INDIA WANA KITU GANI AMBACHO SISI HATUNA? Nakumbuka miaka ya nyuma, viongozi wetu walikuwa wakipata matibabu yao nchi za ulaya. Hata baadhi ya watu wenye fedha zao walikwenda kutibiwa Ulaya. Ubaguzi wa rangi ulipoanguka kule Afrika ya kusini, safari za matibabu ya Ulaya zikapungua na kuelekea Afrika ya kusini. Tulianza kusikia sifa za hospitali nzuri za Afrika ya kusini na huduma za hali ya juu zilizokuwa zikitolewa kule Afrika ya kusini. Viongozi na baadhi ya watu wenye fedha zao walianza kuelekea Afrika ya kusini kupata matibabu. Serikali ilianzisha mfumo wa kuwatuma wagonjwa kutibiwa Afrika ya kusini. Siku za hivi karibuni mambo yamebadilika tena kuhusu matibabu nje ya nchi. Sasa viongozi na watu wenye fedha zao wanakwenda India kwa matibabu na serikali imeendelea na mfumo wake wakuwatuma watu India kutibiwa na hasa kwenye hospitali za Appolo.Ni vigumu kufahamu vigezo vinavyotumika serikari kufikia hatua ya kumpeleka mgonjwa kutibiwa India; hata hivyo leo hii kuliko kule nyuma idadi kubwa ya wagonjwa inakwenda kutibiwa India kwa kulipiwa na serikali. Tunasikia sifa za matibabu mazuri yanayopatikana India. Ugonjwa ukishindikana kwenye hospitali zetu hata na Hospitali kubwa ya Taifa Mubimbili, wagonjwa wanatumwa India. Na kusema ukweli kasi ya kwenda India ni kubwa zaidi ya ile ya Ulaya na Afrika ya kusini ya miaka iliyopita. Nimekuwa nikijiuliza swali, India wana kitu gani ambacho sisi hatuna? Hospitali ni nzuri? Wana wataalamu wazuri? Wana vifaa vya kisasa? Huduma ni nzuri? Au ni kitu gani wanacho sisi hatuna? Madaktari wao wanasoma vyuo gani ambavyo madaktari wetu hawezi kwenda kusoma? Vifaa vya kisasa wanavipata wapi ambako dhahabu yetu haiwezi kuvinunua? Tuna almasi, tuna Tanzanite, tuna mbuga za wanyama, tuna mazao ya biashara kama kahawa, pamba, korosho na mengine; tunaweza vipi kushindwa kununua vifaa vya kisasa kwenye hospitali zetu? Kama tunaweza kununua mashangingi ya mawaziri, makatibu wakuu, wakurungenzi na viongozi wengine kama wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, tunashindwa kununua vifaa vya kisasa vya hospitali zetu? Kama huduma nzuri ndo inazifanya hospitali za India kusifika, “Huduma” hiyo inanunuliwa wapi ili na sisi tukainunue? Jumatano ya tarehe 6.6.2012, nilipopanda ndege ya Qatar, kumpeleka mtoto wangu mchanga kwenye matibabu India, swali hili lilirudia tena na tena kwenye kichwa changu “ India wana kitu gani ambacho sisi hatuna?”. Roho yangu ilinisuta kusafiri mbali hivyo kwa matibabu ya mtoto. Kwa nini hakutibiwa na kupona ndani ya nchi yangu? Binafsi nina imani tuna madaktari wazuri sana, ila inashangaza inafika mahali wanaamua kuwatuma wagonjwa nje ya nchi. Nakumbuka kuwasikia madaktari wetu wakilalamika kwamba hawana vifaa vya kisasa. Kwa maneno mengine wangeweza kufanya vizuri zaidi kama wangekuwa na vifaa vizuri. Hata hivyo huduma nzuri ya matibabu inategemea tu vifaa vya kisasa au kuna zaidi ya hapo? Kama vile kujenga utamadui wa kujituma, kujenga utamaduni wa kupenda kazi, utamaduni wa kutanguliza kuyaokoa maisha maana maisha yakiondoka hayarudi tena; kutanguliza huduma kabla ya kutanguliza mshahara? Wakati ninatafuta msaada kutoka kwa ndugu, marafiki na jamaa zangu kuniwezesha kwenda India kwa matibabu ya mtoto wangu, rafiki mmoja kutoka Amerika aliyekubali kunichangia fedha nyingi baada ya kunisuta alisema “ Privatus, nina imani kuna watoto wengi Tanzania, wanakufa kwa kutopata matibabu… ningekuwa na uwezo ningesaidia wengi zaidi ya kumsaidia mtoto wako. Lakini mimi ni mmoja na nimetokea kumfahamu Privatus. Basi pokea msaada wangu na umpeleke mtoto kwenye matibabu..” Nikiwa kwenye ndege, maneno ya huyo rafiki yangu yalirudi tena kichwani mwangu. Mimi nimefanikiwa kumpeleka mtoto wangu kwenye matibabu na wengine je? Watoto wengi wanakufa kwa kutopata matibabu. Wakati mimi nampeleka mtoto wangu India, kuna watoto wanakufa kwa malaria na kwa ugonjwa wa kuharisha. Mwezi wa tano nilikuwa wilaya ya Nkasi, ambako kuna vijiji havina hata mawasiliano ya simu. Gari la wagonjwa liko umbali wa kilomita 90. Mgojwa anayehitaji huduma ya haraka anafia njiani akipelekwa hospitali. Niliwaona watoto wengi kule Nkasi, wenye ulemavu ambao ungeweza kurekebika; watoto ambao ulemavu wao usigewazuia kwenda shule kama wangekuwa sehemu yenye huduma nzuri. Bahati mbaya watoto hawa hawana uwezo wa kufika Namanyere kwenye hospitali ya wilaya,sembuse Chennai India! Ingawa safari ya kwenda India ilikuwa na lengo la kuyaokoa maisha ya mtoto wangu, kwa njia moja ama nyingine yalilenga pia kufanya uchunguzi wa : India wana kitu gani ambacho sisi hatuna? Nilitamani safari hii kwa siku nyingi; naipata wakati mgumu wa kuuguza mtoto, lakini kama ilivyo mpango wa Mungu, nimebarikiwa kwa njii hii ili niweze kupata jibu la swali ambalo limekuwa likinisumbua kwa siku nyingi. Tulitua uwanja wa Chennai India, saa kumi Alfajiri. Moja kwa moja tulipelekwa hospitali na matibabu ya mtoto yakaanza. Hakukuwa na kupumzika kwanza. Hatukujua ulikucha lini; watu hawa wanafanya kazi bila kuangalia hata na muda. Ndani ya masaa nanane , nilishaelezwa matatizo ya mtoto wangu. Nilishangazwa sana na utendaji kazi wa watu hawa. Mimi nilifikiri tungepokelewa na kupelekwa hotelini kwanza, ili tuoge na kupumzika na kesho yake ndo tuje hospitali. Kumbe kwa wahindi ni “Kazi kwanza” mengine ni baadaye. Ugonjwa ambao sikuelezwa nyumbani ndani ya miezi miwili, niielezwa hapa India, ndani ya masaa manane! Swali bado ni lile lile India wana kitu gani ambacho sisi hatuma? Nyumbani niliambiwa matatizo ya mtoto wangu yataisha jinsi mtoto anavyoendelea kukua. Sikupenda jibu hili maana sayansi daima inatoa jibu la Kwa nini? Madaktari wa India, wamesema vile vile kama walivyosema madaktari wa Tanzania, lakini baada ya kugundua tatizo ni nini! Wale wanaonipenda na kunijali, walipendekeza niende kwenye maombi. Wengine walipendekeza niende kwa TB Joshua kule Nigeria, ili mtoto aombewe na kuponyeshwa kimiujiza. Sikuwakatalia, ila nilitaka nijue mtoto ana matatizo gani. Sasa hivi hata nikienda kwenye maombi,nitakuwa ninajua ninaomba mujiza wa aina gani. Pamoja na furaha ya kufahamu kwa undani ugonjwa wa mtoto wangu, sikuacha kutafiti: India wana kitu gani ambacho sisi hatuna. Swali hili niliwatupia ndugu zetu kutoka Nigeria niliokutana nao hapa Chennai. Kumbe wanaokimbilia India, si watanzania peke yao.Kuna watu kutoka Nigeria, Oman na nchi nyingine. Kwa upande wa Afrika Nigeria inaongoza kiasi kila mtu mweusi anayonekana kwenye hospitali za India, anachukuliwa kuwa Mnageria! Kwa watu wa kawaida mitaani hapa Chennai, Tanzania yetu haijulikani! Kwa hospitali na hasa upande wa malipo, Tanzania inajulikana kwa kutuma watu wengi wanaolipiwa na serikali na sifa kubwa ni serikali yetu kutofuatilia malipo. Bili zote zinalipwa bila kuhoji. Ukisema unatoka Tanzania, unaulizwa kama unalipiwa na serikali. Jibu ni muhimu kwa chumba utakachopata na huduma; ingawa huduma zote ni sawa, lakini malipo yanatofautiana. Wale wanaotumwa na serikali hudma yao iko juu ukilinganisha na wale wanaojilipia. Mnageria kijana, aliyejitambulisha kuwa anafundisha chuo kikuu kule Nigeria, alilijibu swali langu: India wana kitu gani ambacho sisi hatuna kwa kujiamini: “… ndugu yangu, wahindi wanafanya kazi kwa kujituma, wanapenda kazi na wanafanya kazi ili kufikia malengo fulani. Wahindi ni tofauti na sisi waafrika ambao tunafanya kazi ili tupate mshahara”. Huyu kijana kutoka Nigeria, aliendelea kulijibu swali langu kwa kusema kwamba “ … ingawa hapa India kuna rushwa, lakini ni tofauti na kule kwetu Afrika; sisi tunadai rushwa kabla ya kazi, na wakati mwingine mtu anakula rushwa na kazi haifanyiki, lakini India, ikitokea mtu akaomba rushwa atafanya hivyo baada ya kufanya kazi. Kule kwetu daktari, atataka umpatie rushwa kabla ya kukutibu, lakini hapa India, daktari anaweza akataka “tip” baada ya kukutibu”. Kijana huyu aliendelea kunielimisha juu ya mafanikio ya India “…nafikiri India, wamewekeza kwenye Afya. Wamegunduga kwamba huwezi kulijenga taifa kama watu hawana afya njema. Ndo maana wanatumia fedha nyingi kununua vifaa vya matibabu vya kisasa. Wameamua kuwalipa madaktari mshahara mzuri ili kuwashawishi wasikimbilie nchi za nje”. Hili wazo la kuwekeza kwenye Afya, lilinikumbusha kauri mbiu ya “Kilimo kwanza”. Wakati sisi tunakazana na Kilimo kwanza, India wanakwenda mbele na “Afya kwanza”. Wakati sisi Kilimo kwanza umebaki wimbo wa kisiasa, hawa wenzetu “Afya kwanza” wameweka kwenye matendo. Ingawa lengo lao kubwa lilikuwa ni kuokoa maisha ya wahindi na kuhakikisha India ina watu wenye Afya nzuri, “Afya kwanza” kimwekuwa kitegauchumi kikubwa. Kwa vile wametengeneza hospitali nzuri na zenye huduma za uhakika, watu wanatoka nchi mbali mbali kuja kutibiwa India. Gharama za matibabu ziko juu, hivyo “Afya kwanza” inaingiza fedha nyingi za kigeni. Mwanzilishi wa Hospitali za Appolo, ambaye pia ni daktari anasema alianzisha Hospitali hizi baada ya yeye kushindwa kumsaidia jirani yake aliyekuwa anaumwa. Vifaa alivyokuwa navyo daktari huyu havikuwa na uwezo wa kuyaokoa maisha ya jirani yake. Msaada mkubwa ungepatikana nje ya nchi na labda Ulaya. Jirani wa daktari hakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda Ulaya, hivyo alikufa kwa kushindwa kupata matibabu. Tukio hilo lilimsukuma daktari huyu kuanzisha hospitali nzuri. Anasema alifunga safari kuzunguka dunia nzima akiwatafuta madatari wahindi na kuwashawishi warudi nyumbani India kuokoa maisha ya watu. Aliweza kuwapata na kufungua hospitali. Leo hii Appolo wana zaidi ya hospitali 50 na nyingine imefunguliwa Dar-es-salaam Tanzania. Afrika ina madaktari wengi na wazuri, wanafanya kazi nje. Hawa wakishawishiwa kurudi, na serikali za nchi za Afrika zikakubali kuwekeza kwenye Afya, tunaweza kuwa na hospitali nzuri kama za hapa India. Tanzania, tuna madaktari wazuri ambao wametumkia Botswana, Namibia, Amerika na Ulaya. Akijitokeza mtu akawakusanya na kuishawishi serikali yetu kuwekeza kwenye Afya na kuanzisha kampeni ya “Afya kwanza”, ni imani yangu kwamba tunaweza kuwa na hospitali nzuri kiasi cha kuwashawishi watu kutoka nchi nyingine kuja na kutibiwa kwetu. Nafikri India hawana kitu chochote ambacho sisi hatuna! Tumeshindwa kuwekeza kwenye elimu, tumeshindwa kuwekeza kwenye viwanda, tumeshindwa kuwekeza kwenye teknolojia, tumeshindwa kuwekeza kwenye kilimo, basi tuwekeze kwenye Afya, maana Mtu ni Afya. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 6331 22. www.karugendo.net
MADAKTARI WETU MSIGOME, IGA MFANO WA DAKTARI PRATHAP C REDDY WA INDIA. Kila mtu anayejali akisikia madaktari wanataka kugoma ni lazima awe na wasi wasi. Ni wazi kuna wale wasiojali na kulichukulia jambo hili kama la kawaida. Wale ambao wao na jamaa zao wana uwezo wa kwenda kutibiwa nje ya nchi au kutibiwa kwenye hospitali binafsi, mgomo wa madaktari ni msamiati. Lakini wale ambao wanategemea hospitali za serikali, mgomo ni tishio na kama kuna la kufanya wangelilifanya ili kuepusha mgomo huu. Kusikia kwenye vyombo vya habari haitishi zaidi ya kuguswa, ukapeleka mgonjwa wako hospitali akamaliza masaa bila huduma na wakati mwingine ukashuhudia roho ya ndugu yako inakatika mikononi mwamo kwa vile hakuna daktari wa kumshughulikia. Mgomo wa madaktari ni tishio la uhai. Sisi Tanzania tunakazana na kilimo kwanza, lakini nchi nyingine duniani zinakazania Uhai kwanza. India ni mfano mzuri, hawa wamewekeza kwenye afya na uhai. Wakati Tanzania tunawekeza kwenye vitu vingine kama magari ya kifahari na posho kubwa kwa viongozi wetu, nchi nyingine duniani zinawekeza kwenye Afya, kwenye uhai. Uhai ni kitu hadimu, ukitoweka hakuna wa kuurudisha! Wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha tunaulinda uhai, ni wajibu wa kila mtu hata madaktari wetu wakiwemo. Hivyo ninaandika makala hii kuwaomba madaktari wetu waachane na mgomo wambao kwa njia moja ama nyingine utahatarisha maisha ya uhai wa watanzania. Nawasihi sana watangulize uhai wa watanzania kabla ya kutanguliza maslahi binafsi Sina lengo la kusema kwamba madaktari wanakosea kudahi haki zao, na wala sipendi kuitetea serikali kwamba haina fedha za kutimiza ahadi zake kwa madatari. Naungana na madaktari wetu kuishingaa serikali inayofunika matatizo bila kuyatanzua, serikali inayoamini kwamba kila kitu kitakwisha kwa miujiza. Ninajua kabisa kwamba madatari wetu wanalipwa mshahara kidogo, wanafanya kazi nyingi na ngumu kwenye mazingira magumu. Madaktari wetu hawana vifaa vya kutosha kuyakoa maisha ya watanzania wengi. Ninajua jinsi madaktari wetu walivyo na moyo wa uvumilivu na wamekuwa wakiivumilia serikali na ahadi zake za uongo. Muda walioipatia serikali unatosha kwaruhusu kugoma. Ila wakigoma, watakaoumia si viongozi wanaokataa kutimiza ahadi zao, bali ni wananchi wa kawaida. Uhai wa watu wasiokuwa na hatia utapota na ukipotea hauwezi kurudi. Wakati naandika makala hii nimesikia taarifa ya kuchekesha kwamba mahakama ya Kazi imesitisha mgomo wa madaktari. Huku ni kutumia ubabe bila kufikiri. Sawa Mahakama imezuia mgomo wa wazi, lakini haina uwezo wa kuuzima mgomo baridi ambao ni mbaya zaidi. Madaktari watafika kazini kama kawaida, lakini hawatafanya kazi. Watashinda wanazunguka kutoka upande mmoja wa hospitali na kwenda mwingine. Sawa mahakama imeusitisha mgomo, lakini je Mahakama hiyo itashika bunduki ili kuhakikisha kila daktari anafanya kazi? Serikali itafurahi kutosikia dalili za mgomo, lakini je serikali ina uwezo wa mtu anayekataa kuwatibu wagonjwa kwa kisingizio cha ugonjwa? Kwa maoni yangu ni bora waachane na mpango wao wa kugoma. Waachane na kazi za serikali na kujiunga pamoja kuanzisha Hospitali nzuri ya binafsi. Hili ndilo jibu la matatizo yao na serikali ni lazima itafunza na kuanza kuwahudumia watakao baki kwa nguvu zote, vinginevyo hospitali za serikali zitafungwa. Leo serikali yetu inalipa fedha nyingi kuwapeleka viongozi na watu wengine kutibiwa India. Hivyo wadaktari wetu wakijiunga na kujenga hospitali nzuri yenye vifaa vya kisasa, fedha yote ya serikali inayokwenda India, itaelekezwa kwenye hospitali zao nzuri watazozianzisha. Ninawaomba madaktari wetu waige mfano wa Dakta Prathap C Reddy, wa India Aliyeanzisha mahospitali ya Appolo. Daktari huyu alisomea India na baadaye alienda kujiendeleza kusoma Uingereza na Marekani. Alifanya kazi huko kwa muda na baadaye kuamua kurudi India. Aliporudi India, jirani yake alikuwa mgonjwa na alihitaji matibabu nje ya India. Daktari Prathap, alijitahidi kumsaidia jirani kwa uwezo wake aliokuwa nao, lakini kwa vile alikuwa hana vifaa vya kisasa na fedha hazikupatikana kumpeleka jirani yake India kwa matibabu, jina yake huyo alikufa. Tukio hilo lilimsikitisha, maana yeye alikuwa na utaalamu wa kumtibu, lakini hakuwa na vifaa na hakuwa na fedha kumsaidia aende kutibiwa nchi za nje. Tukio hilo lilimsikitisha na kumsonenesha. Hicho ndicho kilimsukuma kuanzisha Hospitali za Appolo. Leo hii hospitali hizi zinasifika India na nje ya India, ni hospitali ambazo zinafanya kazi ya kuyaokoa maisha ya watu wa India na watu wa mataifa mengine. Daktari huyu mwanzilishi wa Appolo, aliwashawishi madaktari waliokuwa wakifanya kazi kwenye hospitali za serikali na kulipwa mshahara kidogo kuachana na kazi za serikali na kuunga naye kuanzisha hospitali nzuri zenye vifaa vya kisasa. Mbali na kuwashawishi madaktari wa ndani ya nchi, alitembea dunia nzima akiwashawishi madaktari wahindi waliokuwa wakifanya kazi Ulaya na Amerika ,kurudi nyumbani kuokoa maisha ya wahindi wenzao. Appolo ilianza mwaka wa 1983, ikiwa na vitanda 150. Leo hii ina vitanda zaidi ya elfu nane, na imewatibu wagonjwa zaidi milioni 26 kutoka nchi 120 na Tanzania ikiwemo. Appolo wana hospitali zaidi ya 53 India na nchi nyingine na Tanzania ikiwemo. Nilipokwenda India mwanzoni mwa mwezi huu, niliambiwa kuna Appolo hospital jijini Dar-es-salaam. Bado naisaka hospitali hii niipata nitawashauri madaktari wetu waende huko jijifunza namna ya kujiunga na kufanya kazi pamoja. Alichokifanya daktari huyu ni kuwakusanya madatari, kutafuta mikopo kutoka kwenye mabenki makubwa na kuanzisha hospitali nzuri yenye vifaa vya kisasa.Madaktari hawa sasa wana mishahara mizuri ambayo wasingeweza kuiipata kule serikalini. Wanatoa huduma nzuri kwa wagonjwa na maisha yao yameboreka. Hili ndilo ombi langu kwa madaktari wetu. Badala ya kuendeleza migomo na kuyaweka maisha ya watu hatarini, ni bora wakaachana na serikali. Wajiunge pamoja na kuanzisha hospitali ya binafsi nzuri na yenye vifaa vya kisasa. Kama mabenki yanawakopesha wafanyabishara wengine, kwanini isiwakopeshe madaktari wetu wanaotaka kujenga hospitali nzuri na yenye vifaa vya kisasa? Ninajua kuna hospitali ya namna hii iliyoanzishwa na madaktari Bingwa wa Muhimbili, ni wazi inajitahidi, lakini bado inasuasua kwa huduma na haina vifaa vya kisasa. Mbaya zaidi ni kwamba madaktari bingwa bado wanaendelea kufanya kazi Muhimbili, wakitoka huko wamechoka, wanakuwa hawana nguvu za kuwahudumia wagonjwa kwenye hospitali hiyo ya binafsi. Dawa pekee ni kuacha kazi serikalini na kujiuunga pamoja kuanzisha hospitali iliyotukuka. Nina imani serikali inayokataa kuwasiliza madaktari leo hii, serikali inayokaa kutoa fedha za kumaliza matatizo ya madaktari, itatoa fedha nyingi kuwalipia viongozi na watu mbali mbali watakaotibiwa kwenye hosptiali binafsi za madaktari wetu. Migomo ni mizuri kushinikiza kudai haki, lakini wakati mwingine si dawa ya matatizo yote. Dawa pekee ni madatari kuachana na serikali na kuanzisha hospitali nzuri ya binafsi. Tanzania tuna madaktari wazuri na wenye sifa za juu nje ya nchi. Ukienda Botswana, Namibia, na nchi nyingine za Ulaya na Amerika, utawakuta madaktari mabingwa kutoka Tanzania. Hawa wakipata mtu wa kuwashawishi na kuwahamasisha kurudi nyumbani,Tanzania tunaweza kuwa na hospitali nzuri ya Afrika ya mashariki na kati. Na, Padri Privatus Karugendo. +255754633122 pkarugendo @yahoo,com www.karugendo.net
“ LIWALO NA LIWE” ULIMI ULITELEZA? “Liwalo na Liwe” ni maneno ya kukata tamaa? Kama Waziri mkuu anafikia hatua ya kukata tamaa, ni bora kusema ameshindwa kazi na kuachia ngazi kabla ya kuleta vurugu na maisha ya watu yakapotea bure; je wananchi nao wakikata tama na kusema “Liwalo na liwe” tutafika wapi? Vurugu na vita popote duniani zinaanza pale viongozi na wanaongozwa wakikata tama na kusema “Liwalo na Liwe”. Au tuseme tu kwamba “Liwalo na liwe” ni maneno ya mtu mwenye kiburi cha madaraka? Ni maneno ya mtu mwenye busara? Ni maneno ya mtu anayeongoza nchi katika mfumo wa kidemorasia? Ni maneno ya kulipenda taifa? Au ni maneno ya mtu asiyejali ambaye kwake kufa na kuishi ni mapacha? Au tuseme ni maneno ya mtu ambaye yuko tayari kupambana akijiamini kwa nguvu alizo nazo na kujiaminisha kwamba hakuna la kumtisha wala kumtikisa? Kiongozi aliyechanguliwa kwa kura za wananchi anaweza asiogope kutikiswa na wale waliomwajiri? Hicho ni kiburi au ni…..? Kama Waziri Mkuu angekuwa kilabuni anakunywa pombe akajisemea “Liwalo na liwe” tunaweza kusema ulimi kumeteleza! Au Waziri Mkuu akiwa nyumbani kwake, anaongea mambo ya kifamilia na kusema “ Liwalo na liwe” hakuna atakayejali maneno hayo isipokuwa ladda familia yake hata kama maneno hayo yakiwekwa kwenye vyombo vya habari. Au Waziri Mkuu, akiwa na viongozi wenzeke wanachapa michapo, akajisemea “ Liwalo na Liwe” hakuna atakayejali. Lakini Waziri Mkuu akisema “Liwalo na Liwe” akiwa amesimama Bungeni; kwenye Jumba tukufu la taifa letu la kutunga sheria na kuishauli serikali; akiwa na akili timamu, akiwa anatoa hoja juu ya jambo linalogusa maisha ya kila mtanzania: Mgomo wa Madaktari, akajisemea “ Liwalo na Liwe”, ni vigumu kuamini kwamba ulimi uliteleza au kwamba alikuwa na maana nyingine ya neno “Liwalo na Liwe”. “Liwalo na liwe” hata kama watu wanakufa hakuna shinda! Mtu mwenye akili nzuri na ambaye anaweza kuchambua mambo vizuri ni lazima afikiri hivyo. Mjadala ulikuwa juu ya mgomo wa madaktari. Serikali ilitakiwa kutoa tamko juu ya mgomo huo: Kwa maana ya itafanya nini ili mgomo huo ufikie mwisho. Madaktari walipogoma mara ya kwanza, walikaa chini na serikali na kujadiliana na kukubaliana lakini serikali ya “Liwalo na liwe” haikutekeleza makubaliano. Uamuzi wa madaktari ukawa ni kugoma tena ili kuishinikiza serikali kutekeleza ahadi zake. Mgomo huu umeshika kasi, huduma kwenye hospitali za serikali unasuasua. Wenye fedha wanawakimbiza wagonjwa wao kwenye hospitali za watu binafsi. Wale ambao hawatibiwi ndani ya nchi (Na waziri mkuu akiwemo) wala hawana habari na linaloendelea. Wananchi wa kawaida wanateseka na wengine wanakufa kwa kutopata huduma. Ni wakati ambao kila mtanzani anasubiri kusikia hatua za haraka za serikali kumaliza mgomo huu. Na mara waziri mkuu anasimama Bungeni na kusema serikali itatoa uamuzi “Mgumu” juu ya mgomo wa madaktari “Liwalo na liwe”. Wakati Waziri Mkuu anatoa maneno hayo, Kiongozi wa mgomo wa madaktari anakamatwa, anapigwa, anateswa na kutupwa kwenye msitu kama ilivyotokea kwa wafanyabishara wa Mahenge. Je hii ndo maana ya “Liwalo na Liwe”? Au Serikali itajikosha na kusema haina habari zozote juu ya tukio hilo? Kuwateka watu, kuwapiga na kuwaumiza na wakati mwingine kutoa uai wao ni matukio yanayotokea kwenye nchi zinazotawaliwa kimabavu. Iddi Amin Dada, aliyekuwa Rais wa Uganda enzi zile, ambaye sisi tulimbatiza jina la Nduli, alikuwa akiwatesa na kutoa uai wa wapinzani wake. Dunia nzima ilimchukia baada ya vyombo vya habari kuonyesha picha za watu aliokuwa akiwatesa na kuwapiga risasi mchana kweupe mbele ya umati wa watu. Baada ya kuona unyama wake, dunia nzima ilimchukia. Picha za Kiongozi wa mgomo wa madaktari zilizosambaa kwenye magazeti na kwenye mitandao ya kijamii, zinaonyesha unyama kama ule wa Iddi Amin. Ingawa hadi sasa hivi serikali inajikosa kutoshiriki; bado kuna kishawishi kikubwa cha kuamini kuwepo mkono wa serikali. Nduli Iddi Amin aliyekuwa jirani yetu, sasa ametuingilia mpaka ndani! Kama “Liwalo na liwe” ina maana yenyewe, basi Serikali ina mpango wa kuwafukuza kazi madaktari waliogoma au kuwakamata na kuwaweka kizuizini? Au kuwakamata na kuwatesa kama ilivyotokea kwa kiongozi wa mgomo? Kwa vyo vyote vile “Liwalo na liwe” si neno lenye nia njema. Tanzania tuna madaktari wachache. Na hao tulio nao, serikali imewasomesha kwa shida. Hadi leo hii tunashuhudia vita katia ya serikali na wanafunzi juu ya mikopo. Wakati tunashindwa kuindesha serikali kwa fedha zetu wenyewe mbaka tupate msaada kutoka nje, tunaweza kupata wapi kiburi cha kuwafukuza kazi madaktari? Ina maana tukiwafukuza, kesho tunawapata wengine? Waziri Mkuu anasema tutatumia hospitali za jeshi. Ziko ngapi hospitali hizi kuweza kutoa huduma kwa watanzania wote? Eti watawarudisha kazini madaktari walioshtaafu! Hili linawezekana, lakini je wakiwarudisha madaktari wastaafu kazini, watanunua na vifaa vipya na vya kisasa? Ugomvi wa madaktari si mshahara na posho bali ni vifaa pia. Lakini hili la vifaa linawekwa pembeni ili kuonyesha kwamba madaktari wana roho mbaya. Madaktari ni watanzania na wanaishi hapa. Wanashuhudia jinsi fedha ya serikali inavyofujwa. Mfano mzuri ni Bunge letu. Kwanza lina wabunge wengi ambao kazi yao haionekani! Bunge linatumia fedha nyingi kuwalipa wabunge wanaoshangilia kila kitu hata mambo ambayo ni hatari kwa taifa letu. Mfano mbunge anayeunga mkono hoja asilimia miambili, kwanini apewe tena muda wa dakika 15 kuongea? Asilimia kubwa ya wabunge wetu wanaunga hoja zote mkono. Hivyo hao wanaounga mkono, kama wangekaa kimya bila kupoteza muda wa kuongea, Bunge la bajeti lingekuwa linakaa siku chache sana na kuokoa fedha nyingi zinazoteketea kule Dodoma. Fedha hizo zingeelekezwa kwenye Afya na kupunguza kelele na migomo ya madaktari. Kuna mambo mengine mengi ambayo yanatumia fedha nyingi bila sababu za msingi. Tuna sherehe za kitaifa ambazo hata bila kuzisherehekea, taifa litasonga mbele. Matumizi makubwa ya viongozi wetu kuanzisa kwa Rais hadi kwa wabunge, yanaweza kusitishwa na taifa likasonga mbele. Hivyo madaktari wanapopiga kelele kutaka vifaa vipya na vya kisasa, wanapotaka waongezewe mshahara, wanafahamu fika kwamba serikali ina fedha. Tumesikia wabunge wakilalamika kwamba Serikali inatuma fedha nyingi kwenye Halmashauri za wilaya, lakini fedha hizi zinapotelea njiani! Fedha hizi zinaingia shimo gani? Tunashuhudia wafanyakazi wa Halmashauri hizi wakijenga majumba makubwa, wanaendesha magari ya kifahari, wana mashamba makubwa, wana mifugo wengi, wanasomesha watoto wao nje ya nchi, wanatibiwa nje ya nchi, wanakwenda kupunmzika na kufanya manunuzi nje ya nchi. Serikali imekaa kimya, sauti yake inasikika kwa madaktari “Liwalo na liwe”. Na, Padri Privatus Karugendo.
MSIPOTEZE MUDA KUIUMIZA MIILI YETU; KAMA MNAWEZA SHUGHULIKIA ROHO ZETU! Makala hii ni kwa yeyote anayehusika; yeyote ambaye ana madaraka makubwa juu ya wengine; yeyote anayefikiri yuko juu ya sheria; yeyote anayefikiri anaweza kutoa uhai wa binadamu mwenzake pale anapotaka na kufikiri kwamba yeye ataishi milele; yeyote anayefikiri kuutesa mwili hadi kifo ni mwisho wa kila kitu; kwamba kama ni matatizo yatakwisha. Makala hii ni kwa viongozi wetu waliotufikisha hapa tulipo; tumefika hatua ya Liwalo na Liwe: Kila mtu akizingatia hilo tumekwisha! Tumekuwa tukiimba amani na utulivu kwa miaka mingi, lakini upepo unavyoanza kuvuma tunaelekea mwisho wa Amani na utulivu. Makala hii inaandikwa na wale wote wanaotetea haki za binadamu, wanaotetea haki zao na wale ambao daima wanajitokeza kuwasemea wengine. Tumekuwa tukisema, na sasa tunasema na tutaendelea kusema hata kama wale wa kusikia wanayaziba masikio; tuna imani kelele zetu ziyazibua masikio yao. Yale yaliyomtokea Dakt Ulimboka, yanaweza kumkuta yeyote Yule awe mwalimu, mwanafunzi, mkulima, mfugaji, mwananchi wa kawaida anayepigania haki za kiwanja chake, mwananchi wa kawaida anayepigania haki za ajira yake au machinga anayepigania haki zake. Kuna dalili zote za kutaka kuwatisha watu wanaopigania haki zao. Vishawishi vya kuwaziba midomo vinaposhindwa, nguvu za ziada ziananza kutumika. Inatisha, inakatisha tama, lakini yule atakayevumilia hadi dakika ya mwisho ndiye atakayetetea haki zake na haki za wengine. Makala hii inaandikwa kwa masikitiko makubwa; ni makala ya majonzi, ya kuomboleza, kulaani, kukemea na kutukana unyamaa huu unaoanza kujitokeza kwenye taifa letu. Tulitegemea kwamba jambo hili la unyama huu mpya katika taifa letu lingejadiliwa Bungeni. Tumewachaguwa wabunge kutusemea na kutuwakilisha; lakini baada ya kusikia Spika wa Bunge letu akisema Jambo la Dakt Ulimboka na sakata zima la madaktari haliwezi kujadiliwa Bungeni kwa vile kesi iko mahakamani; Ingawa kujadili sakata hili si kujadili ushahidi wala kujadili kesi inayoendelea. Ukweli ni kwamba madaktari bado wanaendelea na mgomo; watu hawana huduma na mbaya zaidi Dakt amekamatwa, amepigwa na kuumizwa; Bunge likae kimya? Liwe Bubu wakati unyama unaendelea? Ni Bunge la wananchi au Bunge la viongozi na vigogo wachache? Vitisho vinaendelea na labda watu wengine watakamatwa na kupelekwa msitu wa mateso; hatua hii imetufanya kukata tamaa na kubakia na njia ya kutoa maoni kupitia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Tutajadili vijiweni, tutajadili kwenye daladala na kwenye sehemu zetu za kazi maana huko hakuna Spika wa kuzuia majadiliano. Hatari ya mijadala isiyokuwa na spika wa mwenyekiti, inajulikana duniani kote, moto ukianza kuwaka, kuuzima ni vigumu. Ujumbe wa makala hii ni mfupi: Ni ujumbe kwa yeyote anayehusika kama nilivyotaja hapo juu: Msipoteze muda kuiumiza miili yetu; kama mnaweza shughulikia roho zetu! Tafuta njia, mfumo na mbinu za kuziteka roho zetu! Mwili unakufa, unaoza, unanuka. Hata miili yenu pia itakufa, na kuoza. Lakini roho inabaki na kudumu! Mwenye busara, mwenye hekima, hawezi kupoteza muda wake kuutesa mwili; bali atatafuta njia ya kuiteka roho ya mtu. Kuna njia nyingi za kuiteka roho, na njia hizi ni za wazi na wala si za kificho, njia hizi ni za kukomaza fikra za wananchi kulipenda taifa lao, kulitumikia, kulilinda na kuhakikisha taifa lao linabaki salama kwa vizazi vijavyo. Kiongozi bora ni yule anayetafuta njia zote za kuteka roho za wananchi; akifanikiwa kwa hili anakuwa ametoa mchango mkubwa kwa taifa lake. Kiongozi wa ovyo ni yule anayepoteza muda kuitesa miili ya wananchi wake au kuitukuza miili hiyo. Mwili ni mapambo tu kwenye uhai wa mwanadamu. Mwili unakufa na kuzikwa; hivyo kuutesa na kuufanyia mambo ya kinyama kama alivyofanyiwa Dkt Ulimboka, ni aibu kubwa kwa mtu yeyote mwenye akili timamu. Kwa nini kupoteza muda na nguvu kushughulikia kitu kinachopita na kukiacha kile cha muhimu kama vile roho? Viongozi wa ovyo walioshughulikia miili ya watu na kushindwa kuzishughulikia roho za watu, wamebaki kama vinyago katika historia ya Mwanadamu. Wanatukana na kupambwa na sifa ya mauaji; dunia inawalaani na kubaki kwenye orodha ya watu wa ovyo kupata kutokea hapa duniani. Wale wanaotaka kujiunga na orodha chafu waendekeze utamaduni huu mchafu wa kuwatesa watu wanaotetea haki zao. Orodha chafu ni pamoja na Hosni Mubarak, katika uzee wake amehukumiwa miaka mingi jela, Saddam Hussein, aliyenyongwa hadi kufa kama alivyofanya kwa wapinzani wake, Pol pot, Idi Amin, Mobutu Sese Seko, Nicolae Ceausescu, Slobodan Milosevic, Jean-Claude Duvalier, Ferdinand Marcos, Fulgencio Batista, Antonio Salazar, Alfredo Stroessner, Benito Mussolini na Adolf Hitler. Wote hawa heshima yao ilishushwa na vitendo vyao vya kinyama kuitesa miili ya binadamu. Walishindwa kuziteka roho za watu wao. Hata katika misaafu tunaonywa: “ Basi, msiwaogope watu hao. Hakuna cho chote kilichofunikwa ambacho hakitafunuliwa, wala kilichofichwa ambacho hakitafichuliwa. Ninalowambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong’nezwa, litangazeni kwa sauti kuu. Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja roho...” Matayo:10:26-28. Hapa Tanzania, hakuna mtu mwenye uwezo wa kuangamiza mwili na roho. Hata kwa Dkt Ulimboka, pamoja na mateso yote aliyopatiwa hadi kupoteza fahamu, bado roho yake imebaki imara. Waliutesa sana mwili wake, lakini wakashindwa kuifikia roho yake. Roho haifikiwi kwa vitendo vya kinyama, bali vitendo vya ubinadamu; Haki, wema na huruma. Wakati anapelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi bado alikuwa akisisitiza wenzake kuendeleza mapambano ya kudai haki zao. Mateso ya kinyama aliyoyafanyiwa hayakuigusa roho yake. Uwezo wao unaishia kwenye kuutesa mwili, lakini uwezo wa kuiangamiza roho haupo kwa yeyote yule. Na kama tulivyosikia kutoka kwenye msahafu, kwamba kila kitu kitafunuliwa; je serikali ya kidemokrasia ina siri gani? Serikali ya wananchi, inayochaguliwa na wanachi na kuwekwa madarakani na wananchi ina siri gani kiasi cha kufikia hatua ya kuwakamata watu na kuwatesa? Serikali ya wananchi ina wajibu mkubwa wa kulinda usalama wa taifa, uhai wa wananchi. Na usalama wa taifa, hauna maana ya usalama wa mtu mmoja mmoja, bali usalama wa watu wote. Usalama wa taifa si kumaanisha usalama wa viongozi, ni usalama wa wananchi wote. Usalama wa taifa unapogeuka kuwa wa mtu mmoja au wa viongozi, tunakuwa tumepoteza kabisa maana nzima ya usalama wa taifa. Hoja inayoyejengwa hapa ni kwamba, kama kuna siri ya aina yoyote ile inayolindwa na serikali, ni kwa manufaa ya wananchi wote. Hivyo hakuna sababu ya mtu mmoja kuteswa kwa lengo la kulinda siri za taifa. Hata hivyo kuutesa mwili hakuna maana yoyote ile, maana bila kuigusa roho ni kazi bure. Mfano mzuri, Dk Ulimboka, amepigwa, ameteswa na labda atakufa! Lakini mapambano ya madaktari kudai haki zao yako pale pale! Tumeshuhudia jinsi madaktari walivyokuwa wakisema kwamba tukio la kumpiga mwenzao limewapatia moyo wa kundelea kudai haki zao. Na kama tukiwa wakweli kwa historia; hakuna popote pale duniani ambamko vitendo vya kuutesa mwili vilifanikiwa kubadilisha mawazo ya watu. Viongozi waliotawala kwa mabavu, walijaribu kuwapiga watu, kuwatesa na kuwaua, lakini hawakufanikiwa kufuta roho ya kudai haki. Hata pale ambapo wengine waliendesha mauji ya kimbali bado roho ya kudai haki ilibaki na kudumu. Kumpiga na kumumiza Dkt Ulimboka ni kati ya vitendo vya kinyama vinavyofanywa na binadamu asiyefikiri. Maana mtu anayefikiri vizuri hawezi kumpiga binadamu mwenzake kwa nia yoyote ile; ukimpiga unaumiza mwili wake na roho yake inabaki salama, ukimpiga risasi akafa, unakufa mwili, lakini roho yake inabaki salama. Hadi leo hii tuna roho za watu waliokufa, wako kaburini lakini roho zao ziko salama na zinaishi miongoni mwetu. Roho ya Baba wa Taifa bado tunaishi nayo; roho ya Mkwawa bado tunaishi nayo, roho za mashujaa wote waliokufa wakitetea heshima na maisha ya watanzania bado tunaishi nazo; wao walikufa ili sisi tuweze kuishi kwa uhuru na salama. Hivyo hivyo na sisi lazima tufe tukipambana kulinda uhuru na usalama wa vizazi vijavyo, kinyume na hapo tutakufa na miili yetu na roho zetu! Hivyo kwa kiongozi anayetaka kuiongoza Tanzania, afahamu kwamba kuwapiga watu, kuwakamata na kuwafunga au kuwaua si msaada wa kumsaidia kuwaongoza vizuri. Njia hii imetumiwa na wengi na wameshindwa. Makaburu wa Afrika ya kusini, walimkamata Mandela na kumfunga na kumtesa zaidi ya miaka ishirini na nane, lakini kwa vile hawakufanikiwa kuigusa roho yake, wafuasi wake waliendeleza mapambano hadi alipofunguliwa. Makaburu walifikiri kumfunga Mandela ni kumaliza tatizo, kumbe mbegu ilikuwa imepandwa na inakua kwa kasi ya kutisha. Pamoja na nguvu za jeshi la Arika ya Kusini, hawakufua dafu mbele za nguvu ya Umma. Lakini pia tuko kwenye zama za Demokrasia, mtu anayechaguliwa kuitawala Tanzania, anakuwa na kipindi cha miaka mitano. Baada ya hapo anaweza kuendelea au kuondoka. Na kufuatana na katiba hawezi kupata vipindi zaidi ya viwili , katika hali kama hiyo kuna haja gani kuwa na vyombo vya kuwakamata watu, kuwatesa na kutoa uhai wao kwa lengo la kutafuta maadui wa utawala? Wakati namalizia kuandika makala hii Rais Jakaya Kikwete, anahutubia taifa na kukana kata kata kwamba Serikali haina mkono katika mateso ya Dkt Ulimboka. Na wala sikutegemea Rais, akubali jambo hili la kinyama; na hata akikubali kama ilivyotokea kwa Mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge, hatimaye waliokamatwa na kufikishwa mahakamani waliachiwa huru! Hata kwa Dkt Ulimboka, ni wazi watakamatwa, maana yeye aliwatambua baadhi, ambo hadi sasa inasemekana ni Usalama wa taifa. Kuna mashaka makubwa kama haitakuwa kama ile ya wafanyabiashara wa Mahenge. Hata kama serikali haiusiki na mateso ya Dkt Ulimboka, kwa yeyote anayehusika, apate ujumbe huu kwamba asipoteze muda wake kuitesa miili yetu, bali azishughulikie roho zetu. Lakini ikiwa ni mwendo wa Litakalo na liwe, basi miili yetu iko tayari kupokea mateso ya kutetea haki, ukweli na usawa na roho zetu zitabaki imara! Na, Padri Privatus Karugendo. pkarugendo@yahoo.com +255 754 633122 www.karugendo.net
TUMEKOSEA: TUJISAHIHISHE! Ndani ya juma moja tumeshuhudia mara mbili kwenye vyombo vya habari uchaguzi wa Vijana wa CCM ukivurugika. Vijana wamefikia hatua ya kurushiana viti na kutaka kupigana. Kuna manung’uniko kwamba fedha nyingi(za kuhonga) zinatumika katika kuwachagua viongozi wa umoja wa vijana. Tumeshuhudia pia vurugu kama hizo zikijitokeza kila panapokuwa na uchaguzi ndani ya vyama vya siasa. Jumuia zote za CCM haziwezi kufanya uchaguzi bila vurugu, kutuhumiana matumizi makubwa ya fedha na kuwahonga wapiga kura. Nyuma tulikotoka, hakukuwa na vurugu kama hizi. Watu waliendesha shughuli za vyama vya siasa kwa kujitolea. Watu walijitolea nguvu zao na mali ili kujenga na kuendeleza vyama vyao vya siasa. Wimbi jipya la kufikiri kazi ya serikali ni kutengeneza ajira, ndilo limetufikisha hapa tulipo. Kwa kuchanganyikiwa huku serikali yetu ikaifanya siasa kuwa ajira. Mawazo ya vijana na watu wote ambao wanataka ajira ya mtelemko wanakimbilia siasa. Tumeshuhudia jinsi watu wanavyopambana kuupata Ubunge. Wanatumia fedha nyingi, wakiamini baada ya kufanikiwa, fedha yao itarudi na watapata zaidi. Hivyo wakishashinda wakaingia Bungeni, kazi kubwa ni kuhakikisha fedha inarudi; kazi ya kuwawakilisha wananchi inawekwa pembeni. Si lazima kuelezea kwenye makala hii kwamba hata juzi juzi tuliwasikia wabunge wetu wakitaka kulipwa pensheni wanapomaliza kipindi chao cha kuwa bungeni. Kwa vile wanaamini Ubunge ni ajira, hawaoni sababu ya wao kutopata pensheni kama waajiriwa wengine wote. Siasa si ajira na kamwe kazi ya serikali si kuwatafutia wanasiasa kazi. Tunashuhudia serikali ikiongeza wilaya na mikoa na majimbo ya uchaguzi ili kuwatafutia wanasiasa kazi. Ndo maana tunasikia mtu mmoja anakuwa mkuu wa mkoa, pia mbunge na wakati mwingine ni mwenyekiti wa bodi. Kazi ya serikali si kuwaajiri watu bali ni kujenga mazingira mazuri ya raia wake kuweza kufanya kazi zao za kujipatia kipato ili waishi. Hii ndiyo kazi kubwa ya serikali zote duniani. Kinyume na hivyo ni vurugu kama tunazozishuhudia na kama tulizozishuhudia kwenye historia zikisababisha serikali kuanguka kwa kushindwa kufanya kazi yake. Serikali bora, serikali makini na serikali ya wananchi ni lazima ijenge mazingira bora ya wananchi kufanya kazi zao na kujipatia kipato ili waishi. Mazingira bora ni kama: Kudumisha amani na usalama. Ndiyo maana serikali inakuwa na Jeshi na vyombo vya ulinzi na usalama. Mwalimu Nyerere, alilibatiza Jeshi letu: Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Jina hili si la bahati mbaya; maana yake ni kwamba si Jeshi la Rais, si jeshi la viongozi, si jeshi la chama cha siasa, si jeshi la kidini,si jeshi la matajiri fulani au kikundi fulani cha watu, bali ni jeshi la kulinda usalama wa watu wote wa Tanzania. Uhalali wa kuwepo kwa jeshi hili unatokana ridhaa ya wananchi wote wa Tanzania. Kazi ya serikali ni kutoa elimu kwa wananchi wake. Kujenga shule bora na zenye viwango, kuwaandaa walimu na kuwalipa vizuri ili wafanye kazi nzuri ya kutoa Elimu. Wananchi wakipata elimu nzuri, wanaweza wenyewe kutumia elimu hiyo kuyaboresha maisha yao. Kazi ya serikali ni kujenga mifumo mizuri ya kujenga maadili ya kitaifa. Hakuna taifa linaloweza kusonga mbele bila kuwa na maadili ya kitaifa. Bila kuwa na miiko ya viongozi, bila kuwa na miiko ya wafanyakazi, bila kuwa na miiko ya familia, kuwa na miiko ya vijana nk. Kazi ya serikali ni kuhakikisha wananchi wana afya bora. Ni lazima serikali kujenga hospitali nzuri na zenye huduma ya kisasa. Kuhakikisha hospitali zina dawa na zina madaktari wenye viwango, kuwalipa madaktari vizuri na kuhakikisha wana vifaa vizuri na vya kisasa vya kutoa huduma nzuri kwa wananchi. Kazi ya serikali ni kutengeneza miundombinu ya barabara. Kuhakikisha barabara zote ni nzuri na zinapitika wakati wote . Wanachi wanaweza kusafirisha mazao yao kutoka shambani hadi kwenye masoko. Kazi ya serikali ni kutengeneza pia miundombinu ya maji na kuhakikisha wananchi wote wana maji safi na salama. Ziko huduma nyingine nyingi za kijamii ambazo ni kazi za serikali. Na kazi hizi zinaendeshwa kwa pato litokanalo na jasho la wanachi. Serikali ikiyaweka hayo niliyoyataja pembeni na kujiingiza kwenye mchakato wa kuwatafutia wanasiasa kazi; kuanzisha wilaya nyingi, kuanzisha mikoa mingi na kuanzisha majimbo ya uchaguzi mengi, kutengeneza bodi nyingi na kuwachagua wanasiasa kuwa wenyeviti na wajumbe wa bodi hizo, kuwa na baraza kubwa la mawaziri na kuhakikisha kila wizara ina naibu waziri, makatibu wakuu na manaibu wao, wakurugenzi na manaibu wao, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa wilaya nk ni lazima serikali hiyo iwe kandamizi. Itatoza ushuru mkubwa na kuwakamua wananchi ili kupata mishahara ya wanasiasa na kuendesha shughuli nyingine ambazo hazina ustawi wa wananchi. Ni kuwa na serikali kubwa inayomeza bila kuzalisha! Tuna baraza kubwa la Mawaziri, kwasababu serikali inawatafutia wanasia kazi. Baraza hili la mawazi ni kubwa na ni mzigo mkubwa kwa walipakodi wa Tanzania. Tuna Bunge kubwa, ambalo nalo ni mzigo mkubwa kwa walipakodi wa Tanzania. Na tumefanya makosa makubwa kutengeneza mazingira yanayoufanya ubunge kuwa ajira. Hii imefuta dhana nzima ya uwakilishi. Ndo maana utakuta mtu anayeishi Dar-es-salaam, anapambana awe mwakilishi wa watu Magu – Mwanza. Kwa vile ni ajira yenye kipato kikubwa, mtu anaweza kuwa Dar-es-salaam na kuwakilisha mawazo na hoja za watu wa Magu! Tunawasikia wabunge wakijigamba wakati wa kampeni za uchaguzi kwamba wataleta maendeleo. Kwamba watajenga barabara, kwamba wataleta maji, kwamba wataleta umeme, kwamba watajenga shule, kwamba watajenga hospitali nk. Mbunge si serikali na Mbunge hana uwezo wa kufanya kazi hizo. Mbunge akifanya kazi ya kuleta maendeleo, kwaa maana ya yeye mwenyewe kuleta maendeleo ni lazima awe mwizi au fisadi! Maendeleo yanaletwa na watu wenyewe wakitengenezewa mazingira mazuri na serikali yao. Kazi ya mbunge ni kuwakilisha mawazo ya wananchi kwenye Bunge. Mfano hoja hii kwamba serikali imejiingiza kwenye kazi zisizokuwa zake za kuwatafutia wanasiasa kazi, ingefikishwa bungeni na Mbunge wangu mimi: Ikajadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi. Nisingelazimika kuandika makala hii, nafanya hivyo kwa vile hakuna nafasi ya kukutana na Mbunge wangu; wabunge wetu wako kwenye ajira ya kupata mshahara na posho, hawako tena kwenye kazi ya uwakilishi. Mbunge anayewawakilisha watu wake hawezi kuiogopa serikali au chama chake cha siasa wakati wa kuchangia hoja ndani ya Bunge: Ni lazima awe huru maana daima hatoi mawazo yake bali ya wapiga kura wake. Mbunge anayewawakilisha wananchi hawezi kushangilia kila kitu kinacholetwa na serikali na kuunga mkono kila kitu hata wakati mwingine mambo ya ovyo na mengine ya hatari kwa watu wake kama vile bei ndogo ya mazao na kupanda bei kwa vitu muhimu kama vile mafuta ya taa. Tumekosea kukubali kuigeuza siasa kuwa ajira, tumekosea kukubali serikali kujiingiza kwenye mambo mengine yasiyokuwa na ustawi wa taifa letu, kama vile kuwatafutia wanasiasa ajira. Kosa hili bila kulisahihisha hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo. Tunashuhudia jinsi wanasiasa wetu baada ya uchaguzi mkuu wanavyo tumia nguvu, fedha na muda wao mwingi kujiandalia uchaguzi ujao.Miaka mitano wanaitumia kutafuta fedha na kujiandalia uchaguzi unaofuata. Kwa vile siasa ni ajira ,basi wanasia wanataka kuhakisha wanalinda ajira yao kwa gharama yoyote ile. Maendeleo ya taifa yanawekwa kando na kushughulikia maendeleo ya mtu mmoja mmoja anayefanikiwa kupenyeza kwenye uwanja wa siasa. Vyovyote vile, tumekosea, ni lazima tujisahihishe. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 633122 www.karugendo.net
KWANINI MADAKTARI WASIPATE MSHAHARA WA MILIONI 3? Nimezoea kuzisikiliza hotuba za Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, anazozitoa kila mwisho wa mwezi.Ni utamaduni mzuri ambao unaweza kuboreshwa kwa kuruhusu maswali ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Rais. Maana Rais, ni kiongozi wa nchi, fursa hii ya kuongea na kujadiliana na wananchi inaweza kuchangia ufanisi wa uongozi wake. Mfumo wa sasa wa kutoa hotuba bila maswali kutoka kwa wananchi, unaibua mambo mengi ambayo wakati mwingine Mheshimiwa Rais anakuwa amepotoshwa; kama maswali yangeruhusiwa, labda ufafanuzi zaidi ungefanyika kwa faida ya pande zote mbili. Hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Juni mwaka huu, ilijikita kwa kiwango kikubwa juu ya sakata la madaktari. Rais, alisisitiza kwamba serikali haina uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara wa milioni tatu wanapoanza kazi. Sina lengo la kubishana na Mheshimiwa Rais, bali ni kuuliza ili kufahamu, pia ni kutaka kuonyesha kwamba kama tungekuwa tunauliza maswali,utata wa mambo mengi ungekuwa unapungua. Swali langu ni: Kwanini madaktari wasipate mshahara wa milimioni 3? Ina maana milioni 3, ni nyingi ukilinganisha na kazi wazifanyazo madaktari? Wanakesha wakihudumia wagonjwa, daktari mmoja anahudumia wagonjwa wengi ukilinganisha na nchi nyingine; hawafanyi kazi kwa kufuata saa, kila wakati wako kazini. Ina maana hakuna watanzania wengine wanaopata mshahara wa milioni 3? Ina maana serikali haina fedha za kulipa mshahara huo? Ina maana serikali yetu inaishi na kutenda kwa kuonyesha dunia nzima kwamba haina uwezo wa kulipa mshahara wa milioni 3? Kama serikali ina uwezo wa kununua magari ya milioni 300, na si gari moja – magari mengi! Itaweza kushindwa kulipa mshahara wa milioni 3? Serikali ina uwezo wa kununua ndege ya rais na kuitunza, itashindwa kulipa mshahara wa milioni 3? Serikali inaweza kufanya sherehe za Uhuru (Miaka50) kwa kutumia mabilioni ya fedha; na kusimama kusema haina uwezo wa kulipa mshahara wa milioni 3? Kuna mambo ambayo watu wa nchi za nje wakiyasikia watatushangaa. Wanakuja hapa tunawapokea kwa mabenzi ya gharama kubwa, alafu wasikie tunasema hatuna uwezo wa kulipa mishahara? Wanashuhudia tunavyowapeleka viongozi wetu kutibiwa nchi za nje na kulipia matibabu hayo kwa fedha nyingi. Nimeona fedha iliyotengwa kwa matibu ya Marais wetu wastaafu, bajeti hiyo si ya nchi masikini kama tunavyotaka watu waamini, haionyeshi unyonge wetu wa kushindwa kumlipa daktari mshahara wa milioni 3. Sitaki kugusia dhahabu, Almasi, Utalii na utajiri mwingine mkubwa unaojionyesha wazi kwa matumizi ya viongozi wetu. Viongozi wetu wanasafiri daraja la kwanza kwenye ndege na kulala kwenye hoteli za daraja la kwanza wanapokwenda nje ya nchi. Dunia nzima inajua na pia sisi tunajua kwamba Tanzania si nchi masikini, viongozi wetu hawaonyeshi umasikini huo.Tukisikika tunaongea lugha ya kinyonge na kimasikini wanatushangaa na kuhoji uadilifu wetu wa mawazo na kujieleza. Hoja yangu ni kwamba, mtu anayetoa hoja ya kinyonge, hoja ya umasikini ni lazima awe mnyonge pia, ni lazima naye awe anaishi maisha hayo ya umasikini. Kinyume na hapo ni kujichanganya na kuwachanganya wengine kiasi cha kujiuliza kama tuna fikra pevu au tunaishi kwa vile tumeumbwa na kujikuta duniani? Naogopa kutumia maneno makali ya kutukana. Hatupendi kuambiwa ukweli kwa kisingizio cha kutukanwa. Naogopa yasinikute ya John Mnyika ya kutolewa nje ya Bunge. Kabla ya kutoa hoja yangu, niweke mambo sawa: Si kweli kwamba madaktari waligoma kushinikiza kulipwa mshahara; hili ni kati ya mambo mengine mengi kama vile kuboresha huduma za afya na kupata vifaa bora na vya kisasa. Kutanguliza na kusisitiza hoja moja ya mshahara ni kutaka kuwachonganisha madaktari na wananchi, na hili ni kuwakosea haki. Lakini kwa vile Mheshimiwa Rais wetu amelisisitiza hili la mshahara na kusema kwamba daktari ambaye ataona bila kulipwa milioni tatu hawezi kufanya kazi, basi ajiondoe; kuna haja kulijadili hili. Hawa madaktari wanaandaliwa kwa miaka mingi na kwa fedha nyingi, fedha zinazotokana na jasho la wananchi. Kusema kirahisi kwamba wasipotaka mshahara wa kimasikini waondoke, ni kuwakosea haki wananchi na kuendelea kuwabebesha mzigo wa kuwaandaa madaktari wengine ambao labda nao kesho na keshokutwa watalazimishwa kuondoka. Naanza mjadala huu kwa swali: Kwanini madaktari wasipate mshahara wa milioni 3? Serikali yenye uwezo wa kuanzisha wilaya na mikoa mipya, inaweza kutoa hoja ya kutokuwa na uwezo wa kuwalipa madaktari milioni 3? Zinapoanzishwa Wilaya na mikoa mipya, mbali na fedha nyingi zinazohitajika kuandaa miundombinu; serikali inawaajiri wakuu wa wilaya wapya, wakuuu wa mikoa wapya: Hao ni pamoja na wakurugenzi, Katibu tawala, OCD, Mganga mkuu na wafanyakazi wote wa wilaya na mkoa. Hao wote wanahitaji magari, wanahitai nyumba za kuishi na fedha za kuendesha ofisi. Kama fedha hizo zinapatikana kwa nini mshahara wa madaktari usipatikane? Labda hapa suala ni vipaumbele. Tunaweza kujiuliza serikali yetu ina vipaumbele vipi? Kuanzisha wilaya na mikoa, au kuwalipa madaktari mshahara mzuri ili waweze kufanya kazi ya kuhudumia afya ya watanzania na kuokoa uhai? Tunahitaji watanzania wenye afya na nguvu za kufanya kazi, au tunahitaji wilaya nyingi na mikoa mingi? Kuanzisha wilaya na mikoa, bila kuwa na uhakika wa afya na uhai wa watanzania ni kupoteza tu fedha za wananchi. Serikali yenye uwezo wa kuliendesha baraza kubwa la mawaziri, haiwezi kutoa hoja ya kushindwa kuwalipa madaktari milioni 3. Sipendi kujua mawaziri hawa na manaibu wao wanapata mshahara kiasi gani; swali langu ni je wanafanya kazi? Maana kuna wizara ambazo mbali na kujibu maswali Bungeni, kazi za manaibu waziri hazijulikani! Manaibu waziri nao ni wengi, wana mishahara, wana magari, wanapewa nyumba za kuishi na posho nyinginezo. Serikali ambayo ina uwezo wa kuliendesha Bunge lenye wabunge zaidi ya miatatu, haiwezi kuleta hoja kwamba haina uwezo wa kuwalipa madaktari milioni tatu. Mishahara na posho za wabunge ni nyingi kulinganisha na kazi wanayoifanya.Tunashuhudima mara nyingi viti vikiwa wazi Bungeni; hata wale wanaokuwa waaminifu wa kubaki ukumbini wengine wanasinzia, wengine wanapiga michapo, wengine kazi yao ni kutupiana matusi. Wabunge wasiozidi ishirini ndo wanafanya kazi ipasavyo. Kwa maana hiyo, tunaweza kuwa na Bunge la wabunge ishirini na mabo yakaendelea. Kwa mfano tukiwa na mbunge mmoja kila mkoa, tunaweza kupunguza ukubwa wa Bunge na kuweza kuokoa fedha za kufanya mambo mengine kama vile kuongeza mshahara wa madaktari wetu. Kushughulikia huduma ya maji na kuboresha huma ya afya kwenye hospitali zetu. Serikali inayowaruhusu watu kuingia Benki kuu na kujichotea fedha na kuondoka bila kuwawajibishwa, haiwezi kuleta hoja kwamba haina uwezo wa kuwalipa madaktari milioni tatu. Serikali inayoshindwa kuwadhibiti wawekezaji, wanakuja, wanachota fedha na kuondoka, haiwezi kule hoja kwamba haina uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara wa shilingi milioni 3. Serikali inayoruhusu kuwepo na Mishahara hewa. Tunasikia mabilioni yamepotea kupitia mishahara hewa, na hakuna aliyekamatwa na kuwajibishwa; haiwezi kuleta hoja ya kushindwa kuwalipa madaktari milioni 3. Madaktari wanaishi Tanzania, wanashuhudia yote hayo. Hivyo wanapodai mshahara wa milioni 3, wanajua inawezekana. Wanawafahamu watu waliosoma nao, wanaofanya kazi kwenye maeneo mengine, wana mishahara mikubwa kuzidi hiyo ya milionni 3. Mfano mtu ambaye anakuwa kwenye msafara wa Mheshimiwa rais, ukizingatia safari nyingi za Rais wetu za kuomba misaada huku na kule, anakuwa na mshahara (posho) kiasi gani? Au mtu anayefanya kazi TRA, ana mshahara kiasi gani? Kama hawa wengine, ambao baadhi yao wanafanya kazi nusu nusu, wanalipwa vizuri, kwanini madaktari wetu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu na kuyaweka maisha yao hatarini wasilipwe milioni 3? Tukumbuke, daktari anashughulikia maisha ya watu. Hivyo ni lazima mawazo yake yawe yametulia wakati anafanya kazi na hasa kama anafanya upasuaji; kama kichwani mwake kuna mawazo ya ugumu wa maisha; kama anafikiri juu ya karo ya watoto, kama anafikiri juu ya pango la nyumba, kama anafikiri jinsi ya kupambana na abiria wengine kwenye dalala, kama anafikiria michango ya kijamii ambayo mtu huwezi kuikwepa labda kama unaishi peke yako mwezini, hawezi kuwa na utulivu unaohitajika kutekeleza kazi zake. Mshahara mzuri kama wanaoushikiniza kuupata, unaweza kusaidia kuwapunguzia madaktari wetu msongo wa mawazo na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kulinda uhai wetu. Mwanzo wa makala hii nilisema ni kuwakosea haki Madaktari, kwa kutuaminisha kwamba tatizo lao ni kulalamikia mshahara tu. Tumewasikia wakipiga kelele kwamba hospitali zetu hazina vifaa. Tumesikia serikali ikisema kwamba madaktari wakiendeleza mgomo, itawatafuta madaktari kutoka nje ya nchi na kuwaomba madaktari wastaafu kurudi kazini. Na hapo ndo tunajiuliza swali: Je hao madaktari kutoka nje ya nchi, watakuja kutalii ama kufanya kazi? Kama hospitali hazina vifaa bora na vya kisasa, madaktari hao wageni watakuja kufanya kazi vipi au watakuwa ni madaktari wa miujiza kama ule wa Loliondo? Au kwa vile watakuja madaktari wa kigeni, basi vifaa vitapatakana? Madaktari wetu wanalalamikia viongozi wa serikali kwenda kutibiwa nchi za nje. Hoja yao ni kwamba fedha zinazolipia matibabu yao kule nje, zingeweza kununulia vifaa bora na vya kisasa na watu wengi wangenufaika kwa kutumia vifaa hivyo. Hii ni hoja ya msingi; kuendelea kuwabeza madaktari wetu kwamba wanataka mshahara mkubwa na kuyatelekeza maisha ya watanzania ni kuwakosea haki. Wengine wanapendekeza kwamba madaktari washitakiwe kwa kusababisha vifo vivyolivyotokea wakati wa Mgomo. Hatuwezi kufanya hivyo kablda ya kuiomba serikali iliyo madarakani kuwajibika kwanza kwa uzembe mkubwa wa kulishughulikia suala zima la mgomo wa madaktari. Pendekezo langu ni kwamba serikali yetu ipange vipaumbele vyake kulingana umuhimu wa mambo na kuutanguliza Uhai. Hakuna taifa linawoze kuendelea bila kuwa na raia wenye afya bora. Hivyo badala ya kuanzisha Wilaya na Mikoa, serikali iboreshe kwanza Wilaya na mikoa iliyopo; wananchi wapate maji bora na salama, wananchi wapate barabara nzuri, shule nzuri na hospitali nzuri. Serikali ihakikishe wahudumu wake, wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri na salama. Madaktari wanaoshughulikia afya zetu, wapate mshahara mzuri na kuishi maisha bora na salama. Mwalimu, alitufundisha kwamba Kupanga ni kuchagu. Tukipanga vizuri; na kuainisha vipaumbele vyetu, Madaktari wetu watapata mshahara wa milioni 3 na kuzidi. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 633122 pkarugendo@yahoo.com www.karugendo.net
VYOYOTE VILE, KUTEKWA NA KUTESWA KWA ULIMBOKA NI LAZIMA MTU AWAJIBISHWE. Hata kama tumetangaziwa kwamba aliyemteka na kumtesa Dakt Ulimboka, alitoka nje ya nchi, imetajwa Kenya, ina maana itawaponya baadhi ya watu hapa nchini kuwajibika kwa tukio hilo?;Vyovyote vile ni lazima mtu au watu wawajibishwe! Uzembe unajionyesha wazi wazi. Bila kuziba ufa huu, tutalazimishwa kujenga ukuta! Kama kikundi cha watu wabaya kutoka nje ya nchi wanaweza kuingia ndani ya nchi bila kutambuliwa na kutekeleza kazi yao na kuondoka bila ya kukamatwa, mpaka wao waamue kwenda kanisani kuungama; ulinzi wa taifa letu si uko mashakani?Zamu hii ametekwa Ulimboka, je kesho watu hawa wakiingia na mabomu na kuyatega sehemu mbali mbali si itakuwa hatari kwa taifa letu? Je polisi wanaotiliwa shaka kushiriki sakata zima la kumteka na kumtesa Ulimboka, wataweza kukwepa kuwajibika kwa vile muhusika mkuu amejitokeza? Kwa maelezo ya Kamanda Kova, si kwamba mtu huyu (Aliyemteka na kumtesa Ulimboka) amekamatwa na Polisi, bali mtu mwenyewe alikwenda kanisani kuungama na “Mchungaji” akafanya kazi ya usalama wa taifa. Hadi hapo Polisi, hawawezi kukwepa kuwajibika! Wanashindwa kufanya kazi yao ya upelelezi hadi wasaidiwe na “Mchungaji”? Ni bahati mbaya kwamba Kamanda Kova, hakutaja kanisa ambalo mtu huyo alikwenda kuungama. Tungependa kulijua kanisa hilo na mchungaji huyo. Tujuavyo sisi ni kwamba maungamo ni “siri” kati ya anayeungama na anayeungamisha. Na kamwe, hata kama ni chini ya tishio la kupoteza maisha, Mchungaji au padre, anakatazwa kutoa siri ya maungamo.Kutoa siri ya maungamo ni dhambi ya mauti na haina msamaha popote labda kwa Mungu Mwenyewe. “Usiri” huu wa muungamo ndo uliwajengea watu imani ya kuendelea kukumbatia mfumo huu wa kutubu dhambi. Mtu anataja dhambi zake, anasafishwa na kuendelea na maisha. Nje ya imani, huu ni mfumo mbaya kabisa; mtu anaweza kuendelea kutenda dhambi na kuwanyanyasa wengine kwa vile anajua kuna mtu “Mchungaji” wa kusafisha dhambi zake. Ni mfumo wa mtu kuufungua mdomo wake (Kusema yote machafu) na kuufunga mdomgo wa “Mchungaji”. Kama wachungaji na mapadri wangejenga utamaduni wa kuzitangaza siri za maungamo, basi mfumo huu ungekufa zamani sana. Sasa huyu “mchungaji” aliyeamua kutoa siri za maungamo, na kuamua kufanya kazi na polisi ni nani? Huyu amesoma chuo gani cha Teolojia? Au ni uchungaji wa kujipachika? Mchungaji mchana na usiku ni Polisi? Sijasema alichokifanya ni kibaya kwa taifa letu; sijasema amekosea kushiriki kazi ya ulinzi na usalama wa taifa letu;sijasema amekosea kumfichua huyu mtu aliyetenda unyama wa kumteka na kumtesa Dakt Ulimboka; sote tumechukia na kuguswa na tukio hili na tungependa kumfahamu aliyetenda hivi na ni kwa nini? hoja hapa ni namna mchungaji huyu alivyoshiriki. Mchungaji huyu anataka tuamini kwamba makanisa ni usalama wa taifa? Kwamba makanisa yanafanya kazi na serikali? Waislamu wamekuwa wakipiga kelele nyingi kwamba Serikali inapendelea wakristu na kwamba makanisa yamekuwa yakifanya kazi kwa karibu sana na serikali ya Tanzania. Tumekuwa tukilipinga jambo hili kwa nguvu zote, lakini sasa baada ya Kamanda Kova, kutangaza kwamba mtu aliyemteka na kumtesa Dakt Ulimboka, ameibukia kanisani kwa njia ya maungamo, ni lazima tushawishike kwamba madai ya waisalamu yana ukweli Fulani? Je, Mchungaji huyu ametoa hili la Ulimboka tu, au anatoa mengine? Ushawishi huu wa kanisa kufanya kazi kwa karibu na polisi, unaishia hapo au unaendelea? Je “Mchungaji” huyu anashirikiana na polisi tu au ushawishi wake unaendelea kwenye idara nyingine za serikali? Tuna haki ya kujua, maana kama Kamanda Kova, ameamua kulifichua hili ni lazima aliweke wazi! Vinginevyo ni kuleta vurugu na kuvuruga amani ya watanzania. Inawezekana kabisa kwa kutaka kujikosha, Polisi wanatuingiza kwenye matatizo mengine makubwa: Tutaanza kuhoji umakini wa polisi wetu, tutaanza kuhoji kwa nguvu zote uhusiano wa serikali na Kanisa na wenye imani zao wataanza kuhoji uadilifu wa wachungaji na mapadri juu ya siri za kitubio. Lakini pia kuna hili tatizo kubwa la kufunika mambo ambayo kesho na keshokutwa yatafumuka na kuliingiza taifa kwenye majanga makubwa. Kwa kumkamata mtuhumiwa huyo kutoka Kenya, na kama alivyoeleza Kamanda Kova kwamba atafunguliwa kesi; suala la Ulimboka, litakuwa halijadiliwi tena, tutaambiwa kwamba liko mahakamani. Utamaduni wa mahakama zetu, kesi inaweza kwenda zaidi ya miaka mitatu; suala kama hili la Ulimboka, ambalo limegusa hisia za watu wengi na zaidi vijana wa nchi hii, kulifunika na kuzuia mjadala kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani ni kuchokoza mzinga wa nyuki. Na kuna tatizo jingine la kuleta mahusiano mabaya kati ya nchi na nchi. Tunaweza kuanza kuinyoshea Kenya kidole kwa kutuingizia makundi ya majambazi ya kuwateka na kuwatesa. Hata Kenya, wanaweza kuja juu kwa kuitumia nchi yao kuficha madhambi ya baadhi ya watu wetu. Utamaduni huu wa kuitumia Mahakama kama kinga ya maovu, umeanza hivi karibuni nchi yetu ilipodumbukia kwenye dimbwi la mambo ya ovyo kama vile ufisadi na uporaji wa rasilimali za taifa. Hadi sasa mambo mengi yamefunikwa kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani. Serikali inaposhikwa pabaya inakimbilia mahakamani. Suala likishafikishwa mahakamani, halijadiliwi tena Bungeni, kwenye jamii na kwenye vyombo vya habari. Njia pekee ya kuwanyamazisha watu, njia pekee ya kuwazuia watu kutetea haki zao za msingi ni kukimbilia mahakamani. Ile dhana nzima ya Mahakama kama chombo cha kutetea na kutoa haki sawa kwa kila mwananchi imeanza kupotea. Kinachojitokeza ni Mahakama kugeuka kuwa chombo kandamizi na kulinda maslahi ya wakubwa,serikali na watu wenye fedha. Mbali na kutumia maungamo kumfichua mtu aliyemteka na kumtesa Dakt Ulimboka, na mpango mzima wa kutaka kuitumia mahakama kuzuia mjadala juu ya sakata hili, kuna jambo jingine la kushangaza: Katika hali ya kawaida, tulitegemea mtu aliyetoka nje ya nchi kuja kutekeleza kazi “Mauaji”, angetoroka na kurudi nchini kwao mara baada ya kumaliza kazi yake. Sasa huyu “Mtu wa Ulimboka”, baada ya kazi yake, ambayo aliifanya na kuimaliza bila kukamatwa, akaendelea kuishi Tanzania, bila wasi wasi wowote na bila Polisi kutambua, mpaka Roho wa Bwana alipomwingia akaamua kwenda Kanisani kwa mchungaji kuungama? Na je aliungama kwa lengo la kusafishwa dhambi zake ili aendelee kutenda dhambi nyingine? Ili aendelee kuwateka na kuwatesa watu wengine? Au aliungama kwa kuchukia dhambi aliyoifanya? Na kama ni hivyo si angejisalimisha moja kwa moja kwa polisi na kwa kufuata mantiki, angejisalimisha nyumbani kwao Kenya. Kilio cha madaktari na watetezi wa haki za binadamu ni kwamba suala la Kutekwa na kuteswa kwa Dakt Ulimboka liundiwe tume huru. Tume ambayo badala ya kukimbilia kanisani na nje ya nchi na mahakani itachunguza kiini cha tukio lenyewe hapa hapa nchini. Kwa vile suala hili linaelekea kuwagusa watu wengi na kuibua dalili za kutoaminiana na kulituhumu moja kwa moja Jeshi la Polisi, hekima pekee ni kuliundia tume huru. Vinginevyo tutaendelea kusikikia “hadithi” ambazo hazitatusaidia kuleta maelewano. Vyovyote vile kwa suala la Kutekwa na kuteswa kwa Dakt Ulimboka, ni lazima mtu awajibishwe, vinginevyo ni kuendelea kuwalazimisha watu kujichukulia sheria mkononi! Na, Padri Privatus Karugendo.
KUWAFUTIA LESENI MADAKTARI NI KUWAONEA! Sikupenda kuandika makala hii. Nimepambana sana na nafsi yangu; nimesali na kutafakari, nimeandika zaidi ya mara tano na kufuta; lakini nimefika mahali nikasema liwalo na liwe kama tunavyofundishwa na viongozi wetu! Si kwa maana ya kukata tamaa bali nimekuwa na moyo mkuu! Nilitaka haya nitakayoaandika kwenye makala hii, niyaongee ana kwa ana na wahusika. Bahati mbaya hakuna jukwaa lolote la kukutana nao; ofisini kwao utahitaji siku nyingi kuwapata kama si mwaka mzima. Watu muhimu wanaofanya kazi za kulijenga taifa hawapatikani hivi hivi; simu zao zinazimwa au hazipokelewi? Na wakati mwingine hawana hata muda wa kusoma barua pepe, ingawa wakati mwingine tunawaona wako kwenye mambo yasiyokuwa ya kujenga taifa na wala kuwa na muhimu kwa wananchi wa Tanzania. Nimeamua kuandika kwa kuiogopa historia. Kesho na keshokutwa tunaweza kuwekwa sote kwenye kapu moja. Kutakuwa na maswali mengi nyuma yetu: Walikuwa watu wa namna gani? Walikuwa na akili timamu? Walikuwa wanaipenda nchi yao? Waliishi kwa vile walijikuta hapa duniani au waliishi kwa kutafiti na kutafakari kuwepo kwao hapa duniani? Kwa vile nina imani kwamba kilichoandikwa kimeandikwa. Vizazi vijavyo, watasoma na kutuweka kwenye makundi tofauti. Ujumbe wangu ni mfupi: Kuwafutia leseni madaktari waliogoma na kuwafikisha mahakani ni kuwaonea. Najua, kugoma kwao kumesababisha matatizo makubwa na watu wamepoteza uhai; hata hivyo kwa kulinganisha hawajaleta hasara kubwa kama iliyoletwa na “Vigogo” ambao hadi leo hii wanatembea vifua mbele na kuyafurahi maisha wakati mamilioni ya watanzania wanaogolea kwenye umasikini unaonuka. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama si kuogopa kuchokoza nyuki; nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama si kusoma alama za nyakati. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama si kutamani kuacha nyuma yangu Tanzania yenye amani na utulivu. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama mafisadi na wahujumu uchumi wote wangekamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama viongozi wetu wangekuwa wanalazwa na kutibiwa kwenye hospitali zetu za serikali. Kuna watu wengi hapa Tanzania wanaonewa, wananyanyaswa, wanateswa, wanabambikizwa kesi, tunawaona na wala hatusemi chochote na maisha yanaendelea. Hivyo kuonewa si kitu kipya na wala si cha kushangaza. Tofauti ni moja, kuonewa kwa madaktari ni kufunika mambo bila kutoa jibu. Tunataka kusikia serikali ikikaa meza moja na madaktari na kujadiliana. Tunataka tusikie serikali ikiongeza mshahara wa madaktari, fedha zipo na serikali ina uwezo huo, tunataka kusikia serikali ikiboresha huduma za Afya, fedha zipo na serikali ina uwezo huo. Serikali kuacha kufanya hayo niliyoyataja na kukimbilia kuwafutia leseni madaktari na kuwaburuza mahakani ni kwenda kinyume, tatizo linabaki pale pale na kesho ni lazima tatizo hili litaribuka. Na wakati ukiwadia, sote tutajuta isipokuwa wachache wanaojua pa kukimbilia. Kwa vile walio wengi hawajui pa kukimbilia ni lazima kusema bila ya kuogopa, ni lazima kusema bila kufuata itifaki yoyote ile. Ni bora kulaumiwa na kupuuzwa kwa kusema ukweli kuliko kukaa kimya hadi taifa likajikuta njia panda: Hivyo hoja kubwa katika makala hii ni: Kuwafuita leseni madaktari waliogoma na kuwafikisha mahakamani ni kuwaonea, ni unyanyasaji na ni kukiuka haki za msingi za mwandamu. Ni lazima ukatili huu kusimama mara moja! Ni kweli madaktari walifanya makosa kugoma na serikali ilifanya makosa kushindwa kushughulikia mgomo huo kwa haraka, kwa busara na kwa moyo wa kizalendo. Kama Madaktari wanafutiwa leseni na kufikishwa mahakamani, ni lazima na serikali iwajibishwe kwa namna moja ama nyingine na ifikishwe mahakamani. Damu ya watu waliokufa wakati wa mgomo wa madaktari iko juu ya madaktari na serikali. Haiwezekani serikali kusimama pembeni, kwa vile ina madaraka, haina maana haiwezi kukosea. Kuna historia ya serikali nyingi duniani zilizokosea na kusababisha kuwajibishwa au kukataliwa na wananchi. Tunaweza kufika hapo, maana watanzania si malaika na tunaishi kwenye dunia ambayo imekuwa kijiji kimoja Ninajua inaelezeka. Serikali yetu inataka kutuonyesha inavyoweza kuchukua hatua kali kwa wakorofi. Serikali inataka tutambue kwamba haijalala usingizi, bali ipo kazini. Inataka tutambue kwamba serikali ni chombo chenye madarka na hakuna mwenye uwezo wa kupambana nayo. Na madaraka haya inayapata kikatiba! Hakuna la kubisha hapa. Labda mjinga peke yake ndiye anaweza kuchukua hatua za kutaka kupamba na serikali. Tunazijua na kuzitambua nguvu za dola: Ndo maana tumekuwa tukishangaa ni kwa nini Serikali inashindwa kuwashughulikia wakorofi ambao wameliingiza taifa letu kwenye umasikini? Kwa nini serikali yenye madaraka na nguvu zote hizo imekuwa kimya kuwawajibisha wezi walioingia kwenye Benki yetu kuu na kujichotea fedha? Kwa nini serikali yenye nguvu zote hizo imeshindwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wezi wa Richmond na Rada? Wanajulikana kwa majina na sura zao, lakini wako huru na kuendelea kufurahi maisha na familiazao. Tumesikia kwamba kwa upande wa Uingereza, wezi wao walikubaliana kutowashitaki? Je sisi Tanzania tunakubali kutowashitaki wezi wa Rada, wezi wa fedha hizo zote ambazo zingeweza kuyaokoa maisha ya watanzaia wengi na badala yake tunafutia leseni madaktari na kuwafikisha mahakamani kwa kosa la kudai haki zao za msingi? Ni kuwaonea vijana wetu ambao hasira yao hatutaweza kuizima! Serikali hii yenye madaraka makubwa, inaongozwa na CCM. Chama hiki tawala kilitwambia kwamba kina mpango wa kujivua magamba. Tulitajiwa hadi na majina ya magamba hayo na kwamba watahakikisha watu hao wanafukuzwa kwenye chama. Hadi leo hii hakuna kilichotokea. Wale wote waliotajwa kama magamba bado tunawaona kwenye chama chao. Wameshindwa kuwafukuza, wameshindwa kuwawajibisha! Maana yake ni nini? Wamewaogopa? Mbona hizo nguvu zinazotumika kuwafutia madaktari leseni na kuwafukuza kazi hazitumiki kuwashughulika “Magamba”? Ina maana nguvu za serikali zinatumika kwa wanyonge? Nguvu za serikali zinatumika kwa vijana wadogo wanaoanza kazi? Nguvu za serikali zinatumika kwa walalahoi? Ina maana hawa madaktari hawaoni ukweli huu? Watakubali kufutiwa leseni, watakubali kufuzwa kazi, maana hawana nguvu za kupamba na serikali katika njia za kawaida ambazo zote zinaipendelea na kuibeba serikali, lakini kamwe hawezi kukaa kimya. Wakishindwa kupata jukwaa ni lazima wataingia barabarani au watajibu kwa hasira zao zote kwenye sanduku la kura. Uchaguzi mkuu hauko mbali, madaktari zaidi ya 300 ni wengi kiasi cha kueneza sumu na kuhakikisha chama tawala kinapata haki yake ya kuwekwa pembeni. Na huu wala si utabiri au uchochezi ni kusoma tu alama za nyakati. Sina ulazima wa kutoa mifano hapa. Sote tunajua jinsi vijana wakibanwa na kunyimwa jukwaa la kujieleza na kutoa kero zao, vijana wasipopata kazi na kupata mtaji wa kuanzisha biashara ili kuweza kuendesha maisha yao wanavyofanya uamuzi wa kutumia njia nyingine ambazo si nzuri. Tumeshuhudia Tunisia na Misri. Tumeshuhudia jinsi watoto wadoto wa Afrika ya kusini walivyokuwa tayari kusimama mbele ya risasi na silaha nzito za makaburu kutetea haki zao. Wengi walipoteza maisha yao, lakini hatimaye waliobaki nyumba wanafurahia matunda ya damu ya vijana wenzao iliyomwangika. Mtu yeyote asiyeona ukweli huu ninashindwa neno la kutumia, maana hata “Mjinga” bado ni neno la heshima kwa mtu wa aina hiyo. Tumeshuhudia wanyama wakitoroshwa mchana kweupe? Ardhi inaporwa na kuuzwa kwa wawekezaji wan je, mikataba mibovu ya madini na uwekezaji hewa ambao wawekezaji wamekuwa wakibadili majina ya biashara zao kila baada ya miaka mitano: Mahoteli makubwa yamekuwa yakibadilisha majina, makampuni ya simu nayo yamekuwa yakibadilisha majina; wanachota fedha na kwenda zao. Serikali yenyen guvu zote hizo inashindwa kuchukua hatua? Hatujasikia mtu akiwajibishwa kwa kutorosha Twiga. Kama serikali yetu inaweza kuwawajibisha wakorofi kama madaktari waliogoma, kwa nini serikali hiyo hiyo ishindwe kuwawajibisha watu wanaohujumu uchumi wetu? Tumesikia kwamba daktari mmoja anahudumia watu elfu 30. Maana yake ni kwamba tuna uhaba wa madaktari. Mungu bariki Baba wa Taifa alianzisha Madaktari wasaidizi, ambao wanafanya kazi kwa ngazi ya daktari na ni wachapa kazi kweli ingawa mara nyingi wanasahaulika katika mchakato mzima wa kuongeza mishahara ya madaktari na huduma ya kupewa malazi. Kwa kifupi ni kwamba tuna uhapa mkubwa wa madaktari. Katika hali hiyo, serikali kufuta liseni na kuwasimamisha madaktari ni ujumbe wa wazi kwamba sasa wakati umefika wa kuiwajibishwa serikali yetu. Tumeambiwa kwamba madaktari wetu ni wazuri na wana ujuzi wa hali ya juu, lakini hawa vifaa; sote tunashuhudia jinsi taifa letu linavyotumia fedha nyingi kuwatuma watu kutibiwa nje ya nchi. Katika hali kama hii, madaktari wakidai kupewa vifaa; badalala yake wakafukuzwa, wakafutiwa leseni na kufikishwa mahakani ni ujumbe kwamba sasa wakati umefika wa kuiwajibisha serikali yetu. Kuwafutia leseni madaktari na kuwaburuza mahakani ni kuwaonea! Maana yake hawawezi kujadili tena juu ya suala hili la madai yao. Wataambiwa kesi iko mahakamani. Tumejenga utamaduni wa kuitumia mahakama kama chombo cha kuziba midomo ya watu na kupunguza uhuru wa watu kujadili mambo yanayogusa maisha yao. Serikali ikitaka kitu kisijadiliwe, inakimbilia mahakamani. Ikishafika huko, tunaambiwa kitu kilicho mahakami hakijadiliwi. Walipouawa wafanyabiashara wa Mahenge, watanzania walichukia sana na baadhi walitaka kuchukua sheria mkononi. Serikali ikawatuliza watanzania kwa kuwakamata “wahusika”. Kesi ikwafunguliwa mahakamani. Baada ya kese kufunguliwa mahakani, mjadala juu ya wafanya biashara wa Mahenge ukafungwa. Watanzania wakatulia. Kesi ikaendeshwa miaka, matokeo yake sote tunayajua. Ametekwa na kuteswa Dakt Ulimboka. Watanzania wamechukia kiasi cha kutaka kujichulia sheria mkononi. Mfano mzuri ni mtu yule aliyepata kipigo pale Muhimbili kwa kutuhumiwa kuwa mpelelezi. Serikali inajua kwamba watanzania wamechukia kwa kitendo cha kutekwa na kupigwa vibaya Dakt Ulimboka. Sasa Tunasikia amekamakwa mshukiwa wa kumtesa Ulimboka. Akifikishwa mahakani, ndo mwisho wa mjadala. Tutakatazwa kujadili juu ya sakata la Ulimboka. Kesi itaendeshwa miaka, na matokeo yake sote tunayajua. Kuna watanzania wengi wamelisabishia taifa letu hasara kubwa, lakini hawajachuliwa hatua yoyote ile, kuwaacha hao na kuwageukia vijana ambao ndio kwanza wanaanza maisha ni kuwaonea, ni kuwanyanyasa na kuwanyima haki yao ya msingi. Kama wamekosea, waonywe na kuelezwa makosa yao na si kuwafutia leseni na kuwaburuza mahakamani. Tanzania ni yetu sote, ni lazima tuilinde na kuhakikisha ni salama kwetu na kwa vizazi vijavyo. Ni muhimu! Na, Padri Privatus Karugendo. pkarugendo@yahoo.com www.karugendo.net +255754 633122
AJALI NYINGI TANZANIA NI UZEMBE WETU ! Ni masikitiko makubwa kuwapoteza watanzania zaidi ya miamoja kwa siku moja. Ajali ya Mv Skagit, Imetuletea majonzi makubwa. Miezi tisa baada ya meli nyingine kuzama kule Zanzibar na kupoteza maisha ya watu wengi, Mv Skagit nayo inaendeleza majonzi haya ya kuwapoteza watu wengi kwa siku moja. Ingawa sasa hivi si wakati muafaka wa kuonyesheana kidole na kumtafuta mchawi wa ajali hizi, itoshe tu kusema kwamba ajali nyingi hapa kwetu Tanzania zinatokana na uzembe wetu sote na hasa uzembe wa serikali yetu. Ajali za barabarani, ajali za majini na wakati mwingine ajali za moto ni uzembe wa serikali. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba Mv Bukoba wakati inazama kule ziwa Victoria na kuyapoteza maisha ya watu zaidi ya elfu moja, haikuwa na sifa kabisa za kusafirisha abiria. Ilikuwa na kasoro kubwa ambazo ilikuwa nazo tangia kutengenzwa kwake. Siku inazama ilipakia watu wengi na mzigo kuliko kiwango chake; serikali ikitizama tu! Hata baada ya tukio hilo la kizembe, serikali haikuwajibika wala kuwajibishwa. Baada ya ajali ya Mv Bukoba zimetokea ajali nyingine nyingi kwenye ziwa Victoria na hatujasikia mtu kuwajibika wala kuwajibishwa. Kibali cha vyombo kusafiri ndani ya ziwa kinatolewa na Serikali. Inakuwa je serikali kutoa vibali kwa vyombo chakavu na vyenye hitilafu kuendela kusafirisha abiria? Ajali za barabarani ambazo zinatokea kila kukicha nazo ni uzembe wa serikali. Chanzo cha ajali hizi ni magari chakavu, matairi yasiyokuwa na viwango na yamekuwa yakipasuka ovyo na kusababisha ajali, mwendo kasi, magari kujaza kupindukia na wakati mwingine madreva wasiokuwa na viwango. Yote hayo yako chini ya udhibiti wa serikali. Na wala hili halina ubishi au itikadi. Serikali ikizembea kusimamia ubora wa vyombo vya usafiri na ajali ikatokea, ni lazima serikali iwajibike au iwawajibishe wahusika wakuu. Kuna matuko mengi ya moto na mara nyingi tunasikia ni hitilafu ya umeme. Ukweli ni kwamba vifaa vingi vya umeme havina ubora unaohitajika kuunganisha umeme majumbani na kwa matumizi ya kila siku ya umeme. Usimamizi wa ubora wa vifaa vya umeme na bidhaa nyinginezo zinazoingizwa nchini ni wa serikali. Kama soko letu lina bidhaa bandia, si kosa la mtu mwingine bali ni kosa la serikali. Hivyo hitilafu ya umeme ikitokea, moto ukateketeza mali na kupoteza maisha ya watu ni lazima serikali iwajibike. Kuna ajali nyingine kubwa ambayo kama haijatokea leo, basi itatokea kesho. Kwa kuingiza bidhaa bandia na hasa vyakula na dawa kuna kipindi watu watakufa kwa magonjwa yanayotokana na vyakula hivi na dawa hizi bandia. Mafuta ya kupikia yanachakachuliwa na kuingizwa vitu vya hatari kwa afya ya binadamu; tunasikia watu wanachanganya mafuta ya kupikia na mafuta ya transfoma ili kukaangia viazi; tunasikia kwamba dawa za binadamu zinachakachuliwa; mafuta ya kujipaka na mafuta ya kutengeneza nywele yanatengenzwa kwa kemikali kali na hatari. Ajali hii ya kutokana na vyakula na dawa bandia ikitokea ni wazi utakuwa ni uzembe wetu na uzembe wa serikali yetu. Hoja hii kwamba ajali nyingi msingi wake ni uzembe wa serikai yetu haifuati itikadi; na wala hapa tusiingize suala la dini. Kuna watu wanakuwa na mawazo kwamba tunaisahihisha serikali kwa vile Rais ni Mwislamu. Mawazo haya ni ya kupuuzwa. Ilipozama Mv Bukoba,Rais alikuwa mkristu, napo tulisimama kidete kukosoa uzembe wa serikali iliyokuwa madarakani wakati ule. Si lazima kuwa Mkristu au mwislamu kuutambua au kutoutambua ukweli wa uzembee huu wa serikali yetu, si lazima mtu awe CCM kuutambua au kutoutambu ukweli huu wa uzembe wa serikali yetu, si lazima mtu awe CHADEMA kuutambua au kutoutambua ukweli huu wa uzembe wa serikali yetu. Mtu yeyote mwenye akili timamu ni lazima auone ukweli huu. Tumejenga utamaduni kwamba mtu yeyote anayeisahihisha serikali ni mpinzani na hasa mpinzani wa CHADEMA. Hata kama hoja ni muhimu na inaweza kusaidia kujenga na kuliendeleza taifa, kama ina harufu ya kusahihisha, basi ni upinzani na ni CHADEMA. Pia tunataka kuficha udhaifu wetu nyuma ya udini. Tuache kusema ukweli, tuache kukosoa kwa kuogoa kunyonyeshewa kidole na CCM au na waislamu? Tanzania ni nchi yetu sote, waislamu, wakristu, wanaoamini dini za jadi na vyama vyote vya siasa. Hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine. Ingawa si haki kuibebesha serikali lawama za ajali zote zinazotokea; Kimsingi serikali ndiyo ya kwanza kuwajibika yanapotokea majanga ambayo serikali ina uwezo mkubwa wa kuyakinga, lakini pia na sisi wananchi tuna mchango mkubwa kwa ajali hizi, na chanzo ni uzembe wetu. Kukubali kutumia vyombo vichakavu bila kuhoji ni uzembe wa hali ya juu. Kukubali kupanda meli au gari la abirira lililozaja kupindukia, ni uzembe mkubwa. Wananchi kukubali kuyapokea majanga yote yanayotokea kwa uzembe wa serikali bila kuhoji na bila hatua zozote za kuiwajibisha serikali ni uzembe wa hari ya juu. Kasumba tuliyolishwa na tunayoendelea kulishwa na wajanja wachache ni kwamba ajali ni mpango wa Mungu na kwamba ajali haina kinga! Eti mpango wa Mungu hauna makosa! Tununue vyombo vya usafiri vichakavu, tununue matairi bandia, tununue vifaa vya umeme bandia, ajali itokee tuseme ni Mpango wa Mungu? Ni kutumia vichwa kufikiri au kutumia vichwa kufuga nywele? Ni Mungu gani huyu mwenye mpango hasi wa kuwatesa viumbe vyake?Huyu ni Mungu wa Tanzania peke yake au ni Mungu yule yule anayeruhusu maendeleo ya sayansi na teknolojia yenye uwezo mkubwa wa kuzuia majanga na ajali zisizokuwa za lazima katika nchi nyingine? Nchi nyingine zikitokea ajali kama hii ya Mv Skagit, watu wanaokolewa kwa muda mfupi, sisi inatuchukua siku nzima hadi mbili kuelekea kwenye eneo la tukio. Je na huo ni mpango wa Mungu? Huo ndo mpango wa Mungu usiokuwa na makosa?Tunaandaa bajeti yenye fedha nyingi za posho na vitafunio, tunasahau kuandaa bajeti yenye fedha nyingi za kushughulikia maafa. Tunaandaa bajeti yenye fedha nyingi za kununulia magari na kushindwa kuandaa bajeti yenye fedha yingi za kutetea na kulinda uhai wa watanzania. Tumeambiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwamba kazi ya kichwa si kufuga nywele bali ni kufikiri. Ni kweli kazi ya kichwa ni kufikiri. Kupinga ukweli huu ni ushahidi wa wazi kwamba kichwa kinafuga nywele bila kufanya kazi yake ya mzingi ya kufikiri. Mtu asiyeweza kufikiri na si kufikiri tu bali kufikiri na kutafakari, kufikiri na kuchukua hatua, kufikiri na kuvumbua na kufikiri na kupambana na changamoto za maisha anakuwa si mtu na hana haki ya kuishi! Swali na kujiuliza ni je Utamaduni unaojengeka kwamba kila anayejaribu kuikosoa na kuisimamia serikali (Bunge) ni mpinzani au ni CHADEMA, ni utamaduni wa kichwa kufuga nywele au kufikiri? Kuzima hoja ya kujadili tukio la Mv Skagit Bungeni, ni kichwa kufuga nywele au kichwa kufikiri? Au kukataa ukweli kwamba kumwambia mtu anatumia kichwa kufuga nywele badala ya kutumia kichwa kufikiri ni tusi, ni kutumia kichwa kufikiri au kufuga nywele? Tanzania ni nchi tajiri na ndiyo maana mataifa makubwa yanataka kuja na kuwekeza. Utajiri wa Tanzania unajulikana dunia nzima. Mfano kuzungukwa na nchi zaidi ya tano zisizokuwa na bandari ni utajiri wa kupindukia. Uchumi wa Tanzania unaweza kuendeshwa na bandari tu kama tungekuwa na mipango mizuri. Kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba ni utajiri mkubwa, uchumi wa Tanzania unaweza kuendeshwa na kilimo peke yake kama tungekuwa na mipango mizuri. Kuwa na mbuga za wanyama ni utajiri kupita kiasi, maana kuna nchi duniani zinaendesha uchumi kwa utalii peke yake. Kuwa na madini mengi na kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini ni utajiri wa kutosha. Kusimama na kuitangazia dunia nzima kwamba Tanzania ni nchi masikini ni kutumia vichwa vyetu kufikiri au kutumia vichwa vyetu kufuga nywele? Bahati mabaya au nzuri msemo huu umeanzishwa na kiongozi serikalini; lengo lake likiwa kuwatusi na kuwakejeli wapinzani kumbe ni kinyume chake! Pamoja na ukweli kwamba MV Skagit, ilikuwa na mapungufu makubwa ya kuilazimisha kutoendelea kusafirisha abiria na wale walioiuza meli hiyo walibainisha mapungu hayo wazi bila kificho kuna mambo mengine juu ya meli hii yanayotia mashaka kama kweli tunatumia vichwa vyetu kufikiri au tunavitumia kufuga nywele: Mv Skagit, ilitengenezwa kubeba watu 250 bila mizigo, sisi tulikuwa tunaibebesha watu zaidi ya hao ni mzigo juu yake. Mv Skagit ilitengenezwa kusafiri kwenye mto, sisi tukainunua na kuilazimisha kusafiri baharini! Meli haikutengenezwa kupambana na mawimbi ya baharini. Hivyo aliyekwenda kuinunua meli hii ni lazima angeyajua yote haya na kuacha utamaduni wetu wa kushabikia vitu chakavu bila kupima vitu hivi vitafany akazi kwenye mazingira gani. Mjadala wa Tanzania kuendele kununua vitu chakavu uliungwa mkono na wabunge wengi wa CCM, tena kwa ushabiki wao uliunga mkono hoja hii kwa kuonyesha jinsi wanavyotumia vichwa vyao kufikiri na si kufuga nywele. Yakitokea maafa ya kutokana na vyombo chakavu, wabunge wetu hatuwasikii tena. Hatusikii wakikemea na kusema wale wote waliosababisha uzembe huu “wanyongwe”. Sauti zao zinasikika kwa kuwalaumu madaktari waliogoma kwamba wanasababisha vifo vya watanzania na kwa kosa hilo madaktari “Wanyongwe” au wafukuzwe kazi. Hatuwezi kukataa kwamba mgomo wa madakrati ulisabisha vifo, tukio ambalo si la madaktari peke yao bali na serikali pia, ila ukilinganisha vifo vinavyosababishwa na ajali za kizembe, huwezi kuwahukumu madaktari “Kunyongwa” kabla ya hukumu ya watu wote wanaongiza bidhaa bandia, watu wote wanaosababisha ajali zinazopoteza maisha ya watu wengi kama hili ya Mv Skagit. Kama tunaweza kuwa wakali kwa madaktari wetu, kwa nini tusiwe wakali kwa serikai yetu ambayo inaendelea kukumbatia vitendo vya kizembe nak uendelea kusababisha vifo vya watu wengi? Tusitafute visingizio na hakuna mchawi! Ajali hapa kwetu zinasabaishwa na uzembe wetu na kwa kiasi kikubwa ni uzembe wa serikai yetu. Tujifunze kuwajibika na kuwajibishana ndipo tutalinda uhai wetu wa kulilinda taifa letu la Tanzania. Na, Padri Privatus Karugendo. www.karugendo.net pkarugendo@yaoo.com +255 754 633122
JE! SASA NA HILI LIMEPITA? Niungame wazi kwamba nilipoandika makala yangu ya wiki iliyopita yenye kichwa cha habari “MTAMBO WA KUINGILIA MAWASILIANO YA SIMU: CHADEMA WANGEFANYA SUBIRA!”, sikujadiliana na mtu yeyote na nilikuwa sijapata habari zaidi juu ya suala hili zaidi ya yale niliyoyaona na kuyasikia kwenye taarifa ya habari. Hivyo na mimi sikuwa na subira nikafanya haraka kuwanyonyeshea CHADEMA kidole lakini kwa nia njema. Hoja yangu ya msingi ilikuwa ni kumkamata mtu huyo kwanza ndipo atangazwe. Nilikuwa naona ugumu wa kumwajibisha mtu huyo bila kuwa na ushahidi wa kutosha na hasa kumkatamata akiwa kazini. Pia nilihofu uwezekano wa mtu huyu kuficha mitambo yake mara baada ya kutambua kwamba njama zake zimegundulika. Kwa mtazamo wangu, nilifikiri mtu wa aina hii ni lazima ashughulikiwe na kujua malengo lake na kujua anatumwa na nani? Anatumwa na baba yake? Anatumwa na kikundi cha matajiri Fulani au anafanya kazi peke yake kwa manufaa yake mwenyewe? Je mtambo huo wa kuingilia mawasiliano ya watu ni kati ya mbinu za kugombea madaraka 2015? Nilifikiri maswali kama haya, ambayo ni muhimu kwa kila mtanzania yangejibiwa baada ya kumkamata “Jasusi” huyu. Leo, ninapoandika makala hii, tayari nimeongea na watu mbali mbali na kupata undani wa suala hili kwa mapana na marefu yake. Kumbe CHADEMA walichokifanya ni sahihi kabisa. Wangechelewa kufichua njama hizi za kijasusi, hali ingekuwa mbaya na baadhi ya wanachama wa CHADEMA wangefikishwa mahakamani na labda kufungwa kwa kosa la kutishia maisha ya mtu kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno. Kwenye utamaduni wetu uliojengeka wa kuitumia Mahakama kama kufunika maovu yote na kuwanyamazisha watu; kama wabunge wa Chadema wangekamatwa na kufikishwa mahakamani, mpango mzima wa kijasusi ungefanikiwa. Kesi ingeendelea miaka; Bungeni hakuna mtu angeruhusiwa kujadili; kwenye vyombo vya habari tungefungwa midomo maana kesi ingekuwa mahakamani; kuandika juu yake ni kuingilia uhuru wa mahakama. Pia tumesikia Bungeni ikitajwa wazi na kambi ya upinzani kwamba kuna mtambo wa kuingilia mawasiliano ya simu na hasa ujumbe mfupi wa maneno.Hadi leo hatujasikia serikali ikikanusha jambo hili, hivyo inawezekana kuna ukweli? CHADEMA, waliitisha vyombo vya habari na kusema wazi wazi kwamba kuna mtoto wa Kigogo, ameingiza mtambo kutoka Israeli, na kwamba mtambo huo ndo ulizalisha ujumbe mfupi wa vitisho aliotumiwa Kada wa CCM. Hadi leo hii hatujsikia serikali ama CCM wakikanusha jambo hili la mtambo wa kuingilia mawasiliano. Tunawafahamu CCM na serikali ya CCM walivyo wepesi wa kukanusha; kwa hili wamekaa kimya. Siwezi kusema wamedharau, maana huo si utamaduni wao. Ingawa kwa tukio la sasa mtambo huu umewalenga CHADEMA, inawezekana kesho na keshokutwa ukawalenga CCM wenyewe. Sasa hivi ndani ya CCM kuna kambi mbili kubwa. Kuna kambi ya Lowassa na kambi ya Membe. Kama mtoto huyu wa kigogo anayesemekana kuingiza mtambo huo yuko kambi ya Membe, basi na kambi ya Lowassa, haitakuwa salama. Na kama mtoto huyo wa kigogo yuko upande wa Lowassa, basi kambi ya Membe, haitakuwa salama. Vyovyote vile mtambo huu na mtoto huyu wa kigogo ni adui wa Umma. Huyu ataivuruga Tanzania, sitaki kuamini kwamba mtu huyu ana nguvu kuliko watanzania wote. Inawezekana ana nguvu ya fedha, lakini hawezi kuwa na nguvu ya umma. Swali ninalojiuliza kwenye makala hili ni Je, sasa na hili limepita? Hakuna wa kuwajibishwa? Hakuna wa kuhojiwa? Hakuna wa kushitakiwa? Tunaanzazisha utamaduni wa kuwa na Miungu watu? Watu wanaoweza kufanya lolote, wakati wowote na wasiguswe wala kuwajibishwa kwa vile ni watoto wa vigogo au ni vigogo wenyewe?Tunaendelea kulea azembe na kuendekeza matukio yasiyokuwa na tija kwa taifa letu? Hapa Tanzania tuna mambo mengi yanayoibuka na kuzimika bila jibu lolote na bila mbinu na mikakati ya kuhakisha mambo hayo “Mabaya” hayaibuki tena. MV Bukoba ilizama na kupoteza maisha ya watu, likapita na kana kwamba tukio hilo halijawahi kutokea, yakatokea matukio mengine kama hilo na kupita! Mabomu yakalipuka na kupoteza maisha ya watu, nalo likapita; yakaliputa tena mara ya pili, nalo hilo likapita! Lilipoibuka suala la Richmond, tulitegemea jambo hili lingefika mwisho wake na kuwekewa mikakati ili jambo hili lisitokee tena; la kushangaza ni kwamba la Richmond, lilipita na maisha yakaendelea kama kawaida na kesho na kesho kutwa kuna hatari ya kutokea Richmond nyingine. Likaibuka la EPA, nalo likapita! Likaja la Dowans, nalo kikapita! Balali, akafa na kuzikwa kule Amerika, nalo likapita! Likaja la Jairo, nalo likapita! Ulimboka akatekwa, akapigwa na kuumizwa vi baya sana; mshukiwa akakamatwa, hata bila kutuonyesha sura yake, tukaambiwa kesi iko mahakamani, hilo nalo limepita. Sasa na hili la mtambo huu wa kijasusi wa kuingilia mawasiliano ya watu unaomhusisha mtoto wa “Kigogo” nalo limepita? Katiba ya Tanzania, inazuia mtu kuingiliwa kwa mambo yake ya faragha. Kuingilia mawasiliano ni kuingilia mambo ya faragha na kuivunja katiba. Kwa maoni yangu, suala hili si la CHADEMA peke yao, hili ni la watanzania wote. Na hasa hili linawahusu zaidi Makampuni ya simu. Kama makampuni haya bado yanataka kuendelea kufanya biashara hapa Tanzania, ni lazima yafanye kazi ya ziada kurudisha imani ya watanzania. Maana kama mawasiliano ya wateja yanaingiliwa kwa makusudi mazima; ni wazi wateja wao wataanza kususia mitandao yao. Ni lazima kuwahakikishia wateja wao kwamba suala kama hili halitajirudia tena na punde likitoea, wao watakuwa watu wa kwanza kulitangaza na kumkamata mhusika badala ya jambo hili kugunduliwa na wateja wenyewe. Jambo la uhakika kufuatana na maendeleo ya teknolojia, makampuni ya simu ni lazima yanafahamu uingizwaji wa mtambo huu wa kuingilia mawasiliano. Kama ujumbe wa vitisho ulitoka CHADEMA, ni lazima makampuni haya ya simu yafahamu. Na kama haukutoka huko ni lazima wafahamu. Hivyo kwa suala hili ambalo linaelekea kuleta vurugu katika taifa letu, makampuni haya ni lazima yawe ya msaada mkubwa. Kwa vifaa vya kisasa kama GPS, ni rahisi kugundua mtu mwenye mtambo kama huo na sehemu aliyopo. Na hasa kama mtu huyu anaingilia mitambo ya makampni haya ya simu, ni kazi rahisi makampuni haya kumnasa mtu huyu na kumtangaza hata kama mtu huyu ni mtoto wa “Kigogo”. Ni dhambi kubwa kuliacha na ihili likapita. Mtu huyu ambaye ameanza mbinu chavu za kuingilia mawasiliano na kutengeneza ujumbe wa vitisho vya kutoa uhai anaweza kufanya mengine zaidi; anaweza kuanzisha vikundi vya kuteka watu na kuwatesa na wakati mwingine kutoa kabisa uahi wao; anaweza kutengeneza mitambo ya kuiba kura au kutengeneza mitambo ya kuiba fedha kwa kutumia mtandao. Vyovyote vile nia ya mtu huyu si njema na ni lazima watanzania tukawa macho na kuanza kuchukua hatua kwa watu wabaya na wenye nia mbaya na taifa letu la Tanzania. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 6331 22. www.karugendo.net
KUICHEZEA ELIMU YETU NI DHAMBI KUBWA: TUTAJUTA! Waswahili wanasema majuto ni mjukuu. Serikali inashangilia kwa kuwashinikiza walimu kurudi kazini; wenye upeo mkubwa wa kuchambua masauala ya kijamii na kuona mbali wanasikitika na kusononeka: Kutangaza mgomo kilikuwa ni kilele; nyuma yake kuna mambo mengi. “ Haya mambo mengi” kuyafunika kwa nguvu za dola ni aina fulani ya mabavu ya kijinga. Mgomo wa walimu na hatua za serikali kuitumia mahakama kuubatilisha mgomo huo ni mchakato wa kuichezea elimu yetu na kama wasemavyo waswahili majuto ni mjukuu. Kuichezea elimu ni dhambi kubwa! Ni uchawi mkubwa. Kama sisi tulipata elimu bora kwanini tutake watoto wetu wabaki na ujinga? Wamalize darasa la saba bila hata kujua kuandika majina yao? Tulifundishwa na walimu bora ambao waliipenda kazi yao na kuitekeleza kwa moyo wote. Walimu wetu walikuwa wanafundisha kwenye mazingira mazuri. Kulikuwa na yumba za walimu, madarasa yalikuwa na madawati, tulikuwa na vitabu na vifaa vingine vya kufundishia.Ualimu ilikuwa ni kazi ya kuheshimika katika jamii na sisi tuliwapenda walimu wetu nao walitupenda kama watoto wao. Serikali ya Mwalimu Nyerere ilitoa kipaumbele kwa elimu, leo sisi tunafikiri elimu ni kitu cha mwisho! Huu ni uchawi zaidi ya mtu anayeamua kunyonya maziwa yake mwenyewe na kuawaacha watoto wake wakifa kwa njaa! Hakuna taifa lolote duniani linaloweza kuendelea bila vijana wake kupata elimu bora. Msingi wa maendeleo ni kuwaandaa watoto kwenye msingi bora wa elimu. Kwa maana hiyo, walimu popote duniani ni watu wanaoheshimika na daima wanajengewa mazingira ya kuwawezesha kuendeleza kazi ya kulielimisha taifa. Tanzania tunataka kufanya kinyume; Ingawa Rais wetu anasema serikali inawathamini sana walimu, lakini ukweli ulio mbele yetu ni kinyume kabisa. Walimu wetu hawalalamikii mishahara peke yake, bali nyumba za walimu, madarasa, madawati, vitabu, vyoo na wakati mwingine usafiri wao na wa wanafunzi. Haiwezekani kwamba serikali haina fedha za kununua madawati, kununua vitabu, kujenga madarasa, kujenga nyumba za walimu, kujenga vyoo, kuwapatia usafiri wanafunzi na kuwaongezea walimu mshahara. Serikali itwambie ni kipi kati ya hivyo inakitekeleza kwa ukamilifu? Hadithi kwamba serikali haina uwezo zinachosha masikio ya kila mtanzania. Tuambiwe kwamba serikali haina uwezo wa kuongeza mishahara, lakini shule zote zina madawati, tuambiwe kwamba serikali haina uwezo kwa kuongeza mishahara ya walimu lakini shule zote zina nyumba za walimu, zina madarasa na zina vitabu vya kutohsa. Kuna ujumbe unaozunguka kwenye mitandao ya kijamii ukisema: "Kitaeleweka tu kwa walimu vinginevyo darasani itakuwa hivi: a) 1 + 3 = 13, b) 73-3= 7, c) 3 mara 3 = 333, d) 7 mara 2 = 77, na kwenye physics usiseme kila formula itakuwa reciprocal. hivyo ndo plan B kwa walimu wa science sipati picha kwa wa history, "Binadamu wa kwanza alikuwa NYERERE. Kazi ipo." Ujumbe huu umeanza kusambazwa walimu walipoanza mgomo wao. Wakionyesha kwamba endapo mgomo wao ukaingiliwa na serikali, watakuwa na mpango B. Na kweli sasa Serikali kupitia mahakama ya kazi wameuingilia mgomo huu kimabavu, bila majadiliano na makubaliano kwa pande zote mbili. Ni wazi sasa mpango B wa mgomo baridi utaanza kutekelezwa. Hata kwa mjinga yoyote asiyekuwa na akili ya kufiki na kuchambua mambo, atatambua kwamba tunaelekea kuichezea Elimu yetu na matokeo yake ni kujuta. Kuna ambao wataupuuzia ujumbe huu wa walimu wa kuanza mgomo baridi na kuna ambao ujumbe huu hauwagusi kabisa, maana kama mtoto anasoma shule ya binanfsi kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, au mtoto anasoma nje ya nchi, ujumbe huu si wake kabisa. Lakini kwa wale (ambao ndio wengi) wanaotegemea shule za serikali, ujumbe huu si wa kupuuzwa. Tatizo kubwa tulilonalo ni kwamba wale wanaowasomesha watoto nje ya nchi, wale ambao watoto wao hawasomei kwenye shule zetu hapa nchini, ndio wanafanya maamuzi juu ya elimu yetu. Hawana uchungu kwa chochote wakatakahoamua. Hawana uchungu endapo walimu wataamua kufanya mgomo baridi Walimu walipotangaza mgomo, kuna mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini aliniambia hivi “ Ni kutangaza tu mgomo, lakini ukweli ni kwamba walimu tuligoma miaka mingi”.Ukweli wa mwalimu huyu ni matokeo tunayoyaona kwenye viwango vyetu vya elimu. Tunasikia namba kubwa ya watoto wanashinda mtihani wa darasa la saba, bila kujua kusoma wala kuandika. Mahakama ya Kazi, imetoa hukumu na kuwalazimisha walimu kurudi kazini. Ni wazi hakuna anayefurahia walimu kugoma, lakini pia kushangilia Mahakama kuwalazimisha walimu kurudi kazini bila majadiliano ya kumaliza madai ya walimu kwa njia ya amani ni kujidanganya. Walimu, wataitii mahakama, lakini hawatafanya kazi kwa moyo. Na hii ni hatari kubwa kwa elimu ya watoto wetu. Mgomo baridi ni mbaya kuliko mgomo wa wazi ambao hekima na busara vikifuatwa, mgomo huo unamalizika na walimu wanarudi kazini kama kawaida. Kutumia “Mabavu” kumaliza mgomo wa walimu ni kuliletea taifa letu janga kubwa. Walimu wataingia kwenye mgomo baridi na hata polisi wakitumika, haiwezekani kuwalazimisha kufundisha, na wakilazimishwa watafundisha ovyo ovyo na watoto wetu watamaliza shule bila kuwa na elimu bora. Mabavu yalitumika kuumaliza mgomo wa madaktari. Hadi leo hii kuna malalamiko kwamba huduma kwenye hospitali zetu za Serikali si nzuri. Madaktari wako kazini, lakini kwa vile malalamiko yao hayakushughulikiwa, hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi. Wanaoumia ni wananchi wa kawaida, viongozi wetu hawatibiwi kwenye hospitali zetu, wao wanakwenda kutibiwa nje ya nchi. Ingawa migomo si mizuri kwa maendeleo ya taifa, lakini na kuizima kiubabe si vizuri kwa maendeleo ya taifa letu. Tutaendelea kurudi nyuma kwasababu namba kubwa ya watumishi wa umma wanafanya kazi kwa kulazimishwa na si kufanya kazi kwa mapenzi na moyo wa kizalendo. Si kweli kwamba serikali yetu haina fedha za kuwalipa mshahara mzuri walimu, madaktari na watumishi wengine. Fedha tunazo nyingi na nyingine wajanja wachache wanaendelea kuzichota na kuziingiza kwenye mifuko yao, Mahakama inawatizama tu! Sote tunaishi Tanzania, walimu wanaishi Tanzania, madaktari wanaishi Tanzania.Sote tunashuhudia magari ya kifahari wanayoendesha watoto wa vigogo, tunashuhudia mahekalu ya vigogo, ya watoto wao na vimada vyao; tunashuhudia watoto wa vigogo wanakwenda kusoma nje ya nchi, tunashuhudia vigogo wakipanda ndege kwenda kutibiwa, kupumzika na kufanya manunuzi nje ya nchi. Fedha hizo wanazipata wapi? Zinachotwa hapa hapa Tanzania. Tumeanzisha wilaya za kisiasa, mikoa ya kisiasa bila kuwepo na hitaji la muhimu na haraka kuanzisha wilaya hizi na mikoa hii. Fedha nyingi zitatumika na kwingineko zimeaanza kutumika kuanzisha wilaya na mikoa. Tungekuwa na nia ya kuboresaha elimu yetu, tungeanza kushughulikia kero za walimu kabla ya kuamua kutumia fedha nyingi kwenye mradi huu mkubwa wa kuanzisha wilaya mpya na mikoa mipya. Tuna baraza la mawaziri kubwa bila sababu zozote za msingi. Baraza hili linatumia fedha nyingi ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye mishahara ya walimu, madaktari na watumishi wengine wa serikali na kuchochea mambo mengi kufanywa kwa ufanisi mkubwa. Wengi tulitegemea kumsikia Rais Kikwete, akisema kwamba kwa vile Serikali haina fedha na walimu wanadai nyongeza ili wapate motisha wa kuwafundisha watoto wetu, basi serikali inaachana na mpango wake wa kuanzisha Wilaya mipya na mikoa mipya, serikali inapunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, serikali inapunguza matumizi mengine ya serikali yasiyokuwa ya lazima: kama chai, posho na safari nyingine za nje ili fedha zitakazookolewa kwenye zoezi hilo zisaidie kulipa mishahara ya walimu. Badala yake Rais, anasema serikali haina fedha hivyo walimu wanataka wasitake ni lazima warudi kufundisha. Hawawezi kufundisha hawa! Kitakachofanyika ni kuichezea elimu ya watoto wetu. Hitaji la sasa hivi si kuanzisha wilaya na mikoa. Mfano Karagwe, imegawanywa mara mbili kutengeneza Wilaya za Karagwe na Kyerwa. Lakini hili halikuwa hitaji la watu wa Karagwe. Hitaji lao ni maji,hospitali,soko la kuuza mazao yao kwa uhakika, walimu, vyumba vya madarasa, madawati, barabara na umeme. Karagwe kuna tatizo sugu la maji na miaka yote halijapatiwa uvumbuzi, barabara nyingi za wilaya ya Karagwe, zinapitika kwa shida wakati wa mvua, shule nyingi za Karagwe, watoto wanakaa chini na shule nyingi hazina vifaa vya kufundishia. Kuyaweka matatizo hayo yote pembeni na kukimbila kuanzisha wilaya mpya ambayo itahitaji mabilioni kuianzisha ni kuwachelewasha watu kupiga hatua ya maendeleo. Kama tunalipenda taifa letu, kama tunawapenda watoto wetu, kuna umuhimu na hitaji la haraka kukutana na walimu na kujadiliana nao juu ya madai yao. Bila kufanya hivyo walimu hawatafundisha. Ndo maana wameanza kusambaza ujumbe kama huo hapo juu kwenye mitando ya kijamii. Watakwenda shuleni na kufundisha mambo mengine kinyume. Matokeo yake watoto wataingia mitaani kudai haki yao ya kufundishwa. Juzi tumeshuhudia wanafunzi wakiandamana nchi nzima. Serikali inafikiri kwamba watoto hao wanafundishwa na kulazimishwa na walimu wao kufanya maandamano. Kufikiri hivyo ni “Upumbavu”. Watoto hao wanapitia manyanyaso makubwa; wanasafiri kwa shida kwenda shuleni, wanasukumwa na makonda, wanasimama kwenye dalala, wanashinda njaa bila chakula, wanakaa chini, hawana vyoo shuleni. Nyumbani wanashuhudia maisha yanavyopanda, wanasikia wimbo wa mafisadi, rushwa na uporaji wa maliasili. Wakati huo huo wanashuhudia watoto wengine wakipelekwa na mashangingi shuleni na kusomea kwenye shule za kifahari. Hawa ni binadamu na yote hayo wanayaona; hivyo si lazima wasukumwe na mtu, wanasukumwa na jamii yetu iliyofilisika kimawazo. Makala hii ni wito kwa serikali kuachana na mfumo huu wa kutumia mabavu kuwalazimisha walimu kurudi kazini. Pia ni ushauri wa bure kwamba kuitumia mahakama kama chombo cha kuzima sauti za wanyonge ni dhambi kubwa; wanyonge wakitambua kwamba hakuna sehemu yakukimbilia kudai haki zao, wataamua kuingia barabararni na hili likitokea hakutakuwa na sabababu ya msingi ya kumtafuta mchawi au kufikiri kwamba migomo inaendeshwa na vyama upinzani; migomo hii inaratibiwa na serikali iliyo madarakani kwa tabia yake ya kufumbia macho mambo mengi ya ukweli. Tusichezee elimu ya watoto wetu kama tunalipenda taifa letu. Na, Padri Privatus Karugendo. www.karugendo.net +255 754 633122.
WAHARIRI WAMEISALITI MWANAHALISI Wahariri wa vyombo vya habari Tanzania wana umoja wao. Tumeshuhudia wakifanya mikutano yao kwenye mahoteli makubwa na wakati mwingine wakisafiri mikoani kufanya mikutano yao. Imani yetu ni kwamba umoja huu si wa kunywa chai, si wa kukutana na kupiga soga au kujadili mishiko bali pamoja na mambo mengine muhimu ya umoja huu ni sauti ya pamoja. Sauti ya kutetea haki, sauti ya kupinga kuonewa na wamiliki wa vyombo vya habari na kupinga uonevu wowote unaoweza kutoka serikalini na kuhakikisha vyombo vya habari ni jukwaa huru la majadiliano. Vyombo vya habari ni mhimili mkubwa katika jamii yetu, ukiachia mbali serikali, mahakama na Bunge. Hivyo wahariri wanaoviongoza vyombo hivi ni watu muhimu na wana ushawishi mkubwa katika jamii. Ni muhimu kabisa watu hawa kuwa na sauti ya pamoja ili mhimili huu muhimu uwe na nguvu za kutosha kutetea haki na kusimamia ukweli. Bila sauti ya pamoja, sauti ya uzalendo, vyombo vya habari vinaweza kuleta vurugu katika nchi au vinaweza kuleta ukombozi. Kuna mifano mingi ambayo imetolewa kila wakati kiasi cha kuyaumiza masikio ya watanzania. Si muhimu kuirudia mifano hii kwenye makala hii, labda yakitukuta ndo majuto yatakuwa mjukuu. Inashangaza kwamba sauti hii ya pamoja, sauti ya kutetea haki sauti ya kupinga kunyanyaswa na kuonewa haijasikika kulitetea gazeti la Mwanahalisi. Badala yake tunashuhudia chuki binafsi na wivu; tunashuhudia usaliti wa wazi wazi na labda kwa vile sasa hivi waandishi wa habari wanaingizwa serikalini na wengi wao kupandishwa hadi kuwa wakuu wa Wilaya, wanaamua kuusaliti umoja wao ili kesho na keshokutwa nao wapandishwe? Tulitegemea kuwaona wahariri wakitumia nguvu zao zote, magazeti yao, mikutano yao na hata maandamano ya amani kupinga kitendo cha Serikali kulifungia gazeti la Mwanahalisi. Nguvu zilizotumika kulifungia gazeti la Mwanahalisi, zinaweza kutumika kuyafungia magazeti mengine pia.Wahariri wamekaa kimya kana kwamba hakuna jambo kubwa lilitokea katika umoja wao. Inawezekana na wahariri hawa wanainyoshea kidole Mwanahalisi? Nao wanaamini Mwanahalisi ni gazeti la uchochezi? Kwamba Kubenea ni kichwa ngumu? Kwamba ameonywa na hakusikia? Kwamba sasa amekipata? Ina maana wahariri hawa wanashangilia msiba wa mwenzao? Bahati mbaya au nzuri wahariri wengi ni vijana. Na tujuavyo vijana mara nyingi wanakuwa msatari wa mbele kutetea haki na kutaka mabadiliko. Katika hali ya kawaida, bila kuzingatia itikadi yoyote ile kitendo cha kulifungia gazeti la Mwanahalisi, na kulifungia kwa kuandika habari iliyokuwa inafichua unyama aliofanyiwa Dkt Ulimboka, kingepigiwa kelele na wahariri hadi mbingu zikasikia. Inatia shaka kama wahariri hawa ni vijana wa kweli au ni vijana wa “kutengenezwa”? Ni vijana wanaosubiri kuelekezwa la kufanya na Baba? Ni vijana wanaoendelea kunyonya kidole hadi wanazeeka? Ni vijana wenye tabia ya kujipendekeza na kuhakikisha uwezo wao wa “kufikiri” wanauwekeza na kuufungia kwenye sanduku lisilofunguka milele? Kimya hiki cha wahariri kinashangaza sana. Inawezekana ni aina Fulani ya upambanaji? Ukimya unahesabika katika sauti ya pamoja, sauti ya kutetea haki? Au wakati umefika kuamini kwamba wahariri wetu wamefungwa midomo na serikali? Au ni wafanyakazi wa Serikali? Juzi hapa tumeshuhudia Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, akiwaita wahariri na kuongea nao. La kushangaza, au labda kulikuwa na maelekezo? Hatukushuhudia hata mhariri mmoja kujitokeza kuuliza swali juu ya Mwanahalisi au kumweleza Rais wetu ukweli kwamba kulifungia gazeti katika nyakati hizi tulizomo ni kichekesho: Wahariri wangemwelezea Rais, kwamba kitendo cha kulifungia gazeti la Mwanahalisi, kilisaidia kuusambaza ujumbe uliokuwa kwenye gazeti hilo ambao serikali haikutaka wananchi waufahamu. Kitendo cha kulifungia gazeti hilo lilitafutwa na kurudufiwa na kusambazwa Tanzania nzima. Na wale wanaosoma mtandao, ambao wengi wao ni vijana, waliusambaza ujumbe huu kwenye mtandao na hadi leo hii ujumbe huu unazunguka. Wahariri wangemweleza Rais, ukweli kwamba hata akiamua kuvifungia vyombo vyote vya habari, watu watatumia mitandao ya kijamii, wataendelea kusoma habari hata kwa kutumia simu zao za mkononi. Hivyo kulifungia gazeti kwa vyovyote vile si nyenzo ya kuzuia uchochezi au kuzuia habari ya aina yoyote ile kusambaa. Wahariri wangemkumbusha Rais ahadi yake ya kutengeneza ajira milioni moja. Kulinfungia gazeti la Mwanahalisi ni kusitisha ajira za vijana waliokuwa wakilitegemea gazeti la Mwanahalisi na kwamba kitendo hiki ni cha kikatiri na hakivumiliki. Vijana wanajitafutia kazi ili waweze kuendesha maisha yao, juhudi zao zinazimwa na mtu mmoja mwenye madaraka makubwa bila kujadiliana na vyombo husika? Kuna baraza la habari Tanzania, mbona halikusishwa? Lakini la msingi zaidi wahariri hawa wangehoji juu ya kosa la Mwanahalisi. Suala la kukamatwa, kupigwa na kuteswa kinyama kwa Dkt Ulimboka, limekuwa na utata. Yanasemwa mengi na watu wengi wanahusishwa. Mwanahalisi wamefanya utafiti na kutaja jina la mtu ambaye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwasiliana na Dkt Ulimboka. Mtu huyu kufuatana na namba yake ya simu alikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na Dkt Ulimboka na ushahidi unaonyesha anafanya kazi Ikulu. Hapa kosa la Mwanahaisi liko wapi? Ulimboka mwenye alisema aliyemkamata na kumpiga anamfahamu,ni mtu walikutana Ikulu na siku hiyo alimpigia simu mara nyingi. Walichokiandika Mwanahalisi, ndicho hicho alichokisema Ulimboka. Rais, hata angesema mara miamoja kwamba Serikali haiusiki, haitasaidia kama hamkani au kumkubali mtu huyo anayetajwa na Mwanahalisi. Tulitegemea wahariri kumkumbusha Rais, Ikulu kukana kwamba mtu huyo si mfanyakazi wake. Ili mtu huyo akamatwe na kuhojiwa juu ya suala zima la Ulimboka. Kwa njia moja ama nyingine Mwanahalisi iliwasaidia Polisi kufanya kazi yake ya upelelezi. Tulitegemea wahariri wamtake Rais, kueleza kwa kina na ufasaha utamaduni huu unaojengeka wa kuitumia mahakama kuzima sauti za watu. Au mahakama kutumiwa kuwanyanyasa wanyonge kama ilivyofanyika kwa mgomo wa madaktari na walimu. Au hata kwa suala zima la Ulimboka, kwamba sasa hivi suala hilo liko mahakamani na kulijadili ni kuingilia kesi iliyo mahakamani. Tulishuhudia mchezo wa kuigiza uliotumika kulifikisha suala la Dkt Ulimboka mahakani. Huyo mkenya aliyekamatwa wakati alipokwenda kuungama kanisani, na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kumteka na kumtesa Dkt Ulimboka, hajasikika tena. Hiyo kesi yake itasikilizwa lini? Na je mbona sura yake haikuonyeshwa kwenye vyombo vya habari? Au ni kutaka kulinda usalama wake? Ina maana usalama wa huyu jambazi kutoka Kenya ni muhimu kuliko maisha ya watanzania? Hatukushuhudia wahariri wakiuliza maswali ya kumsaidia Rais wetu na watanzania. Tunataka tusitake tuna matatizo makubwa. Madaktari wanagoma, walimu wanagoma, watu wanatengeneza makampuni ya kuiba umeme, wanauza umeme miaka saba bila kukamatwa, Bunge linatunga sheria ambazo hata kabla ya kuanza kutumika zinaonekana zina kasoro, serikali inalipa mishahara hewa, magazeti yanafungiwa… kuna kasoro sehemu Fulani na kasoro hizi ni lazima zijadiliwe vinginevyo hatuwezi kufika mbali. Wahariri wa vyombo vyetu vya habari wana mchango mkubwa katika hili. Ndo maana wengi wetu tulitegemea kwa suala la Mwanahalisi, ambalo linaelekea kuzima uhuru wa majadiliano na uhuru wa kuibua yale yaliyojificha ambayo ni “adui” wa Umma, lingepigiwa kelele na wahariri wetu. Usaliti wao kwa Mwanahalisi ni mauti yetu na ni mauti yao pia! Na, Padri Privatus Karugendo.