizozizoea kila kukicha kila msanii anatunga nyimbo za mapenzi.

Karola, si msanii wa kutafuta jina na wala hana majivuno. Ni mtu anayependa kazi yake na kuiheshimu. Ni mnyenyekevu, mkimya kiasi na wala hana maneno mengi. Kikubwa kwake ni kujivunia uafrika wake na kuhakikisha kazi zake na mwonekano wake vinaitangaza Afrika. Ni mtu asiyependa kujitangaza kwenye vyombo vya habari. Dume challenge, ndiyo iliyo iliyomfunua zaidi kwenye vyombo vya habari. Karola, alikuwa jaji wa shindano hilo ambalo washindani walikuwa ni wanaume na majaji wengine walikuwa ni wanaume.

Wale waliopata bahati ya kufuatilia shindano hili la Dume Challenge, watakubaliana na mimi kwamba mama huyu mbali ya kuwa msanii wa nyimbo, bado ana vipaji vingine vikubwa. Kwenye shindano hili, hekima, busara, huruma, upendo vilijitokeza wazi kwa Mama huyu ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu kwa miaka mingi. Alionyesha roho ya umama, kuwajali vijana waliokuwa wakishindana, kuwaelekeza, kuwafundisha na kuwatia moyo, lakini pia alikaripia pale ilipolazimu. Ni miongoni mwa akina mama wengi wa Tanzania, wanaofanya mambo mengi makubwa na mazuri, lakini hawajitangazi na wala hawasikiki!

Ingawa mama huyu hasikiki sana, lakini akipanda jukwaani, akianza kuimba ni nadra mtu kubaki amekaa kwenye kiti. Nilishuhudia mwenyewe Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, wakati wa tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alipounyanyua ukumbi mzima wa Nkrumah. Sauti yake nzito na ya kukwaruza kidogo, haiwezi kumwacha mtu amekaa. Zaidi ni kwamba anaimba kwa hisia kali na kuonyesha kuguswa na uhai wa Taifa la Tanzania.

Sio jambo rahisi na wanamuziki wasio wengi duniani wanaweza kufanya. Tunazungumzia kuimba na kutumia kifaa chochote cha kimuziki (kama gitaa, piano, ngoma nk) wakati huo huo. Karola ni mmojawapo miongoni mwa wanamuziki tulionao nchini Tanzania ambao wanaweza kufanya hivyo, anaweza kuimba na wakati huo huo kucharaza gitaa. Na baadaye akapata nafasi ya kurudi nyumbani kupumzika na kufurahi na familia yake. Mungu amemjalia watoto wawili. Picha zinazonyeshwa kwenye mtandao, anaonekana ni mama mwema ndani ya familia yake.

Karola Daniel Amri Kinasha alizaliwa Machi, 1970 huko Longido mkoani Arusha. Baada ya kumaliza masomo ya elimu ya msingi huko Longido, alihamia jijini Dar Es Salaam ambako alipata elimu ya sekondari na ya chuo kikuu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Karola amekuwa akijihusisha na masuala ya muziki tangu mwaka wa 1987.Ameshiriki katika miradi na matamasha mbalimbali ya kimuziki, ndani na nje ya Tanzania.Karola, anatoka kwenye kabila la Wamasai jirani na mpaka wa Tanzania na Kenya. Yeye ni miongoni mwa watoto 8 wa familia yao. Baba yake aliweza kucheza akodiani, kaka yake aliweza kupiga piano na gitaa, mama yake aliimba kwenye kwaya ya kijiji. Inaonyesha jinsi Karola, anavyotoka kwenye familia ya wanamuziki. Lakini pia alishiriki nyimbo na ngoma za wanakijiji na kufurahia mashujaa wa Kimasai walivyokuwa wakiimba na kujigamba.Ndugu zake na Karola, walipoanza kutoka nyumbani kwenda shuleni, walileta aina mbali mbali ya miziki kutoka dunia nyingine. Kaka zake Esto, Abedi na Oculi, walimletea nyimbo za Calypso, nyimbo za Injili na aina nyingine za nyimbo za Kizungu, nyimbo za Tanzania na za kikongo, wakati Dada yake Juddy, alimletea nyimbo za Afrika ya Kusini.

Rafiki yake wa karibu anasema hivi juu ya Karola:

“Carolla namfahamu miaka mingi. Nilisoma naye Zanaki Girls Secondary School. Alikuwa anapenda sana kuimba wakati huo. Alikuwa anajua nyimbo zote za Boney M na ABBA, tena alikuwa anaziimba vizuri mpaka walimu walichukia na kusema kuimba Kizungu ni kasumba!”

Hivyo haishangazi, baadaye Karola, kuibuka mwimbaji mzuri anayependa na kujivunia utamaduni wa Mwafrika. Bendi yake ya Shada, ilianza kwenye miaka ya mwisho ya 80, ikilenga kutoa muziki wa Kitanzania, wenye maonjo ya Kitanzania. Albamu yake ya pili ijulikanayo kama Maono, iliipaisha bendi ya Shada ndani na nje ya Tanzania.

Karola, kwa namna yake, amekuwa mwanaharakati wa kutetea haki za wanamuziki wa Tanzania. Pia ni kati ya watu waliopambana kurudisha somo la muziki kwenye shule za Tanzania. Mama huyu amepata tuzo ya “MA Africa Awards in South Africa”.

Mama huyu ni Mwanaharakati wa kutetea usawa kijinsia kwa namna yake. Ametumia sanaa, kuonyesha msimamo wake na kutoa ujumbe wa usawa wa kijinsia kwa kutumia nyimbo zake. Lakini pia ameyatumia maisha yake mwenyewe kuonyesha jambo analolisimamia. Kujiingiza kwenye fani ambayo kwa namna Fulani ilionekana ni ya wanaume peke yao ni msimamo wa kimapinduzi na wa kiwanaharakati. Na kama tulivyosema hapo juu, yeye alikuwa mwanamke jaji peke yake ndani ya mashindano ya Dume Challenge. Mama huyu hapigi kelele nyingi kutetea usawa wa kijinsia, matendo yake yanapiga kelele zaidi. Ni mama wa mfano na wa kujivunia kuwa naye katika taifa letu la Tanzania!

Na,

Padri Privatus Karugendo,

www.karugendo.net

+255 754 633122MWANA MAMA BEATRICE SHIMENDE KANTIMBOSafu ya Mwana Mama, imeanzishwa kwa lengo la kuandika na kutangaza mchango wa akina Mama katika taifa letu la Tanzania. Wanawake wana mchango mkubwa, lakini mara nyingi mchango wao unafunikwa kiasi kwamba vyombo vingi vya habari vinatawaliwa na sifa za wanaume. Akiandikwa mwanamke inakuwa ni kashifa za ngono na mambo mengine kama hayo. Wakati wanawake wana mchango mkubwa: Uvumilivu, kuishi kwa matumaini, kutokukata tama na kubwa zaidi hawa ni mama zetu. Hakuna mtu anayekuja hapa duniani bila kuzaliwa na Mwanamke. Hivyo tunataka tusitake ni lazima tutambue kwamba mwanamke ana mchango mkubwa katika jamii yetu.

Leo katika safu yetu ya Mwana Mama tunawaletea Beatrice Shimende Kantimbo, mkazi wa Kwembe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam wilayani Kinondoni ,mama ambaye amepambana na ugonjwa wa mguu kwa miaka 15. Jana amerudi kutoka nchini India, akiwa amepona!

Mapokezi makubwa aliyoyapata mama huyu Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Dar-es-Salaam ni ishara kwamba ugonjwa wa mama huyu uliwagusa watu wengi. Na labda sasa wakati umefika wa kuacha kuchangia tu sherehe za ndoa na kuanza kuchangia matibabu na elimu ya watoto wetu. Watanzania tunasifika sana kwa vikao vya harusi na kuchanga fedha nyingi za harusi kuliko tunavyochangia wagonjwa na elimu.

Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa mama huyu mwenye umri wa miaka 48, ambaye kabla ya kupata ugonjwa huu alikuwa mchapakazi akijishughulisha na shughuli mbalimbali za biashara na nyingine kama msherekeshaji aliyejulikana kama Kimbaumbau.

Mama huyu ameonyesha uvumilivu mkubwa. Hakukata tama wala kukubaliana na wale waliomshauri mguu wake ukatwe. Pamoja na maumivu makubwa aliyokuwa nayo mama huyu, daima alionyesha matumaini na tabasamu lilitawala uso wake. Aliishi kwa imani na matumaini. Mme wake naye amekuwa mfano wa kuigwa; alisimama kidete kumhudumia mke wake kwa miaka yote hiyo 15 hadi kumsindikiza India. Huyu ni mwanaume wa mfano!

Habari za Mama huyu zilipoanza kuandikwa kwenye vyombo vya habari, mama huyu alihojiwa akisema:

“NIMEKUWA nikiteseka kwa kuuguza mguu wangu kwa miaka 15 sasa, hakika napata maumivu makali sana, naomba Mungu anisaidie na awajaze moyo wa huruma Watanzania wenzangu ili niweze kwenda kutibiwa.”

Alisimulia jinsi alivyoanza kuugua mguu wake: “Nakumbuka mwaka 1998 nikiwa kwenye biashara zangu pale Ubungo, kuna kitu kilinichoma hapa (anaonyesha pajani) maumivu yake yalikuwa mithili ya sindano, hata hivyo hayakudumu sana wala hapakuwa na alama yoyote.

“Baada ya dakika chache nikajihisi homa kali. nikaanza kutetemeka mwili mzima, nikaamua kwenda hospitali inayojulikana kwa jina la Neema, Daktari akanipima, akagundua nilikuwa na malaria.

“Wakati huo mguu haukuonyesha dalili zozote za maumivu wala jeraha. Malaria ilikuwa kali, nikalazwa kwa muda wa wiki mbili pale hospitali. Nikaruhusiwa, nikarudi nyumbani na hapo ndipo nilipoanza kuona mguu unavimba. Kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo mguu nao ukazidi kuvimba”

“Baadhi ya madaktari wa Muhimbili walinishauri nikubali kukatwa mguu. Wanasema nyama imeoza na mfupa wa mguu umeharibika. Mimi sikukukubaliana na ushauri wao kwa sababu baada ya kupigwa X-ray 2007 iligundulika tatizo kubwa lilikuwa kwenye mishipa ya kupitisha maji kutokana na nyama kuharibika. Sio mfupa.

“Nilikataa kwa imani kuwa nitapona tu. Nikijiangalia nina uwezo wa kusimama na kutembea isipokuwa tu kinachonipa taabu kwa sasa ni nyama za mguu zimekua sana kiasi kwamba nikitembea zinagusa mguu wa kushoto, hivyo naomba Wasamaria wema wanipe msaada ili niende India kwa matibabu zaidi.” alisema.

Kilio cha mama huyu kilisikika, lakini si kwa kasi iliyotegemewa. Mwanzoni ilitia mashaka kama watanzania wameishiwa na moyo wa huruma. Mama huyu alikuwa akionekana akilia kwa maumivu kwenye vyombo vya habari na hasa ITV, lakini uchangiaji ulienda polepole. Sam Mahera, mtangazaji wa ITV, alikuwa akihamasisha uchangiaji kwa mbinu zote na kwa nguvu zote, lakini uchangiaji haukushika kasi haraka, hata hivyo baadaye watanzania walifunguka na kuweza kumchangia mama huyu. Na sasa amerudi akiwa ametibiwa.

Pamoja na furaha kubwa ambayo watu wameonyesha Mama huyu kurudia hali yake ya kawaida, wana maswali mengi ya kujiuliza: Hivi huko India kuna nini? Ina maana Madaktari wa India wamesoma zaidi ya wetu wa hapa Tanzania? Mbona ugonjwa wa mama huyu haukutibiwa hapa kwetu mpaka mama huyu alipolazimika kusafiri hadi India. Au tatizo ni vifaa? Kama tatizo ni vifaa, kwa nini serikali yetu isinunue vifaa ili kuweza kuokoa maisha ya watanzania wengi? Si wa Tanzania wote watapa bahati ya kuchangiwa fedha kama alivyochangiwa Beatrice. Kuna watanzania wengi ambao maisha yao yanapotea kwa kushindwa kupata matibabu kwa wakati.

Ugonjwa wa Mama Beatrice, utufumbue macho. Walio wengi waliamini hakuna la kufanya zaidi kwenye mguu wa Mama huyu. Pendekezo lilikuwa ni kuukata. Sasa Wahindi wameutibu? Wana nini hawa? Kama wana utaalamu zaidi, kwa nini serikali isiwapeleke vijana wakajifunza utaalamu huo?

Tumesikia kwamba pamoja na michango ya wananchi, serikali pia imechangia kiasi kikubwa kwa matibabu ya Mama Beatrice. Ni jambo zuri kwamba serikali imesaidia. Hata hivyo kwa nini serikali inaamua kusaidia imechelewa? Mama huyu amekuwa kwenye maumivu makali kwa muda wa miaka 15. Miaka hii ni mingi kwa mtu kuishi na maumivu kiasi hicho.

Tunampongeza Beatrice Kantimbo, kupona mguu wake: Ametufundisha uvumilivu, kuishi kwa matumaini na kujiweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kutufunulia ukweli kwamba magonjwa mengi yanatibika watu wakiwa na mshikamano wa kuchangiana fedha za matibabu nje ya nchi. Kwa kuujua ukweli huu ni lazima sasa sote kuwa macho ili watu wasipoteze maisha yao kwa kushindwa kupata fedha za kwenda nje ya nchi kutibiwa. Magonjwa yanayotibika, yasitoe uhai wa watanzania: Tuishinikize serikali, kama inashindwa kuziboresha huduma za afya, basi itenge fedha za kutosha za kuwasafirisha watu nje ya nchi kutibiwa. Uhai, ukitoka haurudi, hivyo ni jukumu letu sote watanzania kuulinda uhai wa kila Mtanzania kwa gharama yoyote ile.

Na,

Padri Privatus Karugendo

+255 754 633122

.MWANA MAMA SAIDA KAROLI
Katika safu yetu ya Mwana Mama, leo hii tunawaletea Saida Karoli, mwana mama mwimbaji aliyevuma kwa nyimbo zake za Maria Salome, Kaisiki, Ndombolo na Mimi nakupenda. Mwana mama aliyejaliwa sauti nzuri nzuri ya kuimba na ufundi wa kupiga ngoma na kucheza. Mashabiki wake walimbatiza jina la “Wanchekecha”.

Ingawa umaarufu wake ulidumu kwa muda mfupi na baadaye kuzimika kama mshumaa, hakuna ubishi kwamba Mama huyu alikuwa mwimbaji wa kwanza Tanzania kupata umaarufu mkubwa nje na ndani ya nchi. Ni bahati mbaya kwamba mama huyu hakuwa na elimu ya kutosha kuweza kupigania mafanikio yake; mapromota waliomwibua ndo hao hao walioamua kumzika baada ya kuvuna kiasi cha kutosha kutokana na jasho na msanii huyu.

Saida Karoli (amezaliwa tar. 4 Aprili, 1976, Kagera) ni mwanamuziki wa nyimbo za asili ya Kihaya nchini Tanzania.

Saida alipata elimu ya msingi mwisho darasa la tano tu ambapo ilibidi aache shule kutokana na kukosa msaada kutoka kwa baba yake ambaye hakuwa anaitazama sana elimu ya mtoto wake hivyo hakuweza kuendelezwa

Saida alikulia katika kijiji cha Rwongwe mkoani Kagera na kutokana na mila za ukoo wake wasichana walikuwa hawaruhusiwi kushiriki katika shughuli za kimuziki.

Hata hivyo kwa vile mama yake alikuwa na kipaji cha muziki alimpa moyo na kumfundisha masuala mbalimbali ya kimuziki.

Akiwa na miaka 20 mama yake mzazi alifariki dunia lakini Saida aliendelea kujijengea kipaji chake cha uimbaji na upigaji ngoma.

Kukua kwake kimuziki Kipaji cha usanii wa muziki kwa Saida kilijitokeza ghafla baada ya kujikuta akichukuliwa na kudhaminiwa na FM Productions Ltd waliokuwa mkoani Kagera wakitafuta wasanii wenye vipaji kwa ajili ya kuwaendeleza.

FM ilimchukua Karoli wiki tatu tu kurekodi nyimbo yake ya kwanza ilotoka na kuishitua Dar es Salaam mzima pamoja na nchi za jirani za Afrika Mashariki.

Albamu yake ya kwanza ilizinduliwa tarehe 2 Septemba mwaka 2001.

Albamu hiyo ilipata mafanikio makubwa na kupata umaarufu mkubwa sana kwakuwa albamu hiyo ilikuwa na vionjo vingi vya kabila la Kihaya.

Albamu hiyo ilijulikana kama Maria Salome. Japokuwa mashabiki wake waliibatiza jina la Chambua kama Karanga kutokana na maneno aliokuwa anaimba katika nyimbo ya Maria Salome nyimbo iliobeba jina la Albamu.

Albamu hiyo ilifuatiwa na ziara kubwa alizokuwa anafanya katika nchi za jirani kama vile Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya ambapo alipata mafanikio makubwa na Saida kujikuta akibatizwa na kupewa jina la malkia wa nyimbo za asili.

Mara tu Saida kutoa albamu yake, wimbo wa Maria Salome ulipanda chati katika Kumi bora za Maredio kadha wa kadha nchini Tanzania na kufikia namba moja ikishikilia nafasi hiyo kwa wiki sita mfululizo.

Nyimbo zingine zilizotamba katika albamu hiyo ni pamoja na Kaisiki na Ndombolo.

Baada ya miezi mitatu tu tangu kutoa albamu hiyo, Karoli alipata mwaliko wa kuimba Uganda akialikwa na Kabaka wa Buganda katika sherehe ya kiutamaduni kama mmojawapo wa mwanamuziki aliyefanikiwa Afrika na kujulikana sana nchini Uganda na pia kumfanya kuwa mwanamuziki wa mwaka katika sherehe ile nchini Uganda.

Kujulikana kwake kwa kasi nchini Uganda kulisababishwa na matumizi ya lugha ya Kihaya, lugha inayofanana zaidi na lugha ya Kiganda inayotumika na Waganda wengi, sauti nyororo na ya kuvutia na vionjo kibao vya kuvutia vya kijadi katika nyimbo zake.

Mnamo mwezi Juni mwaka 2003 Saida akatoa albamu nyingine nzuri iliyokwenda kwa jina la Mapenzi Kizunguzungu na kuweza kuteka soko la muziki tena kwa mara ya pili kutokana na vionjo kama vya awali vya kijadi.

Hata hivyo Saida Karoli ametoa shukrani zake za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu wa FM Productions LTD bwana Felician Mutta kwa kuona kipaji chake na kumpandisha chati kama mojawapo wa wanamuziki maarufu chini Tanzania.

Mutta amesema nia yake kwa msanii huyo ni kuona Saida anajulikana na kushika cha katika bara zima la Afrika na kuweza kufanya ziara za kimuziki nchi nyingi tu duniani.

Kutokana na uwezo alionao na kipaji katika masuala ya muziki ni rahisi kugundua kuwa mwanamuziki huyo ana kiwango cha kuweza kupata mashabiki wa muziki wake mbali na Tanzania na Afrika ya Mashariki tu, bali hata nje ya Afrika

1. Maria Salome

2. Kaisiki

3. Ndombolo

4. Mimi NakupendaMWANA MAMA RHODA KAHATANOKatika safu yetu ya Mwana Mama, tunawaletea Mama Rhoda Kahatano. Mama huyu aliyeaga dunia mwaka wa 2010, ni miongoni mwa wanawake waliojitoa kulitumia taifa letu kwa nguvu zao zote, mama mzalendo, mchapakazi na mwadilifu lakini machache yameandikwa juu yao.

Mama Rhoda Kahatano, alikuwa msomi, mwanasiasa, kiongozi, mcha Mungu na zaidi ya yote alikuwa “Mama”. Siku za mwisho za maisha yake, yeye na mme wake Mzee Kahatano, walianzisha shule ya Sekondari kule Bunju Dar-es-Salaam. Wanafunzi walimbatiza mama huyu jina la Bibi na mme wake aliitwa Babu. Kwao shule si kitegauchumi kama ilivyo kwa watu wengi wanaoanzisha shule; Familia ya Kahatano inaichukulia shule hii kama familia yao kubwa: Kuwafundisha watoto, kuwapatia elimu na maadili bora. Jinsi walivyowalea watoto wao wa kuzaa ndivyo wanavyolenga kuwalea watoto wote watakaojiunga na shule yao.

Shule hii ya sekondari, ilianzishwa kwa lengo maalumu. Familia ya Mama Kahatano, iliwapoteza watoto wawili wakubwa, waliokuwa wasomi na wenye kuonyesha matumaini ndani ya familia. Misiba hii iliiyumbisha familia ya Kahatano, lakini kwa vile walikuwa na imani isiyoyumba, aliamua kuanzisha shule ya sekondari kama njia pekee ya kuwaenzi watoto wao. Shule hii kwao ni kama fanaka na kitulizo kikubwa. Kwa kujenga shule hii wanaamini Mungu, ameyafuta machozi yao ya kuwapoteza watoto na kuanzisha maisha mapya yenye matumaini si kwa familia ya Kahatano peke yake bali kwa familia nyingi zenye watoto wanaohitaji elimu.

Katika hali ya kawaida misiba ya watoto wao ilitosha kuiyumbisha familia. Lakini Mama Rhoda Kahatano na Mzee Kahatano, kwa vile walikuwa ni watu wa imani na walimwamini Mwenyezi Mungu kwa kila jambo, walimshukuru Mungu kwa matukio hayo ya kuumiza na kuamua kuendelea na maisha. Na hili liliwezekana kwa vile familia hii ilikuwa ni ya mfano: Pamoja na Mama huyu kuwa Mwanaharakati wa kupigania haki za binadamu na haki za wanawake, familia yake ilibaki imara na kuchomoza miongoni mwa familia za kuigwa.

Nina imani Familia ya Kahatano, imezisaidia familia nyingi kwa ushauri. Na kwa baadhi ya viongozi wa serikali walioyumba na kuteteleka katika familia zao, walipata msaada mkubwa kutoka kwa familia ya Kahatano. Hivyo kama walishindwa kuimba sifa za uchapakazi wa mama Kahatano ndani ya serikali, basi wangeziimba sifa za Mama huyu kuwa mfano bora wa familia na mshauri mkubwa wa ndoa nyingi.

Nilipoitembelea shule hii mwaka mmoja kabla ya kifo cha mama huyu, aliniambia kwamba mtaji wa kwanza wa kuanzisha shule hiyo ulitokana na posho zake za Ubunge. Wakati wabunge wakichukua mikopo kununua magari ya kifahari, yeye alichukua mkopo kuanzisha shule. Kwa kusaidiana na mme wake aliyekuwa amestaafu kazi za kuajiriwa na kwa misaada mingine ya ndani na nje ya nchi, shule ilisimama. Yeye na mme wake waliendesha shule hiyo wakati mama Kahatano akiwa anateswa na ugonjwa. Hata hivyo mama huyu hakuonyesha mateso aliyokuwa nayo, aliendelea kuonyesha matumaini kwa wanafunzi na wote walioitembelea shule hiyo kwa kuelezea mipango ya zaidi ya miaka ishirini mbele. Hakuwa mtu wa kukata tama.

Mama Kahatano alifanya kazi mbali mbali katika taifa la Tanzania. Alikuwa mkuu wa Wilaya, Afisa Elimu wa Mkoa, Mbunge, Mwana harakati, Mcha Mungu na alikitumikia chama chake Cha Mapinduzi katika ngazi mbali mbali. Walimu wa mkoa wa Kagera na wanafunzi waliosoma enzi za Mama Kahatano akiwa Afisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, wanakumbuka uchapakazi wa mama huyu ambaye mbali na kuwa kiongozi alikuwa “Mama”. Alielekeza, aliongoza, alishauri, alionya, aliyasikiliza matatizo ya walimu na kutafuta ufumbuzi na aliinua kiwango cha elimu katika Mkoa wa Kagera.

Waliopata bahati ya kukutana na Mama Kahatano, watakubaiana na mimi kwamba mama huyu alikuwa Mama mwenye hekima na busara. Hakuwa mpole ki hivyo kwa watu wavivu, lakini alikuwa na huruma na utu wa kuwajali wote waliomzunguka na wote aliowatumikia. Alijaliwa kipaji cha kumbukumbu, aliwakumbuka karibia watu wote aliokutana nao kazini na kwenye jamii. Yeye Mzaliwa wa Mkoa wa Mbeya, aliyeolewa mkoa wa Kagera na kujizingarisha kiasi cha kuwazidi hata wale wazawa wa mkoa wa Kagera.

Rambirambi za Serikali wakati wa kifo chake hazikutoa picha kamili ya Mama huyu ambaye ni miongoni mwa watu wachache waliolitumikia taifa hili kwa moyo wao wote. Tanzania tumekuwa na utamaduni wa ovyo wa kuwasahau kwa haraka watu wanaolitumika taifa hili. Na bahati mbaya hayajaandikwa mengi juu ya mama huyu. Salaam za Rambirambi kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete zilisema kwa kifupi sana:

“Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, Bibi Sophia Simba, kufuatia kifo cha mmoja wa wanachama wake hodari Bibi Rhoda Kahatano aliyefariki usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Bunju A, jijini Dar-es-Salaam.

Katika salamu hizo Rais Kikwete amesema amemfahamu na kufanya naye kazi katika chama na serikali na kumuelezea kuwa mwanachama dhabiti, aliyeshirikiana vyema na wenzake na mwajibikaji mkubwa.

“Alikuwa nguzo imara katika kusimamia masuala ya chama na serikali na mwajibikaji ambaye anakumbukwa wakati wote kwa ushirikiano na upendo mkubwa kwa wenzake siku zote”. Rais amesema

“Tutamkumbuka kwa kupenda kutoa ushauri, ushirikiano, upendo na ucheshi kwa watu wote na wakati wote” Rais amesema na kumuomba Mwenyekiti wa UWT, amfikishie rambirambi zake kwa Mume, watoto na wana familia ya Marehemu Rhoda Kahatano kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Marehemu Rhoda Kahatano alizaliwa Tukuyu, Mbeya tarehe 15 Desemba, 1941. Aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya mkoani Kagera kabla ya kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka mwaka 1995 hadi 2000.

Amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Mjumbe wa UWT katika kipindi cha uhai wake.

Ameacha mume, watoto na wajukuu.”

Pamoja na shukrani kwa serikali kukumbuka kutoa rambirambi, hatuwezi kusita kusema kwamba mengi hayakusemwa juu ya mama huyu:

Maisha ya Mama Rhoda Kahatano, yanaonyesha ukakamavu aliokuwa nao katika kuishi na kutenda kazi. Ushiriki wake katika makambi ya “GirlGuide” Dar-es-salaam, Zambia na Denmark, ni ushahidi wa kutosha juu ya ukakamavu wake. Pia mama Rhoda alishiriki kikamilifu harakati za Umoja wa mataifa kuwajengea nyumba watu wasiokuwa na makazi na kushiriki mikutano ya harakati hizi nchini Sweden. Na uongozi ndani ya jumuiya za wanawake zilimpeleka hadi Korea ya Kusini na Hawaii. Ni mama aliyechapa kazi bila kuchoka ndani ya serikali, kwenye chama chake cha CCM na ndani ya mashirika ya kidini.

Mwaka 1962 hadi 1963, alikuwa kwenye Umoja wa vijana wa chama TANU. Mwaka wa 1963 mpaka 1966 alikuwa Katibu wa UWT mkoa wa Arusha. Mwaka 1972 mpaka 1975, alikuwa katibu wa UWT tawi la Wizara ya Elimu makao makuu.

Mama Rhoda Kahatano, alikuwa ni msomi aliyepata Diploma ya Elimu ya watu wazima mnamo mwaka 1974 na digrii ya ualimu kutoka Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam mwaka 1980. Mbali na digriini ya ualimu alisoma mambo mengine mbali mbali: Chuo cha Siasa Kivumoni, Diploma ya lishe kutoka Muhimbili, Cheti cha Maendeleo ya jamii kutoka Tengeru na Israel. Cheti ya utawala kutoka Swaziland na cheti cha Kingereza na kutengeneza mitaala kutoka Ethiopia.

Mama Rhoda Kahatano alijiunga na shule ya msingi Rungwe mnamo mwaka wa 1950 hadi 1955, aliingia shule ya msingi ya kati ya Kisa mwaka 1956 hadi 1957. Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari alijiunga na Chuo cha ualimu cha Mvumi na kupata cheti ya ualimu daraja la pili.

Kazi kubwa ya Mama Rhoda Kahatano, alikuwa ni mwalimu. Mbali na kuwa afisa Elimu wa Mkoa, alifanya kazi kwenye nafasi mbali mbali katika wizara ya Elimu. Alikuwa kiongozi kwenye Umoja wa Wanawake Tanzania na kuiwakilisha Tanzania kwenye mikutano mbali mbali nje ya nchi. Alikuwa Mbunge wa viti maalumu na kuifanya kazi hiyo kwa umahiri mkubwa. Inawezekana serikali imesahau kwa haraka mchango wa Mama huyu, lakini walimu na wanafunzi wake wana wajibu mkubwa wa kuziimba sifa za mama huyu na kuiga kila jema alilolifanya kwenye wizara ya Elimu.

Mungu, amlaze mahali pema peponi Mama yetu Mwalimu Rhoda Kahatano.

Na,

Padri Privatus Karugendo.

MWANA MAMA
Ananilea Nkya

Safu hii ya Mwana mama imekuwa ikikuletea wasifu wa Mwana Mama, ni jitihada za kuhakikisha mchango unaotolewa na wanawake walio hai na wale waliotangulia mbele ya haki unafahamika. Vyombo vyetu vya habri vinatawaliwa na mfumo dume, kiasi kwamba utafikiri wanaoishi ndani ya taifa hili ni wanaume peke yao. Hivyo tumeamua kuwafutatilia wanawake popote walipo na kuandika juu yao, ili jamii itambue mchango wao na historia ya nchi yetu iandikwe kwa usahihi!

Leo hii tunawaletea Mwana mama Ananilea Nkya. Huyu ni mama jasiri ambaye amejitokeza kupagania haki na usawa wa wanawake na watoto. Amepambana kukomesha ukeketaji, mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia na hasa kuhakikisha vyombo vya habari vinaandika na kufichua madhambi yote ya kuwanyanyasa na kuwatesa wawanawake na watoto.

Mama huyu ameongoza maandamano kupinga aina zote za uonevu katika taifa letu. Alipotekwa nyara, kupigwa na kuumizwa Dkt Ulimboka, Mama Ananilea, alikuwa mstari wa mbele kupinga unyama huo hadi akakamtwa na kuhojiwa na polisi. Msimamo wake, kuongea kwa kujiamini bila kuogopa, vimepelekea watu wengi kuhoji kama Mama huyu ameolewa! Kana kwamba mtu aliyeolewa, hana haki ya kuwa jasiri au kuzungumza kwa ukali juu ya mausala yanayokiuka haki nausawa. Ukweli ni kwamba mama huyu ameolewa, ana ndoa yake nzuri na watoto watatu.

Ukipata bahati ya kufanya kazi na Mama huyu ndipo unapoapata kumtambua na kumfahamu; Mama anayefanya kazi kwa kujitoa bila hata kuangalia posho na malipo; Mama anayependa kufuata muda na kuhakikisha kila kazi inafanyika kwa uhakika na utimilifu. Mama Mzalendo ambaye analipenda taifa lake na kuchukia kwa nguvu zote mfumo dume na ukatili wa ina yoyote ile wa kijinsia. Ni wazi utagundua kwamba hafanyi kazi zake ili kujijengea jina; anasukumwa na uzalendo ndani ya moyo wake. Ni mama anayetaka kuunganisha nguvu katika kufanikisha mambo; amekuwa mstari wa mbele kutaka mashirika yote yanayotetea haki za binadamu, haki za wanawake na watoto kuungana na kuwa na sauti moja. Nia yake ya kutaka kuunganisha nguvu, inampambanua na mashirika mengi yanayofanya kazi kwa lengo la kutengeneza fedha; anajipambanua na watu wote wanaofanya kazi kwa lengo la kujijengea jina na kutafuta sifa. Mama huyu anapenda majadiliiano na kuheshimu maoni ya watu wengine.

Mama huyu anauchukia ufisadi kwa chukio kamili. Anapinga mfumo wa watu wachache kupora rasilimali za taifa. Daima anasema “ Tunawaandalia watoto wetu vita. Ufisadi huu, ni lazima watoto wetu wachinjane. Hivyo ni wajibu wote sote kusimama na kusema hapana, ili tusiache maafa nyumba yetu”Mama Ananilea Nkya, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) tangia 2001 hadi mwaka huu alipomaliza kipindi chake.Anaelezwa kama miongoni mwa watu walio mstari wa mbele kupigania haki za kijinsia Tanzania. Jina la mama huyu linasikika pia katika nchi za Sweden, Holland, Ujerumani, Italia. Amesimama kidete kupaaza sauti yake juu ya ukeketaji, ukatili wa wanawake na watoto, habari za wanawake kuandikwa kwenye vyombo vya habari na usawa wa kijinsia katika vyeo vya kisiasa.Tarehe 2 Mwezi wa tatu 2010 Balozi wa Marekani Tanzania Alfonso E. Lenhardt alimtunukia mama huyu Tuzo ya Mwanamke Jasiri wa 2010 katika utetezi wa usawa, fursa sawa na haki za wanawake na watoto Tanzania. Wakati anatukiwa tuzo hiyo, alikuwa kwenye unaharakati zaidi ya miaka 20.

Wakati wa kumkabidhi tuzo hiyo Balozi wa Marekani alikuwa na haya ya kusema:

"Mama Nkya kupitia tuzo hii ya mwanamke jasiri wa mwaka 2010 unatambuliwa kwa jitihada zako kutumia vyombo vya habari kuhamasisha jamii kujua haki zao, kukemea kwa nguvu ukatili wa wanawake na kupigania mabadiliko ya sheria kandamizi kwa wanawake...Jitihada zako za kufundisha waandishi wa habari wanawake na kuwawezesha wanawake kujitetea wenyewe kumeleta mabadiliko makubwa kwa jamii ya Watanzania,"

Balozi huyo alisema Tanzania inaweza tu kupata mafanikio iwapo wanawake watashirikishwa kikamilifu katika shughuli za ukuaji wa uchumi na kwamba njia bora ya kufika huko ni kuhakikisha wanawake wanapata elimu ya vyuo vikuu.

Alisema kupigania haki za wanawake ni suala la msingi ambalo wanawake na wanaume kwa pamoja wanapaswa kujivunia nalo kwani si suala la wanawake tu kwani linahusu haki za binadamu.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Nkya aliishukuru Marekani kwa kubuni tuzo hiyo na kwamba imeonyesha namna nchi hiyo inavyounga mkono mapambano mbalimbali ya wanawake katika kupigania haki zao. Alisema wanawake wanapambana ili kuweza kushiriki katika masuala ya maendeleo ili hatimaye wanufaike na rasilimali za nchi na kwenye huduma za afya,elimu, mirathi, uchumi na uongozi wa nchi yao.

Alisema ana hakika kuwa baada ya muda, tuzo hiyo itazaa matunda ya neema hasa kwa wanawake wengi wanaotaabika kwa mambo mbalimbali mijini na vijijini ambao wanapambana ili wapate haki ya kuthaminiwa utu wao.

Alisema wanawake wengi nchini hawana amani wala furaha kwa sababu ya mifumo kandamizi imewapora haki na fursa ya kutoa maamuzi kuhusu mambo yanayohusu maisha yao na familia zao na wameporwa pia fursa ya kushiriki katika vyombo vya kutoa maamuzi.Mmama huyu alianza kazi ya uandishi wa habari 1982 RadioTanzania na wakati anajiunga na TAMWA 2001, alikuwa amepanda hadi Naibu Mhariri ndani ya RedioTanzania na kuendesha kipindi cha kutetea haki za wanawake –MWANGAZA.

Mama huyu anaamini kwamba uandishi wa habari ni kazi ya kuheshimika duniani ambayo ikitumika vizuri inaweza kuchangia kuibadilisha dunia hii kuwa sehemu nzuri ya kuishi kwa viumbe vyote.

Mwaka 1987, yeye na wanawake wengine 11 waandishi wa habari, waliungana kuunda TAMWA kama chombo cha kupigania na kulinda haki za wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari. Na mwaka hadi mwingine mchango wa TAMWA unaonekana na kusikika ndani na nje ya Tanzania. Na kwa uongozi wa Mama Ananilea, mchango wa TAMWA umesikika zaidi kufikia hatua ya kutomtenganisha Ananilea na TAMWA, kila ikitajwa TAMWA, kinachokuja kichwani mwa watu ni Ananilea!

TAMWA imechangia utungaji sera, mfano SOSPA 1998, ambapo kwa mara ya kwanza sheria inatambua ukeketaji kuwa ni kosa la jinai na kuongeza miaka ya wabakaji kuwa 30 hadi kifungo cha maisha.

Mama huyu anaamini kwamba hata kama nchi itapiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ,kama heshima na haki ya wanawake havizingatiwi, maendeleo hayo yatatiliwa mashaka.

Mama huyu ana digrii ya Uzamili ya Uandishi wa Habari kutokaCardiff, UK 1992, Digrii ya kwanza kwenye Taaluma za maendeleo kutoka Kimmege, Ireland 2008 (Daraja la kwanza), Na Diploma ya uandishi wa habari aliyoipata Dar-es-salam kutoka Tanzania School of Journalism,1986. Alitunukiwa Tuzo ya Waziri Mkuu ya Mwanamke bora mwanafunzi na tasinifu bora ya uandishi wa habari.

Aliteuliwa kwenye bodi ya wakurugenzi wa huduma ya utangazaji 2001-2003. Kamishina wa Tume ya UKIMWI2008-2011. Mbali na kazi za ofisi Mama huyu hupendelea kucheza mpira wa kikapu, kuangalia taarifa za habari na kuwezesha shughuli za maendeleo ya vijijini.

Juhudi zake za kupenda kuchochea maendeleo ya vijijini zimejionyesha kwenye mradi wa kujenga nyumba bora katika kijiji cha Mwarazi – Morogoro, ambako alienda na kuishi siku kadhaa na wanakijii na kutengeneza kamati ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba bora 60.

Kwa kifupi, huyo ndiye Mama Ananilea Nkya!

Na,

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 633122.

www.karugendo.net


MWANA MAMA PENINA MHANDO.Leo katika safu ya Mwana mama, tunawaletea Penina Mhando ambaye anajulikana pia kama Penina Mlama. Huyu ni mwandishi wa NGUZO MAMA na nguli wa sanaa za maonyesho ambaye pia ni mwandishi mahiri wa tamthiliya za Kiswahili. Huyu ndiye mtunzi wa Hatia, Tambueni Haki Zetu, Heshima Yangu, Pambo na Lina Ubani! Wakati Waswahili wanasema kwamba la kuvunda halina ubani, mama huyu anasema la kuvunda lina ubani! Mwenyewe aliigiza mchezo alioutunga mwenyewe wa Lina ubani na kuwasisimua watu wengi.

Huyu ni mama mpole na mnyenyekevu, hana mbwembwe za kisomi, maandishi yake yanachoma na kufikirisha zaidi ya anavyoonekana yeye mwenyewe. Ni mwanamapinduzi na mwanaharakati wa haki za binadamu kupindukia. Siku za hivi karibuni ameipumzisha kalamu yake lakini, kilichoandikwa kimeandikwa. Maigizo aliyoyatunga, yakitinga jukwaani ni lazima kila mtu aguswe na utunzi huo na kutambua msimamo wa mwandishi huyu mkimya anayependa kuzunguza kwa kalamu na maigizo.

Akiigiza sehemu ya Mama Liundi, kwenye kesi iliyovuma hapa Tanzania, ya mama aliyewanywesha watoto wake sumu kwa kisa cha kufuzwa na bwana wake, ndipo unapotambua uwezo mkubwa wa profesa Penina Mhando. Akiigiza unaona picha nzima kana kwamba tukio hilo ndo linatokea. Ni mama mwenye kipaji kikubwa na msomi ambaye anajishusha ili kutoa mchango wake katika jamii.

Huyu si mtu wa maneno, bali matendo. Inawezekana anatoa ujumbe kwa wasome wenzake kwa ujumbe wa maagizo: “ Mimi ni msomi kama nyinyi, fuateni mfano, jishushe tulijenge taifa letu, maana la Kuvunda lina Ubani”. Nimemlisha maneno hayo, lakini mwenye macho si lazima kumwambia tazama!

Mama Penina Mhando alikuwa mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kwa miaka mingi kabla ya kwenda Nairobi Kenya kufanya kazi na Baraza la Wanawake Waelimishaji wa Afrika (Forum for African Women Educationalists – FAWE) , kwenye ofisi ya makao makuu, jijini Nairobi.

Mama huyu ambaye ni profesa, alizaliwa mnamo mwaka 1948, katika Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro. Alifanikiwa kumaliza masomo ya juu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo alipata: B.A (Hons) – Elimu, Lugha na Sanaa za Maigizo, M.A. – Sanaa za Maigizo, Ph.D – Sanaa za Maigizo.

Penina alifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sanaa za Maigizo kwa kupanda ngazi kuanzia Msaidizi wa Mkufunzi, Mkufunzi, Mkufunzi Mkuu hadi Mhadhiri Mshiriki.

Pia mama huyu alishiriki uongozi kwenye Idara hiyo ya Sanaa na Maigizo kama Mwongozi, Idara ya Sanaa ya Muziki na Maigizo, akiwa na majukumu ya kupanga na kuendesha mipango ya ukufunzi, utafiti na huduma kwa jamii, ushiriki wa kina katika mipango ya Maendeleo ya Maigizo ambapo maigizo yalitumika kama njia ya kuhamasisha jamii katika kiwango cha shina, kwenye maeneo ya vijijini:

Pia Mwongozi Mshiriki wa Kitivo – Utafiti na Uchapishaji, Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii akiwa na majukumu ya kupanga, kusimamia na kukagua utafiti na sera ya uchapishaji na mipango katika idara kumi na mbili (12) za Kitivo. Majukumu haya yalikuwa pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa fedha kwa utafiti wa Kitivo na uchapishaji,

ikiwa pamoja na majarida ya wakufunzi:

Pia Kaimu Mwongozi wa Kitivo, Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii Akiwa na majukumu ya kupanga, kuratibu na kukagua utafiti wa ukufunzi na huduma Ushiriki katika uwekaji wa sera zinazohusiana na mipango ya mafunzo. Uongozi wa idara kumi na mbili (12) na idara moja ya utafiti, zote zikiwa chini ya Kitivo:

Pia,Ofisa Mkuu wa Ukufunzi (Deputy Chancellor) Akiwa na majukumu ya kusimamia, kuratibu na kukagua shughuli za utafiti na ushauri katika Vitivo vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo viwili vishiriki. Chuo Kikuu cha Dar-es Salaam kina Vitivo 10 na Taasisi za Utafiti 10.Majukumu yalikuwa uwekaji wa sera uhamasishaji wa fedha kutoka serikalini na kwa wafadhili kwa kuendesha mipango ya utafiti sehemu/vifaa vya ukufunzi, pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi na walimu, Uratibu wa shughuli za kawaida za utawala za Chuo Kikuu zinazohusiana na uingiaji (Admissions) wa Wanafunzi, Utafiti na Uchapishaji, Maendeleo ya /Walimu na Wafanyakazi, Stashahada za Juu, Uhusiano wa Nje na Miradi, Ukufunzi katika Chuo Kikuu, Ualimu na Uajiri.

Pia alishirikia shughuli za kijinsia kwenye chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kama Mratibu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Shughuli za Kijinsia cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akishughulikia upungufu wa uwiano wa kijinsia katika uingizaji wa wanafunzi, uajiri na wakufunzi na wafanyakazi, masomo pamoja na maslahi yote kwa ujumla Mratibu wa Mradi wa TUSEME ambao unatumia sanaa katika kumwezesha msichana kufanya vizuri zaidi katika masomo Mratibu wa Mpango wa Sanaa ya Maigizo kwa Maendeleo ambao unatumia Sanaa ya Maigizo kuwawezesha wanawake katika vijiji kupata mafanikio katika maendeleo.

Pia mama huyu ameshiriki mambo mengi ya kijamii kama, Mratibu wa mpango wa kumwendeleza mtoto kupitia sanaa katika shule za msingi jijini Dar es Salaam.ufundishaji wa waalimu na kuendesha Tamasha la Watoto la Maigizo Na mambo mengine kama vile; Mwanachama - Chama cha Sanaa cha Paukwa, Mratibu - Kikundi cha Maigizo cha Watoto cha Chuo Kikuu wakati ule akiwa Mratibu - TUSEME: Elimu ya Demokrasia kwa wanafunzi wasichana na shule za sekondari nchini Tanzania, Mwanachama - Kamati ya Uendeshaji wa Semina za Lugha katika mabadiliko yanayotarajiwa katika muundo wa ukufunzi, Mwanachama - Chama cha Wanawake wa Afrika katika Utafiti na Maendeleo (African Associationfor Women for Research and Development– AWARD).

Tunzo ambazo Prof. Penina Mlama amewahi kupata ni kama ifuatavyo: Tunzo ya Nane ya Utafiti wa Sayansi ya Jamii katika Afrika ya Mashariki na Kusini, Tunzo ya Utafiti wa Masomo ya Marekani – New York University ,Tunzo ya Mfuko wa Rockerfeller katika Sayansi ya Jamii kwenye Upembuzi wa Maendeleo, Shindano Maalum la Jinsia na Maendeleo – Shirika la Utafiti wa Sayansi ya Jamii katika Afrika Mashariki, Mwigizaji Bora wa Kike katika filamu ya “Mama Tumaini” TFC/NORAD, Tamasha la Filamu la SADDC, Harare, Tunzo ya Shaaban Robert kwa Uhamasishaji wa Kiswahili nchini Tanzania, 1999, iliyotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa

Mwanamke wa Mwaka – Taasisi ya Marekani ya Maisha ya Watu, USA.

Katika maisha yake ya kazi yake, Prof. Penina Mlama amejishughulisha

na kazi nyingi za utafiti wa kina, na kuweza kuchapisha idadi kadhaa ya

vitabu na makala, pamoja na utengenezaji wa filamu na maigizo mengi.

Huyo ndo Mama Penina Mhando, ambaye amefanya mambo mengi, ingawa hasikiki sana siku hizi, lakini mchanga wake katika taifa letu ni mkubwa.

Na,

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 633122

www.karugendo.net.


MWANA MAMA

Leo katika safu hii ya Mwana Mama tunawaletea Sista Martha Mwasu Waziri kutoka Kondoa, Huyu ni ni mshindi wa TUZO ya Mama Shujaa wa Chakula 2021-2013, ambaye aliibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia zawadi ya vifaa vya kilimo vyenye thamani ya shilingi milioni 10.

Sister Mwasu aliibuka kidedea kwa kuwaangusha washiriki wenzie 13 walioingia katika kinyanganyiro hicho kutokana na kuwa na juhudi na ubunifu mkubwa aliouonyesha kwa kipindi cha wiki mbili alizokuwa akiishi katika kijiji cha Maisha Plus zilizomsababisha kupata kura nyingi kutoka kwa wananchi Nafasi ya pili ilishikiliwa na Bi.Emilian Eligaisha kutoka Karagwe na kupewa zawadi ya vifaa vya ujenzi vya milioni 3, nafasi ya tatu ikichukuliwa na Bi. Tatu Abdi Kutoka Lushoto ambapo alipewa shilingi 700000

Akizungumza wakati akikabidhi zawadi kwa mshindi wa tuzo ya hiyo Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. January Makamba alisema kuwa kuna kila sababu ya kuboresha mazingira rafiki kwa wakulima hususani kwa akina mama kwani shughuli zote za kilimo zinafanywa na wanawake

Alisema kuwa Fikra dume, sera dume, pamoja na mipango dume huzaa matokeo dume hii inasababishwa na kuleta utofauti wa jinsia katika utekelezaji na uwajibikaji wa maendeleo

Makamba alisema kuwa asilimia 95 ya chakula tunachokula kinazalishwa na akina mama, cha kushangaza asilimia 99 ya wasiyozalisha chakula ndio wanaomiliki ardhi, na kusababisha kuwa na unyanyasaji wa kijinsi unaomgusa moja kwa moja mwanamke

Sista Martha, ni mtawa wa kanisa Katoliki huko Kondoa. Kwa maelezo yake mwenyewe alianza kutamani maisha ya utawa akiwa na umri mdogo. Alijitahidi kujiunga na mashirika ya kitawa mara tatu akishindwa kwa sababu za afya yake mbaya. Baadaye alifanikiwa na kujiunga na utawa. Mama huyu mwenye umri wa miaka 45, leo hii ni kielelezo cha mwana mama shujaa. Ushindi wake wa Maisha Plus, haukuwa wa kubahatisha.

Huyu ni Mwana Mama asiyekata tamaa. Maisha yake ya kupigania maisha ya utawa bila ya kukata tamaa ni mfano mzuri wa kupambana na maisha. Alijaribu mara tatu kujiunga na utawa anashindwa, alikini hakukata tamaa, aliendelea mpaka akafanikiwa. Lakini pia kama tutakavyoona huko mbele, huyu ni mwana mama aliyebadilisha maisha ya wanakijiji chake kwa kuanzisha mbinu ya kilimo kwa kuikomboa ardhi iliyoonekana haina faida yoyote.

Kawaida tumezoea watawa kukaa ndani na kusali. Na kuna watu wengi hata na baadhi ya viongozi wa dini wanaoamini kwamba maisha ya watawa ni kukaa ndani na kusali. Lakini kwa Martha, maisha ni sala na kazi. Ameonyesha tofauti na kupigana hadi Taifa na dunia nzima imetambua kwamba utawa si kukaa tu ndani ya nyumba. Mtawa kushinda Maisha Plus, halikuwa jambo la kawaida. Sista huyu amekuwa akiongoza juhudi za kupata ardhi katika kijiji chake. Akiwa na umri wa miaka 17, aliona umuhimu wa kupambana kukomboa ardhi ambayo alikuwa ni ya mchanga mchanga na mto wa vipindi. Kila mtu alibeza jitihada hizo, lakini mama huyu shujaa, akukata tama. Kwa jitihada hizo na kwa kusaidiana na wanashirika wenzake amefanikiwa kupata eka 18.

Katika ardhi hii iliyokombolewa na kutengenezwa vizuri ili iweze kutumika, Sista Martha na wenzake wanaweza kuendesha kilimo cha miwa, mahindi, mihogo, ndizi na viazi. Wanazalisha miwa kiasi cha kuuza na kupata faida. Pia wanatumia sehemu ya ardhi hii kufuga mbuzi na kuku. Kilimo na ufugaji vimeinua uchumi wa shirika la masisita na wanaweza kuishi maisha bora ya kujitegemea. Pamoja na kilimo, kwa vile ardhi hiyo ina mkondo wa maji ambao unakuja wakati wa masika, waliamua kutengeneza pia na bwawa la samaki. Baada ya muda, na hasa wakati wa kiangazi bwawa hilo la samaki lilikauka. Wale waliokuwa wakimbeza sista Martha, ndo walipata nafasi nzuri ya kumcheka na kuona sasa kushindwa kwake kumefika. Kama Waswahili wasemavyo kwamba ukishikwa unashikamana. Hapo ndipo Sista Martha, alipoonyesha ubunifu wake. Alianzisha mkakati wa kuyalinda mazingira kwa kupanda miti na kuhakikisha matumizi mazuri ya maji. Ingawa mama huyu hana elimu ya juu, lakini ameweza kutoa mchango mkubwa wa matumizi ya ardhi na utunzaji wa mazingira.

Kupambana na bwawa lililo kauka, kilikuwa ni kigezo kikubwa cha watu kumkubali na kuona kwamba huyu ni mbunifu na mwenye kuona mbali. Kwa kuona mfano huo wa Sista Martha, zaidi ya wanakijiji 300, wamejiunga kwenye makundi zaidi ya matano na kushirikiana na Sista Martha, kuitumia ardhi iliyoonekana haina faida yoyote, ili kuendesha kilimo na kufuga. Wote wanasema bila kuona mfano wa Sista Martha, wasingejishughulisha na kilimo hicho ambacho siku za nyuma kilionekana kama ni mchezo tu wa kuingiza.

Mafanikio ya Sista Martha, katika kijiji chake na ndani ya shirika lake, mafanikio yake ya kushinda shindano la Maisha Plus, vinampatia mama huyu nafasi ya kuonekana ni mama shujaa katika jamii. Huyu ni miongoni mwa wanawake wengi kule vijijini wanaotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa letu, lakini mama hawa hawasikiki. Na hawa watawa, wako wengi wamefanya mambo mengi makubwa, wamefanya kazi kwa hospitali, wametunza watoto wadogo kuwafundisha maadili na kuwaendeleza kwa kuwafundisha kazi za mikono na wakati mwingine hawa ndo mama wanaofundisha watoto kuanza kusoma na kuandika, lakini masisita hawa hawasikiki popote pale. Wamebaki kuwa watawa wa kanisani na kanisa linameza sifa zao zote. Viongozi wao kama mapadri na maaskofu ndo sifa zao zinachomoza kila kukicha. Ndo maana safu hii ya Mwana Mama imeamua leo kukuletea habari za mama huyu ambaye kwa nafasi yake ametoa mchango chanya kwenye taifa letu.

Na,

Padri Privatus Karugendo.EMILIANA ALIGAESHA MAMA SHUJAA WA CHAKULA – MAISHA PLUS 2012.


Katika jitihada za kuwaletea wasomaji wetu wasifu wa Mwana mama leo tumeamua kwenda vijijini. Wiki iliyopita tulikuwa Singida, na sasa tumesogea mbali kidogo hadi mkoa wa Kagera. Lengo ni kuwaletea habari za mama zetu wanaoishi pembezoni sambamba na wale wanaoishi mijini, wasomi, wanasiasa, wafanyakazi, wafanyabiashara hata pia wanawake wa ndani wanaochangia maendeleo katika taifa letu. Hata hivyo kila mama ana mchango mkubwa; wa kuzaa, kulea na kutunza familia; mafanikio ya familia, mafanikio ya mtu binafsi na hata mafanikio ya taifa, nyuma yake kuna mwanamke!

Mwana mama aliyeshika nafasi ya pili katika shindano la Mama shujaa wa Chakula Maisha Plus 2012, ni Emiliana Aligaesha, kutoka Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Karagwe. Mama huyu mwalimu mstaafu mwenye umri wa miaka 69, ni mkulima wa migomba, mahindi, maharagwe na kahawa. Anaendesha kilimo hai na kuwa mfano kwa ndugu, jamaa na marafiki wanaomzunguka.

Kilimo hai, ni kulima kwa kutumia mboji, bila kutumia mbolea za kemikali. Kutandaza nyasi kwenye shamba na kuhakikisha matumizi ya jadi kupambana na wadudu ili kuepukana na matumizi ya dawa za kemikali. Mazao yanayotokana na kilimo hai, yanakuwa na bei kubwa nje na ndani ya nchi. Mfano kahawa iliyolimwa kwa mfumo huu wa kilimo hai, inakuwa na bei ya juu kwenye soko la dunia, maana wenzetu wanaepuka matumizi ya dawa za kemikali ambazo zimeonyesha kuwa na athari kubwa kwa afya ya binadamu, viumbe, ardhi na mazingira pia.

Mbali na kilimo, mama huyu pia ni mfugaji. Ana ng’ombe sita wa kisasa. Anazalisha maziwa na kuuza. Anapata kipato, lakini pia anachangia kuboresha afya ya jamii inayomzunguka. Pia mifugo hii inamsaidia kupata mbolea ya kuweka kwenye shamba lake na kuepukana kabisa na matumizi ya mbolea ya chumvi chumvi

Msimamo wake, aliourithi kutoka kwa mama yake ni kwamba “ mtu yeyote anayeingia shambani, akakata ndizi na kwenda kuipika bila kuangalia magugu yaliyo shambani, anakuwa ni mwizi”. Huo ni msimamo wa mtu mchapakazi. Maana yake ni kwamba, kabla ya kukata ndizi shambani ni lazima kuhakikisha magugu yanapaliliwa! Watu wote, na hawa wa wilaya ya Karagwe, wakifuata msimamo huo wa kupalilia kabla ya kukata ndizi, watakuwa na mashamba mazuri na kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara.

Mama huyu amekuwa mjane, tangia mwaka 1992. Mshahara wake wa ualimu usingemtosha yeye na familia yake, hivyo aliamua kuingia kwa nguvu zote katika kilimo na kufanya uamuzi wa kufuata kilimo hai. Ana ekari sita ambazo anazilima kwa mfumo huu wa kilimo hai na kuzalisha kahawa kwa wingi. Kilimo hiki cha kilimo hai kimemwezesha kuwasomesha watoto wake tisa hadi kwenye ngazi ya vyuo.

Pamoja na kilimo hiki cha kukuza kipato cha familia yake, mama huyu pia amekuwa akizalisha miche ya kahawa na mazao mengine na kuwauzia wakulima wengine. Amekuwa ni mtafiti katika suala zima la kilimo hai na kusaidia kuendesha mafunzo ya wakulima katika vijiji vya wilaya ya Karagwe.

Mama huyu amefuta mawazo ya wengi kwamba wakulima wadogo wadogo hawana faida na kilimo. Yeye ni mkulima mdogo, lakini kwa vile analitunza vizuri shamba lake, ameweza kupata faida kubwa. Kwa kutambua jitihada zake chama cha Ushirika cha Kahawa cha Karagwe (KDCU) mnamo mwaka wa 2005, kilimteua mama huyu kuwa mjumbe wa Halmashauri ya Ushirika huo, akiwa ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 9 ya nyuma.

Wilaya ya Karagwe, inazalisha kahawa kwa wingi. Hili ndilo zao kuu la biashara la Wilaya hii. Na kama ilivyo kwa mfumo dume, kazi nyingi za kuhudumia zao hili zinafanywa na wanawake, lakini mapato yanakwenda kwa wanaume. Imani kwamba wanaume ndo wana uwezo wa kupanga matumizi na kutunza familia. Bahati mbaya kwa asilimia kubwa wanaume wamekuwa wakifaidi asilimia kubwa ya mapato ya kahawa kuliko wanawake na watoto.

Mama Aligaesha, ameweza kuonyesha wazi kwamba hata wanawake wakipata nafasi, si lazima iwe kwa kuwa mjane kama yeye, wanaweza! Yeye ameweza kuyatumia vizuri mapato ya kahawa kwa kuwasomesha watoto na kutengeneza maisha bora kwa familia yake na jamii inayomzunguka.

Mbali na kuwa mwanachama wa chama cha Ushirika cha Kahawa cha Karagwe, mama huyu pia ni mwanachama wa shirika la KADERES. Shirika hili linaendesha umoja wa kuweka na kukopa. Na limefanya kazi kubwa kuviendeleza vikundi hivi na kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu vijijini. Pia shirika hili la KADERES, limekuwa mstari wa mbele kuendeleza Kilimo hai na kutafuta soko zuri la kahawa nje ya nchi. Shirika hili sasa hivi limeanzisha kampuni ya kuuza kahawa nje ya nchi. Mwaka huu, shirika hili limewalazimisha watu wanaonunua Kahawa wilaya ya Karagwe kupanga bei nzuri, baada ya shirika hili kupitia kampuni yake ya kuuza kahawa kutangaza bei nzuri ya shilingi elfu moja miatano kwa kilo. Mama Emiliana Aligaesha, amekuwa ni mwanachama hai wa shirika hili la KADERES, na ni mmoja wa wale wanaofaidi soko la nje la Kampuni hii ya KADERES.

Pia shirika la KADEES, lilimuunga mkono mama Emiliana Aligaesha, kwenda kwenye shindano la mama shujaa wa chakula-Maisha plus. Haikushangaza mama huyu kuchukua nafasi ya pili kwenye mashindano haya, maana huyu ni mama aliyetoka kwenye mazingira ya kuchapa kazi na ni shujaa kwa miaka mingi. Huyo ndiye Mama Emiliana Aligaesha, mshindi namba mbili ya Mama Shujaa wa chakula – Maisha pulus 2012.

Na,

Padri Privtus Karugendo.


MWANA MAMA

TATU ABDI JUMA.

Katika safu yetu ya Mwana Mama, leo tunakuletea Tatu Abdi Juma, kutoka Lushoto Tanga. Mama huyu mwenye umri wa miaka 49 alishika nafasi ya tatu katika shindano la Mama shujaa wa Chakula 2012. Yeye ni mkulima na mfugaji. Ana shamba lenye ekari sita, ana ng’ombe 4, kondoo 8 na kuku 20.

Mashindano ya Mama shujaa wa chakula, yameanza kuwaibua wanawake wanaofanya mambo makubwa lakini walikuwa hawajulikani. Ndo maana tunapendekeza mashindano haya yaendelee na yaungwe mkono na wale wote wanaotetea haki za wanawake na kutamani kuona wanawake wanamiliki mali nakutoa mchango katika kuliendeleza taifa letu la Tanzania. Kuna walioanza kuyabeza mashindano haya, lakini sasa inaelekea walikuwa wakijidanganya. Ukweli unajionyeshana sisi sote ni mashuhuda wa ukweli huu. Tulikuwa tunabaki kuimba wimbo wa wanawake wanaweza, wakati kuna wanawake wanaoitekeleza kaulimbiu hii kwa vitendo. Hivyo wale wote wanaotetea haki za wanawake wangebuni mbinu za kuwaibua wanawake hawa na kuacha maneno matupu.Hapana shaka kwamba baada ya mashindano ya mama shujaa wa chakula, kuna mashirika na makampuni yatakayokuwa yameguswa na maisha na jitihada za Tatu Abdi Juma na kutaka kumpatia mtaji zaidi. Na kwa njia hii wanawake wengine watanufaika. Bila shindano hili, mama huyu asingefahamika na juhudi zake zingebaki kijijini kwake na ndani ya familia yake.

Vijijini kuna wanawake wengi kama Tatu Abdi Juma. Wanalima, wanafuga na kufanya miradi mingine ya maendeleo, tatizo ni kwamba hawana masoko ya uhakika wa kuuza mazao yao na bidhaa nyinginezo wanazozizalisha. Ni kazi ya serikali kuliona hili na kulishughulikia. Badala ya kuendelea kuimba wimbo ule ule tuliouzoea wa “Wanawake wanaweza”, zibuniwe mbinu za kuwatafutia wanawake hawa masoko ya uhakika.

Tatu Abdi Juma, analima kilimo cha kisasa, alipata mafunzo kwenye chuo cha Kilimo na mifugo Tengeru na pia alisaidiwa na shirika Oxfam kupata ujuzi zaidi. Analima kilimo cha kumwagilia. Katika shamba lake ana uwezo wa kuvuna majunia 20 ya mahindi kutoka kwenye heka moja. Analima pia viazi mviringo na maharagwe. Kwa vile anafuga kisasa, ana uwezo wa kupata lita 200 za maziwa.

Mama huyu ni mjane na mfano wa kuigwa kwa wanawake wa Lushoto na Tanzania nzima. Kufuatana na utamaduni wa wilaya ya Lushoto, kama ilivyo kwa tamaduni nyingi za Tanzania, ardhi ni mali ya wanaume. Kule Lushoto, wanaitia Shamba la mzee. Na tamaduni za kule mwanaume anakuwa na wanawake wengi zaidi ya watatu. Ni nadra sana kijana mwenye umri wa miaka 30 kuwa na mwanamke mmoja.

Tatu aliolewa akiwa na umri wa miaka 20, kama mke wa pili. Kwa maoni yake mwenyewe ni kwamba wanawake wanatumika kama jembe au trekita la kulimia na kuzalisha mali. Hivyo alitumia muda mwingi akilima kwenye shamba la mme wake. Kwa vile alikuwa kwenye ndoa ya wake wengi, maisha yake yalikuwa magumu pale mme wake alipofariki.

Ndugu na jamaa wa mme wake walimfukuza kwenye ardhi aliyokuwa akilima na kuzalisha chakula. Alinyang’anywa mifugo yake na fedha zake zaidi ya shilingi 600,000. Kwa vile yeye ni mama shujaa, alipambana kupitia serikali za mitaa na hatimaye alifanikiwa kupata nusu ya arithi ya mme wake na kuendeleza kilimo na ufugaji.

Alijiunga kwenye vikundi vya wanawake na kufanikiwa kupata mikopo ya fedha na mifugo. Mafanikio yake ya leo yanatokana na juhudi ya kufanya kazi na kupambana na maisha bila kutegemea msaada na kuomba omba.

Tanzania tuna kasumba ya kufikiri kwamba ili tuendelee ni lazima tupate misaada kutoka nchi za nje. Ukweli ni kwamba tuna utajiri mkubwa. Kinachohitajika ni kufanya kazi na kutengenezewa mifumo mizuri ya kupata mitaji na soko la uhakika.

Na jambo la msingi ni kuhakikisha kila mwananchi ana haki ya kumiliki ardhi. Tunasema kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Hivyo bila watu kumiliki ardhi ni vigumu kilimo kikawa uti wa mgongo. Tumeona mfano mzuri wa mama huyu ambaye kwa kutumia ardhi ameweza kuendesha maisha yake. Ilivyowezekana kwa mama huyu inawezekana pia kwa kila Mtanzania.

Changamoto anayoipata mama huyu ni kutokuwa na vifaa vya kilimo vya kisasa na magomvi ya wakulima na wafugaji. Haya ni matatizo sugu ya Tanzania. Watanzania wengi wanaendesha kilimo cha jembe la mkono na wakulima na wafugaji wamekuwa na migogoro ya ardhi. Wakati wakulima wanahitaji ardhi kulima mazao wafugaji wanahitaji ardhi kutunza mifugo yao.

Tunachojifunza hapa ni kwamba ni muhimu kuwa na sheria inayoruhusu wanawake kumiliki ardhi; kwa vile ndoa za wanawake wengi ni sehemu ya utamaduni wa Mtanzania, basi iwepo sheria ya kuhakikisha kila mwanamke anapata haki katika ndoa yake na hasa haki ya kumiliki ardhi. Jambo la pili tunalojifunza ni kwamba ili kuzalisha na kupata faida kubwa ni lazima kutumia vifaa vya kisasa. Hivyo ni wajibu wa serikali kuwawezesha wakulima kupata vifaa vya kisasa. Tusiendelee kuimba wimbo wa kilimo kwanza, bila kufanya jitihada za kukiendeleza kilimo. Jambo la tatu ni kwamba ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugani ni lazima kupanga vizuri matumizi ya ardhi yetu: Na mipango hii isiwe na upendeleo wa upande wowote. Jambo la tatu la kujifunza ni kwamba kule vijijini wako wanawake wengi kama huyu Mama Tatu, tatizo ni kwamba hawasiki! Hivyo tuwaibue, ili tukomeshe utamaduni wa kulalamika na kuimba nyimbo za wanawake wanaweza!

Na,

Padri Privarus Karugendo.


MWANA MAMA AMINA CHIFUPA.

Kati safu yetu ya Mwana Mama, leo tunawaletea mwana mama Marehemu Amina Chifupa. Ni mwana mama aliyeishi miaka michache hapa duniani, lakini alitoa mchango mkubwa katika taifa letu na kupendwa na watu wengi. Kifo chake kilitufundisha kwamba sila lazima kukaa miaka mingi duniani ndipo mtu atoe mchango wake. Mtu anaweza kuishi miaka michache na kuacha makubwa nyuma yake, ndivyo ilitokea kwa mwana mama Amina Chifupa.

Mchango wake mkubwa ni kujitokeza wazi wazi kupambana na dawa za kulevya. Kitu kikubwa ambacho watanzania wengi wanakumbuka ni pale Amina Chifupa, aliposimama Bungeni na kusema “ Hata kama ni mume wangu anauza dawa za kulevya, nitasimama na kumtaja bila kuogopa”. Iliaminika alikuwa na majina ya wauza unga, na habari za kuaminika ni kwamba majina hayo aliyapeleka Ikulu. Na kuna wakati hata Rais Kikwete, alitamka kuwajua watu hao, ingawa hadi leo hakuna aliyewekwa ndani kwa biashara hii inayoharibu vijana.

Tutamkumbuka Amina Chifupa kwa ucheshi na uwezo mkubwa wa kujenga hoja mbalimbali ndani na nje ya Bunge. Katika kipindi kifupi akiwa Mwanasiasa kijana, aliweza kusimama na kujipembua na wabunge wengine kwa kusimama kidete kupiga vita biashara ya mihadarati ambayo aliamini inaua vijana ambao ni viongozi wa kesho.

Kwa ufupi Amina Chifupa alikuwa ni mbunge ambaye alisimama kidete kutoboa siri za biashara za mihadarati na kuna wakati alipata kutishiwa na Polisi na kulazimika kumpa ulinzi kwa muda kutokana na vitisho hivyo. Amina alifariki akiwa na msuguano na baadhi ya viongozi wa UVCCM ambao walituhumiwa kumwona kuwa tishio katika nafasi ya uenyekiti wa Umoja huo ngazi ya Taifa.Taarifa za madaktari wa Lugalo zilionyesha kuwa Amina alifariki kutokana na shinikizo la damu na kisukari, magonjwa ambayo haikuwahi kushuhudia wakati wa uhai wake. Wengine wanadai kilichomuua Amina, mmoja ni kujitoa kwake mhanga katika vita dhidi ya mihadarati kwa maana ya dawa za kulevya. Kifo chake kiliacha maswali mengi na kila mtu alikuwa na la kwake.

Kuna uvumi kwamba alikuwa na siri nyingi, na baadhi ya vigogo waliogopa siri hizo kuwekwa wazi. Maana kama alikuwa tayari kutoboa siri hata za mme wake, angeficha siri za nani? Ujasiri wake, wengine waliuchukulia kuwa ni “Uchizi”. Na Chizi si mtu wa kuamini! Mungu ndiye anajua, lakini kifo cha Amina Chifupa, kiliacha mengi nyuma yake.Majuma mawili kabla ya kifo chake Spika wa bunge la 9 Samuel Sitta aliwatangazia wabunge kuhusu kuugua kwa Amina na akawaomba wabunge wamwombee aweze kupona haraka Na hapo ndipo habari zikazagaa Tanzania juu ya ugonjwa wa Amina Chifupa Hata hivyo watu hawakuamini kwamba ugonjwa huo ungeyatoa maisha ya Amina Chifupa, mwana mama aliyekuwa amejitengenezea jina kubwa kwa kusimama kidete kutetea maisha ya vijana.Tarehe 26, 2007 ilikuwa ni siku ya Jumanne ambayo kwa watunza kumbukumbu za matukio yanayogusa jamii ni siku ambayo haitosahaulika kirahisi nchini Tanzania kufuatia Taaarifa za kushtua, baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Amina Chifupa Mpakanjia kufariki dunia. Na jambo la kushangaza, alikufa siku kupinga dawa za kulevya duniani. Yeye alipiga vita kwa nguvu zote dawa hizo za kulevya na Mungu akamchukua siku hiyo hiyo.Amina Chifupa alifariki akiwa na umri wa miaka 26 majira ya saa 3:00 katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Lugalo Dar es Salaam kwa maradhi ya mfadhaiko wa akili yaani “depression”. Kuugua kwa Amina kulianza kama mzaha huku kukigubikwa na habari za yeye kutalikiwa na mumewe Mpakanjia.Msiba wake Dar-es-Salaam na Njombe alikozikwa ulikusanya watu wengi:

Miongoni mwa waombolezaji waliojumuika na familia ya Chifupa, ni Mama Maria Nyerere, Mwanasiasa Mkongwe Mzee Rashid Kawawa (marehemu), Profesa Mark Mwandosya wakati huo akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Katibu wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad, John Mnyika wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Vijana CHADEMA, baadhi ya wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi wa kawaida.Maelfu ya wakazi wa Jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake siku ya Jumatano ya Juni 27, 2007 walifurika pembezoni mwa barabara za Bagamoyo na Kambarage wakiwa wameduwaa, wenye majonzi wakiupokea mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM Amina Chifupa.Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam wakati huo Hemed Mkali alisema kuwa kifo cha Amina kimedhihirisha kuwa kweli alikuwa anaumizwa na matatizo ya dawa za kulevya nchini kwani kimetokea siku iliyotengwa na dunia kupiga vita dawa za kulevya.Meya wa Jiji la Dar wakati huo Adama Kimbisa alisema Amina alikuwa kijana mwenye kusimamia ukweli, haki na maadili. Kimbisa alisema katika vikao mbalimbali jambo na kulitetea kwa kufuata misingi ya haki.Mkurugenzi wa Clouds FM Joseph Kusaga alimwelezea Amina Chifupa ilikuwa ni hazina kwa taifa hasa kwa wasichana wadogo kutokana na kipaji alichojaliwa kujiamini katika maisha yake tangu utotoni.Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) wakati huo Profesa Mark Mwandosya alisema kifo cha Amina kimeacha changamoto kubwa kwa serikali na wadau wengine kushughulikia tatizo la kushamiri kwa dawa kulevya nchini.Kwa upande wake Maalim Seif Shariff Hamad Katibu Mkuu wa CUF alisema Amina alishughulikia kero mbalimbali zinazoiathiri jamii bila kujali itikadi za kisiasa, alikuwa mwanasiasa chipukizi aliyejitolea kushughulikia kero za wananchi bila woga.

Amina alizaliwa Mei 20, 1981 mjini Dar es Salaam, alisoma Shule ya Msingi Ushindi, Mikocheni Dar (1988-1994) kabla ya kujiunga na masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Wasichana ya Kisutu, Dar (1995-1998). Elimu ya Juu ya Sekondari alisoma katika shule ya Makongo (1999-2001) kabla ya kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habri cha Royal (2001-2003) ambako alifuzu Diploma ya Uandishi wa Habari.Mwaka 1999 alianza kazi ya Utangazaji wa Kituo cha Redio cha Clouds FM cha Dar na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mama Shughuli.Katika CCM aliwahi kuwa Kamanda wa CCM wa umoja wa Vijana katika tawi la Mikocheni A jijini Dar na alikuwa Katibu wa Kamati ya Uchumi ya UVCCM mkoa wa Dar, aliwahi kuwa Mama Mlezi wa UVCCM na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) matawi ya Bunju na Mbagala.Amina Chifupa, anakumbukwa kwa kutetea maisha vijana bila kuangalia itikadi. Aliyatetea maisha ya vijana wote wa Tanzania. Hakupenda dawa za kulevya kutumia kuharibu maisha ya vijana wa Tanzania. Huyu alikuwa Mwana Mama jasiri, ambaye hata kama ni marehemu anastahili kutunukiwa tuzo ya Mama Jasiri, inayotolewa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania.Na,

Padri Privatus Karugendo

www.karugendo.net

+255 754 633122

MWANA MAMA
Ananilea Nkya

Safu hii ya Mwana mama imekuwa ikikuletea wasifu wa Mwana Mama, ni jitihada za kuhakikisha mchango unaotolewa na wanawake walio hai na wale waliotangulia mbele ya haki unafahamika. Vyombo vyetu vya habri vinatawaliwa na mfumo dume, kiasi kwamba utafikiri wanaoishi ndani ya taifa hili ni wanaume peke yao. Hivyo tumeamua kuwafutatilia wanawake popote walipo na kuandika juu yao, ili jamii itambue mchango wao na historia ya nchi yetu iandikwe kwa usahihi!

Leo hii tunawaletea Mwana mama Ananilea Nkya. Huyu ni mama jasiri ambaye amejitokeza kupagania haki na usawa wa wanawake na watoto. Amepambana kukomesha ukeketaji, mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia na hasa kuhakikisha vyombo vya habari vinaandika na kufichua madhambi yote ya kuwanyanyasa na kuwatesa wawanawake na watoto.

Mama huyu ameongoza maandamano kupinga aina zote za uonevu katika taifa letu. Alipotekwa nyara, kupigwa na kuumizwa Dkt Ulimboka, Mama Ananilea, alikuwa mstari wa mbele kupinga unyama huo hadi akakamtwa na kuhojiwa na polisi. Msimamo wake, kuongea kwa kujiamini bila kuogopa, vimepelekea watu wengi kuhoji kama Mama huyu ameolewa! Kana kwamba mtu aliyeolewa, hana haki ya kuwa jasiri au kuzungumza kwa ukali juu ya mausala yanayokiuka haki nausawa. Ukweli ni kwamba mama huyu ameolewa, ana ndoa yake nzuri na watoto watatu.

Ukipata bahati ya kufanya kazi na Mama huyu ndipo unapoapata kumtambua na kumfahamu; Mama anayefanya kazi kwa kujitoa bila hata kuangalia posho na malipo; Mama anayependa kufuata muda na kuhakikisha kila kazi inafanyika kwa uhakika na utimilifu. Mama Mzalendo ambaye analipenda taifa lake na kuchukia kwa nguvu zote mfumo dume na ukatili wa ina yoyote ile wa kijinsia. Ni wazi utagundua kwamba hafanyi kazi zake ili kujijengea jina; anasukumwa na uzalendo ndani ya moyo wake. Ni mama anayetaka kuunganisha nguvu katika kufanikisha mambo; amekuwa mstari wa mbele kutaka mashirika yote yanayotetea haki za binadamu, haki za wanawake na watoto kuungana na kuwa na sauti moja. Nia yake ya kutaka kuunganisha nguvu, inampambanua na mashirika mengi yanayofanya kazi kwa lengo la kutengeneza fedha; anajipambanua na watu wote wanaofanya kazi kwa lengo la kujijengea jina na kutafuta sifa. Mama huyu anapenda majadiliiano na kuheshimu maoni ya watu wengine.

Mama huyu anauchukia ufisadi kwa chukio kamili. Anapinga mfumo wa watu wachache kupora rasilimali za taifa. Daima anasema “ Tunawaandalia watoto wetu vita. Ufisadi huu, ni lazima watoto wetu wachinjane. Hivyo ni wajibu wote sote kusimama na kusema hapana, ili tusiache maafa nyumba yetu”Mama Ananilea Nkya, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) tangia 2001 hadi mwaka huu alipomaliza kipindi chake.Anaelezwa kama miongoni mwa watu walio mstari wa mbele kupigania haki za kijinsia Tanzania. Jina la mama huyu linasikika pia katika nchi za Sweden, Holland, Ujerumani, Italia. Amesimama kidete kupaaza sauti yake juu ya ukeketaji, ukatili wa wanawake na watoto, habari za wanawake kuandikwa kwenye vyombo vya habari na usawa wa kijinsia katika vyeo vya kisiasa.Tarehe 2 Mwezi wa tatu 2010 Balozi wa Marekani Tanzania Alfonso E. Lenhardt alimtunukia mama huyu Tuzo ya Mwanamke Jasiri wa 2010 katika utetezi wa usawa, fursa sawa na haki za wanawake na watoto Tanzania. Wakati anatukiwa tuzo hiyo, alikuwa kwenye unaharakati zaidi ya miaka 20.

Wakati wa kumkabidhi tuzo hiyo Balozi wa Marekani alikuwa na haya ya kusema:

"Mama Nkya kupitia tuzo hii ya mwanamke jasiri wa mwaka 2010 unatambuliwa kwa jitihada zako kutumia vyombo vya habari kuhamasisha jamii kujua haki zao, kukemea kwa nguvu ukatili wa wanawake na kupigania mabadiliko ya sheria kandamizi kwa wanawake...Jitihada zako za kufundisha waandishi wa habari wanawake na kuwawezesha wanawake kujitetea wenyewe kumeleta mabadiliko makubwa kwa jamii ya Watanzania,"

Balozi huyo alisema Tanzania inaweza tu kupata mafanikio iwapo wanawake watashirikishwa kikamilifu katika shughuli za ukuaji wa uchumi na kwamba njia bora ya kufika huko ni kuhakikisha wanawake wanapata elimu ya vyuo vikuu.

Alisema kupigania haki za wanawake ni suala la msingi ambalo wanawake na wanaume kwa pamoja wanapaswa kujivunia nalo kwani si suala la wanawake tu kwani linahusu haki za binadamu.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Nkya aliishukuru Marekani kwa kubuni tuzo hiyo na kwamba imeonyesha namna nchi hiyo inavyounga mkono mapambano mbalimbali ya wanawake katika kupigania haki zao. Alisema wanawake wanapambana ili kuweza kushiriki katika masuala ya maendeleo ili hatimaye wanufaike na rasilimali za nchi na kwenye huduma za afya,elimu, mirathi, uchumi na uongozi wa nchi yao.

Alisema ana hakika kuwa baada ya muda, tuzo hiyo itazaa matunda ya neema hasa kwa wanawake wengi wanaotaabika kwa mambo mbalimbali mijini na vijijini ambao wanapambana ili wapate haki ya kuthaminiwa utu wao.

Alisema wanawake wengi nchini hawana amani wala furaha kwa sababu ya mifumo kandamizi imewapora haki na fursa ya kutoa maamuzi kuhusu mambo yanayohusu maisha yao na familia zao na wameporwa pia fursa ya kushiriki katika vyombo vya kutoa maamuzi.Mmama huyu alianza kazi ya uandishi wa habari 1982 RadioTanzania na wakati anajiunga na TAMWA 2001, alikuwa amepanda hadi Naibu Mhariri ndani ya RedioTanzania na kuendesha kipindi cha kutetea haki za wanawake –MWANGAZA.Mama huyu anaamini kwamba uandishi wa habari ni kazi ya kuheshimika duniani ambayo ikitumika vizuri inaweza kuchangia kuibadilisha dunia hii kuwa sehemu nzuri ya kuishi kwa viumbe vyote.Mwaka 1987, yeye na wanawake wengine 11 waandishi wa habari, waliungana kuunda TAMWA kama chombo cha kupigania na kulinda haki za wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari. Na mwaka hadi mwingine mchango wa TAMWA unaonekana na kusikika ndani na nje ya Tanzania. Na kwa uongozi wa Mama Ananilea, mchango wa TAMWA umesikika zaidi kufikia hatua ya kutomtenganisha Ananilea na TAMWA, kila ikitajwa TAMWA, kinachokuja kichwani mwa watu ni Ananilea!TAMWA imechangia utungaji sera, mfano SOSPA 1998, ambapo kwa mara ya kwanza sheria inatambua ukeketaji kuwa ni kosa la jinai na kuongeza miaka ya wabakaji kuwa 30 hadi kifungo cha maisha.Mama huyu anaamini kwamba hata kama nchi itapiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ,kama heshima na haki ya wanawake havizingatiwi, maendeleo hayo yatatiliwa mashaka.Mama huyu ana digrii ya Uzamili ya Uandishi wa Habari kutokaCardiff, UK 1992, Digrii ya kwanza kwenye Taaluma za maendeleo kutoka Kimmege, Ireland 2008 (Daraja la kwanza), Na Diploma ya uandishi wa habari aliyoipata Dar-es-salam kutoka Tanzania School of Journalism,1986. Alitunukiwa Tuzo ya Waziri Mkuu ya Mwanamke bora mwanafunzi na tasinifu bora ya uandishi wa habari.

Aliteuliwa kwenye bodi ya wakurugenzi wa huduma ya utangazaji 2001-2003. Kamishina wa Tume ya UKIMWI2008-2011. Mbali na kazi za ofisi Mama huyu hupendelea kucheza mpira wa kikapu, kuangalia taarifa za habari na kuwezesha shughuli za maendeleo ya vijijini.Juhudi zake za kupenda kuchochea maendeleo ya vijijini zimejionyesha kwenye mradi wa kujenga nyumba bora katika kijiji cha Mwarazi – Morogoro, ambako alienda na kuishi siku kadhaa na wanakijii na kutengeneza kamati ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba bora 60.

Kwa kifupi, huyo ndiye Mama Ananilea Nkya!

Na,

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 633122.

www.karugendo.net

MWANA MAMA,


MAIMUNA KANYAMALA.

Mama Maimuna Kanyamala, ni mwanamke wa nne kupokea tuzo ya mwanamke jasiri inayotolewa na Balozi wa Amerika, Tanzania. Wakati akipokea tuzo hiyo, alitoa maneno yanayoonyesha kwamba tuzo hiyo hakuipata kwa bahati mbaya bali alistahili asilimia mia moja

“…ukatili dhidi ya wanawake unawaumiza, unawaletea ulemavu na kuwaua wanawake wengi zaidi ya malaria, vita, kansa na ajali za barabarani”

Wimbi kubwa la mauaji ya wanawake vikongwe yamefanyika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Mauaji ya albino yamefanyika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Lakini pia kumekuwepo na ukatili wa kutisha wa wanawake katika mikoa ya kanda ya ziwa, hasa Musoma, Mwanza na Shinyanga. Mama Maimuna Kanyamala, amefanya kazi katika mazingira haya ambayo mfumo dume umesimika mizizi na amepigana bega kwa bega na wanaharakati wengi kutokomeza vitendo hivi vya kuwanyanyasa na kuwatesa wanawake.Mama Maimuna Kanyamala ni miongoni mwa wanawake sita walioamua kuanzisha shirika la Kivulini mnamo mwaka 1999 na amekuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika hili hadi leo hii. Shirika hili ni la kutetea na kulinda haki za wanawake Mkoani Mwanza na maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria. Juhudi za mama huyu, zilimpelekea kuchukiwa na wanaume na kumpachika majina kama “Adui wa wanaume” na mtu “anayewapatia kichwa kikubwa wanawake” .Baadhi ya watu wanafikiri hawa wana mama wanaojitolea kutetea haki za binadamu hawana ndoa. Wanafikiri wanaweza kusimama na kukemea vitendo vya unyanyasaji wa wanawake kwa vile wao hawana wanaume. Jambo hili si la ukweli. Mama Kanyamala, alikuwa na ndio yake nzuri mpaka pale alipofiwa na mme wake siku za hivi karibuni. Ni mama wa watoto watatu, aliowalea vizuri na kuwapatia maadili bora.Mama Maimuna Kanyamala ana uzoefu mkubwa na amesomea masuala ya maendeleo ya Jamii.

Ana digrii ya uzamili katika taaluma za maendeleo aliyoipata katika chuo cha Holly Ghost College, Kimmage Manor, Ireland.Mama huyu pia amesomea mambo ya ustawi wa jamii katika chuo cha Ustawi jamii na kupata cheti daraja la kwanza. Pia ana diploma ya uongozi na katibu muhtasi kutoka chuo cha biashara cha Shinyanga.Pia mama Huyu amesoma mambo mbali mbali ya kuendesha mashirika yasiyokuwa ya serikali kutoka sehemu mbali mbali kama vile chuo cha MS-TCDC , USIS & USAID Tanzania, Catholic Relief Services Tanzania, World Bank Institute, REPOA Dar es Salaam

: Jinsia na Haki za binadamu, Ushawishi na utetezi, uhamasishaji, usimamizi wa fedha na utawala, bajeti na matumizi, tathimini nkKabla ya kuanzisha KIVULINI, alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi sehemu mbali mbali, Uzazi wa mpango wa Taifa, na afisa utawala katika mradi wa kuendeleza makao makuu Dodoma na kuongoza kitengo cha utetezi katika shirika la kutetea haki za watoto la Kuleana.Hata hivyo uwezo mkubwa na ujasiri wa mama Maimuna Kanyamala umeonekana kwenye kuliongoza shirika la Kivulini, ambalo kwa maoni ya wengi shirika hili limekuwa sehemu ya maisha ya mama huyu. Utetezi wa haki za wanawake na watoto, ni kitu kilicho kwenye damu yake.Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanawake lenye makao yake makuu jijini Mwanza linalokutanisha watu wa jinsia zote kujadili, kutafakari na kutafuta suluhisho la ukatili majumbani. Neno Kivulini linalotambulisha shirika hili linatokana na neno kivuli, kwa maana ya chini ya mti au paa ambako watu hukutana na kujadiliana kwa amani juu ya matatizo yao katika jamii. Ndoto za kivulini ni kujenga jamii salama isiyokuwa na ukatili ambayo haki za wanawake zinathaminiwa na kuheshimiwa.

Si kivuli cha maneno, ni kivuli kweli. Ukifika Jijini Mwanza, utakiona kivuli hicho kinachowakusanya watoto, vijana, wazee wake kwa waume, kama si majadiliano juu ya usuluhishi katika familia, watakuwa wanajadili mbinu za kutumia kutokomeza ukeketaji, kupambana na ukatili majumbani, kuomba msaada wa kisheria juu ya mirathi, midahalo juu ya vyanzo vya ongezeko la ukatili katika jamii, kujengewa uwezo juu ya ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa habari.

Ingawa jiji la Mwanza lina mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserikali, Kivulini ni shirika pekee lilioanzishwa na wanawake na linalishughulikia kuzuia ukatili majumbani. Pia ni shirika pekee lenye mfumo wa kushirikiana na makundi mbalimbali katika jamii kama viongozi wa mitaa, vijiji, dini, vikundi vya kijamii na wanaharakati wa kujitolea.

Shirika la kivulini linachukua jukumu la kujenga uwezo wa kuelewa madhara ya ukatili unaotendeka majumbani miongoni mwa makundi mbali mbali na kuyaachia makundi hayo kubuni mbinu za kukomesha ukatili majumbani. Wawezeshaji wa Kivulini, hawachagui wala kupendekeza mbinu yoyote. Kazi yao ni kuelekeza ,kushauri, kuchochea, kuhamasisha na kupandikiza mbegu ya ujuzi na utaalam katika mfumo mzima. Maamuzi ya nini kifanyike yanabaki mikononi mwa walengwa!

Jambo jingine la pekee katika shirika hili, ni kwamba wanawaachia uhuru wanajamii kuchagua ni kitu gani wangependa kujifunza kuhusiana na sheria za mirathi, ndoa, jinsia, stadi za maisha, ushauri nasaha, uchumi nk., wakichagua jambo la kujifunza, kivulini inashughulika kumtafuta mtaalamu. Mfano, wanajamii wanaleta maombi juu ya mdahalo wanaoutaka na njia wanayoitaka kuitumia, kama ni kwa njia ya filamu, ziara za kimafunzo, uchoraji, muziki, msaada wa kisheria hasa pale wanawake wanapodhalilishwa. Ikilazimu, wanasheria wao wanakwenda kutoa msaada wa kisheria mahakamani au kutoa ushauri.

Kinachovutia Kivulini na kuleta matumaini ni kwamba wakati mashirika mengi yanakuwa na malengo ya kuhudumia maeneo makubwa, jambo linalozorotesha mafanikio, Kivulini inahudumia maeneo machache. Pia inakuwa rahisi kuunda vikundi vya majadiliano na ushirikishwaji. Kwa njia hii wameweza kupambana na changamoto kubwa ya mtazamo wa dini katika suala zima la kuleta uwiano kati ya wanaume na wanawake, mitizamo ya kimila na desturi, jinsi ya mazoea ya mwanamke na mwanamme ambapo katika baadhi ya maeneo mwanamke anaonekana ni sawa kunyanyaswa na changamoto ya wanandoa kutokuwa wazi juu ya kipato chao na wanakitumiaje. Changamoto hizi wamekutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi kwa vile wanahudumia maeneo machache, wanashirikisha walengwa, wanatengeneza jukwaa la majadiliano, wanasikiliza zaidi kuliko kusikilizwa.

Wanaume wa Mwanza waliichukia Kivulini na Mama Kanyamala, pale shirika hili lilipomsaidia mwanamke kumshitaki mme wake aliyemkata masikio. Mahakama, ilimhukumu mwanaume kwenda jela kwa kitendo hicho.

Lakini kwa ujumla sasa hivi watu wengi wamezielewa juhudi za Kivulini, baada kuona malengo yake ya kutetea haki za wanawake na watoto zinaleta matunda mema. Pia, Kivulini ilionyesha pia kuwatetea wanaume wanaonyanyaswa na wake zao. Imeeleweka kuwa hiki ni kituo cha kutetea haki za binadamu bila ubaguzi wowote ule.

Ingawa jitihada za kuitengeneza Kivulini, ni za wachangiaji wengi, lakini Mama Maimuna Kanyamala, ametoa mchango mkubwa zaidi. Ndio maana safu hii ya Mwana Mama, imeamua kumleta kwenu mama huyu jasiri na mzalendo wa taifa letu.

Na,

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 6331 22

www.karugendo.net

MWANA MAMA.
LUCY SELINA LAMECK SOMI.

Ingawa jina hili la Mwana Mama Lucy Lameck halisikiki sana siku hizi, lakini mama huyu ni kati ya wanawake wachache walioingizwa serikalini baada ya uhuru. Mchango wake ni mkubwa kama ulivyokuwa kwa wanaume wengine waliolitumikia taifa letu kwa uaminifu uliotukuka! Alianzia kwenye chama, akiwa Mwanamke wa TANU, kama walivyokuwa akina Bibi Titi na wenzake. Lakini huyu kwa vile alikuwa amesoma, hakusukumwa jikoni na kulea watoto kama walivyotendendewa wanawake wengine wa TANU bali aliendelea kupambana serikalini na kutoa mchango wake kwenye baraza la mawaziri na kwingineko.

Ingawa kasi ya kuwapatia wanawake nafasi za juu serikalini haikuwa kubwa, lakini wale wachache waliozipata nafasi hizo walionyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuonyesha kwamba msemo ule wa “Wanawake wanaweza” ni kichekesho kama si tusi kwa wanawake. Tungekuwa makini wa kutunza kumbukumbu, tusingekubali kuimba wimbo huu ambao sasa unaanza kuwa kama fasheni na silaha ya wanaume kukwamishana na kuwekeana vizingiti kama ilivyotokea kwa spika wa Bunge. Wanawake, walipigania uhuru wa taifa letu, watashindwa vipi kushiriki uongozi? Kama wanawake waliweza huko nyuma, watashindwa kuweza leo hadi tukumbushane kwamba wanaweza? Ni uamuzi tu wa kukubali kuwatoa jikoni na kulea watoto kwa kutengeneza mifumo ya kuwawezesha kutembea na wakati, kuliko kuendelea kuimba wimbo ule ule kila kukicha.

Lucy Selina Lameck Somi, alizaliwa Kilimanjrao katikati ya miaka ya 1930. Baba yake alikuwa mkulima na wakati mwingine alifanya kazi ya usafirishaji. Mama yake, petronilla Lameck Somi, alijihusisha sana na siasa, wakati Lucy na dada zake watatu walipokuwa wadogo. Katika kitabu cha Wanawake wa TANU, Lucy anasema:

“Kila mara Nyerere alipokuja Moshi, alimtembelea mama yangu nyumbani, akanifahamu mimi na kutammbua kazi niliyokuwa nikifanya.Tulikuwa tunakula pamoja kila jioni, kwa hiyo akawa rafiki wa familia. Nyerere alimfahamu mama yangu kwa vile mama alikuwa anajihusisha sana na siasa kwa miaka mingi.TANU ilipoanzishwa, sote tulifanya kazi ya kuandikisha wanachama” (Wanawake wa TANU uk 78)

Lucy, kwa ujana wake na kiwango chake cha elimu, alikuwa wa kipekee, miongoni mwa wanawake wanaharakati wa TANU. Alitambuliwa kitaifa kama sauti yenye shauku kubwa ya kupigania hali za maisha ya wanawake baada ya uhuru.

Lucy alisoma shule ya msingi kijijini kwake, Moshi Njoro. Alisoma shule ya kati huko Kilema na sekondari huko Tanga, ambako alisomea vilevile miaka mitatu ya unesi na ukunga. Baada ya kumaliza masomo ya unesi, Lucy alichagua kurudi Moshi mwaka 1955. Huko Moshi alihudhuria masomo ya jioni ya kupiga chapa na hatimkato, akaanza kufanya kazi KNCU.

Alijiunga na chama cha TANU kama mwanachama wa kawaida na kufanya kazi ya kuandikisha wanachama hadi mwaka 1957. Alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya Wilaya ya Moshi ya TANU hadi 1957, alipoondoka kwenda masomoni Chuo cha Ruskin ,Oxford. Huko alisoma diploma ya Utawala,Sayansi ya Jamii, Saikolojia na Uchumi.

Alipoongea na mwandishi wa Kitabu cha Wanawake wa TANU, alisema:

“Ni vigumu kuelezea ni kwa nini nilijiunga na Tanu nikiwa mdogo hivyo. Nakumbuka vizuri kwamba sikupenda kabisa kufanya kazi chini ya mfumo wa ukoloni kwa sababu kulikuwa na ubaguzi wa wazi wa rangi. Kwa mfano manesi wa Kiafrika walitendewa vitu tofatui na Wazungu.Chakula kilikuwa tofauti, nyumba, saa za kazi, saa za kula, mtizamo wao mzima kuhusu sisi ulikuwa tofauti… ni mkusanyiko wa vitu vingi. TANU ilipokuja, ilikuta watu waliokuwa tayari kukiunga mkono. Halafu, unafika mahali unajikuta kuwa ni wa daraja la chini katika nchi yako…Kulikuwa na shule za Kizungu kwa watoto wachache wa Kizungu, shule za Wahindi kwa Wahindi walioshika uchumi wa nchi, halafu tulikuwa na shule masikini,silizokwisha, hizo zilikuwa za Waafrika…” (Wanawake wa TANU uk 80-81)

Mwaka 1960 Lucy Lameck, alikwenda Amerika chuo Kikuu cha Michigan, na huko alisoma mahusiano ya kimataifa. Aliporudi alifanya kazi ndani ya chama na baadaye alichaguliwa na rais kuingia Bungeni.

Mwaka 1962,Mwalimu Nyerere, alitambua mchango wa wanawake katika chama, na alifahamu fika kwamba kushiriki kwao kikamilifu kunahitajika katika kuendeleza nchi. Enzi hizo wimbo uliozoeleka siku hizi wa “Wanawake wanaweza” ulikuwa haujavumbuliwa! Hakuna aliyekuwa na mashaka juu ya uwezo wa wanawake; hivyo Mwalimu, alimteua Lucy Lameck, kuwa waziri mdogo wa Ustawi wa Jamii na Ushirika. Na mwaka 1966, alihamishiwa Wizara ya Afya na Nyumba hadi 1972. Hivyo alifanya kazi ya unaibu waziri kwa muda wa miaka 10, alipoondoka na kuweka nguvu zake katika shughuli za wanawake na jimbo lake la uchaguzi. Aliendelea kuchapa kazi na kuisaidia jamii iliyomzunguka hadi 1980, aliaga dunia Machi 21,1992.

Njozi ya Lucy Lameck kwa wanawake ilikuwa kuanzishwa kwa asasi za mafunzo mbalimbali katika kila wilaya, zitakazotoa elimu ya kilimo na ustawi wa mama na mtoto, pamoja na teknolojia inayofaa kwa kupunguza ugumu wa kazi za wanawake. Njozi hii ingetekelezwa, ingefuta kabisa ule wimbo wa “Wanawake wanaweza”. Jitihada pekee ya mkomboa mtoto wa kike ni kuhakikisha anakwenda shule; wasichana wana uwezo sawa na wavulana na hakuna ulazima wa kuwaisha watoto wetu kasumba ya “Mtoto wa kike anaweza”. Uwezo wa mtoto wa kike upo na wala hakuna haja ya kuutungia wimbo na kuwafanya watoto wa kike wawe wanyonge na kufikiri kwamba ni lazima kila wakati waonewe huruma.

Lucy Lameck alipiga vita mila na desturi zinazozuia wanawake kutofikia usawa na wanaume. Aliamini kwamba ni lazima ziwepo harakati za kupigania haki sawa kwa wanawake katika ngazi zote za kijamii ,kuanzia ngazi ya chini ya umma, kwenye chama na bungeni. Na kwamba tafiti kuhusu matatizo ya wanawake zinazofanywa na Chuo Kikuu ca Dar-es-salaam na asasi nyingine ziongeze kasi, maana wanaume watashawishika juu ya umuhimu wa mabadiliko kwa kutumia taarifa za kisayansi pekee. Hili ni muhimu zaidi ya ule wimbo. Taarifa za kisayansi zitaonyesha jinsi mtoto wa kike anaweza kuelewa mambo sambamba na mtoto wa kiume.

Kuwataja watu waliojitolea kulijenga taifa letu kwa uzalendo na uaminifu mkubwa, bila jina la Lucy Lameck, ni kuisaliti historia ya taifa letu. Tumekuwa na utamaduni wa mfumo dume wakati wa kuandika na kusimulia kumbukubu za kulijenga taifa letu. Mara nyingi yanatajwa majina ya wanaume peke yao, kwakati nchi yetu imejengwa na akina mama wengi waliojitoa muhanga kulitumia taifa letu kama Lucy Lameck.

Kwa maneno yake mwenyewe Lucy Lameck, anasema : “… Na hatukuanza kwa kuvaa nguo ghali na dhahabu, tulikuwa wanyenyekevu, wanawake wa kawaida tu, wawakilishi wa watu maskini wa vijijini na nchi hii.. Ukiniuliza kama kulikuwa na mwanamke aliyefikiria suala la mshahara bora, nina wasiwasi sana. Ni kweli, wanawake walikuwa na matatizo, na wanawake wa TANU walikuwa na matatizo… lakini tulijifunga kibwewbe kuitumikia nchi yetu” (Wanawake wa TANU uk 114).

Hivyo Lucy Lameck, kama walivyo wanawake wengine walishiriki kiasi kizima kulijenga taifa letu. Ni muhimu kuwakumbuka na kuwaenzi kama inavyofanyika kwa wanaume.

Na,

Padri Privatus Karugendo.


MWANA MAMA

Dkt HELEN KIJO BISIMBA

Helen Kijo Bisimba, ni jina linalosikika Tanzania na nje ya Tanzania.Huyu ni mama shupavu, jasiri, mpambanaji na mwanaharakati wa kutetea haki za Binadamu ambaye ameamua kujitoa kutoa mchango wake katika kuendeleza na kulinda ustawi wa taifa la Tanzania.

Tumezoea kusema kwamba Nabii hasifiki nyumbani! Inawezekana ni hivyo kwa mama huyu, ambaye kazi anazozifanya zinaheshimika na kusifiwa kwenye ulingo wa kimataifa kuliko hapa nyumbani? Inawezekana ni kwa vile kazi anayoifanya Mama huyu inaigusa serikali jichoni au kwa vile amejifunga kibwebwe kupambana na mfumo dume na kutaka kuutokomeza?Au labda ni kwa vile bado viongozi wengi kwenye ngazi ya maamuzi katika taifa letu ni wanaume?

Juzi, sote tumeshuhudia kwenye vyombo vya habari Mama Helen Kijo Bisimba akisoma taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za binadamu kuamua kuiburuza serikali ya Tanzania kwenye Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) iliyoko The Hague, Uholanzi. Hiki ni kitendo cha ujasiri na kujitoa, maana ni wachache wanaoweza kudhubutu kufanya hivyo bila kuogopa matokeo yake.

Hata hivyo kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kinachoongozwa na Mama Helen Bisimba, kimekuwa mstari wa mbele kutetea haki za watoto, wanawake na watu wote wanaokandamizwa; kunyanganywa ardhi yao na matuko mengine ya kifisadi yanayoendelea katika taifa letu. Kituo hiki kimekuwa sauti ya wanyonge.

Mama huyu amejitofautisha na baadhi ya watu wanaoziongoza NGO mbali mbali katika taifa letu la Tanzania; hata kama NGO hizo zinakuwa ni za kutetea haki za binadamu, viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi kwa malengo ya kupata mshahara tu! Au kwa lengo la kujenga majina yao na kujitafutia sifa. Ni tofauti kabisa na Mama Helen Kijo Bisimba, ambaye Kituo cha Sheria na Haki za binamu kimekuwa sehemu ya maisha yake. Helen Kijo Bisimba ni Kitucho cha Sheria na Haki za Bianadamu; na Kituo cha sheria na Haki za Binadamu ni Helen Kijo Bisimba: Bila unafiki na kujipendekeza anaonekana wazi kuguswa na kila aina yoyote ile ya ukiukwaji haki za binadamu katika Taifa letu. Amekuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi, rushwa na uporwaji wa rasilimali katika taifa letu. Ameshiriki kuipigania demokrasia na utawala bora na kilio cha katiba mpya katika taifa letu. Haogopi kusimama na kusema wazi msimamo wake na msimamo wa Kitucho cha sheria na Haki za Binadamu. Yuko tayari kusema hata yale yasiyopendeza kwenye masikio ya watawala.

Mama huyu aliyezaliwa mnamo mwaka wa 1954 mkoa wa Kilimanjaro, ndiye Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambacho kinalinda na kutetea haki za binadamu za kila mtanzania na kuhakikisha kwamba kila raia anakingwa na aina zote za udhalilishaji.

Mapenzi ya kutetea haki za binadamu na moyo wa unaharakati yalionekana kwake kwenye miaka 70 alipokuwa akisoma sekodari ya Korogwe kule Tanga. Alifukuzwa shule kwa muda, baada ya kukataa shinikizo la walimu wake kuomba msamaha kwa barua ya kudhalilisha aliyoandikiwa Mwalimu mkuu wa shule. Alikataa kuomba msamaha wa kosa ambalo yeye hakutenda. Kwa vile alikuwa msaidizi wa kiranja wa shule alikubali kufukuzwa kuliko kuomba msamaha, baba yake mzazi alikwenda kumwombea msamaha, lakini walimu walikataa. Mpaka yeye alipoamua baadaye kuzungumza na walimu na hatimaye kuomba msamaha kwa kosa ambalo hakulitenda mwenyewe. Tukio hili lilimjengea moyo wa ujasiri ambao hadi leo hii zaidi ya miaka 40, amekuwa akitetea haki za wanyonge, wanaume,kwa wanawake, vijana kwa wazee.

Mama huyu, alikuwa kati ya watu wa kwanza kumshughulikia Dk Ulimboka, alipotekwa, pigwa na kuteswa. Kila mtu alishangaa jinsi mama huyu alivyopata habari haraka juu ya tukio hilo la kinyama na kufanya haraka kushiriki kutoa msaada kwa Dk Ulimboka. Alimsaidia kumfikisha Hospitali na kuendelea kuishinikiza serikali ifanye uchunguzi wa kina kubaini watu waliofanya unyama huo.

Wakati wa mgomo wa Madaktari, sauti ya Helen Kijo Bisimba ilisikika kote kwenye vyombo vya habari. Yeye na wanaharakati wengine waliishinikiza serikali kufanya haraka kumaliza mgomo huo ili kunusuru uhai wa raia wasiokuwa na hatia. Na kati hali isiyokuwa ya kawaida Mama huyu na wanaharakati walikamatwa na polisi na kuhojiwa wakati walipofika Muhimbili, kutaka kujua kinachoendelea.

Mwaka 2001, alikuwa Mwanamke mwanaharakati wa kwanza kupinga na kulaani mauji yaliyotokea Zanzibar. Kitendo hicho kilimletea sifa ndani na nje ya Tanzania. Mwaka 2008 alikuwa Mwanamke wa kwanza kupokea tuzo ya Mwanamke jasiri inayotolewa na Balozi wa Amerika nchi Tanzania

Mama huyu amekuwa mstari wa mbele kupinga Hukumu ya kifo. Siku ya kupinga hukumu ya kifo inaangukia siku yake ya kuzaliwa ambayo ni tarehe 10 Oktoba, hivyo mwaka huu anapoazimisha miaka 58 ya kuzaliwa, ana imani kubwa kwamba iko siku adhabu hii ya kifo itakuja kufutwa nchini Tanzania.

Mama huyu ni kati ya watu wanaotamani kuona Tanzania inawaruhusu wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni kuendelea na masomo. Na elimu ya kujitambua inafundishwa shuleni, maana kwa maoni yake wakati mwingine wasichana wanapachikwa mimba kwa kuwa na ulewa mdogo juu ya kujamiana; na kwamba wazazi wasione aibu kuongea na watoto wao juu ya suala la kujitambua na mahusiano, maana ukimya katika sula hili ni hatari zaidi kuliko faida.

Mama huyu yuko mstari wa mbele kupinga vifo vya wanawake wakati wa kujifungua na vifo vya watoto wadogo.Ameunga mkono na kushiriki kampeni zote zinazoendelea za kupambana kupunguza vifo vya mama wajawazito. Pia kwa kupitia Kituo cha Sheria na Haki za binadamu anaongoza kampeini ya kutokomeza ukeketaji, kuwarithi wajane na aina nyingine ya unanyasaji kwa wanawake.

Mama huyu alianza kukiongoza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu mwaka 1996, na ni mmoja wa waanzilishi wa kituo hiki cha kutetea na kulinda haki za binadamu. Ni mjane tangia mwaka 1994. Ana watoto wanne, wawili ni mainjinia, mmoja ni daktari na mwingine ni mhasibu. Lakini pia anatunza watoto yatima nyumbani kwake na ni mwanachama wa wanawake wajane katika Kanisa anapoabudu.

Mbali na kuwatunza watoto yatima nyumbani kwake, yeye amekuwa sauti ya watoto wanaojilea na kujitunza. Wakati kuna watafiti wanaopinga Tanzania kuwa na familia za watoto wanaojilea wenyewe na kujitunza, Mama Helen Kijo Bisimba, anaamini kwamba Makete na Karagwe, alikofanyia utafiti wa tasinifu yake ya shahada ya uzamifu, kuna familia za watoto wanaojilea na kujitunza kutokana na janga la ugonjwa wa Ukimwi.

Mwaka 2008 mpaka 2001, alichukua likizo ya masomo na kwenda Uingereza kuchukua shahada ya uzamifu kwenye Sheria na Haki za binadamu. Tasinifu yake ulikuwa ni utafiti juu ya haki za watoto. Alitaka sauti ya watoto wa Afrika isikike, alitaka kujua jinsi watoto wanavyouelewa mfumo wa serikali. Anaamini kwamba kwa kuelewa mawazo ya watoto, serikali yoyote inaweza kutenda vizuri siku zinazokuja , maana watoto wa leo ndiyo viongozi wa kesho.

Kabla ya kujiunga na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mama huyu alikuwa mwalimu wa kiingereza na Kiswahili katika Taasisi ya Elimu ya Watu wazima alikofanya kazi kwa kipindi cha miaka 10. Marehemu mme wake ndiye aliyemshauri kusomea sheria. Wakati anajiunga na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, alikuwa bado anafundisha Taasi na kujitolea kwenye shirika la WILDAF (Women in Law and Development in Africa) ambalo aliliwakirisha kwenye mkutano wa wanawake wa Beijing mwaka 1995.

Mama huyu ni kiongozi wa mfano. Hata wafanyakazi wenzake wanampenda na kumheshimu. Wengi amewaambukiza roho ya kutetea haki za binadamu na ujasiri wa kusimama kidete mbele ya haki. Ukifika kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, unakutana na Mkrugenzi ambaye licha ya kuwa kiongozi wa kituo hicho ni mama mwenye sifa zote za umama; kulea, kuelekeza, kujali,kutokuwa na uroho wa elimu,kuwashughulikia wengine, kuguswa na matatizo ya wengine na kuambukiza roho ya ujasiri kwa awafanyakazi wenzake.

Mama huyu pamoja kazi kubwa alizonazo za kuiongoza kituocha Sheria na haki za binadamu, bado ana nafasi ya kuhihudumia familia yake, kuangalia mpira na watoto na wajukuu zake na pia kupata nafasi ya kuimba kwenye kwaya ya kanisa.

Huyo ndiye Helen Kijo Bisimba, mwanamke shujaa, jasiri, msomi, mzalendo, mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu.Na,

Padri Privatus Karugendo.

MWANA MAMA.
BIBI TITI MOHAMED

Tunapotaja waasisi wa Taifa letu, majina yanayosikika ni ya wanaume. Lakini ukweli ni kwamba hata wanawake walitoa mchango mkubwa wakati wa kupigania uhuru wa taifa letu. Kati ya wanawake wanaotajwa ni BibiTiti Mohamed. Ingawa kuna jitihada za makusudi kuhakikisha jina hili linafutika na kusahaulika, bado mzimu wa mama huyu unajitokeza na kuendelea kutuchokoza ili tuendelee kuchimba, kutafiti hadi ukweli uwekwe wazi na mama huyu apate heshima na nafasi kubwa miongoni mwa waasisi wa taifa letu.

Bibi Titi Mohamed ni mmoja wa viongozi wazalendo waliokuwa na nguvu, uwezo mkubwa na umuhimu wa pekee nchini Tanzania. Wale walio waaminifu wa historia ya taifa letu, wanasema baada ya Mwalmu Nyerere, alifuata Bibi Titi, kwa mvuto, uwezo wa kuongoza, upeo na uzalendo. Alizaliwa Dar-es-salaam mwaka 1926, baba yake alijulikana kama Mohamed bin Salim, alikuwa mfanyabiashara na mama yake Hadija Binti Salim, alikuwa mkulima na mama wa nyumbani. Hawa wazazi wa Bibi Titi, walitokea Rufiji, mama yake alijulikana kama Mmatumbi mwenye nguvu za kuogofya.

Bibi Titi alisoma shule ya msingi kwa miaka minne tu. Hilo halikuwa jambo la kawaida hata kidogo kwa msichana wa Kiislamu katika miaka ya 1930. Wakati ambapo wasichana wa kizazi chake walishiriki katika vikundi vya ngoma, ni wachache mno walioweza kuwa waimbaji na kuigiza pamoja na haiba kubwa. Hivyo, pamoja na kwamba alikuwa ni mwanamke wa kawaida wa mjini, Bibi Titi alikuwa na silika iliyomwezesha kushirikiana na kukaa na wenzake, na hivyo kuweza kuwahamasisha na kuibuka kuwa kiongoizi.Alipokuwa Dar-es-salaam, ambapo ni kwao,Bibi Titi aliweza kutambua uwezo wake, na baada ya kufanya hivyo, kuondoa wasiwasi na kujiimarisha kwenye jukwaa la siasa za mjini. Kufikia mwishoni mwa mwaka 1955, Bibi Titi Mohamed alikuwa kiongozi muhimu wa TANU. Alikuwa ameonesha wazi uwezo wake wa kuhamasisha makundi makubwa ya Waafrika walioishi Dar-es-salaam ili kuunga mkono harakati za kizalendo.

Bibi Titi alipohutubia mkutano wa kwanza wa Kitengo cha Wanawake cha TANU, Julai 8,1955, wanawake 400 walijiunga na chama. Kufikia Oktoba mwaka huo walishafika wanachama 5,000 walioingizwa kwenye chama na Bibi Titi.

Aliwahamasisha wanawake kujiunga na chama: “Nawaambieni kwamba tunataka uhuru, na hatuwezi kupata uhuru kama hamtaki kujiunga na chama. Tumewazaa wanaume wote hawa. Wanawake ndio nguvu ya duni hii. Sisi ndio tunaozaa dunia. Nawambia kwamba inatubidi kujinga na chama kwanza..” (Bibi Titi – Wanawake wa Tanu uk 37)

“Niliweza kusafiri kwa miezi mitatu mfululizo, Ningeweza kuwa Mwanza, halafu nikaenda Musoma ambapo ningepata telegram iliyonitaka niende Dodoma. Nikiwa Dodoma Napata telegram nyingine kwenbda Mbeya…”

“Mimi sikujinga na TANU nikitarajia chochote… Rafiki zangu walikuwa wananiuliza, unataka kuwa malkia wa nchi? Sikutaka kuwa malkia. Nilitaka kuwa huru. Sikutarajia chochote zaidi. Nilitaka kujenga nchi yangu, kufanya maisha yetu yawe bora, nilitaka elimu kwa watoto wetu, na nilitaka kupata ardhi… Wazungu walikuwa na mashamba makubwa na sisi tulikuwa vibarua tu. Vibarua katika nchi yetu? Kwa nini? Hilo mimi sikulipenda… nilitaka maendeleo kwa watu..” (BibiTiti –Wanawake wa TANU uk 41).

Hivyo Bibi Titi, alitembea nchi nzima ya Tanzania, akiwahamasisha wanawake na wanaume kujiunga na TANU. Alifanya kazi bega kwa bega na Mwalimu Nyerere na wapambanaji wengine wa wakati ule wa kupigania Uhuru wa wa Tanganyika. Alifanya kazi kubwa kuzidi hata wanaume wengine waliokuwa wakipigana kwa kujificha ili wasipoteze kazi zao serikalini.

Ndoa yake ilivunjika kwasababu ya kujihusisha na siasa “Boi mwenyewe aliniruhusu kuingia TANU, tena ndiye eliyenunua kadi yangu ya uanachama. Sio hivyo tu, TANU ilimwandikia barua kumwomba nisaidie katika shughuli za TANU. Lakini mwishowe hizi safari zilimshinda. Nilikuwa nakaa nje ya nyumbani kwa miezi mitatu, na nikirudi naweza nisikae hata siku kumi kabla sijasafiri tena. Boi akaniambia kwamba anataka kuoa mke mwingine. Nikamwambia sawa, niache na kazi yangu kwasababu nimeshaizoea…Kwa hiyo Boi akamuoa Khadija, lakini walishindwana, wakaachana. Akaniambia kama nampeda niache hiyo kazi. Nikamwambia siwezi, kama unataka kuoa tena, endelea. Akakataa ,akasema nawezi kuoa tena. Nilifunga mizigo yangu nikaondoka..” (Bibi Titi- Wanawake TANU uk 45).

Katika maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Waingereza, usiku wa Desemba 9,1961, Bibi Titi Mohamed na Julius Nyerere walikaa kwenye jukwaa moja, wakiwa pamoja na waheshimiwa wengine. Kufuatana na wachambuzi wa historia ya Tanzania, ni kwamba wakati wa kupata uhuru yawezekana kuwa Nyerere na Bibi Titi walikuwa ndio viongozi pekee waliojulikana nchi nzima wakati Tanganyika inapata uhuru.

Uhuru wa kisiasa ndo ulikuwa lengo kuu kwa Bibi Titi na wanawake wanaharakati wa miaka ya 1950. Hata hivyo, uzalendo na nguvu waliyowekeza katika TANU haikuishia katika kuwapa nguvu ya dola. Waliwekwa pembeni na kushauriwa waingie jikoni, kutunza nyumba na kuwalea watoto.

Hata hivyo Bibi Titi, aliponzwa zaidi na uwazi wake na msimamo wake wa mawazo. Alijisimamia na hakuwa na unafiki. Azimio la Arusha, lilijenga ukuta mkubwa kati yake na Nyerere na viongozi wengine wa TANU. Yeye alikuwa wazi kuelezea wasi wasi wake juu ya Azimio la Arusha. Wengine, na hasa wanaume walilikubali Azimo la Arusha kwa unafiki na matokeo yake wanaume hao hao walizika kule Zanzibar.

Kama kuna kosa kubwa alilolifanya Mwalimu Nyerere, ni kushindwa kugundua unafiki wa viongozi wanaume waliokuwa wamemzunguka na kushindwa kutambua na kukubali uwazi na uaminifu wa watu kama Bibi Titi waliokuwa na mawazo tofauti, lakini ya kizalendo na ya kujenga.

Tunaweza kusema kwamba Bibi Titi, ni kati ya watu waliopigania uhuru lakini hawakufaidi matunda ya uhuru. Wakati wenzake wakifurahia uhuru na kujilimbikiza mali kwa unafiki huku wakijificha nyuma ya siasa ya Ujamaa, yeye alikuwa gerezani. Alipotoka gerezani hakuweza kufurahi maisha, maana jamii ilikuwa inamnyanyapaa. Dosari ya kuingizwa kwenye uhaini ilimchafua kiasi cha kujikuta anaishi bila kuwa na marafiki. Hata na wale walioshirikiana naye kupigani uhuru, walimwogopa.

Ni vigumu pia kuthibitisha kama maisha ya ukimya aliyoishi Bibi Titi nje ya siasa kwa miaka mingi baada ya kuachiwa, aliyachagua ama alishurutishwa kufanya hivyo. Katika mahojiano na Ruth Meena baada ya kutoka kifungoni, Bibi Titi alieleza kuwa hakuwa huru sana kushiriki na wenzake kwa sababu walikuwa waangalifu mno wakiwa naye. Alitania akisema, “Mtu angeweza kufikiria kwamba nilikuwa na ugonjwa wa kuambukiza”

Bibi Titi alionesha kutoridhika kwake na sera ya chama wakati alipopinga kutofuatwa kwa demokrasia katika mchakato ulioambatana na kutangazwa kwa Azimio la Arusha Februari 1967. Pia, hakukubaliana na kipengele (a) sehemu ya 5 ya Azimio kilichohusu maadili ya uongozi. Hususan, hakukubaliana na kipengele kilichosema kwamba kiongozi wa TANU au serikali hawezi kumiliki au kupangisha nyumba. Hakukataa kwa siri, na hivyo alijiuzulu kutoka Kamati Kuu ya Chama kwa mujibu wa maadili ya uongozi, kuliko aachie haki yake ya kujipatia kipato. Jambo hili lilielezwa katika vyombo vya habari, vikitoa picha iliyomwonesha Bibi Titi kuwa alithamini zaidi faida ya biashara na idadi ya nyumba zake kuliko kazi ya siasa chini ya TANU. Lakini Bibi Titi mwenyewe, alijitetea kwamba alinunua nyumba moja kwa kuuza vito vyake vya dhahabu na nyumba ya pili alinunua kwa mkopo. Yeye alikuwa ameamua kujipatia hifadhi,kwake na kwa binti yake kwa njia hii, wakati washiriki wenzake waliamua kuoa wake wengi na kunywa pombe.

Msimamo huu wa wazi ulimwingiza matatani hadi akaingizwa kwenye mkumbo wa uhaini. Aliwekwa ndani miaka miwili na nyumba zake zilitaifishwa. Alipoachiwa kutoka ndani aliishi maisha ya taabu sana na kufanya biashara ya kuuza mafuta ya taa. Baadaye nyumba zake zilirejeshwa na mwaka 1985, Mwalimu Nyerere, alionyesha dalili za kumsamehe.

Hata hivyo, jina lake na mchango wake mkubwa wa kupigania uhuru vilipotea na kufunikwa! Ni wajibu wa watanzania kufufua majina kama haya, ili vizazi vijavyo vipate historia isiyopinda ya taifa letu.

Na,

Padri Privatus Karugendo.