"THE DA VINCI CODE" SI NYOKA WALA NGE

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

“THE DA VINCI CODE” SI NYOKA WALA NGE


“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata ;pigeni hodi, nanyi mtakaribishwa. Aombaye hupewa, atafutaye hupata, na apigaye hodi hukaribishwa. Je, kuna ye yote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate atampa jiwe? Au, je, akimwomba samaki atampa nyoka? Kama, basi nyinyi, ingawaje ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema yote wale wanaomwomba.”( Matayo 7:7-11).

Imani ni kupiga hodi, imani ni kuomba na imani ni kutafuta. Dini zote zinaishi kwa msingi huu: ni kupiga hodi, ni kuomba na kutafuta. Tunaambiwa kwamba atafutaye hachoki hadi pale anapofanikiwa kupata anachokitafuta. Kwa vile dunia yetu ina milango mingi ya kufunguliwa kabla mtu hajafikia mwisho wa safari ya maisha yake, ni lazima mtu aishi kwa kupiga hodi hadi mwisho wa maisha yake! Hivyo kupiga hodi si kazi ndogo. Vilevile na kutafuta si kazi ya mchezo. Katika kutafuta kuna mengi, kuna kupekua, kuna kuchimba, kuna kuhoji hili na lile. Ili mtu awe Mkristu wa kweli, awe Mwislamu wa kweli au awe muumini wa kweli wa dini yoyote ile ni lazima atafute bila kuchoka. Ni lazima aombe bila kukoma. Na kama anavyosema Matayo, Baba yetu wa Mbinguni, hawezi kutoa nyoka badala ya samaki, na hawezi kutoa mawe badala ya mkate! Mtu, akiomba samaki, akapata nyoka, au akaomba mkate akapata mawe, ajue amekosea, na sala yake inakuwa haikuelekezwa kwa Baba yetu aliye mbinguni, Baba mwenye wema, haki na huruma.

Je, kanisa letu hivi sasa linatoa mkate au mawe? Linatoa nyoka au samaki? Linatoa mayai au nge? Ni kanisa la masikini au matajiri? Ni kanisa linalosikiliza, linalojali na kuwakumbatia watu wa jinsia zote? Ni kanisa lenye wema, haki na huruma? Kilio cha Theolojia ya Ukombozi ni nini? Wanyonge wana sauti katika kanisa? Walei wana nafasi gani? Wanawake na vijana wana nafasi gani katika kanisa? Kuuliza maswali haya, kuchimba na kupekua zaidi ili kubainisha ukweli huu, si kulipinga kanisa. Mwenye wasi wasi na hili, imani yake ni bandia. Ninashindwa kuuona ukasuku katika kuhoji, katika kupiga hodi. Huwezi kupiga hodi bila ya kuwa na uhakika wa usalama ulio ndani ya nyumba, huwezi kupiga hodi bila kujua malengo na madhumuni ya wenye nyumba. Na wenye nyumba ni lazima wawe na uwezo wa kuelezea nyumba yao na yote yaliyo ndani ya nyumba yao, vinginevyo wanakuwa wapangaji wa muda! Kwa maoni yangu, kasuku ni yule anayepokea kila kitu bila kuhoji. Akipokea nyoka ni sawa, akipokea samaki ni sawa, akipokea mawe ni sawa na akipokea mkate ni sawa. Huyu ndiye kasuku asiyekuwa na uchaguzi wala utashi!

Jinsi Dk.Francis Rutaiwa, anavyoshangaa kwamba itawezekana vipi John, asiwe kwenye Karamu ya mwisho,(Angalia RAI Toleo 615: “ Karugendo ameshindwaje kuchambua The Da Vinci Code”) ndivyo na sisi tunaoutafuta ukweli, tunaotafuta na kupiga hodi, tunavyoshangaa ni kwa namna gani Maria Magdalena, apotee kwenye uso wa historia ya kanisa. Kwa John, inaweza kueleweka. Hata Dk. Francis Rutaiwa, anajua fika kwamba hakuna Injili hata moja inayotaja urafiki wa karibu kati ya Yesu na John. Hakuna Injili yoyote ile inayonyesha umuhimu wa John katika maisha ya Yesu Kristu. Tunachokisikia ni kwamba kuna mtume aliyependwa sana na Yesu. Jina la mtume huyu halitajwi kwenye Injili, ni namna gani mtume huyu alibatizwa jina la John, ni jambo la kufanyiwa utafiti. Hivyo kuwepo na kutokuwepo kwa John, kwenye karamu ya mwisho si jambo la kutia shaka. Kwa Maria Magdalena, ni tofauti. Na mtu yeyote anayeficha ukweli juu ya ukaribu wake na umuhimu wake katika maisha ya Yesu, hatupatii samaki, bali nyoka, hatupatii mkate bali mawe, hatupatii mayai bali nge!:

“Yesu alipofufuka mapema Jumapili, alijionyesha kwanza kwa Maria Magdalena, ambaye Yesu alikuwa amemtoa pepo saba. Naye Maria Magdalena akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo walikuwa wanaomboleza na kulia. Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalena amemwona, hawakuamini” ( Marko 16:9-10).

Injili zote nne zinakubali kwamba Maria Magdalena, ndiye alikuwa mtu wa kwanza kumshuhudia Yesu mfufuka. Imani ya Kikristu, ina msingi mkubwa katika kufa na kufufuka kwa Yesu Kristu. Tendo la ufufuko si jambo la kawaida na si jambo ambalo watu wangeweza kulikubali kwa urahisi. Inashagaza kuona Yesu, anaamua msalaba huu wa kushuhudia ufufuko wake kuuweka mikononi mwa Maria Magdalena, badala ya kuuweka mikononi mwa John, Petero au mitume wengine wanaume! Inawezekanaje mtu huyu aliyeaminiwa na Yesu hivyo, apotee kabisa katika uso wa sura ya historia ya Kanisa? Kuuliza swali hili si kulipinga kanisa. Ni kutaka kuutafuta ukweli. Jinsi umuhimu wa Maria Magdalena, unavyofunikwa ndivyo wanawake wote wananyimwa nafasi ya msingi katika kanisa, na hasa katika kanisa katoliki. Kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi kanisa la mwanzo lilivyoongozwa na kutunzwa na wanawake. Ukweli huu unajionyesha kwenye matendo ya mitume na kwenye barua za mtakatifu Paulo. Hata hivyo Yesu mwenyewe na umati wake walitunzwa na wanawake!( Luka 8:1-3).

“Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi.”(Yohana 12:3).

Kitendo hiki kilileta utata na mashaka makubwa miongoni mwa mitume. Hawakupenda ukaribu ulioonyeshwa na Maria Magdalena kwa Yesu. Walitegemea Yesu, amkaripie na kumlaani. Lakini ukweli ni huu:

“Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko. Nawaambieni hakika, po pote ulimwenguni, ambapo Habari Njema itakapohubiriwa, tendo hili alilofanya litatajwa kwa kumkumbuka yeye” (Matayo 26:12-13).

Tendo hili linatajwa wapi katika Kanisa Katoliki? Ni nani anayemkumbuka Maria Magdalena kwa tendo lake alilofanya la kuisafisha miguu ya Yesu Kristu? Uzushi wa Dan Brown, uko wapi? Kanisa linawakumbuka mitume wanaume peke yao. Kanisa la Mtakatifu Petero, la Roma, limepambwa na sanamu za mitume wanaume. Hakuna sanamu ya kuonyesha kumbukumbu ya Maria Magdalena, akisafisha miguu ya Yesu Kristu. Yanakumbukwa mambo mengine, lakini yale ambayo Yesu, mwenye alisema yatakumbukwa yametupwa kapuni! Kwanini mtu anayeisoma Injili kwa makini na kutafakari asihoji jambo hili, kwa nini isionekane wazi kwamba kuna kusudi la kuficha ukweli? Kuna tatizo gani Maria Magdalena, akipewa hadhi sawa sawa na Mtakatifu Petero? Kuna tatizo gani mwanamke akiwa Padri, Askofu, Kadinali au Papa? Ni wapi Kristu mwenyewe alipoelekeza kwamba wanawake wasishike nafasi ya uongozi?

“Walipokuwa katika safari, waliingia katika kijiji kimoja. Hapo mwanamke mmoja, aitwaye Marta, akamkaribisha. Marta alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake. Marta, lakini alikuwa anashughulika na mambo mengi ya kufanya. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, ‘Bwana, hivi hujali hata kidogo kwamba dada yangu ameniacha nitumikie peke yangu? Mwambie basi anisaidie.’ Lakini Bwana akamjibu, ‘ Marta wee, unahangaika na kusumbuka kwa ajili ya vitu vingi. Kitu kimoja tu ni cha lazima. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayekiondoa kwake.” ( Matayo 10:38-42).

Hiki kitu alichokichagua Maria ni kitu gani? Ni kitu gani hiki ambacho hata Yesu, ambaye ni Mungu, anakitambua kwamba ni kitu muhimu na bora? Ni kitu gani hiki ambacho Yesu, anasema kwamba hakuna mtu atakayekiondoa kwake? Tunaambiwa kwamba Maria, alikuwa ameketi karibu na Yesu, akisikiliza mafundisho yake. Inawezekana kitu hicho ni Neno la Mungu? Inawezekana Maria Magdalena, ni mtu pekee aliyelisikia neno la Mungu na kulishika? Inawezekana neno hili ndilo lililompatia moyo wa ujasiri wa kumfuata Yesu hadi msalabani? Ujasiri ambao hatuusikii kwa mitume wanaume? Inawezekana ndio sababu iliyomsukuma Yesu, kujionyesha kwanza kwa Maria Magdalena, baada ya ufufuko?

“Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye.”( Yohane”( Yohane14:23).

Je, inawezekana kile kitu alichokipata Maria Magdalena, ni kwamba Baba na Mwana walikuja kwake na kukaa naye? Inawezekana kwa njia hii Maria Magdalena, alishiriki Umungu wa Kristu? Maana kutokana na yale tunayoyasoma kwenye Injili, ni kwamba Maria Magdalena, alimpenda Yesu Kristu. Na kama alimpenda, alilishika neno lake, na kama alilishika neno lake ni lazima Baba na Mwana walikuja na kukaa naye? Na kama hili ni kweli, basi huyu ndiye mwamba wa kuwa msingi wa kanisa la Yesu Kristu! Inawezekana sifa anayopewa Mtakatifu Petero, ni ya Maria Magdalena? Injili ya Magdalena, inafichuzwa ugomvi mkubwa uliokuwepo kati ya Maria Magdalena na Mtakatifu Petero; uvomvi uliokuwa unasababishwa na wivu. Hata hivyo Injili nyingine zinaonyesha kwamba hakukuwa na uaminifu kati ya Petero na Maria Magdalena, maana Petero, hakuamini ujumbe wa Maria Magdalena, kwamba Yesu amefufuka hadi yeye aliposhuhudia Kaburi wazi!

Sifa hii ya mtu kuwa na kitu bora na muhimu; “ Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayekiondoa kwake”, tunaisikia kwa Maria Magdalena peke yake. Pia, sifa ya mtu kukumbukwa siku zote; “ Nawaambieni hakika, po pote ulimwenguni, ambapo Habari Njema itakapohubiriwa, tendo hili alilofanya litatajwa kwa kumkumbuka yeye”, tunaisikia kwa Maria Magdalena peke yake. Sifa ya mtu wa kumshuhudia Yesu Mfufuka, kitu ambacho ni msingi wa imani ya Kikristu, anayo Maria Magdalena. Iwe je tena mtu mwenye sifa zote nyeti, afutike kabisa katika uso wa historia ya kanisa?

Ingawa Dan Brown, analileta hili kwa njia ya riwaya, haina maana ni kitu cha kipuuzi. Riwaya, zina mafundisho, riwaya zinaubeba ukweli wa maisha katika jamii. Riwaya zinatumika kuielimisha jamii. Yesu, mwenyewe alitumia riwaya, katika mafundisho yake. Msamaria mwema ni riwaya, mtoto mpotevu ni riwaya. Kuna riwaya nyingi katika mafundisho ya Yesu Kristu. Hata Agano la kale, limetawaliwa na riwaya tupu!

Tunataka tusitake sasa hivi dunia inapita katika changamoto kubwa. Kuna maswali mengi yanayohitaji majibu. Kanisa kama sehemu ya dunia, haliwezi kukaa pembeni, ni lazima lishirikiane na dunia nzima kutoa majibu; kama linatoa samaki liseme linatoa samaki, kama linatoa nyoka liseme linatoa nyoka na ni kwa nini, kama linatoa mikate, liseme linatoa mikate, na kama linatoa mawe, liseme ni kwa nini, kama linatoa mayai liseme na kama linatoa nge liseme ni kwa nini. Sasa hivi dunia nzima inaongea lugha ya demokrasia, je kanisa linaongea lugha hii? Sasa hivi dunia inakazania majadiliano na ushirikishwaji, je kanisa linayazingatia haya? Kuna swala zima na usawa wa kijinsia na vita dhidi ya mfumo dume, je Kanisa, na hasa kanisa katoliki linasema nini kuhusiana na wimbi hili la mageuzi?

Ndio maana mimi nikawaomba Maaskofu wetu na wanateolojia wakisome kitabu cha “The Da Vinci Code”, ili waweze kutuongoza katika mjadala huu ambao haukwepeki na waweze kutufungulia mlango wa nyumba yenye ukweli na usalama. Jaziba, imani ya woga na unafiki, uongo, kupindisha ukweli na matusi kama ya Dk.Francis Rutaiwa, haviwezi kutufikisha mbali!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment