UPWEKE SI USEJA WALA USIMBE

MAKALA HII LICHAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.

UPWEKE SI USEJA WALA USIMBE

Makala yangu ya juma lililopita: Sote ni dhaifu tusaidiane, niligusia swala la upweke. Lengo langu kubwa lilikuwa kuweka wazi kwamba kati ya sababu zilizomfanya padri kulawiti ni upweke; si kwa vile yeye ni mseja, bali kwamba alikumbwa na upweke! Pia makala zangu za nyuma wakati wa matatizo ya Kanisa katoliki la Amerika, kuhusiana na kashfa za mapadri kuwanyanyasa watoto kijinsia, niligusia juu ya :Padri ni viumbe wapweke; si kwa vile mapadri ni waseja, bali kwa vile wamezungukwa na mazingira ya upweke. Baadhi ya watu hawakukubaliana na hoja yangu na kuibua mawazo kwamba mimi ninafikiri kwamba upweke ni useja na usimbe. Kwamba upweke unawashambulia mapadri kwa vile ni waseja!

Ingawa kuna baadhi ya waseja waliofanikiwa kupamba na upweke na kuishi maisha ya kuheshimika na utukufu bado kuna ushahidi wa kutosha kwamba watu wasiokuwa na wenzi wa maisha, waseja na wasimbe, wanakumbwa na upweke kwa asilimia kubwa. Ulevi, mfadhaiko, magonjwa ya akili, ubinafsi wa kupindukia na uzinzi ni kati ya magonjwa yanayowashambulia kwa wingi watu wasiokuwa na wenzi wa maisha. Ni vigumu kuyatenganisha magonjwa haya na upweke! Hili halina ubishi. Shaaban Robert, aliwahi kughani kwamba: Msimbe na ibilisi watakosaje kudarana! Yeye akuwa anatetea maisha ya ndoa. Kwamba mtu akiishi maisha ya usimbe au useja anakumbwa na vishawishi vingi na kuvuruga amani katika jamii anamoishi. Shaaban Rober, hakuona tofauti kati ya msimbe na Ibilisi. Kwa maoni yake upweke halikuwa jambo jema, ili mtu kuukwepa upweke ni sharti aishi maisha ya ndoa!

Lakini pia kuna ushahidi wa kutosha kwamba hata na watu walio kwenye ndoa wanakumbwa na upweke. Mfano mtu anayeikimbia familia yake na kuamua kujenga kiota nje ya familia yake anakuwa nasukumwa na upweke. Mtu anayeamua kuacha ndoa yake ya kwanza na kuolewa kwingine, anakuwa nasukumwa na upweke. Watu wanaoamua kuyamaliza maisha yao wenyewe, kujiua kwa kushindwa maisha ya ndoa, wanakuwa wanasukumwa na upweke. Ni wangapi kwenye ndoa wanaozifahamu nafsi za wenzi wao? Wakafahamu mipango yao, furaha yao, udhaifu wao na matatizo yao? Ndoa zilizo nyingi, mwanamke anajifungia kwenye nafsi yake na mwanaume anajifungia kwenye nafsi yake; Mwanamke anakuwa na mipango yake, marafiki zake, matumaini yake ( wakati mwingine anapanga kuyamaliza maisha ya mme wake ili arithi mali), na mwanaume anakua na mipango yake, marafiki zake, matumaini yake ( wakati mwingine ana wanawake wengine na watoto nje ya ndoa na amewarithisha mali bila mke wa ndoa kutambua!) huo ni upweke katika maisha ya ndoa! Ni upweke huo huo unaowafanya watu wawili wanaolala kitanda kimoja kuwa na ufa wa zaidi ya kilometa kumi kati yao. Ni upweke huo huo unaomkaribisha ibilisi kwenye ndoa na kusababisha kuzuka kwa tabia zisizo za kawaida kwa wanandoa!

Upweke hauna maana ya mtu kuishi peke yake ndani ya nyumba. Kuna watu wanaoishi peke yao ndani ya nyumba lakini si wapweke na kuna watu wanaishi na watu wengi kwenye nyumba, wanaishi kwenye familia ya watu wengi lakini nafsi zao, nyoyo zao zimejaa upweke wa kupindukia!


Upweke unaweza kumkumba binadamu yeyote yule, aliye kwenye ndoa au asiye kwenye ndoa, anayeishi peke yake au anayeishi na watu wengi. Upweke ni ukosefu wa mawasiliano kati ya mtu na mazingira yanayomzunguka, ni ukosefu wa mawasiliano kati ya mtu na watu wanaomzunguka, ukosefu wa mawasiliano kati ya mtu na familia, kati ya mtu na marafiki zake, kati ya mtu na jamii. Upweke ni hali ya mtu kujifunga ndani ya nafsi yake. Upweke ni hali ya mtu kujisifia yeye mwenyewe, kucheza akajishangilia yeye mwenyewe, kupiga ngoma akaicheza yeye mwenyewe, kujilaumu yeye mwenyewe na kujihukumu yeye mwenyewe! Upweke ni chanzo cha woga na kutojiamini. Mtu anaogopa watu wengine wasimfahamu jinsi alivyo ndani ya nafsi yake. Anajenga mipaka na ngome kubwa hadi anageuka kuwa fumbo kwake yeye mwenyewe na kwa jamii inayomzunguka!

Upweke unazaa ubinafsi wa kupindukia, unazaa mashindano. Kwa vile hakuna anayejua kilicho kwenye nafsi ya mwenzake, matokeo yanakuwa ni mashindano. Enda ikawa mtu akajua yaliyo kwenye nafsi ya mwenzake, mashindano yanaweza kupungua, na mashindano yakipungua, matatizo ya dunia hii yanapungua na vita itakoma!; maana watu wengi wakigundua kwamba nafsi zao zinabeba mambo yale yale! Kwanini kushindana kama furaha yenu ni moja, taabu yenu ni moja, matumaini yenu na malengo yenu yanafanana?

Upweke unazaa dhambi ambazo zingeepukika kama upweke ungedhibitiwa na kupatiwa tiba ya kudumu, Jukumu la kuufukuza upweke ni la kila binadamu maana kila binadamu anaumbwa na nafsi yake iliyofungwa hadi pale yeye anapoamua kuifungua. Na, anaifungua vipi? Ni sawa na yai na kuku, ni kipi kinatangulia? Ni mtu kuifungua nafsi yake au ni jamii inayomzunguka kumsaidia mtu kuifungua nafsi yake? Haya ndiyo mambo ya kukaa na kujadiliana badala ya kulaumiana na kunyosheana kidole.

Nimesema kwamba upweke ni kukosekana kwa mawasiliano kati ya mtu na mazingira yanayomzunguka, kukosekana kwa mawasiliano kati ya mtu na mtu, mtu na familia na mtu na jamii. Swali ninalojitokeza ni mbona kuna mawasiliano ya kutosha katika jamii yetu. Mfano tuna vikundi mbali mbali vya kusaidiana katika jamii yetu. Kuna vikundi vya makabila, vikundi vya kijinsia, vikundi vya vijana na wazee. Pia kuna vikundi vya burudani; kunywa pombe, kucheza muziki, kucheza michezo mbali mbali. Mara nyingi mawasiliano kwenye vikundi hivi yanakomea kwenye kusaidiana kwenye misiba, sherehe, burudani na kusaidiana kiuchumi. Hakuna vikundi ambavyo watu wanakusanyika kufunuliana nafsi zao, kupata nafasi ya kuzigusa nyoyo zao. Hakuna vikundi ambavyo mtu anaweza kujiweka mbele ya kikundi na kueleza matatizo yake binafsi ndani ya moyo wake. Si jinsi anavyohukumiwa na wanakikundi, sivyo anavyoonekana mbele ya kikundi, hapana! Jinsi yeye mwenyewe anavyojifahamu, yeye mwenyewe anavyojipima na kujifanyia tathmini, kama yeye ni mwizi, mwenye wivu, mwenye majivuno, mwenye choyo, mwenye kushindwa kutawala tamaa za mwili wake. Akajifunua wazi mbele ya kikundi na kuomba msaada. Kikundi kama hiki hakipo! Hata vikundi vya dini havifikii hapo. Hata viongozi wetu wa dini hawafanyi hivyo; kwamba padri ajifunue wazi mbele ya mapadri wenzake, mbele ya Askofu, hakuna labda kama ni maungamo, na tujuavyo tabia ya maungamo ni kufumbua kinywa chako na kuwalazimisha wengine kufumba vinywa vyao, matokeo yake hakuna ushauri, hakuna kurekebisha na hakuna msaada mkubwa wa mtu kubadilisha mtindo wa maisha!

Hata kwenye kikundi kidogo kama familia, hakuna nafasi ya wanafamilia kugusana nyoyo zao, mwanafamilia kujifunua wazi kwa wanafamilia wenzake, wakamfahamu, wakamthamini, wakamheshimu na kumsaidia. Au mwanamke kujifunua wazi mbele ya mume wake na mwanaume kujifunua wazi mbele ya mke wake; mfano kwamba nimevutiwa na mwanamke fulani, ninakuomba msaada wako, au nimevutiwa na mwanaume fulani, ninaomba msaada wako! Kitu kama hiki hakipo! Ndio maana upweke unaendelea kutushambulia!

Kuna mifano mingi kwenye jamii yetu inayoonyesha jinsi upweke unavyotushambulia lakini bahati mbaya hatutunzi kumbukumbu na hatukubali kujifunza kutokana na matukio mbali mbali. Juzi tu kule Shinyanga, limetokea tukio la mtu kufanya mapenzi na mjukuu wake na baada ya kitendo, babu aliamua kuyamaliza maisha ya mjukuu wake. Hiki ni kitendo cha kinyama. Huyu hana tofauti na padri aliyelawiti! Huyu ni mgonjwa ambaye upweke umemfikisha pabaya. Kabla ya hukumu yeyote dhidi yake ni lazima atafutiwe tiba. Hakuna adhabu inayoweza kufuta kumbukumbu ya tukio hili. La msingi ni kwamba tukio kama hilo lisitokee tena kwenye familia hiyo, lisitokee tena kwenye jamii yetu. Na njia ya kufanikisha hili ni kutafuta tiba badala ya adhabu.

Ipo mifano mingi ya watu kufanya mapenzi na watoto wao, watu kufanya mapenzi na wanyama na matendo mengine yasiyokubalika katika jamii. Yanatokea, yanapita na tunaendelea kukaa kimya. Wanaoyatenda makosa haya wanapata adhabu, wanafungwa miaka 30,50 na wengine wanafungwa maisha, lakini matendo yenyewe yanaendelea kila kukicha!

Kwa vile viongozi wetu wa dini wanatoa picha ya kuwa wao ni watakatifu na wanaishi dunia tofauti na ya kwetu, wanaishi kwa usiri mkubwa na kuzungukwa na mafumbo, yakiwapata, tunawashangaa na kuwa na maswali mengi. Tunawalaani na kuwatupa kwenye kapu la Ibilisi kama alivyofanya Shaaban Robert kwa wasimbe. Kumbe matukio haya ni ya kawaida na yanamtokea kila binadamu!

Na yakitokea viongozi wetu wa dini wanapoteza muda mwingi kujitetea, kutoa adhabu kwa wahusika na kuendelea kukazania sheria, mafundisho na mapokeo ya dini zao. Wanasahau kutafuta chanzo cha matatizo na kutoa tiba.

“Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako”.(Yohana 17:21)

Haya ni maneo ya mtu aliyepambana na upweke. Yeye anakwenda mbali zaidi. Mawasiliano kati ya mtu na mtu si kufunuliana tu nafsi, bali ni kuwa ndani yake kiasi kwamba: “Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya baba, Mwana hukifanya vile vile. Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe…” (Yohana 5:19-20)


Kumbe kuufukuza upweke ni pale mtu anapokuwa na mtu au watu ndani yake, ni pale nafsi ya mtu inapokuwa imejaa watu wanaojua afanyayo hata kama mtu huyu huyafanya kwa kificho, apendayo hata kama mtu huyu hupenda kwa kificho, achukiayo hata kama mtu huyu huchukia kwa kificho! Upweke unakimbia pale mtu anapowakaribisha watu wengine nafsini mwake, watu wanaoweza kujua furaha yake, uchungu wake, imani yake na matumaini yake.

Hii si kazi ya mchezo. Hii si kazi ya kumwachia kila mmoja kutafuta njia yake. Hii si kazi ya kubahatisha na mtu au kikundi cha watu kufanya watakavyo. Tumeona jinsi upweke unavyomshambulia mtu mmoja mmoja, familia, vikundi na jamii nzima. Hivyo huu ni mradi wa pamoja. Huu ni mradi unaohitaji ushirikiano, majadiliano, maisha ya kijumuiya na imani isiyoyumba, isiyokuwa na ubaguzi wala unafiki. Hii ni kazi inayohitaji imani imara. Ni kazi yenye utatata na changamoto kubwa. Maana ni vigumu kuingia kwenye nyoyo za watu, kuwa ndani mwa watu na kuziingilia nafsi zao bila ya kugusa miili yao! Nafsi, nyoyo, vimefunikwa na mwili, zinatunzwa na mwili wenye mvuto, wenye tamaa na uchu! Mtu anawezaje kuifanya kazi hiyo kwa usalama bila kukwazika yeye mwenyewe na kuwakwaza wengine? Ni sawa na mtu atakaye kula muhogo, ni lazima achafuke mikono kwa kushika udongo, ni lazima aumenye muhogo, kuuparuza na hatimaye kuula. Kuufukuza upweke ni sawa na kazi ya kuchimba dhahabu, ni kazi yenye adha kubwa, inachosha, ina hatari ya kupoteza maisha, ni sawa na kucheza na kifo mikononi mwako, wanaoifanya kazi hii hawachoki, hawaogopi wala kukata tamaa, maana wanajua mwisho wake ni tunu ni lulu!!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment