SAFINA MARIA MAGDALENA JESUS

MWANA MAMA MCHUNGAJI SAFINA MARIA MAGDALENA JESUS.

Leo katika safu yetu ya Mwana Mama, tunawaletea Mchungaji Safina Jesus. Yeye mwenyewe, anapenda ajulikane kwa jina lake kamili ambalo ni: Mchungaji Safina Maria Magdalena Victoria Jesus. Waliomfahamu siku za nyuma na hata alipokuwa akiishi na kufanya kazi nchini Uingereza, walimfahamu kwa jina la Safina Yussaph Haruna. Ni mwana mama aliyekulia kwenye imani ya Ukatoliki, akaingia kwenye imani ya  Uislamu na hatimaye kupokea wito wa kuwa mchungaji na kupokea kipaji cha uponyaji mwaka 2011, akiwa nchini Uingereza. Kwa ufupi ni kwamba ni mama aliyeonja imani zote, Ukristu wa dhehebu mbali mbali na Uislamu.
Hapana shaka kwamba uzoefu wake wa imani hizi zote ndo unamsukuma kuwa na hamu na shauku la kuanzisha nyumba ya ibada, kanisa la watu wote; wenye imani tofauti, maoni tofauti lakini wenye nia na lengo la kujenga jumuiya yenye mshikamano na upendo. Jumuiya yenye maendeleo na heshima kwa binadamu wote bila ubaguzi wa aina yoyote ile.
Mbali na mvuto wa mama huyu kwenye huduma ya uchungaji na uponyaji, ni mapenzi yake kwa watoto yatima. Amejipanga kufungua kituo cha watoto yatima kule Kigamboni, ili watoto hawa wapate elimu ya kuwasaidia kuacha kuzurura mitaani na kuomba omba. Yeye ana imani kwamba haitoshi kumsaidia mtoto Yatima chakula na nguo, maana mahitaji ya kila siku ni lazima yaendelee maisha yake yote; hivyo ni lazima kumsaidia mtoto yatima ili aweze kujisaidia mwenyewe.

KITUO cha watoto yatima kinatarajiwa  kujengwa jijini Dar es Salaam ambacho kitachukua watoto zaidi ya 1000 na kwamba watoto hao watapewa elimu ya ufundi kwa ajili ya kujiandaa na maisha ya kujitegemea na kuachana na kuombaomba
  “Watoto watajifunza kupitia walimu waliobobea ili kuweza kuwa chachu  ya kujiajiri baada ya umri wa kujitegemea na kuongeza nguvu kazi ya taifa. Hatuwezi kuendelea kuhubiri injili wakati watoto wako mitaani, hivyo lazima tuwe na njia mbadala za kuweza kusaidia taifa hili ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya watoto yatima ambao watapata elimu ya kiroho na elimu ya kujitegemea kwa kuwa na ujuzi,” alisema Safina .
Pia anasema alipokuwa nchini Uingereza kiu yake ilikuwa inamtuma kufanya jambo linalohusiana na watoto akiwa nchini Tanzania kwa kujenga kituo ambacho kitakuwa sehemu ya chuo kwa ajili ya watoto yatima na mitaani kupata elimu ya ujuzi mbalimbali.

Mwana mama huyu alizaliwa Iringa mnamo mwaka 1979, Baba yake anatokea Iringa, wakati mama yake anatokea Bukoba. Baada ya masomo yake, alifanya kazi kwenye jiji la Dar-es-Salaam na hasa kwenye sekta ya mahoteli. Baadaye alihamia nchini Uingereza na kuishi kwenye bonde la Bevois na kufanya kazi Bexhill,East Sussex kwenye kanisa la Mtakatifu Barnabas. Ni wakati huo alipoitwa kumtumika Bwana Yesu.
Mama huyu, alipata daraja la uchungaji kutoka kwa Mheshimiwa sana Askofu Mkuu Richard Palmer, wa Episcopal Free Church ya Southampton. Na baada ya kumpatia daraja hilo Askofu Mkuu huyo alisema hivi juu ya Mama huyu: “ Nafurahi sana kuwa na mchungaji huyu kama mtumishi, nafikiri atakuwa mzuri sana, ni mtu aliyejitoa kwa moyo wake wote kwa huduma hii”.
Lengo la mama huyu hapa Tanzania, ni kujenga uhusiano kati ya Kanisa la Mtakatifu Barnabas na Tanzania; kuamusha imani ya kumpenda na kumtumikia bwana Yesu Kristu kwa matendo. Pia ana ndoto za kupanua huduma hii kwenye nchi mbali mbali za Afrika na popote pale ambapo roho mtakatifu atamwelekeza.
Wakati anajiandaa kupata sehemu ya kujenga nyumba ya Ibada, anaendelea kusali na kuhubiri kwenye nyumba yake maeneo ya Kimara. Anawakaribisha watu wa imani zote, maana lengo lake kubwa ni kuijenga jumuiya ya watoto wa Mungu, wanaokutana kusali pamoja na kushirikiana kujenga jumuiya yenye amani na maendeleo.
Mama huyu anapinga mwenendo wa Mashoga na wasagaji; anapinga kwa nguvu zote watu wanaokubali na kukumbatia utamaduni huu, pia anapinga kwa nguvu zote wanaowalaani na kuwatenga mashoga na wasagaji.  Msimamo wake ni kwamba watu hawa pia wanahitaji huruma ya mwenyezi Mungu. Kazi ya jamii si kuwatenga watu hawa na kuwalaani, bali ni kwasikiliza, kusali nao na kutafuta njia ya kuwasaidia na kuwabadilisha. Anatoa ushuhuda wa kuwasaidia baadhi ya watu hawa na sasa wameachana na tabia hiyo. Hivyo nyumba yake ya ibada inawakaribisha wa watu wa aina zote.
Pia Mama huyu ni miongoni mwa wanaoamini kwamba Bwana Yesu, aliliacha kanisa lake mikononi mwa Mwanamke, yaani Maria Magdalena. Biblia inaeleza vizuri kwamba Maria Magdalena, ndiye aliyesifiwa na Bwana Yesu, kuyafahamu mafundisho yake na kuyashika. Ingawa baadaye mfumo dume, uliingia kanisani mnamo mwaka 321 ukiongozwa na Mfalme Constatine wa himaya ya Warumi, na kubadilisha ukweli wote wa kanisa kuachwa mikononi mwa mwanamke. Hivyo anawahimiza wanawake popote walipo kujitokeza kuliongoza kanisa. Wanawake kujitokeza kupokea huduma ya uchungaji na utumishi.
Mambo manne yanamtofautisha mama huyu na wachungaji wengi tuliowazoea: Kwanza ni mtizamo wake juu ya watoto Yatima; lengo lake la kuwasaidia watoto yatima ili baadaye wajisaidie wenyewe ni tofauti na nyumba za watoto yatima tulizozizoea za kuwapatia chakula, malazi, matibabu na wakati mwingine masomo, bila mpango mzima wa kuwaandalia maisha ya baadaye.
Pili, msimamo wake juu ya mashoga na wasagaji ni tofauti kabisa na kauli nyingine ambazo tumezizoea na kuzisikia. Hili la kuwapokea, kuwasikiliza na kuwasaidia kubadilika ni jipya kabisa na ni jambo zuri na la kuungwa mkono na wanaharakati wote wa kutetea haki za binadamu.
Tatu; mpango wake wa kuwashirikisha watu wote wa imani mbali mbali, kusali pamoja na kufanya kazi pamoja, ni muhimu sana hasa wakati huu ambapo dalili za kutoelewana miongoni mwa imani mbali mbali hapa chini linaanza kujitokeza.
Nne, imani yake kwamba Kanisa liliachwa kwenye Uongozi wa mwanamke, ni jambo linalomtofautisha Mwana mama huyu na wachungaji wengine tuliowazoea. Hivyo huyu ni Mwana mama wa mfano kwetu sote. Huyo ndiye Mchungaji Safina Maria Magdalena Victoria Jesus.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

TGNP

TGNP NA MPANGO WA UTAFITI SHIRIKISHI WA URAGHABISHI.
 
Katika jitihada zake za kupambana na mfumo dume, uliberali mamboleo na mifumo yote kandamizi na kupambana ili rasilmali ziwanufaishe wanawake walioko Pembezoni, TGNP imeanzisha mpango wa utafiti shirikishi wa uraghabishi. TGNP, imeamua kuukumbatia mpango huu kwa vile unatoa nafasi pana ya ushirikishwaji hadi ngazi ya vijijini na kuchochea kuibua kero na changamoto nyingi ambazo zinahitaji majibu ya jamii nzima.
Mpango huu unatumika kama mbinu muhimu ya kujifunza, kutafakari, kuchambua na kutekeleza mikakati mbali mbali ya ujenzi wa Tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi lililokita katika ngazi za msingi ya kijamii na lenye uwezo kwa kudai uwajibikaji katika kutoa huduma bora, kusimamia rasilimali za taifa ili ziwanufaishe makundi yaliyoko pembezoni hususani wanawake.
Lengo kuu na mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi ni kuwezesha ushiriki wa wanawake, wanaume, makundi na mitandao katika ngazi ya jamii kufanya uchambuzi wa hali halisi kwa mrengo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi; kuibua kero na changamoto zinazokabili makundi husika  na za pamoja. Mpango huu pia unalenga katika kukuza uwezo na uelewa wa  uchambuzi wa kero zinazoikabili jamii.
Tamko la TGNP kwa vyombo vya habari lilitolewa tarehe 9.6.2013 ni la mpango huu ulioendeshwa kwenye wilaya tatu za Mbeya vijijini, kata ya Mshewe, Morogoro vijijini Kisaki na Kishapu – Shinyanga. Katika makala hii tutajadili mrejesho wa utafiti huu ambao ni wa aina yake.
Changamoto za uwekezaji na mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wananchi, ilijitokeza katika utafiti huu na mfano mzuri ni Kata ya Mshewe Mbeya vijijini. Katika kata hii utafiti ulibaini mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wawekezaji; ardhi nzuri na yenye rutuba imetolewa kwa wawekezaji kiasi kwamba wenyeji hawana mashamba na wanalazimika kuwa vibarua kwenye mashamba ya wawekezaji. Mbaya zaidi ni kwamba wawekezaji wenyewe wanawalipa kidogo. Mfano wanawake wanalipwa kati ya shilingi 2,500 hadi elfu3 kwa siku. Pamoja na kulikwa kidogo, wanakumbana na rushwa ya ngono na manyanyaso mengine hali inayosababisha ongezeko la magonjwa ambukikizi yakiwemo VVU na Ukimwi.
Changamoto hii ya mgawanyo mbaya wa ardhi imejitokeza pia katika kata ya Kisaki, Morogoro mjini, ambapo wakulima wadogo wadogo wanapambana na wafugaji. Kwa vile wafugaji hawana maeneo ya kutosha kwa mifugo yao, wanaingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuleta vita mbaya. Kwa upande mwingine wafugaji wanatumia fedha kuwahonga viongozi ili wasisumbuliwe wanapoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima. Matumizi ya fedha ni kupokonya wanyonge haki zao ni tatizo sugu kwa wananchi waishio pembezoni.
Suala jingine muhimu lililojitokeza kwenye utafiti huu wa TGNP kwenye wilaya tatu, ni upatikanaji wa maji safi na salama. Pamoja na sera ya taifa kwamba maji yawe umbali wa mita 400 kutoka kwa makazi ya watu, bado maeneo mengi hapa Tanzania yana tatizo kubwa la kupata maji safi na salama. Watu wa Kishapu na  Mshewe, ni miongoni mwa wananchi wa Tanzania ambao bado wana tatizo hili kubwa. Kijiji cha  Ilota- Mshewe, wananchi wanalazimika kuchangia maji machafu na mifugo. Tatizo hili la maji sai na salama ni kubwa sana katika vijiji vya Isoso na Lubaga katika kata ya Kishappu, wanawake wanatembea mwemdo mrefu na katika mazingira hatarishi kutafuta maji; mazingira haya yanasababisha mimba za utotoni, ubakaji na vipigo kwa wanawake wakichelewa kutoka kuchota maji. Na nyongeza ni kwamba muda mwingi na rasilmali vinatumika kusaka maji kitu kinachoongeza hali ya umasikini katika jamii ya watu hawa Kishapu.
Ukosefu wa huduma bora za afya ni suala jingine lililoibuliwa na mpango wa utafiti shirikishi wa uraghabishi. Mfano kati  ya wanawake 20 walihojiwa katika kijiji cha Ilota, Mbeya vijijini ni mwanamke mmoja tu ndiye aliyetaja kujifungulia hospitali. Umbali wa hospitali na vituo vya afya unawalazimisha wanawake wengi kuzalia nyumbani kwa wakunga wa jadi. Hii ni hatari kwa mama na mtoto na kuna ukweli wa wanawake wengi kupoteza maisha wakati wa kujifungua na watoto kutopata huduma muhimu za chanjo wakiwa na umri chini ya miaka 5.
Kata ya Kisaki Morogoro vijijini, tatizo si hospitali wala kituo cha afya, tatizo ni dawa na wahudumu wa afya katika vijijini vya Gomero, Station na Nyarutanga. Vijiji hivi vina majengo mazuri, lakini hakuna dawa na wahudumu. Mbali na tatizo hilo, pia inapobidi wananchi wanachangia gari la wagonjwa silingi 70,000, ili kumpeleka mama mja mzito kwenye hospitali ya Mkoa Morogoro mjini. Hali hii ni hatari, maana wanawake wengi wanaweza kupoteza maisha yao kwa kushindwa kulipia hizo shilingi elfu 70,000.
Ukiachia masuala hayo yaliyotajwa hapo juu, utafiti huu wa TGNP, ulibaini kwamba tatizo la msingi ni uongozi mbovu na rushwa. Hili lilitajwa kila sehemu iliyofanyiwa utafiti. Kwamba uongozi mbovu na rushwa vinasababisha ukosefu wa huduma za msingi kwa wanawake na wanaume walioko pembezoni. Na kwamba kuna usiri wa taarifa za mapato na matumizi, viongozi kutowashirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo, viongozi ngazi za vijiji kuruhusu video za ngono na viongozi kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Ni mengi yaliyojitokeza kwenye utafiti huu, ila yametajwa machache ili kufikisha ujumbe kwa wahusika, ili wajaribu kutafuta majibu ya kuondoa unyanyasaji wa wanawake na wasichana katika wilaya hizi zilizotembelewa na watafiti wa TGNP pamoja na maeneo mengine ndani ya taifa letu. Mfano tatizo la maji linasababisha vipigo kwa wanawake, ubakaji, elimu duni kwa wasichana, mimba za utotoni na ukosefu wa kipato.
Serikali kuu na serikali za mitaa zinaweza kuyatumia matokeo ya utafiti huu kurekebisha matatizo yaliyoorodheshwa hapo juu: Mfano serikali kuirejesha ardhi ya Kata ya Mshewe inayomilikiwa na wawekezaji wa n nje na ndani ya nchi, kwa manufaa ya wananchi sasa na vizazi vijavyo. Pia serikali itenge maeneo ya wafugaji katika kata ya Kisaki, ili kuepesha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Huduma ya kupatikana maji safi na salama ishughulikiwe katika vijiji vilivyotajwa na ambavyo havikutajwa. Utafiti huu umeonyesha wazi kwamba maji safi na salama ni muhimu kwa watanzania wote. Huduma ya hospitali pia nayo iboreshwe. Pia ni muhimu kuwepo na mfumo wa kuwawajibisha viongozi wote wanaokiuka maadili ya kazi zao ili kuondokana na aina zote za rusha na ukatili wa kijinsia hasa ukatili kwa wanawake na wasichana.
Lakini pia viongozi wawakilishi hususan madiwani na wabunge wanaweza kutumia matokeo ya utafiti kudai uwajibikaji wa serikali kwa wananchi katika ngazi zote kupita bajeti, ripoti ya mkaguzi wa serikali, kudai sera ya haki ya uhuru wa wananchi na mikakati mbali mbali ya maendeleo.
Vyombo vya habari, taasisi za utafiti na makundi ya kiraia yanaweza pia kuutumia mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi kuibua masuala ya wanajamii na kujenga uwezo wa wanajamii kuhoji na kudai uwajibikaji. Hapana shaka kwamba mpango huu wa utafiti shirikishi na uraghabishi ndio unafaa kabisa kubainisha chanzo cha vurugu za Mtwara. Mpango huu unamruhusu kila mshiriki kuzungumza bila kuogopa na kwa njia hii ya uraghabishi, watu wanajifunua na kujiweka wazi.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net

Nani anajali?

MTOTO WA AFRIKA, NI NANI ANAJALI?
 
Kauri mbi ya siku ya mtoto wa Afrika mwaka huu inasema: “Kuondoa Mila zenye kuleta madhara kwa watoto: Ni jukumu letu sote”. Tarehe 16.6.2013, kama kawaida ilikuwa ni siku ya Mtoto wa Afrika .Baadhi ya watu wameikumbuka, lakini inaelekea moto wake unaendelea kupunguka na kubakia ni siku ya watoto wa shule, kukutana na kuimba nyimbo, kucheza ngoma na maigizo. Watu wazima wanaanza kuikwepa siku hii. Jana kwenye taarifa za habari ilionekana asilimia kubwa ya watoto na asilimia ndogo sana ya watu wazima. Pamoja na jitihada za kuikwepa siku hii ukweli unabaki pale pale kwamba yaliyotokea Soweto miaka hiyo yanaweza kutokea tena popote kwenye nchi hizi za Kiafrika na Tanzania ikiwemo. Matendo ya ukiukwaji wa haki za watoto ikiwemo na uporaji wa ardhi yamekuwa mengi. Binafsi nimejenga utamaduni wa kuandika makala kila tunapoikumbuka siku hii ya mtoto wa Afrika. Ninaamini mchago wangu huu unaweza usiwanufaishe watanzania wa leo, lakini kama wasemavyo kwama “Kilichoandikwa kimeandikwa” ni imani yangu kwamba mchango wangu utawanufaisha hata watanzania wa kesho. Na ndiyo maana nimeamua kuuliza katika makala haya: Mtoto wa Afrika, ni nani anajali?
 
Kauri mbiu ya mwaka huu ni mwiba mkubwa kwetu sote. Tuna mfumo gani wa kuondoa mila zenye kuleta madhara kwa watoto wetu? Tuna mfumo gani wa kutokomeza uporaji wa ardhi, tuna mfumo gani wa kuwaambukiza watoto wetu moyo wa uwajibikaji na uzalendo? Tuna mfumo gani wa kujenga mila zenye ustaarabu na kuachana na mila za kishenzi kama zile zinazoanza kujitokeza katika jamii yetu: Watu wanapigwa wanaumizwa na wengine wanauwa, watu wanasingiziwa na kubambikiziwa kesi; wanaotenda matendo haya ya kinyama bado wanaendelea kudunda na kupandishwa vyeo. Tuna mfumo gani wa kuwafundisha watoto wetu kusema ukweli? Kuwa waaminifu, kuacha uchakachuaji, kuacha tabia ya kuuza bidhaa bandia. Tuna mfumo gani wa kufundisha uadilifu? Elimu mbovu ni kujenga mila zenye kuleta maafa! Tumeshuhudia watoto wetu wakishindwa vibaya, tumeshuhudia watoto wetu wakifundishwa kwa kutumia vitabu bandia ambavyo havina viwango: Alimu mbovu ni maafa matupu!
 
Mnamo mwaka 1976, Kule Soweto, Afrika ya kusini, maelfu ya watoto weusi wa shule waliingia mitaani na kufanya maandamano ya zaidi ya nusu kilomita, wakipinga elimu duni waliyokuwa wakiipata na kudai kufundishwa kwa lugha yao. Walifanya maandamano ya amani kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa serikali ya makaburu. Ujumbe huu ulikuwa mchungu kwa wakubwa na hawakuwa tayari kuusikiliza. Kama kichaa anavyoweza kutumia bunduki kuua mbu, ndivyo makaburu walivyofanya kwa wanafunzi hao. Mamia ya wasichana na wavulana walipigwa risasi na kupoteza maisha yao.  Kwa vile bunduki inaua mwili, lakini fikra na roho vinaendelea kuishi, maandamano hayo hayakuzimwa kwa risasi! Machafuko yaliyofuatia tukio hili yalipoteza maisha ya mamia ya watu na kuacha majeruhi kadhaa.
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshuhudia matatizo mengi ya watoto. Tunashuhudia watoto wetu wanavyosukumwa kila siku kwenye daladala, watoto wanavyosoma kwa shida, shule za msingi wengine wanakaa chini, sekondari wanasoma bila kuwa na walimu wa kutosha, matokeo yake  wanafanya vibaya na kushindwa kuendelea na masomo ya juu. Lakini pia na wale wanaofanikiwa kuendelea na masomo ya juu, tunashuhudia wanavyonyanyaswa na Bodi ya mikopo. Tunashuhudia watoto wetu wakikoswa ajira, tunashuhudia watoto wetu wakibugia dawa ya kulevya, wakilewa pombe, wavulana wakisuka nywele na kujifananisha na wasichana, wasichana wakitembea nusu uchi na baadhi ya watoto wetu wakiikimbia nchi kwenda kuishi ughaibuni.  Kwa asilimia kubwa maisha ya mtoto wa Kitanzania, yanakuwa ni ya shida.
 
Binafsi, nimeamua mwaka huu niandike juu ya Mtoto wa Afrika  na uporaji wa ardhi na mtoto wa na elimu mbovu. Kwanini, nimeamua kuandika hivyo: chanzo cha siku ya mtoto wa Afrika, ni maasi yaliyofanywa na watoto wa Soweto, kwa kukataa kunyanyaswa. Walikuwa wakipata elimu duni ukilinganisha na ile ya Wazungu. Pia, walitaka elimu inayotolewa kwa lugha yao. Kule Soweto, watoto walianza kutambua kwamba wale waliokuwa wakifundishwa katika shule nzuri ndio waliokuwa wakipata kazi nzuri na vyeo vya juu katika serikali. Hali ya kutamani hali bora ya maisha kwa siku za mbele, hali ya kutaka kuwa na vyeo na nafasi nzuri za kazi, iliwafanya wanafunzi kukataa elimu duni waliyokuwa wakiipata. Hawakuogopa nguvu za jeshi la Makaburu. Walikuwa tayari kupambana bila silaha – na kweli wengi wao walipoteza maisha. Watoto wa Soweto, walitambua kwamba kujifunza kwa lugha za kigeni wasingepata maarifa yenyewe. Walitaka wafundishwe kwa lugha ya kwao, lugha inayofanana mazingira yao, lugha inayogusa maisha halisi, lugha inayoweza kuharakisha maendeleo. Hoja yangu ni kwamba Bila kuwa waangalifu, inawezekana na sisi hapa Tanzania, tunaandaa Tanzania ya kesho yenye maasi kama ya Soweto.
 
Bila kuwa na elimu nzuri na bora, watoto wetu wakasoma na kupevuka kifikra6/15/2013, tutakuwa tunajiandalia majanga ya Soweto; bila kuwa na ardhi ya kuwarithisha watoto wetu tunakuwa tunaliandalia taifa letu migogoro na majanga ya Soweto.
 
Kumetokea wimbi la uporaji wa ardhi. Watu wenye fedha wananunua ardhi kubwa kwa kisingizio cha kuwekeza. Matokeo yake vijana wengi watajikuta hawana ardhi na wataikataa hali hii. Na tunavyosikia kwenye vyombo vya habari sehemu nyingine hali hii imekataliwa mapema. Tunasikia kule Manyara jinsi watu wanavyovamia mashamba, kukata mazao na kuwashambulia wanao miliki mashamba. Tukio la Tegeta, la kukatana mapanga katika harakati za vijana kufukuzia mbali waporaji wa ardhi, ni la kusikitisha na kutafakarisha; na ni fundisho pia kwamba vijana wakiamua kudai ardhi yao, patachimbika.
 
Mgogoro wa ardhi wa Loliondo, tumeshuhudia jinsi ulivyovuruga amani kwenye maeneo hayo na kupanda mbegu ya maasi na chuki kwa vizazi vijavyo. Mashirika mbali mbali yasiyokuwa kiserikali yamepiga kelele juu ya suala hili la uporaji wa ardhi, lakini kelele hizi zimekuwa kama ile sauti iliayo nyikani. Mashirika haya yamekuwa yakijitahidi kutengeneza majukwaa ya majadiliano, ili watanzania tukae pamoja na kujadiliana juu ya uhai wa taifa letu.
 
Ardhi ni muhimu sana kwa maisha yetu ya leo na vizazi vijavyo; uchumi wetu unategemea kilimo; bila ardhi hatuwezi kulima, hatuwezi kupata chakula na mazao ya kuuza na kujipatia fedha za kigeni. Hivyo ni muhimu sote kusimama pamoja kupinga wimbi hili kubwa la kupora ardhi yetu. Tuhakikishe kila Mtanzania ana ardhi yake ya kutosha na kupiga vita kwa nguvu zote ardhi kuwa mikononi mwa watu wachache.
 
Tunapoikumbuka siku mtoto wa Afrika, ni bora tukazingatia umuhimu wa ardhi kuwa ustawi wa mtoto wa Afrika. Tukiilinda ardhi yetu leo, tunaepusha machafuko ya ardhi kesho na keshokutwa.  Pia tunapoikumbuka siku ya  mtoto wa Afrika ni muhimu sana kutambua elimu  bora kwa watoto wetu italiepusha taifa letu na wimbi kubwa la machafuko. Hivyo basi, Mtoto wa Afrika, ni nani anajali? Ni mimi? Ni wewe, ni yeye? Ni wao au ni sisi sote! Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki watoto wote wa Afrika.
Na,
Padri  Privatus Karugendo.
+255 754 633122

Tujifunze kutoka kwa Mandela



TUJIFUNZE KUTOKA KWA MZEE MANDELA

Wakati dunia nzima inaendelea kumwombea Mzee Mandela, apate afya njema na kupona ugonjwa uliomlaza kitandani zaidi ya majuma mawili sasa, ni lazima watanzania tujifunze kutoka kwake. Mzee Nelson Mandela, ni kati ya watu wachache waliofanikiwa kuyaishi na kuyashika mafundisho magumu. Mafundisho ambayo waliowengi tunayaita ndoto, lakini tunayafundisha na kuwahimiza watu wengine wayashike na kuyafuata.Alipohukumiwa kifungo cha maisha,Mzee Mandela, alipokea hukumu hiyo bila ya woga, ni kitu alichokifahamu hata kabla ya kuanza mapambano na serikali ya makaburu. Alifahamu nguvu na uwezo wa serikali ya makaburu. Alijua walivyokuwa wameshikilia vyombo vya dola na silaha nzito nzito, alijua angekamatwa na kufungwa au kuuawa.Pamoja na kuyajua yote hayo aliamua kuendelea kupambana na makaburu kwa vile alitanguliza uhai wa taifa lake na wala si uhai wa maisha yake binafsi. Lakini pia alijua jinsi nguvu na uwezo wa makaburu vilivyokuwa vinaishia kwenye kuutesa mwili wake bila ya kuwa na uwezo wa kuigusa roho yake hata hivyo mafundisho magumu ambayo roho yake haikuwa na uwezo wa kuyakwepa yalikuwa mbele ya macho yake:
 “ Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho..” (Matayo 5:28).
Makaburu waliutesa mwili wa mzee Mandela, alifanyishwa kazi za suluba,alidhalilishwa,alipokonywa uhuru wake,alinyimwa uhuru wa kuwa na familia yake,alinyimwa uhuru wa mawasiliano, alipofiwa na mtoto wake wa kiume, alinyimwa ruhusa ya kuhudhuria mazishi yake. Unyama wote aliofanyiwa akiwa gerezani uliugusa na kuutesa kwa kiasi kikubwa mwili wake tu,lakini roho yake ilibaki madhubuti. Alipochaguliwa kuwa Rais wa kwanza mwafrika wa Afrika ya kusini huru, Mandela, alimshangaza kila mtu pale alipowakumbatia adui zake na kukaa nao meza moja ya chakula. Hakulipiza kisasi! Unyama aliotendewa gerezani,haukuigusa roho yake! Mzee Mandela, amekuwa mwalimu wa kuwafundisha watu kuishi na kuyashika mafundisho magumu, mambo ambayo tumezoea kuyaita ndoto.Watanzania tuna utamaduni wa kuogopa mwenye nguvu na uwezo wa kuua mwili.Pia tuna utamaduni wa kulipa kisasi, wawe ni viongozi wa dini au viongozi wa serikali,tabia hii ipo. Tujifunze kwa Mzee Mandela: Mwili unateswa, unanyanyaswa na kudhalilishwa na mwanadamu, lakini roho ya ukweli, amani na wema viko juu ya uwezo wa mwandamu! Hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kuiua roho ya wema, hata kama mtu huyo angekuwa na nguvu za kidunia kama za Amerika!Pia tujifunze kwamba ukipambana na mtu, ukimshinda, mnashikana mikono na kukumbatiana – si kujenga chuki wala uhasama!

 Watu wanaouona mwanga huu wameanza kugundua kwamba yale tunayoita mafundisho magumu na ndoto yanawezekana, Mzee Mandela, ametuonyesha mfano:
Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino’. Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la pili..” (Matayo 5:38-39).
 Haya ni mafundisho magumu ambayo yamewashinda watu wengi hata na wale walioyafundisha na kuyaeneza. Hadi leo hii hata viongozi wa dini bado mafundisho haya yanawapatia shida. Bado wanashikilia ‘Jicho kwa jicho, na jino kwa jino’. Migogoro inayowakumba viongozi  wa dini inasababishwa na kutokubali kupigwa shavu la kulia, na kugeuza la kushoto. Wakipigwa kofi, wanarudisha. Hii inavuruga amani na kuleta magomvi yasiyoisha. Mandela, hakurudisha kofi! Alisamehe! Mafundisho magumu yalikuwa mbele ya macho yake na roho yake iliyoandaliwa kwa umakini na kwa miaka mingi haikuwa na uwezo wa kuyakwepa:
Mmesikia kwama ilisemwa:  ‘Utampenda jirani yako, lakini utamchukukia adui yako.’ Lakini mimi nawaambieni,wapendeni maadui wenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi…” ( Matayo  5:43-44).

Tunakumbuka jinsi Mzee Mandela, alivyowashauri wamarekani:  “Tumejifunza jinsi ya kuishi na maadui zetu, nanyinyi mjifunze kuishi na maadui zenu..”

Tume ya maridhiano ya Afrika ya Kusini, ilifanya kazi kwa uhuru na kumsikiliza kila mtu. Haikuwa na upendeleo wala kukikumbatia chama tawala. Haki ilitendeka kwa kila mwanachi na watu wote walifurahia kazi yake.Hizo zilikuwa mbinu za Mzee Mandela, za kukumbatia mafundisho magumu ya kumpenda adui.

 Mzee Mandela, alipompoteza mtoto wake wa kiume kwa ugonjwa wa UKIMWI, kwa masikitiko makubwa(maana huyu ndo mtoto pekee wa kiume aliyekuwa amebakia) alitangaza wazi mbele ya vyombo vya habari bila aibu kwamba mtoto wake alikufa kutokana na ugonjwa wa UKIMWI. Hapa pia mafundisho magumu ambayo roho yake haikuwa na uwezo wa kuyakwepa yalikuwa mbele ya macho yake:
Jihadharini na chachu ya Wafarisayo, yaani unafiki. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila siri itajulikana. Kwa hiyo, kila mlichosema gizani, watu watakisikia katika mwanga, na kila mlichonong’ona, faraghani,milango imefungwa,kitatangazwa juu ya nyumba.” (Luka 12:1-3).
Hili limekuwa fundisho jingine kutoka kwa Mzee Mandela, la mafundisho magumu ambayo wengi wetu na hasa Barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara, tumekuwa tukidhani ni ndoto. Tumezoea kusikia watu mashuhuri wakifa kutokana na shinikizo la damu,kisukari, ugonjwa wa muda mrefu na ugonjwa wa ghafla nk. Ni nadra kusikia mtu mashuhuri amekufa kwa UKIMWI. Ugonjwa huu, umezungukwa na unafiki mkubwa.Ndo maana ugonjwa huu umekuwa wa hatari katika nchi zetu hizi masikini. Ugonjwa unafichwa na unafiki unaendelea kutawala.Hawa watu mashuhuri wanaokufa kwa shinikizo la damu wanatoa mwanya wa wenzi wao kuendelea kusambaza virusi vya UKIMWI, hakuna anayeshughulika kuchukua tahadhari maana shinikizo la damu si ugonjwa wa kutisha kama UKIMWI!! Matokeo yake ni janga kama tunavyoendelea kushuhudia. Ni lazima tumpongeze Mzee Mandela, kwa ujasiri wake na tuendee kujifunza kutoka kwake.

Mzee Mandela, alipougua ugonjwa wa saratani ya kibofu cha mkojo, alitangaza wazi. Hakuficha ugonjwa wake.Alipatiwa matibabu, na sasa anaendelea kuishi! Hapa Tanzania, tumewapoteza watu wengi kwa ugonjwa huu kwasababu ya aibu na unafiki! Pia watu wanakufa kwa kuficha magonjwa ya zinaa yanayotibika kwasababu ya aibu na unafiki. Magonjwa yakigusa sehemu za siri, watu wanakuwa na aibu.Aibu hii inatokana na mawazo ya kulichukulia tendo la ngono kama la aibu. Ingawa kuna ukweli kwamba si magonjwa yote yanayozishambulia sehemu za siri yanasababishwa na tendo la ngono. Baadhi ya watu wakiugua sehemu za siri, wanataja kichwa,tumbo na mgongo. Madaktari wanatibu kichwa,tumbo na mgongo, kumbe mgojwa ana saratani ya kibofu cha mkojo au magonjwa mengine ya zinaa. Inapotokea bahati ya kuugundua ugonjwa,mgonjwa anakuwa amezidiwa na kufa! Aibu na unafiki vinasababisha vifo visivyokuwa vya lazima katika taifa letu na katika nchi nyingine za Kiafrika.


                                                                                 
Lengo la makala hii ni kuonyesha jinsi tulivyo na mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mzee Mandela. Bahati mbaya viongozi wetu wa dini na serikali ni woga. Hatujapata viongozi wa kuyashika na kuyaiishi mafundisho magumu kama alivyofanya Mzee Mandela. Hatujapata viongozi wasiogopa macho na masikio ya watu, viongozi wasiojali kudhalilishwa na ikibidi kuupoteza uhai wao katika harakati za kutetea ukweli na kupingana na unafiki.

Tunapojifunza kutoka kwa Mzee Mandela, ni lazima tumwangalie yeye na historia yake. Si kwamba misimamo yake hii ya kuishi na kuyashika mafundisho magumu, ilimnyeshea kama mvua. Ni mtu aliyefanya  maandalizi, ni mtu aliyeitafuta elimu akiwa na malengo katika maisha yake – hakusoma tu kwa vile kusoma ni lazima – hakusoma kuishinda maitihani, bali alisoma kwa vile alikuwa na lengo la kuikomboa nchi yake. Lengo hili lilijaa kwenye roho
yake. Hata ungeupiga na kuumiza mwili wake, usingeliligusa lengo lililokuwa kwenye roho yake.Alijiandaa kwa maamuzi magumu –alijua jinsi njia ya kulifikia lengo lake ni kupitia kwenye maamuzi magumu. Alijifunza na kujiandaa kulitanguliza taifa lake kwa kila kitu. Hakuaangalia tumbo lake,cheo chake au biashara yake (mambo ya mwili) aliangalia uhai wa taifa zima(mambo ya kiroho) . Mungu amsaidie, hata uhai wake ukiondoka, tutaendelea kuishi na roho yake.
Na,

GAIDI NI NANI?

 
SWALI LANGU KWA RAIS OBAMA: GAIDI NI NANI?
 
Juzi nilikutana na mtu wa kawaida kwenye mitaa, akaniambia yeye hafurahishwi na ujio wa Baraka Obama, maana rais huyu anakuja Tanzania kufuatilia maslahi ya Amerika. Na mwingine akaniambia Raisi Obama, anafuatilia nyendo za China, na kasi kubwa ya China kushirikiana na nchi zinazoendelea. Kuna wengine walioniambia kwamba Obama, ataleta neema kubwa Tanzania. Kila mtu ana mawazo yake juu ya ujio wa Obama Tanzania. Kule Afrika ya kusini, tumeshuhudia wanafunzi wakiandamana kwa mabango kupinga ujio wa Rais Baraka Obama, kwenye nchi yao. Tunaweza kusema ujio wa Obama katika nchi za Afrika, utapokelewa kwa hisia tofauti. Pamoja na ukweli kwamba Obama ni mwana wa Afrika, bado kuna ukweli kwamba yeye kama Rais Amerika, ujio wake ni nguvu za Amerika na sera za Amerika. Na tujuavyo Amerika iko mstari wa mbele kupambana na ugaidi unaofafanuliwa kwa misamiati ya kimarekani.
Ningepata bahati ya kukutana Rais Obama, bahati ambayo ni ndoto za mchana, ningemuuliza swali langu moja: Gaidi ni nani? Sina lengo la kuutetea ugaidi kwenye makala hii, ninajua ugaidi ni mbaya, unawagusa waliomo na wasiokuwemo; usumbufu wa kusafiri nchi za nje unatugusa sote, mtu ukipanda ndege unakuwa na wasi wasi, ukiwa kwenye majengo makubwa na kwenye mkusanyiko wa watu roho haitulii! – hakuna aliye salama mbele ya ugaidi na hasa ugaidi huu wa kulipua ndege na majengo. Ninachofanya kwenye makala hii ni kuwataka wasomaji wangu  tutafakari juu ya Ugaidi. Ukienda Afghanistan na Iraq, watu watakwambia gaidi ni Osama au ni Wamarekani? Wakati Afrika ya Kusini ikipigania uhuru wake, Mandela, alikuwa ni gaidi namba moja. Hata kule Kenya wakati wa huru, wapiganaji wa Mau Mau, walijulikana kama Magaidi. Hivyo kila mtu anaweza kuwa gaidi kutegemeana na nyakati na mapambano yaliyopo. Ndo maana ningetamani sana kusikia Mheshimiwa rais Obama, ana jibu gani kuhusu gaidi! Yeye kwa maoni yake gaidi ni nani?
Kuiingilia nchi huru kijeshi kama Amerika ilivyofanya kule Pakistan katika harakati za kumwangamiza Osama, ni ugaidi au ni kitendo chenye baraka zote kwa vile ninalenga kuyalinda maisha ya watu wenye thamani kubwa hapa duniani? Kitendo hicho kingefanywa na nchi nyingine kingelaaniwa kwa nguvu zote. Kwa vile kimefanywa na kiranja wa dunia, sote tunafyata mkia na kushangilia.
Je ugaidi ni njia mojawapo wa wanyonge kutetea haki zao? Ugaidi ni njia mojawapo ya kupigania uhuru na haki ya kujitawala? Mwenye nguvu kubwa kama ilivyo Amerika njia pekee ya kupambana naye ni ugaidi? Inawezekana Osama, alikuwa akiwatetea wanyonge? Bila kutaka kuingia sana kwenye mjadala wa ugaidi na ugaidi ni nini, niendeleze swali langu kwa Raisi Obama. Gaidi ni nani?: Je kifo cha Osama kitamaliza ugaidi duniani? Kwamba baada ya yeye kufa hatusikii tenda vitendo vya kigaidi? Bila kuwa na dunia yenye haki na usawa; dunia ambayo kila mtu anaruhusiwa kuishi na kuheshimiwa; dunia ambayo binadamu wote tunatumia rasilimali kwa usawa; dunia ambayo haina ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa dini ugaidi utakwisha?
Kwa Amerika Osama, alikuwa gaidi na kwa watetezi wa haki za Waislamu, Osama alikuwa shujaa na mtetezi wa wanyonge. Wakati Wamarekani wanashangilia kifo cha Osama; kinyume kabisa na utaratibu wa maisha ya mwanadamu, maana tumefundishwa kupenda adui na kutoushangilia msiba wa mwenzio, Pakistan maandamano yanaendelea kupinga mauaji wa Osama. Maana yake ni kwamba uelewa wa Ugaidi kwa Wamarekani, ni tofauti kabisa na uelewa wa ugaidi kwa watu wa Pakistan na nchi nyingine ambazo bado ziko kwenye harakati ya kujikomboa kiuchumi na kupiga hatua ya maendeleo.
Dunia nzima inapigana na ugaidi. Inataka kutokomeza ugaidi. Kusema kweli hata na mimi ugaidi siupendi kabisa. Ugaidi unawaingiza waliomo na wasiokuwemo, unapoteza maisha ya watoto wadogo na watu wema na wapenda amani.  Hatuwezi kufanikiwa kupambana na ugaidi kama hatukubali kufutilia mbali mawazo potofu kwamba kuna binadamu bora kuliko wengine. Kama hatukubali kufuta mawazo kama ya le ya Hitler, kwamba kuna kitu kama “Royal Blood”. Watoto wa Gaza, wanaoshuhudia unyama wa leo unaofanywa na Waisraeli, hawezi kulifuta hili akilini mwao mpaka pale watakapokuwa na kushika bunduki au kuvaa mabomu na kwenda kulipiza kisasi kwa kujilipua.
 
Obam, alipoitembelea Israeli, alisema hata yeye hawezi kumvumilia mtu anayerusha makombora kuelekea walikolala mabinti zake wawili. Hivyo hivyo hakuna mtu yeyote duniani anayeweza kuvumilia kuona maisha ya watoto wake yakiteketea. Hata Wapalestina hawawezi kuvumilia hilo. Hakuna mtu anayeweza kuvumilia hilo; kama hana nguvu za kutosho atajaribu kutumia mbinu zozote zile kuyalinda maisha ya watoto wake, maisha yake binafsi na maisha ya watu wengine wanaomzunguka. Inawezekana mbinu hizi zikawa na sura ya ugaidi, lakini kwa vyovyote haziwezi  kuwa na tofauti kubwa na yule anayetumia nguvu za kijeshi kuyalinda maisha ya mtoto wake au watu wake.
 
Waisraeli, wanasema wanawalinda watu wao. Kama wao wana haki ya kufanya hivyo, kwa nini na Wapalestina wasiwe na haki ya kuwalinda watu wao. Rais wa Amerika, Mheshimiwa Barack Obama, anasema Amerika, itashirikiana na kila mpenda Amani. Ni imani yangu kwamba dunia nzima inapenda Amani. La msingi ni kuhakikisha kwamba tunayatumia yote tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa usawa. Tunaitutumia ardhi kwa usawa na kuyalinda mazingira kwa pamoja, tunatumia chakula kwa usawa na kuhakikisha kwamba hakuna anayekufa kwa njaa, vinginevyo njaa inaweza kuvunja amani, wanaokufa kwa njaa wanaweza kushawishika kuchukua silaha ili kupambana na wenye chakula kingi. Tutumie maji kwa usawa, vinginevyo vita mbaya inayoweza kutokea huko mbele ni kugombania maji. Hadi leo hii kuna sehemu hapa duniani ambako maji yanavunja amani. Kwa ufupi ni kwamba tutumie rasilmali za dunia hii kwa usawa. Maana yake ni kwamba, Obama, asishughulike tu na usalama wa Amerika, bali atafute chanzo cha  yale yanayoweza kuvunja usalama si wa Amerika peke yake bali wa dunia nzima. Dunia ikiendelea kugawanyika kwenye makundi ya walionacho na wasiokuwa nacho, wenye madaraka makubwa na wanyonge, wenye damu safi na wenye damu chafu, wenye dini bora na wenye dini duni, wenye rangi bora ya ngozi na wenye rangi duni, wenye haki na wasiokuwa na haki, itakuwa ni ndoto kujenga Dunia yenye amani. Kama Obama, anasimamia mabadiliko, kama kauli mbiu yake katika kampeni na katika utawala wake – ni lazima ahakikishe mabadiliko ya kweli yanakuja si Amerika peke yake, bali dunia nzima. Mwenyezi Mungu, alituumba tufaidi kila kilicho hapa duniani kwa usawa!
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

NDOA YANGU NINGEJUA

UHAKIKI WA KITABU:  NDOA YANGU “NINGEJUA.....!”
 
1.     Rekodi za Kibibliografia.
 
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni NDOA YANGU ‘Ningejua...!’, Kimeandikwa na Charles B Misango. Kitabu hiki kina namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 433 022. Kitabu kina kurasa 109 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
 
II. Utangulizi
 
Kitabu hiki kinaitwa Ndoa Yangu Ningejua...!  Haina maana kwamba mwandishi anaandika juu ya ndoa yake, bali kwa vile ameamua kuandika juu ya ndoa anataka kila mtu aichunguze ndoa yake na yeye akiwemo. Kwa maoni ya mwandishi kama angeandika “Ndoa yako” au “Ndoa zenu” ingekuwa sawa na kuwanyoshea wengine kidole kana kwamba ndoa yake haina changamoto zozote zile. Ni Ndoa yangu... tunaiboresha vipi? Au tuseme: Ndoa yangu, Ningejua....  ningeiboresha au ningefanya chaguo zuri? Au ningezingatia maadili na busara ya kuiongoza ndoa; kuwaunganisha watu wawili ni kazi kubwa ambayo bila uvumilivu na kuchukuliana ni muungano wenye mashaka!
 
Lengo kubwa la mwandishi ni kumwalika kila mwenye ndoa kuichunguza ndoa yake na kutafakari kwa kulinganisha na yale anayoyaandika mwandishi katika kitabu hiki. Msukumo wa kuandika kitabu hiki umetokana na ukweli kwamba siku za hivi karibu na hasa kwenye Jiji la Dar-es-Salaam, ndoa nyingi zinafungwa na sherehe kubwa zinafanyika kwenye kumbi mbali mbali, na jinsi ndoa nyingi zinavyofungwa kwa mbwe mbwe ndivyo ndoa hizo zinavyovunjika na nyingine zinakuwa na changamoto, vurugu na migogoro nyingi baina ya familia za bwana harusi na bibi harusi.
 
Kosa liko wapi? Kwa nini hakuna amani kwenye ndoa?  Tumekosea wapi kama jamii? Haya ndiyo maswali ambayo mwandishi anajaribu kuyajibu baada ya kufanya utafiti wake na kuwahoji watu mbali mbali wenye ndoa.
 
Mwandishi wa kitabu hiki ambaye pia ameoa, maana kwenye shukrani anasema hivi: “ Shukrani za pekee zimwendee MKE WANGU ambaye kwa maisha yake, amenisaidia pasipo yeye mwenyewe kujua, jinsi maisha ya ndoa yanavyoweza kubadilika kutoka namna mmoja hadi nyingine na njia ya kukabiliana nayo”. Kwa wengi mwandishi huyu anajulikana kama MC Kibonge, ingawa ni mwembamba kwa maana ya neno hilo – labda kwa vile mambo yake ni ya “Ubonge bonge” kama alivyoandika kitabu hiki juu ya ndoa. Huyu ni mwandishi aliyebobea na kwa wale wanaosoma gazeti la Tanzania Daima watakuwa wanakutana safu yake ya Nani anajali..., Alifanya kazi kwenye gazeti la Kiongozi na sasa ni mmoja wa wahariri wa gazeti la kila siku  la Tanzania Daima.
 
 
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
 
 
Nitafanya uhakiki wa kitabu hiki, lakini kwanza kwa kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Mwandishi alifanya utafiti juu ya maisha ya ndoa na dodoso lake lilikuwa na maswali kwa wenye ndoa, matokeo yake ndio yalimsukuma kuandika kitabu hiki. Nina imani kama angekutana na majibu chanya, asingeweza kupoteza muda wake kuandika kitabu hiki. Kwa ufupi tu, tutayaangalia baadhi ya maswali:
 
Swali la kwanza kwa wanawake: Kama ungejua Mumeo atakuwa na tabia alizonazo sasa ungekubali akuoe? Jibu lilikuwa ni ama Ningekubali au Nisingekubali.  Wanawake 93 kati ya 100 waliofunga ndoa ya kanisa, walisema kuwa wasingekubali kuolewa. Watano walisema wangekubali, wakati wawili waliobaki walisema kuolewa ama kutoolewa kwao yote sawa. Lakini hata wale watano waliokubali walipotakiwa waseme msingi wa kukubali kwao, baadhi ya majibu yao yalisitisha. Watatu kati yao walisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwa waume zao wanawapenda na ni waaminifu na wa kweli kati ndoa zao.
 
Swali hilo hilo waliulizwa wanaume, na majibu hayakuwa tofauti sana, maana wanaume 79 kati ya 100 walihojiwa walisema wasingekubali kuwaoa wanawake hao kama wangefahamu tabia zao, ni 12 tu ndio waliosema wangekubali kuwaoa.
 
Swali la pili kwa wanandoa lilikuwa: Je, Umeoa/kuolewa na Mtu uliyemtaka; Ni chaguo lako halisi. Hapa jibu lilitakiwa Ndiyo au hapana. Ukweli uliojitokeza ni kwamba wengi wamefunga ndoa na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati. Wanaume 49 kati ya 100 yalisema walifunga ndoa na watu ambao hawakuwataka na wanawake 73 walisema waliolewa na wanaume ambao hawakuwa chaguo lao. Kwa lugha nyingine ,ndoa 120 kati ya 200 zilifungwa pasipo hiari wala upendo wa dhati wa wanandoa wenyewe.
 
Utafiti huu umebaini sababu nyingi za kuwalazimisha watu kuolewa bila upendo wa kweli, na sababu hizo ni kama vile Kukosa uaminifu wakati uchumba, Kupata ujauzito bila kutarajia na kulazimika kuolewa na huyo aliyekupatia ujauzito na wakati mwingine kulazimishwa na wazazi.
 
Matatizo katika ndoa yanasababisha ndoa kuvunjika, lakini wakati mwingine ndoa inaendelea hivyo hivyo kwa matatizo. Mtafiti alichunguza na hili pia kutaka kujua:  Sababu gani zinakufanya Uendelee kuishi na Mkeo/Mumeo hadi sasa? Ni watoto? Ni kwa vile ndoa ya kidini? Ni kuogopa laana za wazazi? Ni kuvumilia, Ni upendo? Au ni kuishi kwa mazoea?
 
Wanawake 9 katika ya 100 waliohojiwa walisema wanaishi kwenye ndoa hata kama ina matatizo kwa sababu ya upendo kwa waume zao. Na 4 kati ya hao wanasema pamoja na ukatili wanaoupata katika ndoa zao bado wanaendelea kuwapenda waume zao. Wanawake 86 katika 100 walihojiwa walisema wanaendelea kuishi kwenye ndoa kwa sababu ya watoto wao. Ni wanawake 3 tu kati ya 100 walihojiwa waliosema wanaogopa laana ya wazazi wao.
 
Kwa upande wa wanaume ni kwamba 16 kati ya 100 aliohojiwa walisema pamoja na matatizo kwenye ndoa wanawapenda wake zao na wala hawajuti kuwaoa. Na wanaume 51 walisema ni kwa vile ni ndoa ya kanisa ndio maana wanaendelea kuvumilia matatizo kwenye ndoa zao na wanaume 24 walisema wanavumilia kwa sababu ya watoto. Waliobaki, ingawa majibu hayakufanana sana, lakini maana halisi  ni kwamba kwao kuishi kwenye ndoa au kutokuwa na ndoa ni sawa sawa, wanaishi kwa mazoea tu!
 
Swali jingine la utafiti lilikuwa: Nini chanzo kikubwa cha matatizo katika ndoa?  Je ni kwa kutokuwa  na kipato kizuri pande zote mbili? Au ni wazazi wa pande zote mbili au ni mtu binafsi ndani ya ndoa yake au ni umasikini na kumuasi Mungu?
 
Wanawake 33 kati ya 100 walihojiwa walisema chanzo cha matatizo katika ndoa ni kipato kizuri cha waume zao kinachowafanya wawe na “jeuri” ya kutumia fedha katika starehe na kuiacha familia ikiteseka. Wanawake sita, walisema chanzo ni wazazi wao na 14 walisema chanzo ni wakwe zao. Wanawake saba, walisema marafiki wao wa kike ndio wanasababisha matatizo katika ndoa zao. Kwa bahati mbaya, hakuna mwanandoa aliyekubali kwamba yeye binafsi amechangia kuleta matatizo katika ndoa yake, kila mmoja anajaribu kutafuta mchawi nje ya ndoa.
 
Kwa upande wa wanaume, 13 kati ya 100 aliohojiwa walisema chanzo ni kipato kidogo, hii inasababisha wanawake kuwadharau na vurugu inaanzia hapo. Na wanaume 14 walisema shinikizo la wazazi na hasa mwanamke akichelewa kuzaa ndo chanzo cha vurugu. Katika majibu yote hakuna mwanandoa aliyesema kuwa chanzo cha matatizo ni kuwa mbali na Mungu. Wote wanafikiri wakienda kwenye ibada mara kwa mara wanakuwa karibu na Mungu, hawaangalii ukaribu wa Mungu na maisha yao ya siku kwa siku kwenye ndoa zao.
 
Swali la kizushi, ni kwamba kama talaka ingeruhusiwa mambo yangekuwa vipi? Kusema kweli asilimia 70, wangeomba talaka na kuachana na ndoa zao. Na hili linaonyeshwa na ukweli kwamba wanaume 78 katika ya 100 walihojiwa walikubali kuwa na mahusiano ya kingono nje ya ndoa zao, na wanawake 62 pia walikubali kutembea nje ya ndoa zao.
 
Pia kuna utata wa watoto. Kwa vile siku hizi mtu anaweza kupima DNA, kuna mshangao mkubwa wa kujitokeza; inasemekana kwamba asilimia kubwa ni watoto wa kubambikizwa; wanaume wengi wamekuwa wakiwatunza watoto ambao si wao; ni watoto wa nje. Lakini mtafiti alipoulizia wanaume kuwa na watoto nje ya ndoa asilimia 12, walikubali kuwa na watoto nje ndoa. Na fumbo kubwa linabaki watoto wengi kuwa na baba tofauti na wale wanaojulikana rasmi.
 
Mazingira yanayokizunguka kitabu hiki ni utata katika ndoa, vurugu na magomvi hadi ndoa kuvunjika. Ni kwamba ndoa nyingi hazina amani na hasa ndoa zinazofungwa siku za hivi karibuni hazidumu. Tatizo liko wapi? Tufuatane na mwandishi wa kitabu kuona majibu.
 
IV. Muhtasari wa Kitabu
 
Kitabu hiki kina sura sita, baada ya kutanguliwa na dibaji, shukrani na utangulizi. Dibaji ya kitabu hiki imeandikwa na mheshimiwa Msgr. Padri Deogratias H. Mbiku wa jimbo katoliki la Dar-es-Salaam. Ina maana hiki si kitabu cha mzaha, maana padri huyu ni mgongwe katika Kanisa Katoliki, msomi na mtu anayeheshimika katika jamii. Kukubali kuandika dibaji, ina maana alikisoma kitabu na kuona kinafaa kwenye jamii yetu.
 
Katika dibaji, padri Mbiku, anasema hivi: “ Katika nyanja za dini, jamii, Serikali na siasa, ndoa ni  muhimu sana; kwa sababu bila kuwa na ndoa nzuri na imara, dini, jamii, Serikali na hata siasa zitalegalega na kukosa maadili mema, haki na amani miongoni mwa watu...”. Juu ya mwandishi anasema “ Mwandishi wa kitabu hiki anazungumzia kwa undani na ufasaha sababu za kuvunjika kwa ndoa: sababu za msingi ni ubinafsi, kukosa maandalizi ya kina; binadamu wenzetu; na ibilisi... Lakini mwandishi haachii uchambuzi wake kwenye sababu tu, bali pia anatoa ushauri na rai kuhusu nini kifanyike ili kuboresha ndoa. Hatimaye, anaongelea wajibu wa Kanisa katika kuzishughulikia ndoa ili ziwe msingi imara kwa jamii, dini, Serikali na hata siasa”
 
Utangulizi, umeandikwa na mwandishi mwenyewe. Hapa anajaribu kuelezea kwa undani juu ya kichwa cha kitabu kuitwa “Ndoa yangu”. Hakutaka kusema ndoa yako au ndoa yenu, kwa maana kwamba anapozungumzia maisha ya ndoa kwa vilele na yeye anayaishi maisha hao, hawezi kujiweka kando. Lakini pia anaposema ndoa yangu haina maana kwamba anaongelea ndoa yake mwenyewe. Anataka kila mtu atakapokuwa anakisoma kitabu hicho, aseme “Ndoa yangu, ningejua...”
 
Sura ya kwanza ya kitabu hiki ni Ningejua. Kwa kiasi kikubwa sura hii mwandishi anatoa mrejesho wa utafiti alioufanya juu ya ndoa. Mrejesho wa jumla ni kwamba kati ya watu 200, waliohojiwa, 170 wanajuta kufunga ndoa na wenzio, kama wangejua tabia zao mapema, wangefanya uamuzi mwingine. Kadhalika 122 kati ya 200 waliohojiwa wanakiri kufunga ndoa na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati na hawakuwa changuo lao.
 
Katika sura hii ya kwanza, kutokana na maswali ya dodoso: Kama ungejua mumeo atakuwa na tabia alizonazo sasa ungekubali akuoe, Kama ungejua mkeo atakuwa na tabia alizo nazo sasa, ungekubali kumuoa? Mmeo/Mkeo ni chaguo lako halisi? Tunaona kwamba asilimia kubwa katika ndoa wanaangukia mikononi mwa watu ambao hawakuwatarajia. Mwandishi anatoa  asilimia kuonyesha jambo hili. Na sababu kubwa zikiwa ni kulazimishwa na wazazi, kukosa uaminifu wakati wa uchumba, kupata ujauzito kabla ya ndoa na mambo mengine kama kufuata mali na cheo cha mtu.
 
Pamoja na ndoa kuwa na matatizo bado watu wanaendelea kuishi kwenye ndoa hizo. Asilimia kubwa ya wanawake walihojiwa walisema wanavumilia magumu ya ndoa kwa sababu ya watoto. Si upendo na wala si shinikizo la dini, bali nia watoto. Na asilimia kubwa ya wanaume wanavumilia machungu ya ndoa kwa shinikizo la dini.
 
Pia kwenye utafiti huu, mwandishi naweka wazi kwamba wanandoa wengi wanatembea nje ya ndoa na kuzaa watoto nje ya ndoa zao. Asilimia kubwa wanalifanya suala la watoto wa nje ya ndoa kuwa ni la siri na wengine wanalifichua kwa wenzao wa ndoa. Wanaume wanaongoza kuwa na namba kubwa ya watoto wa nje ya ndoa.
 
Sura ya pili ni swali: Nilikosea wapi?
Katika sura hii mwandishi anajaribu  kuangalia sababu zinazopelekea watu kuangukia kwenye chaguo baya na kujiingiza kwenye matatizo ya ndoa.
Kosa la kwanza ni: Hatukujijua! Ni muhimu mtu kujijua yeye ni nani na aliumbwa kwa ajili gani. Ili mtu afanye uchaguzi mzuri na kumpata mwenzi wa maisha ni vyema, ajijue kwanza. Kwa kujiua, anaweza akawajua na wengine na hatima kumjua ni mtu gani anaweza kuwa mwenzi wa maisha.
 
Kosa la pili ni  kwamba:  Hatukujua wito wetu: “ Kila mtu ameletwa duniani kwa sababu maalumu. Hivyo, si kila mwanaume ama mwanamke alipangiwa maisha ya ndoa kama ambavyo wengi wetu tunadhani..” (uk wa 19). Ka kutetea hoja hii mwandishi naonyesha historia ya watu ambao waliishi maisha yao yote bila kuingia kwenye ndoa na wengine walizaliwa wakiwa matowashi. Ili ndoa iwe ya furaha na amani ni muhimu wanandoa wakatambua wito wao.
 
Kosa la tatu: Tulikurupuka! Kwamba watu wanapotafuta wachumba hawatulii na kuchunguza na kutafakari juu ya wachumba wao: “ Ni kama tulirukia gari lililokuwa katika mwendo bila ujuzi..” (Uk wa 22). Mtu anapomtafuta mchumba kwa lengo la kufunga ndo ni lazima ajipatie muda wa kutosha. Uchumba wa siku moja na ya pili kufunga ndoa ni hatari kubwa.
 
Kosa la nne: Hatukuzijua familia za wenzetu: “ Tulitakiwa kujua historia ya maisha ya familia ya wenzetu kikamilifu. Kujua kama wana maisha ya ajabu kama vile uchawi ama  wapenda ushirikina. Maana kama huyu alizaliwa, akalelelewa katika maisha ya aina hii, uwezekano wa yeye kushiriki matendo hayo ni mkubwa...” ( Uk wa 26).
 
Kosa la tano ni: Hatukuwajua wenzetu:
Ni muhimu kumfahamu mwenzako vizuri kabla ya ndoa. Ni muhimu pa kuwafahamu marafiki zake, kufahamu kama huyu ni msiri au ni muwazi? Na je mlikutana katika mazingira gani? Ni mazingira ya kuruhusu mtu kuwa wazi au ni mazingira ambayo yanaweza kuwa ni shinikizo? Je tulikutana kazini? Tulikutana kanisani au kwenye baa? Kama tulikutana kwenye baa, kesho na keshokutwa tabia kama hiyo inaweza kujirudia.
 
Kosa la sita na saba, ni kutojua uzito wa agano. Maana ndoa ni  agano linalowaunga watu wawili, kwa imani nyingine, hawa wanakuwa kitu kimoja. Si wawili tena bali ni kitu kimoja. Je wanandoa tunajua uzito huu kabla ya kufunga ndoa? Tunatafakari juu ya uzito huu kabla ya kufanya uamuzi?
 
 
Sura ya tatu ni swali pia: Ndoa yangu ni mpango wa Mungu?
Mwandishi, anataka tutafakari juu ya ndoa kama mpango wa Mungu. Tunafunga ndoa kujifurahisha au tunafunga ndoa kuendeleza Mango wa Mwenyezi Mungu wa kupendana na kuzaa kwa lengo la kuujaza ulimwengu?
 
Sura ya nne ni swali jingine: Nani maadui wa ndoa yangu? Katika utafiti uliofanywa, ambao unajadiliwa kwenye sura ya kwanza. Wanandoa walipoulizwa swali hili, wote waliwanyoshea wengine kidole, kwamba maadui wa ndoa zao ni ndugu, wazazi na marafiki. Walishindwa kutaja kwamba adui mkubwa wa ndoa ni wanandoa wenyewe. Kuna suala la kuendeleza utoto katika ndoa. Mtu anafunga ndoa lakini anashindwa kuachana na tabia zake za kitoto; hiki ni chanzo cha matatizo katika ndoa nyingi. Pili kuna suala la kuendeleza ukahaba kwenye ndoa na hiki ni chanzo cha matatizo mengi kwenye ndoa. Kuna tatizo la kunyimana tendo la ndoa; likisababishwa na kutembea nje ya ndoa na wakati mwingine unywaji wa pombe kupindukia. Kuna kauli mbovu kwenye ndoa, ujeuri, majivuno na kudharauliana.
 
Ni wazi hatuwezi kukwepa kabisa ushawishi wa wazazi katika ndoa zetu. Bila uangalifu, uhusiano wa wazazi unaweza kujenga matatizo makubwa katika ndoa zetu. Ndugu, jamaa na marafiki nao wanaweza kuleta matatizo makubwa kwenye ndoa. Na la mwisho ambalo watu wengi wanasahau ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.  Ndoa, ambayo haina msingi wa dini ni vigumu kusimama na kustawi. Hayo ndo maoni ya mwandishi juu ya matatizo yanayozikumbwa ndoa nyingi.
 
Sura ya tano ni swali pia: Tufanye nini sasa?
Mwandishi anasema: “ Kwa sisi tulioingia  katika ndoa, sasa si wakati wa kujihukumu wala kuhukumu wengine. Si wakati wa kujua kama tulikuwa na wito wa ndoa ama hapana. Si wakati wa  kuwashambulia wenzetu kwa mabaya yanayotendeka ama yaliyotendeka siku za nyuma ndani ya ndoa zetu. Si wakati wa kujua iwapo tulifunga ndoana watu wasio wetu wala chaguo la Mungu..”. Kwa maoni ya mwandishi, kila wakati ni wakuanza maisha upya. La msingi ni kumrudia Mwenyezi mungu na kuishi kwa kutekeleza mpango wake. Na la msingi ni kujuta na kuomba msamaha, kuwaomba wenzetu wa ndoa msamaha, kuwaomba watoto msamaha na kuiomba jamii nzima msamaha.
 
Sura ya sita: Wajibu wa kanisa.
Katika sura ya mwisho, mwandishi analigeukia kanisa na kulibebesha mzingo mkubwa wa kulinda na kutunza ndoa. Kwa maoni yake ni kwamba Familia ndiyo msingi wa kila kitu. Msingi wa kanisa, msingi ya jamii. Bila kuwa na ndoa nzuri ni vigumu kuwa na jamii nzuri. Hivyo kanisa lina wajibu mkubwa kuhakikisha ndoa zinakuwa imara na zinadumu.
 
V. TATHIMINI YA KITABU.
 
Nianze kwa kumpongeza Charles B. Misango, kwa kazi hii nzuri sana aliyoiandika. Kusema kweli kazi hii inaburudisha, inasikitisha na kufikirisha. Utafiti wake juu ya ndoa, umeweka ukweli wazi. Na kila atakayekisoma kitabu hiki atakuwa makini kumchangua mwenzi wa maisha.
 
Pili, ni maoni ya baadhi ya watu waliokisoma kitabu hiki:
Fred Jackosn wa  Keko Dar-es-Salaam, anasema “ Kama nisingesoma kitabu hiki na kuamua kufuatilia kwa ukaribu historia ya familia na ukoo wa mchumba wangu, ningejikuta naishi na mtu aliyebobea uchawi. Kitabu hiki kimeokoa maisha yangu” (uk wa 109)
 
Naye Betty wa NMB Makao Makuu Dar-es-Salaam, anasema: “ Huu ni funuo wa ajabu sana katika maisha yangu ya ndoa. Kitabu kimenisaidia sana kujua namna gani kudumisha upendo na amani kati yangu na mume wangu, upi wajibu wangu katika ndoa yangu” (uk 109).
 
Na Peter Mizambwa wa Kisarawe, anasema hivi : “ Kama kuna wachumba watakaokisoma kitabu hiki na kuamua kufuata kile kilichoanikwa, hakika wataamua kuanza upya, maana wengi tumechumbiana kienyeji kabisa...”(Uk 109)
 
Kyaruzi-Rc wa Magomeni, anasema “ Hiki ni kitabu kilichoanika ukweli mtupu wa maisha ya wanandoa wengi. Kitasaidia sana kuamsha akili za wanandoa na kurejesha amani katika ndoa nyingi zilizosambaratika na hata zisizo na amani. Kimetoa pia ukweli juu ya wajibu wa Kanisa kuhusiana na malezi ya wanandoa na kitaokoa wengi”
 
Zainabu Rahab wa Mikocheni, naye anasema “ Kitabu hiki ni kioo halisi cha kila mwanandoa. Ingefaa kila aliye katika uchumba akisome kwa makini ili kupata msaada wa Mungu katika safari  ya uchumba...” (Uk wa 109).
 
Tatu, mwandishi wa kitabu hiki ametuingiza ndani ya tafakuri. Utafiti wake unaonyesha wazi jinsi ndoa nyingi zilivyokuwa na matatizo. Swali la kujiuliza sote ni je, ndoa ni Mpango wa Mungu? Je, Mungu alitaka tuishi kwenye kifungo hiki cha ndoa, au mpango wake ulikuwa ni sisi pia kuishi kama wanyama wengine? Ukiangalia asilimia ya wanandoa wanao kwenda nje ya ndoa zao, unakuwa na mashaka. Na je mbona Mwenyezi Mungu, anaendelea kuumba watu wazuri bila kukoma? Mbona hawezi kuviwekea kizingiti vishawishi ndani ya miili yetu? Yeye si ni Muumba wa vyote? Vinavyoonekana na visivyoonekana? Je ndoa ni tendo la ndoa au ni zaidi ya hapo? Mvuto unaokuwepo kati ya Me na Ke, unaweza kufungiwa tu kwenye ndoa? Mbona hata baada ya mtu kufunga ndoa, bado macho yanaendelea kuona na mvuto unabaki? Mvuto ni dhambi au kuutukuza uumbaji wa Mwenyezi Mungu? Kusifia uumbaji wa Mwenyezi Mungu ni dhambi? Na kusifia mipaka yake ni wapi? Kuona na kuacha? Kuona na kugusa? Au Kuiingia kwenye ndoa? Na tuiingie na wangapi kwenye ndoa? Ndoa ya mke mmoja na mwaume mmoja? Mwanaume mmoja wanawake wengi? Au wanawake wengi mme mmoja? Au maisha ya uhuru bila ndoa, lakini tunatenda tendo la ndoa? Ni upi ni mpango wa Mungu? Ni changamoto!
 
Nne, mwandishi ameonyesha wazi kwamba mara nyingi tunachezea kifungo hiki cha ndoa. Hakuna mafunzo kwa vijana. Tumepuuzia mafundisho yetu ya jando na unyago kiasi kwamba vijana wetu wanatenda na kufuata uzoefu wa kila siku bila kuwa na mafunzo ya maisha.
 
Tano, mwandishi anaonyesha wazi kwamba ndoa nyingi zina siri kubwa; watoto wa nje na nyumba ndogo. Hata wale ambao ni watu wa “Mungu” nao wana nyumba ndogo na watoto wa nje. Mungu, apishe mbali maana kufuatana na utafiti wa kitabu hiki, watu wakiamua kupima DNA, ndoa nyingi zitasambaratika maana watoto wengi watagundulika ni wa kubambikizwa.
 
Sita, kitabu hiki kianzishe mjadala kwenye jamii yetu, ili tutafute mamoja na ushauri wa mwandishi, jibu  la tufanye nini ili ndoa zetu ziwe imara. Tufanye nini ili tufanye uchaguzi mzuri wakati wa kuwatafuta wenzi wa maisha.
 
 
VI. HITIMISHO.
 
Kama kawaida yangu, ningependa kuwashauri watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Ni imani yangu kwamba watajifunza mengi kutoka kwenye kitabu hiki na hasa utafiti uliofanywa na mwandishi.
 
Lakini, pia ningependa kuwashauri wale wote watakaokisoma kitabu hiki watafute pia na vita bu vya Dr. Binagwa, juu ya ndoa. Utafiti wa mwandishi wa kitabu hiki unamwandaa msomaji kuvisoma vitabu vya Dr. Binagwa, ambaye anaandika kwa undani juu ya mahusiano kwenye ndoa. Maana, haitoshi kutaja kwamba kuna suala la kunyimana tendo la ndoa, lakini pia kuna maelezo juu ya tendo lenyewe na sababu za kufikia hatua ya kunyimana.
 
Dr.Binagwa, anafafanua vizuri hata juu ya tendo lenyewe. Haitoshi tendo tu, bali kuna namna ya kutenda  tendo hilo. Hivyo kuna mengi juu ya ndoa, na kwa kusoma vitabu hivi, mtu atagundua kwamba ndoa ni kitu kipana ambacho bila mafunzo ni vigumu kukiishi. Ndoa zinavunjika kwa vile sote tumepuuzia suala la kufundisha juu ya ndoa. Ni muhimu kurudisha mafundisho ya Jando na Unyago. Pia ni muhimu kusoma na vitabu vya Jando na Unyago, ambavyo zamani tulivisoma tukiwa sekondari.
 
Mwisho ni ushauri kwa mwandishi, kwamba sasa ana kazi ya kufanya.  Yeye pia ni lazima atafute vita bu vya Dr. Binagwa na kuvisoma na kuona jinsi vinavyomsaidia kuandika kita bu kingine juu ya ndoa. Hiki sasa ni utafiti. Tunataka kitabu cha ndoa kutoka kwa mtu wa ndoa kama yeye na ikiwezekana atoe mifano ya ndoa yake mwenyewe. Kama tunataka kulisaidia taifa letu, na kama tunakubaliana kwamba taifa imara linajengwa na familia imara ni lazima mwandishi aonyeshe hili kwa mifano zaidi.
 
Je watu wawili wanaweza kuishi ndoa yao na ikawa imara? Au wanaihitaji msaada wa ndugu jamaa na marafiki? Tendo la ndoa, ni la wawili, lakini maisha mengine yanayoizunguka ndoa, kama uwazi, kujifunua na kutafuta msaada kwa wengine, kutafuta  ushauri, ndoa na ndoa kusaidiana; kufundishana uvumilivu na kuchukuliana ni jambo la muhimu sana. Hatimaye ndoa si ya watu wawili, bali ni suala la jamii nzima. Ndoa ikibaki kwenye kuta za watu wawili, ni vigumu sana ndoa hiyo kusimama na kudumu.
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122