UCHAGUZI MKUU 2005

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

UCHAGUZI MKUU 2005, TUSEME UKWELI NA TUSIWAPOTOSHE WANANCHI.

Tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2005, tutayasikia mengi. Mengine ya ukweli na mengine ya uongo. Watu wataanza kupakana matope na kuharibiana majina. Kutakuwa na mapambano makali kati ya chama na chama, na ndani ya chama kutakuwa na mapambano kati ya mgombea na mgombea . Kila mtu anataka ashinde na kila chama kinataka kishinde. Hiyo ndiyo siasa na huo ndiyo ubinadamu!

Jambo la msingi ambalo tunapaswa kuliangalia kwa makini ili tuhesabike kati ya jamii iliyostaarabika na inayoheshimika duniani ni lazima tufanye siasa zinazozingatia ukweli. Ni jambo la kawaida katika ushindani wa kisiasa watu kutafuta kuangushana, na kila mmoja anataka kushinda, ili ushindi uwe wa amani, ni lazima washindani kueleza ukweli dhidi ya wapinzani wao. Maana kama lengo ni kuijenga Tanzania bora, yenye amani na utulivu, hakuna haja ya kuupindisha ukweli. Gharama ya kupindisha ukweli ni kubwa na yenye hasara kuliko faida.

Hapa Tanzania, ukiachia mbali kiti cha rais, nafasi nyingine zinazokuwa na ushindani mkubwa ni Ubunge na Udiwani. Hizi zote ni nafasi za uwakilishi. Mbunge anawawakilisha watu wa jimbo lake Bungeni na Diwani anawawakilishia watu wa kata yake kati vikao vya halmashauri ya wilaya. Nafasi hizi zinakuwa na siasa za uongo, chuki, umbea na uhasama. Ni bahati mbaya kwamba baadhi ya wale wanaochaguliwa kwenye nafasi hizi wanafikiria zaidi juu ya posho kuliko kuuzingatia na kuutafakari wajibu wao wa kuwawakilisha wananchi, wajibu wa kuelezea ukweli, kulinda ukweli na kuusimamia ukweli. Kazi hii ni ngumu kiasi kwamba kama watu wangeifahamu vizuri, ni wachache wangeikimbilia!

Siasa hizi za uongo, chuki, umbea na uhasama, zimeanza hivi sasa hata kabla ya muda wenyewe wa kampeni kutangazwa. Waheshimiwa wabunge wamekwishaanza kupita kwenye majimbo yao wakiwaelezea wananchi yale waliyoyafanya kwa kipindi cha miaka mitano inayokwisha na matarajio yao kwa kipindi kingine endapo watachaguliwa. Wengine wameanza kutaja jinsi walivyonunua majeneza kwenye misiba, walivyochangia kwenye misiba, walivyosaidia wagonjwa na wasiojiweza, walivyosaidia kulipa karo za baadhi ya watoto katika majimbo yao, walivyotoa kanga na vitenge, walivyotoa baiskeli na misaada mingine mingi. Kana kwamba kazi ya mbunge ni kutoa misaada! Kwa njia hii walio wengi wanafanikiwa kupindisha ukweli na kuwapotosha wananchi.

Mbali na wabunge walio Bungeni hivi sasa kuna wengine wanaotaka kuwania nafasi hizo. Hivyo wanaanza kutafuta mbinu mbali mbali zenye uongo na ukweli. Wengine wameanza kumwaga mapesa, wananunua kanga, vitenge, pombe na kuwapikia watu pilau. Na wengine wameanza kuvitumia vyombo vya habari kujitangaza na kueneza uongo dhidi ya wapinzani wao. Mfano mzuri ni habari iliyotoka kwenye gazeti hili tarehe 5.Juni, iliyokuwa na kichwa cha habari: “Jimbo la Chitatalilo lakodolewa macho”. Habari hii ililenge kuelezea hali ilivyo katika jimbo la Buchosa, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza.

Mwandishi wa habari hii ambaye anaelekea anamfagilia mtu fulani au anajifagilia yeye mwenyewe maana siku hizi kila mtu anataka kuingia bungeni, anaelezea vizuri kile nilichokigusia hapo juu mwanzoni mwa makala hii; siasa za uongo, chuki, umbea na uhasama. Habari hii aliyoiandika kwa uchu na pupa, haikulenga kuelezea ukweli, bali kuwapotosha wananchi. Na hili si jambo zuri, ni jambo la kupiga vita kwa nguvu zote.
Mwandishi wa habari hii alilenga kuwaelezea watanzania kwamba Kamanda wa vijana wa CCM, wa Jimbo la Buchosa, alichaguliwa kwa mizengwe. Kama habari hii ingeishia katika kuelezea mizengwe na kudhibitishwa kwamba mizengwe ilitumika, basi hili lingebaki katika Chama Cha CCM na uongozi wake – hili lisingekuwa swala la Watanzania wote. Lakini habari hiyo iliendelea hivi: “ Katika kuthibitisha upendeleo huo aliouita wa wazi, alisema kamanda aliyetawazwa amesimamishwa kazi serikalini na kuwa hastahili kwa sasa kupewa heshima kama hiyo. Atawaongoza vipi vijana wakati jamii haijaambiwa kitu kilichofanya afukuzwe kazi?”

Ikiguswa serikali, hili ni swala la watanzania wote. Ingawa serikali yetu inaongozwa na Chama Cha Mapinduzi, lakini wafanyakazi wake wote si lazima wawe wanaCCM – na serikali inaongoza nchi nzima. Hivyo swala linaloigusa serikali ni lazima limguse kila Mtanzania.

Aliyechaguliwa kuwa Kamanda wa vijana jimbo la Buchosa ni Dk.Charles Tizeba. huyu ndiye aliyekuwa Mhandisi wa Jiji la Mwanza, wakati wa sakata la kituo cha mafuta kwenye Barabara ya Makongoro. Mhandisi huyu pamoja na wataalamu wengine wa Jiji la Mwanza, waliishauri serikali kwamba Kituo hicho cha mafuta hakikuwa Barabarani. Serikali haikusikiliza ushauri huo, ikaendelea na zoezi lake la kukivunja kituo hicho. Ukweli ni kwamba kituo hicho hakikuwa Barabarani, hakijawahi kuwa barabarani na hakitakuwa barabarani! Ikitokea huko mbeleni ikaamuliwa kupitisha barabara pale, basi itapita juu kwa juu kama barabara tunazozijua kwenye nchi zilizoendelea zinazopita juu. Kiwanja hicho kilipimwa kwenye miaka ya sitini. Aliyekimiliki miaka hiyo alikuwa na lengo kujenga kituo cha mafuta, alikiomba kiwanja hicho kwa lengo la kujenga kituo cha mafuta. Bahati mbaya hakuweza kufanya hivyo, alikiuza kiwanja hicho kwa mtu mwingine, na mwingine akauza kwa mwingine hadi alipokinunua huyu aliyejenga kituo kilichovunjwa na serikali. Tangia nyuma makusudio ya kiwanja hicho yalikuwa ni kujenga kituo cha mafuta. Mhandisi wa jiji ni mtu wa kujua historia hii yote na kuwa na uwezo wa kusoma ramani ya Jiji vinginevyo anakuwa amekinunua cheti!

Ramani ya Jiji ilivyochorwa, kama Dk.Tizeba, angekubali kwamba kituo hicho kiko barabarani angekuwa ameisaliti taaluma yake ya uhandisi. Leo hii tungekuwa tunaishinikiza serikali imnyang’anye liseni ya uhandisi! Maana hata mtu ambaye hakuenda shule anaweza kuona kwamba kiwanja hicho hakipo barabarani. Asingekuwa na tofauti na wale waliopitisha mikataba hewa ya IPTL na mingine ambayo hadi leo hii tunaipigia kelele.

Kwanini basi Serikali iliamua kukivunja kituo cha mafuta ambacho hakikuwa Barabarani? Haya ndiyo maswali ya kuiuliza serikali ili wananchi wafahamu ukweli. Utakuwa ni uonevu wa hali juu kuwasakama watu waliosimama kidete kuitetea taaluma yao na kusema ukweli.

Haiwezekani mtu anayetetea taaluma yake, anayesimama kwenye ukweli, asiyefanya kazi kwa kufuata tu kama robot, anayejisimamia na kuangalia maslahi ya taifa, awekwe msalabani na kushutumiwa kwa uzalendo wake.

Taifa letu linahitaji viongozi wanaojisimamia, wanaoheshimu taaluma zao, wazalendo na wanaosema ukweli. Tunahitaji viongozi ambao wako tayari kupoteza kazi zao na vyeo vyao vikubwa kwa kutetea ukweli.

Dr.Tizeba, angeweza kusema kwamba Kituo cha Mafuta kilikuwa barabarani, kwa vile Serikali ndivyo ilivyotaka, lakini ukweli ungebaki palepale kwamba Kituo hicho hakikuwa barabarani. Serikali zinakuja na kupita, lakini ukweli unabaki na historia inaweka kumbukumbu. Tunaona jinsi hadi leo Waafrika wanavyodai fidia ya matendo ya Utumwa na ukoloni.

Hivyo mtu anayesimama kutetea ukweli, hata akipoteza kazi, akapoteza mali au hata na maisha yake, vitu hivyo havipotei bure. Vinabaki kwenye kumbukumbu iliyotukuka.

Ni bora wananchi wakatambua hili kwamba wanapomtafuta mbunge wa kuwakilisha jimbo lao ni lazima wamtafute mtu mwenye uwezo na karama ya kutetea ukweli na kuusimamia bila kuyumbishwa na vitisho, rushwa, upendeleo au ubinafsi. Bunge ni chombo muhimu katika Taifa letu. Katiba inasema: “ Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katitika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii” (Ibara 63(2)).


Hivyo hiki ni chombo muhimu kinachohitaji watu makini, wazalendo na wasioupindisha ukweli.

Tuna utamaduni kwamba mkubwa hakosei na akikosea hawezi kuomba msamaha. Lakini kwa serikali inayoongozwa na sera ya Uwazi na Ukweli, ingekuwa bora ikaomba msamaha kwa kuvunja kituo cha mafuta ambacho hakikuwa barabarani, ili akina Tizeba, wasibebeshwe msalaba usiokuwa wao!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment