Wizard of the Crow

UHAKIKI WA KITABU: WIZARD OF THE CROW

1. Rekodi za Kibibliografia.

Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni WIZARD OF THE CROW, Kimeandikwa na Ngugi wa Thiong’o. Mchapishaji wa kitabu hiki ni East African Educational Publishers na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978- 9966- 25 –491-9. Kitabu kina kurasa 768 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi

Wizard of the Crow, au Mchawi wa Kunguru kwa lugha yetu ya Kiswahili na Murogi wa Kagogo kwa lugha ya Kikuyu ni hadithi ndefu kuliko zote zilizoangikwa na Ngugi wa Thiong’o. Hadithi hii iliandikwa kwanza kwa lugha ya Kikuyu na kutafsiri wa na mwandishi mwenyewe kwenye lugha ya Kiingereza. Ni hadithi ambayo kule Kenya watu wanasomeana na kusimuliana kwenye vilabu vya pombe, kwenye starehe mbali mbali na vijiweni. Ni wazi kwenye lugha ya Kikuyu, itakuwa inaburudisha sana kuliko kwenye Kiingereza.

Hadithi hii inamhusu kiongozi wa nchi huru ya kubuni ya bara la Afrika yenye jina la Aburiria. Kiongozi huyu ana magonjwa matano yanayomsumbua na moja wapo ya magonjwa haya ni hasira ambayo watu wanaamini ilisababishwa na mke wake. Mama huyu pamoja na kuwekwa kizuizini na kuteswa, alikataa kutoa machozi. Kiongozi huyu alitamani sana kuyaona machozi ya mke wake, ili ajione kama mshindi. Lakini mama huyu alikataa kulia. Ingawa jina halitajwi, lakini aina ya utawala anaouchora mwandishi unazigusa nchi zote za Afrika na kwa karibu zaidi nchi yake ya Kenya. Uchu wa madaraka, kutesa wapinzani, majungu, kujipendekeza, utajiri wa kupindukia, ukatili na unyanyasaji wa wanawake, kupora mali ya nchi na kupendelea mambo ya nchi za nje kiasi cha mtu kutamani kujibadilisha kuwa kama mzungu, ni magonjwa yaliyojaa katika nchi zote za Afrika.

Hadithi yenyewe ina vitabu sita, maana yake ni vitabu sita ndani ya kitabu kimoja. Bei ya kitabu hiki ni shilingi 45,000! Hivyo kwa kuogopa gharama ya kitabu na watu kuogopa kukinunua, mchapishaji, amejaribu kuvichapa vitabu hivi sita tofauti. Lakini mimi nimesoma kitabu kimoja chenye vitabu vyote sita. Ni vitabu sita vyenye mwendelezo wa hadithi moja.

Vitabu hivi sita ni : Mashetani wa madaraka, ambacho ni ukurasa wa kwanza hadi wa 45, Mashetani wa foleni, ukurasa wa 45 hadi 271, Mashetani wa kike, ukurasa wa 271 hadi 467 Mashetani wa Kiume, ukurasa wa 467 hadi 637 Mashetani waasi ukurasa 637 hadi 727 na Mashetani wenye ndefu ukurasa 727 hadi 768.

Kabla ya kufanya uhakiki wa kitabu hiki ningependa kuelezea mazingira yanayokizunguka.




III. Mazingira yanayokizunguka kitabu

Ukisoma vitabu vya Ngugi vya zamani kama vile Weep Not, Child alichokiandika mwaka 1964, na The River Between alichokiandika mwaka 1965 na vingine vya siku za karibuni kama vile Matigari cha 1987, unakuwa na hisia juu ya majina ya wahusika, kwamba majina hayo ya Kikuyu yanabeba ujumbe mzito ambao msomaji anaenelea kuutambua jinsi anavyosoma hadithi. Hivyo msomaji ambaye si Mkikuyu, hapati uhondo mzima, kwa kutofahamu maana ya majina ya Kikuyu.

Nilipokutana na Ngugi, miaka kumi iliyopita, katika mahojiano naye aliikubali wazo hili la majina ya Kikuyu kubeba maana kubwa kwenye vitabu vyake. Aliniambia kwamba kila jina, kama yalivyo majina yote ya kiafrika, linakuwa na maana fulani inayohusiana na hadithi husika. Mwaka jana, nilikutana tena na Ngugi, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, alinielezea kwamba sasa kwenye kitabu chake cha Wizard of The Crow, amejitahidi kutumia na majina ya Kiswahili, ili hata wale ambao si wa Kikuyu, waweze kufurahia hadithi kwa kuunganisha matukio na majina ya wahusika. Bado ni tatizo kwa wale ambao si Waswahili na si wa Kikuyu, bado kuna haja ya kuyatafsiri majina haya ili ujumbe wa hadithi hii uwafikie watu wote bila ya kikwazo.

Baadhi ya majina ya mawaziri wa Kiongozi wa nchi Ya Aburiria, yako kwenye Kiswahili; mfano Waziri wa Mambo ya nchi za Nje ni Machokali. Huyu ndo macho ya kiongozi wa nchi ya Aburiria, anaangalia kila kitu ndani na nje ya nchi. Waziri huyu alipoona macho yake hayaoni vya kutosha, ili kumfurahisha Kiongozi wa nchi, alifunga safari na kwenda nchi za nje ili macho yake yafanyiwe upasuaji ili yawe makubwa zaidi. Picha ya kuchorwa Kwenye gamba la kitabu, Machokali, anaonekana na macho yasiyokuwa ya kawaida. Waziri wa nchi kwenye ofisi ya Kiongozi wa nchi ya Aburiria, amepewa jina la Sikiokuu, huyu ndo sikio la Kiongozi, kazi yake ni kusikia kila linalosemwa juu ya Kiongozi. Kwa vile masikio yake yalikuwa madogo, kwa kutaka kumfurahisha kiongozi, alifunga safari na kwenda nchi za nje kuyapanua masikio yake. Kwenye gamba la kitabu, anaonekana akiwa na masikio makubwa kichwa kidogo!

Mawaziri na viongozi wengi katika nchi ya Aburiria, walibadilisha viungo vyao vya mwili ili viweze kutoa huduma nzuri kwa Kiongozi wa nchi. Big Ben Mambo, alifanya upasuaji wa ulimi, ili urefuke zaidi, aweze kutoa amri za kijeshi nchi nzima. Na waziri mwingine alipanua pua zake, ili aweze kunusa hatari yoyote ile inayoweza kuwa imelengwa kwa Kiongozi. Na waziri mwingine alifanya upasuaji wa kuongeze ukubwa wa midogo yake, ili aweze kufikisha ujumbe wa kiongozi nchi nzima, kwenye picha iliyo kwenye gamba la kitabu, anaonekana waziri huyu na midomo yake mikubwa kupita kiasi.

Jina jingine linalotumika kwa Kiswahili ni Tajirika. Huyu anapata vyeo vikubwa, anachanganyikiwa na kutamani kuwa kama mzungu, hadi mwishowe anapata nafasi kubwa katika uongozi wa nchi ya Aburiria. Bahati mbaya kwa msomaji ambaye si Mkikuyu, majina ya wahusika wakuu Nyawira, Kamiti na Kaniuru, yanabaki kwenye Kikuyu. Mwandishi, angetoa tafsiri ya majina haya, msomaji angepata uhondo zaidi.

Wizard of the Crow, unaanza kama mzaa. Nyawira na Kamiti, wanamapinduzi wanaoupinga utawala wa Aburiria, walifukuzwa na vikosi vya usalama wakati wa vurugu za kupinga wazo la Kiongozi wa Aburiria, la kujenga mnara kama ule wa Babeli, mnara wa kwenda Mbinguni. Walipokimbizwa na kuingizwa kwenye makazi ya watu, waliamua kuingia kwenye nyumba na kuandika bango lenye Maneno “Wizard of the Crow”, maana yake ni nyumba ya hatari. Polisi aliyekuwa akiwafukuza kwa kuogopa nyumba ya mchawi wa Kunguru, aliogopa kuendelea kuwafukuza. Na Waafrika tunavyoamini uchawi, polisi huyo alirudi kwenye nyumba hiyo kesho yake ili apate huduma. Kiongozi wa nchi alipata habari kwamba polisi wake, aliwafukuza wenye fujo hadi wakatokomea kwenye nyumba mbali na mji; hivyo akaamua kumpandisha cheo kwa kazi yake nzuri aliyoifanya. Polisi yeye akafikiri na kuamini kwamba amepandishwa cheo kwa nguvu za “Wizard of the Crow”.

Polisi huyu, akaeneza habari kwamba kuna Mchawi, mwenye nguvu. Kwamba yeye amepanda cheo kwa nguvu za Mchawi wa Kunguru. Viongozi wote wakakimbilia kwa Mchawi wa Kunguru. Hadi Kiongozi wa Nchi alipokwenda Amerika, kuomba fedha za kujenga mnara wa Babeli, akaugulia kule, madaktari wakatibu na kushindwa, mpango ulifanyika kumsafirisha Mchawi wa Kunguru kwenda hadi Amerika, kumtibu Kiongozi wa nchi.

Kama mzaha vile, lakini inaaminika kwamba viongozi wengi wa Afrika, wanasafiri na wachawi wao. Watu hawa wanapata posho na kutunzwa vizuri. Mchawi, akiamua safari isifanyike, inafutwa bila ya maelezo! Hivyo si kwamba Ngugi, anazua mambo ya kuchekesha tu, bali ni ukweli unaoishi kwenye mazingira ya uongozi wa nchi za Afrika.

Wizard of the Crow, ni kama ilivyo kwa Babu wa Loliondo. Jambo linaanza kama mzaha, lakini linapanuka hadi foleni ya magari elfu moja. Ukisoma kitabu hiki unashangaa sana jinsi Waafrika tunavyofanana kwa mawazo, na jinsi tusivyopenda utafiti. Tunapenda miujiza, ambayo mara nyingi ni kupumbazwa. Ngugi, ametumia mfano wa uchawi na kunogesha hadithi yake, kama afanyavyo mwandishi Gabriel Garcia Marquez.

Ngugi wa Thiong’o, alizaliwa mwaka 1938 kule Kenya. Alisoma Chuo Kikuu cha Makerere Uganda na baadaye Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza. Kitabu chake cha Kwanza Weep Not, Child kiliandikwa mwaka wa 1964. Na mwaka 1965, akaandika kitabu chake cha pili cha The River Between. Na mwaka 1967, aliandika A Grain of Wheat. Mwaka 1982, aliandika Devil on The Cross. Ameandika michezo ya kuigiza kama ule ya “ Nitaoa nikipenda” na kitabu kingine cha Matigari. Sasa hivi anaishi na kufundisha kule California.
Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. Muhtasari wa Kitabu

Hii ni hadithi ya kubuni. Nchi yenyewe inaitwa Aburiria na iko Bara la Afrika. Kama nilivyosema mwanzo, ni wazi jina hili Aburiria, litakuwa na maana fulani katika lugha ya Kikuyu na kama kungekuwa na tafsiri yake, basi hadithi ingenoga kuanzia mwanzoni. Hii ni hadithi ambayo msomaji hapendi imalizike, ni ndefu lakini inachekesha, inasikitisha na kuburudisha; kiasi mtu anatamani iendelee bila mwisho.

Kiongozi wa nchi hii ya Aburiria, ni mwakilishi wa viongozi wengi wa Afrika. Badala ya kuangalia matatizo ya watu wake, anataka kujenga mnara wa kwenda mbinguni. Mnara kama ule wa Babeli. Mawaziri wake, kwa kujipendekeza, wanaunga mkono wazo hili na kupendekeza kwamba ili lifanikiwe nchi iombe mkopo kutoka Benki za chi za nje, ni mfano wa IMF na Benki ya dunia.

Mbali na wazo hili la kiwendawazimu, Kiongozi wa Aburiria, ana tabia ya kuwanyanyasa wanawake. Anatembea na watoto wadogo; mke wake wanapokuja juu na kumkanya, Kiongozi huyu anaamua kumfungia mke wake kizuizini milele yote. Hata hivyo mama huyu anakataa kuonyesha dalili zozote zile za unyonge, anagoma kulia, anagoma kuomba msamaha. Hali hii inamchanganya kiongozi kiasi cha kuugua na kuwa na kilema (hasira) cha maisha rohoni mwake.

Hivyo hadithi yote inazunguka juu ya utawala wa Kiongozi huyu, upinzani juu ya utawala wake, magomvi ya madaraka baina ya mawaziri wake, visa na visasi, sauti ya ukombozi inayoongozwa na Mama Nyawira, ambaye yeye na Kamiti, kwa pamoja wanatengeneza “Mchawi wa Kunguru”.

Hadithi hii imegawanyika katika vitabu sita. Kitabu cha kwanza ni Mashetani wa Madaraka, kitabu cha pili ni mashetani wa foleni, kitabu cha tatu ni mashetani wa Kike, kitabu cha nne ni mashetani wa kiume, kitabu cha tano ni mashetani waasi na kitabu cha sita ni mashetani wenyewe ndevu.

Kamiti, anayekuja kuwa Mchawi wa Kunguru kwa kushirikiana na Nyawira., amesoma India na kupata digrii mbili. Anaporudi Aburiria, hafanikiwi kupata kazi. Kila anapokwenda kutafuta kazi, anaambiwa kazi zimejaa. Anaamua kujitosa kwenye harakati za kupinga utawala wa kiongozi wa Aburiria, katika harakati hizi anakutana na Nyawira; wanashirikiana kuunda taasisi ya “Mchawi wa Kunguru”. Hawakuwa na lengo hilo ila baada ya kufukuzwa na polisi, katika harakati za kujiokoa, wakajikuta wanatengeneza Bango, na kuandika kwamba nyumba yao ni ya mchawi wa Kunguru. Hivyo mchawi wa Kunguru “Wizard of the Crow” ni Kamiti na Nyawira; wote kwa nyakati tofauti walifanya kazi hii ya Mchawi wa Kunguru. maana yake mabadiliko katika jamii yataletwa kwa ushirikiano wa Mwanamke na mwanaume.

Uchawi ( Wizaard of the Crow) wao ni wa kisomi: Wanajua daima watu wanasumbuliwa na matatizo ya kisaikolojia. Hivyo wanajitahidi kuwasoma wateja wao na kuwaelekeza pole pole ili wayatanzue matatizo yao wenyewe. Walijua kabisa kwamba viongozi wote wa Aburiria walikuwa na ugonjwa wa kutaka madaraka, walikuwa na ugonjwa wa kutaka fedha; hivyo waliweza kuwaelekeza huko, na viongozi hao walipona magonjwa yao ya mawazo. Kwa njia hii, jina la mchawi wa Kunguru likawa kubwa; na watu bila kujua siri kwamba mchawi huyu ni watu wawili, yaani mwanamke na mwanaume, wakafikiri ni mtu mmoja mwenye uwezo wa kujibadilisha; siku nyingine utamkuta ni mwanamke na siku nyingine ni mwanaume.

Wachawi hawa wasomi, wanapotaka kufanya tendo la ngono kwa mara kwanza; mambo yanakwama kwa vile hawakuwa na kondomu. Ngugi, amekuwa makini kutuonyesha uchawi wa kisomi. Kama wangekuwa wachawi wa kawaia, basi hata na tendo la ngono lingekwenda kichawi kwa kufanya ngono bila kinga. Maana yake ni kwamba, mwandishi anaandika juu ya uchawi, lakini hana imani na uchawi!

Tajirika, anateuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya kujenga Mnara wa Babeli. Anapoteuliwa, makampuni ya ujenzi yanaanza kujikomba kwake na kumletea bahasha. Tajirika, anajiona amekuwa tajiri na sasa ana kila kitu, labda kitu kimoja: SURA ya KIZUNGU. Anatamani awe mzungu. Mawazo haya yanamchanganya, hadi anaugua ugonjwa usiojulikana. Alibakia kusema neno moja tu ambalo ni “Kama”, kwa maana “ Kama ningekuwa mzungu”. Baadaye, Tajirika, kama ilivyo kawaida ya Waafrika, anatibiwa ( kwa ujanja) na Mchawi wa Kunguru.

Foleni ya watu wanaotaka kazi kwa Tajirika, inakuwa ndefu kupita kiasi. Na foleni nyingine za mahitaji mengine mengi zinaanza nchi nzima. Nchi inakumbwa na ugonjwa wa foleni. Mawaziri wengine wanachukia foleni hizi, lakini wengine wanataka ziendelee kama ishara ya watu kuunga mkono wazo la kiongozi wao la kujenga Mnara wa Babeli. Mwandishi, ametumia foleni, kuonyesha jinsi wananchi walivyo na matatizo mengi.

Baada ya hapo mambo mengi yanatukia; kuanzia wivu, majungu, visasi, hadi kumchonganisha Tajirika na mke wake. Matokeo yake Tajirika, anaanza tabia ya kumpiga mke wake. Sauti ya wanawake ( sauti ya umma) kikundi kilichokuwa kinaongozwa na Nyawira, na kuendesha mapambano chini kwa chini na wakati mwingine wazi wazi, kilimteka Tajirika na kumfikisha kwenye mahakama ya wanawake. Adhabu yake, ilikuwa akatwe uume wake. Aliachiwa kwa msamaha na kuonywa kwamba akijaribu tena kumpiga mke wake, atapata adhabu hiyo.

Mahakama ya wanawake ni sehemu inayochekesha sana kwenye kitabu hiki. Mahakama hii inamaliza kiburi cha wanaume. Maana, mwanaume anakamatwa na wanawake zaidi ya watano, wanamwangusha chini na kumkalia juu. Wanawake wengine wanamzunguka na kuanza kutoa hukumu. Anavyoandika Ngugi, ni kama wanawake wenyewe wanakuwa uchi! Mwanamke mmoja anashikilia upanga wenye makali na kutishia kuukata uume wa mshitakiwa. Lengo zima ni kumtaka mshitakiwa aungame kutoka rohoni kwamba hatarudia tena kumpiga mke wake.

Habari zikavuma nchi nzima kwamba kuna mahakama ya Wanawake; wanaume wakaogopa kuwapiga wake zao. Kikundi hiki cha wanawake cha kupigania haki na uhuru wa nchi ya Aburiria kilikuwa na mikakati mingi na uwezo wa kuingia sehemu nyeti bila kufahamika. Sikukuu ya kuzaliwa Kiongozi wa nchi ya Aburiria, kikundi hiki kilijipenyeza hadi jukwaani, kama kikundi cha ngoma, kumbe kilikuwa na ujumbe mkali. Kilimtaka Kiongozi wa nchi ya Aburiria, kumwachia huru mke wake aliyekuwa amewekwa kizuizini.

Kiongozi wa nchi ana safari ya kwenda Amerika, kutafuta fedha za kujenga Mnara wa Babeli. Bahati mbaya mapendekezo yake yanakataliwa na benki za Ulaya. Matokeo hayo yanamfanya Kiongozi anapatwa na ugonjwa wa ajabu. Mwili wake unaanza kutanuka, madaktari wanajaribu kumtibu wanashindwa. Hadi wasaidizi wa Kiongozi, wanafikria “Wizard of the Crow”. Mipango inafanywa kumtuma “Mchawi” kutoka Afrika, kwenda Amerika kumtibu Kiongozi. Habari zinavuma kwamba Kiongozi ana mimba! Mchawi, anafanikiwa kiasi fulani kumtibu Kiongozi na kumwezesha kurudia Afrika.

Mawaziri wa nchi ya Aburiria, wanaendelea kusalitiana na kuoneana wivu na kuchongeana kwa Kiongozi. Kama ilivyo kawaida ya viongozi wa Afrika, mawaziri hawa wanapotea mmoja baada ya mwingine. Tajirika, aliyeteswa wakati Kiongozi akiwa Amerika, anapanda ngazi hadi kufikia kileleni.

Tofauti na hadithi nyingine ambazo Ngugi, amekuwa akiziandika, zikiishia na mauaji na kumwaga damu. Hii ya Mchawi wa Kunguru, ina matumaini. Pamoja na kuelezea vituko vya uongozi wa Afrika, bado kuna matumaini. Sauti ya wananchi, inayoongozwa na Nyawira na wapambanaji wengine, inachomoza na kuleta matumaini katika nchi ya Aburiria.


V. TATHIMINI YA KITABU.

Nianze kwa kumpongeza Ngugi, kwa kazi hii nzuri sana aliyoiandika. Kusema kweli hadithi hii inaburudisha na kufikirisha. Ni hadithi ya kuchekesha; mtu unacheka mwanzo wa kitabu hadi mwisho. Ni vituko vya kweli na viongozi wetu wanafanya vituko hivyo: wananunua magari ya kifahari, wanajenga nyumba za kifahari, wakati wananchi wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa. Pili nimpongeze pia kwa kusikia kilio chetu na kujaribu kuyatafsiri baadhi ya majina ya wahusika kwenye lugha ya Kiswahili. Ukisoma Machokali, unapata picha ya mhusika, ukisoma Sikiokuu, unapata picha ya mhusika na matendo yake. Ukimsoma Tajirika, unaona kabisa vitendo vyote vya utajiri na ulafi wa Waafrika.

Tatu, ni kwamba tofauti na vitabu vingine ambavyo mwandishi ameviandika siku za nyuma, hadithi hii inaonyesha matumaini. Pamoja na maovu yote ya viongozi wa Afrika, bado Ngugi, anatuaminisha kwamba kuna matumaini. Cheche ya Sauti ya wananchi inaleta matumaini.

Nne, inagawa baadhi ya Wakenya nilioongea nao juu ya kitabu cha “Wizard of the Crow” wanamponda Ngugi, kwa kuandika mambo ya kizamani. Kwa kuendelea kushambulia ukoloni na ubeberu; wanasema Kenya ya leo ina mambo mapya na mawazo ya Ngugi, hayana nafasi tena, bado mimi namuunga mkono kwa msimamo wake. Matatizo ya Afrika yaliletwa na Ukoloni ambao uliutukuza ubeberu na unaendelea kuutukuza. Matatizo ya Afrika yanaletwa na viongozi kama vile wa Aburiria, wanaoshughulikia madaraka na kusahau kuyashughulika matatizo ya wananchi. Matatizo ya Afrika yanaletwa na watu kama Bwana Tajirika, anayetamani kubadilisha sura yake ili awe mzungu.

Tano, Ngugi, amefanikiwa kuwachora vizuri mawaziri wa Kiongozi wa Aburiria. Kule kujipendekeza na kushindwa kumshauri vizuri kiongozi. Ile hali ya kutaka kubadilisha viungo vya miili yao; kuwa na masikio makubwa, macho makubwa, midomo mikubwa na ulimi mrefu ni kuelezea hali ya kutojiamini na kutaka kujipendekeza kwa kiongozi ili kupata faida. Ni wazi Ngugi, ameweka chumvi katika kulielezea hili, lakini ndo ukweli wenyeweye. Wasaidizi wa viongozi wa Afrika wanaogopa kusema ukweli kwa kubembeleza nafasi ya kazi.

Sita, Kisa chote cha “Wizard of the Crow” kinaonyesha jinsi Ngugi, alivyo mwandishi makini na anaifahamu Afrika na matatizo yake. Waafrika tunapenda uchawi, tunapenda miujiza ili tupate mafanikio maishani bila kufanya kazi. Tunachoma misitu na kuharibu mazingira, huku tunaingia makanisani na misikitini kuomba Mungu atupatie mvua; tunaziachia raslimali zetu kusombwa na wageni, na baadaye tunalia kwamba sisi ni masikini; tunaingia kwenye nyumba za ibada kumwomba Mungu aondoe umasikini kwenye jamii zetu. Viongozi wa Aburiria, waliamini kwamba Mchawi wa Kunguru, alikuwa na nguvu za pekee, alitibu na kujua mambo mengine mengi, alikuwa na siri ya mti unaootesha fedha! Kwamba matawi yake ni fedha. Hata kiongozi wa nchi aliamini kwamba mti huo upo, na hivyo hata Benki za Ulaya zikikataa kumpatia fedha ya kujenga mnara wa Babeli, basi mti huo wa kuzalisha fedha ungemsaidia. Ni mfano kama ule wa Loliondo, ambako watu wanaamini kikombe kimoja kinaweza kutibu magonjwa zaidi ya sita na kwamba Mungu, ana uwezo wa kufahamu na kuelekeza kwamba shilingi mia tano zinatosha kulipia matibabu hayo.

Saba, kule kuonyesha kwamba matumaini ya ukombozi wa Afrika yako mikononi mwa wanawake, ni jambo la kupongezwa. Miaka hamsini ya uhuru wa Afrika, wanaume wamelisaliti bara hili; wameleta umasikini mkubwa, wameleta vita ya wenyewe kwa wenyewe; wameleta mauaji kama yale ya Burundi, Rwanda ,DRC, Uganda, Somalia na sasa Libya na kwingineko. Sasa ni zamu ya wanawake, kuliongoza Bara la Afrika. Ngugi, anamchora Nyawira, kama mama wa matumaini.

VI. HITIMISHO.

Ni wazi ningependa kuwashauri wasomaji wangu kukinunua kitabu hiki na kukisoma. Pamoja na ukweli kwamba bei ya kitabu hiki ni kubwa, tunaweza kutafuta mbinu za kukipata. Hata mimi nilisoma cha mwingine. Niliazima na kukisoma. Tukitaka kusoma, kuna njia ya kupata vitabu.

Kuna haja ya kutasiri kitabu hiki kwenye lugha ya Kiswahili. Taasisi ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, imefikisha miaka Hamsini ya kuwepo kwake. Nafikri mojawapo ya kusherehekea miaka hii hamsini, ingekuwa kufanya kazi ya kutafsiri vitabu kama hiki cha Ngugi. Anayoyaandika Ngugi, yanatugusa Waafrika sote. Hivyo tafsiri kwa Kiswahili, ingesaidia kitabu hiki kusomwa na watu wengi.

Pamoja na pongezi nilizompatia Ngugi, bado ana kazi ya kuhakikisha anatoa tafsiri ya majina ya wahusika kwenye hadithi zake. Ni sawa mengine ameyaweka kwenye lugha ya Kiswahili, lakini kitabu chake kinasomwa na watu wengine ambao si Waswahili. Labda kama mwishoni mwa kitabu , angejaribu kuweka ufafanuzi wa majina anayoyatumia ujumbe wake ungewafikia watu wengi na kwa haraka zaidi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.






















0 comments:

Post a Comment