AFRICARE NA MCHANGO WAKE TANZANIA 4

AFRICARE NA MCHANGO WAKE KATIKA JAMII: TANZANIA.( 4 )

MIRADI YA CHANGAMOTO ZA MILENIA.

Kama ilivyodokezwa mwanzoni mwa makala hii ndefu, ni kwamba mwandishi wa makala hii ameshiriki katika miradi miwili ya AFRICARE, mradi wa Huduma Majumbani na Mradi wa Kusogeza huduma ya Umeme vijijini. Makala zilizotangulia zilielezea mradi wa huduma majumbani, na hizi zinazofuata sasa zitajikita juu ya mradi wa kusogeza huduma ya Umeme vijijini.

AFRICARE, inaratibu mradi huu wa kusogeza huduma ya umeme vijijini. Sasa hivi mradi huu umefikia hatua ya kuandaa fidia kwa wanavijiji watakaopisha njia ya umeme. Kama nilivyofanya kwenye makala zilizotangulia, sitafafanua undani wa mradi huu, hiyo ni kazi AFRICARE. Kinachofanyika hapa ni maelezo ya mwandishi aliyebahatika kushiriki hatua hii ya kuandaa fidia kwa wananchi watakaopisha njia ya umeme. Hatua hii ilimwezesha mwandishi kuzunguka kwenye mikoa sita ya Mwanza, Mbeya, Iringa, Tanga, Morogoro na Dodoma. Fursa hii ilimwezesha mwandishi kuhojiana na wanavijiji wengi na kujionea mwenyewe maisha halisi ya kule vijijini.

AFRICARE, ilimwangalia mwandishi kama kibarua wa kawaida aliyekuwa akishirikiana na wengine kutekeleza uratibu wa AFRICARE, mwandishi kwa upande wake aliichukulia fursa hii kama wakati mzuri wa kutafiti na kuandika baadhi ya mambo ambayo mara nyingi vyombo vya habari havitangazi wala kuandika. Na pia ni kutusaidia kutafakari juu ya misaada hii tunayopewa: Je ni misaada? Je, nani anaamua ni wapi pa kuipeleka hiyo misaada? Mradi wa kusogeza umeme uko kwenye mikoa sita ya Tanzania; je nani aliichagua mikoa hii? Haya ni maswali muhimu ya kutusaidia kutafakari na kuchochea uelewa wetu juu ya misaada hii inayotoka kwenye nchi zilizoendelea.

Miradi ya changamoto za milenia kwa walio wengi na hasa mijini (wasomi na waelewa) inajulikana kama Miradi ya Bush au fedha za Wamarekani. Miradi hii ni ya Barabara, maji, Afya, Elimu, umeme nk. Kiasi kikubwa miradi hii iko katika hatua za utekelezwaji. Vijijini miradi hii inajulikana kama miradi ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete, maana wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010 aliahidi vitu vingi ambavyo alijua kwa uhakika vitatekelezwa na mfuko wa miradi ya changamoto za Milenia. Washabiki wa CCM, wanaamini miradi hii ni utekelezaji wa Sera nzuri za chama chao.

Vyovyote vile, ni imani yetu kwamba miradi hii ikikamilika itawanufaisha watanzania wote? Na la muhimu ni kuangalia mbali zaidi; miradi hii ni misaada! Je katika dunia hii kuna msaada wa bure? Kuna mtu anatoa msaada bila ya malengo? Kwa nini mtu akusaidie wakati dola yake inapanda na shilingi yako inazama? Kama ana nia ya msaada kwa nini asihakikishe dola na shilingi vinapanda na kushuka wakati mmoja? Si hoja ya au ushawishi wa kuikataa misaada, ni namna ya kuingiza wazo la kuwa mpole kama Njiwa na mjanja kama nyoka. Tatizo letu kubwa hapa Tanzania na nchi nyingi za dunia ya tatu (AFRIKA) ni kufumbwa macho na upole wa njiwa. Anayeleta msaada ana lengo lake hivyo ni muhimu anayepokea msaada awe na matumaini na malengo ya muda mrefu pia! Bila kuumizana, anayetoa na anayepokea wanufaike sawa au kwa kupishana kidogo.

Katika makala hii nitajadili Mradi wa Kukarabati na uwekaji wa miundombinu mipya ya kusafirisha umeme katika baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara na visiwani. Mradi huu ni wa kusogeza huduma ya umeme kwa wananchi. Hapa kuna maneno mawili ya kuangalia kwa umakini; Kusogeza na Kusambaza. Kitakachofanyika katika mradi huu, ni kusogeza umeme kwa wananchi. Maana yake ni kwamba kama umeme ulikuwa kilomita zaidi ya miamoja kutoka kijiji cha Nyambeba wilaya ya Sengerema, sasa umeme huu utakuwa ndani ya kijiji cha Nyambeba na kazi ya kuusambaza nyumba hadi nyingine itatekelezwa ama na serikali au wananchi wenyewe.

Kama nilivyosema mwanzoni, mradi huu unatekelezwa na Mfuko wa changamoto za Milenia (Fedha za Bush) na kuratibiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la AFRICARE, ambalo nalo pia ni shirika la Wamarekani. Nimebahatika kufanya kazi na AFRICARE katika baadhi ya miradi yao mfano ule wa Kaya, unaotekelezwa katika Mikoa ya Manyara na Mara na sasa huu wa kusogeza huduma ya umeme kwa wananchi.

Tanzania bara, mradi huu utatekelezwa katika mikoa sita; Tanga, Morogoro, Mbeya, Iringa, Dodoma na Mwanza. Na sasa hivi ninapoandika makala hii mradi huu umefikia hatua ya kuandaa fidia kwa mali za wananchi zitakazoadhiriwa na mradi huu wa kukarabati na uwekaji wa miundombinu mipya ya kusafirisha umeme. Wananchi ambao mazao yao yataguswa na njia ya umeme, watalipwa fidia na wale ambao nyumba zao zitabomolewa watalipwa fidia au watajengewa nyumba nyingine.

Nilijaribu kufafanua tofauti kati ya kusogeza na kusambaza. Nikitaka kulenga kwa umuhimu wa huduma hii ya umeme, ingawa kusogeza huduma ya umeme ni muhimu, lakini pia kusambaza ni muhimu zaidi maana kama tutakavyoona ni kwamba wananchi wengi (zaidi ya azilimia 90) kule vijijini hawana uwezo wa kuvuta umeme. Aina maana kwamba huduma zote hizi za kusogeza na kusambaza zifanywe na mfuko wa changamoto za Milenia, shirika jingine au taasisi nyingine inaweza kujitokeza kufanya kazi ya kusambaza umeme vijijini, lakini ni lazima pia serikali ifikirie haraka mkakati wa kusambaza umeme vijijini. Na jambo jingine ambalo ni lazima liwe wazi kwa msomaji wa makala hii ni kwamba mradi huu hautengenezi vyanzo vipya vya kuzalisha umeme bali utatumia vyanzo vilele. Umeme wetu tuliouzoea ambao kila mwaka tunakuwa na tatizo la mgawo, ndo huo huo mfuko wa changamoto za milenia, utausogeza kwenye vijiji katika mikoa sita ya Tanzania Bara na visiwani. Labda, msaada huu ungeelekezwa zaidi katika kutengeneza vyanzo vipya vya umeme?

Nimezungukia mikoa yote sita na kupitia karibia vijiji vyote vitakavyonufaika na mradi huu. Swali langu kubwa kama mchambuzi wa maswala ya kijamii ni: Ni vigezo gani vilitumika kuichagua mikoa hii sita kunufaika na mradi huu? Je ni serikali ya Tanzania iliichagua mikoa hii (kwa vigezo gani?) au Wamarekani wenyewe waliichagua mikoa hii? Na je mikoa yenyewe ilitumia vigezo gani kuchagua wilaya, maana si wilaya zote katika kila mkoa zitapata huduma hii; na Wilaya zilitumia vigezo gani kuchagua vijiji, maana si vijiji vyote katika wilaya vitapata huduma hii. Hili ni swali la uchokonozi, lakini nafikiri ni muhimu katika mkakati mzima wa kuwa wapole kama njiwa na wajanja kama nyoka...... itaendelea.


Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment