TABIA HIZI ZITAENDELEA HADI LINI?

MAKALA HII LICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

TABIA HIZI ZITAENDELEA HADI LINI?

Tarehe 23 mwezi huu kuna ugeni mkubwa Wilayani Magu. Ni ugeni wa kimataifa. Tunasikia kwamba Rais Benjamin William Mkapa, ataambatana na marais wengine watatu wa nchi jirani kufungua awamu ya pili ya mradi wa TASAF wilayani Magu. Habari zinazopatikana ni kwamba Wilaya ya Magu, imefanya vizuri kwenye utekelezaji wa mradi wa TASAF awamu ya kwanza. Kwa vile mradi huu unaendeshwa kwenye nchi nyingine za Afrika, basi marais wageni watakuja kujifunza Magu.

Wenyeji wa Magu, wanakubali kwamba TASAF, imefanya kazi nzuri kwa upande wa mashule, mahospitali na majengo, lakini mradi wa barabara na madaraja imeboronga! Hayo ni maoni ya wenyeji, lakini msemaji mkuu ni serikali. Hivyo ni lazima tuamini kwamba TASAF, ya Magu, imefanya kazi nzuri na ni haki ya Magu, kuupata ugeni mkubwa na kupongezwa.

Kwamba TASAF, imefanya vizuri au vibaya si lengo la makala hii. Na wala si lengo la makala hii kuuliza Magu, kuna nini. Mbali na TASAF, kuna mambo mengi Magu, mfano wavuvi wadogo wanaendelea kunyanyaswa kiasi hawezi kulifaidi ziwa linalowazunguka, uvuvi haramu unaendelea na kushamiri, huku wavuvi wadogo wakisingiziwa kwa uvuvi huo, ambavyo ukweli ni kwamba vigogo ndio wanaongoza miradi hiyo ya uvuvi haramu na viwanda vya samaki vya Wahindi vinaendeleza biashara ya unyanyasaji. Magu, ni wilaya iliyoshambuliwa sana na ugonjwa wa UKIMWI kwa vyanzo ambavyo si kazi ngumu kuvidhibiti! Uzembe kutojali na kutowajibika watu wanaendelea kufa na kuambukizwa virusi. Magu kuna mengi, watumishi wa serikali hawana nyumba, barabara mbovu na tatizo la huduma ya maji. Ni mengi na baadhi rais atasomewa kwenye risala! Lengo la makala hii ni kuhoji tabia zilizozoeleka tangia uhuru za kufanya maandalizi makubwa na kutumia pesa nyingi wakati kiongozi wa ngazi za juu na hasa rais anapotembelea sehemu mbalimbali.

Wanaoijua historia ya nchi hii wanasema kwamba Mwalimu Nyerere, alikataa kulala kwenye nyumba Fulani wakati anatembea mikoani kwa sababu nyumba ilikuwa inanuka harufu ya rangi. Inawezekana nyumba hiyo ilipakwa rangi masaa machache kabla ya Mwalimu kuwasili. Ipo mifano mingine ya namna hii na mingine ni vituko vya mwaka. Mfano shamba la mahindi liliopandikizwa miche iliyokuwa imeng’olewa kutoka kwenye shamba jingine. Mwalimu hakuchelewa kugundua ujanja huo. Viongozi hao waliwajibishwa.

Karne hii kuendeleza vitendo vya kuandaa mazingira mazuri kwa vile rais anatembelea sehemu Fulani ni kurudisha nyuma maendeleo. Si busara kusimamisha kazi kwa vile Rais, anatembelea sehemu Fulani. Rais anapoitembelea sehemu Fulani, anakuwa kazini na wala si likizo ya kula, kunywa na kucheza ngoma. Kama anakagua utekelezaji ni lazima awakute watu kazini. Nchi zilizoendelea zinafanya hivyo. Ni upuuzi mtupu kutumia pesa nyingi kwenye vinywaji na viburudisho vingine wakati wa kufungua miradi ya maendeleo ambayo karibu nusu yake ni mkopo.

Sasa hivi kuna maandalizi makali mjini Magu. Wiki hii nzima inayotangulia ujio wa Rais Mkapa, ofisi zimefungwa. Wakubwa wote wa wilaya, wilaya za jirani na hata kutoka Mkoani, wanakimbia huku na kule kuandaa ujio wa rais. Haya ndio anayapinga Mheshimiwa Lipumba. Kazi zinasimama, ingawa watu hawa watalipwa mshahara kamili mwishoni mwa mwezi. Nchi zilizoendelea mtu hulipwa mshahara kufuatana na masaa aliyofanya kazi. Hakuna mtu katika nchi zilizoendelea analipwa kwa kumaliza juma zima bila kuingia ofisini eti kwa vile alikuwa akiandaa ujio wa rais. Haya yanafanywa na nchi tajiri kama Tanzania!!

Mji wa Magu, ambao ni mchafu siku zote, sasa unasafishwa usiku na mchana. Takataka zilizokuwa zikizagaa kila kona ya mji sasa zinasombwa na kupelekwa kusikojulikana. Mji wa Magu haukuwa na choo( Public toilet), sasa choo inajengwa usiku na mchana! Uwanja wa Sabasaba ambao ni maarufu kwa shughuli kubwa za kijumuia kama vile sherehe za kiserikali, kijadi, soko na mnada, haukuwa na choo. Kwa vile rais Mkapa, atakaribishwa kwenye uwanja huu, choo inajengwa usiku na mchana. Choo hii inajengwa na wafungwa, Wanajenga kwa malipo au kama sehemu ya adhabu ya kifungo chao, ni maswali ya kujibiwa na viongozi wa wilaya ya Magu.

Wafungwa wanashinda wanachimba choo siku nzima, bila chakula bila maji ya kunywa. Hakuna anayejali utu wao au haki zao zi kibinadamu. Kazi ni moja, choo ziwe tayari kabla ya ujio wa rais! Kazi ni moja, sifa! Ili Rais awasifu viongozi wa Magu, kwamba wana (Public Toilet). Na baada ya ujioa wa Rais, Mbunge, ashike bango kwamba aliwajengea watu vyoo kwenye uwanja wa soko. Atumie bango hilo kuombea kura!

Swala hili la vyoo limelalamikiwa na watu wengi. Waandishi wa habari wameandika juu ya jambo hili, hakuna lililotendeka hadi ujio wa Rais. Maana yake ni nini? Ni kwamba uwezo na nyenzo za kujenga vyoo zipo, tatizo hakuna mtu wa kuwasukuma watendaji kutimiza wajibu zao. Au ni kwa vile mbunge hakai kwenye jimbo lake, anakuja wakati wa kuomba kura! Haya si maendeleo na wala si uwajibikaji!

Mbaya zaidi, watoto wa shule za msingi na walimu wao wanakatisha vipindi kufanya kazi za kusafisha uwanja wa sabasaba na maandalizi mengine kama nyimbo, ngoma na burudani nyingine. Hii ni dhambi kubwa tunayowatendea watoto wetu. Badala ya kukaa darasani na kujifunza tunawatumia kufanya kazi ambazo si zao. Haya si maendeleo na wala si uwajibikaji ni unyanyasaji wa watoto!

Ni vyema Rais, kuwatembelea watu wake na kukagua miradi ya maendeleo. Lakini si kitendo cha maendeleo watoto kukatisha masomo kuandaa ujio wa rais. Hata hivyo si kazi ya watoto wa shule kusafisha uwanja wa sabasaba ambao uko kwenye maeneo ya mji. Hizi ni kazi ambazo Halmashauri ya Wilaya inawajibika kuzishughulikia.

Barabara za Mji wa Magu, zimejaa mashimo. Sasa hivi mashimo haya yanazibwa na barabara zinaanza kupendeza. Akiondoka rais, barabara zitarudia hali yake ya kawaida!

Mji wa Magu, una tatizo sugu la Maji. Inawezekana kupita mwezi, bila sehemu Fulani ya mji kupata mgao wa maji kutoka idara ya Maji. Sasa hivi kwa vile kuna ugeni wa Rais, maji hayakatiki. Akiondoka Rais, anaondoka na maji. Matatizo yanakuwa ni yale yale.

Mishahara ya wafanyakazi wa Halmashauri inachelewa kila mwezi. Kisingizio ni kwamba hakuna pesa. Lakini pesa za kutengeneza barabara, kukarabati huduma ya maji, kujenga vyoo, kusafisha mji, kujenga vibanda, kununua vinywaji na vyakula vya msafara wa rais, zinapatikana! Kwani zipatikane pesa nyingi za kutengeneza mambo ya muda, na zisipatikane pesa za kutengeneza vitu vya kudumu na ambavyo ni muhimu?

Viongozi wanaokumbuka wajibu zao kwa vile rais anakuja kuwatembelea, si viongozi wanaolifaa taifa letu wakati huu tunapopigana kujiingiza katika mifumo ya utandawazi, soko huria, demokrasia, utawala bora na uwajibikaji.

Nimeandika makala hii kabla rais hajatembelea Wilaya ya Magu. Ni bora wasaidizi wake waisome na kumpatia habari. Aje akijua kwamba barabara nzuri atakazoziona mjini Magu, Usafi wa mji wa Magu, huduma ya maji na huduma nyingine za jamii kama vile vyoo, ni vitu vilivyoshughulikiwa wiki moja kabla ya ziara yake. Tena ajue kwamba watoto wa shule walikatisha masomo ili kuandaa ujio wake.

Wananchi wanakerwa kabisa na tabia za viongozi hawa wanaoshindwa kuwajibika hadi Rais, atakapowatembelea. Kwa vile hakuna jukwaa la maoni, wananchi wanabaki na hasira. Hivyo ni bora Rais, akakemea tabia hizi za viongozi wachovu. Na pale panapobidi si dhambi viongozi kama hawa kuwaomba wakastaafu kwa manufaa ya Umma. Kwa vile Rais Mkapa, anaelekea mwisho wa utawala wake, ni vyema akaacha amesafisha njia kwa yule atakayerithi nafasi yake. Hii itamsaidia mfuasi wake maana hataanza kazi kwa kupanda chuki ya kuwatimua viongozi wabovu. Pamoja na yote hayo, Karibu Magu, Rais wetu mpendwa na msafara wako. Karibu mgeni mwenyeji apone!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment