MTOTO WA AFRIKA MTOTO YATIMA

MAKALA HII ILITOLEWA NA GAZETI LA RAI 2005.

MTOTO WA AFRIKA MTOTO YATIMA

Wanangu wapendwa, leo ni siku yenu. Siku ya mtoto wa Afrika. Chimbuko la siku hii ni mapambano ya kutetea haki; watoto wenzenu walikataa kubaguliwa na kunyimwa haki zao, walitaka wapate elimu bora na yenye hadhi, walitaka wapate chakula bora, maji safi na salama ,afya njema na usalama kwa ujumla. Watoto hawa walikataa kunyanyaswa na kuamua kusimama na kutetea haki zao. Matokeo yake ni historia tunayoikumbuka hadi leo hii.

Kwa miaka mingi sasa nimejenga utamaduni wa kuwaandikia makala kila mwaka juu ya siku hii ya mtoto wa Afrika. Nimekuwa nikiandika mada mbalimbali zinazowahusu nyinyi watoto: Mfano, mtoto wa Afrika msichana, mtoto wa Afrika mvulana, mtoto wa Afrika mtoto wa mitaani, mtoto wa Afrika Changudoa nk. Leo hii nimeandika Mtoto wa Afrika mtoto yatima.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni watoto yatima wa Tanzania ni jukumu letu sote. Nina imani huu si wimbo mwingine tena kama zile tulizozizoea za MKUKUTA, PCB, DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA, nk. Huu ni lazima uwe wimbo ulio bora maana watoto ni taifa la kesho – watoto yatima ni watoto kama wengine, na kwa vile si mmoja au wawili hatuwezi kuupuzia wimbo huu…..

Kuna mashirika mengi na vikundi vinavyowashughulikia watoto yatima, mfano Kuleana, Dogo dogo Centre, Bona bana, Maisha mapya, SODT nk, vikundi hivi na mashirika haya yanafanya kazi nzuri na muhimu sana tatizo ni kwamba hakuna ushirikishwaji wa jamii nzima. Matokeo yake ni kwamba watoto wanapokuwa na kutaka kujitegemea na kujenga familia, hakuna mwenye kujua la kufanya. Ndio maana ni muhimu jamii nzima kushirikishwa katika zoezi zima la kuwahudumia watoto yatima na wale walio kwenye mazingira magumu.

Tunaambiwa kwamba leo hii kuna watoto milioni mbili yatima hapa Tanzania. Namba hii ni kubwa na inaongezeka kila kukicha. Hivyo wimbo wa kwamba watoto yatima wa Tanzania ni jukumu letu sote si wa kupuuzia! Utafiti uliofanywa mwaka 1999 na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia watoto, UNICEF, libaini kuwepo katika jamii yetu makundi ya watoto wanaohitaji ulinzi maalum. Makundi hayo yanajumuisha watoto wanaolelewa kwenye makazi maalum na kuzaa wakiwa na umri mdogo, watoto wanaofanyishwa kazi majumbani, watoto wanaoishi mitaani, watoto wanaofanya biashara ya mapenzi(ngono) na watoto wenye ulemavu.

Aidha iligunduliwa kuwa idadi kubwa ya watoto hao wanalelewa na bibi zao wenye umri mkubwa (miaka 70 au zaidi), na wengine wanalelewa na watoto wenzao wangali bado na umri mdogo. Walezi walio wengi wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa kuzihudumia familia zao pamoja na kuwalea watoto. Hali hii imesababisha watoto kukosa haki na kuduma za msingi zikiwemo chakula, malazi, mavazi, elimu, makazi na huduma za afya.

Utambuzi zaidi wa watoto walio katika mazingira magumu uliofanywa na idara ya Ustawi wa Jamii, kwa kushirikiana na UNICEF (2000), pia ulibaini kuwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu inaongezeka siku hadi siku. Utafiti huu pia ulibainisha kwamba si watoto wote yatima wanaishi katika mazingira magumu na kwamba si watoto wote wanaoishi katika mazingira magumu ni yatima! Kuna yatima walio na nafuu ya maisha na kuna watoto wasiokuwa yatima lakini wanaishi kwenye mazingira magumu.

Ufuatiliaji wa karibu katika ngazi ya familia na jamii umebaini kuwepo kwa mapungufu kuhusu ufahamu wa mambo muhimu ya matunzo na malezi kwa watoto wa aina hii. Aidha, baadhi ya watoto hao hawapatiwi mahitaji yao ipasavyo kutokana na hali duni ya walezi wao kiuchumi. Pia imegundulika kuwa jamii kwa ujumla haina ufahamu wa kutosha wa kutambua na kushughulikia masuala ya haki za watoto pindi zinapokiukwa. Watoto na vijana wenyewe wanakosa elimu juu ya stadi za maisha, ambayo ingewasaidia kujikinga dhidi ya magonjwa hatari ukiwemo UKIMWI, pamoja na kuendesha maisha yao ya baadaye kwa kujitegemea.

Kuna sera nyingi zimetungwa kuhusiana na watoto: Sera ya Maendeleo ya Mtoto ( Wizara ya Maendeleo ya jamii, Wanawake na watoto), Mwongozo wa Mikakati ya Kuhudumia Watoto Yatima (Idara ya Ustawi wa Jamii), Sera ya Maendeleo ya Vijana (Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo), Sera ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI(Ofisi ya Waziri Mkuu). Pamoja na sera zote hizo bado hatujafikia kiwango cha kumhudumia mtoto ipasavyo. Hatujafika hatua ya kutambua kwamba watoto yatima na hasa wale walio kwenye mazingira magumu zaidi ni jukumu letu sote.

Mfano Idara ya Ustawi Jamii, katika kitengo chake cha: Huduma kwa Familia, Watoto na vituo vya kulelea Watoto wadogo mchana, ina wajibu wa kutoa huduma zifuatazo: - Utambuzi wa watoto waishio katika mazingira magumu
- utambuzi wa mahitaji yao
- Utambuzi wa walezi wao na uwezo wao
- Utoaji ushauri nasaha na upimaji hiari wa Virusi vya Ukimwi
- Msaada kwa mahitaji muhimu hasa ya shule
- Msaada kwa familia zisizo na uwezo zinazolea watoto yatima ili ziweze kuboresha vipato vyao vya kukidhi mahitaji ya watoto wao.
- Kubuni na kuweka mikakati ya kusaidia watoto waishio katika mazingira magumu kwa kushirikiana na jamii yenyewe.

Je, haya yanafanyika? Je sera nzuri nilizozitaja kabla zinatekelezwa? Maswali haya ndio yamenisukuma kuwaandikia makala hii siku ya leo, siku ya mtoto wa Afrika mtoto yatima!

Idara ya Ustawi wa Jamii, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF, tayari imeanzisha na inatekeleza mpango shirikishi jamii wa matunzo na misaada kwa watoto walio katika mazingira magumu. Mpango huu unatekelezwa katika Wilaya sita za Karagwe, Bagamoyo, Kisarawe, Makete, Musoma Vijijini na Magu. Mpango huo wenye misingi ya kijamii unahusisha shughuli mbalimbali zikiwemo uchambuzi yakinifu na utambuzi wa watoto hao.

Nimepata bahati ya kutembelea Wilaya mojawapo kati ya hizi zinazofanya kazi ya kuwahudumia watoto yatima na wengine walio katika mazingira magumu kwa kushirikiana na UNICEF. Ndiyo maana ninaandika makala hii kwa furaha kubwa na matumaini. Nina habari njema kwa Mtoto wa Afrika, Mtoto wa Tanzania, Mtoto yatima na watoto wote wanaoishi katika mazingira Magumu. Wilaya ya Magu, mkoa wa Mwanza, imefanikiwa kulifanya swala hili kuwa la kijamii! Wilaya ya Magu kwa kusaidiana na UNICEF, imefanikiwa kuitekeleza kauli mbiu ya mwaka huu kwa matendo! Kwa vile wameshirikishwa kikamilifu, wananchi wa Magu, wanatambua kwamba: Watoto yatima wa Tanzania ni jukumu letu sote.

Kata zote za wilaya ya Magu, zina timu za utambuzi wa watoto walio katika mazingira magumu. Timu hizi zimeandaliwa na kupatiwa mafunzo ya kuwatabua watoto hawa kutoka kwa timu ya utambuzi watoto walio katika mazingira magumu ya Wilaya, ambayo nayo imeandaliwa nipasavyo. Timu hizi zinawachambua watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kubainisha ni wapi ni yatima, ni wapi waliotelekezwa, ni wapi wanalelewa na babu zao na ni wapi wanalelewa na watoto wenzao. Utambuzi huu unasaidia kuwahudumia watoto kwa urahisi katika mazingira wanamoishi kwa kuishirikisha jamii nzima.

Mbali na timu za utambuzi kitu kingine cha kujifunza kutoka Magu, ni kwamba kila kijiji cha wilaya ya Magu kina Kamati ya kuhudumia watoto walio katika mazingira magumu. Kamati hii inaundwa na watu kumi, wanaume watano na wanawake watano kutoka Serikali ya kijiji, CBO na NGO, watoto, watu mashuhuri katika kijiji na vijana. Kamati hii imeandaliwa kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo utunzaji wa pesa. Hivyo kamati inatunza mfuko wa kuwahudumia watoto walio katika mazingira magumu na ina akaunti kwenye benki. Pesa zote za kuwasaidia watoto katika kijiji, misaada yote inaratibiwa na kamati hii. Wadau mbali mbali wanauchangia mfuko huu wakiwemo wanakijiji wenyewe, halmashauri ya wilaya, NGO na CBO, UNICEF na mashirika ya dini.

Ili mambo yaende vizuri Idara Ya ustawi wa Jamii ya Wilaya ya Magu, imeamua kuunda timu ya ufuatiliaji. Hii ni timu ya watu 17, walioandaliwa na kupatiwa mafunzo ya kufanya kazi hiyo ya ufuatiliaji. Kila mtu amekabidhiwa vijiji viwili kuvilea na kuhakikisha timu ya utambuzi na kamati za vijiji zinafanya kazi. Timu hii ya ufuatiliaji imepokelewa vizuri vijijini baada ya wananchi kutambua umuhimu wa ufuatiliaji, kwamba bila changamoto hiyo uzembe unaweza kuwaingilia!

Takwimu za mwaka jana zinaonyesha kwamba wilaya ya Magu ina watoto 5116 walio katika mazingira magumu na kati yao 2116 ni watoto yatima. Watoto wote hawa wanajulikana kwa sura na mahali wanapoishi kuanzia wilayani hadi vijijini na wanahudumiwa na jamii nzima! Wilaya ya Magu ina idadi ya watu 416,113, ndiyo kusema asilimia 1.2 ya wakazi wa Magu ni watoto walio katika mazingira magumu. Kwa mfumo huu maisha ya watoto hawa yanaelekea kuwa na nafuu.

Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wilayani Magu, Bwana Philibert Kawemama, anaungama wazi kwamba mafanikio yaliyopatikana wilayani Magu, kuhusiana na huduma ya watoto walio katika mazingira magumu yamepatikana kupitia mchakato mzima ya ushirikishwaji. Viongozi wa wilaya kuanzia kwa Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Mipango, Afisa Utawala na wengine wameshirikishwa na kutoa ushirikiano wa hali ya juu, wadau, wananchi na walengwa wameshirikishwa na kutoa ushirikiano. Bwana Kawemama, anaamini mfumo huu ukienea nchi nzima, utakuwa mchango wa kupunguza adha ya watoto walio katika mazingira magumu.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana wilayani Magu kwa kuwahudumia watoto walio katika Mazingira Magumu, bado Bwana Philibert Kawemama, anaona kuna changamoto nyingi katika kazi hii ambazo ni lazima kupambana nazo bila ya kuchoka. Mfano anasema taarifa zinazokuja kutoka vijijini zinaonyesha kwamba watoto yatima wanaongezeka kwa kasi na anasema taarifa kama hizi zipo pia kwenye wilaya nyingine zinazotekeleza mradi kama huu wa Magu. Changamoto nyingine ni ile tuliyoizoea kila siku ya Umasikini huu utaisha lini? Bwana Kawemama, anataja changamoto nyingine kama mmomonyoko wa maadili na unyanyaswaji wa akina mama.

Ili kukabiliana na changamoto hizi, Idara ya Ustawi wa Jamii ya wilaya ya Magu, imeunda pia timu za uwezeshaji haki na sheria katika ngazi ya kata na vijiji. Timu hizi zimeandaliwa kwa kupatiwa mafunzo na nyenzo za usafiri. Baiskeli mbili kwa kila kijiji. Watu hawa wanawasaidia kuwaelimisha watu juu ya haki na sheria na pia wanasaidia kuleta habari kwenye wilaya juu ya mambo ambayo yanahitaji msaada zaidi.

La kujifunza kutoka Magu, ni kwamba wananchi wakishirikishwa katika shughuli zote za maendeleo na kujenga taifa, mambo yanakwenda na kufanikiwa. Matatizo ni pale watu wanapoletewa kila kitu kama msaada bila ya kushirikishwa na wenyewe kuchangia.

Kama imewezekana Magu, kwa nini isiwezekane kwingine? Inawezekana kila mtu akitimiza wajibu wake. Huu ni ujumbe wa matumaini kwako wewe mtoto wa Afrika, mtoto wa Tanzania, mtoto yatima na hasa mtoto anayeishi kwenye mazingira magumu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment