KWANI MALECELA NI BUBU?

MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.


KWANI MALECELA NI BUBU?

Malumbano ya Nikita Naikata, Profesa Mukandala na Ramadhani Kingi juu ya Mzee Malecela, yametuburudisha kweli. Au niseme yameniburudisha. Nina imani kuna wengine wamechukizwa, wamejifunza, wamechokozwa, wameguswa na wengine labda wamepata kichefuchefu. Nikita Naikata, anasema kwamba “Profesa Mukandala akienda kushitaki kwa Nyerere, atakuta naye alishajisahihisha. Naye Ramadhani Kingi, anang’aka “ Hata akijisahihisha Nyerere maandishi yatatapakaa”.

Kinachojitokeza haraka ni kambi mbili zinazopingana. Kambi ya Profesa Mukandala na Ramadhani Kingi, kwa upande mmoja na kambi ya Nikita Naikata, kwa upande mwingine. Kambi zote ni za wasomi. Tofauti inayojitokeza kwa haraka ni utafiti, uchambuzi, umakini, jazba, siasa, Uzalendo, dira na uelewa juu ya Tanzania ya jana, leo, kesho na keshokutwa. Kambi ya Profesa Mukandala na Ramadhani Kingi ni lazima iwavutie watafiti, wachambuzi, watu makini, wazalendo na wenye uelewa wa Tanzania ya jana, leo, kesho na keshokutwa. Kambi ya Nakita Naikata, itawavutia watu wenye jazba na uelewa wa siasa za leo, bila ya kuangalia jana, kesho na keshokutwa!

Kwa bahati nzuri watu hawa watatu wenye kulumbana juu ya Mzee Malecela, ninawafahamu vizuri. Profesa Mukandala ni Msomi, Mhadhiri wa chuo kikuu, mtafiti, mchambuzi na kiasi Fulani ni mzalendo wa mfano; kama si uzalendo wake angekuwa ametimua na kutafuta kazi nje ya nchi hii kama wafanyavyo wengine. Kufuatana na kazi zake nyingi za utafiti na zilizotokea kuheshimika ndani na nje ya Tanzania, akitoa hoja, haiwezi kukabiliwa kwa porojo.

Ramadhani Kingi, ni msomi, mwalimu, mwandishi, mtafiti, mzalendo na mtu mwenye misimamo isiyoyumba na si mtu wa kutawaliwa na jazba – yeye ni mtu wa hoja, huwezi kumkabili kwa porojo – ukimshinda kwa hoja, anakubali kushindwa!

Rafiki yangu Nikita Naikata, ni msomi, mwandishi, mshairi, mwanasiasa , mchekeshaji na mwenye jazba hasa akimpenda mtu au kitu! Wakati mwingine anatumia porojo kujenga hoja juu ya mambo nyeti kama lilivyo hili la Malecela.

Watu hawa watatu wanatokea mkoa mmoja! Na kwa bahati nzuri au mbaya ni mkoa tofauti na ule wa Mzee Malecela- hivyo hapa swala la ukabila liko nje. Wanampinga Malecela kama Malecela na wanamuunga mkono Malecela kama Malecela, si ukabila wala ukanda!

Ukisoma kwa makini makala ya Mukandala, Nikita Naikata na ile ya Ramadhani Kingi, utazigundua sifa nilizotaja hapo juu. Utagundua ni nani anaandika kisomi na kuzingatia utafiti na ni nani anaandika porojo ili litimie lile neno: “Na mimi nina la kusema” (Kangambeo kake!).

Hivi kweli rafiki yangu Nakita Naikata, na usomi wake wote, anaamini Mwalimu Nyerere, alikwazwa tu na msimamo wa Malecela, juu mfumo wa serikali tatu? Na kama hili ni kweli, huyu Nikita, ana ushahidi gani wa kutuonyesha kwamba kule kaburini Mwalimu, atakuwa amebadilisha msimamo wake? Mwalimu Nyerere, angekuwa na historia ya kubadilika badilika, mtu anaweza kusema kwamba labda na kule kaburini alishabadilisha mambo fulani fulani. Hadi anakufa Mwalimu, alikuwa bado anautetea Ujamaa, Muungano na mfumo wa serikali mbili; serikali ya Muungano na serikali ya Visiwani. Pamoja na mabadiliko yaliyojitokeza duniani wakati wa uhai wake Mwalimu, alisita kuukumbatia utandawazi na sera ya ubinafsishaji na soko huria. Jinsi tunavyoendelea kushuhudia mifumo hii haijawa na sura ya kupendeza kiasi cha kufikiria kwamba inaweza kumpendeza mwalimu hadi akabadilisha mawazo yake. Mwalimu, alikuwa anahoji kama CRDB, inaweza kuruhusiwa kufungua tawi lake New York. Je hili limefanyika? Sasa hivi tunawaruhusu Wachina wanafanya kazi ya umachinga hapa Tanzania, je watanzania wanaweza kwenda kufanya umachinga China? Ni lipi la kutufanya tuamini kwamba jinsi mambo yanavyokwenda sasa hivi yangeweza kubadilisha misimamo ya Mwalimu?

Ninashindwa kuamini kwamba ugomvi wa Mwalimu na Malecela ni mfumo wa serikali tatu tu. Ni lazima kuna sababu nyingine ya msingi. Ni lazima kuna udhaifu alio nao Mzee Malecela. Udhaifu huu anaujua Marehemu Mwalimu Nyerere na Malecela mwenyewe.

Mbona hata kabla ya hili la serikali tatu Malecela, hakuwa tena na ukaribu na Mwalimu? Kama si Mzee Mwinyi, kumshika mkono na kumrudisha kundini si angekuwa kama wengine walioupoteza uzalendo na kugombana na Kambarage? Si lazima kuwataja, wale wenye uelewa wa Tanzania ya jana, leo, kesho na keshokutwa wanalijua hili – asiyelijua hili asijiingize katika kuandika mada zinazohitaji utafiti na uchambuzi labda ajitahidi kuandika za udaku na za burudani tu!

Bahati mbaya Mwalimu Nyerere, ni marehemu hawezi kutuelezea zaidi juu ya ugomvi huu. Lakini Mzee Malecela, bado yu hai. Yeye ndiye mtu wa kutegua kitendawili hiki. Kwani yeye ni Bubu? Kwanini anakuwa na tabia ya kukaa kimya kila anapoguswa sahihishwa, kushutumiwa na kulaumiwa?

Magomvi yake na Mwalimu, hadi Mwalimu kuamua kuandika kitabu, Malecela hakusema lolote. Hakukana wala kukubali shutuma za Mwalimu. Hakusema lolote wala kuandika lolote. Alikaa kimya. Ukimya huu maana yake ni nini? Kiburi au dharau? Au ni heshima aliyokuwa nayo kwa Mwalimu? Lakini kama ni heshima, basi asingejitokeza mwaka 1995 kutaka kuwania urais wa Muungano mbele ya macho ya Mwalimu. Inawezekana Malecela ana kiburi na dharau kubwa, maana mwaka huu alisikika akisema kwamba mawazo yaliyo kwenye kitabu cha mwalimu kumhusu yeye yamepitwa na wakati!

Kwamba Mzee Malecela, anafanywa tingatinga inachekesha kweli. Mtu mzalendo, kazi yake ni kutoa mchango wake katika taifa na kupita. Mtu mzalendo hasubiri kupata sifa wala tuzo. Urais, alioutaka Mzee Malecela, hapewi mtu kama zawadi. Urais ni karama, uzalendo wa hali ya juu, kipaji, uwezo, sifa na kukubalika kwa watu.

Ni kweli Mzee Malecela, amelitumikia taifa letu na labda kwa uaminifu mkubwa. Lakini pia kuna watu wengi waliolitumikia taifa letu kwa uaminifu zaidi hata kuzidi wa Mzee Malecela. Wengine wamehatarisha maisha yao, wengine wamepoteza maisha yao, wengine wamekuwa vilema na wengine bado wanaendelea kuhatarisha maisha yao kwa kulitumikia taifa letu la Tanzania. Haina maana wote hao wazawadiwe urais. Tutakuwa na marais wangapi?

Kuna kishawishi cha kufananisha ukimya wa Malecela na hekima. Mfano Yesu, alipoulizwa Ukweli ni kitu gani, alikaa kimya. Hiyo ilikuwa ni hekima kubwa. Hakujibu kwa maneno, lakini kwa matendo aliuonyesha ulimwengu ukweli ni kitu gani. Alikubali kuyapoteza maisha yake kwa nia ya kuwakomboa walio wengi. Alikuwa na uwezo wa kuukwepa msalaba, lakini hakufanya hivyo. Huu ni mfano wa hekima. Lakini Mzee Malecela, anakaa kimya na kuendelea kufanya vitu chini chini. Ukimya wake ni unafiki na ni hatari kubwa.

Baada ya kutupwa kule Chimwaga, amekaa kimya. Hazungumzi wala kuandika chochote. Tunasikia alikimbilia Halmashauri kuu, baada ya kutupwa na Kamati kuu. Inashangaza kidogo kama anavyotaja Ramadhani Kingi, mtu kukimbilia mahakama ya mwanzo baada ya kesi yake kutupwa na Mahakama ya rufaa! Haya ni ya Chama, na tunasikia tu, hakuna ushahidi wa historia. Watanzania, wangependa kusikia anasema nini yeye baada ya kutupwa. Akina Sumaye, wamesema tumesikia na vyombo vya habari vimeandika na inaingia wenye kumbukumbu. Salim, alisema tukasikia na Mwandosya akasema tukasikia. Wengine wametangaza kuvunja makambi yao. Mzee Malecela, hasemi kitu maana yake ni nini? Wengine wanasema kwa niaba yake! Kwani yeye ni Bubu?

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment